Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, December 18, 2013

Mkuki ni kwa Nguruwe-50


`Je unamuafiki huyo shahidi aanze?’ akaniuliza mwenyekiti, na mimi kwa vile sikuwa namfahamu huyo shahidi ni nani hasa, nikajikuta nimeshikwa na kigugumizi cha kujibu, na mwenyekiti akaligundua hilo, akasema;
‘Aitwe huyo shahidi, tumalize mambo haraka, ...’akasema

Kila mmoja alikuwa na hamu ya kumuona huyo shahidi, na wengine walipumua, kwani hakuna aliyejua ni nani ataitwa kama shahidi, na hadi aple mlango unagongwa, wengi bado walikuwa kwenye kutafakari, na kuwazia ni nani huyo binti na atazungumza nini, au kilimtokea nin hadi aitwe kama shahidi.

Mlango ukafunguliwa, na akaingia binti, akiwa kavalia kiheshima na mkononi alikuwa kashika bahasha, na  , hakuwa na kitu kingine, kwanza kwa aibu alipoingia pale mlangoni, hakujua afanye nini, alishikwa na butwaa hasa alipoona watu wote wamegeuza kichwa kumuangalia yeye,...

‘Sogea huku mbele...’ilikuwa sauti ya mwenyekiti, ndiyo iliyompa nguvu na sauti hiyo ilimshitua mume wangu aliyekuwa kainama, sijui alikuwa akiomba au alikuwa akifanya nini, maana tangu azozane na wakili wake, yeye alimua kuinama, na kukaa kimiya, ...

‘Wewe umefuata nini huku...’sauti iliyowafanya watu wageuka, na kuangalia muongeaji ni nani, hakuwa mwingine bali alikuwa ni mume wangu, ambaye alikuwa kasimama nusu, huku akiyatoa macho yasiyooamini kile anachokiona, na mwenyekiti akawa anaangalia hili tukio kwa hamasa ya aina yeka, na mimi kwanza nikatabsamu kuwa shahidi aliyeletwa anastahili, lakini nikajikuta nikiingiwa na huzuni.

‘Haya huyo hapo shahidi wako wa kwaza, unataka uendelee naye mwenyewe, au nishike usukani..?’ akauliza mwenyekiti, lakini mimi niliishiwa nguvu, nilibakia nikiwa nimwangalia yule binti, sijui ilikuwa ni huruma, hasira, au nini sikuweza kuongea, kilichotokea ni mimi kuangusha chozi..

Mwenyekiti akaiona ile hali, akaamua kuendelea mwenyewe, akasema;

‘Kweli inauma, hii isikie kwa mwenzako tu, lakini ukitendewa wewe utaona uchungu wake, na hasa utendewe na mtu unayemwamini, hukutgemea kabisa,...lakini ndio ilivyo, tuweni makini sana, ..hasa nyie wanawake, nawaasa muwe makini sana, na wafanyakzi wenu wa ndani, msipende kuwaacha na waume zenu kwa muda mrefu, au kuwapa kazi ambazo sio stahiki zao...hata hivyo, sio kwamba nasema wanaume wote wana tabia hiyoo chafu, ..hapana, muulizeni mke wangu...’akasema mwenyekiti na watu wakacheka.

‘Huyu hapa mbele yenu ni shahidi, anayezihirisha, urijali wa mume wa familia, hachezi mbali, yeye aliamua kucheza na humo humo ndani, ...jamni huyu sio sawa na binti yake, labda niseme, huyu sio sawa na mdogo wake,....yeye aliamua kula kuku na mayai yake....sitaki kupoteza muda, ngoja tuanze na huyu shahidi wetu...’akasema mwenyekiti.

‘Hebu tuambia jina lako,....na usiogope, hata tunachotafuta ni haki yako,ukiogopa haki yako yote iatpotea, na waliokuharibia masiha yako wataendelea kuyafanya haya kwa watu wengine, ...sisi tunataak haya yakomeshwe, na hili tunaweza kulianzia majumbani kwetu, kama hivi,..likitokea jambo, mkosaji aitwe, aadhibiwe, ikishindana, apelekwe kunakostahiki,...’aaksema mwenyekiti.

‘Haya jitambulishe mpendwa,...’akasema mwenyekiti.

