Tangu mwanzo
wa hii kesi, nilijaribu sana kutokukubali kuwa na wasiwasi na mawazo,... kwani nilijua wazi sina
kosa,...nilijua kuwa mimi sijaua, mimi sio muuaji, na mengi yamenikuta bila hata ya kupenda, kwa hiyo nikajitahidi sana kujipa moyo, kuwa nitashinda, kwa vile sina kosa, haki itanilinda,...nikawa
najiamini hivyo.
Baada ya kufika huyo mpelelezi wa hii kesi yangu na kunihoji kwa kwa jinsi alivyoonekana kujiamini zaidi,na hata kufikia kunishinikiza kuwa mimi ndiye muuaji, badala ya wenzao ambao waliamini kuwa mdada ndiye aliyeua,....nikaanza kuhisi wasiwasi, kuwa huenda nisiipate haki
yangu..;
‘Hii
inaonyesha kuwa wewe na mdada mlikula njama ya pamoja na kufanikisha kumuua
mtoza ushuru....tunao ushahidi wa kutosha,...’akasema.
‘Sio kweli,
...’nikasema nikijitetea baada ya kuona wakili wangu yupo kimiya.
‘Kama sio
kweli, nithibitishie...’akasema akifungua makabrasha yake.
‘Wewe ndiye
uthibitishe kuwa kweli mteja wangu ana hatia, maana wewe ndiye uneyemshinikiza
kuwa ana hatia...’akasema wakili wangu.
‘Sisi
tumeshakusanya ushahidi wa kutosha, ndio maana tunataka kushirikiana na mteja
wako, aseme ukweli ili kuokoa muda...’akasema
‘Mimi huo
ukweli nitausema mbele ya mahakama sio kwako...’nikasema nilipoona jamaa kakazania na kauli yake hiyo.
‘Wewe unadai
ulipigwa na kitu kizito na mtu usiyemfahamu, ukapoteza fahamu, na
ulipozindukana ulimuona marehemu akiwa hai, ...hii ni kuonyesha kuwa marehemu
aliuwawa wakati wewe upo mzima,...kama angaliuwawa wakati wewe umepoteza fahamu
tungeliongea mengine...’akasema
‘Lakini mimi
nilikuwa nimeshatoka nje...’nikasema
‘Ulitoka nje
baada ya marehemu kupigwa risasi, .....ukaogopa na kukimbia...’akasema
‘Sio
kweli,...mimi nilipoona mdada ameshabadilika, na anaweza kunigeukia na mimi,
ndio nikaona nijiokoe, ndio maana nikakimbilia nje, ....niliwaacha wote wakiwa
ndani, na wakati natoka humo ndani, wote walikuwa wazima licha ya wote walikuwa
na majeraha mabaya, walikuwa wote wameumia ...’nikasema
‘Unasema
wote walikuwa wameumia, kwa vipi, unaweza kuelezea jinsi walivyoumia,maana wewe
ulikuwepo na uliona tukio zima la kuumua kwao...,?’ akaniuliza
‘Mdada
nahisi alijeruhiwa kwa risasi, ....wakati wananyang’anyana hiyo bastola, mtoza
ushuru alimjerihi mdada kwa risasi, na mtoza ushuru, alikuwa kaumia kwa
majeraha ya kuparuliwa na makucha ya mdada, na kubamizwa chini, nahisi alikuwa
kavunjika viuongo,....nilimuona akiwa na damu nyingi sana usoni,....’nikasema
na yule askari akawa anaandika kitu halafu akauliza
‘Kama wewe
ulipigwa na kitu kizito kichwani ukapoteza fahamu ukaamuka ukakimbia, na mdada
naye akaja kupigwa na kitu kama hicho hicho kichwani, ina maana kulikuwa na mtu
mwingine ndani, kwanini wewe hukumuona?’ akauliza
‘Mimi
nilipozindukana,nilichojua ni kukimbia, sikuwa na wazo la kuwa kuna mtu
mwingine humo ndani, wazo hilo nimelipata wakati mnanihoji, ....kwa muda huo,
niliyekuwa namuogopa hapo ni mdada, ukimuona alivyokuwa hata wewe ungelikimbia,
kiukweli, sikuwa na wazo la kuwa kuna mtu mwingine humo ndani,..’nikasema
‘Ngoja
tuanze hivi.....’akasema na wakili wangu aliposikia hivyo akasema;
‘Umeshamuhoji
mteja wangu vya kutosha huwezi kuanza tena upya...’akanitetea wakili wangu .
