Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, March 20, 2012

Hujafa hujaumbika-5 na 6Kilikuwa kikao cha wanafamilia, kikao maalumu,na kama kilivyokuwa kikao cha mwanzo muhusika mkuu wa kukiongoza alikuwa mjomba. Mjomba ndiye waliemkubali kama kiongozi wa shuguli hii na amekuwa pia kiongozi karibu shughuli zote za familia hii, na mzungumzaji mzuri na amejaliwa hekima ya uongoi Wakiwa wamekaa wamkimsubiri mjomba aanze, kijana ambaye ni mara ya kwanza kuhudhuria vikao kama hivyo, na mlengwa mkuu alikuwa na katarasi yake akiwa kaodhoresha majina.

‘Ndio... nilikuwa nimeandika majina ya mabinti...hutaamini maana , kila jina lilikuwa na taswira ya msichana kichwani mwangu, unafanya mchezo nini, mzee mzima natafuta mke, mke wa kutafutiwa, lakini kwa namna makini kabisa...’akasema rafiki yangu na kuendelea kunipa kisa chake na sehemu hii ni maalimu kwa jinsi alivyompata mke wake wa kwanza,

‘Ilikuwa sio kazi rahisi kama watu wanavyofikiria...kuwa labda nilifika na kuambiwa haya mke huyu tumekuchaguliwa , hakuna ikiwa, ilikuwa kama kutafuta kazi,...na mimi mwenyewe nililipa kipaumbee sana maana hapo nilikuwa nikitafuta mwenza wa maisha, nilikikoroga nimeumia. Nilitizama jina la kwanza na taswira ya huyo msichana akanijia akilini;

Msichana huyo ana sifa zote,.....wazee wanajua kuchagua bwana, sio mchezo, msicha huyu alijaliwa urefu, umbo la nane, tatizo hapa ni mrefu kuliko mimi, lakini hilo sio tatizo kubwa sana, nikaliwekea nyota. Halafu nikaliangalia jina la pili, huyu naye kajaliwa kila , na mmmh mashallah, ni mke Yule tunayeimuita mbantu, ....utajaza mwenyewe mbantu ni maumbile gani, ila yeye alikuwa mfupi kuliko mimi, sasa kati ya hawa wawili nani zaidi...nikaguna kwanza na kuweka kanyota kwenye hilo jina.

Kukaongezeka majina mengine mawili, hawa wao walisema ni nyongeza kama nitakuwa sijatosheka na hawo wawili, nikaliangalia hilo jina la Msichana wa tatu, yeye ana umbo la kadri, lakini kaongezeka sifa moja ya ucheshi, anaogea huyo. Nikasema moyoni ukiwa naye ndani hutasikia ucomvu, maana mtaongea mapaka basi....nalo nikaliwekea nyota.

Haya jina jingine ambalo hata mjomba alinipa utata kuwa jina hilo halikuwepo katika uchaguzi wa mwisho, wanasema liliondolewa kwasababu aliyelileta kama mdhamini hakuweza kuhudhuria kikao cha mwisho, na likaondolewa, kwani kila jina lilitakiwa mtu wa kulidhamini, mtu ambaye yupo karibu sana na huyo mhusika, na anatakiwa kubeba dhamana kma litatokea tatizo.

Nililiangalia lile jina na moyo ukaanza kunienda mbio, sijui ni kwanini, sidhani kuwa alikuwa na sura ya ajabu sana ukilinganisha na wale mabinti wawili wa mwanzoni, au kwa vile wao niliwakuta wakiwa wamejisopu-sopu...lakini kuna hisia nyingine zilitanda kichwani, niliziita hisia za mvuto wa ndani ambazo wenzetu wanaziita `infatuation’...

Kwanza nilitulia sana katika jina hilo, nikiwa naivuta hisia hatu akwa hatua, nilianzia kwenye macho..jamani motto huyu ana macho mzuri, naona mungu alimpendelea sehemu hiyo, macho makubwa, nyuzi nyingi, halafu yanakuwa kama yamelegea...acha weee...

Nikavuta hisa ya uzuri wa mdomo wake, ...hapo sina la kusema, unajua nikuambie kitu, mungu aliwaleta wanawake duniani kuwa mapambo, uzuri wao ni mapambo, na kila kiungo chake ni kivutio cha nafsi, ina maana unaweza ukampenda msichana kwasababu ya macho yake, au mdomo wake, au umbile lake la huku au kule...lakini hapa kwa wazee wangu kiliangaliwa sana tabia, hulka na mwenendo wake na wa jamii yake.

Binti huyu ni wa pekee, kwani hata sura yake nilivyoivuta, ilikuwa inaonyesha kuchoka, inaonyesha uzalili, inaonyesha huruma, kwa haraka haraka,nilisita kusema lolote kwani wengi wa familia yangu hawakumtilia manani, ...nikawaza, au ni kwasababu ya hali yake, au ni kwasababu ya mzazi anayeishi naye....moyo wangu ukatamani niyajue hayo, vinginevyo, mawazo yatabadilika ...

*********

‘Ndugu wanafamilia hiki leo ni kakao maalumu, kama tulivyopanga, kwasababu tunamshughulikia mtu muhimu sana katika familia yetu –msomi. Na kwasababu ni msomi, tukaona mambo haya tuyapeleke zaidi kisomi kisomo. Wenzetu, wasomi wana mambo,... maana jambo kwanza unatakwia uliwekee mchakato, jinsi gani ya kulifanya, hapo hujalifanya, lakini lazima uwe na mpangiliao wa jinsi ya kulifanya...’akatulia mjomba na kuniangalia, nami nikatikisa kichwa kumkubalia.

‘Pili sasa unachuja ule mpangilia kwa kuangalia kipi cha muhimu zaidi , na hapo unaanza kufuatilia kwa kufanya uchunguzi wa hilo jambo, na wenzetu wanasayansi wanasema wanafanya utafiti, na halikadhalika hata sisi katika maswala yetu ya kila siku hatukurupuki tu, ndio maana unaona tunakuwa na mikutano, kama ule uliopita, ule ulikuwa wa kuweka mipangilio kabla ya kupata jambo lenyewe, na baadaye tukaingia kwenye uchunguzi...hatupo mbali na wasomi...’akasema na kugeuka kiniangalia tena, na wakati huo nilikuwa naandika kitu kwenye karatasi.

