`Hadithi za mizimu na mshetani zilitawala kichwani kwangu kitu ambacho nilikuwa sina imani nacho kabla,…’ akasema Maua na kuendelea kuelezea kuwa labda ilikuwa ni ile picha ya video aliyoiona siku tatu zilizopita na kumteka akili yake, na kuanza kujenga hisia hizo kuwa huenda aliyemuona hapo ni mzuka, au mzimu au shetani…mwili ukafa ganzi ghafla na kusema kimomoyo;
'Sasa hivi nimeingiliwa na shetani’, kwasababau gani aliwaza hivyo, ni kwa kuwa chumba kile hakikutakiwa kuja mtu wa jinsia nyingine, zaidi yao, pili shangazi alikuwa nje na angenimfahamisha Maua kuwa kuna mtu wa dharura kaja na anatakiwa kuonana naye, na shangazi yake ni mtu anayefuatilai sana taratibu zao…sasa iweje mtu kama huyu, kama kweli ni mtu atokee huko alikotoka na kuingia ndani bila kuonana na shangazi, kama sio shetani, haiwezekani…
Haiwezekani hili ni shetani…akili yangu iliamini hivyo, …`nikashikwa na woga ambao sijawahi kushikwa katika maisha yangu, nikakusanya nguvu kupiga ukulele, huku natafuta njia ya kukimbia nje, lakini ningelipitia wapi ili hali hilo shetani au kibwengo au sijui kitu gani …lilikuwa limetanda njia yote ya mlangoni’ aliendelea kutuhadithia Maua huku akionyesha hali ya wasiwasi kama vile ndio siku ile…
’Na wakati nawaza haya mara akili yote ikaanza kunikumbusha maisha yangu yalivyokuwa kabla hadi kufikia siku hiyo ya harusi ya pili, na nini kilinikuta hadi niwe na majonzi ya miaka miwili, karibu hata ya kujiua, na kuapa kuwa sitaolewa tena, na simtaki mwanaume mwingine tena, lakini nikajikuta nikiolewa tena,na siku yaharusi ya pili mara akatokea huyu mzimu…!
Nilimuona ni muzimu kutokana na kisa chenyewe ambacho ningependa kukihadithia kwanza…’ akasema na kujiweka sawa;
`Nisingefikia kuamini hilo kama sio hiki kisa kilichotokea katika maisha yangu, kisa cha kweli ambacho sio mimi tu niliyepata pigo, lilikuwa pigo la watu wengi na pigo la taifa…ni kisa ambacho kilinifanya niamini na mpaka leo bado sijawa sawa kuamini kuwa kweli yule hakuwa mzimu…sijaelewa maana baada ya hapo hatukuweza kuonana tena, hadi hii leo hii.
‘Wakati nimebakia mdomo wazi, huku nimeganda kama mtu aliyegandishwa, wakati nataka kupiga yowe lakini mdomo ukawa umefunguka tu, sauti haitoki, wakati nataka kukimbia lakini miguu ikawa kama imepigiliwa msumari, na mizito kama ya tembo,…hapo hapo kisa cha maisha yangu kikatanda usoni na kujikutwa nimekugubikwa na tukio zima , liikianzia maisha yangu ya mpendwa wangu,, lakini cha ajabu kisa hiki kilianzia pale tangazo liliposikika redioni… wakati huo ikiitwa redio Tanzania…
***********
‘Hii ni Redio Tanzania Dar-es-salaamu, habari zilizotufikia hivi karibuni ni kuwa Meli ya MV Bukoba imezama na inasadikiwa kuwa abiria zaidi ya 600 walikuwa ndani ya meli hiyo na juhudi kubwa zinafanya kuokoa abiria na mali zao. Tutaendelea kuwaulisha zaidi nini kinaendelea…
Wakati taarifa hii ikisomwa Maua alikuwa bafuni akioga, na kutokana na pilika pilika za mchana kutwa za usafi wa ndani, kuosha vyombo kufagia na kufua nguo, kulimia bustani na nyingine nyingi, akawa yupo hoi kwa uchomvu na maji yale yaliyokuwa yakitiririka mwili yalikuwa kama dawa ya kuupooza mwili wake ambao ulichoka kupita kiasi. Mwili haukuchoka tu kwasababu ya hizo kazi bali pia ulichoka kwasababu ya mawazo mengi, mawazo aliyokuwa akipambana nayo…
Michirizi ya maji yaliyokuwa yakimwagika kichwani yalitulinza ubongo wake, na wakati yale maji yakishuka mwilini yalimfanya mwili utulie na kuliwazika na hata kujenga hisia zaidi ya pale, hisia iliyomkumbusha jinsi alivyokuwa akioga na mwezake, kitu ambacho alijifunza kutoka kwake, hakuwadhania kamwe ingelifika siku akaoga na mtu baki, na mtu mwenyewe awe jinsia tofauti, lakini kidogokidogo alijifunza kwa mumewe mpenzi hadi akawa anakubali kuoga pamoja na hata kuogeshana…kweli mume na mke wana raha yao ya kipekee..alipfikiri ahivyo akatabasamu na kucheka, huku akiwaza.
