Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, December 3, 2013

Mkuki ni kwa Nguruwe-39‘Bado mmoja ..’ ikawa ndio wimbo wangu wa motisha, nikijua kuwa sasa nimeshinda, iliyobakia ni kuwaweka wote wale walioamua kuvunja ahadi yao ya uaminifu hadharani, na ikibidi kuwawajibisha, mimi kama mimi nitafanya yale niliyo na uwezo nayo, nay ale yaliyojuu ya uwezo wangu nitawaachia wenyewe ,

Kiukweli ushahidi niliokuwa nao ulikuwa unatosha kabisa, kufanya lolote,  lakini kuna baadhi ya mambo nilihitajika kuyafuatilia, ili kuhakiki, na sikutaka kutumia nguvu, sana, ni hekima ndogo tu....

Tuendelee na kisa chetu.

                                                             *********

Wakati nipo nyumbani nikijiandaa kwenda kumtembelea mume wangu hospitalini, mara nikasikia kuwa nina mgeni, nilipouliza ni nani wakasema ni Inspekta wa polisi, nikajua kuwa sasa mambo yameanza kuvuja, sikutaka mambo haya yafike huko kabla sijamaliza shughuli yangu, kuna watu nilitaka kuwawajibisha wenyewe, ...kama nilivyoahidi wale wote watakaoingilia ndoa yangu wana adhabu yao, ikiwemo mume wangu mwenyewe, hili nililidhamiria kiukweli...

Nikatoka nje kuelekea bustanini, niliagiza huyo mgeni aletwe huko , na mara akaja mkuu huyo akiwa kashikilia mkoba wake, kuonyesha yupo kazini. Alikuwa mtu wa makamo, na hali yake kiafya ilionyesha sio haba, kitambi kidogo, japokuwa ukakamavu wa kiaskari bado ulikuwa kwenye damu, akasogea hadi pale nilipokuwa nimesimama, na mimi nikamsogelea na kunyosha mkono kusalimiana.

‘Samahani kwa ujio huu wa ghafla, unafahamu akzi zetu, pale unapopata taarifa unatakiwa uifuatilie, ningewatuma vijana wangu, lakini kwa heshima nikaona nije mwenyewe,...’akaaza kujieleza.

‘Nashukuru kwa kunitembelea japokuwa nilikuwa na ratiba zangu,kwani sasa hivi natakiwa kwenda kumuona mgonjwa...’nikasema

‘Oh, mume wako anaendeleaje?’ akauliza

‘Hajambo, ..yupo kwenye mazoezi tu ya kawaida, lakini kwa ujumla hajambo...’nikasema

‘Kwahiyo kumbe tunaweza kumtembea na kuongea naye?’ akauliza

‘Mhh, hayo anayeweza kuyajibu ni dakitari wake, kuna jambo mnahitaji kuongea naye,?’ nikamuuliza

‘Ni ya kawaida tu....lakini kama bado hakuna haraka sana, ....’akasema

‘Haya niambie ujio wako kwangu una makusudio geni, maana nyie watu hamji kwa mtu bila lengo maalumu, na mkionekana kwa mtu ujue kuna jambo...’nikasema.

 ‘Ni kweli, nimekuja kwa lengo maalum, lakini sio kwa ubaya,....’akasema na kutoa makabrasha yake, halafu akasema;

‘Katika uchunguzi wetu, tumegundua kuwa yule kijana mdogo wa mume wako alikuwepo siku ile Makabrasha alipouwawa, na alionekana akiranda randa eneo la lile jengo, na baadaye akaondoka na mtu siyefahamika, ...sasa tulitaka kuongea naye, lakini hayupo, na watu wangu wamejaribu kumtafuta bila mafanikio, hata kazini kwake hawajui kaenda wapi, je unafahamu huyu kijana wenu kaenda wapi, maana ni muhimu sana..?’ akaniuliza

‘Kwakweli hata mimi sijui kaenda wapi, na nilishamwambia kuwa asiondoke bila ya kuwasiliana na mimi..’nikasema nay eye akaniangalia kwa mashaka.

