Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, July 20, 2011

EMY;NAOMBENI USHAURI


                                                           HII SIO PICHA YAKE HALISI
Habarini za shughuli? Poleni sana majukumu ya hapa na pale ndugu zanguni.

Mimi naitwa Emy(majina yamehifadhiwa) haya ndiyo majina rasmi niliyobarikiwa na wazazi wangu. Nina kila sababu ya kumshukuru mungu kwa uzima, nguvu, Pumzi paoja na afya njema aliyonipatia bila malipo yoyote yale. Ni huruma zake pamoja na fadhili zake kwetu.

Kma nilivyotangulia kusema hapo juu, hayo ndiyo majina yangu(yamehifadhiwa). Ninaishi Mwanza Tanzania, Nilizaliwa  miaka ya 25 iliyopita hapa Mwanza. Namshukuru mungu alinipatia mume wangu mwaka 2006. Natoka katika familia ya kiumini kweli. Wazazi wangu pamoja na familia yangu yote ni waumini wazuri wa dini. Nina watoto wawili  

Baada ya hayo naomba niwasilishe ombi langu kwanu ambapo nahitaji sana ushauri wenu. Naamini ni makusudi ya Mungu kuwaombeni na kuitolea kuwasilisha hii hoja hewani, ni vigumu sana, lakini natumai ni makusudi ya mungu kuwa huenda miongoni mwenu kuna atakayenisaidia kwa hili tatizo langu, kwa kupitia huyu mwenye blog, natumai nyote mtatoa maoni yenu kwake, ili niweze kuyasoma.

Nilimaliza kidato cha nne  katika shule ya moja huko Mza. Sikufanikiwa kuchaguliwa kuendelea na masomo kwa vile maksi zangu hazikuniruhusu. Wazazi wangu hawakuniacha bali waliniuliza ninataka kipi kwa wakati huo nami sikusita nikasema kile kilichokuwa moyoni mwangu kuwa ninapenda sana masomo ya Computer. Walinishauri niendelee na kidato cha sita lakini baada ya kufeli vile sikuwa na moyo wa kuendelea na masomo hayo. Nimetokea katika familia ya kawaida si ya hali ya chini sana wala si ya hali ya juu. Kwa hilo ninamshukuru Mwenyezi Mungu.

Hitaji langu kuu ni kuendelea na masomo kiukweli baada ya kupata hawa watoto nimejikuta nikiwa katika wakati mgumu sana kila nikifikiria hawa watoto ntawaleaje pasipo baba yao, maana hatuwezi kujua mipango ya Mungu. Hatupaswi kuwaza hayo lakini ni vitu muhimu vya kufikiria. Pamoja na kuwa ninakazi ambayo kiasi kikubwa inanisaidia lakini familia yangu yote inaniangalia mimi. Kuna wadogo zangu ambao ni wanafunzi wawili nimekuwa nikiwasomesha mimi kwa hicho kipato changu cha laki mbili kwa mwezi. Mume wangu naye hajaniacha huwa ananisaidia sana kwa kweli na aliniahidi kuniendeleza. Tatizo ni kwamba naye ukoo wao mzima unamtegemea sana yeye kwa kila kitu na hasa wanafunzi wako watano na wote anawasomesha yeye.

Mda unaenda mbio kila tukipanga mipango yetu kuhusu masomo yangu mwenzangu yanaingilia mambo mengine ambayo ni muhimu zaidi. Navumilia kungojea lakini muda unaniacha, Naomba munisaidie kimawazo, tafadhali, kimawazo, kwani chuo nacho ni gharama kubwa sana.
Msaada wangu ni kwamba katika mawazo tunatofautiana maana hata sasa sijui nikasomee nini?
Maksi zangu ni CIVICS-D, HISTORY-D, GEOGRAPHY-F, KISWAHILI-C, ENGLISH-D, BIOLOGY-D, NA BASIC MATHEMATICS-F. Sijaficha chochote maana najua unapohitaji msaada wa mawazo ni lazima uwe muwazi ili mujue cha kunishauri. Kwa maksi hizo nianzie wapi angalau nipate ajira ya kudumu niendelee kujisomesha taratibu. Naogopa maana mume wangu anamajukumu mengi sana ya familia yao yanambana kiasi kwamba hata kumwambia tena maswala ya shule naona kama ninampa msalaba asiostahili. KWa mahitaji mengine yote ananijalisana mimi pamoja na watoto na tunaishi pamoja kwa kushilikiana kwa kila jambo.

