Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, May 27, 2025

NIANZAJE

Mambo ya kuandika yapo mengi, visa vipo vingi na matukio halikadhalika, lakini nashindwa nianzaje...Nianzeje, najiuliza

Wakati nawaza hivyo, mara nikasikia binti mmoja anaongea kwa hasira, akimfokea mtu mnzima, huyo mtu kwa jinsi alivyojieleza ana miaka sitini na kitu...

'Wewe binti mimi nina miaka sitini na....kukushika kwa kutaka usogee ndio unanikaripia hivyo
'Kwanini unishike, kwanini usiniambie tu wataka kupita
'Ningekuambia huenda usingelijua kuwa ni wewe....nimekushika...'
'Aaah, nyie wazee hamna adabu, kushika shika tu wanawake...
'Hata nikikushika kuna ubaya gani, au wataka ushikwe na mume wako tu
'Achana na mimi wewe mzee
'Au kwa vile wewe ni mnzungu....'
Nahisi alitumia neno hilo mnzungu kwa vile yule binti ni zeruzeru (matatizo ya ngozi)
Abiria wengi walikaa kimia,...ni asubuhi kila mtu anawazia kuwahi kazini na kwa muda ule ilishafika saa mbili hivi
 Nikiwa nimezama kwenye mawazo mara nikahisi mtu aliyekaa karibu ya anakuwa kama anatoa sauti ya kulia, nikageuka kumuangalia....
Ni yule mdada, zeru zeru....kainamisha kichwa sasa anafuta machozi....nilijua labda kakerwa na yule abiria aliyemshika

'Usijali dada...kwenye gari haya yanatokea....'nikasema
'Mhh....wakati mwingine watu wanataka washushiwe hasira zilizojificha....'akasema
'Polee...na samaahni..'nikasema nikihisi nimemkwaza
'Pole na samahani ya nini...?' akauliza na kunigeukia sasa akitabasamu...

 
Ni mimi: emu-three

Saturday, November 23, 2024

Dunia hii .....



Wiki sasa nimekuwa nikimkuta kijana wa miaka 20 au 22 hivi, akiwa amelala pembeni mwa majengo ya maduka eneo la posta, ni kijana ana nguvu, japo  nilipomuuliza anasema ana tatizo la bawasiri, linampa shida sana

'Vipi ndugu yangu waendeleaje

'Sijambo hivyo hivyot tu....ndio nasubiri nipate nauli nirudi kwetu

'Kwani kufika kwenu nauli ni bei gani

'Elif 55

'Sasa hivi una shilingi ngapi

'Nina elif 25, kuna mdada mmoja alinisaidia hizo pesa

'Sasa hivi unafanya shughuli gani yaani ukitoka hapo ulipolala

'Naokota chupa kama unavyoona hapo...'

Alinionyesha mfuko uliopo pembeni mwake, ni mchafu, hata yeye mwenyewe nguo zake zilikuwa chafu, sijui kama anafua au hata sijui kama anaoga.....

Niliwaza sana mbali, ..

Huyu ni kijana mdogo, taifa la kesho, yupo hapo anateseka, yupo kwenye maeneo ya ofisi na maduka, wapo wafanya biashara wenye pesa, wapo wenye bajaji na madaladala, hakuna hata mmoja aliyefikia kumuwazia huyu mtu huyu mwenzetu, au kuulizana je tutamsaidiaje huyu mwenzetu, je huyu kijana ana tatizo gani

Niliwaza hivyo, labda sijui...

Lakini katika dunia ya leo sio rahisi kuwapata watu wa namna hiyo, watu wa kuwawazia wengine, watu wengi wana shida zao, ukiiingia kwenye anga za kila mtu, utakuta kila mtu ana matatizo yake mengi kichwani, anawaza vipi ataishi, vipi ataendesha maisha yake, nk

Nimeona hii niiweke kwenye shajara yetu ya leo...tukiendelea kumfuatilia

Leo tarehe 24, nilipitia tena hapo, nikamkuta kijana wetu amelala...kajikunyata....kalala katandika boksi...wakati napita yupo kwenye usingizi...niliona nisimuamushe, lakini nikakumbuka wajibu wangu, nikamwekea chochote kwenye mkono, akashtuka, alipoona ile pesa akashukuru

Kiukweli sikutaka kumuongelesha maana nilihisi machozi...