Alimuwaza mumewe akiwa anampaka sabuni, alimuwaza mumewe akiwa anamkanda kwa mikono yake yenye nguvu, alimuwaza mumewe,….na alipofika hapo huku akijipaka sabuni mwilini akahisi mwili ukisisimuka na kuanza kusahau kabisa ule uchomvu wa siku nzima, na hali ile ilikuwa ikisindikizwa na mziki uliokuwa ukitoka barazani kwake..
`Mpenzi Zuwena, oooh mpenzi Zuwena ..kweli nampendaaaa….’ akawa anafuatilia ule mziki huku analisugua lile pofu la sabuni kichwani na mwili mzima, na alipoona kuwa sabuni imekolea mwilini akawa anarudisha ile sabuni sehemu inapowekwa, na kabla mkono haujafika sehemu hiyo akiwa kafumba macho kukwepa sabuni isiingie machoni mara ghafla ule mziki ulisimama,
Na moyoni akawa analaani kwanini hawa watu wa redio wanambania, na hata kabla kauli yake hiyo haijaenea moyoni mara akayasikia yale maneno ya taarifa;
'Kuwa kuna taarifa toka Mwanza kuwa meli ya MV Bukoba imezama…akajikuta akisema `eti nini…’na kwasababuu ya ule kelele wa maji aliisikia ile taarifa kwa shida, na kila aliponyosha mkono kuzima hayo maji akawa hafikii kile kifungio cha maji, kwani alikuwa haoni kutokana na sabuni iliyokuwa imeingia machoni…lakini ile taarifa ikawa imepenya kichwani mwake…
Alichofanya hata kabla hajajifuta sabuni vyema, hata kabla hajahakikisha kuwa kaoga na kuondoa mapomvu ya sabuni, na hata kusahau machungu ya sabuni iliyokuwa imeingia machoni, haraka akakurupuka na kuivuta khanga iliyokuwa imetundikwa kwenye kimsumari na kukimbilia nje.
Alikimbilia ndani ambapo sauti ya redio ilikuwa inatokea, ilikuwa ipo sebuleni, na hakujali kuwa shemeji yake Maneno alikuwepo hapo, hakujali kuwa amevaa khanga moja, hakujali kuwa kutokana nay ale maji khanga ile ilikuwa imenatana na mwili na mwili wote ulikuwa unechoreka, alichojali ni kusikia tena ile habari…
Alipofika alimkuta Shemeji yake Maneno akiwa kaduwaa, ikiwa na maana kuwa taarifa ile alishaisikia pia, na kila mtu aliyekuwa karibu na redio yake atakuwa kaipata hiyo taarifa hata kama ni kwa uchache, kwahiyo alichotaka kujua ni uhakika wake, je ni kweli, je kama hakosei ndiyo siku mume wake mpenzi alikuwa anasafiri kwa kutumia hiyo meli, na walishawasilina kuwa alishapata tiketi na ina maana ni miongoni wa abiria waliokuwemo ndani ya hiyo meli…sasa nini kimetokea mapaka izame, na je nini majaliwa yake…akajikuta anamwangalia shemeji yake usoni akisubiri kuwa atamwelezea zaidi…
*************
Maneno wakati anatoka kazini, alikuwa ametekwa na mawazo ambayo amejaribu kwa kila njia kuyaondoa akilini mwake lakini kila siku inavyokwenda mawazo hayo yamekuwa yakimtawala, alijua kabisa kuwa ni kosa kubwa, alijua kabisa mawazo hayo ni mabaya sana, na mwisho wake yanaweza kujenga chuki kubwa sana, lakini amejitahidi kuyaondoa imeshindikana, imekuwa kwake ni mtihani ambao unampeleka pabaya, na asingeweza kuukwepa mtihani huo na kwa makubaliano yake na rafiki yake alitakiwa kupitia kwa rafiki yake na kula na kuhakikisha kuwa mke wa rafiki yake yupo katika usalama …
‘Wewe ndiwe rafiki yangu ninayekuamini ambaye ni zaidi ya ndugu, nakukabidhi familia yangu hii, mke wangu huyu awe mikononi mwako hadi nitakaporudi, …najua unajua jinsi gani tunavyosaidiana na hili sikuhitaji kulisistizia, najua unjua wajibu wako…na ili kuona kila kitu kinakwenda sawa, wewe hujaoa, sipendi kabisa uwe unakula magengeni, uje hapa shemeji yako akupikie, …’ alikumbuka maneno ya rafiki yake mpendwa.
