Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, February 20, 2012

Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli-83 hitimisho-27Mama wawili aliinama chini kwa muda, hakuamini hayo aliyokuwa akiambiwa, akatulia bila kusema kitu, na kumfanya mpelelezi naye atulie akisubiri kilio,....akahesabu moja mbili, tatu ….kimiya, akainua uso kumwangalia mjane, ….mjane alikuwa katoa jicho tu, hasemi, hatingishiki, ….ghafla mama wawili akainuka pale alipokuwa kakaa, taratibu akahesabu hatua, moja mbili tatu, akaingia chumbani kwake na wakasikia mlango ukifungwa na fungua kwa ndani….

Shangazi alipoona vile , mbio mbio akakimbilia kwenye ule mlango na kugonga afunguliwe, lakini haikuwa rahisi hivyo, akabembeleza kila lugha aliyoijua, lakini haikusaidia kitu, na mwishowe akakata tamaa na kumgeukiwa mpelelezi, asikie naye atasema nini;

‘Naona umpe muda, najua hali ilivyo, hakutarajia…, na ndivyo ilivyo katika kufiwa, wengi inapotokea hali kama hiyo tunakuwa hatuamini, lakini yote ni mapenzi ya mungu….naomba tumpe muda, na tuombe Mungu ampe subira, maana hatujui dhamira yake ya kujifungia ndani, je kafanya hivyo kwa minajili gani, hatujui nini kilichopo mioyoni mwa kila mmoja wetu, mjuaji wa yote ni yeye aliyetuumba, na anayemiliki nafsi za kila mja wake, ….’akasema mpelelezi na kumfuata shangazi pale aliposimama na kumshika mkono kumrudisha akae kwenye kiti.

‘Hakikisha unazilinda hizo familia kwa nguvu zako zote, maana hawo sio wenyeji wa huko, …..’Mpelelezi alikumbuka maneno ya Inspekta na kujiona katika wakati mgumu, maana kwa muda ule alitakiwa kuwa kwenye uwanja mwingine wa mapambano, lakini inashindikana mpaka ahakikishe hali ya hapo ipo shwari.

Baadaye wakasikia mlango ukifunguliwa kwa ufunguo kwa ndani, wakajua mama atatoka, lakini haikuwa hivyo, na walipoona kuko kimiya tena, shangazi akamuangalia mpelelezi, na mpelelezi akatingisha kichwa kukubali alichotaka kukifanya shangazi, na bila ajizi shangazi akainuka pale alipokuwa kakaa, huku akiwa kaweka mikono mbele, na baadaye kuifikisha usoni, na akafuta jasho lisilokuwepo, halafu kwa taratibu akaufungua mlangoo na kuingia ndani ya kile chumba, akamkuta wifi yake kakaa pembeni mwa kitanda…

‘Wifi ili usiumie ni vyema ukalia kidogo, ukiumia kindani ndani itakutesa sana….yote hiyo ni mipango ya mungu, sisi tulimpenda ndugu yetu, mume wako kipenzi, lakini yeye kampenda zaidi na yeye ndiye mwenye mamlaka na uhai wetu, hatuna jinsi, tunachotakiwa ni kumuombea heri, ….’akasema wifi mtu na kabla hajamaliza mama alizindukana na kuanza kuongea…..

‘Kwanini wasiniambie pale pale , wanatuleta hadi huku nyumbani,….kwanini nisipate muda wa kumuona mume wangu kwa mara ya mwisho, ….unajua wifi wazee hawo wangeshaniangamiza muda mrefu tu, lakini kwa vile tunapendana na mume wangu, wamehindwa, sasa wameona wamuondoe duniani, najua itakuwa wao na mambo yao ya kimila….’akasema na kutikisa kichwa kama anakubali, na wifi yake alikuwa kaka kimiya tu.

‘Kama sio wao kwanini wasiniruhusu na mimi nikafika hape eneo la msibani, kwani kiutaratibu wao huwa familia zote hukutana huko wanakokuita sehemu ya ukoo, eti mimi siruhusiwi kwenda huko kwenye eneo la msiba na hata mazishi yake nisi hudhurie, kwasababu gani, mimi sio mke wake, …hata kama mtoto hawamtambui, lakini ipo ndoa, …hapana hilo sikubali, nitafanya kila njia niende huko huko kama nikuniua waniulie uko huko…vinginevyo, waseme, kuwa kuna jambo…,’ akainuka pale kitandani na kuanza kutingishika mwili mzima.

