Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, January 14, 2013

Uchungu wa mwana Aujuaye ni mzazi-47
Mama Maua alifungua mlango taratibu, na alipopata upenyo wa kutosha akachungulia kwa  kupitia kwenye ule upenyo mdogo, kuangalia nje, …akaona watu wamesimama, walikuwa maaskari wa msituni, aliwatambua kwa mavazi yao, akajua ndio huo ugeni umeshafika,….akaufunga ule mlango kwa haraka. na moyo ukawa unamwenda mbio, akatulia, na kupangusha macho yake , …halafu akajiangali alivyovaa, alipohakikisha kuwa yupo tayari, akashika mlango, akaufungua kwa mapana.

Na askari wawili wakapiga hatua tatu mbele hadi wakawa karibu na ule mlango, wakainamisha vichwa vyao…na kutulia , na walikaa hivyo kwa muda hadi Mama Maua aliposema;

‘Karibuni wageni….’akajitahidi kutoa sauti, lakini sauti iliyotoka hapo ilikuwa kama sio yake.
Wale askari wawili  wakasogea pembeni, na kuonyesha ishara kwa wenzao, ambao walikwua wamesimama kwa mbali wakiwa na silaha zao. Wale askari waliokuwa kwa mbali wasogea hadi sehemu iliyopo wazi …walipafika pale wakasimama, na wakaja wengine wane wakiwa wamebeba vifaa vyao, ilikuwa ngozi ya chui, na viti vya kienyeji, vilivyopambwa kwa ngozi za wanyama,wakaviweka, sehemu ambayo huenda kiongozi wao atakaa, …halafu wakageuka kumwangalia mama Maua.

‘Huko ndani yupo nani ?’ akaulizwa, na kabla hajajibu, askari wawili wakawa wamesogea hadi pale mlangoni aliposimama Mama Maua.

‘Nipo peke….peke….yangu’akasema akisita hakutaka kusema yupo na mtoto, na kusita kwake kule kukawapa wasiwasi wale maaskari, ….mmoja akasogea mlangoni na kusema;

‘Samahani mama, sisi tunahitaji usalama, hatuna nia mbaya, naomba niingie ndani nihakikisha unayoongea maana kauli yako hainirizishi’akasema yule askari na hata kabla mama Maua hajamaliza yule askari akawa keshaingia ndani.

Baadaye alitoka na kumpa mwenzake ishara….na mwenzako akatoa sauti Fulani, ambayo ilikuwa ya kuashiria jambo, kwani baadaye kulianza kuwasili kikosi kingine, na kati yao kulikuwa na mmoja kapanda juu ya punda, alikuwa ni malikia…..

Maua akawa anamwangalia malikia anavyokuja akiwa juu ya yule punda, aliyewekewa ngozi nyingine iliyotengenezwa na kuwa na kiti kizuri cha kukalia,..akasema kimoyo kimoyo,;

 ‘Ndio malikia kaja peke yake tena….ina maana kaamua kuja yeye badala ya mfalme wao?’ akajiuliza, na akatupa jicho la kujiiba, na kuangali huku na kule kama atamuona mtu wake anayemtafuta, lakini hakuona dalili yake,..moyo haukutulia, na akaona akiendelea kuvumilia anaweza kupata shinikizo la damu, akamsogelea yule askari na kumuuliza …

‘Mfalme wenu yupo wapi?’ akaumuuliza yule mlinzi, yule mlinzi alimwangalia tu bila kusema neno, na Mama Maua akasogea mbele, kwani aliishiriwa kufanya hivyo, na yule mtu askari aliyekuwa akliongoza hupo msafara akatoa ishara na mara malikia akasonge mbele na kikosi chake.

Ule msafara wa malikia ulisogea hadi karibu na mlangon na malikia akateremka, na kumkabili mama Maua, na mama Maua kwa vile alishajua taratibu zao, alipiga magoti mbele ya malikia na kuinamisha kichwa, na malikia akamshika kichwani kama ada yao akambariki, na baadaye akaambiwa ainuke,…

‘Kamachukue mtoto ndani….’akasema malikia kumuamrisha mmoja wa watu wake, na kweli akaingia na kumchukua mtoto. Hawakuongea kwanza, kwani kulikuwa na taraibu za kumhudumia mtoto, na hizo zilitakiwa kufanyika mbele ya mama malikia, ikiwemo kumuogesha, kumpaka aina Fulani ya mafuta ya msituni, ambayo wao wanaamini kuwa yanaondoa magonjwa, nuksi na mengineyo.

Baada ya taratibu hizo, …walimchukua yule mtoto na kukaa naye pembeni, na malikia akamsogelea mama Maua na kumsalimia, na wakaingia ndani na kuanza kuongea mambo mbali mbali,….

