Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, March 21, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-31Tangu mwanzo wa hii kesi, nilijaribu sana kutokukubali kuwa na wasiwasi na mawazo,... kwani nilijua wazi sina kosa,...nilijua kuwa mimi sijaua, mimi sio muuaji, na mengi yamenikuta bila hata ya kupenda, kwa hiyo nikajitahidi sana kujipa moyo, kuwa nitashinda, kwa vile sina kosa, haki itanilinda,...nikawa najiamini hivyo.

Baada ya kufika huyo mpelelezi wa hii kesi yangu na kunihoji kwa kwa jinsi alivyoonekana  kujiamini zaidi,na hata kufikia kunishinikiza kuwa mimi ndiye muuaji, badala ya wenzao ambao waliamini kuwa mdada ndiye aliyeua,....nikaanza kuhisi wasiwasi, kuwa huenda nisiipate haki yangu..;

‘Hii inaonyesha kuwa wewe na mdada mlikula njama ya pamoja na kufanikisha kumuua mtoza ushuru....tunao ushahidi wa kutosha,...’akasema.

‘Sio kweli, ...’nikasema nikijitetea baada ya kuona wakili wangu yupo kimiya.

‘Kama sio kweli, nithibitishie...’akasema akifungua makabrasha yake.

‘Wewe ndiye uthibitishe kuwa kweli mteja wangu ana hatia, maana wewe ndiye uneyemshinikiza kuwa ana hatia...’akasema wakili wangu.

‘Sisi tumeshakusanya ushahidi wa kutosha, ndio maana tunataka kushirikiana na mteja wako, aseme ukweli ili kuokoa muda...’akasema

‘Mimi huo ukweli nitausema mbele ya mahakama sio kwako...’nikasema nilipoona jamaa kakazania na kauli yake hiyo.

‘Wewe unadai ulipigwa na kitu kizito na mtu usiyemfahamu, ukapoteza fahamu, na ulipozindukana ulimuona marehemu akiwa hai, ...hii ni kuonyesha kuwa marehemu aliuwawa wakati wewe upo mzima,...kama angaliuwawa wakati wewe umepoteza fahamu tungeliongea mengine...’akasema

‘Lakini mimi nilikuwa nimeshatoka nje...’nikasema

‘Ulitoka nje baada ya marehemu kupigwa risasi, .....ukaogopa na kukimbia...’akasema

‘Sio kweli,...mimi nilipoona mdada ameshabadilika, na anaweza kunigeukia na mimi, ndio nikaona nijiokoe, ndio maana nikakimbilia nje, ....niliwaacha wote wakiwa ndani, na wakati natoka humo ndani, wote walikuwa wazima licha ya wote walikuwa na majeraha mabaya, walikuwa wote wameumia ...’nikasema

‘Unasema wote walikuwa wameumia, kwa vipi, unaweza kuelezea jinsi walivyoumia,maana wewe ulikuwepo na uliona tukio zima la kuumua kwao...,?’ akaniuliza

‘Mdada nahisi alijeruhiwa kwa risasi, ....wakati wananyang’anyana hiyo bastola, mtoza ushuru alimjerihi mdada kwa risasi, na mtoza ushuru, alikuwa kaumia kwa majeraha ya kuparuliwa na makucha ya mdada, na kubamizwa chini, nahisi alikuwa kavunjika viuongo,....nilimuona akiwa na damu nyingi sana usoni,....’nikasema na yule askari akawa anaandika kitu halafu akauliza

‘Kama wewe ulipigwa na kitu kizito kichwani ukapoteza fahamu ukaamuka ukakimbia, na mdada naye akaja kupigwa na kitu kama hicho hicho kichwani, ina maana kulikuwa na mtu mwingine ndani, kwanini wewe hukumuona?’ akauliza

‘Mimi nilipozindukana,nilichojua ni kukimbia, sikuwa na wazo la kuwa kuna mtu mwingine humo ndani, wazo hilo nimelipata wakati mnanihoji, ....kwa muda huo, niliyekuwa namuogopa hapo ni mdada, ukimuona alivyokuwa hata wewe ungelikimbia, kiukweli, sikuwa na wazo la kuwa kuna mtu mwingine humo ndani,..’nikasema

‘Ngoja tuanze hivi.....’akasema na wakili wangu aliposikia hivyo akasema;

‘Umeshamuhoji mteja wangu vya kutosha huwezi kuanza tena upya...’akanitetea wakili wangu .