‘Nahisi kuna jambo, oooh, mume wangu ina maana sitakuona tena, hata,mazishI yako nisihudhurie, nimekukosea nini jamani, oooh, nilijua tu pale uliponiaga ulisema buriani ya kuonana, sikuelewa hayo maneno ya maana gani….ooooh, mume wangu..oooh..’akaanza kulia , na kulia, ni kila dakika akawa anoneza sauti, na mwili ukawa unatetemeka, mpaka akapandwa na shinikizo la damu, akadondoka chini na kuzimia…

‘Jamani muiteni dakitari, hali ya wifi sio nzuri….’alitoka shangazi mbio mbio, kumwambia Mpelelezi, na mpelelezi bila kusita akapiga simu kumuita dakitari. Na wakati anasubiri akawa anaongea na shangazi.

‘Hali ya binti yenu ni nzuri, hana shaka, ila ilibidi akapumzishwe hospitalini, na madakitari wamemshughulikia na sasa yupo njiani anakuja, hana shida, …’akasema mpelelezi.
‘Na huyo mwingine yupo wapi..?’ akauliza shangazi.

‘Sikutaka kusema zaidi mbele ya mama yake, lakini Rose hatujamuona bado, tunazania huenda huyo jamaa tunayemtafuta kamteka nyara, kwasababu jengo lote hayupo, …’akasema mpelelezi.
‘Sasa atakuwa katokea wapi, na mlango wa kutokea ni mmoja tu, na sisi muda mwingi tulikuwepo hapo mlangoni….’akauliza shangazi.

‘Hata mimi hapo naingiwa na mashaka huenda miongoni mwetu kuna mtu kahusika kumtorosha kinamna, huyo jamaa ni mjanja sana, ana mbinu nyingi sana , kiasi kwamba watu wanamuita kinyonga, lakini za mwizi ni arubaini, tutampata tu…’akasema mpelelezi.

‘Sisi tunachotaka ni binti yetu, huyo mnayemuita kinyonga hatuhusu, kama yeye ni kinyonga anaweza hata kumbadili binti yetu naye apite pale na sisi tusimtambue, …vyovyote iwavyo, tunachoomba ukamfuatilie binti yetu, maana naona hii nchi yenu haikaliki…’akasema shangazi,

‘Wapo vijana wangu wanamtafuta kila kona, mimi nilitaka niwafikishe hapa na kuhakikisha kwua mpo salama, na nje tutaweka walizni wa kutosha, na kama likitokea tatizo nitawaelekeza jinsi ya kuwasiliana na mimi haraka, …na naomba umshauri sana wifi yako asije akakaidi na kwenda kwenye huo msiba, maana wale wazee walinisistiza sana kuwa haruhusiwi kabisa kufika huko, na hawataki kumuona, akionekana lolote litakalo tokea hawatalaumiwa, kwasababu kukitokea msiba kama huo kwa jadi zao mke anaweza akatolewa kafara….’akasema mpelelezi.

‘Eti nini , kutolewa kafara ndio kufanywa nini huko, hapana siamini hayo ninayoyasikia hata katika karne hii….!, kwanini wafanye hivyo wakati huyo ni mke wake halali..?’ akauliza shangazi.

‘Shangazi, nchi hii ipo kwenye mpito, na hali kama hii ipo kwenye nchi zetu hizi za Afrika, mila na tamaduni za namna hiyo zimejikita sana , na baya zaidi zinaendekeza kuwabagua wanawake, …lakini hayo ni ya mpito tu….’akasema mpelelezi huku akiinuka alipomuona dakitari akitoka na shangazi naye akasimama na kutaka kuingia ndani akamuone wifi yake.

‘Subiri kwanza usiingie ndani, kwani amepitiwa na usingizi , anatakiwa atulie kwa muda kwani hali hiyo imetokana na mshituko alioupata, hayupo katika hali mbaya sana, ni kawaida tu, cha muhimu ni kuhakikisha kuwa anatulia hakuna jingine kubwa, …’akasema docta huku akifunga funga mfuko wake wa madawa na vyombo, akatoa karatasi ya gharama za matibabu.