KWa kipato changu hiki cha kudunduluza nimesha weza kuweka kaakibae mpaka sasa nina kama 500,000 ninaomba munisaidie kimawazo nikasomee kitu gani hapo mwakani cha kunisaidia katika maisha yangu. yaani kiwe kitu cha mda mfupi angalau miaka miwili ili nipate ajira maalumu itayonifanya nimudu kuendelea  kuwasaidia ndugu na jamaa katika masomo yao. Na naamini mpaka hapo mwakani angalu ntakuwa nimedunduliza na kuweka kaakiba kidogo.

Najua wapo wanauwezo wa kusaidia watu, ila hawana uhakika, ninani wa kusaidia , kwahiyo kama wapo, ninajua wapo kwa uwezo wa muumba, basi naombeni msaada wenu, hasa wa kimawazo na kama ni zaidi ya hapo, nitshukuru mungu.

Nina mengi sana lakini ni hayo kwa ufupi. Msaada wangu mkuu ni nyie, na ninanukuu maneno ya busara yasemayo , akufaaye kwa ziki , ndiye rafiki wa kweli (a friend in need is a friend indeed) ! Mkumbuke mimi nimwanamke na nataka kuliokoa jahazi la kesho ambalo ni watoto, kama zipo jumuia kama wapo watu wenye nafasi, kama yapo mawazo ya kunielekeza niende wapi,sasa nifanyeje?, Nyie mnajua zaidi, naombeni sana msaada wenu kwa kupitia blog hii. Samahanini sana kama kwa kuliweka hili hadharani kuna ambao watakwazika, lakini nifanyeje, na nimeona njia hii huenda ikanisaidia mimi na familia yangu.

Nategemea mawazo na majibu jema, natanguliza shukurani kwa kusema Mungu awabariki sana
Wanu,
Emy, toka Mwanza.


NB: Hili ni ombi toka kwa huyu mwanadada, mwenye watoto wawili anahitai kusoma, naombeni mtoe ushauri wenye kujenga, tupendane na tusaidianeni huwezi jua unayemsaidia leo, akajikomboa na tatizo lake anaweza akawa na msaada mkubwa kwa wengine ...tukumbuka kama kisa chetu kinachoendelea sasa kuwa `akufaanye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli'

12 comments :

samira said...

naomba aweke namba yake ya simu tuwasiliane

Anonymous said...

Kazana kurudia mitihani yaani kuresit ya form four angalau masomo matatu hasa hayo uliyopata F ya maths na Geography, kisha la tatu chagua kutoka katika hayo uliyopata D, utakuwa umejitengenezea njia ya kusoma elimu ya juu. Hii inaweza kukuchukua mwaka mzima.

Mwaka unaofuata soma High school kwa masomo ya jioni ya mwaka mmoja ili upata cheti cha high school ambacho kitadetermine Open University utasoma nini. Baada ya kumaliza hapo jiregister kwa kozi ya degree ya kwanza open university. Itakuchukua muda kwani hakuna short cut kwenye maisha.

Au baada ya high school certificate waweza kwenda college kusoma kozi yoyote utakayo ona inakufaa.

Subira

SIMON KITURURU said...

Nakunukuu baadhi ya nilionalo nni tatizo kubwa kwa ``.....sasa sijui nikasomee nini? ´´


Mimi naamini ni vizuri ukawa unajua unataka kufanya nini kitu ambacho kitakusaidia ujue usomee nini! Na ukijua usomee nini ndio utajua kihitajikacho hata ki PASI zako za MTIHANI ni nini. Kwa kuwa mimi naamini ukishauriwa na watu wengine na kujikuta unasomea usicho kipenda utafeli tena au ukifaulu hata kufanikiwa kupata kazi baada ya kumaliza masomo hutapenda hiyo kazi!