‘Nataka tuliweke hili sawa, kutokana na maelezo ya mlinzi, ni kuwa mtu aliyeonana naye wakati anakuja kutoa taarifa ya mgeni, ni mtu tofauti na wewe, kama alivyomuelezea kuwa ana ndevu, kavaa viatu vya wazi, na alikuwa na nguo tofauti kabisa na ulizokuwa nazo wewe...’akasema huyo askari mpelelezi

‘Mimi hapo sijui.....huyo mtu mwingine sikumuona...’nikasema na huyo mpelelezi, akauliza

‘Wewe ndiye uliyeongea na mlinzi, ukaenda kuchukua huo mzigo, kwa mtoza ushuru ndio au hapana?’ akauliza

‘Ndio mimi...niliyefanya hivyo?’ nikasema

‘Wakati unaonana na mlinzi,ulikuwa umevaa nguo hizo hizo za awali au ulibadilisha?’ akauliza

‘Nilikuwa nimevaa nguo hizo hizo, sikuwahi kubadilisha nguo, kwanini nibadilishe nguo, hapo sio nyumbani kwangu,....’nikasema

‘Kwahiyo wewe una uhakika kuwa kulikuwa hakuna mtu mwingine humo ndani zaidi yako ?’ akauliza

‘Mimi siwezi nikathibitisha hilo,.. maana kama mlinzi aliona mtu mwingine, basi ina maana kweli kulikuwepo na mtu mwingine, lakini mimi sikuwahi kumuona...’nikasema

‘Kwa maumbile ya mwili kama alivyosema huyo mlinzi, ni kuwa maungo yenu, maumbile ya mwili, sio sura, mnalandana, kuna mawili hapo, wewe uliabadili nguo, ukaweka ndevu za bandia,...ili kutokujulikana na huyo mgeni wenu, au kujificha ili mlinzi asikutambue, ama kuna mtu aliyeshirikiana nanyi, na hamtaki ajulikane...’akasema

‘Hizo ni fikira zako mkuu, naomba umuulize mteja wangu kwa mambo ambayo aliyafanya na kuyaona,...hayo utathibitisha mwenyewe kwenye kazi zako...’akanitetea wakili wangu.

‘Ni kweli nitayafanyia kazi,...ila nina uhakika, kuna mchezo uliochezwa kati ya mdada na huyu mteja, wako, kuficha ukweli,....na kama kulikuwa na mtu mwingine, basi huyo ndiye aliyemuua mtoza ushuru, ...ukiunganisha matukio..’akasema na akawa kama anafikiria kitu, halafu akasema;

‘Swali hapa, inawezekanaje huyo mtu aingie bila mlinzi kumuona, na huyu mteja wako, anasema hakumuona mtu mwingine humo ndani....huoni kuwa kuna kitu kinafichwa hapa..’akasema kama anauliza

‘Kwanini ifanyike hivyo....na kitu gani kinafichwa hapo?’ akauliza wakili.

‘Nilitaka kuongea na mteja wako ili anisaidie kwa hilo, na ili nione kama kweli hahusiki, na kama angenisaidia kuniambia ukweli, na kuthibitisha kuwa kweli kulikuwa na mtu mwingine humo ndani, basi yeye angelikuwa hahusiki tena, tungekuwa na kazi ya kumtafuta huyo mtu mwingine, ...’akasema

‘Hiyo ni kazi yenu,....’akasema wakili

‘Ndio hiyo ni kweli, hiyo ni kazi yetu, lakini kwa raia mwema, anawajibika kuwa mkweli, ili haki itendeke, unapoficha ukweli, ina maana gani, ni kuwa wewe unahusika, kwa njia moja ama nyingine kama sio moja kwa moja...’akasema

‘Hayo utayathibitisha mahakamani, mimi nina imani kuwa mteja wangu hana hatia, ....kama huna maswali mengine naona unipe nafasi nataka kuongea na mteja wangu...’akasema wakili.

‘Kwa hali hiyo basi, kesho huyu mteja wako inabidi aende gerezani, haitawezekana kuendelea kukaa hapa, kwa utaratibu ulivyo, tulimchelewesha hapa ili aweze kuisaidia polisi, kumpata huyo mtu mwingine, ambaye tulifahamu kuwa yeye atathibitisha kuwa kulikuwa na mtu mwingine humo ndani, kwa vile sasa kathibitisha kuwa hakukuwa na mtu mwingine, basi yeye na mdada ndio walioshirikiana kumuua mtoza ushuru...’akasema.