‘Naomba uniandikie sahihi yako hapa….’akasema yule dakitari na kumwangalia mpelelezi, mpelelezi akaichukua ile katatasi ni kuisoma, halafu akaandika saini yake na alipomaliza akamkabidhi yule dakitaru ambaye aliiweka ile katasi kwenye begi lake kuaga kuwa anaondoka na akasema;

‘Kama kutatokea lolote nipigieni simu maana kwa hivi sasa nawahi nimeitwa mahala pengine….’akasema na kuondoka zake.
Alipoondoka huyo dakitari mpelelezi akaangalai saa yake, na kuangalai nje kwa muda kwa kupitia dirishani, halafu akasogea mlengoni mwa chumba, akafungua kidogo na kuchungulia ndani, halafu akarudi na kumuelekea shangazi akasema;

‘Kwa hivi sasa nawaomba mtulie kabisa hapa nyumbani, msijaribu kutoka toka kufuatilia lolote mambo mengine tutayamaliza na kila kitu kitakuwa shwari, …’akasema mpelelezi.

‘Ndio tutafanya hivyo, lakini ukumbuke sisi tumekuja hapa kwa kibali cha muda, hatuna muda mrefu wa kukaa hapa, na ni heri mambo yakaenda haraka, ukichukulia kuwa wifi yangu zio mzaliwa wa hapa kaolewa tu, sasa kuna mambo ya mirathi, hatujui taratibu za huku, na mimi hapa ndiye ndugu pekee nahitajika kuwa naye, ili nijue kipi kitaendaje…?’ akasema shangazi huku akiontesha uso wa huzuni.

‘Hayo yana taratibu zake, hata kama kuna mambo ya kimila, lakini hayataingilia mambo ya kisheria, huyo anakubalika hapa kama raia wa hapa, kaolewa na raia wa hapa na kuzaa hapa hapa, na ndoa yake inakubalika kisheria, …..ila kama yeye mwenyewe ataamua kuukana huo uraia wake, hilo litafuata baadaye, chamuhimu ni kuangalia kuwa hayo yao ya kimilia hatuuaingilii kwanza, kwani hawo wazee hawana utani inapofiki huko kwenye mila zao….’akasema mpelelezi.

‘Mila mila, mila mpaka karine hii, na mila hizo heri zingekuwa na heri kwa wanadamu, lakini mambo yake, mmmh, mimi nayaogopa, ….watu wanakimbili kutoa kafara, eti kafara la damu ya mtu, hawo ni watu au nimuumiani…!’akasema shangazi kwa hasira.

‘Ni watu kabisa na watu wenye heshima zo tu, na hizo ni imani zao, zimejijenga kwenye mioyo yao, na wanafanya hivyo wakiwa na maslahi nazo, sio hivyo hivyo tu, na hizo ni zama zao,zitakuja kupita tu, sizani watoto au wajukuu zao watazifuata tena, ..zmimi nina imani kuwa zitaisha tu….’akasema mpelelezi.

‘Wewe wasema tu,….hujasikia hivi sasa kuna kundi kubwa limezuka duniani, ambalo lina mambo kama hayo, na lengo lao ni utajiri, na utajiri huo umegubikwa na wimbi la damu za watu, …na nasikia ni wasomi, na ni watu matajiri, …sizani kama mambo kama hayo yataisha, kwani wengi wetu tulijua kuwa ni mambo ya watu wa hali ya chini, ….hawo wanaofanya hivyo ni matajiri, watu wakubwa …kuisha labda ndio mwisho wa dunia, ..’akasema shangazi.

‘Hayo ni Makundi tu, na mwisho wake yataisha, hilo liskutie shaka, kila jambo lina mwanzo na mwisho wake, na sizani kaam ubaya unadumu milele, na kiuzoefu na ilivyo kawaida, ubaya hauna mwisho mwema, …yataisha tu..’akasema mpelelezi.