‘Unajua wenzetu wanathamini sana kalamu,ndio maana kila jambo wanaweka kumbukumbu,ndio maana unamuona mjomba pale kaweka kumbukumbu zake za hayo tuliyoyafanya, hatuna shaka naye , huyo ni msomi wa familia na tuna uhakika mambo yake atayapeleka kisomi, hatutaki atuangaushe, lakini hata hivyo sisi ni wazee wake , lazima atusikilize kwanza...au sio wazee...?’ akauliza.

‘Bila shaka mwenyekiti....’wakasema wazee, na mjomba hakutosheka na hilo akawageukiwa akina mama na wao akawauliza na wao wanasemaje na kwa pamoja wakaitikia kuwa yote aliyosema ni sawa.

‘Unajua uwenyekiti sio mchezo, nashangaa wenzetu wanasema ‘zidumu’, kila kitu kidumu, hapana hakuna kinachoweza kidumu, labda yawe maandishi matakatifu, lakini kwa fikira za kibidamu tu, haziwezi kudumu daima, leo zinafaa kesho hazifai,ndio maana tunakuwa na vikao kujadili hayo yaliyopendekezwa awali, mengine yanaweza yakafaa leo kesho yasifae, hata maamuzi yetu tuliyodhamiria yanaweza mwishoni tukaona hayafai..ni kawaida maana binadamu ni mzaifu tu....’akasema na kuniangalia kwa makini.

‘Sasa tusipoteze muda, hapa tumekuja na ajenda moja, ajenda hiyo inatokana na kikao kilichopita, ilikuwa inahusu ombi la mwenetu kuwa keshakua mkubwa, na kukua huko kumemfikisha hadi anataka kuwa na mwenzake,na zaidi ya hayo alituomba msaada wakutafuta huyo mwenzake, sio kwamba asingeliweza kumpata, mbona tunaona jinsi vijana wetu wanavyotuleta wakwe toka mjini, hajui hata kushika jembe, hajui hata ngombe, ng’ombe anaita zinga la mdudud...hatari kubwa hii..’ akasema na kusababisha watu kucheka sana.

‘Kijana wetu kaonyesha ukovu wa kili, kaonyesha elimu yake kivitendo, kuwa hata kama atasoma sana, bado yupo ndani ya jamii husika, hataweza kuishi hewani, ....anakumbuka wapi alipotoka. Angeliweza hata kumuoa mzungu, hashindwi, lakini je huyo mzungu ataweza kuishi na wazee wetu, ataweza kulala nyumba moja na mifugo, ataweza kubeba maji kuni, majani na ndoo na hata motto mgongoni....?’ akauliza na kuwaanglia akina mama, na wao wakasema;

‘Aweze wapi ...hahaha..mnalo akina baba...’

‘Kwahiyo kijana wetu asingelishindwa kuoa, mjini au mzungu, au mnasemaje wazee..?’ akauliza mjomba na kuwaangalia wazee.

‘Ni kweli asingelishindwa kumpata mwenyewe mke wa kuoa, ila uwezekano mkubwa ulikuwa kuona mke kwasabau ya kuoa tu....hata hivyo tunamjua sana kijana wetu, tunamjua wenyewe...’akasema baba mkubwa na wote wakacheka.

‘Sasa kazi ilifanyika, na kama ilivyo desturi zetu ilibidi sisi wazee tuchague wale ambao tunaona wanafaa hapa kijijini kwetu na tulichagua kama watano, kutegemeana na sifa zao, ...na tulipokuwa tunazunguka wkabakia watatu,....hapo tukamuachia yeye atafakari kwanza na hata kupata muda wake mwenyewe kuwachunguza kwa wakati wake, na sisi hatukuwa na mashaka na hilo, kwani yoyote atakaye mchagua kati ya hawo, ...atakuwa mke mwema....au sio akina mama, mke mwema kama nyie mlivyochaguliwa....’akasema mjomba na kuwageukia akina mama.

Akina mama hawakujibu ila wao walipiga vigelegele....na hapo wazee wakageuka kuwaangalia maana ilionekana tofauti,...watapigaje vigelegele wakati jina lenyewe au mwali mtarajiwa mwenyewe hachapendekezwa.

‘Hayo ndio mambo ya kina mama,muda wote wanafikiria sherehe, ....’akasema mjomba na wote wakacheka na hata akina mama nao wakacheka na kwa mzaha wakapiga vigelegelel tena.

‘Sawa tutulie kidogo, kwani tunakwenda na muda, kama tulivyosema tupo na msomi , na wasomi kwao muda ni muhimu sana, hapa alipo anaangalia saa kila mara,kwani anaona tumachelewesha , damu inamchemka. Mjomba usijali,huo mchemko utatulizwa, tuna uhakika kati ya hawo mabinti kama utasema huyu ndiye ananifaa hutaamini mwenyewe, litakalo baki tuachie wenyewe, ..’ akasema mjomba na kuniangalia name nilikuwa nimeonyesha uso wa mshangao,

‘Usijali mjomba, najua hapo unajiuliza maswali mengi, ....ndio ni lazima mkaongee tena na huyo utakaye muona anakufaa, hiyo hatua ipo , lakini sio muhimu sana kwetu, ....labda kwa kujirizisha tu, ili usikie kauli yake mwenyewe, lakini hatutarajii `hapana’.. kutoka kwa yoyote utakaye mchagua kati ya hayo majina.....tuna uhakika na hilo...’akasema mjomba.

Kauli ya mjomba ilinifanya niwaze, maana mjomba aliniambia kuwa hawo mabinti hawajui kuwa wanatafutwa, na mimi nilitahadharishwa kuwa nisiongee nao lolote kuhusu uchumba....sasa inakuwaje na usemi wake huo kuwa ana uhakika kuwa hawo mabinti watanikubali na je wazazi wao watakubaliana na sisi....nikabakia kusubiri.