‘Thibitisha hilo kwa ushahidi, sio kwa dhana, usimtwike mteja wangu kwa kosa ambalo hajalifanya, ...na kwa vile hamjakuwa na uhakika kuwa mteja wangu ndiye anayehusika , basi dhamana ni haki yake....’akasema wakili

‘Hawezi kupewa dhamana, ..kwa hali jinsi ilivyo, angelipewa dhamana kama angethibitisha kuwa kulikuwa na mtu mwingine zaidi yake, ...kwa vile hajathibitisha hilo, huyu tunamweka katika fungu la muhusika mkuu, aliyetenda hilo kosa, na muuaji, hawezi kupata dhamana kwa sasa, kwanza kwa usalama wake, pili, anaweza kufanya lolote kuficha ukweli...’akasema huyo mpelelezi.

‘Kwa akuli yako umesema hamjawa na uhakika, kuwa mteja wangu anahusika, bado mnamtafuta huyo mtu mwingine, kuendelea kumshikilia ni kumuonea, ....kwahiyo dhamana ni haki yake...’akasema wakili.

‘Tutalithibitisha hilo kuwa kweli mteja wako na mdada wanahusika,....ushahidi huo tunao...’akasema

‘Thibitisha...kwani kama ungelikuwa na uhakika huo usingelikuja hapa kumhoji tena..’akasema wakili

‘Mteja wako, alikwenda kumuona huyo mgeni,kama alivyoagizwa na mdada kwenda kuchukua huo mzigo,.... wakapeana hiyo mizigo, huyo mgeni akagundua kuwa kapewa tofauti na makubaliano, akakasirika na kuchukua bastola, akaingia na mteja wako ili kukabiliana na mdada, ...wakati mtoza ushuru, ambaye ndio huyo mgeni, akizozana na mdada, mteja wako, akapata nafsi ya kumuumiza huyo mgeni, na bastola ikamtoka...’akatulia.

‘Kwahiyo bastola akawa nayo mteja wako, ....mtoza ushuru akawa hana ujanja,..hata hivyo, inavyoonekana ni kuwa mtoza ushuru alijaribu tena bahati yake ya kujitetea,  pale alipopata hiyo nyundo na kumgonga nayo mdada kichwani, mdada akadondoka na kupoteza fahamu...’akatulia

‘Wakati anakwenda kupambana na mteja wako, mteja wako ikabidi atumie hiyo silaha na kumpiga risasi mtoza ushuru, na alipogundua hilo akabaki ameduwaa, hakujua kuwa mdada kazindukana,  na mdada alikuwa keshachukua ile nyundo akamgonga nayo mteja wako kichwani..., mteja wako akadondoka, na hapo mdada akawa na hiyo bastola..’akasema

‘Mteja wako alipopata fahamu, na wakati huo mdada hali yake ya kuchanganyikiwa ilikuwa inaanza kurudi, na kama wanavyosema , ile hali yam dada, ya kuchanganyikiwa ikiisha, huwa anadondoka chini na anakuwa kama kapoteza fahamu ....mteja wako alipoona hivyo, akapata nafasi ya kukimbia....’akasema huyo mpelelezi.

‘Hizo ni hisia zako,...unaweza kufikiria vyovyote, hujaonyesha kwa vielelezo, kwa ushahidi wa kihalisia,... unaweza kuthibitisha kwa ushahidi wa vielelezo?’ akauliza wakili

‘Kila kitu kipo tayari, nilichokuja kumuona mteja wako, ni kuona kama kweli anayosema ni sahihi, na kama kweli ana uhakika hakukuwa na mtu mwingine humo ndani...na kama tulivyoona sisi kwa ushahidi tulio nao, mteja wako ana hatia, ....akishirikiana na mdada japokuwa mdada, ana utetezi wa hali yake ya kiafya...na hapo inamuacha mteja wako kuwa mhusika mkuu....’akasema

‘Basi kama mna ushahidi huo, tutaonana mahakamani, lakini kwa hivi sasa mteja wangu ana haki ya dhamana, hamjathibitisha kuwa yeye ndiye aliyefanya hivyo kwa vile kuna utata... kuwa kulikuwa na mtu mwingine, na kihalisia ndivyo ilivyo,...'akasema

