Adam, alipotoka pale
kwake, aliondoka kwa kujificha hadi sehemu ambayo walipanga kukutana na
wenzake, alipofika hapo, akakuta taarifa hiyo kuwa anatafutwa sana na Malikia,
akajua ni kwanini, akaona ili kuzuia shari ni bora amwendee huko huko nyumbani
kwake, lakini akagundua kuwa hawezi kumkuta nyumbani kwake, kwasababu ya msako
wa polisi.
Akamtafuta mtu wa karibu wa Malikia, na huyo jamaa
akamwambia wapi anaweza kumpata Malikia, na hpo hapo akaelekea huko
alipoelekezwa, na huku akielekea huko kwa tahadhari, maana hata yeye ni mmoja wa watu wanaushukiwa kutafutwa na
polisi, kwahiyo ilibidi awe makini, akawa anawaza;
‘Huyu nisipomuona anaweza kwenda kumsumbua Kais, na
nisingelipenda itokee hivyo, ikizingatiwa ana mtoto mchanga, …’akasema na wakati huo alikuwa keshafika eneo
aliloelekezwa, na wakato wote huo, hakujua kuwa nyuma kuna watu wanamfuatilia.
Alipofika mitaa ya vichochoroni, hapo akili yake ikatulia,
na zile hisia zake za jabu ajabu zikaanza kumsumbua, na tangu afike hapo
Mererani, amekuwa akizipuuzia hizo hisia, lakini hapo akahisi kuna
jambo,…akatuliza akili, na kuanza kutafakari, afanye nini kuhusu hizo hisia, zinamuashiria
kitu gani, akakumbuka kuwa polisi wapo kwenye msako, na hiyo hisia inamkanya
kuwa awe na tahadahari.
Akaanza kuingia vichochoroni, kuhakikisha hakuna mtu
anayemfuatilia kwa karibu, aliafanya hivyo hivyo, hadi, akafika mtaa wa kichochoroni, na hapo akahisi yupo salama,
ndipo akaanza kuitafuta ile hoteli aliyoelekezwa, ambayo ipo ndani kwa ndani,
na ukifika hapo huwezi kujua kuna nyumba ya wageni.
Akagonga mlango wa ile nyumba ya wageni, akaona kimiya, akagonga tena, na kusubiri, na
wakati anasubiri, akahisi hisia ya taahdhari,…haraka akageuka nyuma, aliona
kama mtu akijificha kwa mbali,lakini hakuwa na uhakika, lakini hisia zikamtuma
kuwa yupo kwenye hatari,…
‘Lazima kuna mtu ananiufuatilia hii sio bure,…’ akaona ili
athibitishe hilo, arudi huko alipotoka huenda akakutana naye, lakini swali
likamjia kwa haraka je, kama ni askari, atafanaya nini, na yeye wiki nzima sasa
amekuwa akiwakwepa.
Hakusubiri tena kuonana na Malikia, akageuka na kuanza kurudi alipotoka, na hata
alipofika pale alipohisi kuna mtu, hakuona mtu yoyote, akarudi hadi maeneo ya
mjini, na alipofika huko mjini, akatafuta sehemu ya kupigia simu na kumpigia
malikia, hakutaka kabisa kutumia simu yake.
‘Unasikia malikia, kuna watu wanakufuatilia, hapo ulipo
ondoka haraka’akamwambia.
‘Sikiliza wewe…mimi sio wa kuja, hilo nalijua sana,.. na kwa
taarifa yako nipo huku ulipomficha Malaya wako, na ole wake nikimkuta,
atanitambua kuwa mimi ni nani, na huyo kifaranga wenu, atanitajia jina lake
kabla hajafikia muda wake wa kuongea,…’akasema na kukata simu.
Adam, aliposikia hivyo, hakujali tena kuangalai nyuma,
akaanza mwendo wa haraka kwenda huko alipompangia chumba Kais, alijua
asipomuwahi huyo malikia anaweza akafanya lolote baya, na huyo mwanamke
hataweza kuvumilia, na kwa vile ni watu wa huko msituni ambao wanajulikana kwa
hasira lolote linaweza kutokea. Akakumbuka alivyohadithiwa na watu
wanaowafahamu watu wa msituni
‘Wanawake wa msituni ni kama wanaume, wanaweza kupambana
hata na simba, na wana hasira sana, kama mkikosana naye, inabidi ujifunge kweli
kweli, kwani anaweza akakuumbua’alikumbuka jamaa yake akisema.