‘Samahanii kwa kukuingilia, lakini naomba uelewe kuwa sasa hivi nalelewa kama mama malikia, kuna taratibu nyingi ambazo hata mimi zinanipa shida sana, kwani siwezi kujifanyia baadhi ya mambo mwenyewe,…na kiusalama siwezi kuwaingilia, kwani wao wanajua zaidi..inabidi niwasubiri mpaka wamalize kazi zao, …halafu ndio….’akasema malikia na kukatisha kwani alionyeshwa ishara Fulani na watu wake.

‘Mume wako ndio huyo anakuja ?’ akauliza malikia, na mama Mua akaangalia kwe mbele, na kumuona yule mwanaume akija akiwa kavaliwa nguo na tai…huwa mara nyingine anajipenda sana, lakini hakujua wapi kazipatia nguo nzuri ….

‘Sio mume wangu, jamani…ninaishi naye tu humu ndani,….mimi siwezi kuwa na mume mwingine tena, baada ya huyo aliyenipa mimba, ambaye tulipendana sana sikuwahi kufikiria kuwa ninaweza kuachana naye….lakini ndio dunia, na …’akasema mama Maua akitabasamu.

‘Na…na vipi mbona humalizii, usiniambie kuwa uliwahi kukutana na mwanaume mwingine akakuingia akilini, zaidi ya huyo aliyekupa mtoto, …hebu niambie rafiki yangu’akasema malikia huku akitabasamu.

‘Aaah, sio hivyo, unajua kuna hali unaweza ukaipitia na ukazoeana na mtu , ukafikia kusema kuwa huyu anafaa kuwa mume wangu…lakini je huyo mwanaume naye ana mawazo kama yako…na sijui kama kweli ninaweza kumuona tena…’akasema huku akiangalia nje.

‘Unasema kuhusu yule mwanaume aliyekuoakoa…nimekupata, sasa nimejua kwanini ulikuwa ukihitaji uonane neye tena..hilo lipo, nakubaliana nalo, kuwa unaweza ukajiukuta kwenye shida, matatizo na akatokea mtu anakujali na kuwa tayari kukusaidia..ukawa na ye hadi ukamzoea na hata kutamani kuwa naye milele……’akatulia malikia kwa muda.

‘Ni kweli….mimi nakubaliana na wewe,na hayo ni maumbile,….nikuulize mfano akatokea huyo aliyekuapa mtoto na huyo aliyekusaidia ukaambia uchague mmojawapo utamchagua nani?’ akauliza malikia.

‘Sijui….na wala sikuwa nawazia hivyo, mimi nijuavyo, kila kitu huja kwa wakati wake…na kama ikitokea hivyo, basi nitasema mwenye kisu kikali ndiye atakayekula nyama….’akasema mama Maau huku akitabasamu,

Hiyo ilikuwa kwa mara ya kwanza kumuona mama Maua alitabasmu, maana muda wote uso wake ulitawaliwa na huzuni,….hana raha,…na hapo malikia akamwangalia kwa makini na huruma , upendo ukamjaa moyoni, akasema;

‘Hebu nikuulize, mfano huyo mtu aliyekuokoa akaja na kukuambia kuwa yupo tayari kukuoa,. ..lakini ni lazima mkaishi naye msituni utakubali?’ akauliza.

‘Maswali yako ni magumu sana…jibu la swali hilo ni kama swali la mwanamke anayetaka kuolewa, sizani kama ana hiari ya kuchagua wapi pa kwenda, lakini kwanza kuwa na hali hiyo ya kuolewa, kimoja ndio hufauata kingine….’akasema mama Maua.

‘Nimekuelewa mpenda, na natumai…mambo yatakwenda vyema, tusubiri kimoja ili kifuate kingine, au sio?’ akasema malikia.

‘Kwani huyo mfalme atakuja ?’ akauliza.

‘Kimoja ndio kifuate kingine, kwanza tunahitaji kumuona huyo mtu wako, au sio..natumai moyo wako upo radhi kumuona huyo mtu aliyekuokoa zaidi ya mfalme,…au sio?’ akauliza malikia na kabla hajajibu akamuona yule mwanaume anayeishi na mama Maua akipita na kukaa sehemu ambayo kulikuwa na walinzi, hakutaka kuingia ndani.

Malikia alimwangali yule mwanaume kwa nje, halafu akamgeukia mama Maua na kusema;

‘Wengi wanasema huyo ni mume wako,…. lakini hayo hayatuhusu kwa sasa, au sio, kimoja kwanza kingina kitafuattia..’akasema na kutabsamu, lengo lake ni kumfanya mama Maua naye atabasamu, lakini ilikuwa sivyo, mwenzake akaonekana kuingia na ile hali ya huzuni.