‘Nataka
tuliweke hili sawa, kutokana na maelezo ya mlinzi, ni kuwa mtu aliyeonana naye
wakati anakuja kutoa taarifa ya mgeni, ni mtu tofauti na wewe, kama
alivyomuelezea kuwa ana ndevu, kavaa viatu vya wazi, na alikuwa na nguo tofauti
kabisa na ulizokuwa nazo wewe...’akasema huyo askari mpelelezi
‘Mimi hapo
sijui.....huyo mtu mwingine sikumuona...’nikasema na huyo mpelelezi, akauliza
‘Wewe ndiye
uliyeongea na mlinzi, ukaenda kuchukua huo mzigo, kwa mtoza ushuru ndio au
hapana?’ akauliza
‘Ndio
mimi...niliyefanya hivyo?’ nikasema
‘Wakati
unaonana na mlinzi,ulikuwa umevaa nguo hizo hizo za awali au ulibadilisha?’
akauliza
‘Nilikuwa
nimevaa nguo hizo hizo, sikuwahi kubadilisha nguo, kwanini nibadilishe nguo,
hapo sio nyumbani kwangu,....’nikasema
‘Kwahiyo
wewe una uhakika kuwa kulikuwa hakuna mtu mwingine humo ndani zaidi yako ?’
akauliza
‘Mimi siwezi
nikathibitisha hilo,.. maana kama mlinzi aliona mtu mwingine, basi ina maana
kweli kulikuwepo na mtu mwingine, lakini mimi sikuwahi kumuona...’nikasema
‘Kwa
maumbile ya mwili kama alivyosema huyo mlinzi, ni kuwa maungo yenu, maumbile ya
mwili, sio sura, mnalandana, kuna mawili hapo, wewe uliabadili nguo, ukaweka
ndevu za bandia,...ili kutokujulikana na huyo mgeni wenu, au kujificha ili
mlinzi asikutambue, ama kuna mtu aliyeshirikiana nanyi, na hamtaki ajulikane...’akasema
‘Hizo ni fikira
zako mkuu, naomba umuulize mteja wangu kwa mambo ambayo aliyafanya na
kuyaona,...hayo utathibitisha mwenyewe kwenye kazi zako...’akanitetea wakili
wangu.
‘Ni kweli
nitayafanyia kazi,...ila nina uhakika, kuna mchezo uliochezwa kati ya mdada na
huyu mteja, wako, kuficha ukweli,....na kama kulikuwa na mtu mwingine, basi
huyo ndiye aliyemuua mtoza ushuru, ...ukiunganisha matukio..’akasema na akawa
kama anafikiria kitu, halafu akasema;
‘Swali hapa,
inawezekanaje huyo mtu aingie bila mlinzi kumuona, na huyu mteja wako, anasema
hakumuona mtu mwingine humo ndani....huoni kuwa kuna kitu kinafichwa hapa..’akasema
kama anauliza
‘Kwanini
ifanyike hivyo....na kitu gani kinafichwa hapo?’ akauliza wakili.