'Na ukiangalia mtiririko wa hayo matukio, mteja wangu asingeliweza kuyafanya yote hayo kwa wakati mmoja,  kwa muda huo mfupi, na kwa maelezo yenu, kutoka kwa kauli ya mlinzi,inaonyesha wazi kabisa kuwa kulikuwa na mtu mwingine aliyekuwa na ndevu,....na hata nguo alizokuwa kazivaa ni tofauti...'akatulia akageuka kuniangalia na kusema;

'Je kwa kumshikilia hivi, ina maana huyu mteja wangu, ndiye huyo mtu, hapana, kwa dalili hizo, na kwa jinsi tukio lilivyokuwa, sio yeye kabisa, kazi ni kwenu kumtafuta huyo mtu mwingine,na wakati mnafanya hivyo, hamuwezi kuendelea kumtesa mteja wangu kwa kumshikilia, dhamana ni haki yake .....’akasema wakili.

‘Inawezekana kabisa huyu mteja wako alivaa ndevu za bandia...na kubadili nguo, ikionyesha kabisa kuwa walikuwa na dhamira hiyo, ....haiwezekani huyo mtu mwingine apite pale getini mlinzi asimuone, haiwezekani kabisa kwasababu ukuta wote umezungushiwa waya za umeme, na tumeona kwenye kumbukumbu za huo mtambo wa usalama, umeme haukuwahi kuzimwa,...sasa huyo mtu mwingine alipitia wapi....?’ akauliza

‘Hiyo ni kazi yenu kutafuta ili kuhakikisha kuwa haki inatendeka, ...’akasema wakili.

‘Hilo tutalithibitisha mahakamani, hatuna shaka nalo,haki itatendeka, na muhusika atahukumiwa ...na kwa hali hiyo mteja wako kesho anakwenda gerezani,...’akasema

‘Hapo mtakuwa hamjatendea haki mteja wangu, inabidi tukutane na hakimu kuliangalia hilo, dhamana ni haki ya mteja wangu...’akasema wakili

‘Tutaona itakavyokuwa,.....kama mnataka hivyo, tutakutana mahakamani kuona kama kweli mteja wako anastahiki hiyo dhamana,...lakini wakati hayo yanafanyika hatuwezi kuendelea kukaa na huyu mtu hapa kituoni, sheria zipo wazi, kesho anakwenda gerezani...’akasema huyo mpelelezi na kuondoka.

**********

‘Usijali hiyo ndio kawaida ya hao watu, inabidi wafanye hivyo, vitisho, mashinikizo, kudhania,....wakijua kuwa kama unahusika, utaghadhibika na kuanza kuropoka ovyo, ....’akasema wakili.

‘Kwahiyo ina maana kweli kesho watanichukua kunipeleka gerezani?’ nikauliza

‘Hawataweza kufanya hivyo, nina uhakika kuwa bado hawajawa na uhakika na ushahidi wao, na bado wanakuhitaji kuhakiki maelezo yao, cha muhimu, usikubali kabisa kuongea nao bila kuwemo wakili wako,...mpaka sasa kinachowachanganya ni huyo mtu mwingine, hata mimi najiuliza kuhusu huyo mtu mwingine, je ni kweli hakukuwa na mtu mwingine zaidi yako wewe na mdada?’ akaniuliza

‘Mimi sikuwahi kumuona huyo mtu mwingine....lakini inavyoonekana ni lazima kulikuwa na mtu mwingine ambaye aliweza kumgonga mdada na nyundo na kufanya hivyo kwangu...’nikasema

‘Aliingia kwa kupitia wapi?’ akauliza

‘Huenda aliruka ukuta...’nikasema

‘Nilifanya utafiti huo kwa kuchunguza ule ukuta,....sio rahisi mtu kuruka juu, labda kuwe na mawasiliano ya kuzima umeme.., na hilo lingelifanyika ndani...ina maana kuwe na mtu wa nje na ndani wanawasiliana kuwa azime umeme na alipoingia huyo mtu , wakauwasha kabla kelele hazijaanza kusikika, ni kitendo cha haraka sana, hata hivyo kumbukumbu zake,hazionyeshi hivyo ...’akasema