‘Haiwezekani, ina maana haat nyie hamfahamu huyu kijana kaenda wapi, ....Je hata mume wako hafahamu wapi kijana wenu alipokwenda...? ‘ akauliza

‘Hafahamu kabisa,  maana jana nilipofika kumuona yeye, mwenyewe aliniulizua, kwani anaona ajabu siku mbili kupita bila mdogo wake kufika kumuona,.... sio kawaida yake..’akasema

‘Ina maana katoroka, au kuna kitu kimemtokea, maana msije mkakaa kimiya kumbe yupo kwenye matatizo?’ akaniuliza

‘Kwanini atoroke...mimi sizani kama yupo kwenye matatizo, huenda ni katika kuhangaika, kutafuta masilahi, aliondoka kufukuzia kazi zake, akakwama mahali, na hataki kusema wapi alipo, unafahamu tena vijana...lakini kauli yako hiyo ya kusema katoroka, ina nitia mashaka, kwanini unasema hivyo?’ nikamuuliza

‘Sisi katuka uchunguzi wetu, tuna mambo tulitaka kumuuliza, tunahisi kuna mambo anayafahamu, unajau bado tunafuatilia kesi ya Makabrasha.....’akasema

‘Kwahiyo mnamshuku kwa msingi gani, kuwa anafahmu muuaji, au yeye kashiriki, au ni kutaka kufahamu mambo ambayo huenda yatawasaidia kumpata huyo muuaji?’ nikamuuliza.

‘Tunahisi yeye anaweza kutusaidia, ....kumpata huyo muuaji, ‘akasema.

‘Mhh, kama angelikuwa anafahamu hilo, angelisema, maana ukumbuke Makabrasha alikuwa ndiye wakili wao, na alikuwa hajafanikisha malengo yao, wasingeliweza kukaa kimiya kama wanamfahamu huyo muuaji...’ nikasema

‘Makabrasha alikwua haaminiki, inawezekana, huyo kijana anamfahamu huyo muaaji, lakini hana uhakika kuwa kweli huyo jamaa kafanya hivyo, akiogopa kujiingiza, au pia inawezekana alishirikiana na huyo muaaji, ,....’akasema.

‘Hilo nalipinga, maana ujue Makabrasha alikuwa ni kama ndugu yao, pili alikuwa ni wakili wao .....’nikasema.

‘Yote yawezekana, ndio maana nilitaka niongea nay eye, sisi ni wataalamu wa ammbo hayo, nikiongea naye tu, ninaweza kuhakiki hayo ninayotaka kuyafahamu, kama hahusiki hatutamlazimisha,...’akasema

‘Nakumbuka mara ya kwanza ulisema aliyefanya hivyo, atakuwa mtu wa ndani na ikiwezekana atakuwa mfanyakazi wa humo akishirikiana na watu wa nje, ina maana mnahisi kuwa huyo aliyekuwa nje ni huyo kijana?’ nikamuuliza.

‘Ni moja ya mambo ambayo tunayafuatilia, kuhakiki, ndio maana tunataka kumuhoji, kuna ushahidi huo kuwa huenda ni yeye aliyekuwa nje,...lakini kama ulivyosema , ni kwanini wamuue mtu kama huyo,..hata sisi tunashindwa kuunganisha huo ukweli, mpaka tumuone, ila tunahisi huyo kijana atakuwa anahusika, kwa namna moja au nyingine,...sasa kinachotufanya tuzidi kumweka kwenye kundi la wahusika, ni huko kutoweke kwake kwa ghafla...’akasema

‘Mimi sijui kama kweli katoweka , hiyo kauli bado sijakubaliana nayo, kwani sio mara ya kwanza kufanya hivyo, nilishawahi kumkanya kuhusu hiyo tabia ya kuondoka, na kukaa kimiya,....’nikasema.

‘Kwahiyo hiyo sio mara ya kwanza kuondoka ghafla?’ akauliza

‘Sio mara ya kwanza, ..ni tabia yake, na mwenyewe hujitetea akisema kazi zake zinamfanya awe hivyo, anaweza kuitwa mahali, akajikuta hana mawasiliano, au hataki kufahamika yupo wapi, kwasababu ya ushindani wa kibiashara..ndivyo anavyojietetea....’nikasema.

