Wakati nipo nyumbani nimejipumzisha , tukisubiria siku ya
hukumu, mara akaja mwanasheria wa hiyo familia ya marehemu mume wangu, alifika
akiwa mnyonge na alionekana mwingi wa huzuni, na alipofika alinisalimia kwa
upole na adabu, nikamkaribisha kiti kukaa, na hakufanya hiyana akakaa kwenye
sofa na kutulia kidogo.
Akawa anamwangaia mtoto wangu akiwa anacheza sakafuni, …nikamwambia
mtoto akacheze nje, nikijua haya mazungumzo aliyokuja nayo huyu jamaa yanaweza
yasimstahii mtoto kusikia.
‘Mtoto anakuwa haraka, natamani ningekuwa na mtoto…’akasema,
‘Muda muafaak utafika utakuwa naye, kwani wewe na mchumba
wako hamjaafikiana lolote?’ nikamuuliza nikimwangalia kwa macho ya huruma.
‘Baada ya ile kesi, aliondoka, …unajua hakufika hata
kuniaga,….’akasema
‘Lakini alisema ana haraka, ….kuna kesi aikuwa akiifuatilia…’nikasema
‘Najua aliona kuwa akifika nyumbani kwetu, na wakati kaka
yangu keshakasirika, hakutakuwa na amani, nahisi keshanitoa kwenye moyo wake..’akasema.
‘Hiyo sio kweli, mwanadada anakupenda sana,….wewe tu
hujajituliza kwake, …’nikasema.
‘Ttaizo kupenda kwake ni kwa masharti, na mimi nijuavyo,
ukipenda hata chongo utaliita kengeza, huangalii lolote zaidi ya kupenda, sasa
yeye keshaona mambo ambayo yamemkwaza, na sijui kama atakubaliana tena na
uchumba wetu…’akasema.
‘Masharti ni kawaida kwenye mahusiano, na hayavunji upendo,
cha muhimu ni kukaa pamoja na kuyaangalia hayo masharti , na kama kweli
mnapendana mtakubaliana, …sioni kama kuna shida, …’nikasema.
‘Unajua shemeji, pamoja na hayo, hata mimi moyo wangu
unaanza kuingia doa, na…na…..’akasita kuongea.
‘Kwanini uingie doa,…kwani wewe humpendi?’ nikamuuliza.
‘Nampenda…ni mtu tuliyezoeana, na kiukweli tumetoka naye
mbali, lakini bado nina majukumu,…na kiukweli, najikuta kwenye njia panda,….pamoja
na majukumu hayo, pia hata moyo wangu unahisi kupenda….’akasema.
‘Majukumu gani hayo shemu?’ nikamuuliza nikianza kuhisi
jambo.
‘Shemeji nilishakuambai toka awali, kuwa pamoja na kuwa kaka
yangu, aliniachia wewe nikutunze na mtoto, lakini pia moyo wangu ulishakupenda…yaani hiyo ni
kweli kabisa….sizungumzi I kwa ajili ya haya majukumu, nazungumiza kutoka ndani
ya moyo wangu,….shemeji nakuomba tafadhali kubali nichukue nafasii ya kaka
yangu….’akasema na mimi hapo nikakunja uso, nilitamani nimfukuze, lakini
nikaona nitumie busara.
‘Shameji yangu huko sio kupenda, huko ni kutamani, wewe
ulishapenda mtu, hadi kufikia kufunga uchumba,…na kama ulivyosema mumetoka
mbali na mchumba wako, …jiweke wewe kwenye nafasi yake, ungelijiskiaje kama
ungelifanyiwa hayo unayotaka kumfanyia…shemeji kumbuka mlipotoka, rejesha moyo
wako nyuma, nina imani kuwa mtaendeleza upendo wenu…’nikamwambia.
‘Kwani shemeji, hata kama nikumuoa yeye, na wewe ukawa mke
wangu wa pili kuna ubaya gani?’ akauliza.
‘Kwa mila zetuu hakuna ubaya…lakini kwa hali halisi , hasa
ukizingatia maamuzi yangu mimi mwenyewe hilo halitawezekana, hata kama
ingelikuwa huan mchumba mwingine, kwangu mimi nimeshaamua, kuishi kivyangu…..mwenzangu
ameondoka, na sitaki kumsaliti….’nikasema.
‘Hapo una kufuru, ndoa inakufa pale mmoja anaptangulia
ahera, hayo ni mapenzi ya mungu, na hatuwezi kuyakana, na ukisema hivyo kuwa
hutaki kuolewa tena, ina maana unapinga mapenz I ya mungu…maisha ndivyo
yalivyo,….’akasema.
‘Hilo nalifahamu kabisa,..kuwa hayo ni mapenzi ya mungu,
kuwa mpende umpendaye ipo siku mtatengana naye, ..na kweli tumeshatengana naye,
sina jinsi ya kumrejesha,…..hata hivyo, mimi sijatulia, na uamuzi wangu ni huo
huo…..ninaona kuwa nitaweza kuishi bila kuwa na mume….huo ndio uamuzi wangu,
ilimradi nisivuke mipaka…’nikasema.
