Aliitwa shahidi alIyejenga nyumba naye akaelezea jinsi gani
alivyokutana na mlalamikaji, wakaingi naye mkataba wa kujenga hiyo nyumba na
alisema kuwa aliwahi kumuuliza huyo mwanamama mlalamikaji jinsi gani
alivyozipata hizo pesa, akasema kuwa pesa hiyo aliipata kutona na kushinda
promosheni ya kampuni moja ya simu;
‘Je wewe kwa akili yako uliamini hayo maneno?’ akaulizwa.
‘Mimi kama fundi wa ujenzi, nitaamini kila kitu
nitakachoambiwa na bosi wangu, siwezi kumpinga..kwasababu sio kazi yangu
kupekenyua maisha ya watu, kazi yangu ni kujenga..’akasema.
‘Lakini nauliza kwa akili yako mwenyewe uliweza kuamini kuwa
huyo mwanamama alishinda hizo pesa,..au kuna lolote ulisikia zaidi ya hilo?’
akauliza na swali hilo likapingwa kuwa shahidi analazimishwa kuongea hisia
zake, na sio hali halisi.
‘Wakati unajenga ulisikia nini, kuhusiana na hizo pesa za
ujenzi…’akauliza swali, na swali hilo likapingwa kuwa shahidi anaulizwa kusikia
kwa watu wengine, …..
‘Lakini muheshimiwa hakimu, hapa ninachouliza ni hali
halisi, kuwa kama huyo mama hakupata pesa hizo kwa ajili ya ushindi wa hiyo
promosheni basi atakuwa kazipata kwa njia nyingine…ninachojaribu kutafuta hapa
ni jinsi gani nyingine iliyofanya hizo pesa zikapatikana’akajitetea
‘Basi jenga msingi wa hoja yako….kwa kupitia shahidi sio kwa
hisia kutoka kwa watu wengine, natumai unafahamu nini unachokifanya kama wakili’hakimu
akasema.
‘Huyo mama alikuambia kuwa alipata pesa hizo kwa promosheni,
lakini kuna njia nyingine angeliweza kuzipata hizo pesa sawa si sawa?’
akauliza.
‘Ndio inawezekana zipo njia nyingi, na sio kazi yangu kujua
hilo…’akasema huyo shahidi
‘Wewe unaliwazia nini, kuwa huenda kama sio hiyo promosheni,inawezekana
huyo mama alizipata hizo pesa kutoka kwa njia ipi nyingine?’ akauliza
‘Inawezekana, ndio kama binadamu niliwaza hilo kuwa huenda
alizipata kutoka kwa mume wake, pia nilisikia watu wakisema kuwa huenda hizo
pesa….’akakatizwa kujibu hizo swali kuwa
anahisi badala ya kusema ukweli kutoka kwake mwenyewe. Wakili yule akageuka
kumwangalia hakimu, kama vile anazuiwa kupata hoja yake.
‘Je baada ya kukamilisha huo ujenzi uliwahi kukutana na mume
wa mlalamikaji?’ akaulizwa shahidi.
‘Mara nyingi sana,….huyo mume wake nilimfahamu kabla na hata
baada ya kutoka jela yeye na mkewe waliwahi
kuniita mara kwa mara kujenga baadhi ya sehemu, kwenye nyumba yao hiyo
na duka…’akasema.
‘Je marahemu alisema nini kuhusu hiyo nyumba…?’ akaulizwa.
‘Mara nyingi alikuwa akimsifia mkewe kwa juhudu zake za
kuweza kukamlisha hiyo nyumba, na pia niliwahi kumuuliza gharama za ujenzi wa
nyumba kuwa ni za mkewe au na yeye alichangia’akasema.
‘Na alijibuje?’ akauliza.
‘Alisema hayo ni maswala yake ya ndani na mkewe, ila siku
moja alisema aliwahi kuibiwa pesa zake, huenda ndizo hizi zilizojenga hiyo
nyumba…wakati yeye akiwa jela’akasema.
‘Je kipindi anaongea hayo maneno huyo marehemu alikuwaje?’
akaulizwa na wakili mwanadada.