‘Hiyo sio kawaida kabisa, kama ni hivyo kwanini kazini kwake wasifahamu wapi alipo?’akauliza

‘Ndivyo anavyofanya hivyo, ....sio jambo geni kwetu...akirudi nitamfahamisha kuwa unamtafuta....’nikasema

 ‘Ni bora ufanye hivyo, kwasababu wanafamilia wa Makabrasha wanataka hiyo kesi ikamilike, na wanadai kuwa kuna njama za kuficha ukweli, na wameshapeleka malalamiko ngazi za juu...’akasema

‘Ni nani kafanya hivyo?’ nikauliza

‘Ni mwafamilia wao mmoja ambaye ni mwanasheria, ni mmoja wa watoto wake, acha yule mkubwa, yule tuliongea naye tukamalizana, alkini kuna mmoja mkorofi,anajifanya anafahamu sana sheria,....’akasema

‘Kazi ipo, kwahiyo mkaamua kuanza tena upelelezi au.....?’nikamuuliza

‘Sio kuanza upelelezi, mbona upelelezi ulikuwa unaendelea, japokuwa sio ule wa haraka haraka, maana tulifika mahali tukasema muuaji ni mmoja wa maadui za marehemu, lakini sio kwamba tulishafunga jalada lake,..hapana,bado tunachunguza....’akasema.

‘Nawatakia kila-laheri, maana mauaji hayo, yalinitia doa, kwahiyo akipatikana huyo muuaji, hata mimi nitakuwa katika wakati mzuri hata ikibidi kuwashitaki nyie kwa kunisingizia mambo nisiyohusika nayo...’nikasema.

‘Huwezi kutushitaki, sisi ni moja ya kazi zetu...’akasema akijiandaa kuondoka.

‘Haya nashukuru kwa hilo, nitafanya kama ulivyoniomba, na inaonekana huyo muaaji ni mjanja sana, kafanya mauaji na imeshindikana kumfahamu ni nani, isije ikawa ni watu wako...’nikasema

‘Hiyo haipo, sio watu wangu...ni tetesi za mitaani tu, hilo nakuhakikishia, ni mmoja wa maadui za marehemu, na tutampata tu....ni swala la muda...’akasema.

‘Lakini mnafanya hivyo kwa shinikizo la wanafamilia, nyie mlishakata tamaa..’nikasema.

‘Hapana hatukuwa tumekata tamaa, ila ushirikiana wa wananchi umekuwa mdogo, ni kama vile watu walitaka mtu huyo afe tu. Sisi bado tupo kazini, tutapambana na hawo watu,na  kama kuna watu wanafahamu muuaji watuambie, sisi hatuwezi kuwashika watu kama hakuna ushahidi, wao kama wanafamilia, kama kuna watu wanawahisi watufahamishe,...maana mzazi wao, alikwua kajijengea maisha ya kuwa na maadui wengi, hata ndani ya familia yake mwenyewe, hata marafiki zake, sasa ni nani unaweza kumhisi,  hiyo sio kazi rahisi....’akasema

‘Lakini ni moja ya kazi zenu, msikwepe majukumu...’nikasema

‘Hilo silikatai, lakini ili tufanikiwe, tunahitajia ushirikiane wenu,...na nilikuwa nataka kukuuliza,kuna tetesi kuwa kuna vitu viliibiwa kwako, na sasa umevipata ni kweli au si kweli?’ akaniuliza

‘Vitu gani hivyo?’ nikamuuliza.

‘Nimesikia kuwa kuna mikataba yako ilipotea, ..na umeshaipata, je ni nani aliichukua?’ akaniuliza

‘Mimi sijafika kwenu kulalamika kuhusu kuibiwa, je ulishawahi kuniona kuja kwako kulalamika kuhusu kuibiwa?’ nikamuuliza

‘Hujashitakia hilo...lakini unaweza ukaacha kutokana na shinikizo, na tunahisi uliogopa, kufanya hivyo kwa sababu ya ujanja wa Makabrasha,..na ndio maana kipindi kile tulikushikilia, tukijua huenda uliamua kumuondoa kwa tabia yake hiyo, tukakosa ushahidi, sasa tumesikia kuwa ulichokuwa ukikitafuta, umekipata,baada ya Makabrasha ku-uwawa,hebu niambie ukweli, maana huenda ikatusaidia katika uchunguzi wetu..’akasema

‘Mkuu mimi sina cha kukuambia,...kama ningelikuwa na tatizo hilo ningelishawaambia, na kwanini niogope kuwaambia kwa shinikio la mtu kama Makabrasha, mimi simuogopi yoyote inapohusu sheria, na nikiwa nimesimamia kweli ukweli na haki, mimi nina wanasheria wangu, wangelifanyia hilo kazi...’nikasema.

‘Sawa, lakini kama kuna lolote unalifahamu, tueleze, na ukimuona huyo kijana mwambie aje kituoni, asije akasubiri tukatumia nguvu, kwani hata kama atajificha waoi sisi tutampata tu....na kama kuna lolote wewe unahisi litatusaidia kuimaliza hiyo kesi kama raia mwema, tunakuhitajia ushirikiane nasi,...’akasema akiondoka.