‘Nilitaka
kuongea na mteja wako ili anisaidie kwa hilo, na ili nione kama kweli hahusiki,
na kama angenisaidia kuniambia ukweli, na kuthibitisha kuwa kweli kulikuwa na
mtu mwingine humo ndani, basi yeye angelikuwa hahusiki tena, tungekuwa na kazi
ya kumtafuta huyo mtu mwingine, ...’akasema
‘Hiyo ni
kazi yenu,....’akasema wakili
‘Ndio hiyo ni
kweli, hiyo ni kazi yetu, lakini kwa raia mwema, anawajibika kuwa mkweli, ili
haki itendeke, unapoficha ukweli, ina maana gani, ni kuwa wewe unahusika, kwa
njia moja ama nyingine kama sio moja kwa moja...’akasema
‘Hayo
utayathibitisha mahakamani, mimi nina imani kuwa mteja wangu hana hatia,
....kama huna maswali mengine naona unipe nafasi nataka kuongea na mteja
wangu...’akasema wakili.
‘Kwa hali
hiyo basi, kesho huyu mteja wako inabidi aende gerezani, haitawezekana
kuendelea kukaa hapa, kwa utaratibu ulivyo, tulimchelewesha hapa ili aweze
kuisaidia polisi, kumpata huyo mtu mwingine, ambaye tulifahamu kuwa yeye
atathibitisha kuwa kulikuwa na mtu mwingine humo ndani, kwa vile sasa
kathibitisha kuwa hakukuwa na mtu mwingine, basi yeye na mdada ndio
walioshirikiana kumuua mtoza ushuru...’akasema.
‘Thibitisha
hilo kwa ushahidi, sio kwa dhana, usimtwike mteja wangu kwa kosa ambalo
hajalifanya, ...na kwa vile hamjakuwa na uhakika kuwa mteja wangu ndiye
anayehusika , basi dhamana ni haki yake....’akasema wakili
‘Hawezi
kupewa dhamana, ..kwa hali jinsi ilivyo, angelipewa dhamana kama angethibitisha
kuwa kulikuwa na mtu mwingine zaidi yake, ...kwa vile hajathibitisha hilo, huyu
tunamweka katika fungu la muhusika mkuu, aliyetenda hilo kosa, na muuaji,
hawezi kupata dhamana kwa sasa, kwanza kwa usalama wake, pili, anaweza kufanya
lolote kuficha ukweli...’akasema huyo mpelelezi.
‘Kwa akuli
yako umesema hamjawa na uhakika, kuwa mteja wangu anahusika, bado mnamtafuta
huyo mtu mwingine, kuendelea kumshikilia ni kumuonea, ....kwahiyo dhamana ni
haki yake...’akasema wakili.
‘Tutalithibitisha
hilo kuwa kweli mteja wako na mdada wanahusika,....ushahidi huo tunao...’akasema
‘Thibitisha...kwani
kama ungelikuwa na uhakika huo usingelikuja hapa kumhoji tena..’akasema wakili
‘Mteja wako,
alikwenda kumuona huyo mgeni,kama alivyoagizwa na mdada kwenda kuchukua huo
mzigo,.... wakapeana hiyo mizigo, huyo mgeni akagundua kuwa kapewa tofauti na
makubaliano, akakasirika na kuchukua bastola, akaingia na mteja wako ili
kukabiliana na mdada, ...wakati mtoza ushuru, ambaye ndio huyo mgeni, akizozana
na mdada, mteja wako, akapata nafsi ya kumuumiza huyo mgeni, na bastola
ikamtoka...’akatulia.