‘Alikuwa amelewa….’akasema shahidi.
‘Na akiwa hajalewa anasemaje ukimuuliza swali kama hilo,
kuhusiana na gharama ya nyumba…?’ akauliza wakili mwanadada.
‘Anasema hayo ni maswala yao na mkewe, na anaishia kumsifia
mkewe kuwa ana akili sana, na ana bahati kubwa sana…’akasema.
‘Kwanini alisema mkewe ana bahati kubwa sana…?’ akaulizwa.
‘Ni kwa vile aliweza kupata hizo pesa kwa bahati nasibu..’akasema.
‘Kwahiyo aliwahi kukuambia kuwa mkewe alishinda hiyo
promosheni?’ akaulizwa
‘Ndio…’mwanadada akamgeukia wakili mtetezi na kumwambia anaweza kuendelea shahidi na wakili mtetezi akasema
‘Sina swali jingine..’
********
Akaitwa mjumbe naye akatoa ushahidi wake, na wakati haya
yanaendelea mara mwanamama mlalamikajai akamnong’oneza wakili wake;
‘Nataka unisimamishe…’akasema mwanamama mlalamikaji.
‘Hapana huu sio muda muafaka wa wewe kusimama, utaharibu
kila kitu,…wewe niachie mwenyewe.’akasema.
‘Nataka nisimame nikaonyeshe huo ushahidi wanaoutaka….nimechoka
na uwongo wao’akasema mwanana mlalamikaji.
‘Ukaonyeshe ushahidi gani, wewe mwenyewe unajua fika kuwa
hatujaweza kuupa ushahidi muhimu, lakini nina imani tutaupata tu …ninachohitajia hapa ni kupoteza muda, ili
kesi iahirishwe ili tuweze kuupata huo ushahidi, maana bado kuna watu
wanaendelea kutafuta, ….kuna dalili kuwa kweli ile stakabadhi ya malipo,
iliyoonekana kuwepo kwa jina la mtu mwingine ilikuja kuwekwa baadaye,……’akasema.
‘Mimi nina ushahidi wa kuweza kuimaliza hii kesi,naomba
unisimamishe ….usiwe na shaka na mimi nisimamishe na utaona ni nini nitakachokifanya,….’akasema
na wakili akatulia akiwaza jambo, na mara akakumbuka yule mtu aliyekuwa na
mfuko wa Rambo, na sasa huo mfuko wa Rambo upo mikononi mwa huyu mwanamama.
‘Humo kwenye mfuko kuna nini…?’ akauliza na kabla hajajibiwa
na huyo mwanamama , muheshimiwa hakimu akauliza
‘Mlalamikaji shahidi wako tafadhali, tufanye haraka kidogo
….’ Akaita hakimu huku akimwangalia wakili mwanadada
‘Muheshimiwa hakimu, sasa nitamsimamisha
mlalamikaji…’akasema na hakimu akajikuta mwenyewe akishindwa kuficha hisia
zake, akauliza;
‘Kwanini umsimamishe haraka hivyo, huna shahidi wengine, mbona
bado kuna orodha ndefu ya mashahidi wako, na hawajapata muda wa kutoa ushahidi
wao….huoni kuwa utahitimisha kesi kabla ya wakati wake….una uhakika na hilo
wakili , maana tunahitaji haki itendeke…?’ akasema hakimu.
‘Muheshimiwa hakimu, …nina uhakika na hilo….nataka
nimsimamishe mlalamikaji’akasema na hakimu akasema mlalamikaji apite mbele na
ale kiapo na taratibu nyingine zikafuatwa…
‘Hata kule kwa upande wa utetezi, hawakuamini hilo, na
wakaona ndio nafsi yako ya kuhitimisha kila kitui, wakili wao na mwanasheria wakawa
wanateta kimiya kimiya…huku wakishindwa kuficha hisia zao kwani kwenye nyuso
zao kulionekana tabasamu la ushindi.