‘Hapo mimi sielewi..kumbukumbu gani hizo?’nikauliza

‘Umeme wa ulinzi uliopitishwa kwenye hizo waya, unaunganishwa na vyombo vilivyopo ndani, ambapo, kila tukio la kuzima au kuwashwa hujionyesha kwa muda wa tukio hilo, na hali kama hiyo inakuwepo huko kwa watu wa ulinzi walioweka hizo nyaya za usalama,.... hakukuwa na kuzima au kuwashwa kwa muda huo, limethibitishwa hilo,....kwa wiki nzima, hakujakuwa na kuzimwa kwa umeme kwa huduma hiyo ya ulinzi...’akasema

‘Kwa hali hiyo, kama kuna huyo mtu, basi atakuwa kapitia pale pale getini, sasa ilikuwaje apite bila mlinzi kumuona, je kuna muda mlinzi alitoka, kwa kumbukumbu za mlinzi, hakuwahi kutoka muda wote huo, na anasema alikuwa pale pale mlangoni kwa muda wote huo....’akasema

‘Mna uhakika gani kuwa mlinzi anasema ukweli?’ nikauliza

‘Kutoka na historia ya huyo mlinzi, ni mtu anayeifahamu sana kazi yake, na ana kumbukumbu ya hali ya juu, ...labda..’akatulia kidogo akiwaza

‘Labda nini?’ nikauliza

‘Aweze kumpitisha mtu, kwa urafiki au kuhongwa,...na kwa maana hiyo atakuwa ameshirikiana na hao watu, kitu ambacho hakiwezekani kutokana na jinsi anavyofahamika huyo mlinzi, ni mwaminifu na mchapa kazi...’akasema na mimi hapo akili ikanikumbusha kutokana na tabia ya huyo mlinzi, nikasema;

‘Hilo la kuhongwa inawezekana,huyo mlinzi naona kama ana tabia hiyo...na kwa maisha yetu, unatoka nyumbani huna kitu, una majukumu mengi, unafikiri huyo mlinzi hawezi kuhadakika kwa pesa nzuri, akawa kampitisha mtu...kwa pesa, mimi nahisi atakuwa kafanya hivyo...’nikasema

‘Una uhakika gani na hilo?’ akauliza

‘Niliwahi kuongea na huyo mlinzi kabla, siku ya mwanzo kufika hapo kwa mdada, aliniambia kuwa wakati mwingine anakuwa na hali ngumu..., na mdada hapendi kusumbuliwa, lakini mtu aliyekuja ana jambo muhimu la kuonana na mdada, alisema kama atarizika na huyo mtu, kwa njia ya kumsaidia huyo mtu, yeye inabidi kwenda kuonana na mdada, anakwenda kumbebembeleza mdada, ili aonane na huyo mtu..hapo unafikiri atafanya hivyo bure....’nikasema

‘Uliwahi kufanya hivyo kwake?’ akaniuliza

‘Nilifanya hivyo kama kumsaidia, aliponielezea kuwa siku hiyo hana kitu,  lakini sio kwa ajili ya kumuona mdada, maana siku nilizofika hapo nilifika nikiwa na miadi na mdada, sijawahi kufika bila kuwa na miadi naye...’nikasema.

‘Kama ni hivyo, ....hapo ninahisi, inawezekana kulikuwa na mtu mwingine aliyeingia...inabidi nilihakiki haraka iwezekanavyo, kama hamna,kuna kazi kubwa sana, inabidi uniambi ukweli ulivyokuwa kabla kesi hii haijafika mahakamani...’akasema

‘Kwa vipi?’ nikamuuliza

‘Kutokana na ulivyoniambia,...kama huyu mlinzi analalamika hali ngumu, na sasa yupo kwenye wakati mgumu, hana pesa, naweza kuupata ukweli kwa njia hiyo, na kama nitafanikiwa kuupata huo ukweli, basi tutakua kwenye nafasi nzuri ya kuimaliza hii kesi mapema..’akasema

‘Mimi hapo sina uhakika bado...sikuwahi kumuona huyo mtu mwingine..’nikasema nikijaribu kuziita kumbukumbu za tukio lile.