‘Kitu tunachojivunia katika familia hii ni kuwa kila familia nyingine aingeliomba binti yao aolewe kwetu...hiyo ni sifa ya kujivunia, na hili hallikuja hivi hivi tu, hapana ni kwasababu ya juhudi zetu, kutokana na juhudi za wazee wetu,...bidii za kazi , tabia njema,..sura ya mvuto....eeh, achilia mbali utaraji, na sasa tunaongoza kwa usomi...tupo mbele daima, na mke anaykubaliwa hapa kachunguzwa na kukubalika....ili asitoe mbegu mbovu...’aliposema hivyo watu wakaangua kicheko.

‘Watu wanatuita Wasomali, ndio damu yetu ya mababu imetokea huko juu, walikotokea watukufu...angalia hata nywele zetu, kihistoria babu wa babu, sijui wangapi, alitokea huko juu,akaja hapa akaoa mke ,na mke aliyemuoa ni chotara wa damu ya wenzetu toka huko mashariki ya mbali iliyokutana na mzungu na baadaye kukatokea mchangayiko hapo hadi tukatokea sisis.
‘Nasikia kuwa bibi wa bibi sijui wangapi ametokea katika ukoo wa mrembo anayesifiwa hata katika nyimbo, anaitwa nani yule...Kleopatra....’akasema na hilo jina K-l-e-o-p-a-t-raa’ alilitamka kimadaha.

Akina mama wakatulia kumuangalia , nafikiri wengine walikuwa hawajui ana maana gani kutaja hilo jina kwahiyo wakabakiwa na mawingu kichwani, na yeye alilijua hilo akafafanua kwa kusema.

‘Inasadakiwa huyu Kleopatra alikuwa mzuri sana...na alikuwa anajua kujipamba, vito vyeka alivyokuwa akivivaa,ni vya thamani,...fikiria mwenyewe vito vya thamani unavyovijua wewe, na huyu namlinganisha na Mwelekevu aliyemtaja mtunzi mahiri anayeitwa Shabani Robert...ukisoma sana hivi vitabu utapata shida kutafauta mke wa kuoa, maana ...mmmh, lakini sisi hatupati shida, maana tunatafutwa, kwahiyo tunachagua kwa hao wanaotutafuta hatuna shida....’akasema na kumgeukia kijana wao.

‘Sasa muda umefika, hebu angalia hayo majina, naona umeyaorodhesha hapo, umeyapanga kwa mpangilia wa nani zaidi, hata kama hujayapanga hebu tuambie nani zaidi kati ya hawo ...ambaye anaweza kuingia ndani ya famila hii....kama nilivyosema, hapa...nina maana ndani ya familia hii anaingia yule tu aliyekubalika....hatufanyi makosa....’akasemamjomba na kumwangalia kijana wake akiwa kashika karatasi.

‘Ongea kijana kuwa huru, hatutakusakama kwa yoyote kati ya hawo uliowachagua, walikuwa watu kama siksei, au ....?’ akauliza baba mkubwa.

‘Wapo wanne,.....samahanini kidogo, sio watatu tena, wapo wane, yupo mmoja aliongezeka, tuliongeza mmoja baadaye, nitakuja kuwaambia kwanini ilitokea hivyo..’akasema mjomba.

‘Aaah, mbona unakiuka makubaliono,huyo wanne alitoka wapi, ....?’ akauliza mama mmoja.

‘Hamuniamini mimi mwenyekiti wenu, kama hamuniamini basi natoka kwenye kiti akae mwingine, hili jina lilipendekezwa awali, lakini katika mchujo , halikuonekana kwasababu zizizo julikana, nafikiri yule aliyelipendekeza, hakuwahi kufika mapema kikaoni na hata hivyo tulisema akiwepo tutaliweka katika nafasi yake, kwasababu huyo binti anastahili, tatizo ni mtizamo usio sahihi....ngojeni kwanza tusimvuruge kijana, mpo na mimi au mumeniengua..?’ akauliza mjomba kwa sauti yake ya nguvu.

‘Tupo na wewe...’wakasema na akina mama wakapiga vigelegele.

‘Jamani raha siraha...?’ akasema baba mkubwa

‘Raha...’walioitikia wengi ni akina mama na kufululiza kwa vigelegele, na hapo ilichukua muda kutulia maana hapo kila mtu alikuwa akiongea lake, na ilionekana wazi, wengi wao walitaka kuyajua hayo majina, hasa ya huyo wa nne aliyeongezeka.

*********

‘Wazee wangu nashukuru sana, kwakweli mumenipa faraja kubwa sana,sikutegemea kabisa kama mambo haya ya kikubwa, yana raha hivi, maana vikao kama hivi tulikuwa haturuhusiwi kuhudhuria ndio maana hatukuwa tunajua nini kinachoongelewa...’ nikasema na kukohoa kidogo, maana kuongea huku wazee wamekutizama inataka moyo.

‘Sasa nimeamini kuwa wazee ni watu wa kuheshimiwa, kweli nyie mna busara,na yule atakaye wadharau kuwa hamfai katika shughuli za kijamii, eti mumepitwa na wakati, basi wao ndio hawajui maana ya kupitwa na wakati, hawaoni mbali, wapi walipotoka na wapi wanapokwenda, uoni wao ni wa leo leo....’nikasema na hapo hapo nikachuku karatasi yangu kama vile nasoma, lakini sikuwa na haja nayo kati hawo mabinti walishakuwa kichwani mwangu, lakini ....

‘Ongea kijana.....tunataka tukusikie maana wewe ndiye utashika usukani mjomba wako akiondoka....’akasema baba mmoja na wote wakapiga makofi.

‘Mnasema nini ,yaani mumeshaanza kunitafutia mrithi kabla sijafa.....’akasema mjomba kama kutishia na watu wakacheka na yeye akacheka na kumuonyesha kijana aendelee kuongea.