‘Mimi nakuona huruma sana naona kama unaishi maisha ya taabu, kwani huyo mwanaume, anajulikana sana kuwa ni  mlevi, na muuza pombe kali…na akilewa huwa mkorofi sana, na hili tumaliogopa hasa kwa mtoto…’akasema malikia.

‘Ndio yeye mwanaume aliyeamua kuishi name, kwa kipindi hiki cha shida, siwezi kumtupa, ….pamoja na mapungufu yake namshukuru sana kwa kunijali,…kwani kuna wakati nazidiwa, mwanaume wa watiu anahangaika huku na kule ninitafutia dawa, japokuwa si lolote, anahotegemea ni kipato kidogo kwa kuuza hizo pombe....’akasema mama Maua akionyesha uso wa huzuni.

‘Lakini ….mama Maua, nakuomba ufikirie sana ombi letu,…kama ulivyosema, umeguswa sana na huyo mwanaume aliyekuokoa, sasa kama je huyo mwanaume akaja na wazo la kukuoa,…utakubali. Hata kama hilo halikuwezekana,  sisi pia tulishafikia maamuzi ya kukukuchukua ukaishi pamoja nasi huko msituni, ..najua unayoaona maisha ya huko kuwa sio ya kawaida, lakini mbona mimi nimeyazoea, …..ni maisha mazuri tu ukiyajulia, …’akasema malikia.

‘Hapana, nashukuru kwa ombi hilo, lakini sitaweza tena kuishi huko, ….mengi yaliyotokea huko, ni machungu sana, sitaweza kutazamana na watu wa huko…..’akatulia kidogo huku akikimbuka yaliyotokea nyuma; jinsi alivyojifungua na baadaye akachukuliwa kwenda kutupwa ziwani ili aliwe na mamba,..je ataweza kuishi  na watu waliomtambua kama mkosi wa jamii zao,….hapana huko sio pa kwenda tena.

‘Nashukuru sana kwa kunijali hivyo, lakini sitaweza kwenda kuishi huko tena ….’akasema huku akiangalia nje, maana kulikuwa na sauti zikiongezeka.

‘Najua utakubali tu, hasa akija huyo mwanaume aliyekuokoa, ….’akasema malikia huku naye akiangalia nje, na kweli nje kukawa na kikosi kingine kinaingia  na mama Maua alipoangalia akaona huo msafara unaoingia kwenye eneo lao,…akawaona punda wawili, ambao waliokuwa wakikokota gari kwa nyuma yao, na ndani ya hilo gari linalokokotwa, ….kulikuwa na watu wawili..

Mama Maua akainua kichwa vizuri kuwaangalia wale watu wawili, mmojawapo alikuwa ni mzee….akamkumbuka, yule mzee, …mzee mteule, mzee aliyemuheshimu sana kwa busara zake, alikuwa kajaa mvi kichwa kizima, lakini kilichomvutia sana na kumfanya moyo wake usitulie ni yule aliyekuwa pembeni mwake….

‘Oooh ndiyo yeye…’akajikuta akisema kwa sauti.

‘Ndio ndio yeye….’akasema malikia akitabasamu.

Yule mtu alikuwa kavalia kiaskari, na kichwani kavalia kofia, kofia ambalo lilimfunika kichwa kizima…kama vile vile….akatabasamu na akageka kumwangali malikia, na malikia akatabsamu pia. Malikia akainuka na kumshika mkono mama Maua na kumwambia.

‘Haya twenda ukampokee…’

‘Lakini, …mfalme yupo wapi?’ akauliza mama Maua.

‘Kimoja kwanza, ndio kifuate kingine…au sio ’akasema malikia huku akitabasamu, na mama Maua akatabasamu….lile tabasamu la uhakika, tabasamu ambalo malikia hakuwahi kuliona kwa huyu mama kabla, …wakaondoka wote wawili kwenda kuwapokea hawo wageni maalumu….

NB: Kulikuwa na muendelezo wa sehemu hii lakini muda, jamani muda…unakimbia kama nini..

WAZO LA LEO: Sisi sote ni wana wa Adam, hatuna haja ya kuzarauliana, kama umejaliwa kipato, hali nzuri, sura nzuri, nk, usijione sana na kuwadharau wenzi wako. Ukumbuke sura nzuri, kipato ulicho nacho, maisha bora, uongozi nk ni wa kupita tu, kuna leo na kesho, kuna kupanda na kushuka, …shukuru mungu kwa majaliwa hayo, na watendee wema wenzako, ili upate baraka kutoka kwa mwenyezimungu.

Ni mimi: emu-three

No comments :