‘Kama ni hivyo, basi...itabidi tupambane mahakamani bila ya uhakika...unapigaan bila silaha, lakini kama uliyosema ni kweli, tutashinda tu...’akasema

‘Hata hivyo, mbona huyo askari mpelelezi anaongea kama ana uhakika fulani, ni kama wana ushahidi mkubwa ndio maana ananishinikiza kwa kosa ambalo sijalifanya, anavyoongea utafikiri alikuwepo, akaona jinsi ilivyo kuwa, anajitungia tu habari zisizokuwepo, mbona hawa watu wananitaka ubaya...’nikasema

‘Ndio hapo unapoona umuhimu wa kuwepo mawakili,...watu wengi hapa nchini hawajaona umuhimu wa mawakili, na kwasababu hiyo haki zao, zinapotea bure,na wengine wanajikuta wakihukumiwa kwa kosa sio lao...angalia kwa hili,  kama nisingelikuwepo hapa,unafikiri ingelikuwaje...’akasema kama anauliza

‘Wangenifunga kwa kuleta vurugu, maana ni lazima ningekosana naye, hawezi kusema kuwa mimi nimeua, wakati sijafanya hivyo, ananitia hasira sana, nasota humu ndani wakati sijafanya kosa,...na ni nani huyo muuaji, na kwanini aumie mtu mwingine wakati huyo muuaji yupo nje, watanilipa nini kwa hii adhabu wakija kumgundua huyo mtu...’nikawa kama nauliza

‘Wakati mwingine ili kupata ukweli, ...inabidi iwe hivyo, inabidi watu wasio na hatia kuumia kwa muda, kwa ajili ya kufichua ukweli uliofichika, kwa vile ukweli na haki una mitihani mingi, kwasababu ya dhuluma kuwa jambo la kawaida kwa watu,....pole sana, ...’akasema

‘Na mtaonana saa ngapi na huyo wakili aliyemleta mdada....?’ nikamuuliza nilipomuona akijiandaa kuondoka

‘Muda wowote, lakini nina shaka, huenda asikubali kuonana na mimi....’akasema

‘Kwanini?’ nikauliza

‘Hata siku moja, maji na mafuta hayapatani....katika kazi yetu hii nimejifunza mengi, kila fani ina mitihani yake, na fani yetu hii imeingiliwa na wajanja wajanja, ....na mtu wa namna hiyo anaogopa sana kukutana na yule mtaalamu wa ile fani,kwani anajua ataumbuliwa....hata hivyo nitajitahidi nionane naye, ili nione yeye kagundua nini, ...’akasema

‘Una uhakika kagundua kitu?’ nikauliza

‘Kama yupo karibu na mdada, uwezekano huo upo, na kwa kumtumia yeye huenda nikawa na nafasi ya kufichua ukweli wa hili tukio, nahisi kuna mengi yamejificha hapa, japokuwa hata wewe hujaniambia ukweli ninaohisi upo...’akasema

‘Ukweli gani huo...?’ nikauliza

‘Ukiwa tayari kuniambia , utakuwa umesaidia mengi sana, na jinsi unavyozidi kuchelewa kuaniambia ndivyo unavyozidi kuweka mazingira ya hii kesi kuwa ngumu, na usipokuwa makini, unaweza ukahatarisha hata maisha yako mwenyewe...’akasema

‘Kwa nini unasema hivyo?’ nikauliza

‘Kutokana na uzoefu wangu, na kesi kama hizi,....watu hawa hawataki siri yao igundulikane, na wakiona kuna mtu anaweza kuwatia matatani, hawasiti kumuondoa duniani....na wewe upo kwenye hiyo hatari..’akasema

‘Lakini mimi sihusiki na hao watu, na wala siwajui hao watu ni akina nani...’nikasema kwa kulalamika

‘Kama kweli huhusiki ungelishaniambia ukweli,....kuficha kwako ukweli inaonyesha unafahamu mengi, na hayo unayoyafahamu ndiyo yatakayokuweka pabaya, yanaweza kuwa kisu cha kukumaliza wewe mwenyewe, ...’akasema na kuniangalia kwa makini

‘Mbona unanitisisha muheshimiwa...’nikasema

‘Wakati mwingine , ndio maana naona ni heri ubakie hapa hapa, ukipelekwa gerezani sizani kama utakuwa na nafasi ya kwenda mahakamani, unaweza ukapotelea huko huko, ndio wasiwasi wangu mkubwa, ...na pia...hata ukipewa dhamana, inaeza ikawa ni hatari zaidi,hapo najikuta kwenye mtihani wa jinsi ya kukutetea...inabidi nikuambie huo ukweli, ili uone hali ilivyo, sio kwamba nakutisha, .....maisha yako yapo kwenye hatari kubwa...’akasema