‘Unaonaje ukiniachia mimi…..’akasema mwanasheria kwa sauti
iliyosikika, akimuomba wakili wake, na wakili wake, akasema;
‘Lakini kweli mna uhakika hawana ushahidi mwingine, kama
stakabadhi ya malipo, …nahisi kama kusimama kwake kunaweza kuwa wameshapata huo
ushahidi…..’akasema
‘Waupate wapi huo ushahidi, mimi mwenyewe nilifika ofisini
kwenye hiyo kampuni, nikaiona hiyo stakabadhi ya malipo, ilikuwa imeandikwa
jina tifauti kabisa na la huyo mama…ni ujanja ujanja wanataka kuutumia, hawana
lolote,….wewe ngoja nimchemshe kidogo huyo mwanamama, japokuwa namuonea sana
huruma….’akasema
‘Sawa mkuu, uwanja ni wako…
Mlalamikaji akaanza kujielezea, ilivyokuwa, jinsi
walivyokutana na marehemu, akaelezea jinsi walivyofika Dar na maisha ya Dar,
halafu akaelezea jinsi marehemu alivyokamatwa, kama alivyowahi kuelezea awali….
‘Nikabakia mimi peke yangu na kuanza kuhangaika, na ilifikia
sehemu nilikata tamaa kabisa ya maisha, na ndipo hapo nikapigiwa simu kuwa nimeshinda
promosheni ya simu….’akasema mara wakili mtetezi akasimama na kumkabili, hapo mlalamikaji akamwangalia wakili huyo kwa uso wa huzuni na wasiwasi, akijua jinsi gani wakili anavyoweza kumuuliza maswali makali ya kumafanua yeye aonekane mwongo.
‘Je unaweza kutuambia ulipigiwa kwenye simu gani, unayo hiyo simu hapa
kama ushahidi, na je namba yake ilikuwa namba gani, ili tuweze kuhakiki, maana watu wa
simu wanaweza kuyarudia maongezi yenu na kuthibitisha hayo unayoyasema?’
akaulizwa.
‘Sikumbuki hiyo namba ya simu , kwani baadaye hiyo simu
iliibiwa…’akasema na yule wakili akatabasamu na kusema;
‘Muheshimiwa hakimu, unaona, hata namba ya simu huikumbuki,
kwa vile sio kweli, ingelikuwa ni kweli, ungelikumbuka vyema hiyo namba kwani
ndiyo iliyokupatia pesa…nani anaweza kusahau kitu kilichompatia bahati kama
hiyo..’akasema wakili huku akitamba kwa kutemba huku na kule.
‘Katika maisha yetu sio rahisi kukumbuka kila kitu, ni nani
anaweza kufahamu kesho kutatokea nini, na ni nani angelijua kuwa mume wangu
angelifariki,…..na ni nani angelijua haya yote yangelitokea, na ni nani
angelijua kuwa vitu kama hivyo vya karatasi ya malipo vingehitajika….ni siku
nyingi zimepita na hatukuweza kuona umuhimu wake tena…, kama ningelifahamu haya
yote kuwa yangelitokea, ningelitunza kila kitu….lakini’akasema kwa uchungu na
kabla hajaendelea wakili mtetezi akasema;
‘Kwa hali kama hiyo, ni nani atakuamini, je tumwamini
marehemu au tukuamini wewe, fikiria mimi mwenyewe niliongea na marehemu uso kwa
uso, kama ndugu yangu, akanifahamisha hivyo kuwa nyumba kajenga kwa pesa yake…,
na akataka niandike maandishi ya kulinda mali yake, je kwa vile kafariki ndio
nibadili kauli yake….?’akasema huyo mwanasheria ambaye aliamua kumsaidia wakili
wake.
‘Kuna makosa yalifanyika, nahisi kuna mbinu zilifanyika,
huenda wewe huzijui, na kama unafahamu, basi umeshiriki katika kuhadaa…’akasema
mwanamama, na yule wakili hakujali hayo maelezo akasema;
‘Hebu niambie, kama ungelikuwa wewe ndio mimi, upo sehemu
yangu ungelifanya nini…kumbuka yule ni ndugu yangu, kaniomba nifanye hivyo, je
ni kuamini wewe kuliko ndugu yangu, sasa angalia huyo sasa ni marehmu, wewe
huoni kuwa tukiamini maneno yako na kumpinga marehemu kwa vila hayupo duniani, tutakuwa
tunakiuka kauli ya marehemu, na tutakuwa hatumtendei haki,….wewe huoni hiyo?’