‘Haya yetu macho, ….na kweli mwisho wa uabaya ni fedheha tu….lakini huku nako kumezidi, vita ani visivyoisha, hadi…oh, nani tena huyo….’akasema na kabla hajamaliza mara mlango ukagongwa, na mara akaingia askari mmoja na kumuita mpelelezi pembeni. Wakateta kwa muda, na baadaye wakatoka nje wote wawili, haikuchukua muda mara wakaingia na jamaa mmoja, akiwa kavaa kofia kubwa , na midevu mingi, mdomoni kaweka kiko, akipuliza mosho utafikiri gari mosho, na mkononi kashikilia bakora, …

‘Mimi ni mmoja wa familia ya marehemu, nimekuja hapa kumchukua shemeji, nikiwa na maana mke wa marehemu na mtoto wake, kuna mambo mengine ya kimila wanatakiwa kuhudhuria…’akasema huyo mtu.

‘Wewe ni ndugu wa familia kivipi…maana mimi sikujui, ile familia naijua vyema,….hebu niambie wewe ni nani, na umezaliwa na mzee yupi pale….?’ akauliza mpelelezi huku akitilia shaka, maana yeye alionana ana kwa ana na wazee, wazazi wa marehemu, wakamwambia kuwa mke wa marehemu haruhusiwi kabisa kukanyaga kwenye maeneo yao,

‘Mimi ni ndugu yake marehemu nilikuwa sipo kwa muda, na taarifa hiyo ya msiba nimeipata nikiwa njiani kuja kuwaona na mambo mengine ya kifamilia, na nilipofika nikawa na mambo mengine, nilipogundua kuwa mke wa andugu yangu hajafika eneo ambalo sote tunatakiwa tuwepo, nikaondoka kuja hapa kumchukua, sikuongea sana na wazee hao maana walikuwa katika mambo yao ya kimila, ila ilivyo ni kuwa mke wa marehemu anatakiwa awepo pale kukamilisha taratibu nyingine, hilo linajulikana wazi…’akasema huyo mtu.

‘Hapana…, nafikiri hukuonana na wazee wahusika,…. mimi nimeongea nao, na wakaniagiza nini nije nimuambie mjane, mke wa marahemu, na nafuata walichoniagiza, wewe kakutuma mzee yupi..?’ akauliza mpelelezi.

‘Mimi ni ndugu wa marehemu najua taratibu zote, na mke wa marehemu ni shemeji yangu, na huenda kiuataribu nikamrithi mimi, sasa sihitaji kuagizwa na mtu, natakiwa kuwajibika, tusipoteze muda,. Waambie shemeji na binti yake wavae au wajitayarishe tuondoke, kwanza wapo wapi, mbona siwaoni hapa….?’ Akauliza akiangali huku na kule na hakutaka kabisa kumwangalia shangazi.

‘Nafikiri hatujaelewana, umenisikia swali langu, kakutuma mzee gani, …maana hivyo hatutaelewana , na kiutaratibu wetu hataondoka mtu hapa, nenda huko kama wanahitajika mimi mwenyewe nitakuja nao , na kwa hivi hawapo hapa, kama huna jingine, naomba uondoke, maana hatutaki mabishano mengi yaendelee hapa, kutokana na hali ilivyo….’akasema mpelelezi.

‘Unajua wewe unaingilia mambo yasiyokuhsu, haya ni mambo ya kimila, na wewe ni mtu wa serikali, hutakiwi kuyaingilia, na unasema hawapo humu ndani , ….mbona nimeambiwa kuwa wapo humu ndani, au mnataka kunificha hata mimi…’akasema huyo jamaa.

‘Nani kakuambia wapo humu ndani…?’ akauliza Mpelelezi na kumwangali kwa mashaka,
‘Haya habari ndio hizo, najua wapo humu ndani, na binti naye hajafika huku, maana nasikia alikuwa haonekani,…?’akaulia akiangali huku na kule.

‘Nikuulize swali, nini hasa kilichokuleta humu, …naona unachunguza chunguza na hata yasiyo kuhusu, au una jambo jingine hujatuambia….?’ Akauliza mpelelezi.