‘Shemu kibiandamu, hilo haliwezekani, hutaweza kukaa peke
yako usiingiwe na vishawishi….na kwanini ukufuru…ni lazima uwe na mwenzako,
kwanza mtoto atajihis mpweke, hana baba…hulioni hilo?’ akauliza.
‘Mtoto ataelewa, na keshaanza kuelewa, hilo nitalifanyia
kazi, ninachohitajia ni kumjenga kimaadili, na kumjenga apende kazai kama babu
na bibi yake, maisha niliyolelewa mimi ya kupenda kazi kujituma na kutokupenda
kutegea, ndiyo nitakayomfundisha mwanangu,…na elimu, itakuwa ndio taa ya maisha
yake, hatapata shida…’nikasema.
‘Nakuomba sana shemeji, ….jana tu nimeota, marehemu
akinikumbusha ahadi yetu, kuwa sitakuacha uteseke,..sitamuacha mtoto ateseke…sasa
nifanyeje…shemeji naomba usinitese, nasema tena, mimi nafanya haya kwa vile
nakupenda, sio kwa…vile….’mara simu yangu ikaita…
‘Unaona mchumba wako huyu ananipigia…..samahani nakwenda
kuipokea, maana sijui ananipigia kwa maswala gani, na huenda asingelipenda
asikie tunachokizungumza…..’nikasema.
‘Sawa …mimi ngoja nikacheze nje na mtoto, mkimaliza kuongea utaniita…’akasema
na kutoka nje
********
Nilipomaliza kuongea na wakili mwanadada, nikatoka nje na
kumkuta shemeji yangu akicheza na mtoto, kwakweli ilionekana wameivana, na
nilipokuwa namuangalia kumbukumbu za mume wangu zikatanda kichwani, ….hawakuwa
na tofauti sana, sura maumbile…..kasoro tabia kidogo, kwa vile huyu ni msomi,
na marehemu mume wangu aliishia kidato cha nne, akawa hakufauu , kwenda mbele,
kuna mambo wanatofautiana sana…
Hapo niliposimama nilihisi machozi yakinitoka, nikiwa, hali
ya kibinadamu, huwezi kuamini, unaona kama jana tu, nilikuwa na mume wangu,
tunapendana, na tulikuwa na mipango mingi ya pamoja, lakini leo nipo peke
yangu, mjane, na mtoto…..oh, yote ni mapenzi ya mungu, lakini kwa ujumla inauma
sana,…usiombe kufiwa na mume…
'Shemeji, mtoto ananiuliza lini nitakuja niishi hapa na yeye….’akasema.
‘Usianze hayo tena..nafikiri umenielewa,....na usimtumie mtoto kama kisingizio,ninachokuomba kwako wewe ni kujitahidi sana kuongea na mchumba wako,...mimi nimechunguza sana, jinsi gani anavyokuangalia, anavyoongea akizungumza kuhusu wewe, kwa ujumla anakupenda sana…’nikasema.
‘Ina maana mnaongea kuhusu mimi, mnapokutana, na hata sasa hivi kwenye simu mlikuwa mkiniongelea mimi...manaongea nini kuhusu mimi...?’ akaniuliza akiniangalia kwa makini.
‘Hapana sio kwamba tunakuongea kwa nia ya uchumba wenu, ila anapokugusia wewe kwa namna moja au nyingine, hisia zake usoni, zinaonyesha hivyo…na leo kwenye simu hatujaongea kuhusu wewe, na wala hajui kuwa
upo hapa, yeye kaongelea mambo ya kesi yetu, na amesema atakuja kwenye hukumu…..alikuwa akiniambia kuwa nisimuone yupo kimiya, kuna mambo mengine anayafuatilia…ni hivyo tu shemeji, ila sauti yake inaonyesha unyonge fulani...’nikamwambia.
‘Anyway..shemeji, najua kabia kama wanafamilia, mlitajia kuwa mmoja wetu atafika hapa, na mimi niliona hilo, kwani kesi ni haki ya kila mtu, kesi sio kujenga uadui, kesi ni sehemu ya kutafuta haki pale unapoona kuwa haki hiyo haikuweza kupatikana katika njia nyingine...kwahiyo ujio wangu huu, ni wa heri, ni wa kutafuta muafaka.....’akasema.
‘Shameji mimi na wazazi wangu, hatukuwa na mawazo hayo kuwa mtakuja kwa heri.....maana kama yako alivyofanya pale mahakamani, ilionyesha wazi kuwa mnatafuta shari,....hata hivyo hukumu haijatoka, na nyie mlishajiwekea uhakika wa kushinda, sijui baada
ya huo ushahidi mnatarajia nini tena…’nikasema.
‘Baada ya huo ushahidi , kwangu mimi, kama nilivyoahidi sina
jinsi , bali ni kutimiza ahadi yangu, japokuwa kaka kapinga kabisa na
hakubaliani na huo ushahidi, na amesema yeye atapinga hadi hatua ya
mwisho….’akasema.