‘Sitaki kuwapotezea muda,maana anayenifaa keshapatikana, kama mlivyosema kuwa hatakataa, basi mimi kilichobakia ni kumtaja tu, ....’niksema huku nikitakari kwa makini na kina mama wakapiga vigelegele.
‘Nisingelipenda kutaja kwa majina, kama nilivyoshauriwa, ila kwa sifa zake tu, su sio...?’ nikasema na kuuliza kama anavyopenda kuuliza mjomba na mama mmoja akasema kwa sauti;

‘Kweli mwana wa nyoka ni nyoka, maana unavyoongea utafikiri mjomba wako...umerithi kila kitu...’akasema huyo mama na wenzake wakacheka.

‘Macho yalinivutia nikawa sioni, yalikuwa makubwa ya mvuto na nyusi zisizohitaji wanja...mdomo wake ulinipa pambaja nikawa nodondokwa na mate kama fisi aliyeona mfupa, sijui niseme nini kwa sifa zake ni maridawa...licha ya kuwa ni mdhaifu,...licha ya kuwa hana hadhi kwa wasio mjua, lakini kwa maulana ana hadhi na kiti chake kitakuwa kitukufu,... ‘ nikawa nongea kwa mshairi yasiyo na vina, sikujali sana.

‘Lakini japo kuwa sura yake imechoka, kwa jua na mihamaniko ya kimaisha, sura yake ya asili imetulia kama ua waridi mtini. Yeye namafananisha na yule muelekevu katika vitabu vya hadithi, na hata ninaweza kusema kamzidi Yule binti wasifa anayeitwa Kleopatra....kwangu mimi ni mahabubu, kwangu mimi ni kila kitu....’nikasema na vigelegeel na shangwe vilitanda.

‘Huyohuyu.....huyo huyo, mtaje jina lake.....’wakina mama wakasema huku wakipiga vigelegele.
Baadaye ghafla mama mzazi akashituka na kuomba kuongea, alionyesha wasiwasi na kusema ;

‘Hivi huyo unayemsema sio yule binti tunayemuita binti mjane...yule anayeishi na huyu mwanamke asiye na haya, anayetembea na hata vijana wadogo....kama ni huyo mimi simkubali, kwanini mumeliweka jina lake, ....nani alifany ahivyo....’mama akawa mbogo.

‘Kweli ....ndiye huyo, akasema baba mtu...mwenyekiti hapo umevuruga kikao, hilo jina halikuwepo na huyo mtu hatukuwahi kumjadili, nakumbuka tulimjadili mwanzoni kabisa, lakini jina lake halikuwahi kupita, kwasababu hakuwepo mdhamini wake....unakumbuka mwenyekiti...sasa kwanini umekwenda kinyume na makubaliano na kwa msingi gani...?’ akauliza baba mtu.

‘Lakini hebu tuambizane nini ubaya wa huyo binti, ni kwasababu ya mama yake au ukoo wake au yeye mwenyewe...?’ akauliza mama mwingine.

‘Ukoo hauna matatizo kabisa, matatizo ni kwa huyo mama anayejifanya mzungu, na kutembea uchi, mama mzima unavaa nguo fupi,na ukifika kwake unaweza ukamkuta kavaa khanga moja, hebu fikiria na ule mwili, sehemu kubwa anabakia uchi...anatuzalilisha akina mama...’akasema mama mwingine.

‘Sasa kama ni hivyo mimi sioni ubaya wa huyo binti...ukoo wao uko safi, tabia yake ipo safi....sura kajaliwa kinachotakiwa ni mafuta kidogo na lishe,au sio, mimi nilikuwa mmdhamini, wake tatizo siku hiyo ya kikao nilisafiri...yule binti ni mke mwema, hawo wengine wote waliochaguliwa hawamfikii huyo, aliyeharibu ni mama yake huyo anayeishi naye....’akasema baba mmoja na kuingwa mkono na baadhi ya akina mama.

Mwenyekiti aliwapa nafasi ili kila mmoja apate kuongea na kusikia mawazao ya kila mtu, nia hasa ni kuhakikisha kuwa hakuna dukuduku lolote miyoni mwao, na pia alitaka kujua kwanini hawampendi huyo binti. Akayasikia hayo mawazo na mwishoni akasimama na kutoa kauli yeye kama mwenyekiti nay eye kama yeye akasema;

‘Kwa taratibu zetu za kimila, kiongozi akionekana kafanya jambo kinyume na makubaliano anatakiwa kuachia ngazi, na mimi kama kiongozi muadilifu nafanya hivyo hivyo,...na sio kwamba nimekubali kuwa nimefanya makosa, hapana, mimi nipo katika njia ya haki na ukweli, ila kiutaratibu lazima kwanza niachie ngazi, kwasabubu kuna dukuduku kuwa huenda nimeenda kinyume na makubaliano..hili haliwezi kuondolewa nikiwa bado mwenyekiti.’akasimama na kuondoa kwenye kile kiti.

Wakati anaondoka watu wakawa wanaongea kila mmoja na lake, ikabidi yeye mwenyewe asimame kwanza na kusema, kiutaratibu mwenyekiti akiondoka kwenye kiti chake, kuna kaimu wake, lakini kama ni kwa makosa, au shutuma, basi anayetakiwa kuja hapo ni kiongozi wetu wa wazee wa hekima, kahiyo kwa moyo wa taadhima namkaribisha kiongozi wa wazee, na kiongozi wetu mpendwa, shika hatamu na suluhisha hilo tatizo, na kama nitaonekana na hatia basi sheria za kimila zifuate mkondo wake, au sio jamanii...’akasema mjomba na kukaa pembeni na huku bado minong’ono ya watu ilikuwa ikiendelea kila mmoja akiwa na lake.

‘Jamni naombeni tusikilizane kwanza, maana limezuka hili jambo, na mimi kama kiongozi wa wazee, kama mniitavyo, basi nimewajibika kusimama mbele yenu tuone jinsi gani tunaweza kulisuluhisha hili jambo....’akasema mzee ambaye ndiye kiongozi wa wazee.