‘Mimi naitwa Tabia...’akasema kwa sauti ya kinyonge

‘Tabia,..tabia yako ni ya upole, au sio, mchapakazi, au sio, ...sasa nasikia kuna kitu kilitokea, wakati unafanya kazi kwenye nyumba moja, kilipotokea ukakimbia jiji, ni kwanini ulikimbia jiji...?’ akamuuliza mwenyekiti.

‘Sikukimbia jiji, niliambiwa niondoke, la sivyo yatanikuta makubwa, na...na...’akasita kuongea

‘Hebu sasa tuanze, maana nilikuwa nakuweka sawa, hebu niambie, wewe ulikuwa ukifanya akzi wapi , na kwa nani/’ akaulizwa

‘Mimi nilikuwa mfanyakazi wa ndani wa nyumba, ya ya...’akageuka kuniangalia mimi

‘Ya mke na mume wa familia tunayoiongelea ..ngoja nimsaidie...’akasema mwenyekiti.

‘Ulifanya kwenye hiyo nyumba kwa muda gani?’ akaulizwa

‘Kwa zaidi ya mwaka mmoja...’akasema

‘Hebu niambie, wakati upo hapo, kulitokea nini, kilichokufanya uondoke, uliamua kuacha kazi , kwa vile umepata mume huko kwenu au ilikuwaje?’ akauliza mwenyekiti.

‘Niliondoka baada ya kugundua kuwa nina uja uzito...’akasema na watu wakaguna

‘Jamani msigune, ndio hali halisi, na tunapoongea hapa watu wanafikiria tunamuonea mlalamikiwa, sasa ngojeni masikie wenywe, haya tuambie, unasema ulipata uja uzito, kumbe wewe badala ya kufanya kazi za ndani ulikuwa ukifanya uhuni na wavulana wa mitaani eehe...’ aaksema mwenyekiti kwa sauti ya nzito, kama kumtisha huyo binti.

‘Hapana mimi sio muhuni, sijawahi kufanya uhuni na mvulana yoyote, ...’akasema

‘Unasema hujawahi kufanya uhuni na mvulana yoyote, sasa hiyo mimba uliipaat kutoka mbinguni, hebu sema ukweli, ...’akasema mwenyekiti

‘Mimi nilikuwa smjui mwanaume, yoyote, nilikuwa nafanya kazi zangu na sikupena haya yaotokee, ..niliapa kwa mama yangu kuwa sitakuwa muhuni, na nilipochukuliwa na ....wazazi wangu hawo, nilijua kuwa nimefika mahali salama....sikutarajia kuwa hayo yangelitokea,....akaanza kusimulia;

***********

Mama yangu ni mjane, baada ya kufariki baba, kwa ghfla,sisi tulibakia na mama kwenye kiban kibovu tu,tukiwa watoto watano, na alituacha tukiwa masikini sana, mama akawa anaangaika sana kututafutia riziki, na sisi japokuwa tulikuwa wadogo, lakini tulijijua kuwa hatuna mtu atakayetusaidia, kwani baada ya msiba, vitu vilivyokuwepo vichache viligawanywa, na wanandugu wakachukua kile walichoona kinawafaa, tukabakia mikono mitupu.

Mimi nilikuwa mkubwa ukilinganisha na wadogo zangu,kwani mimi nilikuwa mtoto wa kwanza nna kwa vile ni mwanamke , nilionekana mkubwa kidogo, basi ikawa kazi kubwa ni kumsaidia, kila tukitoka shule tunajipanga, huyu afanye hiki na yule afanye kile, ili tu tuweze kumpunmguzia mama kazi za nyumbani..

‘Kazi kubwa ya mama ilikuwa kutengeneza vyungu, kwa kutumia udongo wa mfinyazi, alikuwa akienda huko mlimani kuutafuta na akileta anatengeneza vyungu vya kupikia, mama alikuwa mtaalamu sana wa kazi hiyo, lakini hata hivyo kazi hiyo ilikuwa hailipi, kwani akijitahidi sana anakuwa katengeneza vyungu, hata kumi havifiki, na bei za kijijini ni ndogo, ni kazi nzito, lakini tungefanyeje...kuna kipindi tunakuwa hatuna hata senti moja, nyumbani, inabidi mama aende kwa majirani kuomba hata kazi ya kulima, au kuosha vyombo ili angalau tupate pesa ya kula, ndio maisha niliyokulia hayo.