‘Na ole wake umguse mtoto wake, wana hasira hawo, ni sawa na
kuku umguse kifaranga chake, atakutoa macho…..’akakumbuka, na hapo akajua huko
kutakuwa na vita vikali, maana na Malikia naye hana dogo…akazidiwa anaweza
kutumia silaha yoyote, na kumtoa roho mwanadamu mwenzake, kwake kazi rahisi,
tu….
Alifika sehemu ya nyumba hiyo, akagonga mlango , kulikua
kimiya, akagonga tena, na mara mlango ukafungulia, akajikuta yupo uso kwa uso
na malikia, wakaangaliana kwa macho ya kuulizana bila kusema neno, na Adam,
akageuka nyuma, akahisi hali ile ile ya kuwa kuna mtu anamfuatilia, akahisi
mwili ukimsisimuka kwa woga,..lakini kwa
muda ule hakujali, alichojali ni kuhakikisha usalama wa Kais na kichanga chake.
‘Yupo wapi Kais, ….maana naona nyumba ipo kimiya?’ akauliza.
‘Ndio jina la huyo Malaya wako, eeh, Kais, jina gani hilo
lisilo na mvuto …..’akasema Malikia akiwa kakunja uso kwa hasira.
‘Nimekuuliza swali, yupo wapi Kais, maana huyo ni mgeni hapa
mjini, na hahusiki lolote na maisha yetu, na ukumbuke ana mtoto
mchanga..’akaanza kuongea Adam.
‘Hayo maelezo yote ya nini,….mimi hayanihusu, kinachonihusu
ni pesa yangu unayotumia kuhongea ,Malaya wako, na kulelea watoto wasio wako,
toka lini ukawa msamaria mwema, mtu ambaye hata senti moja yako hutaki ipotee hivihivi…’akasema
Malkia akitokeza kichwa nje kuangalia huku na kule.
‘Kwanza niambie huyo jamaa aliyesimama pale mbele ni jamaa
yako?’ akauliza Malikia.
‘Jamaa gani, mimi sikuja hapa na mtu yoyote, nipo peke yangu’akasema Adam,
huku akiangalia huko nje bila ya kuona mtu yoyote, lakini kwenye hisia zake
alihisi kuwa kweli kunawezekana kuna mtu bado anamfuatilia, lakini kila
akigeuka huwa hamuoni.
‘Tatizo lako haupo makini kabisa, na hujajifunza kila
ninachokufundisha, sasa naona una doa jeupe kisogoni mwako, uwe makini,….’akasema
Malikia akiwa bado anaangalia nje kwa makini.
‘Nilihisi kuna mtu, nikampoteza….sizani kama atakuwa kaja
hadi huku, nimechukua tahadhari zote, lakini nahisi….., ‘akasema Adam, akiwa na
wasiwasi, akikumbuka jinsi alivyoteseka siku moja aliposhikwa na kuweka
mahabusu, na akaambiwa kuwa hapo ni mahabusu tu, huko jela ndio balaa…akaanza
kuhisi wasiwasi.
‘Tatizo lako huyajui haya maisha ya kutafuta pesa, unachojua
wewe ni kutumia tu, hujui pesa hizo unazotumia zina jinsi yake ya kuzitafuta, na
maadui wapo kila kona, na nimepata taarifa Komandoo yupo hapa mjini….’akasema
Malikia.
‘Kwani huyo Komandoo ni nani, maana kila mtu anamuongelea
yeye tu, ana tofauto gani na askari wengine?’ akauliza Adam.
‘Ipo siku utakutana naye, utajionea mwenyewe, huyo hajali
pesa, akiamua kazi ni kazi tu, na huwezi ukajificha, popote ulipo atakupata tu,
sijui ni mwanga yule jamaa….sasa kwako wewe nahisi jela inakunukia, na mimi
sikubali kukamatiwa hapa…nilikufuata kwa kazi maalumu…’akasema huku
akichungulia tena nje.
‘Kazi gani kipindi kama hiki….’alalamika Adam, na Malikia
akamwanalai usoni, kwa macho ya kumsimanga, akahisi moyo wa huruma ukimwingia,
kitu ambacho anajiuliza kwanini anapokutana na huyo mwanaume inakuwa tofauti na
wanaume wengine…akamsogelea na kumshika shavuni kwa mkono wake lakini, akasema;
‘Huu sio muda muafaka wa kukupa hiyo kazi,….mimi naishia,
tafuta muda tuonane tena haraka, ukiwa na pesa yangu, la sivyo, utaozea
jela….hilo nakuhakikishia, …na kama sio jela, utarudishwa kwenu na jeneza’akasema
Malikia huku akichukua mfuko na haraka akatoka nje.
‘Sasa unakwenda wapi, hujaniambia kuhusu Kaisi na mtoto wake, umewapeleka
wapi?’ akauliza.
