Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, January 5, 2011

Aisifuye mvua imemnyea-18

‘Uamuzi mkubwa ni nyie mkubaliane, mimi ..’ Maua akanyamaza, kwani mlango ulifunguliwa ghafla, na wote wakageuka kutizama nani kaufungua mlangoni bila hata hodi na sauti nyororo ikasema kwa madaha. …


‘Mimi nitawasiadia kutatua tatizo hili msiwe na shaka…’

 Mrembo, ambaye kila mmoja mle ndani alikiri kuwa kweli ni  mrembo aliibuka kianina yake, siunajua tena warembo waliosomea kazi yao. Shingo zote zikaelekea kwake, mmmh, kila mtu alimtamani sembuse Docta wangu. Hebu tuendelee na kisa chetu ili tuone mrembo huyo alivyobadili hali ya hewa mle ndani na kuleta mabadiliko, na je ni mabadiliko gani hayo. Endelea na kisa chetu....

***********

Ilikuwa imebakia masaa machache ndege iondoke, kwenye kochi la mbele wanapokaa abiria wanaosubiri kusafiri, palikuwepo msichana mrembo na wengi wa abiria walikuwa na hamu sana ya kumwangalia, msichana yule hakulijua hilo, mawazo yake yalikuwa kwa jamaa waliyekaa naye karibu,akageuza uso kumwangalia yule jamaa, na uso wake ukajaa tabasamu. Jamaa nay eye alikuwa kazama ndani ya mawazo yake, kwahiyo hakuona tabasamu la yule binti.

Yule binti, moyoni akawa anawaza mengi, akajisemea akilini, siamini kuwa leo mimi ni mke wa mtu, mtu niliyempenda kwa moyo wangu wote,na sikujua kabisa kuwa nitakuwa mke wake zaidi ya…hapana, lakini imekuwa hivyo, kumbe ndivyo mapenzi yalivyo, unapenda lakini hujui unapendwa pia, na umpendaye akawa hajui nini kilichopo kwenye nafsi ya mwenzake, mpaka muda muafaka ufike.Aligeuka bila wasiwasi akamshika begani yule jamaa aliyekaa karibu naye, na kisha kichwa chake akakiegemeza kwenye bega la yule jamaa, akamwegemea na kutabasamu tena, moyoni akasema ,tendo kama hili nisingeliweza kulifanya hivi, najisikia kama nipo peponi.

‘Vipi Mpenzi nakuona upo mbali sana, unajua sasa tunakwenda nchi za watu, nchi ambazo tamaduni zake ni tofauti na za kwetu, najua wewe ni mwepesi kujifunza mambo au sio, naomba sana ulinde heshima na tamaduni zetu na silka zetu ziwe pale pale. Na huko tukifika lazima usomee udakitari, ndilo chaguo langu kwako, natumai siku tukirudi hapa utakuwa unaitwa Docta au sio , kwani natumai ni fani nyepesi kuingia akilini mwako, u mwepesi sana kushika vitu, nina imani hiyo, lakini tutaona tukifika huko, au sio Mpenzi. Akambusu shavuni na wote wakainuka kuelekea sehemu ya kukaguliwa tayari kwa kuingia kwenye ndege.

Wakati wanakaguliwa mizigo yao, Docta alijikuta akiwaza siku ile alivyoweza walivyopambana na rafiki yake, lakini akatokea muokozi , na hatimaye mambo yakawa kama miujiza, kumbe aliyopanga mungu hayageuki, kweli nimeamini hili, akatabasamu alipomkumbuka rafiki yake , sio kazi rahisi namjua sana , lakini hatimaye kukatokea lisilo tegemewa. Kweli nimemwamini rafiki yangu hashindiki kirahisi, namjua sana rafiki yangu huyu, hashindiki katika maswala kama hayo, yupo radhi kwa lolote, akamgeukia mpenzi wake na kumbusu. Huyu ndiye chaguo langu, na ndiye mungu aliyenichaguliwa, nitampenda siku zote.