Wingi wetu, ulikuwa mzigo sana kwa mama, na ukumbuke baba alifariki akatuacha tukiwa tunasoma shule ya msingi, mimi nilikuwa darasa la saba, na wenzangu, la sita, la tano la nne, na la tatu, na wamiwsho alikuwa darasa la pili,tulipishana mwaka mmoja mmoja wa shule, japo kimuri tulipishana kidogo. Ilibidi tusome kwa shida, haat nguo za shule, zilichakaa, ikawa tunaweka viraka, na wengi walianza hata kututania, kuwa sisi ni viraka.....’akasema

Darasa la saba nilimaliza kwa shida sana, kwa vile mimi ndiye mkubwa, basi ilikuwa kama mimi ndiye msaidizi mkubwa wa mama, nilitakiwa kuamuka asubuhi sana, kumsaidia mama, ili aweze kukusanya, vile vyungu vilivyokuwa tayari, maana tulikuwa tukivichoma usiku,na asubuhi, tunavitoa ili vipoe, vingine vinavunjika, ndio hivyo tena...’akatulia.

Nilipomaliza darasa la saba tu, watu wengi wakaja kunitaka, niende nikafanye kazi kwao, kama mfanayakazi wa ndani, kutokana na jinsi walivyoniona, kuwa ni mchapakazi, sikupena kabisa niondoke nimuache mama yangu, lakini pia tulihitajia pesa kwa ajili ya kuwasomesha wadogo zangu, basi mtihani ukaanzia hapo, niende kwa nani..

Kabla hatujaamua ndio lsiku moja likaja gari, na wakaja hawa wazazi wangu , ambao mama alikubali niondoke nao,mama alisema anawafahamu vyema, na aliona kuwa watatusaidia kujikwamua kimaisha, angalau wadogo zangu waweze kusoma na kufika mbali sio kama mimi niliyeishia darasa la saba ...’akatulia.

‘Wageni hawo, waliongea na mama wakakubaliana, na kesho yake nikachukuliwa na kuja huku Dar, na kama ujuavyo, kila mmoja kule kijijini anatamani sana kuja huku, kwahiyo hata mimi nilifurahi sana, na nilishukuru kuwa nimapata kazi kwa watu wenye uwezo. Nikaiga familia yangu na wadogo zangu na mama alizidi kuniusia kuwa nifanye kazi kwa bidii nizije nikandanganyika na kuingiwa na tamaa, na kujiunga na wahuni, mimi nikamuahidi kuwa sitafanya lolote baya.

Mshahara wangu wa kwanza wote niliutuma kijiji kwa mama, na mama yangu mpya alikuwa akinijali sana, alinisaidia mambo mengi, na kuanza kunisomesha msomo ya jioni, nikaanza kuelewa maisha na jinsi gani ya kuishi kisasa, sio kama nilivyokuwa huko kijijini, na alikuwa akinisaidia kunipa peza za kuwasomesha wadogo zangu kila nilipomweleza matatizo ya nyumbani kwetu...’akatulia kidogo.

Kwakweli mimi darasani sielewi, ninachojua ni kufanya kazi, nikamwambia mama asipoteze pesa zake bure, kwania litaka kunisomesha sekondari, kiujumla kichwa changu ni kizito sana darasani, akaniuliza kitu gani rahisi ninaweza kukisomea au kukifanya, nikamwambai ufundi, na nikachagua ufundi wa kushona, na kweli huo nikauwezea sana...akaninunulia cherehani, nikawa nashona nguo hapo nyumbani, na alikuwa na mpango wa kunifungulia duka langu...lakini oh bahati haikuwa yangu....’akaanza kulia.

‘Aaah, tulishakuambia, ujikaze, mambo ya kulia hapa hatuyataki...yote ni mitihani ya maisha, unachotakiwa ni kumkabidhi mungu, ..usilie mwanangu ongea...’mama yangu akamwambia na kumpa moyo.

‘Ndoto zangu za kuwa mtu maarufu zikazimwa kama taa ya kibatili,maana nilikuwa na ndoto za kuwa mwanamitindo, nishone nguo za kila aina,lakini ndio hivyo tena yakanikuta makubwa ambayo sikuyatarajia...kwasababu ya ...ya...’akasita kusema huku akigeuka kumwangalia mume wangu ambaye kwa muda huo alikuwa kainamisha kichwa chini.