Akawa kama anauliza.
‘Hatutatenda vibaya kwasababu sio kweli,….hayo mumezua
baadaya ya mrehemu kufariki…’akasema mwanamama mlalamikaji, akionyesha hisia za
uchungu.
‘Ndugu muheshimiwa hakimu, lengo la kutetea haki hiyo, haki
ya kumuliki, sio kwamba tunafanya hivyo kwa vile ni mali,…kwa vie nyumba yenye
thamani kubwa,… kwani tunaweza tukajenga wenyewe nyumba kama hiyo, …mimi nina
kazi, Napata mshahara, ninaweza nikajitahidi nikajenga nyumba kama hiyo,
kwanini nipoteze muda kupigania vitu kama hivyo…nafanya hivi kwa vile
najitahidi kutetea kile alichoniagiza marehemu, natetea haki ya marehemu, sio
kwamba mtu akifa basi haki yake ipotee, haiwezekani kabisa…’akasema huku
akimwangalia hakimu na baadaye watu waliohudhuria,halafu akamgeukiwa
mlalamikaji,…akamwangalia kwa muda, na baadaye akawageukiwa watu waliohudhuria,
akasema;,
‘Mwenzetu anapofariki, anakuwa hana mtetezi tena, kwahiyo
inategemea nyie wanandugu mliobakia, kama alitaka jambo fulani lifanyike, ina
maana kuondoka kwake, kutategemea nyi e wanandugu mliobakia dunia, muweza
kumsaidia kutetea haki yake, na kama alitoa kauli yake, ni haki yenu nyie mliobakia
dunia kuitekeleza, ….na ndicho sisi tunachokifanya, hatuna zaidi, hatuna haja
na hiyo mali,…..’akatulia.
‘Ni kweli kuwa aliacha mjane, ni kweli kuwa aliacha mtoto,
lakini vyote hivyo kipindi ananielekeza kutayarisha hiyo hati, nilimuuliza, na
akasema mjane na mtoto wake wote ananiachia mimi, vyote hivyo vitakuwa kwenye
mikono yangu, nihakikishe kuwa familia yake haiteseki…je kwa hali kama hiyo
mimi mlitaka nifanye nini….niake kimiya nimsikilize huyu mwanamama, kwa kutaka
nini kwake….’akamgeukiwa mwanamama mlalamikaji.
‘Kwahiyo, ndugu mlalamikaji, sifanyi haya kwa matamanio
yangu, eti kukudhulumu jasho lako, hapana nafanya haya kutokana na kauli na
maandishi ya marehemu, ..kamwe sitadhulumu jasho la mtu, kama kweli ulijenga
kwa pesa yako, …basi ni haki yako…na mimi ningelipata ushahidi wa kuthibitisha
hilo, …..nisingelipoteza muda wangu hapa’akatulia na kumwangalia wakili
mwanadada aliyetaka kusema jambo, lakini wakili yule hakusema kitu.
‘Sasa hebu tuambie una ushahidi gani, wa kuthibitisha hayo
yote, maana katika kulipwa kitu kama hicho ni lazima kungelikuwa na kumbukumbu
ya malipo, na nina uhakika kuwa huna kumbukumbu hiyo na kama unayo….sijui,…au
huenda uligushi, …kama unayo kwa sasa, basi onyesha kwenye mahakama hii ili
tuthibitishe hilo…’akasema huku akishika kidevu kama kuzarau.