Alishukuru sana lile tukio la mwisho, mrembo alitokea kusikojulikana, mrembo mwenye sifa zote, kweli alikuwa mrembo, msomi na alionekana msemaji sana, na alivutika kwa kila mtu aliyemuona, na sijui ilikuwaje amuone tofauti, lakini mmmh. Anakumbuka jinsi alivyojitokeza pale mlangoni na kusimama kama vile wale wrembo wa ushindani wa urembo wa dunia wanavyosimama wakikaguliwa ili wapate ushindi, mwanzoni alifikiri ni Rozi, lakini alikuwa msichana mwingine tofauti , alikuwa zaidi mara mbili ya Rozi na kauli yake ya kwanza ilimfanya kila mtu mle ndani amwangalie kwa mshangao.

Akayakumbuka maneno yake alivyosema.`Mimi nitawasaidia kutatua tatizo hili, msiwe na wasiwasi..’ ina maana alikuwepo nje kwa muda akisikiliza yanayotokea mle ndani, na kweli alikuwa kama mtatuzi wa tatizo ambalo lilishaanza kuleta mgongano way eye na rafiki yake wa siku nyingi. Je ingekuwaje kama yule msichana asingetokea, ina maana urafiki ungekwisha, ina maana labda yeye angekubali matokeo na ingekuwaje baadaye. Kweli rafiki yake anajua kukamia jambo, …Hapana hilo lisingekubalika, akaguna na kulikumbuka lile tukioa kama mtu anayeangalia picha nzuri akilini.

Alimkumbuka yule msichana jinsi alivyosogea taratibu kama mtu anyehesabu hatua akimsogelea rafiki yake,..anakumbuka jinsi rafiki yake alivyobakia mdomo wazai akawa kashikwa na kigugumizi asijue nini la kufanya, hadi yule msichana alipomfikia pale alipo na kumshika mkono. Halafu yule msichana akamgeukia Docta wangu akatabasamu…lile tabasamu lilikuwa la aina yake!

‘Haya natumai mchezo wa kuigiza umeisha sasa ni maswala ya kufanya kweli, wewe uliwaambia nini wazazi wangu kuwa unakuja kutoa posa, tukakuandalia kila kitu hukuja , nikasikia eti umekutana na mtoto wa mitaani…’ alipotamka hilo neno mtoto wa mitaani akamwangalia Maua kwa dharau, na kusema

‘Mtoto mwenyewe ndiye huyu, mmmh, nakushangaa, sana, hivi wewe umevutika nini na huyu mtoto wa mitaani, heambaye hajui hata urembo, mpangilio wa kuvaa, ndio ni mzuri, lakini mmmh, hebu u mwangalia, na jaribu kulinganisha yeye na mimi uone nani zaidi….’ Akamsogelea Maua na ksuimama karibu naye, halafu akamgeukia Maua kwa dharau, kainua kidole chake chenye ukucha mrefu akakipitisha kwenye midomo ya Maua. Maua alikuwa kashikwa na butwaa tu, hakujua afanye nini, zaidi ya kutulia kimya.

‘Naomba nisimwage mtama kwenye kuku wengi , twende ukawaone wazazi wangu na kama nikunikana unikane mbele yao na unajua wazi nini kitatokea, kama unaitaka kazi yako ya udakitari au la….umeshasahau fadhila sio, umesahau..’ Docta wa Sinza akazinduka kwenye mshangao akamtizama Maua halafu akamtizama yule msichana, na harakaharaka akamshika yule msichana mkono, na kumvuta kutoka naye nje, aliona kuna jambo lingesemwa mle ndani na lingeishia kumvunjia heshima yake, altoka na yule msichana bila hata ya kuaga.

Maua alibakia kaduwaa, macho yakiwa yamemtoka bila kuaminini kilichotokea pale , akajikuta akitikisa kichwa halafu akamwangalia Docta wake kuwa atasema kitu, lakini Docta wake alikuwa kimya.Baadaye Docta wake akasema kwa sauti ya chinichini bila kujitambua, `’Hivi rafiki yangu hajaacha ile tabia yake ya shule, hivi alikuwa na nia gani kuafanya hivi…’ Halafu akamwangalia Maua huku anatabasamu akasema

`Maua samahani kwa hili, sikujua kabisa rafiki yangu ana malengo gani na wewe, na ndio maana nilitangulia kusema kuwa uwe mwangalifu na maamuzi yako, na sijui kama alishafikia hatua ya kukutaka wewe uwe rafiki yake, ningelijua hilo mapema ningekushitua, lakini n….yote ni heri, kila kitu hutokea kwa wakati wake…’ akasema Docta wangu na kuwageukia wale wazee.