‘Hebu tuambie ndoto yako hiyo ilizimikaje, kwa maana ulikuwa unaishi na watu wenye uwezo wangeliweza kukusaidia sana tu, na nakumbuka  mwanzoni nilipowatembelea ulionekana mwenye furaha,ukasema kuwa umewapata wazazi wazuri wanaokujali...?’ mwenyekiti akauliza

‘Ndio mwanzoni mambo yalikuwa mazuri sana, sikuwa na shida, na niliwaona wazazi wangu ninaoishi nao ni kama baba na mama yangu, na kwa ujumla wao walikuwa wachapakazi kweli, hawakutaka mchezo, na wakanikuta na mimi ni mchapakazi kama wao, japokuwa ni za nyumbani, kwahiyo kila mmoja alikuwa akiamuka asubuhi anakimbilia kwenye kazi yake, hakuna muda wa kuongea, na mimi nilikuwa nafanya kazi yangu vyema, bila ya kusimamiwa,...ghafla nikahisi mabadiliko, maabdiliko hayo niliyaona kwa baba, akawa analewa sana....’akasita kidogo pale mume wangua lipoinua uso kumwangalia.

‘Usimwangalie, wewe ongea ,hana lolote kwa sasa, hawezi kukufanya lolote....’akamwambia mama, ambaye alionekana kama muongozaji wake.

‘Kabla hata ya hapo, nilipokuwa nimekaa hapo kwa mwezi mmoja tu, nilikuwa nimeshabadilika sana, mwili wangu ukawa mkubwa, nikawa naonekana msichana,m, mmmh....’akatulia na mwenyekiti akasema;

‘Msichana mrembo...eeh’akamalizia mwenyekiti

‘Ndio ndivyo walivyokuwa wakiniambia watu, lakini mimi sikujali, maana nilikuwa nafahamu ni kitu gani kimenileta hapa Dar, nikawa nawajibika ipasavyo, sikuwa na muda na watu wa mitaani hasa wavula, ambao walikuwa wakinisumbua kile nilipokuwa nikitoka, kwenda dukani au sokoni, ...huko nje niliweza kabisa kuwashinda, sikuwapa muda wa kuongea name, lakini tatizo likawa ndani,....’akatulia kidogo.

‘Ulikuwa unanyanyaswa, au hayo mabadiliko yalikuwa yapi, mpaka nyumbani kuwe ni mtihani kwako?’ akauliza mwenyekiti.

‘Baba, nilimuona  baba akinitizama kwa macho yaliyonitisha..sivyo kama ilivyokuwa mwanzoni’akasema

‘Kwa vipi hebu fafanua..na ulihisje hivyo, kwani mama yeye alikuwa hakuangalii, kama anavyofanya baba ?’ akaulizwa na mwenyekiti.

‘Ni kama ..ya tamaa, maana anakutizama mpaka unaona aibu, kuna siku nilimuuliza mama mbona baba ananitizama hivyo,mama akasema hajawahi kumuona baba akifanya hivyo, akaniambia nifanye kazi zangu, nisiwe namwangalia baba, kwani utajuaje kuwa mtu anakutizama, kama wewe humwangalii, nikaona aibu kwanini nilimwambia mama hivyo, hata siku moja nilipomuona baba ananitizama nikaona ngoja nimuulize kama baba yangu, yeye, akasema siku hizi  nimekuwa mrembo sana...’akasema

‘Kauli hiyo ikanikwanza, nikaona nimwambia mama tena, kesho yake, nilimuona baba kanikasirikia, na hakutaka hata kuitikia salamu yangu, nikahisi huenda waliongea na mama kuhusu hayo niliyomwambia, na hali ikatulia kidogo, lakini baadaye, nikaona ile hali inarudi tena, baba akawa ananifuata hata sehemu ninyofanya kazi na kuanza kunitania, mimi kwa vile niliona ni baba yangu, nafurahi,naongea naye tu, ila kwa tahadhari, kwani mama alishaniambia kuwa nisipoteze muda kwa kuongea ongea...’akasema.

