Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, March 12, 2012

Hujafa Hujaumbika-1
Ndugu yangu matatizo yaliyonikuta unaweza ukakufuru mungu ukasema kuna mkono wa mtu, lakini licha ya yote hayo sikuwahi kufikiria kua nitakwenda kwa mganga wa kienyeji kwani hawo watu hawakosi la kukudanganya,lakini kutokana na hli ilivyokuja kunibana nilishawishika hasa kutokana na marafiki zangu, walionishauri nifanye hivyo,...eti niende kwa mtaalamu nikajiangalie....mwanzoni nilibeza kauli hiyo moyoni nikisema `nitakwendaje kwa mganga wa kienyeji wakati najijua, wakati najua kabisa mchwawi wangu ni nani....’

`Mchawi tena, ...eeh, na mchawi mwenyewe kumbe ulikuwa ukimjua, ulmijua juaje, hebu tupo uhondo,ingawaje ni shida....?’ nikauliza kwa kushangaa

‘Kama hujapatwa na matatizo huwezi kujua ugumu wake,.... ndio mchawi wangu namjua,....lakini sikumjua kwa kupitia kwa mganga...’akasema na kugeuka huku na kule kama vile anamuona huyo anayemuita mchawi wake.

‘Ulimjuaje na wakati wewe umesema huwaamini hawo wataalamu....?’ Nikamdadisi.

‘Unajua hata nisingelikwenda huko kwa hawo wanaoitwa wataalmu, bado nilikuwa namjua huyo mchawi wangu, lakini nilisukumwa kwenda huko na rafiki zangu ambao nilikuwa nikitumia nao wakati ninazo, Wao walinishauri kuwa nitapata dawa ya ufumbuzi, wakadai kuwa mambo kama hayo yanaweza yakatokea na bila kufafanuliwa huwezi kujua jinzi ya kuyatatua, na ya kuwa yupo mtaamu wa mambo hayo, kuna mmoja alifikia hadi kunipeleka kwa huyo mtaalmu anayemjua yeye.

‘Na wewe ukaenda hebu niambie ilikuwaje.....?’ nikamuuliza.

‘Tulipofika huyo mtaalamu alianza manyanga yake mara akaanza kunguruma kama simba mara akaanza kusema ; `huyu mwanamke anakuchezea, ...huyu mwanamke kaizamisha nyota yako...ana mkosi ,lazima mkosi uondolewe, la sivyo utaokota makopo, atakufukuzia ndugu, atakufukuzia wazazi...ondoa huo mkosi...’ akasema maneno mengi ambayo sikutaka hata kuyasikia, mwenzangu akaitikia `tawire.’

`Sasa mbona anachosema huyo mtaalamu ndivyo unavyodai kuwa ndio matatizo yako,huoni kuwa kapiga ramli sawa sawa....au unasemaje...?’nikasema kwa kuuliza kiutani.

‘Hata rafiki yangu aliniambia hivyo hivyo, alidai kuwa huyo mtaalamu alimsaidia akafanikiwa, ..nikashawishika nikaenda na tulipofika kwa huyo mganga, nilikata tamaa, maana hali niliyoikuta halafu naambiwa anatengenezea watu maisha watajirike sikuamini,..’ akasema huku akitabasamu.

‘Chumba anapoishi kimejaa makorokoro,humo humo kitanda.....kama yeye anaweza hivyo, mbona hali yake inakatisha tamaa, ....unajua nilipotoka hapo, sikutamani kurudi tena maana tuliagizwa kuku, mayai ya khanga, sijui nywele za msichana bikira....yaani nilichoka.

‘Tukiwa njiani niliwaambia wenzangu mimi sitarudi tena hapo, nikawaambia kuwa mimi sihitaji kumpata mchawi,maana mchawi wangu namjua mwenyewe.....

`Wewe kweli umeloga ina maana hata kujitengeneza unashindwa, nakushauri kesho turudi,kama tutakosa hivyo vitu unampa pesa yeye atakutafutia...vinginevyo bwana sisi tutakuacha kivyako vyako....’akamishauri huyo rafiki yangu.

‘Hapana,haya ya kwangu sio ya kulogezewa ndugu zanguni, mimi ninachotaka ni dawa kama ipo, sio kumtafuta mchawi,... najua nini kinanitafuna, lakini bado sijakata tamaa....’nikawaambia wenzangu.