‘Ndugu mlalamikaji kama kweli unayo, sisi kwa moyo mmoja
tutabatilisha hayo yote na kukukabidhi mali yako, maana kweli hiyo itakuwa ni
mali yako, …ulijenga kwa jasho lako…kama kweli unayo, na ukathibisha hivyo,
basi nyumba na duka havikustahili kuwepo kwenye mali za urithi za marehemu, pili
unasema hata namba ya simu huna, hivi ni kweli kwa hali ya kawaida upate pesa
nyingi kama hizo usikumbuke kabisa hiyo namba yako ya bahati….nina mashaka
makubwa na malalamiko yako hayo…’akasema akimwangalia mlalamikaji kwa macho ya
huruma.
‘Na je inawezekanaje ushinde, kwa pesa nyingi kiasi hicho,
hata watu wa kampuni hiyo wasikukumbuke….kwa hali yoyote sisi tunaolalamikiwa
tunakuwa na mashaka na malalamiko yak o hayo na tunaona unatumia mwanya huo
kudai mali ya marehemu, kwa vile hayupo duniani, na wengi tunaona kuwa mtu
akifa hana lake…..hapana , mtu akifa kama alikuwa na haki yake bado itaendelea
kulindwa kisheria kama alivyotaka iwe, na sis ndicho tunachokifanya, tafadhali
heshimuni kauli za marehemu, msipende mali za dezo …..’akatulia na kuangalia
watu ambao walikuwa wametulia kimiya wakimsikiliza.
‘Ndugu muheshimiwa hakimu, sisi tunaolalamikiwa tunasema
tena, je walalamikaji wana ushahdi gani, kama vile hati ya malipo, japo moja
tu, ili tuwe na ushawishi wa madai yao hayo, aionyeshe hii mahakama yako
tukufu,..kuachilia mbali ushahidi wa maneno, wa kuongea, ….’akasema
akimwangalia wakili mwanadada.
‘Kuongea kila mtu anaweza kujenga hoja na kuwashawishi
watu,….na huenda akaweza kufanya hivyo, hata kama anayoongea sio kweli, lakini sio
hapa. Hapa ni shemu ya kutafuta haki, haki kwa ushahidi wa vitendo, wa vitu,
…kwahiyo sisi kisheria, bado tunahitaji ushahidi halisi. Je unayo huo ushahidi
kuweza kuishawishi mahakama kuwa kweli wewe ndiye uliyelipwa hizo pesa na wala
sio udanganyifu…’akasema huyu wakili akiwa kamkazia macho huyo mwanamama, na
yule mwanamama akasema.
‘Je na wewe unao ushahidi kuwa ndugu yako ndiye aliyejenga
hiyo nyumba kwa pesa zake, na pesa hizo alizipatia wapi, wakati alikuwa
amefungwa jela….?’ Akauliza huyo mwanamama na watu wakawa kama wanaguna, maneno
ya huyo wakili mtetezi yalionekana kuwagusa watu, na kila mtu alihisi kuwa huyo
mwanamama huenda alikuwa akidanganya ili apate mali ya marehemu kiujanja.
‘Hilo tulishaliongea awali, kuwa marehemu pamoja na shughuli
zake nyingi, alikuwa akijishughulisha na biashara ya kutafuta madini, na hilo
linafanywa na wakazi wengi wa hapa, kama unavyoona, kuwa eneo letu limezungukwa na aridhi yenye
madini, na yeye katika kuhangaika akajaliwa kupata hizo pesa….sio ajabu wengi
wamefanikiwa hivyo hivyo. Tatizo la huyu marehemu alipopata hizp pesa alikuwa
na wenzake, ….na wenzako walipogundua hilo, wakataka kumdhulumu, na ndipo akaamua
kukimbilia Dar…’akasema.
‘Una uhakika na hayo maneno yako,…na je unawezaje
kuithibitishia hii mahakama kuwa kweli unayozungumza yana ukweli, yapo wapi
maandishi kuwa pesa hiyo aliipata kwa kuuza madini, upo wapi ushahidi wa
kulipwa hizo pesa, maana tujuavyo ni kuwa wengi wakiuza madini wanauza kwenye
makampuni makubwa ambayo hutoa stakabadhi za malipo….je upo wapi ushahidi
wako?’ akaliza mlalamikaji.