‘Umesahau kuwa nyumba hii ni ya ndugu yangu, nahitajika kujua kila kitu, wakiwemo wanafamilia na wageni, hujui kwamba nilitakiwa niwe hapa sehemu aliyokuwa akiishi ndugu yangu, hujui kuwa mimi ndiye natakiwa kurithi kila kitu, huna habari kuwa mali ya ndugu yangu inajumuisha na mali yangu….hata hivyo huna haja ya kujua, utajua baadaye….’akasema huku akiangali huku na huko.

‘Mimi kiutaratibu natakiwa niwasindikize mke na mtoto wake, na kwa taarifa yako mimi natakiwa kuwa mrithi wa mke wake, na ….na mali yake, kwahiyo kila kitu kinachomuhusu ndugu yangu, nahitajika kukijua, …serikali haiingilii hapa, wakiingilia tutapambana nayo, …ujumbe huo nakupa, kama wewe ni mwakilishi wao , waambia wahusika, wasijaribu kuingili mambo ya kimila, watajuta…kwanza nimeshangaa, maana nilisikia wamakumaliza hawa wahuni…..lakini sawa hayo hayanihusu sana…
’akasema huyo mtu kwa dharau na kuondoka kwa mwendo wa pole pole na alipofika mlangoni akageuka na kuwatiazama na sasa macho yake yalimwangalia shangazi kwa muda, akataka kama kurudi lakini akasita na kuuliza;

‘Wewe mna uhusisiano gani na marehemu au mke wa marehemu?’ akauliza huku anamwangalia shangazi, na kabla shangazi hajasema kitu mpelelezi akadakia;

‘Hayo hayakuhusu, nafikiri nimeshakueleze hali halisi , kama itakuja muda wa kutambulishana ni baadaye sio sasa …’akasema mpelelezi.

‘Hivi nikuulize wewe una……aah, ngoja nisiongee mengi, …’akageuka na kuondoka.
Mpelelezi akatoa simu yake na kuanza kuongea nayo, akawa anatoa amri kwa vijana wake;
‘Mfuatilie huyo mtu aliyetoka hapa, hakikisha unamfuatilia kila hatua na uwe makini asijue…’akasema na kugeuka kumwangalia shangazi.

‘Haya ndio maisha ya hapa, wazee huku wanautawala wao , wana nguvu ya ajabu, kwani sehemu kubwa bado inatawaliwa na wakuu wa jadi, lakini hayo yataisha pole pole, maana mambo ya kisiasa na demokrasia yanaingia kwa kasi..’akasema mpelelezi.

‘Yaani huyo mtu alivyo anatisha, namuhisi vibaya…., anavyoonekana sio kama alivyo, nahisi ni mtu mwingine, aliyejificha kwenye hiyo miguo-guo yake ananukia hatari tupu….’akasema shangazi.

‘Tutajua ukweli karibuni, hawawezi kucheza na nuvu ya dola, …’akasema mpelelezi na mara simu yake ikaita;

‘Ehe, nipe taarifa, eti nini….’akasikiliza kwa muda halafu akageuka kumwangalia shangazi

‘Itabidi niwaache maana siamini, huyo jamaa aliyetoka hapa eti kawapotea kiajabu, huyo jamaa anaonekana sio kama alivyokuwa akionekana, ngoja nikaonane nao huko huko….’akasema mpelelezi.

‘Nilijua tu, jinsi alivyokuwa akionakena, ni kama chui ndani ya ngozi ya kondoo , lakini hawo maaskari wako kweli wanajua kazi yao, kwani ilikuwaje…?’akauliza shanagzi kwa shauku.

‘Eti alifika akaingia kwenye jengo moja la vipodozi na nguo , hilo ni duka ambalo wengi wanaoingia hapo ni wanawake au kama ni mwanamume anakuwa kamsindikiza mkewe tu, na huyu jamaa alipokuja hapa alikuja na mwanamke mmoja alimuacha ndani ya gari, waliingia naye humo, na maaskari wakawa nje wanamsubiri, wanasema hawakuwahi kumuona akitoka, na aliyetoka ni yule mwanamke ambaye aliingia kwenye gari peke yake akaondoka, baadaye hawo vijana ndio , wakaamua kuingia kukagua wakakuta hayupo..’akasema mpelelezi.

‘Na walipowauliza wahusika, au hawo wanawake waliokuwa hapo ndani walisemaje, …wote ni washirika wake nini….?’ Akauliza shangazi.

