Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeSaturday, December 7, 2013

Mkuki ni kwa Nguruwe-43


 Niifuata maelekezo kama walivyotaka wao, walichokuwa wakifanya ni kuniamuru, kwa kunielekeza kuwa nielekee wapi, nikate kushoto au kulia, hadi tukafika maeneo yasiyokuwa na umeme, eneo hio ilikuwa na majengo mapya mapya, na nikaambiwa nisimamisha gari, nikafanya kama walivyoniamurisha na nilipotaka kugeuka kuwaangalia ni nani, maana nilishahisi kuwa wapo wawili, kiyoo cha kuangalia nyuma walikuwa wameshakigeuza kwa juu ili nisiweze kuwaona kwa nyuma.

Wakati nataka kugeuza kichwa, mkono wenye kitambaa ukapitishwa puani kwangu na aliyefanya hivyo, akanishika shingoni kama mtu anayenikaba, na mwenzake akasema;

‘Mbona unamkaba, hukusikia bosi alivyosema, bosi alisema tusimdhuru sehemu yoyote, atajua mwenyewe ni nini cha kufanya tukimfikisha..’akasema mwenzake na hapo nikajua ni yale yale niliyotaka kumfanyia rafiki yangu, ndio yamenigeukia mimi, sikuweza kujitetea maana kile kitambaa walichoniwekea puani, kilinivunja nguvu zote, viuongo vyote vikalegea, japokuwa kwa mbali  niliweza kusikia wanachokiongea.

‘Sasa ningewezeje kumweka hii dawa...kwanza haijaingia vyema huoni bado yupo macho...’akasema na wakanishikisha kile kitambaa puani, na nlipuvuta pumzi, nikahisi nikizama kwenye giza, sikujitambua tena.

Sijui ilipita muda gani, lakini nahisi ni karibu ya saa moja au nyuma kidogo, ..nilihisi kitu kikipita puani, na hapo nikapiga chafya mfulululizo, hadi nikashikwa na kikohozi, na hapo hapo nikawa kama mtu aliyekuwa kwenye ndoto ya majinamizi, maana mwili mzima ulikuwa umelegea siwezi hata kuinua jicho, nilihisi kama mtu anataka kunikaba, au kufanya jambo, na nikawa najaribu kupambana ili niweze kumzuia, lakini sikuweza kabisa kuinua mkono,...

Ikapita muda, na taratibu akili yangu ikaanza kunirejea kama mtu anayetoka usingizini, bado wakati huo mwili mzima ulikuwa umelegea, nikajaribu kuinua mkono, mkono ulikuwa kama haupo kwenye mwili wangu mara nikasikia sauti kwa mbali, ikisema;

‘Naona kama keshaanza kuzindukana....mnaweza kumrejesha kwenye gari lake, lakini hakikisheni, anazindukana kabisa ndio muondoke, mlindeni asije akaumizwa na watu, tukaja kupata lawama, kazi tuliyomuhitajia imekamilka, kila kitu chake kirudisheni kama kilivyokuwa....’sauti ikasema

‘Bosi ina maana tumuache hivi hivi tu....’nikasikia sauti ikisema

‘Wewe ulitaka kumfanya nini, acha tamaa, za kijinga, hapa tunachotakiwa kufanya ni hivyo ninavyokuambia, kazi yetu ni kufuata maagizo, tunachohitajia sisi ni pesa si vinginevyo, hatutafuti mengine, hayo unayoyataka wewe sio utaratibu wetu, na ole wenu mumuguse, huyo ni hatari kuliko ,mnavyofikiria, ...’sauti ikasema

‘Kama ni hatari huko mbele akizindukana itakuwaje...?’ akauliza mmojawapo

‘Ndio maana nawataka mumurudishe kwenye gari lake, na hakikisha mnamkalisha kwenye kiti chake aonekane kalala kwenye gari lake, akizindukana, atajijua mwenyewe, sisi kazi tumeshamaliza, tunakwenda kuchukua mshiko wetu, ...cha muhimu hakikisheni kuwa yupo salama, na mkiona kuwa kazindukana, poteeni mbali kabisa, ukibakia hapo akikubamba, utalia mwenyewe, na ukishikwa ukafunua mdomo wako, utakuwa mgeni wa mchwa..’sauti ikasema

‘Sawa bosi tumekuelewa...’nikahisi mmoja akisema wakanibeba, na mmoja akawa anasema kichichini.

