Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, October 1, 2010

Je Wazawa sio watendaji bora ofisini?


‘Hongera bwana nasikia umeanzisha kampuni yako, ni hatua nzuri kwa wazawa kumiliki kampuni, sijui nitume maombi kwako?’ Nikamshika mkono jamaa yangu nakukumbuka enzi zetu za shule.


‘Hubadiliki sura bwana wewe, upo wapi siku hizi, manake kukutana na `wajumbe’ inakuwa bahati ya ajabu.

‘Mimi nipo hapa na pale, na kama unavyoona umri umekwenda na waajiri sasa wanataka damu changa, wazungu nk, kwahiyo, inabidi ubangaize hapa na pale’nikamwambia huku akinivuta tukae mgahawani.

‘Bwana mimi nimeweza kuanzisha kampuni yangu, ilikuwa kama mchezo, ilianza kama mradi wa familia, na tukaweza kupata mwekezaji toka nje (mbia),ambaye tuliingia naye mkataba kama mwekezaji mwenza. Baadaye yeye akarudi kwao, akaniachia majukumu mwenyewe, nikaona, ujuzi wa elimu yangu niutumie ipasavyo, nikaamua kuachana na ajira , ili nijikite rasmi kwenye mradi wetu huu. Na kweli kimoja kikazaa kingine, nikachukua mkopo, nikaimarisha miundo mbinu, nikaboresha uzalishaji, sasa ni kampuni kubwa…lakini..’ hapa akakuna kichwa, nikajua kuna kitu kinamkwaza.

‘Lakini kuna kitu kinanihangaisha, nacho ni nguvu kazi, wafanyakazi hawanifurahishi, hasa wazawa. Hutaamini, nimetafuta mhasibu kutoka India, meneja mkuu kutoka Ulaya, na mameneja wengine wanatoka Canada, na sasa hivi namtafuta meneja mwingine toka hukohuko Ulaya, sikupenda iwe hivyo kwasababu nawalipa hela nyingi sana, ila kutokana na uzoefu wangu, wazawa hawajitumi…’ akakuna kichwa.

‘Mhhh, naona sera zenu wazawa-wawekezaji mliobahatika ni hizo hizo..’ nikamkatisha.

‘Sio kuwa napenda, lakini ukiwa mjasiriamali, unahitai faida, unahitaji utendaji bora, unahitaji muelekeo, sasa huwezi kuupata mpaka upate watendaji wenye muono wa mbali. Wafanyakazi wazawa, kila siku shida, matatizo, hili na lile, sasa wamekuja kufanya kazi au kupata sehemu ya kutatua matatizo yao, hili silipati kwa hawa jamaa, mkisha ingia nao mkataba, ni kazi kwa kwenda mbele…’ akasema huku anapokea simu na kuanza kuongea kiingereza nafikiri na hawo mameneja wake.

‘Siwapingi, ila ninaomba nikuulize swali langu moja, je unaweza kwenda Morogoro na gari lilojazwa nusu tanki, na ukijua kabisa petrol au mafuta yanahitajika tanki zima ndani ya gari lako?’ akaniangalia kwa makini, huku anakuna kichwa, baadaye nikamuona kama anaona nampotezea muda wake.

‘Sikuelewi ndugu yangu, na naona niwahi ofisini, au ulikuwa na maana gani?

‘Nyie mliojaliwa, mnapomuajirii huyo jamaa toka Ulaya, au Uhindini, mnamlipa mshahara mara kumi ya mzawa, ina maana ni sawa na kujaza gari `fully tanki’ na ziada, ina maana safari yako utafika bila wasiwasi, huna mawazo ya kukatikiwa na `uwese’ njiani. Huyu mzawa unamlipa mshahara kiduchu, msharaha wa pitia mkononi hadi tumboni. Na hata kushiba hashibi, hilo ni gari uliloweka nusu tanki ukitegemea ufike Morogoro, utafika kweli?’ nikamuona anacheka.

‘Hili ni tatizo lenu wawekezaji, ili mtu afanye kazi kwa bidiii, anahitaji tulizo la kuifikiria kazi yake, na hili huanzia toka nyumbani. Mzawa anayepewa pesa kiduchu, ana matatizo ya watoto, wagonjwa wanahitaji matibabu, wanahitaji elimu bora, anadaiwa kodi ya nyuma, ana tegemezi, ana matatizoo kibao, unafikiri akili yake itatulia kazini? Sasa angalia huyu Mzungu, umemuita, umemkodishia nyumba, unamlipia ada watoto wake, anapata matibabu ya kisasa kwa gharama yako, mashahara wake anautumia robo tu mwingine anawekeza, kwasababu ni mkubwa! Huyu mtu ana utulizo wa akili na akili yake inawaza kazi tu, kwasababu mengine umeshamtimizia sio sawa na mazawa uliyempa kiduchu na bado unamtegemea ukufanyie kazi kama huyo Mzungu. Jaribuni kuwaweka sawa, jaribuni kuwajali na wao kwani wao ni binadamu kama hawo Wazungu…’ nikamuona nimemgusa, lakini akainuka kwenye kile kiti huku anaangalia saa yake.

‘Wewe bwana acha kutunga stori zako, bado hujaacha tu –u Hadley Chase wako. Hizo ni hadithi, huwezi kumlipa mzawa kama Mzungu, kwa kazi gani, afanye kazi kama huyo mzungu kama sita…’ akasema huku anaondoka.