‘Samahanini sana kwa yaliyotokea, rafiki yangu huyu namfahamu sana, ana katabia ka kupenda, na katamaa, tamaa, na mara nyingi hapendi kushindwa, lakini nilisikia aliiacha kabisa hii tabia kwa shinikizo la baba yake huyu msichana, kwani baba yake huyu msichana ni tajiri mkubwa na ndiye aliyemfadhili huyu rafiki yangu kusoma na hata kumfungulia hii hiyo hospitali anayoimiliki. Mzee huyo alishaamini kabisa kuwa rafiki yangu atamuoa binti yake. Sasa sijui kumetokea nini, kwani sikuwahi kumuulizia rafiki yangu kuwa mahusiano yake na huyo binti yalikuwa yameishia wapi.

Kwakweli sasa nimegundua mengi, kwani nilipokuwa nikimtajia Maua alikuwa akishikwa na kigugumizi Fulani, kuonyesha kuwa alikuwa amevutiwa na Maua, na huenda ndio sababu iliyomfanya aanze kukatisha mahusiano yake na msichana wake huyo wa siku nyingi, sijui zaidi kwa uhakika. Umshukuru sana Mungu wako Maua, kwani kama ungeenda zaidi ya hapo ungelijuta sana….’ Docta akaangalia saa yake na wakati huo huo mama mwenye nyumba akatabasamu na kusema.

‘Ndio maana moyo wangu ulikuwa ukisita kila mara, sikupenda sana hii tabia yake yakuwalika watoto wangu chakula cha machana. Mume wangu unaona, haya nilikuambia kuwa huyu mtu ana aenda ya siri, lakini hukunisikiliza maoni yangu. lakini sawa tumajionea wenyewe yaliyotokea, sasa Maua ujue nini wanume walivyo. Unatakiwa kuwa mwangalifu sana kabla ya maamuzi hasa yanayohusu mapenzi , hasa yanahusu uamuzi mkubwa wa rafiki wa kweli wa maisha, …nani wa kukuoa. Naona ujiandae muondoke …au nawafukuza jamani, lakini muda umeenda eti jamani’ akasema mama huku anacheka.

Docta akatabasamu na kumwangalia Mpenzi wake, akilikumbuka tukio lile, alimsogelea Mpenzi wake na kumbusu shavuni na moyoni akasema `usiwe na waswaisi na mimi, hapa umepata mume mwema..’ akakaa kwenye kiti cha ndege huku akimuonyeshea Mpenzi wake jinsi ya kujifunga ule mkanda wa kiti cha ndege. Mpenzi wake, mkewe akamwangalia mume wake usoni akatabasamu.

Docta akaangalia nje ya ndege , na mara akili yake ikamrudisha kwenye tukio lile tena na kuendelea kuyavuta mawazo yake ya tukio ambalo kwake aliliona lilikuwa nuru mpya ya maisha yake, na kukumbuka jinsi harusi ilivyofanyika kwa haraka bila hata kutarajia iwe hivyo, na bahati nzuri ikawa kubwa kinyume na mtarajio yake, kweli hakuna shughuli ndogo. Yeye alipanga iwe ndogo, iishe mapema ilia pate muda wa kujiandaa kwa safari yake, ambayo ndiyo iliababisha harusi hiyo ifanyike, isingekuwa hiyo safari harusi ilikuwa bado kabisa.

Siku ile walipoondoka kule Sinza, walifika nyumbani usiku, na Maua akwa anaongea na wazazi wake. Docta akaingia chumbani kwake, na mara akapokea simu , alipoiangalia akakuta ni simu ya nje. Alihisi kuna jambo muhimu sana kutoka kwa hawa watu. Na akagundua kuwa ainatoka kule alipokuwa akifanyia kazi kwa mkataba. Simu ile ilimwelezea kuwa anahitajika haraka kwani kuna nafasi ipo wazi na yeye ndiye anahitaji kuiziba, na pia kuna kozi anatakiwa kuikamilisha katika hatua za masomo yake ya udakitari bingwa.