‘Kwahiyo
bastola akawa nayo mteja wako, ....mtoza ushuru akawa hana ujanja,..hata hivyo,
inavyoonekana ni kuwa mtoza ushuru alijaribu tena bahati yake ya kujitetea, pale alipopata hiyo nyundo na kumgonga nayo
mdada kichwani, mdada akadondoka na kupoteza fahamu...’akatulia
‘Wakati
anakwenda kupambana na mteja wako, mteja wako ikabidi atumie hiyo silaha na
kumpiga risasi mtoza ushuru, na alipogundua hilo akabaki ameduwaa, hakujua kuwa
mdada kazindukana, na mdada alikuwa
keshachukua ile nyundo akamgonga nayo mteja wako kichwani..., mteja wako
akadondoka, na hapo mdada akawa na hiyo bastola..’akasema
‘Mteja wako
alipopata fahamu, na wakati huo mdada hali yake ya kuchanganyikiwa ilikuwa
inaanza kurudi, na kama wanavyosema , ile hali yam dada, ya kuchanganyikiwa
ikiisha, huwa anadondoka chini na anakuwa kama kapoteza fahamu ....mteja wako
alipoona hivyo, akapata nafasi ya kukimbia....’akasema huyo mpelelezi.
‘Hizo ni
hisia zako,...unaweza kufikiria vyovyote, hujaonyesha kwa vielelezo, kwa
ushahidi wa kihalisia,... unaweza kuthibitisha kwa ushahidi wa vielelezo?’
akauliza wakili
‘Kila kitu
kipo tayari, nilichokuja kumuona mteja wako, ni kuona kama kweli anayosema ni
sahihi, na kama kweli ana uhakika hakukuwa na mtu mwingine humo ndani...na kama
tulivyoona sisi kwa ushahidi tulio nao, mteja wako ana hatia, ....akishirikiana
na mdada japokuwa mdada, ana utetezi wa hali yake ya kiafya...na hapo inamuacha
mteja wako kuwa mhusika mkuu....’akasema
‘Basi kama
mna ushahidi huo, tutaonana mahakamani, lakini kwa hivi sasa mteja wangu ana
haki ya dhamana, hamjathibitisha kuwa yeye ndiye aliyefanya hivyo kwa vile kuna
utata... kuwa kulikuwa na mtu mwingine, na kihalisia ndivyo ilivyo,...'akasema
'Na ukiangalia mtiririko wa hayo matukio, mteja wangu asingeliweza kuyafanya yote hayo kwa wakati
mmoja, kwa muda huo mfupi, na kwa
maelezo yenu, kutoka kwa kauli ya mlinzi,inaonyesha wazi kabisa kuwa kulikuwa
na mtu mwingine aliyekuwa na ndevu,....na hata nguo alizokuwa kazivaa ni
tofauti...'akatulia akageuka kuniangalia na kusema;
'Je kwa kumshikilia hivi, ina maana huyu mteja wangu, ndiye huyo mtu, hapana, kwa dalili hizo, na kwa jinsi tukio lilivyokuwa, sio yeye kabisa, kazi
ni kwenu kumtafuta huyo mtu mwingine,na wakati mnafanya hivyo, hamuwezi
kuendelea kumtesa mteja wangu kwa kumshikilia, dhamana ni haki yake .....’akasema
wakili.
‘Inawezekana
kabisa huyu mteja wako alivaa ndevu za bandia...na kubadili nguo, ikionyesha
kabisa kuwa walikuwa na dhamira hiyo, ....haiwezekani huyo mtu mwingine apite
pale getini mlinzi asimuone, haiwezekani kabisa kwasababu ukuta wote
umezungushiwa waya za umeme, na tumeona kwenye kumbukumbu za huo mtambo wa
usalama, umeme haukuwahi kuzimwa,...sasa huyo mtu mwingine alipitia wapi....?’
akauliza
‘Hiyo ni
kazi yenu kutafuta ili kuhakikisha kuwa haki inatendeka, ...’akasema wakili.
‘Hilo
tutalithibitisha mahakamani, hatuna shaka nalo,haki itatendeka, na muhusika
atahukumiwa ...na kwa hali hiyo mteja wako kesho anakwenda gerezani,...’akasema
‘Hapo
mtakuwa hamjatendea haki mteja wangu, inabidi tukutane na hakimu kuliangalia
hilo, dhamana ni haki ya mteja wangu...’akasema wakili
‘Tutaona itakavyokuwa,.....kama
mnataka hivyo, tutakutana mahakamani kuona kama kweli mteja wako anastahiki
hiyo dhamana,...lakini wakati hayo yanafanyika hatuwezi kuendelea kukaa na huyu
mtu hapa kituoni, sheria zipo wazi, kesho anakwenda gerezani...’akasema huyo
mpelelezi na kuondoka.