Kwahiyo amua kwanza nini unataka na kumbuka chochote kile uchaguacho itakuwa sio kitu rahisi kufanikisha. Kitahitaji kujitoa moyo kisawasawa!

ni wazo tu!

emu-three said...

Samira sikumbuki kama uliwahi kunipa e-mail yako, ili kama huyu mwanadada ataamua kukupa namba ya simu yake niweze kukutumia, ama kwa maoni yenu nayashukuru sana, na natumai wapo wengi wana maonii zaidi tuendelee kuyatoa ili niweze kumwakilishia ....Tuendelee kuwa pamoja.
Kuhusu kisa chetu, ni cha utu uzima kidogo, ndio maana nikishaandika inabidi nipitie tena kwa uangalifu nikijaribu kukichuja kiwe kwa kila rika...KARIBUNI SANA

samira said...

m3 nimekuemail my email tupo pamoja

emu-three said...

Nasikitika Samira hiyo -email haijaingia kwenye inboksi yangu, labda ulikosea e-mail adress, hebu angalia vizuri!

chib said...

Jamani mimi huwa saa nyingine ni mtundu sana wa kusoma habari kwa kina, hasa linapokuja suala la maombi, kwani nimekuwa napokea maombi kadhaa wa kadhaa kwa wenye shida za kweli na wengine basi tu, si wajua tena.
Muombaji kidogo amenichanganya wakati aliposema... hapa ninamnukuu.... "baada ya kupata hawa watoto nimejikuta nikiwa katika wakati mgumu sana kila nikifikiria hawa watoto ntawaleaje pasipo baba yao"
Ukisonga mbele, tena anadai mume wake huwa anamsaidia sana, na baadaye..... hapendi kumuambia kuhusu suala la masomo, ati ....
Sasa nje ya topik, huyo mume sio baba wa hao watoto au.....
Mtaniwia radhi, hua nikikutana na walakin, moyo huwa mzito....
Ngoja nitafakari ushauri....

emu-three said...

Mkuu Chib, hebu irudie tena hiyo paragrafu;

``Hitaji langu kuu ni kuendelea na masomo kiukweli baada ya kupata hawa watoto nimejikuta nikiwa katika wakati mgumu sana kila nikifikiria hawa watoto ntawaleaje pasipo baba yao, maana hatuwezi kujua mipango ya Mungu. Hatupaswi kuwaza hayo lakini ni vitu muhimu vya kufikiria.

Hapa alikuwa akiweka fikira kuwa `kama ikatokea mzazi mwenzake wa kiume akatangulia mbele ya haki' ...kama ikatokea,
Hii ni hulka yetu wanadamu mara nyingi tunawaza hivyo kuwa kama ikitokea mwenzako akaondoka utaishije...sio kama `NIKIONDOKA DUNIANI...
Nafikiri ndivyo ilivyo, na kwakuwa mwenyewe anaweza kuisoa hiyo hoja yako anaweza akajielezea zaidi.
Tupo pamoja mkuu, ni kweli kuna watu wengine wanahitaji msaada wa kikweli, lakini kuna wengine hawasemi ukweli na hili ni janga kubwa, na tunaliona mitaani sasa hivi. Tunatakiwa tuwe makini kwa hili. Ila kwa huyu kweli inaonekana anahitaji `ushauri wetu' naomba tumsaidie kwani ushauri wake ni wa kujenga, anahitaji ushauri wa elimu...!

Anonymous said...

Jamani sijui watu wakoje. Yaani kuweka tu hiyo email yangu wameanza kuntumia mail za hovyo. Tafadhali emu-three nnaomba uitoe, wamenikatisha tamaa kabisa. Imefikia wakati jamani tuelimike.

Anonymous said...

Asante sana emu-three kwa msaada wako. Huyo alieomba namba yangu naomba umpatie email adress yangu!-Emmy

emu-three said...

Pole sana Emmy, nimeiondoa e-mail adress yako...! Hawo watu hawajui wakimfanyia mtu ubaya ipo siku utawarudia, kwanini tusiwe na hekima kwa wenzetu..!

chib said...

Nimekusoma vizuri mkuu, na nimeelewa sentensi kamili sasa. Pia ninampa pole huyo aliyeomba msaada na kuishia kukejeliwa au kunanihii kwa email za watu ambao hawajatulia