‘Ndugu hakimu, mlalamikaji anauliza swali ambalo halihusiani
na kesi yetu hii,lakini kama atashikilia kauli yake hiyo, sisi tunaweza kuipata
hiyo staakbadhi, lakini sio kwa leo, maana haikuwa na umuhimu kwa kesi hii hapa
…na sisi tumemuuliza yeye kisheria kwa vile yeye ndiye anayedai kuwa pesa hiyo
aliipata kwa kulipwa na kampuni ya simu, na sio sisi kudai kuwa pesa hiyo
tumelipwa kutokana na kuuza madini…kama anahitajia kesi nyingine, madai mengine
kuhusiana na hilo, tunaweza kuja kuthibitisha hayo….’akasema.
‘Sasa nyie mnataka nitoe ushahidi gani kuhakikisha kuwa
kweli nililipwa hizo pesa, wakati hali halisi nilishaielezea..?’ akauliza na hapo
wakasikika sauti kutoka kwa mmoja wa watu waliohudhuria kwenye hiyo mahakama
akisema;
‘Waonyeshe huo ushahidi…..’na watu wakageuka kuangalia sauti
ilipotokea lakini hakukugundulika kwa haraka ni nani alitamka maneno haya ,….labda
kwa wale waliokuwepo karibu na mzungumzaji,… hata hakimu ambaye alitaka kusema
neno akatulia na akawageukia wazee wa mahakmaa na kuanza kuteta nao jambo na
wakili mtetezi akasema, bila kujali kuwa hakimu anaongea na wazee wa mahakama
akasema;
‘Tunahitaji ushaidi wa kumbukumbu za malipo, ambazo
zitathibitisha kuwa kweli ulilipwa hizo pesa….vinginevyo kwa vile mnataak
kulipaka jina la marehemu, tutafikiria kuchukua hatua nyingine…’akasema huyo
mwanasheria akimsaidia wakili wake.
Yule mwanamama,
akageuka kuangalia kule walipokaa watu, ilionekana alikuwa akimtafuta
mtu kwenye kundi hilo, na watu wote wakageuka kufuata macho yake, lakini hakuna
cha tofauti kilichoonekena, na watu waliokuwepo pale wengi wao walikuwa
wametulia kimiya wakifuatilia hayo malumbano,…
Baadaye huyo mwanamama akamgukia wakili wake ambaye
alionekana naye akiangalia kule walipokaa watu, ambapo mwanzoni alimuona yule
mtu aliyekuwa na huo mfuko wa Rambo, na alipoona mteja wake, anaangalia huko, akasema
‘Endelea kuongea, usijali watu na usijali maelezo yake, nia
yake ni kukuchanganya ukate tamaa, usikate tamaa ukitetea haki yako…uwanja ni
wako,….’akasema akiagalia saa yake kwani kwa mtizamo wake muda wa hiyo kesi
umekwisha kwahiyo hapo itakuwa nafasi yake ya kuomba kuiahirisha hiyo kesi hadi
siku nyingine,ambapo angeliweza kupata ushahidi wa kutosha kutetea hoja yao...kauli
ya mwanamama mlalamikaji ikamshitua wakili wake, yule mwanamama alisema;
‘Nataka kuutoa huo ushahidi wanaoutaka,..tumalizane na hii
kesi’akasema.
‘Ushahidi gani….?’ Akauliza mwanadada akiwa anamuangalia
mwanamama mlalamikaji kwa kushangaa, maana siku zote wanahangaika kuutafuta huo
ushahidi na hawakuweza kuupata, na hawakuwa na ushahidi wowote wa maana, …Na
alipoona yule mwanamama akiuchezesha ule mfuko, akauangalia ule mfuko wa Rambo, ambao bado
yule mwanamama alikuwa kaushikilia mkononi.
‘Ninataka kuutoa huo ushahidi wanaoutaka wao,nimeshaupata ….je
ukipatikana kesi yetu itakwisha na hakutakuwa na malumbano tena, maana mimi
sitaki hizo kauli zao za kusema mimi nataka kumzulumu marehemu….’akasema huku
akiinua ule mfuko wa Rambo, aliokuwa ameushika mkonononi na yule wakili akamsogelea
na kuuchukua ule mfuko, akaingiza mkono ndani na kutoa kilichoko ndani yake, ulikuwepo mkoba mdogo wa akina mama, akautoa,, halafu
akamwangalia huyo mwanamama.