‘Kama bado muda huu unamuwaza huyo Kais, badala ya kuwaza
jinsi ya kujitoa kwenye mtego wa maaskari, hivi huoni kuwa umeshazungukwa na
maaskari, hao watu wanakufuatilia ndio hawo vijana wake, wanachotafuta ni muda
muafaka wa kukunasa, kuwa makini, mtoto wa mama, ….unadeka sana,….haya
nakutakia kila la heri, na kwa jibu la
swali lako, utalipatia huko huko jela , zubaa hapo hapo uone….’akasema Malikia
na akitokomea mitaani.
Malikia, akatoa khanga kwenye mkoba wake, akachukua wigi,
akalivaa, halafu taratibu akatoka nje, na haikuchukua muda, kukawa kimiya,
akabakia Adam, akihangaika huku na kule, hakujua wapi Kais, kaeleeka na mtoto
mchanga, au huenda Malikia kamtimua…..na mara hisia za hatari zikatanda akilini
mwake.
Adam, akatoa kichwa nje, na kuangali huko na kule, lakin
hakuona mtu, ila alihisi kuna mtu…..hisia zikamtuma hivyo….kuna mtu yupo nje,
anamsubiri. Akarudisha kichwa ndani na kwa haraka akaanzakukagua mle ndani,
ndipo akakuta kuwa nguo na vitu vyote vya Kais havipo, na hata nguo za mtoto
hazipo, akajua huyo mwanamke atakuwa keshaondoka, na kama keshaondoka atakuwa
kaelekea wapi na mtoto, …akatoka nje, na kuwauliza majirani.
‘Yule mama mwenye mtoto asiyejua Kiswahili vyema, ameondoka
na mtoto wake, amesema anahisi sehemu hiyo haina usalama kuishi na mtoto wake,…alituambia
ukija, kama unamuhitaji unaweza kumpata sehemu
ile ulipomchukulia’akaambiwa.
‘Aliondoka peke yake?’ akauliza.
‘Ndio alikuwa peke yake….’akaambiwa.
Adam, aliposikia hivyo, akajua huyo mwanamke huenda karudi
kule eneo la mlimani na lengo lake ni kurudi huko kijijini kwao. Akaona ni
vyema kumfuata huko huko, lakini safari hii akaona awe mwangalifu, kwani hizo
hisia kichwani mwake, zinamtahadharisha kuwa kuna hatari, kwahi kwanza cha
muhimu ni lazima amjue huyo anayemfuatilia nyuma ni nani, na je kuna usalama
kwake, asije akawa ni polisi.
Kabla hajaondoka, akaanza kutafuta ….
Akafunua godoro, na kuangalia pale alipokuwa kauweka mzigo
wake, …hakuna kitu, akaanza kuingiwa na wasiwasi, akaliondoa godoro lote,
hakuona kitu, akachukua kistuli, akapanda juu yake, na kwa juu akafunua
kifuniko cha mbao, ambacho alikibadua mwanzoni na kwa juu akaweka sehemu ya
mzigo wake, na hapo ahkuona kitu, ….
‘Huyu atakuwa na Malikia, maana yeye ndiye alinifundisha
mbinu hizo za kuficha mizigo ….hakuna angeligundua kuwa nimeficha mzigo
mwingine sehemy kama hiyo, na sizani kuwa ni Kais, huyu hawezi kujua nimi
umuhimu wa huo mzigo, au ni huyo jamaa aliyekuwa akinifuatilia, ….hapana huyo
atakuwa ni Malkia.
‘Yaani kaamua kuchukua mzigo wote na pesa yangu yote,
..nitaishije mimi, …hata mimi sikubali’ ‘ mara akasikia sauti za watu wakiongea
kwa nje, akachungulia dirishani, ….akaona ni jamaa wawili wageni usoni mwake,
mmoja alikuwa akionyeshea kidole mlangoni kwake,
‘Hawa ni polisi….’akasema kwa wasiwasi, akageuka na kuangali
dirishani la nyuma,, akalifungua na kuchana nyavu zake ambazo zilikuwa kama
nguo, na bila kupoteza muda, akaruka, na kuanza kukimbia,….