‘Kwanini unasema hivyo,...unaonekana kama unawafahamu hao watu?’ nikauliza

‘Hii kazi sijaianza leo, ...na kiukweli mimi mwenyewe nilishawahi kuingizwa kwenye mikono ya hao watu, lakini baadaye wakaona sifai,...mitego yao mingi niliweza kukwepa,...japokuwa wakikukamia, huwezi kukwepa, nahisi waliona sio mtu wanayemtaka, wana akili ay kumsoma mtu...’akasema

‘Ni watu gani hao?’ nikamuuliza

‘Cha muhimu ni wewe uwe mkweli,..sijui kwanini, mimi naumiza kichwa changu kukusaidia wewe, lakini wewe unakuwa kama vile huna shida,huioni hatari iliyopo mbele yako,...sielewi, na kila mara ninapokutana na hizi kesi, nakutana na watu wa aina yako..too sturbon(mkaidi, mtukutu).’akasema akishikashika kichwa.

‘Kiukweli, nimechoka kufanya kazi za aina hii, na huenda ikawa kazi yangu ya mwisho kufanya, nataka niachane kabisa na hizi kazi za namna hii,...ni hatari tupu...na kabla sijafanya hivyo, nataka niweke historia,...hili kundi ni lazima lipatikane,...’akasema huku akisimama kuondoka

‘Kundi,..kundi lipi hilo,...!?’ nikauliza kwa mshangao na yeye hakunijibu akawa anaanza kuondoka, na nilipoona hivyo nikauliza;

‘Sasa muheshimiwa, mimi nitegemee ni nini?’ nikauliza

‘Inawezekana upo ndani ya hilo kundi bila ya wewe kujijua, ukawa unatumiwa, lakini anyway, yote ni wewe tu, nikuambie ukweli, ni ukweli wako tu, ndio utakaoweza kukuokoa,  vinginevyo, utaniambia, kama utakuwa na nafasi hiyo ya kuniambia, vinginevyo, huenda ikawa historia kuwa kulikuwa na mtu kama wewe...’akasema na mara nikasikia mtu akiongea, na yeye akawa keshafika mlangoni, na alipoangalia huko nje, akageuka na kuniambia;

‘Wakili wako huyo .....kaja,..na kumbuka kazi niliyokupa, hujanipa taarifa bado,....’akasema na kuondoka, huku nikiwaza ni kazi gani aliyonipa, na huyu mtu ana maana gani, mbona ananitisha hivi,...

‘Mhh, naanza kuogopa....’nikasema na mara wakili huyo mwingine akaingia.

‘Mdada anasema hivi, huhitaji wakili mwingine,...huyu wakili wako hakufai, uachane naye, vinginevyo, ....’akaanza kuongea kabla hatujasalimiana.

NB: Mtandao , mtandao,...hata sijui nifanye nini..ok, hata hivyo, nimejitahidi kufanikisha sehemu hiyo, ninachoweza kuwaambia wapendwa wangu, ni ijumaa njema na kuwatakia wikiendi njema

WAZO LA LEO: Sio kila anayekuchekea ni rafiki wako wa kweli, ndio maana wengine husema `hapendwi mtu hapa, kinachopendwa leo ni pesa, kinachopendwa leo ni mali, na utajiri, utu hakuna tena.

 Ukitaka kulijua hilo hebu jipime wewe mwenyewe, kwa kuangalia mali ulizo nazo na jinsi ulivyoweza kuzipata, kama hakuna doa la uchafu wa dhuluma,kuwa kwa namna moja au nyingine ulitenda isivyo halali ili kufanikisha kuupata utajiri huo, au mali hiyo. Ukweli ni mgumu, lakini ukiangalia kwa makini,utaligundua hilo.

Imefikia hatua hata haki yako ili uipate unajikuta kwenye mtihani wa kuinunua. Hii ina maanisha nini, ni kuwa dhuluma imeshaota mizizi, ili upate,...unatakiwa upatikane,..ilivyo ni kuwa watu hawaogopi tena kuitenda dhuluma, ilimradi hugunduliki,   mwenye nacho anataka zaidi, na asiyekuwa nachao anaota ndoto na yeye apate hata kama kupata huko nikwa dhuluma, .....hii ni hatari. 

Ni mimi: emu-three

No comments :