‘Yule ni mtaalamu akikuambia kitu , ni kweli kwani kawasaidia wengi, mimi nikiwa mmojawapo....’akasema huyo mwenzangu.
Kesho yake nilipwahadithia wenzangu kijiweni, wengi wakanicheka wengine wakanishauri mengine.

‘Walikuambiaje....’nikamuuliza

‘Achana na kwenda kwa waganga wa kienyeji wewe,nenda kwa watu wa mungu wakakuombee....hujasikia wengi wameombewa, sasa wewe unasubiri nini...’akasema rafiki yetu mwingine na ikawa kama mzaha siku hiyo, na siku zilizofuata nikawa siwaoni hawo marafiki zangu, wakaanza kunikimbia mmoja mmoja, na ikafika siku nikifika kijiweni siwaoni tena maana sina cha kutoa,....’akasema na kutabasamu.

`Kwahiyo ukarudi kwa huyo mtaalamu, au ilikuwaje....?’ nikamuuliza

‘Nirudi kufanya nini, nilishaona hakuna zaidi ya hilo ninalolijua mimi....’akasema na kutulia kwa muda.

‘Hebu niambie matatizo haya yalianzia wapi, maana huko ni mwishoni au sio , nini hasa kilitokea mpaka ikafikia hapo..?’ nikamuuliza , nilipoona anataka kumalizia kisa wakati hajanimabia chimbuko lake.

‘Huenda naweza kusema kwa haraka haraka kuwa uliyesababisha haya yote ni mke wangu, lakini wakati mwingine najilaumu mimi mwenyewe,kuwa yote hayo yametokana na uzembe wangu binafsi, udhaifu uliojijenga tangu nikiwa mdogo. Na nimegundua kitu kuwa haya maisha ya ukubwani, mara nyingi,ukichunguza sana, chimbuko lake hutokana na maisha uliyoishi utotoni,hata kama wazazi walijitahidi sana kukulea, lakini kunaweza kukawa na jambo moja likajijenga mapema mwilini mwako kama hukuwahiwa.

‘Hapo napo kweli, inawezekana kwani wewe siumekulia huko kijijini , kabla ya kuja huku mjini,unafikiri matatizo haya yalianzia kijijini,....?’ nikamdadisi ..
Nitakuelezea kwa mapana, wapi nilipoanzia maisha yangu, wewe subiri, kama kweli unataka kisa kizima inabidi utulie, nakumbia utatunga kitabu’ akageuka kuangalia nje ,nami nikatikisa kichwa kukubali.

‘Hapa nakupa kama muhtasari tu,lakini naamini mara nyingi matatizo tabia na utashi vyaweza kuwa chanzo chake ni maisha ya utotoni, lakini ukiwa mkubwa unaweza ukajirudi kama umepata ufahamu wa kuyachuja na hasa ukipata elimu bora. Mimi nilipata bora elimu,ndio maana naishia kusingizia utoto au mke wangu.

Nakumbuk kabisa siku niliposema huyu sasa ndiye mke wangu,...ndipo mambo yalipoanza kuwa magumu, pesa ikawa haitoshi tena, nikipata inapukutika kama barafu kwenye jua, ....tena umenikumbusha, nakumbuka siku ile niliposema kuwa huyo mke sasa ndiye mke wangu halali, kuna jambo lilitokea....’akatulia kidogo na kuwaza.

`Jambo gani.....?’ nikamuuliza nilipomuona katulia.

‘Nakumbuka kabisa niliona taswira ya baba yangu akiniangalia kwa ukali, ....nilizania kuwa ni kwasababu nilikuwa nimekwazana na wazazi wangu,...lakini sasa nimejifunza kuwa radhi ya wazazi sio lazima wakutamkie, hapana,...
‘Nasema hivi kwasababu wazazi wangu hawakuwa na radhi na huyo mwanamke, kwani mwanamke huyo aliwazarau wazazi wangu nakuwaona wachafu, na hata walipokuja kunitembelea aliwafanyia mambo ya ajabu ajabu..hapo nilikuwa naishi naye tu, sijaamua kumuoa, na kipindi hicho mke wangu wa kwanza nimeshamtimua.

‘Kwanini uliachana naye...?’ nikauliza haraka.