‘Sawa rafiki yangu, naona kama unanipa usia siku zote unasafiri sijawahi kusikia maneno kama haya, …usiniambie unaanza kutoniamini…’ akasema Maneno kwa mazaha.
‘Sio hivyo, safari ni hatua, nani ni vyema, na hili nakuambia kama nilivyoambiwa na wazazi wangu kuwa unapkwenda safari, hakikisha unaikalisha familia yako na kuiasa kwani safari ni hatua…sio kwamba sikuamini nakujua ulivyo, tumetoka mbali wewe ni rafiki wa kweli, rafiki wa kila hali, ambaye humfaa mwenzake sio wakati wa raha tu hata wakati wa shida, kwani akufaanye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli..’ akasema rafiki yake
‘Bwana Mhua hilo lisikutie shaka, nitailinda mali yetu…na huko unapokwenda ukipata mke kama shemeji yangu usiache kunishitua maana unaona …nahisi kuchelewa, lakini ipo siku, …lakini apatiakne mtu kama shemeji, zaidi ya hapo sioi…’akasema Maneno.
‘Hilo nikirui lazima twende kijijini , nitahakikisha unaoa, sipendi kabisa ukae hivi hivi…mimi nimeshatangulia kuoa, kama tulivyopanga safari hii ni ya kwako…tutampata tu hata zaidi ya shemeji, kaza buti,tunza heshima yako na muombe mungu sana kwani mke mwema hupatikana katika imani njema ya dini, na zaidi ni kumuomba mungu…’akasema Mhuja.
Maneno haya yalimchoma sana Maneno mpaka akahis si vyema kwenda kumuona shemeji yake kwani kwa hali aliyo nayo atashindwa na huenda akamwambia nini anachohisi…na hili amekuwa akilipanga siku nyingi kuwa atamwambai ukweli kuwa …..akasita kufikiri hivyo tama inavyomtuma, akasita kuliweka neno analolitaka moyoni mwake…
Wakati anawaza yote haya hakujua miguu nayo ilikuwa inachepuka na tahamaki yupo nyumbani kwa rafiki yake, akasita kupiga hodi, lakini baadaye akajipa moyo na kusema, leo nitajitahidi kumwambia shemeji ukweli jinsi gani ninavyojiskia kuhusu yeye, najua ni dhambi, lakini naona kama ni dhambi zaidi kama nitaliweka moyoni liendelee kunitesa…nitamwambia huenda naye akaua jinsi ya kunisaidia, huenda nay eye anajisikia jinsi ninavyojisikia…lakini kama nitamuudhi..halafu rafiki yangu akajua …mungu wangu ni heri nitokomee, eti urafiki umekufa sababu ya kumtamani mke wa rafiki yangu….hapana hilo halitatokea, nitamwambia shemeji ukweli tu..kama nayeye anajisikia hivyo..huenda …huenda…
Alishangaa kuona kupo kimiya kasoro redio iliyokuwa ikisikika kutoka sebuleni ikipiga miziki na salamu za mchana, akajiuliza huyu shemeji kaenda wapi, mbona nahisi ukimiya au kajilaa sebuleni huku redio ikimtumbusiza, ngoja nimshitue kidogo…, akaashika kitasa cha mlango na kuingia haraka….akakuta sebule ipo tupu hakuna mtu, …akaingia ndani na kufunga mlango na kwenda moja kwa moja kukaa kwenye kochi, akatulia na kwa mbali akasikia maji yakitoka bafuni, akajua kuwa sheemji yake atakuwa anakoga,
Na muda huo hisia zikawa zinajijenga akilini, na akawa akijiuliza huyu shemeji atakuwaje akiwa anaoga , hana nguo…akajikuta akiwaza zaidi ya hisia zake…akainuka na kutembea huku na kule , halafu akarudi akakaa, na kusema kimoyo moyo…hii sasa ni dhambi, hii sasa inanipeleka kubaya…!
