Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, November 10, 2009

Mtoto umleavyo

Ilikuwa siku moja kwenye sikukuu, tulialikwa na rafiki yetu aishiye mitaa ya matawi ya juu, mitaa hii inajulikana jinsi ilivyojengwa vizuri, bustani zinatunzwa vizuri na mitaa yake imajipanga vyema, sio kama maeneo yetu ambayo unaweza ukamwaga maji dirishani yakamwagikia chumbani kwa mwenzako kwenye nyumba ya pili.
Siku hiyo naikumbuka sana, kwani shemeji yangu aliamua kutuchukua kwenye kimin-bus cha kazini kwao, basi bwana familia zetu zilijazana humo, si tumealikwa bwana, hatukujali mwenyeji wetu amejiandaa vipi, sie tunachojua kuwa wao wa matawi ya juu, wanazo, na hata tukifika shule nzima tutapata huduma tu.
Tulifika masaa ya mchana, kijua kilikuwa kikiwaka vilivyo, lakini kwa wenzetu, miti na bustani vilisaidia kuifanya hali ya hewa iwe na upepo mwanana. Tulikuwa tumeshalowana majasho ingawaje tulikuwa ndani ya bus, siunajua tena foleni za Dar. Unaweza ukatulizwa kwenye mataa masaa mawili, bwana barabara anaita upande mmoja tu, wengine wanasema kapigiwa simu na bosi wao kuwa anakuja, na muda aliopiga simu alikuwa bado anakoga, sasa mpaka avae, atoke barabarani, nyie manasota kwenye mataa. Hizo ni poroja za wasotaji!
Tuliteremka na watoto wetu kwa kifijo, sio unajua tena watoto wetu wa mitaa ya kwetu, wakipanda gari basi kwao ni hadithi. Walishuka kwa makelele, kiasi kwamba wenyeji walikuwa wakichungulia madirishani huku wanashangaa, wakizani wamevamiwa na watoto wa mitaani.
Tuliingia ndani, lakini watoto kama kawaida yao wakabaki nje, na huko nje tulisikia vumbi lao, kwani waliona mpira umehifadhiwa na wenyeji, wao wakauchukua na kuanza kucheza kwenye bustani za watu. Yule binti mfanyakazi wa pale, akabaki ameduwaa, atafanyaje kuwakataza wageni anaona sio jambo jema. Hata watoto wa wenyeji wetu wakabaki wameduwaa, wakiona kitu cha ajabu. Wao siku zote wanakatazwa kucheza kwenye bustani, na mpira wanachezea kwenye viwanja maalumu, sasa leo wanaona maajabu, watoto wenzao wanacheza na kupiga mpira huku na huko, bila kujali kuwa hizo ni bustani maalumu, na sio viwanja vya mpira, bila kujali maua mazuri yaliyokuwa yakitunzwa kwa umaridadi, hawa ndio watoto wetu wa mitaa ya kwetu
Hawa ni watoto wetu ambao hukua kutegemeana na mizingira waliyolelewa, huwezi kuwalaumu, kwao mpira ni popote, wanataka wawe mahodari kama hawo wanaowaona kwenye TV. Hawajali watu wanaowashangaa, hawajali hata watoto wenzao wenyeji, na kujiuliza kwanini wao hawataki kucheza na wao, na wamebaki kuwashangaa.
Wenyeji wetu walielewa hilo, na nilisikia mmoja akisema, `Mhh, hawa ni watoto wa uswahilini’, wao sio waswahili tena, wao wanaoishi kizungu, ni waoto wa uzunguni. Ilikuwa ni kero kwao, kwanza mualiko waliotegemea ni wa watu wasiopungua watatu, sie tulikuja na darasa zima, ilibidi waharibu bajeti yao, kwani wao huishi kwa bajeti maalumu, lakini sie hatukuweza kuwaacha watoto wetu majumbani, kwani furaha yetu ni kuona watoto wetu wanafurahi. Kama wasemavyo kuwa, kwa tajiri ni mali yake kwa masikini ni watoto wake.
Tofauti ya watoto hutegemeana na wazazi na maeneo wanapoishi. Watoto wanaiga watoto wanajifunza na watoto hubadilika kutegemeana na nyie walezi. Wapo ambao hawawezi kula mpaka waombe kwa mola wao, wapo ambao wakiwekewa chakula wanagombea utafikiri chakula hakiwatoshi. Wapo ambao shikamoo kwa wakubwa haibanduki mdomoni, wapo ambao kusalimia mpaka waombwe. Wapo ambao wanajua haki yao lakini wapo ambao hawajui hata sehemu ya kulala ni wapi, watoto wa mitaani, wengine hawamjui hata mzazi mmoja, wanachojua ni majalala na kuombaomba mitaani na barabarani.
Hivi ni vizazi tofauti, makuzi yao ndiyo tegemeo la kesho. Wakilelewa vyema, tunataraji taifa jema la kesho na wakilelewa vibaya matokeo ni taifa bovu lisilo na nidhamu. Na tofauti yao inavyozidi ndivyo tunavyoona makundi ya walinacho na wasionacho.Lakini yote hata yanategemeana na utaratibu sio tu wa mzazi pekee, bali hata wa kitaifa. Mitaa, bustani, na maeneo ya viwanja vya michezo na taratibu nzuri za mazingira yetu yanaweza yakamjenga mtoto ajue ni wapi pa kuchezea mpira na wapi pa kupumzikia. Tukumbuke kuwa mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.

From miram3

2 comments :

Anonymous said...

Hongera mzazi, nahisi wewe ni baba mwenye busara, mungu akuzidishie. Nashangaa sana watu hawakuungi mkono, toeni comments, mmpe moyo miram3.

Anonymous said...

Wabongo bwana, mpira unaweza ukachezwa hadi chumbani, hawaangalii uharibifu.