‘Inabidi nieleze kawaida zetu kwa kifupi, hasa kukitokea jambo kama hili, hii ni kwa manufaa ya kijana wetu ambaye ni mara ya kwanza kuhudhuria kikao kama hiki,....’ akasema huku akimwangalia kijana wao ambaye alikuwa katulia kimiya akifuatilia mambo yanavyokwenda

‘Ngoja niwaambie taratibu za kimila za familia hii,....kwanza niwaambie kuwa na sisi tuna katiba zetu, kwani katiba ni nini, katiba ni utaratibu uliokubalika na jamii au nchi au sio....na sisi tuna katiba zetu, lakini katiba zetu za kimila zipo vichwani mwa wazee , jamii husika ...sisi, ..na ni vyema tukawa tunaielezea mara kwa mara kwa vizazi vyetu ili nanyi mkarariri taratibu zetu...hatuhitaji kuandika katiba....’akatulia na kuangalia huku na kule.

‘Katika taratibu zetu likitokea jambo kama hili lililotokea hapa, wanachama wako, ambao ndio waliokuweka, zaidi iya mmoja akakunyoshea kidole, kuonyesha dukuduku lake kuwa umekengeuka jambo ambalo lilipewa kipaumbele, kama hili, na kutokana na sababu kadhaa ukakiuka. Au ikasadikiwa kuwa umekiuka, …kama kiongozi muadilifu, lazima kwanza utoke kwenye kiti chako cha uenyekiti, hata bila kuambiwa...’akasema mzee huyo na kutulia kidogo, na watu wote walitulia kimia

‘Kwanza najiuliza kwanini ung’ang’anie kiti wakati wale waliokuweka wameshakunyoshea kidole….hata kama huna kosa, lakini watu zaidi ya mmoja wana kero na wewe,...ondoka, ili kupatikane nafasi ya kuthibitisha uhalali wa hiyo kero, .... achia ngazi usafishwe kwanza ndio baadaye uendelee na wadhifa wako, ….halafu ukiangalia sana uongozi kama huu wetu wa kijamii ni wakujitolewa haulipwi kitu, ....ni wito na heshima unayoipata, ....kwa ujumla unajitolea tu, utang’ang’ania ili iweje…’akatulia yule mzee.

‘Baada ya kusema hayo na kabla hili swala sijalifikisha kwa wazee ambao ndio wahusika wakulijadili ni vyema nikamuhoji mwenyekiti wenu mbele yenu maswali machache , ili kuondoa dhana kuwa huenda mwenyekitii atakula sahani moja na sisi, hii pia ya kumhoji kiongozi kwa jambo kama hili ni utaratiibi wetu na kawaida yetu;...’akamgeukia mwenyekiti pale alipokuwa kakaa, naye kwa heshima akasimama na kusogea mbele akatulia;

‘Kwa makubaliano ya kwanza ya wajumbe wengi,yalikubaliwa majina matatu, kamasikosei, je kwanini uliongeza hilo jina lanne?’ akauliza mzee.

‘Hilo jina la nne, liliongezwa baada ya mimi kukutana na wazee wasaidizi wako na hilii lilitokea baada ya mdhamini wake kujitokeza, akiwa na maelezo ambayo baada ya kuyasikiliza mimi,niliona niwahusishe viongozi wenzangu, lakini kwa bahati mbaya viongozi wenzangu hawakuwepo, walisafiri kwa mambo ya dharura, nikaona njia njema ni kuwaita wazee ambao ni wasaididzi wako, na kipindi hicho na wewe pia hukuwepo,kwasababu hizo hizo zilizowafanya wasaidizi wangu kutokuwepo....’akasema mwenyekiti.

‘Kwanini ulichukulie hilo jina uzito maana majina matatu yalitosha kabisa, hebu tueleze hilo jina la nne lilikuwa na umuhimu gani kwako,au kwa jamii au kwa familia hii,...?’ akauliza mzee.

‘Wengi mnamjua huyu binti,na wengi wamekuwa wakitafuta njia za kumsaida na kikwazo kikubwa kimekuwa ni mama yake. Najua wengi wanaitizama ile familia kwa jicho la mama huyo kuwa tabia yake inaweza ikawa imemharibu huyo binti, na hatafaa kwa familia yetu hii. Lakini wengi walioishi karibu na huyoo binti wamegundua msimamo wake, na adabu aliyo huyo binti, tangu alipokuwa mdogo hadi sasa ni mwali, hakuweza kujiingiza kwenye vishawishi, na ameendelea kumtumikia huyo mama yake kama mtumwa wake....’akasema mjomba.

‘Mimi niliwapa hoja hiyo na wao wakakutana, na baadaye wakaniita tukakukutana kwa pamoja , tulikumbushia vikao vingi vilivyopita ambavyo moja ya ajenda zake ni hii ya huyu binti ya kutafuta njia za kumsadia huyo binti aondeke hapo kwenye makucha ya huyo mwanamke,.... kwani hana hatia, kwani ni kiumbe dhaifu,ambacho kinateseka bila kosa,....’ akasema Yule mzee kwa sauti ya huruma.

‘Siku nyingi tumekuwa tukiulizana ni njia gani za kumsadia ili hali mama yake yule keshaahidi kuwa hakuna mume atakaye muoa bila ya ridhaa yake, na.....,hakuna mtu atayeamua kinyume na matakwa yake....hili tuliliongelea na sisi kwa pamoja tukaona njia pekee ya kusadia kama itatokea hivyo ni hii, lakini iwapo kijana wetu atamkubali...hakuna aliyemgusia huyo kijana, na hakuna aliyempa ushauri kuwa amchague yeye , sisi tuliliweka jina lake tu, basi, mengine yaliyotokea ni maaumzi ya kijana wetu...’akatulia mjomba baada ya kusikia watu wakinong’ona

‘Tutulieni kidogo,....hapa mimi kama mzee wenu najaribu kuwaweka sawa, muone nini kilifanyika,ili hata tukikaa pembeni msitie shaka na maamuzi yetu, najua hasa wazazi wa kijana mnalipinga hili kwa nguvu zote, lakini kuna maswala mengine mnatakiwa muyaangalie kwamtizamo wa kijamii, mtizamo wa kusaidia,mtizamo wa mzazi kwa mtoto wa mwingine, tuchukuliea huyo binti angelikuwa ni wa kwako , bahati ndio hivyo umefariki dunia na bahati itokee nafasi ya kurudi dunia ukayaona hayo anayotendewa binto yako ungelisikiaje...?’ akauliza na kuwaangalia wazee wa huyo kijana.