‘Huu mwili, laini namna hii, tutaishia kuubeba tu...hawa watu hawana akili kweli, ...’akasema

‘Unajua wewe utakufa kwa ukimwi, wewe unapenda mambo hayo sana, kama umelaaniwa nayo, mwili tu unakusumbua,..tunachokitafuta hapa  ni pesa, tufanye kazi yetu tulipwe, ..ukishapata pesa, watu kama hawa utawapata wengi, ....’sauti nyingine ikasema.

‘Sawa bwana,...pesa yenyewe , shilingi ngapi, ...aheri ile ya wenzetu, wabakaji, wanabaka na bado wanalipwa...’akasema.

‘Kubaka nako kazi, ..ile sio kazi ya kufanya, ni hatari tupu, na umewasikia wenzako, ...sasa hivi wanatafutwa na polisi, safari hii wameshindwa, nasikia wamepewa kazi, kabla hawajaifanya wakafumwa, ngoja wafukuzwe na polisi,karibu wakamatwe..nilikutana na yule jirani yako, akikimbia utafikiri yupo kwenye mbio za dunia, na akaniomba nauli, anataka kupotea hapa jijini.’mmoja akasema

‘Kwani walitumwa kwanani?’ mmoja akauliza

‘Kwa binti mmoja , nasikia katoka majuu usiku wa leo, hajakaa sawa wakamwingilia,kwanza walikula mkong’oto maana huyo binti sio mchezo, kilichowasaidia ni hiyo dawa ya nusu kaputi, walifanikiwa kumnusisha, hapo ndio wakamuweza, wakambeba, sasa walisahau kuwa nyumba hiyo kuna mtu mwingine,alikuwa chumba cha pili, huyo mwenzako kawapigia simu polisi..

‘Ehe, ikawaje..?’ akauliza na wakati huo, wameshanifikisha kwenye gari langu , wakawa kwenye harakati za kuniweka kwenye kiti, nilikuwa bado nimelegea lakini akili ilishaanza kufanya kazi,sikutaka kuwashitua ili nisikie ni nini wanakiongea, nikaendelea kufumba macho.

‘Basi bwana kama kawaida yao, maana wanapofanya hiyo shughuli, wanairekodi, kwahiyo walipomfikisha huyo binti kwenye kichochoro, walichoona kina usalama, wakaanza kuweka vyombo vyao vya kuchukua hilo tukio, ili wakamuonyeshe tajiri wao, wakati wanajiandaa, wapo tayari, kufanya mambo yao, mara king’ora cha polisi kikasikika, na hawo polisi walifanya hivyo makusudi, maana hawakujua hawa jamaa  wamejificha wapi...’akasema

‘Oh, kwahiyo kazi ikavurugika...wakakamatwa...?’ akauliza mwenzake

‘Wakamatwe wapi, ...tatizo lao waliposikia king’ora cha polisi hakuna aliyemwangalia mwenzake kila mmoja akajua njia yake, wakaacha kila kitu hapo, polisi wakafika na kumuokoa huyo mwanadada...na vitu vyote vikachukuliwa kama ushahidi, na mijamaa hiyo inatafutwa kama alimasi...kwasababu wanajulikana, na huyo dada anawafahamu, ...’akasema

‘Mhh, hapo kazi ipo....’akasema

‘Nafahamu kukamatwa sio rahisi, watakuwa wameshavuka milima na mabonde, hawataonekana hapa hadi mwaka upite, tatizo, hawana pesa, maana kazi hawakufanya...je wataweza kuvumilia, ...huko walipokwenda labda wakavunje nyumba za watu na kuiba, na hiyo sio fani yao....’sauti ikasema.

‘Mhh, umenitisha, kwahiyo polisi wamecharuka, ...naogopa, tuondoke zetu, kama ni hivyo polisi watakuwa kwenye patroo zao, hebu mwangali, nimemuona kama anajitingisha, keshaamuka yule, twende zetu...’sauti ikasema

‘Una uhakika..?.’akauliza mwenzake.