**********
‘Usijali
hiyo ndio kawaida ya hao watu, inabidi wafanye hivyo, vitisho, mashinikizo,
kudhania,....wakijua kuwa kama unahusika, utaghadhibika na kuanza kuropoka
ovyo, ....’akasema wakili.
‘Kwahiyo ina
maana kweli kesho watanichukua kunipeleka gerezani?’ nikauliza
‘Hawataweza
kufanya hivyo, nina uhakika kuwa bado hawajawa na uhakika na ushahidi wao, na bado
wanakuhitaji kuhakiki maelezo yao, cha muhimu, usikubali kabisa kuongea nao bila
kuwemo wakili wako,...mpaka sasa kinachowachanganya ni huyo mtu mwingine, hata
mimi najiuliza kuhusu huyo mtu mwingine, je ni kweli hakukuwa na mtu mwingine
zaidi yako wewe na mdada?’ akaniuliza
‘Mimi
sikuwahi kumuona huyo mtu mwingine....lakini inavyoonekana ni lazima kulikuwa
na mtu mwingine ambaye aliweza kumgonga mdada na nyundo na kufanya hivyo
kwangu...’nikasema
‘Aliingia
kwa kupitia wapi?’ akauliza
‘Huenda
aliruka ukuta...’nikasema
‘Nilifanya
utafiti huo kwa kuchunguza ule ukuta,....sio rahisi mtu kuruka juu, labda kuwe
na mawasiliano ya kuzima umeme.., na hilo lingelifanyika ndani...ina maana kuwe
na mtu wa nje na ndani wanawasiliana kuwa azime umeme na alipoingia huyo mtu ,
wakauwasha kabla kelele hazijaanza kusikika, ni kitendo cha haraka sana, hata
hivyo kumbukumbu zake,hazionyeshi hivyo ...’akasema
‘Hapo mimi
sielewi..kumbukumbu gani hizo?’nikauliza
‘Umeme wa
ulinzi uliopitishwa kwenye hizo waya, unaunganishwa na vyombo vilivyopo ndani,
ambapo, kila tukio la kuzima au kuwashwa hujionyesha kwa muda wa tukio hilo, na
hali kama hiyo inakuwepo huko kwa watu wa ulinzi walioweka hizo nyaya za
usalama,.... hakukuwa na kuzima au kuwashwa kwa muda huo, limethibitishwa hilo,....kwa
wiki nzima, hakujakuwa na kuzimwa kwa umeme kwa huduma hiyo ya ulinzi...’akasema
‘Kwa hali
hiyo, kama kuna huyo mtu, basi atakuwa kapitia pale pale getini, sasa ilikuwaje
apite bila mlinzi kumuona, je kuna muda mlinzi alitoka, kwa kumbukumbu za
mlinzi, hakuwahi kutoka muda wote huo, na anasema alikuwa pale pale mlangoni
kwa muda wote huo....’akasema
‘Mna uhakika
gani kuwa mlinzi anasema ukweli?’ nikauliza
‘Kutoka na
historia ya huyo mlinzi, ni mtu anayeifahamu sana kazi yake, na ana kumbukumbu
ya hali ya juu, ...labda..’akatulia kidogo akiwaza
‘Labda nini?’