‘Huu ndio ushahidi wenyewe?’ akauliza,
‘Fungua hiyo pochi, …’sauti ikasikika tena kutoka kwa
waliohudhuria kwenye hiyo mahakama, na yule wakili akafungua ule mkoba na
kukutana na karatasi zilizokunjwa , na akazifungua, na kuanza kuzisoma kwa
haraka, akasema;
‘Payment voucher….mmh,
to, amount,….exactly….’akainua macho na kumwangalia huyo mwanamama
mlalamikaji huku uso ukionyesha kushangaa,h alafu akageuka kumwangalia hakimu
ambaye kwa muda huo alikuwa akiteta na wazee wa mahakama, na ilionyesha wazi
hakimu alitaka kumaliza kesi, huenda kutoa muda wa kuisikilza tena baadaye au
kusubirisha hukumu.
Akageuka kuwaangaia watu walioshiriki kwenye mahakama hiyo,
halafu akapitisha macho na kuangalia sehemu ile ambayo mwanzoni alimuona mtu
akiinua huo mfuko wa Rambo, na akamuona mtu, ambaye kwa muda huo alikuwa kainama
chini, akiwa na kofia pana, akiwa kama anasoma kitu, hakuweza kubahatisha kuwa
ni mtu gani, akaona ageuke kumuuliza mteja wake,
‘Umeupatia wapi huu ushahidi, ..na nakumbuka nilimuona mtu
akiwa na huo mfuko ni nani huyo mtu?’ akauiliza huku akiwa na hamasa ya
kumtambua huyo aliyempa huo ushahidi.
‘Je kwasasa ni lazima
kumfahamu huyo mtu, maana kinachohitaka hapa ni huo ushahidi, na umepatikana,
hata hivyo aliyenipa huo ushahidi hakutaka ajulikane kwasasa, ila amesema
mtaongea naye baadaye, kwani anataka uwe
wakili wake kusimamia kesi yake ya malalamiko…’akasema.
‘Kesi gani tena hiyo ya malalamiko?’ akauliza na mara wakashituliwa
na sauti ya hakimu ikasema;
‘Je mlalamikaji una ushahidi wowote wa kuthibitisha hayo
yote, …kuwa ulishinda na kulipwa hizo pesa, au tumalize hii kesi maana muda
umekwisha..’akasema hakimu akimwangalia wakili wa mlalamikaji?’
‘Ndugu hakimu, kabla sijatoa huo ushahidi, namakumbusha
mtetezi kwa kauli yake kuwa ukipatikana huo ushahidi, basi anatabatilisha
umiliki wao kwenye hizo mali walizozimiliki isivyo halali…je wapo tayari kwa
hilo?’ akauliza. Hakimu akageuka kumwangalia wakili mtetezi, ambaye alipoona
karuhusiwa kujibu hilo swali akasema;
‘Ndugu muheshimiwa hakimu, sisi tuna imani kuwa hawa watu
hawana ushahidi wowote, wanachotaka kwa sasa ni kupoteza muda, ili kesi hii
ichukue muda mrefu, sisi kauli zetu zilisikika na kuwekwa kwenye kumbukumbu
hatuna haja ya kuzirejea,…’akasema huyo wakili mtetezi.
Wakili mwanadada akasema; ‘Namuomba nimsimamishe mtu wa
kampuni ya simu waliolipa hizo pesa …’akasema.
‘Wa nini…?’ akauliza hakimu akinangalia saa yake.
‘Ili athibitishe huo ushahidi wetu..’akasema wakili
mwanadada, na hakimu akamuangalia wakili wa utetezi kama anapingamizi lolote, lakini wakili wa utetezi
alikuwa akiteta na mwenzake, na pasipo na kujali akasema;
‘Hatuna pingamizi muheshimiwa hakimu, tuna uhakika kuwa
hawana ushahidi …’akasema na yule shahidi wa kampuni ya simu akafika pale mbele
, na wakati huo mlalamikaji alikuwa keshaondoka kwenye kiti cha mashahidi.