‘Nenda wewe ukahakikishe, unasikia ulivyo ambiwa, huyo dada sio mchezo, kwa vyote pesa na anazijua kuzipiga,,...mimi naondoka zangu...’sauti ikasema na mara kukawa kimiya, walikuwa wameshaondoka, na mimi nikajaribu kuinua mkono, na huku nikijikagua, sikuhisi maumivu sehemu yoyote, nikajinyosha na kukaa vyema, nikafunga viyoo, nikataka kutoka nje ya gari, mara nikaona gari likija mbele yangu.

Mimi nikawasha gari langu, lakini kabla sijaanza kuendesha, gari hilo likiwa limeshafika, walikuwa ni polisi, wakasimamisha gari lao karibu na gari langu, na silaha zao mikononi, mmoja akasogea kwenye gari langu na kugonga kwenye kiyoo, mimi nikashusha kiyoo, akaniangalia kwa makini akaniomba kitambulisho, nikamuonyesha leseni yangu, akaikagua halafu akasema;

‘Una tatizo lolote bosi..?’ akauliza

‘Nahisi hakuna tatizo, gari lilinizimikia , lakini naona lipo sawa...’nikasema, na sauti kavu ya kulazimisha ikanitoka, ilikuwa kama sio ya kwangu, nilihitajika kupata kitu cha kulainisha koo, na yule askari aliposikia hiyo sauti akaniangalia na kusema;

‘Sehemu hizi sio nzuri, kuna watu wabaya huku, kuna kesi nyingi za wahuni, wavuta bangi na wabakaji, kama kuna tatizo lolote, tuambie, vinginevyo, ni bora uondoke kabisa eneo hili..’akasema na mimi sikutaka kumsikiliza tena, nikaondoa gari langu na sasa nikawa na kazi ya kutafuta njia ya kurudi nyumbani.

*************

Ilikuwa ni saa nane za usiku nilipofika nyumbani, na mlinzi wangu alikuwa keshaanza kuingiwa na wasiwasi, aliponiona akanijia na kuanza kuongea;

‘Bosi, nilishaingiwa na wasiwasi, ungelichelewa kidogo inganibidi niwapigie wakubwa zangu simu, sio kawaida yako kutoka usiku, na kuchelewa kurudi kama leo, kuna tatizo lolote?’ akaniuliza

‘Hakuna tatizo..’nikasema na sikutaka kuongea na mtu nikakimbilia ndani, na cha kwanza ni kunywa dawa , ni dawa maalumu za kuvunja nguvu za madawa kama hayo waliyonunusisha puani, kwani sikutaka nibakiwe na athari ya hayo madawa waliyonipulizia puani, nilihakikisha nimeyaondoa kabisa mwilini, na baadaye nikaoga, huku nikijikagua kuhakikisha kuwa nipo salama, na kilichofuata hapo ni kutafuta usingizi, nililala hadi saa tatu, asubuhi.

Niliamusha na kelele za mlangoni, nikatoka na kukutana na msaidizi wangu wa kazini, nikamwambia sijisikii vyema, na akaniambia kuwa nina kikao cha kukutana na familia yangu, saa nne, nikamwambia asijali nitafika huko muda ukifika.....

Nilijiandaa, na nilipokuwa tayari nikaenda kuchukua laptop yangu, haikuwepo...sikuamini, maana hapo nilipokuwa nimeiweka sio rahisi mtu kuigundua, lakini imeshachukuliwa,...nikajua huenda waliochukua ni hawo watu walionikamata jana...nikatoka na kwenda maktaba,huko niliona kila kitu kipo kama kilivyokuwa japokuwa kuna dalili za kutaka kuvunjwa...

Hawa watakuwa hawo watu wa jana, na kwanini wachukue laptop yangu tu...?’ nikajiuliza, na mara nikakumbuka,.