Mara redio ikasimamisha mziki uliokuwa ukipigwa na tangazo likasikika, tangazo lililo piga moyo wa Maneno kama kisu kikitua moyoni , na kujikuta akishika kifuani, na kwanini iwe hivyo, ameshawahi kusikia matangazo ya kutisha , lakini hili limeugusa sana moyo wake kwanini…
‘Meli imezama na ilikuwa na abiria zaidi ya 600, na humo lazima alikuwemo rafiki yake , kwani jana tu ndiye aliywasiliana na rafiki yake kuwa keshapata tiketi na wapo tayari kuingia ndani ya meli na alikuwa kapiga simu kuwajulisha hilo…akamtakia safari njema…sasa hilo tangazo, ina maana shemeji atakuwa kalisikia hilo tangazo, kama hajaliskia ni lazima atafute njia ya kumwambia asije akamuumiza kimawazo… …na kabla hajamaliza hisi zake mara mlango ukafunguliwa na mara akaingia shemeji , akiwa na khanga moja, mapofu bado yapo kichwani, …. Khanga ile kutokana na maji maji imemganda mwilini na…
Maneno akajikuta akipepesa macho na kujikuta akikagua mwili wa shemeji yake huku akiwa katayahari, ina maana keshaliskia hilo tangazo, basi dunia nzima imeshalisikia hilo tangazo, akainua uso wake na kukutana na macho ya shemeji yake ambaye alishaanza kulengwa lengwa na machazo , yale macho yalidai kujua zaidi , …na hakuwa na zaidi ya lile tangazo hakuwa na zaidi ya kuongeza, akageuzo uso kuiangalia ile redio akiomba lile tangazao lirudiwe tena ili liokoe ile hali, lakini kilichokuwa kikisikia ni ule mziki wa `Zuwena’
Yakatangazwa majina ya watu waliokuwamo kwenye ajali hiyoooo
Mmoja wapo kati ya watu hao alikuwamo mpenzi Zuwena
Nikatoka bila kujitambua mikono kichwani huku ninalia
Mbio kwenda Hospitali kwenda kumuona mpenzi Zuwena
Sijui kama yuko hai au Zuwena amekwisha kufa
Maringo na mikogo yangu kwa siku hiyo vyote vilikwisha
Mammy Zuwena
Ooo mpenzi Zuwenaaaa
Maua aliposikia ule wimbo akajikuta machozi yakimtoka na kuingiwa na kigugumizi akitamani kupiga ukulele….akamwangalia shemeji yake, ambaye sasa kageuka akmkagua mwilini, na inavyoonekana hana analojua la zaidi ya hilo tangazo na alipojikagua mwenyewe kuona nini shemeji yake anakiangalia , akagundua hilo na hapo akakimbilia chumbani kwake na kujitupa kitandani …
Maua alimwacha Maneno akiwa kaduwaa, na kutahayari, …bila kujua la kufanya, alikuwa akishindana na mawazo mengi kichwani,…huenda shemeji kamuhisi vibaya vile alivyomtizama kwa tamaa….akawa pia anajiuliza kimawazo je alikuwa akiwaza kuhusu hilo tangazo zaidi au alikuwa akimuwaza shemeji yake na ile hali aliyomuona nayo ambayo hajawahi kumuona akiwa hivyo na khanga moja, halafu akakumbuka kitu na haraka, akafungulia redio kusikiliza huenda habari ikarudiwa tena…
Ni mimi: emu-three
5 comments :
Mhhh yaani we acha tuu,Hongera sana ndugu yangu kwa kazi hii njema!!!!!!
Ndugu yangu yaani nashukuru sana kwa kunipa moyo maana ninapoona kimia hakuna aliyesema lolote nahisi kisa hakina mvuto. Maoni ya watu hutoa hamasa ya kuendelea
katika dhiki, dhiki ni muhimu kwa rafiki
m3 tupo pamoja usijali
hii habari inaumiza hasa kwa mwenye mpendwa wake.. na huyu shemeji nae vp kutamani wa mwenzie kha!
Post a Comment