`Ikazidi, kwani nilishawahi kumfuma baba akinichungulia,....’akasema na watu wakaguna

‘Akikuchungulia kwa vipi?’ akaulizwa

‘Kama nimetoka kuoga, nikiingia chumbani kwangu,kama mama hayupo, baba anaweza kuingia chumbani kwangu ghafla na kujifanya kauliza kitu, na wakati huo huenda nilikuwa nipo uchi, kwani .....’akatulia

‘Tunaelewa endelea..’akasema mama.

‘Kuna kipindi alikuwa akija usiku nimelala, na kuanza kunifunua nguo...nikishituka, anasema alikuwa akinifunika vizuri,....’akasema

‘Oh, muongo mkubwa wewe, unawadanganya watu , mimi niliwahi kukufanyia hivyo, nitakukomesha kwa uwongo wako...’mume wangu akasema kwa hasira na wakili wake akamtuliza.

‘Je alikuwa akifanya hivyo, akiwa amelewa?’ akaulizwa

‘Hapana hiyo ilikuwa mwanzoni kabla hajaanza kulewa, na alipooanza kulewa, ndio akaanza visa vyake...’akasema.

‘Haya tuambie hivyo visa vyake vilikuwaje...’ akasema mwenyekiti

‘Alianza kunitongoza...’akasema na watu wakaguna

‘Eehe, alikuambiaje, na ulijuaje kuwa anakutongoza, na wewe ulimjibuje vipi?’akaulizwa

‘Aliniambia kuwa ananipenda sana, na anataka...anataka tuwe wapenzi wa siri...’akatulia kidogo.

‘Akasema atanifundisha jinsi ya kupata raha ya mapenzi,...’akatulia kiogo.

‘Kwa kipindi kile mimi sikuwa namuelewa ana maana gani, ila akilini mwangu ikanituma kuwa huyu anataka nifanye naye kiteno kibaya, ..’.nikamwambia.

‘Wewe nakuheshimu kama baba yangu, kwanini unaniambia mambo kama hayo, yeye akasema hajanizaa, na mimi ninaweza kuwa hata mke wake, na yupo tayari kuninunulia chochote hata kunijengea nyumba ya kifahari huko kijijini,...mimi nikamwambia mimi nawaheshimu wao kama wazazi wangu siwezi kufanya jambo kama hilo, na mama yangu alinikataza kabisa kufanya huo uchafu, kwani mimi bado mdogo, na natakiwa kufanya hayo mambo nikiolewa...’akasema

‘Ulimwambia hivyo huyo baba yako, na ulijuaje kuwa anataka mfanye mambo machafu, ?’ akaulizwa

‘Ndio nilimwambia hivyo, yeye aliniambia kuwa anataka tufanye mapenzi, ...mapenzi alikuwa na maana gani, nilifahamu kuwa ananitaka kwa mambo machafu , mama alishaniambia hayo kuwa mwanaume akisema anataka kufanya mapenzi na wewe anamaana gani, ....’akasema.

‘Baba hakuchoka  kunibembeleza na aliniambia nikumwambia mama hayo anayoniomba, atahakikisha narudi kijijini na kuwa masikini wa kutupwa,...nikaaogopa sana, kwani kule kijijini kweli baba yangu huyo wanamuogopa sana....’akasema

‘Kwanini wanamuogopa?’ akaulizwa

‘Wanasema baba huyu ni tajiri na anaweza kukufanya lolote asifungwe, kwa vile ana kampuni yake kubwa, na anajuana sana na polisi...na pia anajuana sana na yule mwanasheria aliyekufa,...’akasema

‘Huyo mwanasheria aliyekufa naye alikuwa akiogopewa sana, kuliko hata baba, kwasababu wanasema anafahamu  uchawi wa kisasa, anaweza akakuangalia hivi akakuambia yoye unayofikiria kichwani mwako,anaweza kujua kitu gani ulikuwa ukifanya nyumbani kwako,,...anaogopewa sana kule kijijini, na huyo alikuwa rafiki mkubwa wa baba yangu huyu ...’akasema

‘Kwahiyo alipokutongoza alikuambia kuwa usipomkubalia atakuloga au atakufanya nini?’ akaulizwa

‘Hakusema kuwa ataniloga,yeye  alisema atahakikisha mimi na familia yangu tunasota, tutakikimbia kijiji,na kuwa omba omba...na mama yangu atakufa kwa kihoro...mimi niliogopa sana alipofikia kusema mama yangu atakufa kwa kihoro..hata hivyo sikumkubalia alivyotaka yeye...’akasema