Namuomba mola amsaidie kijana huyu apate nauli, arudi kwao, na ikiwezekana wapatikane wasamaria wema wamchangie akatibiwe....yangu ni duwa!

Wiki imepita, leo tena nikapita pale anapolala huyu kijana....kiukweli sio sehemu ya kulala mtu, pachafu, na hata yeye mwenyewe nguo alizovaa ni chafu....lakini utafanyaje, nilimsalimia na kutoa chochote akashukuru....alisema sasa imebakia elif 18 atimize nauli

Ni mimi: emu-three

Wednesday, November 8, 2023

HURUMA INAYOUMA-Utangulizi


'Docta, huyu sio mtoto wangu, ….’akasema mdada.

‘Sio mtoto wako…! ' Akasema docta kwa mshangao, na mdada akawa kimia

'Kama sio mtoto wako, wazazi wake wapo wapi…au wewe ni nani kwake?’ docta akauliza, akiangalia saa yake, akikumbuka anahitajika kwenda wodini kuna mgonjwa alihitajia huduma yake.

‘Docta mimi ki-ki ukweli, s-sijui, hutaamini lakini sijui….’kauli iliyomfanya docta aweke peni mezani, akaangalia simu ya mezani, akitarajia kuitwa muda wowote.Lakini  kwa kauli hiyo ya mdada ilimfanya ahisi kuna jambo linakuja.

Docta akaangalia saa yake tena,….halafu akamwangalia yule mdada, hakuweza kuona sura ya huyi mdada vyema kwani kwa muda ule huyo mdada alikuwa kainamisha kichwa chini. Docta akamuangalia mtoto aliyebebwa na huyo mdada, halafu akamuangalai  tena yule mdada. Docta alitafuta jambo kwa wawili hao, huku akichelea muda…!

‘Unajua sikuelewi, kama wewe sio mzazi, wewe ni nani kwa huyo mtoto…?’ akauliza docta

‘Docta , naomba tu unielewe, mimi sijui wazazi wake wapo wapi, mtoto anaumwa, ni huruma ..ni…huruma yangu tu….’akasema sasa huyo mdada kwa sauti ya huzuni.

‘Sawa…lakini kwanza unielewe… ili mtoto atibiwe, eeh, si tunahitaji maelezo, eeh….kwanza kadi yake ya kliniki unayo..?’ akauliza docta

‘Si nimekuambia mimi siwajui wazazi wake, …mimi sina kadi yake… na hata sijui kama ana kadi….’akasema mdada

Docta akahema kama kuchoka hivi….akaangalia saa yake ya mkononi, halafu akataka kama kusimama, akaangalia simu ya mezani…ni kama alitaka kuitumia, au kusubiria kuitwa, akamuangalia mdada…

‘Mdada..!, sijui nikuite hivyo,...sijui kama unanielewa, na sijui kama tutaelewana, huyu ni mtoto mdogo, unasikia sana….umempataje mimi sijui eeh…si wewe umekuja naye, au..?’akasema docta lakini mdada alimkatisha kwa kauli iliyomshfanya docta agwaye kudogo

‘Docta,….naomba msaada wako..!’akasema mdada.

 Msaada….!

Docta kusikia hiyo kauli akilini akasema,…yah…kama nilivyowaza, yale yale….!

Lakini docta hakutaka kulichukulia hilo analoliwaza akilini kwa haraka, kwanza akavuta subira, akawa anamuangalia yule mdada,….mdada alikuwa kimia, bado akiwa kainamisha kichwa chini akimuangalia yule mtoto.

‘Msaada…!, unaomba msaada gani…?’ akauliza docta

Mdada aliendelea kukaa kimia,… halafu baadae yule mdada akainua kichwa na kumtizama docta, mara moja paah…halafu akarudisha macho chini.

Docta aliyaona yale macho, yale macho yalikuwa kama  yanalengwa lengwa na machozi. Hata hivyo, docta hakuweza kumuona vyema,…Hata hivyo,Docta machozi ya wagonjwa ameyazoea!