nikauliza
‘Aweze
kumpitisha mtu, kwa urafiki au kuhongwa,...na kwa maana hiyo atakuwa
ameshirikiana na hao watu, kitu ambacho hakiwezekani kutokana na jinsi anavyofahamika
huyo mlinzi, ni mwaminifu na mchapa kazi...’akasema na mimi hapo akili
ikanikumbusha kutokana na tabia ya huyo mlinzi, nikasema;
‘Hilo la kuhongwa
inawezekana,huyo mlinzi naona kama ana tabia hiyo...na kwa maisha yetu, unatoka
nyumbani huna kitu, una majukumu mengi, unafikiri huyo mlinzi hawezi kuhadakika
kwa pesa nzuri, akawa kampitisha mtu...kwa pesa, mimi nahisi atakuwa kafanya
hivyo...’nikasema
‘Una uhakika
gani na hilo?’ akauliza
‘Niliwahi
kuongea na huyo mlinzi kabla, siku ya mwanzo kufika hapo kwa mdada, aliniambia
kuwa wakati mwingine anakuwa na hali ngumu..., na mdada hapendi kusumbuliwa,
lakini mtu aliyekuja ana jambo muhimu la kuonana na mdada, alisema kama
atarizika na huyo mtu, kwa njia ya kumsaidia huyo mtu, yeye inabidi kwenda
kuonana na mdada, anakwenda kumbebembeleza mdada, ili aonane na huyo mtu..hapo
unafikiri atafanya hivyo bure....’nikasema
‘Uliwahi
kufanya hivyo kwake?’ akaniuliza
‘Nilifanya
hivyo kama kumsaidia, aliponielezea kuwa siku hiyo hana kitu, lakini sio kwa ajili ya kumuona mdada, maana
siku nilizofika hapo nilifika nikiwa na miadi na mdada, sijawahi kufika bila
kuwa na miadi naye...’nikasema.
‘Kama ni
hivyo, ....hapo ninahisi, inawezekana kulikuwa na mtu mwingine
aliyeingia...inabidi nilihakiki haraka iwezekanavyo, kama hamna,kuna kazi kubwa
sana, inabidi uniambi ukweli ulivyokuwa kabla kesi hii haijafika mahakamani...’akasema
‘Kwa vipi?’
nikamuuliza
‘Kutokana na
ulivyoniambia,...kama huyu mlinzi analalamika hali ngumu, na sasa yupo kwenye
wakati mgumu, hana pesa, naweza kuupata ukweli kwa njia hiyo, na kama
nitafanikiwa kuupata huo ukweli, basi tutakua kwenye nafasi nzuri ya kuimaliza
hii kesi mapema..’akasema
‘Mimi hapo
sina uhakika bado...sikuwahi kumuona huyo mtu mwingine..’nikasema nikijaribu
kuziita kumbukumbu za tukio lile.
‘Kama ni
hivyo, basi...itabidi tupambane mahakamani bila ya uhakika...unapigaan bila
silaha, lakini kama uliyosema ni kweli, tutashinda tu...’akasema
‘Hata hivyo,
mbona huyo askari mpelelezi anaongea kama ana uhakika fulani, ni kama wana
ushahidi mkubwa ndio maana ananishinikiza kwa kosa ambalo sijalifanya,
anavyoongea utafikiri alikuwepo, akaona jinsi ilivyo kuwa, anajitungia tu
habari zisizokuwepo, mbona hawa watu wananitaka ubaya...’nikasema
‘Ndio hapo unapoona
umuhimu wa kuwepo mawakili,...watu wengi hapa nchini hawajaona umuhimu wa
mawakili, na kwasababu hiyo haki zao, zinapotea bure,na wengine wanajikuta
wakihukumiwa kwa kosa sio lao...angalia kwa hili, kama nisingelikuwepo hapa,unafikiri
ingelikuwaje...’akasema kama anauliza
‘Wangenifunga
kwa kuleta vurugu, maana ni lazima ningekosana naye, hawezi kusema kuwa mimi
nimeua, wakati sijafanya hivyo, ananitia hasira sana, nasota humu ndani wakati
sijafanya kosa,...na ni nani huyo muuaji, na kwanini aumie mtu mwingine wakati
huyo muuaji yupo nje, watanilipa nini kwa hii adhabu wakija kumgundua huyo
mtu...’nikawa kama nauliza
‘Wakati
mwingine ili kupata ukweli, ...inabidi iwe hivyo, inabidi watu wasio na hatia
kuumia kwa muda, kwa ajili ya kufichua ukweli uliofichika, kwa vile ukweli na
haki una mitihani mingi, kwasababu ya dhuluma kuwa jambo la kawaida kwa watu,....pole
sana, ...’akasema
‘Na mtaonana
saa ngapi na huyo wakili aliyemleta mdada....?’ nikamuuliza nilipomuona
akijiandaa kuondoka
‘Muda
wowote, lakini nina shaka, huenda asikubali kuonana na mimi....’akasema
‘Kwanini?’