********
Malikia alifika sokoni, na alijhisi kuwa kuna mtu yupo nyuma
yake anamfuatilia kwa muda mrefu, akajua ni hawo vijana waliokuja karibuni,
ambao hajazoeana nao, akawa anatafuta njia ya kumvuta ili amuone sura yake
lakini kila aliposimama , jamaa huyo hujificha…
‘Huyu anaonekana ni mgeni wa kazi hii, ngoja nimuonyeshe
kuwa mimi ni mtoto wa mjini’akasema na kujichanganya na watu pale sokoni,
akaingia kwenye mgahawa halafu akaingia chooni, alipotoka alikuwa sio yule
Malkia wa mwanzo, na akaelekea kule alipotoka, hakufika mbali,akakutana na yule
jamaa ambaye kwa muda huo alikuwa akihangaika kumtafuta mtu wake.
‘Vipi kaka yangu unamtafuta nani?’ akamuuliza, na yule jamaa
akashituka na kusimama kumwangalia huyo mwanadada, kwanza alionyesha uso wa
mwanaume pale anapomuona binti mrembo, na baaadaye akajifanya kujionyesha yupo
kazini, akasema.
‘Hapana simtafuti mtu…..’akasema na kugeuka kutaka kuondoka.
‘Kama unamtafuta Malikia najua wapi pa kumpata’akasema huyo
binti
Yule jamaa akashituka na kugeuka kumwangalai huyo mwanadada,
na huyo mwanadada akageuka uso haraka kuelekea kule sokoni, kama vile
anamuonyeshea yule askari huko alipo huyo Malikia.
‘Nani kakuambia kuwa namtafuta Malikia, na wewe ni nani,
mbona unafanana naye sana, Malikia ni ndugu yako?’ Safari hii akashindwa
kuficha ile sauti yao ya kiaskari .
‘Wengi wanasema hivyo hivyo, kuwa nafanana na Malikia,
….lakini hatuna udugu wowote na yeye, Nimekuona ukimfuatilia toka kule,
hukuweza kujificha, kwa jinsi ulivyokuwa ukimfuata kwa nyuma na kumtizama
tizama, …haya niambie una nia ya kumpata huyo malikia au umeghairi uliponiona
mimi….?’ akamuuliza.
‘Wewe niambie yupo wapi, ….mengine sina haja nayo?’ akasema.
‘Mengine yapi…afande, unafikiri mimi ni Malaya au,…mimi
nimeamua kukusaidia tu, sina haja ya mengine, twende huku nikakuonyeshe alipo
huyo Malikia maana kila mwanaume akiingia huu mji anampapatikia huyu binti,….
mungelimjua vyema huyo mwanamke, mngekuwa waangalifu sana….’akaambiwa, na yule
jamaa kwanza alisita kumfuata huyo binti, lakini baadaye akaamua kumfuata nyuma
huyo dada, huku akidadisi;
‘Kwanza kwanini unaniita afande, kwani…’akasita kidogo , na
baadaye akauliza swali jingine, kwani huyo Malikia yupoje, inaonekana ni mtu
wako wa karibu japokuwa sio ndugu yako, huyo Malikia yupoje, hebu niambie….?’
Akalegeza sauti na kuuliza.
‘Utamjua mwenyewe ukikutana naye, haina haja ya kuumiza
kichwa chako, pesa yako itaongea, kama huna pesa, sizani kama mtaelewana….’akaambiwa
na wakati huo walishafika kwenye mgahawa mmoja, mlango wake ulikuwa na pazia
kubwa jeupe, na walisikika wateja wakiongea kwa ndani, na yule jamaa akaangalia
huku na kule kwa nje, ..baadaye akanyosha mkono kulifungua lile pazia
Hapo hapo wakati ananyosha mkono, akahisi hatari, alipotaka kugeuka kuangali
kwa nyuma yake, kitu kizito kikigonga kichwani kwake, hakuweza hata kujitetea,
akaona vinyota, na giza likatanda usoni, alichosikia kwa mara ya mwisho ni
sauti nyingi zikibishana, nyingine zinasema hivi, nyingine hivi;
‘Huyu ni kibaka, achomwe moto,….. nendeni mkachome moto huko
mbali sio hapa hotelini kwangu…hapana msimchome moto sio kibaka…’fahamu
zikampotea.
NB: Hayo ndio maisha
ya Kais na Adam, je hawa wataishia wapi, naona sehemu ijayo turudi porini tujue ni nini kiliendelea pale tulipoishia.
WAZO LA LEO: Jitahidi sana usitawaliwe na tamaa, hasa tamaa mbaya,
ni vyema ukarizika na kile ulichojaliwa nacho, kama unataka zaidi fanya yale yaliyo mema, epuka vishawishi vibaya, usitamani vya watu, kwani tamaa mwisho wake ni
mauti.
Ni mimi:
emu-three
2 comments :
Sasa ni mwendo wa kusua sua...sio mbaya hata hivyo ubarikiwe sana
Hiyo display yako ya nyuma nimeipenda sana
Post a Comment