‘Swali hilo ni zuri, lakini huyo binti yupo hapa siku nyingi, hamkuliona hilo tatizo, ila mumeona hivi kwasasa, kwa vile kijana wetu anataka kuoa, .....kwanini mnaliona la maana hivi sasa, ina maana kijana wetu anachukuliwa kama chambo, ...’ akasema baba mtu na kumwangali kijana wake.

‘Hebu jaribuni kumfikiria huyu kijana, anahitaji mke , sio matatizo, ...nyie wote ni mashahidi kuhusu tabia za huyo mama yake anamlea, na amefikia hatua ya kuwarubuni hata mabinti wa wenzie, kwa kuwauza kwa matajiri....hasa yule tajiri wa ziwani,....je huyo binti yake atakuwa salama kweli, kweli hatakuwa kaingizwa kwenye hizo kashifa, tukumbuke ukiuza ukiwa kwenye uturi wa kunukia na wewe utanukia pia,....hapana sisi kama wazazi hatumkubali huyo binti....’akasema baba mzazi na mama akawa akiunga mkono.

‘Sawa sisi tumeya sikia hoja yako,na tutakuja kukuita baadaye kwenye kikao cha usuluhishi kama itaamuliwa hivyo na ili kwanza usikie hoja zetu na maamulzi yetu , hakutakuwa na kipangamizi kama kutokana na hoja yako hiyo,lengo letu ni kuliweka hili jambo sawa,...kwani kwenye wengi hapaharibiki neno...’akasema Yule mzee huku akiwaangalai watu waliokuwa wametulia kimiya.

‘Wewe kama mzazi hebu jaribu kufikiria kuwa yule ni binti yetu, amezaliwa hapa tunamuona,na mama yake alikuwa miongoni mwa akina mama waliolelewa vyema, tulikuwa tukisaidiana naye kwa shida na raha, leo hii kaondoka duniani, ndio tunaamua kumtendea hivi,...’akasema Yule mzee huku akimwangalia baba wa kijana.

‘Sio kwamba nalilitetea hilo, ila mimi kama mimii ndio maoni yangu,na fikira zangu na ndio ulikuwa mtizamo wa wazee waliofikia hadi kumuongeza katika hiyo orodha, na bila hata kumshawishi kijana wetu,...yeye mwenyewe alipomtembelea na kumuona, akaona anamfaa...., kwahiyo haikutendeka kinyume, lakini ngoja tukalijadili, ...’ akasema na kutulia kidogo halafu akawageukiwa watu na kusema;

‘Msaidizi wa menyekiti, endelea na kikao, sasa wazee wa usuluhishi, tunaomba nusu saa hivi tukutane kikao maalumu cha wazee...huku nyie mkiendeela na mjaala wa mambo mengine ....sawa..

‘Sawaa.....’wakaitikia.


********

6

Hayo yakiwa yanaendeela huko kwa wanafamilia hawo, hukuu kwa mama Kibonge, au kama wanavyopenda kuita wengine, kwa binti yatima, kulikuwa na vumbi likitimka, maana baba wa familia alikuwa kajaa mawimbi, hasa baada ya kumuona mkewe , akiwa kakumbatiana na kijana, kijana mwenyewe bado likuwa hajamjua vyema, lakini alipoambiwa ni kijana wa nani, akajikuta akiingia ndani na kuchukua panga kuelekea nyumbani kwa hiyo familia,..

‘Sasa unataka kufanya nini mume wangu...?’ mke mtu akamzuia na haraka akalishika lile panga na kumnyang’anya mumewe, akalitupia nje, mume akatulia huku akihema kwa hasira, akageuka kumwanglai mkewe, na mkewe atasema.

‘Sikiliza mume wangu,...hilo labda niseme ni mambo ya huyo kijana, na imetokea hivyo kwasababu kasomea nje,..unajua wazungu, wanapenda kusalimiana kwa kukumbatiana, hata mimi nilijikuta nikishikwa na butwaa, lakini kwa vile nawajua wazungu, basi nami nikaona nisijivunge, nisalimiane naye kizungu..ndio pale ulipofika ukakuta tunasalimiana hatukuwa na lengo baya...tatizo lako mume wangu, hujui dunia inavyokwenda....’akasema mke huku akimpapasa papasa mumewe huku akimsogelea na kujaribu kumkumbatia.

‘Sikiliza wewe mwanamke, nimeshasikia taarifa zako nyingi chafu,....mimi nimekuwa nikivumilia tu,maana sijawahi kushuhudia kama nilivyoshuhudia hii leo hapa, .....mimi nataka nikawaonyeshe hawo wenye huyo kijana na wanajamii kuwa sipendelei kabisa hayo unayoyafanya, kwani nimesikia kuwa unatabia ya kutembea na vijana wadogo wadogo,...’ akasema mume kwa hamaki.

‘Ongea nakusikia mume wangu.....maana sasa majungu ya mitaani yameshakuingia....’akasemamke mtu huku akicheka kwa dharau.

‘Ndio kwani uongo, wewe siunapenda kujifanya wewe ni mzungu, kila unayesalimiana naye hasa akiwa kijana mwanaume unataka mpaka mkumbatiane...haya yametoka wapi,kwanini tuige mambo ya aibu kama hayo, wewe ni mke wa mtu, tena mama mzima, hayo ya vijana yanakuhusu nini...sasa sikiliza, mimi nataka nikayamalize huko kwa huyo kijana au niyamalize hapa hapa kwako , leo hii...maana usifikiri nimekuwa dhaifu kwasababu ya limwili lao hili,...ninaweza nikakucharaza bakora, na hata kukutia makonde..na kukupa talaka yako mara moja....’akasema mume huku akijikurupua kuondoka kwa mke wake.