nikauliza
‘Hata siku
moja, maji na mafuta hayapatani....katika kazi yetu hii nimejifunza mengi, kila
fani ina mitihani yake, na fani yetu hii imeingiliwa na wajanja wajanja, ....na
mtu wa namna hiyo anaogopa sana kukutana na yule mtaalamu wa ile fani,kwani
anajua ataumbuliwa....hata hivyo nitajitahidi nionane naye, ili nione yeye
kagundua nini, ...’akasema
‘Una uhakika
kagundua kitu?’ nikauliza
‘Kama yupo
karibu na mdada, uwezekano huo upo, na kwa kumtumia yeye huenda nikawa na
nafasi ya kufichua ukweli wa hili tukio, nahisi kuna mengi yamejificha hapa,
japokuwa hata wewe hujaniambia ukweli ninaohisi upo...’akasema
‘Ukweli gani
huo...?’ nikauliza
‘Ukiwa
tayari kuniambia , utakuwa umesaidia mengi sana, na jinsi unavyozidi kuchelewa
kuaniambia ndivyo unavyozidi kuweka mazingira ya hii kesi kuwa ngumu, na
usipokuwa makini, unaweza ukahatarisha hata maisha yako mwenyewe...’akasema
‘Kwa nini
unasema hivyo?’ nikauliza
‘Kutokana na
uzoefu wangu, na kesi kama hizi,....watu hawa hawataki siri yao igundulikane,
na wakiona kuna mtu anaweza kuwatia matatani, hawasiti kumuondoa duniani....na
wewe upo kwenye hiyo hatari..’akasema
‘Lakini mimi
sihusiki na hao watu, na wala siwajui hao watu ni akina nani...’nikasema kwa
kulalamika
‘Kama kweli huhusiki
ungelishaniambia ukweli,....kuficha kwako ukweli inaonyesha unafahamu mengi, na
hayo unayoyafahamu ndiyo yatakayokuweka pabaya, yanaweza kuwa kisu cha
kukumaliza wewe mwenyewe, ...’akasema na kuniangalia kwa makini
‘Mbona
unanitisisha muheshimiwa...’nikasema
‘Wakati
mwingine , ndio maana naona ni heri ubakie hapa hapa, ukipelekwa gerezani
sizani kama utakuwa na nafasi ya kwenda mahakamani, unaweza ukapotelea huko
huko, ndio wasiwasi wangu mkubwa, ...na pia...hata ukipewa dhamana, inaeza
ikawa ni hatari zaidi,hapo najikuta kwenye mtihani wa jinsi ya kukutetea...inabidi
nikuambie huo ukweli, ili uone hali ilivyo, sio kwamba nakutisha, .....maisha
yako yapo kwenye hatari kubwa...’akasema
‘Kwanini
unasema hivyo,...unaonekana kama unawafahamu hao watu?’ nikauliza
‘Hii kazi
sijaianza leo, ...na kiukweli mimi mwenyewe nilishawahi kuingizwa kwenye mikono
ya hao watu, lakini baadaye wakaona sifai,...mitego yao mingi niliweza
kukwepa,...japokuwa wakikukamia, huwezi kukwepa, nahisi waliona sio mtu
wanayemtaka, wana akili ay kumsoma mtu...’akasema
‘Ni watu
gani hao?’ nikamuuliza
‘Cha muhimu
ni wewe uwe mkweli,..sijui kwanini, mimi naumiza kichwa changu kukusaidia wewe,
lakini wewe unakuwa kama vile huna shida,huioni hatari iliyopo mbele yako,...sielewi,
na kila mara ninapokutana na hizi kesi, nakutana na watu wa aina yako..too sturbon(mkaidi, mtukutu).’akasema
akishikashika kichwa.