‘Wao walidai walimuona akiingia na huyo mwanamke, na akawa kabakia sehemu ya wageni, ambapo hakuna mtu anakujali sana, , na kwa vile alikuwa mwanaume, walijua kamsindikiza mke wake, na kuna muda walimuona akiingia chooni, na toka hapo hawakumuona tena, na mwanamke wake aliaga muda sio mfupi, akaondoka, wao hawakuwa na shauku yoyote na wao, kwahiyo hawajui wapi, ni nani hawo,…’akasema mpelelezi.

‘Hapo mimi siamini,…lazima kuna jambo hapo, nafikiri anajuana na hao wanawake wa humo ndani….’akasema shangazi.

‘Inawezekana, au iswe hivyo, ila ninauhakika kuwa, atakuwa alitoka hapo hapo, akiwa kajibadilisha kwa kuvaa nguo za kike…huyo jamaa ana mbinu za kila aina….’akasema na wakati anataka kuondoka mara simu yake ikaita, akaiskiliza kwa muda, halafu akasema, ;

‘Hakikisha hakuna mtu mwingine anayeingia humo au kutoka, na hakikisha kuwa kuna ulinzi wa kutosha,na huyo dakitari akitoka muhakikishe kuna usalama, na yupi dakitari mliye Muita hapo…..?’

‘Oooh, huyo safi ni mtu wetu, ….ila muhakikishe kuwa mumemuwekea mtu wa kuhakikisha anafika kwake salama, na kumpa tahadhari zote, ….sawa kama mumefanya hivyo, inatosha, ….mimi nipo njiani ila napitia sehemu, kuna jambo nafuatilia nitafika huko muda sio mrefu…..ila narudia tena, hakikisha hakuna anyetoka au kuingia huo ndani,nafikiri unanielewa,….’alipomaliza kuongea akamgeukia shangazi na kusema;

‘Rose kapatikana lakini hali yake sio salama, ila yupo dakitari anamshughulikia, hilo tuachieni kwa sasa, nitawajulisha zaidi baadaye …’akasema na hakusubiri shangazi kumuuliza swali akaondoka.

‘Shangazi alibakia akiwa kaduwaa, na akaona ni vyema akamfahamishe wifi yake kwani alisikia kitu kama sauti ndani, alipoingia ndani akakuta hakuna mtu, akaingia sehemu ya choo cha ndani, akakuta hakuna mtu, akaanza kuhaha kwa wasiwasi, …..

Nb Leo ndio sehemu yet hiyo inaishia hapo, kulikoni, Jumatatu njema. Nawashukuru noye kwa kuwa pamoja nami na wale wanachangia Muungu awabariki sana.

WAZO LA LEO:Msibaa uusikie kwa mwenzako tu, kufiwa ni mtihani mkubwa sana. Na mara nyingi Utajua umuhimu wa mtu pale anapotoweka,....!

Nachukua nafasi hii kuwapa pole wale waliofiwa na waume zao au na wake zao, na hasa wale ambao baada ya kufiwa wamejikuta pia wakizalilishwa kwa kunyang'anywa mali walizochuma na waume zao, wakati wanahangaika wanandoa hawa hawa wanandugu hawakuwpo, hawajui jinsi walivyoumia, jinsi walivyojinyima, sasa mmoja kati ya wanandoa hawo kaondoka, wanandugu wanakuja, wanajitokeza....na hata kama wapo mayatima, hakuna anayewajali tena, jamani tunajichumia laana, mali hiyo ni sawa na kumeza bomu tumboni...
Ni mimi: emu-three

4 comments :

Anonymous said...

kama movie, twashukuru sana

Rachel siwa Isaac said...

Mungu awabariki Wajane na Yatima!!nakubaliana nawe ndugu wa mimi yaani kama wamemeza bomu Tumboni,Kazi nzuri zaidi ndugu wa mimi!Pamoja sana tuu!!!

emu-three said...

Ndugu wa mimi R.S.I na mchangiaji wa mwanzo, Anoyn., mungu awabariki sana kwa kuwa nami, Tupo pamoja

AMMY K said...

duuh mwisho mwisho inatia uchungu.