‘Najua hayo mume wangu, lakini kumbuka wapi tulipotoka, na umri kama huu , tukikimbilia kuachana, huoni ni aibu, hata hivyo hayo unayoyasema kama unaona hayafai basi i swala la kuambizana, tu....mimi nitayaacha kama yapo na kama ni kweli, lakini unatakiwa kujua kuwa huenda sababu kubwa ni wewe...’ akasema mke mtu, huku akiwa kmashikilai mume wako bara bara na mumewe akamwangalia kwa mshangao.

‘Sababu kubwa ni mimi, kwa vipi,mimi sio muhuni,ulizia wato wote huko ziwani watakuambia, ....wewe ndiye kila mtu anakusema kwa tabia yako mbaya....’akasema mume mtu.

‘Kwanini niwe na tabia mbaya, hujiulizi hilo kwanini...hebu nikuulize swali, je mtoto aliyeshiba kwao anaweza kwenda kuomba kwa jirani, je mtoto aliyelelewa vyema anaweza kwenda kufanya mabaya kwa jirani...ni maswali machache tu ya kujiuliza mume wangu, mimi huenda sababu kubwa ya kufanya hayo yote kama yapo kweli ni wewe...naukweli ndio huo....’akasema huyo mama.

‘Unanichekesha kweli,mimi niliwahi kukushauri ufanya hayo machafu unayoyafanya, mambo ya aibu matupu,ole wako nije nikufume,.....tabia yako mbaya umekuja nayo, nilipokuoa,ulijifanya una adabu, ukanihadaa mpaka nikalainika, mpaka tukasababisha mke wangu wa kwanza akatoweka duniani...hata sitaki, niyakumbuke hayo hayo ya zamani...na nimesikia kuwa una tabia ya kunitesea binti yangu maana nimesikia kuwa unamfanya kama mtumwa wako....” akasema mume mtu.

‘Sikiliza mume wangu, sisi tunaweza kukaa wiki mimi sikujui...hata mwezi mzima, labda nitumie nguvu, hivi wewe unanifikiriaje mimi..umenioa nije kuwa sanamu yako, kuwa mtumishi wako wa nyumbani....naona sasa unataka nikupe ukweli...’akashika kiuno na huku khanga ikiwa inamvuka.

‘Sikiliza babu wee, mke anathamani yake na mke kaolewa kuja kutimiza wajibu wake kama mke, hebu niambie mimi hapa nimekuja kuwa mtumishi wako, au sanamu yako ya kuiangalia na kusema eehe,mke wangu .....ndio maana kazi hizo namuachia binti yako,....mimi nina mambo muhimu niliyoletewa hapa na wewe unayapuuzia, ......hebu niambie kwanini hutaki kunifanyia yale ninayotaka,angalau baadhi....unafikiri mimi sijisikii niwe kama wenzangu....’akasema mke mtu.

‘Nishakuambia mimi ni mwanakijiji, ninaishi kutokana na silka na tabia zetu, wewe unataka mambo ya kizungu, mambo ya kuiga ili iweje....huoni aibu tukishikana na kukumbatiana mitaani, tena waakti mwingine hujali kuwa tupo njiani,...kwanza huo muda upo wapi,mimi nikirudi hapa nimechoka,nahitaji muda nipumzike kidogo,...’akasema huku akipiga miayo ya kuchoka na usingizi.
Mkewe akamwangalia mumewe na y eye akajifanya kupigamiayo na kusema; ‘Hata mimi naona kuchoka,maana mume anakuja kwa mkewe, anajua sasa mambo barabara..hata zawadi moja huna,
....aah, shida tupu...’akasema na kugeukia mlangoni.

‘Zawadi zawadi, hawo samaki hujawaona, kanipokea binti yako, wewe unataka zawado gani toka ziwani...’akasema huku akiendeela kupiga miayo.

‘Angalau ukija, mjali mkewe, nataka kukubusu hutaki, nataka kukufanyia masaji,hutaki, wewe hapo unayemfikiria ni mpenzi wako kitanda, au sio....?’ akasemamkewe huku akimwangalia mumewe.

‘Hayo mambo yako, hayo...,unaleta mambo yako ya kizungu....hivi wewe unajua kazi ya uvuvi, tunakesha huko ziwani, unakung’utwa na mbu, ....unabeba mizigo mzito, hizo ngalawa kuizisukuma kuingia majini, kuvuta manyavu...ni kazi nzito kweli, mwilo unachoka, kwahiyo hayo unayoyataka kila nikija unatakiwa uyapumzishe kwanza....’akasema mume mtu.

‘Sasa unaanza kujijua, hebu fikiria mtoto wako ana njaa, wewe anamwambia atulize njaa huku huna dalili hata ya kupika, eti mpakahapo chakula kitakapopatikana huku kwa jirani kipo tele,unafikiri huyo mtoto atafanya nini.....mwezi sasa, kila mudaumechoka....mara sitaki mambo hayo yakuiga, mara...ninadai mambo ya gharama, mara.....’ akasonya na kukaa kwenye kiti.


‘Sasa kwani sio kweli, wewe ulitaka nijiue, mbona huna huruma wewe mwanamke...wewe unachojali ni hisia na tamaa zako za kimwili, hunijali na mimi afya yangu, huwazii maisha, huwazii jinsi ya kutafuta kwa jasho lako,....wewe hapo ulipo uanwaza kupata hata bila kutoa jasho,unataka uchochoro, dhuluma na hadaa tu, mimi hivyo siwezi....’akasema mume mtu huku akiinuka kutaka kuondoka.

‘Tulia hapa tuongee, nataka nikufunde wewe mwanaume, ....unajua hayo yote yanayotokea sasa umeyasababisha wewe mwenyewe, ....nimeshakuambai tulia nikufundishe hatua kwa hatua, jinsi mumeanavyotakiwa kumtendea mkewe, ....nimejaribu weee, lakini ni kama mbuzi kupigia gitaa , mimi ninakuhakikishia kuwa ukifanya ninavyotaka hata huko kuchoka kutaisha...’ akamvuta mume wake ili akae karibu naye.