‘Hizi hapa ni stakabadhi za malipo, naomba uchukue muda
kuzichunguza na utuambie ni kitu gani…na je ni za uhakika, hazijagushiwa kama
anavyodai wakili mtetezi..?’ yule shahidi akazichukua zile nyaraka na kuanza
kuzifungua na kuziangalia vyema , halafu akasema;
‘Hii ni payment
voucher, ni nakala ya mlipwaji, huwa tukilipa pesa kuna kuwa na nakala
mbili, moja tunabakia nayo kwenye kumbukumbu zetu na nyingine anaondoka nayo
mlipwaji..’akasema.
‘Je ni ya ukweli nakala hiyo, umeichunguza vyema, kuwa kweli
inatoka kwenye kampuni yenu na haikugushiwa kama walivyodai watetezi…?’
akaulizwa.
‘Ni ya ukweli inatoka kwenye kampuni yetu, haina
shaka…’akasema.
‘Je unaweza kutaja jina mlipwaji kwenye nakala hiyo, na
ililipwa kwa ajili gani…’ akaambiwa huyo shahidi na yule shahidi akaanza kusoma
jina la mlipwaji na kiasi cha pesa na maelezo ya kwanini pesa hiyo ililipwa….
‘Muheshimiwa hakimu tunawakilisha ushahidi walioutaka
walalamikiwaji, na kutokana na kauli yao, sisi hatuna zaidi…’akasema wakili
mwanadada, na kumfanya wakili mtetezi na msaidizi wake wabakie wameduwaa…na
mara kwa nyuma ikatokea sauti ya ukali ikisema;
‘Haiwezekani, hatukubali kamwe….mimi kama kaka mkubwa wa
familia sitakubaliana na hilo….’ Watu wote wakageuka kuangalia hiyo sauti
imetoka wapi………
NB: Haya...KUMEKUCHA, ushahidi ndio huo...sijui ndio wenyewe au..., na kama ndio huo, je
wanafamilia walalamikiwa watakubaliana nao, je watachukua hatua gani, tusikose sehemu ijayo ya kisa hiki,
wema hauozi. Kwakweli natamani nipate moderm, haraka iwezekanavyo..
WAZO LA LEO: Siku
hizi watu hawaogopi kusema uwongo, kuzulia wenzao ubaya, na zaidi ya hayo, watu
hawaogopi kudhulumu mali za marehemu. Wapo ambao walioaminiwa na marehemu alipo
kuwa hai, wakapewa dhamana hzio, ili kuzitunza au kuwakabidhi wanaostahiki, baadaye
mlengwa alipofariki,wanageuka kuwa mawakala wa kuzihujumu hizo mali,na kuwaacha
mayatima na wajane wakihangaika
Jamani, kumbekeni kula mali ya mayatima na wajane ni dhambi
kubwa sana, na kumbukeni kuwa, na nyie hamtakaa milele kwenye hii dunia,
mtaondoka, na jinsi mlivyowatendea wenzenu na nyie watoto wenu watatendewa
hivyo hivyo….kumbukua dhambi ya dhuluma haidumu.
Ni mimi:
emu-three
6 comments :
dhuluma mbaya na m'mungu apendi na haki ya mtu aipotei bure.
haki ya mtu haipotei bure
dhuluma mbaya kwa kweli.....ila watu inapofika kwenye jambo hili husahau kabisa...tupo pamoja...
Ni kweli kabisa mnayosema dhulma haifai na haki itaonekana. Ubarikiwe M3
Ni kweli kabisa mnayosema dhulma haifai na haki itaonekana. Ubarikiwe M3
Kweli kbs hali ya mtu haiendi hivi hv dhulma mbaya jamani hii Ni fundisho kwa wote. Ubarikiwe m3 kwa kutupa darasa na kutuburudisha.
Post a Comment