Docta kwa uzoefu wake, akahisi kuna jambo, na hayo machozi sio kama yale aliyoyazoea, hata hivyo,aliona avute subira, hakuwazia tena huyo mgonjwa mwingine wa wodini,…

Kuna jambo kwa huyo mdada na mtoto….Aliwaza hivyo!

Yule mdada sasa taratibu akainua uso, na sasa akamtizama docta, moja kwa moja, macho ya mdada yakakutana na macho ya docta, hapo sasa ndio docta akaweza kumuangalia vyema huyo mdada, na machoni kulikuwa kukavu,

Mhh...…. Docta aliguna hivyo kimoyo moyoni

‘Docta, ninaomba umtibie tu huyu mtoto tujue ana shida gani….hilo tu docta….’akasema huyo mdada, kabla docta hajahitimisha uchunguzi wake wa kuwalinganisha wawili hao kama kuna uhusiano wowote mdada aliongea hivyo .

Docta, kwa haraka akachukua peni na kuandika kitu kwenye kadi, halafu…

Na mara simu ya mezani ikaanza kulia…


NB. Ni tukio nililokutana nalo hospitalini, na diary yangu ikaona sio vyema lipite bure.....Ni kisa cha mdada na mtoto, Je huruma yake iliishia wapi? Je kuna nini nyuma ya pazia.....

KARIBUNI SANA KWENYE SEHEMU YA INAYOFUATA



i mimi: emu-three

Friday, September 22, 2023

TUSAIDIE TUPATE BARAKA


Nikiwa nimekaa ndani ya gari la daladala, macho yangu yalivutiwa na abiria wanaogombea kuingia ndani ya dala dala hilo. 

Abiria wanaotaka kuingia walikuwa wengi zaidi ya uwezo wa gari hilo....kwahiyo ilikuwa mshikemshike, na kati ya hao abiria, nilimuona mtoto , nahisi anaweza kuwa kati ya miaka mitano au sita, akiwa na sare zake za chekechea nahisi

Kwa vile abiria walikuwa wengi, na kila mmoja anataka kuwahi kuingia, hakuna aliyemjali huyo mtoto, walimsukumia nje...lakini yule mtoto akawa naye anajitahidi kushindana ili naye awahi kuingia, kwa bahati mbaya akadondoka chini

Hakuna aliyemjali....walioweza kuingia wakaingia, na wengine wakabakia nje, sasa wale waliobaki nje ndio wakamuona huyo mtoto, ...

'Vipi umeumia..?' mmoja wa abiria akamuuliza
 Yule mtoto akawa analia...huku akijifuta futa, na kuokota mkoba wake wa madafutari, na bado akijaribu kuona kama ataweza kuingia

''Endesha gari....' konda wa hilo dala dala akasema, bila kujali kuwa kuna mtoto alianguka, na hakutaka hata kumsaidia angalau aingie

Baadhi ya abiria walioingia ndani wakawa wanamsema konda, asimamishe garii amchukue huyo mtoto

'Wanafunzi wameingia wengi sana, na hata akiingia atakaa wapi...'akasema konda na dala dala likwa limeingia barabara kuu, mtoto akabakia kituoni na abiria wengine.

Hatukifika mbali gari likakamatwa na trafiki kwa makosa ya kupitia njia za mkato...ikawa ndio mwisho wa safari hiyo, kwasababu trafiki alisema hilo gari sio mara ya kwanza, kahiyo linahitajika kituo cha polisi

WAZO LA LEO: Wakati mwingine tunazikataa baraka zetu sisi wenyewe...tuwasaidie wenye shida, kwani kutokana na wao, ndipo baraka zilipo.
Ni mimi: emu-three

Friday, September 8, 2023

NI KIPI KIPYA NIJIFUNZE...


KIPI KIPYA!

Niandike nini ambacho hakijawahi kuandikwa, niseme nini ambacho hakijawahi kusemwa, nione kitu gani kipya ambacho hakijawahi kuonwa, nisikie nini kipya ambacho hakijawahi kusikiwa....nahisi kila kitu kina msingi, ...na sie ni waendelezaji tu, labda, taaluma na mitandao ambayo inakuwa kila siku , lakini hata yenyewe ina asili yake!

Ni mimi: emu-three