Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, April 29, 2011

mwana umleavyo ndivyo akuavyoWakati narudi nyumbani nilimkuta kuku wangu mmoja akihangaika pembeni  mwa sufuria ya maji, nikagundua kuwa mmoja wa vifaranga vyake kimetumbukia ndani ya ile sufuria na kifaranga huyo hawezi kutoka, na hapo mama kuku akawa anahangaika huku na kule, cha ajabu mimi niliposogelea pale yule mama kuku akanirukia kuniparura. Nikasogea pembeni, nikaona nitumie njia nyingine ili niweze kumtoa yule kifaranga ndani ya ile sufuria, kwani ilikuwa na maji, na jinsi nitavyochelewa kumtoa yule kifaranga ndivyo maisha yake yatakavyozidi kuwa hatarani.
 Nilitumia njia ya kumpiga yule mama kuku kwa ufagio mrefu mpaka akasogea mbali nami kwa haraka nikafanikiwa kumtoa yule kifaranga, akiwa katika hali mbaya, kwani alikuwa kalowana chachapa, nikamweka juwanii na mara mama kuku akaja mbio kutaka ni kuniparura, nikaosgea pembeni …nikamuona mama kuku akijaribu kumdonoadonoa mwanae ili aondokane na yale maji, na baadaye akamwingiza ndani ya mbawa yake na kulala naye kwa muda. Haikuchukua muda yule kifaranga akatoka akiwa kachangamka kidogo, lakini akarudi pale pale kwenye sufuria, anaruka kutaka kuingia mle ndani ya sufuria tena. Niliona jambo jema ni kuyamwaga yale maji na kuiondoa kabisa ile sufuria….
Tukio hili likanikumbusha mtoto wa irani yangu. Mtoto huyu alipenda sana kucheza na watoto wangu, ikawa mara kwa mara napotelewa na viisenti vyangu, nikawa nagombana sana na watoto wangu. Lakini nikiwa na mashaka kuwa watoto wangu wangu walivyo hawana tabia ya kuchukua pesa bila kuomba, nikaingiwa na mashaka na hawa watoto wanaokuja kucheza na watoto wangu.
Katika kuchunguza nikagundua kuwa kuna mmoja wa watoto hawa sio mwaminifu, ikabidi nimwambie mwenzangu kuwa awe mwanagalifu na hawa watoto wanaokuja kucheza na watoto wetu, kweli tunawapenda wanakuja kucheza na watoto wetu, lakini tabia zao zinanitia mashaka. Basi tukaona ni vyema kuwaarifu wazazi wa hawa watoto kuwa kuna baadhi ya watoto wadokozi, na ni vyema tukawakanya, ikawa ni kosa, kuwa tunawashuku watoto wa wenzao kwasababu hatutaki waje kucheza nyumbani kwetu.
Mama mmoja jirani yetu ni mmoja wa watoto tunaowashuku kuwa sio waaminifu, alikuja kuchota maji na katika maongezi akawa anatuhadithia kuhusiana na `bahati’ ya mtoto wake kuwa siku kadhaa mwanae amekuwa akipata bahati ya kuokota vitu vya thamani, ikiwemo pesa, akasema kuwa siku mbili kadhaa, mtoto wake amekuwa akiokota shilingi elifu tano, na siku nyingine akamletea shilingi elifu kumi..’ akasema kwa furaha.
‘Kaokota elifu kumi, elifu tano na wewe unakubali kweli kuwa kaokota?’ mama Nanihii akamuuliza kwa mshangao.
‘Sasa ningefanyaje, nilimshukuru sana Mungu kuwa kasikiliza kilio cha mja wake masikini, kumbuka siku hizo nilikuwa sina hata hela ya kule, baba Nanihii kahangaika siku kutwa bila kupata angalau kibarua, mara mtoto huyo kaleta hela kasema kaokota, ilibidi nipige magoti kumshukuru mungu, kuwa kaniokoa, na imetokea hivyo mara nyingi, na hata siku moja aliokota simu ya maana kweli, tukaamua kuiuza, ili tupate hela za kodi ya nyumba, Mungu ni mkarimu ukiomba anakupa bila hata kutegemea…’ akasema kwa furaha.
Aliposema hivyo nikakumbuka siku nilipopotelewa na shilingi elifu kumi yangu, nilikuwa nimeiweka kwenye kabati, mara nikapata mgeni nikatoka, niliporudi haipo, nikatafuta na kuulizia kila mtu hakuna alaiyekubali kuwa kaiona, mwisho wa siku nikakimbilia kuwagombeza watoto wangu kuwa kama kuna mtu kaanza tabia hiyo nitawachapa vibaya sana…basi siku hiyo ikapita, mara ikatokea tena nikapoteza shilingi elifu tano…nikaona sasa hii imezidi, nikasema lazima niweke mtego nione ni nani kaanzisha tabia hiyo.
 Siku moja nikawa nimetoka kazini, nikaweka pesa zangu kwenye kabati, nilikuwa nimesahau kabisa mambo ya kupotelewa na pesa, kwani tulishazoea wenyewe, tukiwa na watoto wetu hata uweke hela wapi haipotei, tatizo lilianza hapo watoto wetu walipoanza kukaribisha watoto wenzao …siunajua tena watoto kupendana ndio asili yao.