‘Siku moja alikuja nyumbani, huwa ana kawaida ya kuja akifahamu kuwa mama hayupo, na ananiambia niache kazi zote tongee, na siku hiyo akanituma pombe, akanywa na kunilazimisha mimi ninywe, nilikataa kabisa,...kuna muda akanituma maji ya kunywa nikaenda kumletea, akanywa, na mimi nikaondoka kufanya kazi zangu , baadaye akaniita, nikashangaa ananimiminia maji ya kunywa na kuniambia ninywe, kweli nilikuwa na kiu, lakini niliingiwa na wasiwasi nikijua huenda kaweka kitu.

Akanishika kwa nguvu mpaka nikayanywa yale maji..yalikuwa hayana ladha nzuri, sijui ilikuwaje, maana niliona macho yote mazito, ...nikawa sina nguvu tena, akanibeba, hadi chumba cha akiba, akanilaza kitandani...hapo akaanza kulia ...

‘Niliumia sana siku hiyo, aliniumiza..alinishika kwa nguvu, na sikuwa an nguvu za kujitetea mwili wangu wote ulikuwa umelegea, lakini niliweka kuhangaika, na.....akaniumiza....sikuamini yaani baba yangu niliyemuamini kama baba yangu mzazi, alifikia hatua ya kunifanyia hivyo,mungu ndiye anayejua, ...nikakumbuka mama alivyoniusia, nikajitahidi kutimiza wajibu, nikawa namuogopa mungu, lakini baba akayaharibu yote hayo,..ningefanya nini, ..ina maana sisi kwa vile ni masikini wetu ndio watufanyie wanavyotaka, niliumia sana siku hiyo...’akawa anaongea huku akiwa analia.

‘Endelea, usilie, ongea ili watu wasikie, unyama wa mtu anayejiona mwema usoni kwa watu kumbe kavaa ngozi ya kondoo..’akasema mama.

‘Alipomaliza shughuli zake, akaondoka, huku akisema nikimwambia mtu ataniua, atamuua na mama yangu...sikuweza kumwambia mama, wiki nzima nikawa kama mgonjwa, nikawa nalia,hadi mama akaja kunifuma nikilia, sikuweza kumwambia, kwa vile niliogopa kuvunja ndoa ya watu, na pia kwa vile baba alinitishia kuwa nikimwambia mama atamuua mama yangu. Nilimwambia kuwa nimemkumbuka marehemu baba yangu alivyokuwa akinipenda.

‘Tatizo mama kipindi hicho alikuwa na kazi nyingi, na kila unachomuambia anakuamini, hakupenda kunidadisi sana, akanipa pole, na kunishauri kuwa nisikumbuke sana kwani hayo ni mapenzi ya mungu, halafu akaniuliza kuwa baba ananisumbau tena,...kwa kuogopa nikamwambia hanisumbui...

‘Ikapita hiyo siku, na wiki nikijua hilo limekwisha, siku moja akiwa amelewa akanijia chumbani, ilikuwa usiku akanishika kwa nguvu,....na karibu aniue, alinikaba nikafikiria kuwa huenda alikuwa anataak kuniua, nilipigana naye sana, lakini akanizidi nguvu, baadaye akaanza kunizalilisha tena, ...yaani karibu nimtapikie akwa jinsi nilivyo kuwa najisikia, harufu ya pombe na matendo yake, ...nilijua nafanyia yote hayo kwa vile mimi ni masikini, nitasema nini nieleweke kwa jamii, akafanya alichotaka akaondoka...kesho yake nikataka kumwambia mama, lakini ikashindikana, kila nilipotaka kumwambia mama, baba anakuwa karibu, na siku ikapita., Siku ikipiata unajikuta umesahahu, ukikumbuka inaishia kulia.

Basi nikaona niache tu iwe kama iwavyo, akawa akifika, usiku anajifanya halali na mama, anakuja kulala chumba chaakiba, akiona kupo kimiya anakuja kwangu..nikawa najitahidi hivyo hivyo, ila sikuwa na raha, nikawa nalia sana, na kuanza kukonda, na baadaye ndio nikagundua kuwa nina miimba..sikujua kuwa ni mimba, siku hiyo nilikwenda kupima malaria, nilikuwa najisikia vibaya sana, mama akaniambia nikapime malaria, ndio docta akaniambia nina mimba...