Alishikwa na butwaa, kwani mambo mengi yalikuwa hayajakamilika na katika maelezo yake wakati anaondoka kule , ni kuwa anarudi nyumbani kukamilisha maswla binfasi ya nyumba na kufunga ndoa . Swala la nyumba keshalikamilisha lakini ndoa bado. Hajapata mke, nan i muhimu sana, kwani alishajaza kwenye mkataba wake ambao alishautanguliza kuwa ana mke. Nitaonekana muongo, na hili ni jambo nisilolipenda, lazima nifanye jambo la haraka, na sijingine ni kuoa haraka iwezekanavyo. Ni nani wa kumuoa haraka hivi. Akawaza kichwani

Akaona sasa wakati muafaka wa kuongea na baba swala hili umefika. Akatoka pale chumbani kwake, na kufika chumba cha maongezi ambapo aliwakuta wazazi wake bado wakiongea na Maua, wakiwa na furaha. Alifurahi sana moyoni mwake akasema hili nataka liwe kweli, wafurahi wakiwa na mke mwana wao, naomba mungu unikubalie dua yangu, naomba Maua anikubali niwe mume wake. Akamsogelea baba yake na kumuomba kuwa ana maongezi naye ya faragha. Mama akashangaa, lakini akaendelea kuongea na Maua, akiua hayo ni maswala ya baba na mwanae.

Akamwelezea baba yake kuhusiana na simu aliyoipokea na nini tatizo lililopo mbele yake kwa sasa. Baba mtu akashangaa na kumwambia mbona hapo hakuna tatizo kabisa, sisi wazazi wako tulishajiandaa na tulikuwa tunasubiri kauli yako tu. Baba akamkumbusha kuwa alishawahi kumpigia simu akiwa huko nje kuwa wamemtafutia msichana mzuri anayeendana na yeye, na wanavyojua msichana huyo bado yupo, na hajaolewa. Ni swala la kwenda kwao na kutoa taarifa tu, kwani waliwahi kuongea na msichana huyu akasema yeye hana kikwazo kwani anakufahamu sana.

‘Hapana baba yule sio chagua langu, nafikiri chaguo langu ni huyu msichana wa hapa…,’ akasita na taswira ya binti mwingine mrembo ikamwingia kichwani, akatikisa kichwa na kuendeela kusema `nimpempenda sana msicha huyu tulie naye na nina uhakika atakuwa mke mwema kwangu…’ akasema Docta.

‘Una maana Maua…hapana mwanangu, unatakiwa upate mke ambaye anaendana nawe ambaye utaweza kwenda kuishi naye huko, Maua kweli anaweza kuishi nawe Ulaya…, huoni itakuwa shida kwako, hajasoma, na mazingira aliyokulia…ooh, mwanangu mbona unajipa shida sana, huyu tuachie hapa atakuwa mfanyakazi wetu na najua atapata mume wa aina yake, lakini wewe huendani na yeye kabisa. Mimi hapo naona umekosea, …’ Baba akasema na kumwangalia mwanae kwa makini.

‘Baba sijakosea kabisa, huyu ndiye ninaye mpenda. Ingawaje sijaongea naye kiundani kuhusu swala hili, lakini, nahisi atanifaa sana katika maisha yangu, nitamtengeneza nipendavyo mimi na anaweza kujibadili kutokana na matakwa yangu. Naomba sana baba mumkubali huyu msichana hana tatizo zaidi ya kuwa kalelewa katika mzingira magumu…’ akamshika baba mkono na baba akaona hana la kupingana na mwane akakubaliana naye. Na baada ya mazungumzo ya nini kifanyike na mikakati ya ndoa ya haraka ikajadiliwa na baba na mwana, ikabakia baba kwenda kumshawishi mke wake. Mke wake alikuwa kapinga sana tangu awali kuwa mtoto wao amchumbie Maua, je safari hii atakubali.