‘Nikimuona nitamshauri hivyo....’nikasema

************

Nilipomaliza kuongea na mkuu wa upelelezi, niliondoka hadi hospitalini , na nilimkuta mume wangu akiwa kwenye mapumziko baada ya mazoezi, alionekana kuchoka kidogo, sikutaka kuongea naye sana, kwani alitakiwa kupumzika, ila yeye akaanza kuongea;

‘Mdogo wangu yupo wapi, ,mbona haji kuniona....?’ akauliza

‘Nafikiri kazi zimekuwa nyingi, nitamwambia nikimuona’nikasema

‘Nasikia kuwa polisi wanamtafuta, kwani ana kosa gani?’ akaniuliza

‘Kwakweli mimi sijui,...na inaonekana una vyanzo vingi vya habari, kwanini unajihanganisha na wewe hustahili kufanya hivyo, unatakiwa kujali afya yako kwanza’nikasema

‘Mimi nazungumza kuhusu mdogo wangu...’akasema kwa ukali, na mimi nikakaa kimiya nikimsikiliza.

‘Mke wangu nilishakuambia kuwa mdogo wangu ni mtu muhimu sana kwangu,sitafurahia kama ananyanyaswa, au kusingiziwa mambo ambayo hajafanya,nilikuambia kuwa umlinde , sasa wewe unasema hujui lolote..mbona mimi nimefahamu kuwa polisi wanamtafuta’akasema

‘Yule sio mtoto mdogo anafahamu ni nini anachokifanya, ...na kutafutwa na polisi ni jambo la kawaida, kama hana hatia unafikiri watamfanya nini, au unafahamu lolote kuhusu yeye, kuwa huenda ana jambo kalifanya?’ nikamuuliza.

‘Hajafanya kitu bwana....kama kuna tatizo lolote waje waniulize mimi..’akasema kwa kujiamini

‘Wakuulize wewe kuhusu nini?’ nikamuuliza

‘Kama wanahisi kafanya kosa, waje waniulize mimi, kwasababu yule ni mdogo wangu...’akasema

‘Ina maana akifanya kosa lolote huko alipo, waje wakuulize wewe kwani yule ni mtoto mdogo, yeye umri wake, uanastahili kushitakiwa, na hata kuhukumiwa, kama kafanya kosa, ...’nikasema.

‘Mke wangu mimi nimeshakuhisi kuwa una jambo dhidi ya mdogo wangu, nimeshakushitukia unamtafuta nimi mdogo wangu, kama kuna lolote dhidi yangu pambana na mimi, usimshinikize mdogo wangu kwenye mambo yanayonihusu mimi, nikuambia ukweli, kama kuna lolote unalifahamu ambalo linamfanya mdogo wangu ashindwe kuja kuniona, naomba unifahamishe, ...maana kama nikifahamu kuna jambo baya dhidi yake, ambalo wewe unalifahamu, ukanificha, mke wanguhatutaelewana...’akasema akiniangalia na kwa kujiamini sana.

‘Mimi sijui lolote, kama ningelifahamu hilo, ningelishakuambia, ukumbuke yeye alikuwa kama mtoto wangu nimemuhangaikia hadi hapo alipofika, sasa kwanini nishindwe kumfuatilia hilo....labda kama kafanya makosa, na kakimbia, mimi siwezi kujua...’nikasema.

‘Huwezi kujua, kweli unaweze kusema kitu kama hicho...!?’ akaniuliza kwa mshangao.

‘Nikuulize kwa mara ya mwisho kuonana naye, alipokuja kukuona alikuambia nini?’ nikamuuliza na yeye akatulia kidogo, na baadaye akasema;

‘Kuna vitu nilimtuma, akasema kabati halifunguki, na akasema huenda wewe umebadili kitasa, na akaniambia mambo yamekuwa mabaya, ...sikumuelewa, na hatukupata muda wa kuongea naye kwa undani maana nilikuwa kwenye ratiba maalumu, ambayo haikutakiwa kusubiria...’akasema

‘Ulimtuma nini, kwanini hukuniambia mimi, au kumtuma kwangu ili niweze kukupatia hivyo vitu ..kuna siri gani kati yako na mdogo wako?’ nikamuuliza

‘Hicho nilichomtuma ni mambo yangu mimi na yeye, kuna mambo mengine yanahusu maswala yangu, mimi  na yeye, sikutaka kukusumbua, kama ningelikuhitajia wewe, ningelikuambia tu,...lakini nikirudi nyumbani tutaangalia kwani nahisi kuna mambo mengi nahitajia kuyaweka sawa,...ni lazima tuwe na makubaliano,ya kimsingi, bila hivyo mambo hayatakwenda vyema, na sioni kwanini, ufunge kabati langu, ...’akasema kama analalamika.