‘Unasikia mimi nimechoka, hapa nina usingizi wa kufa mtu....’akalalamika mwanaume.

‘Mbona hunielwei wewe mwanaume, ina maana kurudi kwako nyumbani ni kuja kulala, siungelala huko huko....sikiliza wewe mwanaume, timiza wajibu wako kama mwaaume, uone kama mimi sitatulia, uone kama utasikai tena hayo unayodai unayasikia, kwanini hutaki kunielewa...kwani mamo mengi ya kuongea, kuna hayo ya binti yako unayemtetea kuwa eti watu wanasema namtesa huku anataka upate sifa ya kuwa na binti mchapakazi, aolewe na na familia bora....kwa mtindo huo...atadodea hapa nyumbani..’akasema mke mtu...

‘Ataolewa tu, na kuna tetesi kuwa kuna familia bora inamtaka, wewe subiri tu...’akasema mume mtu.

‘’Whaat’, akashituka na hata kuangusha chombo alichokuwa kakishikamkononi, akamwangalai mume wake akiwa kakodoa macho ya hasira, halafu akaokota kile chombo na kusema;

‘Sijakusikai vyema ....familia gani hiyo,mbona sijasikia hilo na mimi masikio yangu yapo aridhini nasikia kila kitu kinachoongewa....kwanza sikia, nilishakumabia Tajiri yule wa ziwani keshanigusia kuwa anamtaka huyu binti yetu, anamtaka awe mke wake .....na kilichokuwa kikisubiriwa ni wewe....’akasema mama.

‘Eti nini, sitaki kusikia hilo...yule baba ana balaa, ana wake wawili sasa baada ya kufiwa na wake zake wale wawili wa mwanzo, licha ya hao aliokuwa akioa na kuacha, ....sasa unataka binti yetu naye yakamkuta hayo, ....wewe mamakweli mwenye huruma na mtoto wake. Sitaki kabisa kusikia hilo , binti yetu ataolewa na familia zinazokubalika, sio huyo jamaa yako, anayeoa kila siku...hilo hatutakubaliana nalo,...kama unataka nenda kaolewe wewe....kwanza sialikuwa rafiki yako.....’akasema baba.

‘Ndio alikuwa rafiki yangu, lakini kabla hujanioa, .....pesa zake zilikuwa zinamuasha, akavutika na umbo langu, kwanini nisimkune, kwanini nisizitumie, ....lakini hayo yalishapita, ...na kwa vile najua kuwa ana pesa zisizo na kazi, ndio maana nataka binti yetu akaolewe huko, ili utajiri ule nasi tuufaidi....hilo mimi nitahakikisha linafanikiwa,....mimi ndiye namlea huyu binti na najua ni wapi kunamfaa..’ akasema huku akiwa kashika kiuno

‘Haolewi huko nimeshakuambia..., kwasababau lengo lako sio zuri, unachofikiria wewe ni utajiri, lakini hufikirii maisha ya huyo binti, ...unaelewa hawo wake zake walikufa na ugonjwa gani...?’ akauliza mume mtu

‘Kufa si kufa tu, yoyote anaweza akafa kwa ugonjwa wowote. ....lamuhimu ni kijipanga jinsi ya kumkamua atoe hizo hela zake, mengine yatajileta baadaye. Unanieelwa wewe mwanauma,hivi wewe unataka ukae katika maisha haya hadi lini,....bahati inakujai unipa mgongo....sasa sikia, ataolewa, labda kama mimi sio mwanamke wa shoka..binti Bonge.’akasema na mara mlango ukagongwa...

Natamani kuendelea, lakini ngoja niishie hapa tukutane sehemu ijayo: Nimeziweka sehemu mbili 5 na 6, Kwasababu niliazima jembe mahala kwa siku moja, nikaona nafasi ndio hii hii....

WAZO LA LEO: Msikilize hata umuonaye ni mjinga akiongea, kwani hata huo uunao ni ujinga kwako ,unaweza kukusaidia kuujua ujinga wake, na huenda ukawa sio ujinga,ila ni mtizamo wako.Ni mimi: emu-three

5 comments :

Anonymous said...

Nimekukuta kwenye kibaraza fulani unasoma hadithi za watu, muulize yule aliyepublish kitabu cha hadithi zake amefanyaje.

Halafu wewe ni noma yaani nilivyoona unasifia ile story nikacheka tu sikutaka hata kukoment, yote maisha bora tufike duh!!

emu-three said...

`Umenikuta kwenye kibaraza fulani nikisoma hadith za watu....'

Ni kweli, maana ukipata nafasi unajaribu kupitia vibaraza vingine, kwani hawo ni majirani.

Nimejaribu kuwasiliana naye, lakini inaonyesha yupo busy....nitamjaribu tena , kwani ni jirani yangu mwema (wa blog)!
Tupo pamoja

Anonymous said...

natamani nikujue

Mzee wa Changamoto said...

Mara zote nimekuwa nikisema kuwa NI UJINGA KUAMINI KUWA UTAWEZA KUIELIMISHA JAMII KIMAANDISHI IWAPO WEWE HUSOMI.
Big Up mkubwa kwa kusoma, maana huko ndiko KUNOA BONGO, na ndiko kunakotuwezesha kupata uhongo

Anonymous said...

Sidhani kama huyo jirani yako atakwambia amefanyaje akaweza kupublish, yataka moyo kwani wewe ni maji marefu kwake. Na wengine hawawezi competition, wewe tafuta kitabu chake, angalia nani amepublish kisha anzia kutokea hapo. Na peleka link ya blogu yako kwa Michuzi na Mjengwa waombe wakutangazie. Muombe pia yule dada wa Uturn, mwandikie kuwa unataka kupublish kitabu hujui uanzie wapi, atoe hiyo kama post kwenye blogu yake watu wengi wanasoma kule watakujibu kukupa mbinu mbali mbali za kupublish, you never know!