Baba yule baadaye alimuita mkewe wakaongea naye kwa muda mrefu na hatimaye wakakubaliana na waliporudi barazani ambapo Maua alikuwa akiongea na Docta, wakawa wanatabasamu.

‘Unajua kwanini wazazi wana furaha kiasi hicho,,’ Maua akamuuliza Docta.

‘Labda kwasababu nimerudi kuishi nao, unajua hata mimi nina furaha sana kwani nawaona kama wazazi wangu kabisa, na nitajitahidi nikae nao hapa , labda wao wanifukuze…’ akasema Maua

‘Kweli Maua, lakini kuna jambo muhimu limetokea, na naomba ulipokee kwa moyo mkunjufu sana. Maua utajisikiaje kama ukiwa mke wangu..’ akasema Docta, na kumgeukia Maua. Na Maua akashituka na alikuwa kashika romote ya runinga ikamdondoka mkononi.

‘Wewe acha utani huo, mimi niwe mke wako, ….acha utani huo Docta. Unataka kuleta yale yale ya rafiki yako Docta wa Sinza. Mimi ningekushauri sana, umuoe Rozi, au yule msichana aliyetokea siku ile kwani anasifa zote zinazoendana na wewe,lakini mimi mbona haiji. Wakati nipo na Rozi , aliniambia kuwa anakupenda sana na mlikuwa mkiwasiliana, eti Docta…, hapana Docta mimi siwezi kuwa mke wako, hivi watakuangaliaje wanajamii, na mimi sinitaonekana nimekupa kitu…hapana Docta, nakushauri kwa moyo mkunjufu muoe yule msichana aliyetokea siku ile , yeye ana sifa zote…, na nakumbuka jinsi ulivyomwangalia sana siku ile, kasoma, ana urembo na…’ akasema Maua huku machozi yanamtoka na akageuka kuwaangalia wazazi wale waliosimama pembeni ya mlango, ….

Docta akakuna kichwa na akilini akawaza mengi, …

Je ilikuwaje, na huyo mrembo mpya aliwezaje kuiteka akili ya Docta, tukumbuke kuwa huyo ndiye mchumba wa Docta wa Sinza, sasa ilikuwaje hapo, tuzidi kuwepo jamaniiiiii!

Ni mimi: emu-three

6 comments :

elisa said...

Asante kwa kuendeleza huu mkasa..mmh natamani nijue mwisho wake !!

emu-three said...

Elisa, elisa, unatamani kujua mwisho wake, ukiujua basina stori inakuwa hainogi tena, hutaamini hapa nilipo , hata mimi siujui mwisho wake utakuwa vipi, kwani nikiujua, basi naanza kutafakari stori nyingine...mmmh, subira huvuta heri, utamu baaado kabisa, ukirejea mwanzoni mwa stori utagundua hili...!

elisa said...

nakumbuka mwanzo kabisa..mimi napenda sana kusoma mikasa/hadithi ...naweza kusoma hata kurasa 200..na bado nikakumbuka mwanzo wake, ..sijui nisemaje ..napenda kusoma hadithi/mikasa sana sana, na ni mfuatiliaji mzuri, sasa wewe umenifikisha.

Candy1 said...

Eh? Docta wa Maua kavuta picha ya msichana mrembo? Eeeeeeh M3 doh! Unajua kuzua mengine mapyaaaaaa...U never know labda mchumba wa Docta wa Sinza anaweza kumfuata Dcota wa Maua huko hukoooo...hahaha haya umeshasema na ww mwisho huujui..mi shabiki tu naendelea kuwepo :-)

samira said...

M3 yaani kama alivyosema elisa mimi pia napenda kusoma hadithi/mikasa tangu nilipokuwa mdogo mpaka leo hii basi siku hizi sichezi mbali na hapa anyway nasubiri mwisho nione yaani maua na docta wangu

Anonymous said...

What's Going down i'm new to this, I stumbled upon this I've found It positively
useful and it has helped me out loads. I'm hoping to contribute & help different customers like its aided me.

Great job.

my weblog