‘Nilifunga hilo kabati,kwasababu kuna vitu vilipotea, na hatujajua ni nani alivichukua, wewe ulisema hujavichukua, kwahiyo nikaona ili kulinda usalama wa vitu vyetu, ni muhimu kubadili kila kitu. Nitakupa ufungua wa kabati lako, ukitoka,kwa hivi sasa ninao, hili ni kwa usalama wa vitu vyote mle ndani...’nikasema

‘Kuna vitu nahitajika kuvichukua, na mara nyingi namtuma mdogo wangu, huoni itakuwa vigumu kuvipata?’ akaniuliza

‘Ukihitajia vitu vyako, niambie mimi, au mtume mdogo wako kwangu, mimi nitampatia,...’nikasema.

‘Mhh, haya,....nikitoka hapa tutayaweka sawa,....mimi ni mume wako, nahitajia kujua kila kitu, na ilitakiwa mimi ndiye nifanya hivyo, lakini naona wewe unajiamulia mwenyewe tu, ...nikitoka hapa ni lazima niweke mambo sawa,  itakuwa  so vyema kila mtu anafanya anavyotaka...’akasema

‘Hamna shida ukitoka tutayamaliza, na sio kila mtu, aliyefanya hivyo ni mke wako, na nimefanya hivyo kwa nia njema, na nitashukuru sana ukirudi nyumbani...maana sasa hivi kila kitukipo sawa, usijali ...’nikasema na yeye akaniangalia, na kusema;

‘Mke wangu, kuna kitu gani umemfanya mdogo wangu mpaka akaamua kukimbia?’ akaniuliza

‘Ina maana kakimbia?’ nikamuuliza kwa mshangao

‘Sio kawaida yake, nahisi kuna kitu,....kama unahusika na hilo, ni bora uniambie mapema, sitaweza kuvumilia, kama kweli unahusika na hilo..’akasema

‘Mimi sijakuelewa, ...hebu kwanza nikuulize, umeshapona na kuweza kukumbuka yote yaliyotokea nyuma, maana docta kaniambia sasa hivi umeshaanza kujijua na kukumbuka mambo yaliyopita,?’ nikamuuliza.

‘Usikwepe swali...nimekuuliza kuhusu mdogo wangu...’akasema

‘Ndio maana nataka niwe na uhakika, kabla sijakuambia lolote, na ili niwe na uhakika na hilo nataka unijibu swali langu kwanza...’nikasema

‘Swali gani unataka kuniuliza?’ akauliza huku akiwa kakunja uso, sio yule niliyemfahamu siku mbili mbili tatu zilizopita, ni yule mume wa zamani.

‘Unakumbuka siku alipouwawa Makabrasha je ulikuwepo wakati anapigwa risasi?’ nikamuuliza

‘Ni nani kakuambia hayo....?’ akauliza akionyesha mshituko.

‘Nimekuuliza swali nikiwa na maana,  je ulikuwepo au hukuwepo, ndio au hapana, sitaki maelezo, nisije nikakuchosha?’ nikamuuliza

‘Hapana, sikuwepo mimi nilikuwa naumwa, .’akasema.

‘Hapo sasa inaonyesha umepona, unakumbuka, kama unafahamu kuwa siku hiyo ulikuwa unaumwa, ndio maana hukuweza kwenda huko, basi inaonyesha unakumbuka vyema, ...ni bora ukumbuke vyema, maana watu wanaweza kukudhania kuwa ulikuwa unajifanya unaumwa, kutokana na kuonekana sehemu mbali mbali, na wakati huo huo watu wanafahamu kuwa upo hospitalini..’nikasema na yeye akabakia kimiya, na baadaye akasema;

‘Hayo hayakuhusu, usijitumbukize kwenye maswala yasiyokuhusu, utajitakia matatizo ambayo sipendi wewe uyapate, wewe ni mke wangu, ninajali sana usalama wako, hayo mambo mengine uwaachie wanaume...’akasema kwa kujiamini

‘Una uhakika na hilo, kuwa hukumbuki kilichotokea, ....maana kama ulionekana huko, ujue polisi wanasubiri upone wakuulize hilo swali, ni bora ukaniambia ukweli ili nijue jinsi gani ya kuwasaidia,...’nikasema.