‘Basi huwezi kupata utendai sawa kati ya Mzungu unayemlipa vizuri na Mzawa unayemlipa kiduchu. Mtaishia kupata gharama nyingi kwa kuwaajiri wazungu, wakati mngewalipa wazawa nusu au hata robo ya hiyo gharama, na kazi ingefanyika zaidi ya hawo wazungu…lakini najua huo ni uono wa kuona mzungu ni bora kuliko mwafrika, hiyo ni kasumba…unakumbuka somo la siasa…’ nikaongea nikijua mwenzangu anaona nampotezea muda.

Hilo ni tukio la wiki, sijui nyie mnasemaje kuhusu wazawa na uajiri wa wageni, je ni kweli wzawa sio watendaji wazuri ukilinganisha na `wadhungu' au watu toka nje, na ni kwasababu gani kama ni kweli na kama si kweli kwanini waajiri wanaona hivyo?


Ni mimi: emu-three

6 comments :

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

...kuna aina (shule mbili) za maoni kuhusu suala hili..

1. Wazawa wakipewa kazi hawawezi. Hii inakuwa na kwa makusudi ama kwa kupenda

2. kwamba wazungu wanaweza. kwa nini wao waweze na siye tusiweze? elimu yaweza kuwa tatizo?

miaka kadhaa ilopita KCB ilikuwa inaongozwa na na wazawa wote kama shirika la umma. Walikuwa wanapata hasara kila leo kwa kuwa shirika lilikuwa linaingiliwa na wanasiasa.

kuona hivo wakaajiri CEO, mkurugenzi wa fedha na afisa utumishi mkuu toka nje ya africa (MZUNGU). kwa mwaka wa kwanza faida ikawa maradufu na sasa (japo uongozi wa juu umerejea kwa wazawa) KCB ndani ya kipindi hicho cha uongozi wa wazungu iliweza kujitanua na kuanzisha matawi tanzania, uganda, sudani kusini na sasa wanaelekea rwanda.

miaka michache ilopita serikali yetu ilikuwa na menejimenti za shirika la ndege na tanesco zilizokuwa zinaongozwa na wageni...mnajua nini kilichotokea.

kwa hiyo kinachotakiwa si elimu ama mzawa/mzungu BALI UTASHI wa kufanya kazi.

siku hizi watu hawaajiri mtu kwa vyeti bali utashi na mie ndicho nadhani wazawa kama ilivo kwa wazungu kinatakiwa.

'We hire 80% of attitude and 20% skills" ndo trend ya siku hizi.

Na kwa taarifa yako....unaweza kuwa na mshahara kama anaopata Mwanyika wa Barrick (ambaye ndo analipwa vizuri zaidi kuliko ma-CEO wazawa hapa Tz) lakini output zikawa zero!!!! Take it from me!

Anonymous said...

Hii sio sawa kuwa wazawa hawatendi kazi vyema kama wageni, hii ni dhana potofu. Mimi nawakubali sana wazawa, we fikiria mtu nakaa saa moja na nusu hadi saa kumi na mbili yupo ofisini, na kiasi anacholipwa ndio hicho.
Wazungu wanakuja wanapewa gari, wanalipiwa nyumba, wanatibiwa na nk, na kufanya kazi kwake ni kwa mkataba, wengine kwa masaa, nk
Watulipe mshahara kama huo wanaolipa wazungu waone kazi...Mtanzania anapiga kazi sio mchezo, kama unabisha kaulize huko Namibia nk, utaambiwa, tatizo hapa kwetu hatuthaminiwi!

Anonymous said...

m3 leo umewapa ukweli wao hao waajiri wetu. Hii ni kweli kabisa huwezi ukafanya kazi kwa ufasaha iwapo nyumbani kwako kuna matatizo. Lakini pamoja na hayo yote huwa tunajitajidi sana kujituma ktk kazi.

Waajiri wana kasumba mbaya sana, kwavile hapa Bongo ajira ni shida ndio wanatumia fimbo ya kutunyanyasa kiivyo. Ni mbaya sana.
Hata kama utendeji wako wa kazi ni mzuri kuliko hata huyo mzungu, lakini ni bado tunaonekana hatujui. hata mimi hii inaniuma sana.

Nimefurahi sana leo m3 kutoa hii stori, kwani kama kuna mwajiri yeyote atakae isoma itamgusa sana. Labla awe na kasumba ya unyanyasaji, kuona wazungu ni bora kuliko mwafrika.

Na kweli huwezi kuweka mafuta nusu tangi halafu huende safari ndefu bila kusimama uongeze njiani. Lakini ukiweka full, huwezi pata shida njiani na wala usimamisimami ni moto mdundo hadi mwisho wa safari yako.

EDNA said...

Watanzania tuna ile kutokujiamani na dhana potofu kuwa mtu kutoka ulaya ndiye anayeweza kuongoza company au shirika..Siamni kuwa kweli wazawa hawawezi kufanya kazi.Ujumbe ni mzuri M3

Anonymous said...

Mchangiaji wa kwanza umenikuna, ni kweli kuna dhana kuwa `elimu' ndiyo `utendaji' lakini wako wangapi wenye elimu lakini utendaji wao ni hakuna. Unaweza ukasomea udakitari, lakini huna utashi wa udakitari, nini utakachofanya kama sio kupiga bla-bla siku ziende , lakini kama umeusomea kwa utashi, utakuwa na huruma na wagonjwa...

Simon Kitururu said...

Nimemsimulia kitu kuhusu hili akanipiga swali: Si nasikia WAZAWA huwa awasomei kitu wanachopenda ila kombinesheni tu zilichoruhusu kitu ambacho chaweza kufanya aliyetaka kuwa mjenzi kujikuta kasomea kilimo na kilimo hana mori nacho?