Nilipotoka pale nikapitia duka la dawa za mifugo nikanunua sumu ya kuulia wadudu, baada ya kuuliza na kuambiwa hiyo dawa binadamu akinywa anakufa mara moja,..akilini , nilishazamiria kujiua tu, sikujiona binadamu mwenye thamani kwenye hii dunia, kwani sikuweza kuvumilia tena,nilishaona kuwa nimefanya makosa makubwa, kwanini sikumwambia mama yangu huyo wa kufikia mapema...nilijiona mzembe, ...mkosaji asiye na maana .

Akilini mwangu, nilijua hata nikimwambia mama kwa sasa hataweza kuniamini tena, ataona mimi nilikubali kirahisi , na atanichukulia mimi ni mzinzi, Malaya. Na pia sitaweza kumwambia mama, yangu mzazi, nitamuumiza sana, mama ambaye siku zote alikuwa akinionya,nisije kujiingiza kwenye uchafu wa zinaa, je nitmwambieje mama yangu,  nikaona bora nikajiue tu....niondoke kwenye hii dunia, wabakie wenye pesa zao.

Nilipofika nyumbani nikaikoroga ile sumu kwenye kikombe cha plastiki, ilikuwa haiwezi kuonekana maji hayakubadilika rangi, nikaweka kwenye meza karibu na kitanda changu, nikachukua karatasi na kuandika ujumbe nikielezea kila kitu ilivyotokea...

Nilipomaliza hiyo kazi ya kuandika,... sikutaka nife kabla sijatimiza wajibu wangu, kwahiyo nikahakikisha nimefanya kazi zangu zote za nyumbani,...nilipomaliza nikaoga, nikamuomba mungu, nikaingia chumbani kwangu,nikaichukua kile kikombe, ambacho kilikuwa na maji niliyochanganya  na ile sumu ....

Wazo likanijia, kuwa nisifie chumbani kwangu, nikaona sehemu nzuri ya kufia ni kule kule nilipozalilishwa , nikavua nguo zangu za kawaida, nikachukua gauni kubwa jeupe, refu, lenye mikono mirefu, nikalivaa, halafu moja kwa moja nikaenda chumba ambacho baba huwa analala, nikamuomba mungu tena, na kulia, nikisononeka, na kila uchungu ulivyonizidi, ndivyo tamaa ya kujimaliza ilivyozidi kunijia, kuna muda nilikuwa nasita kufanya hivyo, nikimkumbuka mama yangu, lakini baadaye nikaona jambo jema, ni kuondoka hapa duniani, bila kupoteza muda nikanywa yale maji niliyokuwa nimechanganya na sumu...

NB: Tuendelee na huyo binti, au ..tukutane sehemu ijayo.

WAZO LA SIKU: Tuweni na ubinadamu kwa wafanyakazi wetu wa ndani, visa vingi vinaelezewa jinsi gani wafanyakazi hawa majumbani wanavyonyanyaswa au kuzalilishwa, lakini wengi wanaofanyiwa hivyo wanashindwa kuongea ukweli kwa wazazi wao kwa kuogopa , na wengi wanaofanyiwa hivyo ni watoto wa kike,wasichana.


Akina mama mnaoishi na wafanyakazi wa ndani, mliowachukua mabinti wadogo, tujaribu sana kuwa karibu na hawa wasichana, tukumbuke kuwa hawa ni watoto wa wenzetu, mama zao ni kama wewe,  tukiona mabadiliko yoyote, yasiyo ya kawaida, tutumie busara kuwahoji hawa mabinti,, huenda kuna jambo linaloendelea kwa huyo binti, mchukulie huyo kama ni mtoto wako, ujue litakalofanyika kwake ni sawa na lingelifanyika kwa watoto wako mwenyewe. Hakupenda awe hivyo, na wewe umepewa dhamana kutoka kwa mzazi wake, tusije tukaona kuwa kwa vile huyu sio mtoto wangu haijalishi sana, ...hiyo ni sawa na kusema mkuki ni kwa nguruwe tu, huwezi jua,maisha ni kupanda na kushuka,.
Ni mimi: emu-three

No comments :