‘Kwanini niliachana naye,..’ akacheka na kuangalia juu, halafu akasema `Kwasababu alikuwa mshamba wa kijijini...hahaha, ndivyo nilivyokuwa nikimuita siku nilipokutana na huyo mrembo, mtoto wa mjini, lakini cha ajabu wote hawo walitoka kijijini na walisoma shule moja, ila mwenzake alipomaliza shule tu, akapata mwanya wa kuingia mjini, akawa mrembo wa mjini, huyo mke wangu wa kwanza yeye hakubahatika kufika mjini , alifika pale nilipomuoa mimi....ndivyo nilivyowatofautisha.

‘Ama kwa wazazi wangu, kunichagulia mke, sikuweza kukubaliana nalo, kwani hadi sasa hilo siwezi kusema wazazi wangu walikuwa sawa, kwani mke ni mke wangu, na wao hawakuwa na mamlaka ya kuingilia maisha yangu ya ndoa, lakini je kweli huyo mke alikuwa mke kweli, hapo ndipo najiona mjinga.

‘Hapo ndipo nasema wazazi wangu waliona mbali tofauti na uoni wangu, ambao uliangalia zaidi maumbile, uzuri wa sura na raha za huyo mke,na kweli alikuwa akijua kumpagawisha mwanamuem sio sawa na mke wangu wa awali.

‘Ingawaje kila mmoja ananilaumu mimi kuwa ni limbukeni wa mapenzi, lakini mimi nitaendelea kumlaumu huyo mke wangu hadi kesho, kwani isIngelikuwa yeye nisingelimuacha mke wangu wa kwanza na isingelikuwa yeye nisingelikosana na wazazi wangu, na kutokana na yeye nilijikuta nikitumia zaidi ya kipato changu, hapo najua utaniuliza hizo pesa zaidi nilikuwa nikipatia wapi, nitakuelezea baadaye lakini kwanza ninunulie soda nipooze koo.

`Maisha ya mwanadamu hayatabiriki,ni ya kuoanda na kushuka,ni mitihani ya hapa na pale,na huwezi kujihakikishia kuwa umefanikiwa na kujipongeza, kabla hujafika mwisho, na unajua mwisho wa maisha ni wapi, kama sio jaburini, nakuambia kweli, maana hujafa hujaumbika....’.

Akasema rafiki yangu nami sikuwa na jinsi, japo sikuwa na mpangilio huo wakutoa ngama yangu, lakini niliingiwa na hamu ya kujua nini kilimsibu huyu jamaa, maana ukimuona sasa na jinsi alivyokuwa awali utafikiri ni watu wawili tofauti, nikamnunulia soda na wakati akinywa soda ndipo akaanza kunisimuli kisa chake cha maisha yake ambayo huenda kikawa ni fundisho kwetu, huenda kikatufunza jambo ambalo labda na sisi tumo ndani yake, au tunasumbuliwa nalo, na tupo mbioni kuingia mkenge.


NB. Haya tuishie hapa kwa leo, ili niweze kukusanya kumbukumbu(data), maana ni siku nyingi kidogo ,

Je mnasemaje tukihadithie au tutafute kisa kingine?

Kisa hiki ni muhimu kwa wale wanaotarajia kuanza maisha, wale waliopo kwenye ajira au wale waliopo kwenye ndoa na ndani yake wanajikuta wakipambana na matatizo na hata kufikia kuachishwa kazi, au kuachana na wake zao au mke kuachana na mume wake...Kwani hata kama upo kwenye mafanikio bado usijigambe kuwa hawo wamjitakia,hapana, katika maisha haya huwezi ukajiamini moja kwa moja,...hebu jiulize yule aliyeamuka asubuhi na mara akakutana na ajali,au akapatwa na kiharusi, sasa hivi ni mahututi Muhimbili,au nyumbani,unafikiri alijitakia,....

Ndio mmaana tunasema,kablahujafika mwishowa safari jijue upo kwenye mapambano, kwasababu `hujafa hujaumbika.


Ni mimi: emu-three

4 comments :

Anonymous said...

TWENDE BAB KISA MBONA KINAVUTIA JAMANI KAZA BUTI

Yasinta Ngonyani said...

Ndugu wangu hiki kisa kitafunza wengi kwa hiyo ushauri wangu ni kwamba kiandike....raha kweli kwa sisi wengine tusiokuwa na vitabu viiiingi vya hadithi:-)

Mija Shija Sayi said...

Tupo pamoja kaka..

emu-three said...

Nawashukuruni sana, wewe wa mwanzo usiye na jina, dada Yasinta na Dada Mija. Tupo pamoja daima