‘Ina wezekana ni shemeji yangu, huenda alitaka kuhakikisha kuwa sina zile kumbukumbu zake za diary yake, amejidanganya...’nikasema kimoyomoyo

Wakati nataka kuondoka, nilipotoka nje, niliona boksi limewekwa mlangoni, sikulishika kwanza, nikamuita mlinzi, kwani msaidizi wangu wa mambo ya ndani, alikuwa kawapeleka watoto shule, Mume wangu alishatoka hospitalini, na alikuwa akikaa kwenye nyumbe yetu nyingine, tulikubaliana iwe hivyo.

‘Hili boksi kaweka nani hapa?’ nikamuuliza, akasema yeye hafahamu

‘Hufahamu ina maana huu mzigo umeingia wenyewe humu, kuna mtu kaingiza, wewe hukuwepo getini?’ nikauliza kwa ukali

‘Bosi nilikimbia kidogo kununua sigara, nilipokuja , sikuangalia huko , hata hivyo, ...mmh, ndio, niliona mtu akitoka waakti natoka dukani, nikajua ni wafanyakazi wako, ....kwani sio boksi lako bosi,..?’akasema

‘Haya lifungue mwenyewe, kama ni bomu utajua  mwenyewe jinsi gani ya kulitegua...’nikasema na huyo mlinzi akiwa na wasiwasi akalifungua, ...

‘Oh, ni laptop yangu...’nikasema huku nikiitoa, nikaikagua, ilikuwa haina tatizo lolote, nikaingia nayo ndani cha kwanza ilikuwa kuangalia ni ile diary ya shemeji,...kila nilipojaribu kuiifungua inasema haifunguki, haifanyi kazi, na mwisho ikasema haipo kabisa...nikajua kuwa ni huyo shemeji yangu

Kabla sijaifunga hiyo laptop yangu, nikaona ujumbe kwenye komputa ulikuwa umeandikwa kama barua pepe, ulisema;

‘Samahani sana shemeji imenibidi nitumie njia hii, ili kuzipata kumbukumbu zangu, ambazo nyingi ni mambo yangu binafsi, na si vyema watu wengine wakayafahamu, natumai ulifika salama, hakuna lolote lililotokea dhidi yako, na kila kitu chako kipo salama, japokuwa kuna vitu nilishindwa kuvichukua kwenye kabati la kaka, kaka aliniagiza, lakini hakijaharibika kitu, mtamalizana nay eye, ninachokuomba ni kumsaidia kaka, na mimi unisamehe sana kwa kutokukukutimizia yale uliyoyataka....

‘Huna adabu kabisa,unafikiri hilo ulilolifanya litasaidia kitu, tatizo huyu kijana hanielewi mimi, yeye hujui kuwa mimi ni mjanja zaidi yako...’nikasema, nikachukua kidude cha mtandao, nikaweka mawasiliano, nikaingia kwenye mtandao, nikatafuta kumbukumbu zangu, nikaona ninachokitafuta, nikafungua, nikaiona kumbukumbu  iliyoandikiwa diary ya shemeji, ipo kama ilivyokuwa...nikatabasamu, nikainakili tena kwenye laptop yangu.

Nilipohakikisha kuwa kila kitu kipo sawa, nikampigia simu, rafiki ya mume wangu, ili kuhakikisha kuwa nay eye atakuwepo kwenye kikao, kwani bado alikuwa akihangaika na mke wake,...

‘Vipi upo, maana siku hizi wewe hukai nyumbani kwako?’n ikamuuliza

‘Ni kawaida tu, ...nipo nitafika kwenye kikao, na mke wangu keshafika, alifika jana usiku, na amekubali kuwepo kwenye hicho kikao, anasema ana yake ya kuongea, baada ya hapo anarudi huko alipokuwa, sijamuelewa, tutaona baada ya kikao...’akasema.

‘Vyema kabisa, nimefurahi kusikia hivyo, je uliwahi kuongea naye lolote na akaweza kukuambia chochote.... ?’ nikamuuliza

‘Hataki kuongea lolote, anasema yote atayaweka wazi hapo kwenye kikao, ...nahisi kuna jambo kubwa linamkera, maana hata wazazi wake, wanasema kawa  mtu aliyepagawa, hana raha,...sijui ana tatizo gani...’akasema

‘Pole zake, ndivyo ilivyo, majuto mara nyingi huja baada ya kitendo, tunapofanya mambo bila kuangalia mbele,mwisho wake unakuwa mgumu, ...natumai atakuwa mkweli, na ukweli ndio utakaoweza kumsaidia...’nikasema.