‘Mimi sikumbuki bwana, hayo sijui umeyapata wapi, ina mana ndilo lililomfanya mdogo wangu akimbie, kama ni hilo, umemshinikiza mdogo wangu mpaka akakuambia mambo ambayo hutakiwi kuyafahamu, utaniweka mahali ambapo sitakuelewa, ....’akasema kwa hasira.

‘Utanielewa siku ikifka, maana sio mimi tu ninayehitajia huo ukweli, hata mkuu wa upelelezi anahitajia huo ukweli, hata watoto wa Makabrasha wanahitajia huo ukweli, na hata huyo docta anayekuhudumia hapa atapenda kujua ukweli, kuwa kweli muda wote huo ulikuwa unaumwa au ulikuwa na mambo yako, isije ikawa ulipona, ukawa unasingizia, ili kufanikisha mambo yako...’nikasema

‘Unasema nini,.! yaani wewe umdiriki kusema mimi siumwi, hivi wewe mwanamke una ubinadamu kweli, siwezi kuamini haya...’akasema kwa sauti ya unyonge.

‘Kuumwa ulikuwa unaumwa kweli, lakini matendo yako yananitia mashaka, nahisi kuna muda ulikuwa umepona, ukaamua kutumia , ili kuweza kukamilisha mambo yako, sasa sijui, ....kama ulipona lini, je ulipona baada ya Makabrasha kuuwawa, au kabla ya hapo, ....hilo litakuwa juu yako na docta anayekuhudumia, cha muhimu ni ukweli...nausubiriahuo ukweli, siku utapoona umepona kweli, uwe tayari kuelezea kila kitu....na wote wanaohusika, na tukimalizana, huenda Inspekta naye atakuwa akikusubiria ......

‘Wewe mwanamke, usijifanye upo juu...nakuonya kwa hilo, usijiingize kwenye matatizo, unakumbuka mkataba unasema nini, mume ndiye...’akataka kuongea na mimi nikasema.

‘Huo ulikuwa mkataba wako, ...ongea kuhusu mkataba wetu, je mkataba wetu unasema nini, hilo ndilo la muhimu, ama kuhusu maswala ya mkataba usiwe na shaka nayo, mimi ninachokihitajia ni afya yako, ...ukipona mambo ya mkataba yatajielezea halafu nimesahau jambo....’nikasema na yeye akaniangalia kwa mashaka, ...nikamsogelea kama kumnong’oneza;

‘Eksi, wako, mpenzi wako yule wa kujifunzia, na yeye kakimbilia kwao...nahisi kafahamu kuwa mliyoyafanya yameshagundulikana...sasa sijui, huenda wapo na mdogo wako, au....’nikakatiza maana mlango ulifunguliwa

Nilimuona mume wangu akihangaika, akaniangalia halafu akatabasamu kidogo, akakunja uso, kuonyesha chuki fulani,...halafu akasema;

‘Tutapambana huko huko, ....siogopi lolote, ...nafikiri ulikuwa hujanitambua,mimi sio yule mume wako wa zamani , mume bwege, nimeshajitambua, nikuambie ukweli, mimi siogopi polisi au yoyote yule, hilo nimeshajipanga vyema tu....’akasema na docta akawa keshaingia,

‘Karibu sana....’nikasema na kugeuka kumwangalia docta, huku moyoni nikisema;

`Bado mmoja...’.

Nb Je ni kweli kuwa mume wa huyo mdada alikuwa akisingizia kuumwa, je ni kweli anahusika na hayo yote, na swali kubwa hadi sasa, ni nani aliyemuua Makabrasha, ...?


WAZO LA LEO: Maisha ya ndoa sio kuonyeshana ubabe, kuwa ni nani zaidi, maisha ya ndoa ni makubaliano , yenye lengo jema, kwani wanandoa ni kitu kimoja, ili mfanikiwe kwenye safari yenu ya upendo na furaha, ni vyema kila mmoja akajiona ni muhusika mkuu, kwa nafasi yake. Kila mmoja amjali mwenzake,amsaidie mwenzake, amjali na hapo  hekima busara na upendo ndivyo viwe dira yenu.
Ni mimi: emu-three

1 comment :

Pam said...

duh hii kali kuliko how comes upendo wooote upotee na kuwa visasi!