Mara nikasikia mchakato wa mtu akitembea, nikainuka pale nilipokuwa nimejilaza kwenye kochi, nikaona mkono ukinyoshwa kuelekea kwenye kabati, lakini kiwiliwili na sura ilikuwa imezuiwa na mlango sikuweza kumuona vizuri kuwa ni nani, nikainuka taratibu , bila sauti, na kwa mshangao nikaona ni yule yule mtoto wa jirani yangu ambaye anamsifia mwanae kuwa anaokota hela mara kwa mara. Nilishikwa na hasira, lakini nikasema ngoja nione mwisho wake.
 Yule mtoto akainyakua ile hela akawa anajiandaa kuondoak nikamtokea ghafla, akashituka na kuitupa ile hela chini…nikamuuliza alikuwa anafanya nini, akasema kwa haraka aliiona hiyo hela chini akaikota na alikuwa akitaka kuniletea.
‘Kuniletea wapi, wakati ulikuwa unatoka nje?’ nikamuuliza
‘Nilifikiri ulikuwa nje, ndio maana nilikuwa nakuletea…’ Akasema kwa wasiwasi. Nikambana sawasawa mpaka akakubali kuwa aliichukua kwa bahati mbaya, na nikamwambia asiposema ukweli naenda kuwaleza wazazi wake hasa baba yake …akalia sana na hata kupiga magoti kuwa nimsamehe hatarudia tena.
‘Kama unataka nikusamehe niambie ukweli umeshaniibia mara ngapi..?’ nikamuuliza. Akaomba msamaha sana na nilipomwambia tena kuwa nitamsamehe kama akiniambia ukweli, akasema kaniibia mara tatu, mara ya kwanza elifu kumi mara ya pili elifu tano na mara nyingine elifu mbili…’ hebu fikiria kama ingekuwa wewe ungefanyaje.
 Nilichofanya nikumpeleka hadi kwa wazazi wake na kuwalezea ukweli, hutaamini mtoto yule alipofika kwao akakataa kata kata kuwa hakuwahi kuchukua hela kwangu na pia hajawahi kuchukua hata senti moja kwangu. Nikabakia mdomo wazi.
‘Nawaombeni sana mumchunge huyu mtoto wenu kwani tabia aliyo nayo sio tabia nzuri…ana tabia ya udokozi…’ nikawaambia. Wazazi wale wakamfokea na hata kumchapa viboko, lakini nasikia tulipoondoka wakadai kuwa tunamsingizia mtoto wao kuwa ni mdokozi.
 Siku zikapita na hata miaka, yule mtoto kawa mkubwa, na tabia aliyozoea ikawa imeikita, na kama wahenga wasemavyo samaki mkunje angali mbichi…kijana yule akawa na tabia yake ya kudokoa, sasa hadokoi tu, ila inaiba simu za watu madirishani, anakata nyavu za madirisha anatoa simu, au saa, na hata laptop. Watu wakalalamika mwishowe wakachoka, wakaamua kumvizia, na za mwizi ni arubaini wakamnasa.
 Siku hiyo nipo kazini mama Nanihii akanipigia simu kuwa kuna msiba, nikauliza msiba gani, akaniambia ni msiba wa jirani, kijana wa jirani kauwawa, alikuwa akiiba akakamatwa akapigwa mpaka akapoteza maisha. Kuulizia ni nani akasema ni yule kijana aliyekuwa akiiba vitu kwa kupitia madirishani….
 Jamani ujumbe wa Ijumaa ya leo ni kuwa tuwe makini sana na watoto wetu, hasa wanapoleta vitu ka vile `zawadi’ au `wakisema eti wameokota kitu’ …kama akileta kitu mwambie kakipta wapi, mbane sana …jamani nwaombeni tusitumie shida zetu kuwarubuni watoto kwa sifa ambazo baadaye zitawaharibu maisha yao…tusiwe wakali pale tunapoambiwa ukweli kuhusu tabia mbovu za watoto wetu, la sivyo tutakuwa kama yule kuku, ambaye msamaria mwema anataka kumuokoa mwanae, lakini yeye anakuwa mbogo,… anadhania kuwa, watu wanataka kumharibia mwanae, watu wana nia mbaya na watoto wao…Jamani Mwana umleavyo ndivyo akuwavyo 


Ni mimi: emu-three

2 comments :

Anonymous said...

Kisa chenye hekima maadili na maonyo kwa wazazi, lakini du wapo kimia:-) m3 usikate tamaa,tupo pamoya

Yasinta Ngonyani said...

Mmmh! ujumbe huu una mafunzo mengi na mazuri kwa wazazi/walezi. Umenikumbusha nilipokuwa nyumbani Songea mtoto mmoja alimpiga kijana wangu na kwa hekima niienda kwa walezi wake na kuwaambia kuwa mtoto wao kampiga mwanetu, wakanijibu kuwa binti yao huwa hapigi wenzake...nilisikitika sana ...Ila nikaishia kusema mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Mimi leo nakuambia kwa kutaka kumfundisha kwa pamoja. Lakini wengine watafanya kama alivtofanyaiwa huyu kijana...