‘Kwahiyo mnatarajia kukata rufaa mkishindwa?’ nikauliza.
‘Rufaa ya nini, huko ni kuzidi kujizalilisha, maana kauli
yetu ilisikika mahakamani, na ukitenda kinyume chake inaonyesha kuwa umezamiria
uhasama, na sisi ni watu wazima tunastahiki kuwa hekima za kiutu uzima, …mimi
sina zaidi …nimeshasalimu amri, na nisingelingojea hiyo hukumu,kama
isingelikuwa kaka yangu…’akasema.
‘Ulitaka ufanye nini na kesi ipo mahakamani, na huenda
mkashinda..’nikasema.
‘Hamna cha kushinda pale, ushahidi muhimu ulikuwa ni hiyo
stakabadhi, …ile ni karata ya ushindi, na inadhihirisha wazi kuwa kweli
ulishinda hiyo bahati …na fedha ulizojenga hii nyumba na duka inatokana na hiyo
bahati, kwasababu ndugu yetu alisema kuwa pesa yake iliibiwa…na nani, hilo ndilo
halijawahi kujulikana…’akasema.
‘Labda mimi ndio nilimuibia hizo pesa zake,…si ndivyo nyie mlivyodai,
…’nikasema.
‘Hapana …mimi nimeshakuamini,…sina shaka na maneno yako
tena, kazi kubwa kwangu ni kumshawishi kaka, ambaye bado ana kesi mbili
zinamuandama, badala ya kutulia na kuangalia jinsi gani atapambana na hizo kesi
yeye kahamaki kwanini nikakubaliana na kushindwa kwa hii kesi…’akasema.
‘Kwahiyo sasa ni nini uamuzi wenu, …..kukata rufaa, au
kusambaratika kwa familia, maana kama nyie hamkubaliani na kaka yenu, kiongozi
wa familia, ni nini kitafuta hapo?’ nikamuliza.
‘Familia haiwezi kusambaratika, kwasababu ya mtizamo wa mtu
mmoja, nay eye kuwa kiongozi wa familia sio kwamba ni yeye ni kila kitu, yeye
kama binadamu huwa anaweza kukosea, na anatakiwa kukubali kukosolewa, na
nimemwambia wazi kama yeye atakuwa hakubaliani na ukweli akawa anang’ang’ania
sera zake za ubabe, uongozi hatahuweza, na hali kama hiyo inaweza
ikamfunga…’akasema.
‘Yeye akasemaje..?’ nikauliza.
‘Amesema yeye kama kiongozi wa familia hawezi kukubali
kushindwa kirahisi na,mna hiyo, na hasa ikizingatiwa kuwa aliokuwa akishindana
nao ni wanawake, ….alisema wazi wazi , kuwa mwanamke hawezi kumshinda mwanaume,
na ukiona mwanaume umeshindwa, basi hujakamilika….’akasema.
‘Kwahiyo kushindwa kwenu inaonyesha hamjakamilika kwa
mtizamo wa kaka yako....hiyo sio kweli, huko ni kutokubali ukweli, ….hivi
kweli haoni kuwa anajizalilisha, kwanza
kutaka kuficha ukweli, pili kudhulumu na sasa kujitia ubabe na kutokutimiza
ahadi, nakumbuka aliahidi na yeye hivyo hivyo kuwa ushahidi ukipatikana
hatakuwa na kipingamizi…sasa anataka nini…?’ akauliza na mara mtoto akaingia
ndani kwa haraka.
‘Unakimbia nini..unaogpa nini?’ akauiliza.
‘Baba mkubwa anakuja…’akasema .
‘Baba mkubwa, baba mkubwa gani huyo?’ nikauliza.
‘Atakuwa kaka huenda kaja kunifuata,…
‘Au kuleta vurugu…’nikasema nikijiandaa kwa lolote lile.
Na mara mlango ukagongwa…………
NB: Sio mbaya tukiishia hapa, maana duuh, kazi ipo...lakini yote maisha
WAZO LA LEO:
Mpende umpendaye, ipo siku mtatengana naye, penda ukipendacho ipo siku
utakiacha, fanya ufanyalo ipo siku utaondoka na itabakia ni historia, cha
muhimu ni kujua kuwa hapa duniani tupo safarini, sisi ni marehemu watarajiwa, je wewe umejiandaaje na safari yako hiyo. Tenda matendo mema,
ishi kwa amani na upendo, saidia wasiojiweza mayatima kama una uwezo wasomeshe
mayatima,wasaidie wajane,… kwani hayo ndio masurufu ya safari yetu hii, tukiwa
hapa kwenye kituo cha duniani.
Ni mimi:
emu-three
3 comments :
Hana jipya hiyo na mda maji haachi kutapatapa, hongera zako dada
Hana jipya hiyo na mda maji haachi kutapatapa, hongera zako dada
Ndugu yangu Nancy, tupo pamoja, nashukuru sana, kwa hongera zako.na wengine wote wa kimiya kimiya, tupo pamoja.
Post a Comment