‘Mhh, sijui, ni msiri sana, na hilo ndilo litakalomuangamiza...’akasema

‘Kila jambo lina mwisho wake, nina uhakika yote yatajulikana kwenye kikao, ujiandae kwa lolote lile...’nikasema.

‘Kwanini unasema hivyo, inaonekana unafahamu mengi kuhusu mke wangu?’ akaniuliza

‘Wewe ulijifanya unafahamu yangu, mbona yako yamekushinda, ...usijali, yote yatajulikana kikaoni, natumai wote watafika, wasiwasi wangu ni kuwa shemeji yangu anaweza asifike, na yeye ni mtu muhimu sana....’nikasema

‘Kwani kaenda wapi, maana hata mimi namtafuta kwenye simu hapatikani..?’akaniuliza

‘Kijana amekuwa mtoto wa mjini, anayoyafanya anayafahamu mwenyewe, na kaka yake hajui kuwa anamuharibu mdogo wake, ...nasikitika sana, kwani juhudi zangu zote zimekuwa hazina manufaa, ...’nikasema.

‘Kwani kaka yake kafanya nini cha kumsababishia yeye awe hivyo, unafahamu kutokana na mambo yangu kuwa mengi nimeshindwa kufuatailia mambi yenu,mnisamehe sana, hata wazazi wako nimewaambi hilo, ila kwenye kikao nitakuwepo....’akasema.

‘Ni muhimu sana uwepo, kama mkeo yupo, basi hatima ya yote haya itajulikana, na wasiwasi wangu ni kuwa baada ya hicho kikao huenda kusiwe na urafiki tena, ....’nikasema

‘Kwanini?’ akauliza

‘Kwasababu ukweli ni mzuri sana, lakini unauma,...’nikasema.

‘Sawa hamna shida, mimi sina tatizo,...kama kuna ukweli ninaoufahamu nitausema, kama utasaidia, ...’akasema.

‘Na hasa uwe wa kumsaidia mke wako, ...’nikasema.

‘Yah, mke wangu na wewe pia,....nikuambe ukweli, hapa nilipo nakuwaza wewe, namuomba sana mungu, itokee miujuza, ile hali ay zamani irejee,sina raha kabisa, najuta kwanini haya yametokea, inafikia hatua natamani ndoa yangu ifike mwisho tu, ili nijue moja...’akasema.

‘Ndoa wakati mwingine ni mtihani, na kufaulu kwake, ni wewe na mwenzako, ...kila mtu ana shida zake, hilo nilowahi kukuambia kuwa usione mimi Napata taabu na mume wangu, wapo watu wanapata shida sana na ndoa zao, sio mchezo, lakini mwisho wa yote ni nyie wenyewe, kila mmoja anatakiwa kuwa na maamuzi yake, na mimi nahisi kuwa maamuzi yangu yameshafika mahali pake, karibu sana kikaoni..’nikasema.

‘Haya nakuja na mke wangu,....’akasema na mimi nikaingia kwenye gari kuondoka, wakati nipo njiani nikahisi kuna pikipiki, ilionekana ikinifuata kwa karibu sana, sikusimamisha gari hadi ninafika, na yule mtu mwenye pikipiki, akanipita, na kunipungia mkono, sikujua ni nani, ...mimi nakaingia kwenye kikao

NB: Nawatakia wikiend njema,


WAZO LA LEO: Kila mtenda wema, atakumbukwa kwa wema wake, na wema daima hauozi, Blog yenu ya Diary yangu, inatoa pole kwa wenzetu wa Africa Kusini kwa msiba huo mkubwa wa kuondokewa kwa kiongozi wa kweli, Mzee Nelson Mandela, wema wake, ujasiri wake, na hekima zake, hazitasahaulika kamwe,  twamuomba Mwenyezimungu ampe makazi mema peponi. Ameen.
Ni mimi: emu-three

No comments :