Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, November 16, 2009

Ubinafsi

`Lile jeupe ni la kwangu,

`Hapana lile lina rangi ni la kwangu’

Ilikuwa ni ugomvi wa watoto wawili, walikuwa wamepigana na kuchafuliana ngua, na tulipowaachanisha na kuwauliza, nini kulikoni! Hutaamini chanzo cha ugomvi wao. Wao walikuwa wakitoka nyumbani kuelekea shuleni, njiani wakala amini kuwa likipita gari jeupe litakuwa ni gari la mtoto wa kwanza, na likipita gari lenye rangi linakuwa ni gari la mtoto wa pili, sasa ghafla likapita gari lenye rangi nyeupe na mchanganyiko wa rangi nyingine, hapo ukazuka ugomvi, kila mmoja akidai kuwa lile ni gari lake.

Mimi nilijiondokea huku nikikumbuka mpira uliopita wa Simba na Yanga, wapo jamaa waligombana na hata kuvunja urafiki eti kisa ni kila mmoja alikuwa akidai kuwa timu yake ni bora zaidi. Ukumbuke ugomvi huu ulitokea kabla hata ya mchezo wenyewe. Matokeo mliyasikia. Nikaulinganisha ugomvi huo na huu wa hawa watoto. Ndio ushabiki unakubalika, na kila mmoja ana haki ya kutetea timu yake, lakini usivuke mpaka hadi kuwekeana uadui, huo utakuwa si ushabiki, utakuwa ni utoto, sawa na wale watoto waliokuwa wakipigana huku wanadai magari ambayo hawajui hata wamiliki wake .

Wakati nawaza hili, nikasikia taarifa ya habari ikisema, watu wamepigana hata kuchomeana nyumba kisa ni ukabila, nikacheka nakuwakumbuka wale watoto. Hebu jiulize hawa wanaopigana eti kwasababu ya kutetea kabila lake sijui kwa vipi, anajua chanzo cha hilo kabila!. Waanzili wameshakufa zamani gani, leo hii tunakwidana mashati, hadi kuuana eti kwasababu ya ukabila.

Visa kama hivi vipo hadi maofisini, mabosi huwachagua wafanyakazi wao kwasababu ya ukabila, udini au hata utaifa. Hii inaashiriana nini. Nikacheka nikikumbuka ule ugomvi wa watoto, kumbe hata sisi watu wazima na elimu zetu na utajiri wetu na uongozi wetu hatuna tofauti na watoto wadogo ambao hugombea kitu ambacho hawakijui chanzo chao.

Upo ugomvi wa dini, kila mmoja anadai dini yake ipo sahihi, na labda ungeishia kwenye mijadala ingekuwa vyema, lakini watu hujaa chuki, hadi kuwekeana donge rohoni kuwa watu wa dini fulani hawafai. Hebu jiulize hivi kweli dini ndivyo inavyotaka. Nijuavyo mimi dini zinafundisha upendo, dini nia yake kubwa ni kuleta usalama, amani na upendo. Lakini sisi tumeweka chuki zetu binafsi za ukabila za umimi hadi kwenye maswala ambayo hayahusiani kabisa na fikira zetu. Huu ni ubinafsi , hakuna kingine. Na kama mwenyezimungu angeliweka nafsi zetu wazi, watu tungeogopana, kwasababu ubinfsi umejaa ndani ya nafasi zetu huku tunatafuta upenyo wa kuzionyesha hadarani. Ubinafsi huu umejenga kutu. Kutu mbaya yenye sumu ambayo ipo tayari kuua.

Jamani tuondoe ubinafsi na tujenge upendo, kwani ubinfsi hujenga chuki bali upendo hujenda amani ya kweli, vinginevyo hatutakuwa na tofauti na watoto wadogo ambao akili zao hazijakomaa na kutofautisha zuri na baya.


From miram3

1 comment :

Anonymous said...

Hahaha unanikumbusha mbali kweli, niliwahi kuzichapa na mdogo wangu tukigombea magari yanayopita barabarani. hongera kwa kazi zako nzuri, ipo siku utatoka