‘Kiukweli, nimechoka
kufanya kazi za aina hii, na huenda ikawa kazi yangu ya mwisho kufanya, nataka
niachane kabisa na hizi kazi za namna hii,...ni hatari tupu...na kabla
sijafanya hivyo, nataka niweke historia,...hili kundi ni lazima lipatikane,...’akasema
huku akisimama kuondoka
‘Kundi,..kundi
lipi hilo,...!?’ nikauliza kwa mshangao na yeye hakunijibu akawa anaanza
kuondoka, na nilipoona hivyo nikauliza;
‘Sasa muheshimiwa,
mimi nitegemee ni nini?’ nikauliza
‘Inawezekana
upo ndani ya hilo kundi bila ya wewe kujijua, ukawa unatumiwa, lakini anyway, yote ni wewe tu, nikuambie
ukweli, ni ukweli wako tu, ndio utakaoweza kukuokoa, vinginevyo, utaniambia, kama utakuwa na nafasi
hiyo ya kuniambia, vinginevyo, huenda ikawa historia kuwa kulikuwa na mtu kama
wewe...’akasema na mara nikasikia mtu akiongea, na yeye akawa keshafika
mlangoni, na alipoangalia huko nje, akageuka na kuniambia;
‘Wakili wako
huyo .....kaja,..na kumbuka kazi niliyokupa, hujanipa taarifa bado,....’akasema
na kuondoka, huku nikiwaza ni kazi gani aliyonipa, na huyu mtu ana maana gani,
mbona ananitisha hivi,...
‘Mhh, naanza
kuogopa....’nikasema na mara wakili huyo mwingine akaingia.
‘Mdada
anasema hivi, huhitaji wakili mwingine,...huyu wakili wako hakufai, uachane
naye, vinginevyo, ....’akaanza kuongea kabla hatujasalimiana.
NB: Mtandao
, mtandao,...hata sijui nifanye nini..ok, hata hivyo, nimejitahidi kufanikisha
sehemu hiyo, ninachoweza kuwaambia wapendwa wangu, ni ijumaa njema na kuwatakia
wikiendi njema
WAZO LA LEO: Sio kila anayekuchekea ni rafiki wako
wa kweli, ndio maana wengine husema `hapendwi mtu hapa, kinachopendwa leo ni pesa,
kinachopendwa leo ni mali, na utajiri, utu hakuna tena.
Ukitaka kulijua hilo hebu jipime wewe mwenyewe,
kwa kuangalia mali ulizo nazo na jinsi ulivyoweza kuzipata, kama hakuna doa la
uchafu wa dhuluma,kuwa kwa namna moja au nyingine ulitenda isivyo halali ili kufanikisha kuupata utajiri huo, au mali hiyo. Ukweli ni mgumu, lakini
ukiangalia kwa makini,utaligundua hilo.
Imefikia
hatua hata haki yako ili uipate unajikuta kwenye mtihani wa kuinunua. Hii ina
maanisha nini, ni kuwa dhuluma imeshaota mizizi, ili upate,...unatakiwa
upatikane,..ilivyo ni kuwa watu hawaogopi tena kuitenda dhuluma, ilimradi
hugunduliki, mwenye nacho anataka
zaidi, na asiyekuwa nachao anaota ndoto na yeye apate hata kama kupata huko nikwa dhuluma, .....hii
ni hatari.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment