Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, September 14, 2018

YOTE NI KWA MAPENZI YA MUNGU-48



 ‘Ndugu muheshimiwa hakimu, katika orodha ya mashahidi huyu mtu hakuwepo, jina lake halipo kabisa,…iweje aletwe sasa hivi, na kwaharaka apewe hiyo nafasi, kiukweli sisi tunashindwa, na tunapojaribu kushinikiza ili utaratibu ufuatwe, tunashindwa muheshimiwa hakimu…’akasema mtu wakili wa benki.


‘Kwahiyo unanilaumu mimi, au…?’ akauliza hakimu akimuangalia huyo wakili.


‘Hapana muheshimiwa hakimu….’akasema huyo wakili kwa adabu.


‘Mahakama inafanya kile inachoona ni sahihi, je hayo yaliyoongewa na mashahidi ungeyafahamu vipi kama tusingelifanya hivyo, ..?’ akauliza hakimu na wakili huyo akabakia kimia.


‘Kazi ya mahakama ni kuhakikisha haki inatendeka, wakati mwingine inabidi tufanye hivyo , ili sauti za wengine ambazo zinahitajika kusikika zisikike,…shahidi aliyefika sasa hivi kasema ana ushahidi, na mahakama hii imekuwa ikisubiria huo ushahidi, ..ili haki iweze kutendeka, wewe una wasiwasi gani mpaka hapo…?’ akauliza hakimu


‘Hakuna wasiwasi muheshimiwa hakimu, maana sisi  tunao ushahidi wa kutosha, ushahidi ambao mahakama iliutambua awali, hatuna shaka na hilo…’akasema wakili huyo.


‘Kama ni hivyo, basi,ngoja wenzako na wao waweze kuonyeshe ushahidi wao, kama ni wa halali, tutaliona hilo, ..ili tuhukumu kwa haki,…usilalamika kuwa  utaratibu haupo, utaratibu upo, kwa namna hiyo,…’akasema hakimu.



‘Sawa muheshimiwa hakimu…’akasema wakili yule akigeuka kumuangalia huyo shahidi aliyefika…


Wakili wa upande wa wale wanaodai kuwa madeni sio ya halali, akasogea mbele,…


‘Sio kweli kuwa huyu shahidi hakuwepo kwenye orodha yetu,  shahidi huyu alikuwa muhimu sana kwetu, kwani yeye ndiye aliyekuwa akishirikiana na watu wa usalama, kulifuatilia hili jambo, lakini akaja kuumizwa, na kalazwa hospitalini…’akasema wakili huyo.


‘Na sasa ameweza kugundua ushahidi muhimu kwenye hii kesi,  na muheshimiwa hakimu muda wote amekuwa akisisitizia hilo la ushahidi, maana walengwa, wanaodaiwa kuwa wana madeni, hawakubaliana nayo,…sasa  ushahidi umepatikana, muhimu tuona huo ushahidi ulivyo,…’akasema wakili.


‘Sawa…tuonyesheni, lakini usiwe wa maneno matupu, kiutaratibu wa kibenki, tunahitajia, maandishi, ..…’akasema wakili wa benki, kwa kujiamini



‘Wewe subiria tu,  kila kitu kipo ,..mtu wa kuutoa huo ushahidi ndio huyo,… hapo …’hata kabla hajamaliza hakimu akasema;


‘Wewe shahidii una uhakika unao ushahdii wa kutosha maana muda umekwisha, tusije kupotezeana muda tena hapa,… kama haujakamilika ni bora tuisitishe hii kesi, itakuja kuendelea tarehe nyingine..?’ akauliza hakimu.


‘Ninao huo ushahidi  muheshimiwa hakimu, …’nikasema na kabla hakimu hajasema neno, nikaongea;


‘Na pamoja na huo ushahidi,  nina ombi moja muheshimiwa hakimu …’akasema shahidi huyo mpya


‘Ombi gani tena…?’ akauliza hakimu huku akiangalia saa, na kukunja uso kidogo, kuashiria muda unakwisha


‘Ningelipenda shahidi aliyotoa maelezo mengi awepo hapa mbele, ili athibitishe ushahid huo, na ahojiwe kuhusiana an ushahidi huo, maana yeye ndiye anayeufahamu zaidi, na maelezo yake yatarahisisha kulimaliza hili tatizo, ..’akasema shahidi aliyefika


**********

 Yule shahidi aliyekuwepo awali, akaitwa tena, ..alipoingia na kumuona huyo shahidi mpya aliyefika, akamuangalia, halafu akacheka,…


‘Umepona…?’ akasema hivyo tu, na mimi sikumjibu, nikampisha yeye akae sehemu huyo ya shahidi, na mimi  nikawa nimesimama kama wakili…japokuwa maswali yangu sio ya kama wakili, bado wakili alitakiwa kuniongoza.



‘Umesema umeleta ushahidi, sasa tunataka wewe uutoe huo ushahidi wako, na uendelee kumuhoji huyo mtu uliyetaka kumuhoji kutokana na huo ushahidi…’akasema wakili.


‘Labda kwanza, ningeliomba tuliweke hili wazi, ushahidi wangu pamoja na nyaraka, bado unahitajia maelezo ya huyu shahidi, niliyemtaka aje hapa, nia ni kuthibitisha hizo nyaraka na kupata maelezo yake,…’nikasema


‘Lakini nyaraka hizo, au ushahidi huo unaonyesha dhahiri hilo deni lilitokea wapi, au. Hilo deni ni la nani…?’ akauliza wakili


‘Bila shaka, ushahidi huu unaonyesha deni lilivyotengenezwa, na nani ni muhusika wa hilo deni, …muhimu ni shahid huyu kuwa mkweli,..’nikasema


‘Haya nakuachie undelee na mtu wako,..ningeliwaomba upande wa pili, wasiingilie kwanza, ili tuweze kuupata ukweli, kwasababu nia yetu ni kupata uhakika wa hilo au hayo madeni,…’akasema wakili mtetezi wa madeni.


Wakili wa benki akatikisa kichwa kama kukubali kwa shingo upande, akasema


‘Sisi hatuna shaka, maana ushahidi halali tunao…’akasema


‘Sawa ngoja tuone….’akasema wakili mtetezi wa madeni, akiniashiria mimi niendelee…


*************

Yule shahid aliendelea kuniangalia mimi huku akitabasamu, akijifanya hana wasiwasi kabisa. Ni kweli kwa muonekano wake pale, iliashiria hivyo.



‘Ndugu jina lako halisi ni nani……?’ nikamuuliza, na wakili wa benki akataka kuingilia kati, na …huyo jamaa akawahi kujibu, bila kumjali huyo wakili.


‘Jina langu kama nilivyojitaja awali, naitwa..’akataja jina lake kwa kifupi vile vile.


‘Una uhakika hilo ndio jina lako kamili,…maana naona kama ni kifupi cha majina yako, au wewe una majina mangapi ya kisheria..?’ nikamuuliza.


‘Majina ni majina tu, ..naweza kuyataja kwa kifupi kwa kirefu, ilimradi kunakohusika  nimeshaandika au kutaja majina yangu yote,  au kuna tatizo kwenye hayo majina yangu…’akasema na kama kuuliza.


‘Majina yako kwa kirefu ni nani, nataka uyataje mahakama iyasikie..?’ nikamuuliza, hapo akasita, na wakili wa benki akaingilia kati , akisema mimi napoteza muda, badala ya kuonyesha huo ushahidi nauliza mambo yaliyokwisha kuulizwa.


‘Nina maana yangu kubwa kumuuliza maswali hayo maswali, kwani yanaendana na huo ushahidi nilio nao,…, shahidi huyu ana majina mengi, na katika nyaraka zake za kumbukumbu kaandika majina tofauti tofauti, hii ina maana gani,…?’ nikauliza.


‘Hayo ni majina yangu, nayamiliki mimi, naweza kuandika nipendavyo,..kwani kuna tatizo gani kwenye hayo majina yangu…’akasema


‘Kwanini unatumia ni muhimu sana tukalifahamu hilo…, maana hapa tunautafuta ukweli wa jambo, ukweli wa kumbukumbu zako, ambazo zinaendana na hayo madeni, je unaweza kutuambia ni kwanini unatumia majina tofauti tofauti…?’ nikauliza na hapo akageuka kumuangalia hikimu, alipoona hakimu anamuangalia yeye,  akasema;


‘Natumia majina hayo kwa masilahi yangu binafsi, je kuna sheria inayomkataza mtu kutumia majina yake apendavyo…, ilimradi haikizani na sheria au mahitaji ya serikali, niambie…?’ akauliza huyo shahidi.


‘Ninachotaka kufahamu ni kwanini sehemu nyingine unatumia majina mengine na sehemu nyingine majina mengine, wakati sehemu hizo ulitakiwa uandika majina yako kwa kirefu, …?’ nikamuuliza


‘Jibu rahisi ni kwa kupenda mimi mwenyewe,…. na jibu unalotaka wewe, najua ndivyo unavyotaka wewe, nimekuwa nikitumia majina hayo, nikiwa na maana yangu maalumu kibiashara,…’akasema


‘Tufafanulie tafadhali, au biashara zako ni za siri, kampuni zako ulizoanziasha hutaki watu wakufahamu au, ni sababu gani ya msingi,…?’ nikamuuliza


‘Ni kweli mimi ni mfanyabiashara, nina vitega uchumi vyangu hapa na pale, na sio haramu,…na katika biashara kuna mitihani yake, ushindani wa biashara nk..…mimi nafanya hivyo, kwa nia ya kujihami, kwa namna moja au nyingine,..sihitajii kueleza hili kwa undani zaidi, maana hapa wapo watu wengi, unanielewa hapo..’akasema


‘Jina lako la mwanzo halisi ni lipi…?’ nikamuuliza, akaonekana kukerwa na hilo swali, lakini akasema kwa shingo upande.


‘Majaliwa…’akasema


‘Sio majalala ?…., je hilo la Majaliwa,Ulilitaja hapa mahakamani…?’ nikamuuliza


‘Niliandika hivyo..lakini sikulitaja hivyo, kwa masilahi yangu yangu binafsi, na sikuulizwa nilitaje, kama ulivyotaka wewe, na hali ya kidunia sasa hivi inajulikana, mtu anajijua mwenyewe anachokifanya,.. mwenye kuelewa hilo kama mfanyabiashara,  hana haja ya kudadidi sana kuhusu hilo…’akasema


‘Nakumbuka kwenye maelezo yako, ulisema nesi, au docta sijui aliyeandika jina lako, aliandika kwa dharau..kwa vile mama yako hakuweza kulitaja vyema…kitu kama hicho, wewe uliliongelea hilo jina…hapa nakuuliza unasema jina sio muhimu, huoni kama unatuficha kitu hapo…?’ nikamuuliza.


‘Nikufiche nini bro…, sijaficha kitu kwenye jina langu, kama kuna kitu nimeficha, tuambie, hapa ni sehemu wazi, mahakamani…’akasema


‘Nikuambie…?’ nikawa kama nauliza


‘Ndio niambie, mimi sina shaka na hilo, hayo ni majina yangu na sikufanya hivyo kwa ajili mbaya…’akasema


‘Jina lako unaitwa Majaliwa,…na hayo majina mengine umekuwa ukiyatumia pale unapokuwa na shughuli zako maalumu, au..ni kwa vile hukutaka itambulikane wewe ni nani , kwenye baadhi ya shughuli zako,..’nikasema


‘Unaweza ukawa sahihi, …sijui una maana gani, ukisema maalumu, au shughuli zako…’akasema


‘Sawa, wewe kwa mara ya mwisho ulikuwa mfanyakazi wa kampuni gani..?’ nikamuuliza

Shahidi kwanza akatabasamu, baadae akasema;


‘Ndio ushahid wako huo,… nilijua unapekenyua kwenda wapi,…maana mimi ni mfanyabiashara, nimeshaeleza hilo…’ akasema.


‘Kabla ya kuhamia kuwa mfanyabiashara na muwekezaji, ulikuwa ukifanya kazi gani..?’ nikamuuliza, halafu akatabasamu


‘Hahaha, wewe unazungukaaa, kwanini husemi moja kwa moja…hahaha…, najua ulikuwa unataka kufika huko, ..mimi nilikuwa nafanya kazi benki, sawa, ehee…’akasema akitikisa kicha na kubenua mdomo kama kebehi fulani hivi.


‘Na wakati upo benki ulikuwa ukitumia jina gani…?’ nikamuuliza na hapo akaangalia mbele akitabasamu, ile ya kuonyesha anafurahia hiyo hali.


‘Kumbukumbu zangu zipo wazi, jina hilo hilo , Majaliwa,…’akasema


‘Kwenye baadhi ya  kumbukumbu zako za barua,..hata mawasiliano ndani ya ofisi, ulikuwa ukitumia kifupi,… ulikuwa hupendo kutumia jina lako hilo, wakati wewe ulikuwa sehemu nyeti kama hiyo, ni kwanini labda…’nikamuuliza.


‘Sikumbuki hilo…kuwa nilikuwa natumia jina kifupi,..lakini hata hivyo, kama muajiri wangu angelikuwa na tatizo na hilo, angelisema, au sio…au waliokuwa waajiri wangu kipindi hicho, wamesema lolote kuhusu hilo…’akasema


‘Umeanza kusema hukumbuki…lakini wewe umedai kuwa una akili sana, sizani kama maswala ya kumbukumbu za ofisini , hasa za jina, na ulichokuwa ukifanya, unaweza kusahau,…au ?’ nikamtega hivyo.


‘Hahaha ndugu yangu, usione kwanini nakujibu hivyo, najua unataka nini, kiukweli kama ningelikuwa mtu wa kawaida ningelishasahau yote ya benki, lakini akili yangu ina kumbukumbu kubwa, kama nitasahau baadhi,…ujue ni bahati mbaya tu…’akasema


‘Vizuri, kama ni hivyo utanisaidia sana…’nikasema sasa nikiogea kidogo mbele.


‘Hahaha…najua unaelekea wapi ndugu yangu, tusipoteze muda, mimi nitakuambia hicho unachokitafuta wewe kutoka kwangu…’akasema


‘Kama unakijua ninachokitafuta basi niambie..ili tusipoteze muda…’nikasema


‘Maelezo yangu mengi ya awali, yalilifafanua hilo, wewe hukuwepo,…mimi nililiweka hilo bayanai, kuwa pamoja na mengine mengi,… mimi nilikuwa natafuta namna..ya kuwezesha, haki ya wahanga, haki ya mama yangu mzazi,.., haki ya mama yangu mlezi, haki yangu mimi mwenyewe viweze kufika sehemu kama hii, na haki iweze kutekelezwa,,’akatulia nikajua kamaliza,


Na pale nilipotaka kuuliza swali, akaendelea kuongea;


‘Kwa vyovote vile,…niliyoyafanya, yaliyotokea kwa kupitia kwangu, sikuwa na maana nyingine japokuwa, kuna hili na lile,…kama nilivyosema awali, kuna muda tamaa ya pesa iliniingia, hata hivyo, kama hao walidhulumu walitumia pesa kama silaha yao, ulitaka mimi nifanye nini, eeh….’akawa kama anauliza


‘Kwahiyo nilipokuwa hapo kazini,..ambao wewe umepalenga… ndio nikaona ..nipo kwenye nafasi nzuri, ya kuitumia hiyo silaha ya pesa,..kulifanikisha lengo langu..’akatulia


‘Najua nikisema hivyo, wengi wanafikiria kuwa nilitengeza hilo au hayo madeni hivyo..mimi lango na nia yangu, ni kuwatumia wababe hao walionidhulumu mimi na familia yangu, ili mwisho wa siku wafike hapa..


‘Nia na madhumuni yangu, ni ili kuisukuma haki ije kutendeka, na nilikuwa natamani sana nije hapa niyaelezee hayo niliyoyaelezea, je ningelikaa kimia, ingefika hapa, sasa kama kuna watu wameumia, nawaomba wanisamehe sana, ila wakumbuke mama yangu aliumizwa, tena sana…’akasema.


‘Umemaliza…?’ nikamuuliza


‘Mhh, labda kama unataka maelez o zaidi ya hayo…’akasema


‘Lakini hayo uliyoyaelezea hapa, hayo…’nikaonyeshea ishara ya vidole ya kuaongea…,


‘Ni maneno tu ya kujihami, hayajaweka bayana kuhusu madeni hayo ya watu, na hao watu sio wao waliokufanyia huo ubaya, hilo lipo wazi …mbona umewalenga hao watu, kama mama mjane na watoto wake, …mama mjane na yatima, na sio hao tu wapo wengine,…kwanini unawadhulumu watu haki zao, huna huruma wewe…?’ nikauliza


‘Nikuulize swali moja, je mimi nilikuwepo wakati baba anamtesa mama,..kwanini mimi naumia, nateseka kwasababu ya hilo….damu ..ina nguvu, na…kama nisipofanya hivyo, haki yangu nitaipataje maana ukisema hivyo, ina maana kwa vile sikuwepo, basi nisahau, nisahau pia na kudai haki yangu, si ndio hivyo,…hapana…’akasema


‘Kesi hii msingi wake mkubwa  ni kuhus deni, au madeni ya watu wanayodaiwa, wewe umeshasema kuwa hayo madeni ni halali kwao, wao hawakubaliani na hilo…’akaambiwa na hapo akatikisa kichwa, halafu akasema;


‘Sasa mimi nahusikanaje na hilo, mimi sio banki, …na mimi sasa hivi sio mfanyakazi wa benki siwezi kuliongelea hilo, …nikiongea hayo ya ofisi za watu,..eeh.., ninakiuka masharti ya uajiri…natumai hilo lipo wazi.au..sijaeleweka hapo...’akasema


‘Kisheria, hii sasa ni kesi,..na ni kesi ya madai, ina maana kila jambo la madai, hata kama ni la kiofisi halina usiri tena hapa, mahakama inaweza kuitisha kumbukumbu zote ili kuhakiki hilo,…, kinachotakiwa hapa kwa hii kesi, … kwasasa ni wewe kuelezea uliyowahi kuyafanya ukiwa mfanyakazi wa benki…’akaambiwa


‘Kama yapi…?’ akauliza, hapo nikageuka kumuangalia wakili wangu ambaye alikuwa akitabasamu.


‘Ndio nilianza hivyo, mimi nilijua utaelezea yote hayo, ili uwe mkweli kwa mama yako na kwa jamii,……sasa nakuuliza swali hili, maana umesema wewe sasa hivi haupo benki, je huko benki ulifukuzwa kazi au uliacha kazi.


‘Niliachishwa kazi…sio rahisi mtu kuacha kazi, au sio, labda awe na masilahi mengine…’akasema


‘Kwa kosa gani…?’ nikamuuliza


‘Kwa kosa gani, sijasema nilifukuzwa kazi,…eeh,…mimi sikuwahi kufukuzwa kazi, mimi nilipunguzwa katika zoezi la upunguzwaji wafanyakazi, japokuwa walikuwa bado wananihitajia, kilichochangia sana, ni kutokana na hali yangu ya kiafya, na mimi nikakubaliana na hilo, kiukweli nilikuwa napata shida sana…’akasema.


‘Ni kwa vile ulishawekeza vya kutosha au sio, maana huwezi kuacha kazi kama huna masilahi , kwa mujibu wa kauli yako, au sio…’nikasema.


‘Hahaha, acha wivu ndugu yangu  wewe, najua ushapekenyua pekenyua kila mahali, ukanijua nilivyo na miradi yangu,…hahaha, hiyo ni jasho langu, na …ilibid nifanye hivyo, …haina shaka,…na kila kitu kipo kihalali, hilo na kuhakikishia…’akasema kwa kujiamini kabisa


‘Wakati unafanya kazi benki wewe ulikuwa kitengo gani..?’ akaulizwa


‘Kwanza cha mtandao baadae nikahamishiwa kitengo cha madeni, twende, maana kuna lengo lako sio …’akasema akitabasamu lakini akionyesha uso wa kutafakari, …


‘Kwanini ulihamia kitengo cha madeni…cha mikopo, wakati wewe umesomea na uliajiriwa hapo benki kama mtaalamu wa mitandao…?’ akaulizwa


‘Waajiri wangu waliona ninafaa huko, mimi kama nilivyosema awali, akili yangu iliweza kujua mambo mengi kwa haraka sana,…pamoja na kwamba mimi niliomba kazi benki  kwa kupitia taaluma hiyo ya mitandao.., lakini pia mimi nimesomea mambo ya mahesabu, ..uhasibu, pia masoko eeh, banking..…namshukuru mungu kwa hilo…na kwa muda huo kitengo hicho kilihitajia mtu wa haraka kutokana na mikopo kuwa mingi…’akasema.


‘Kuna taarifa kuwa wewe ulifanya njama mtu aliyekuwepo hapo akafukuzwa, nia ni wewe uweze kushikilia sehemu hiyo, kweli si kweli…?


‘Sio kweli…’akasema  akionyesha kushangaa.


‘Nikimuita huyo mtu akalithibitisha hilo, utasemaje…?’ akaulizwa


‘Muite,eeh, muite,…nia si kuthibitisha hilo tu, aje tupambane naye hapa,..’akasema kwa kujiamini, mimi nikamuangalia hakimu nikaona anatizama saa yake.


‘Kwa vile muda ni mchache, hili tunaliweka kama bakia, tutakuja kulithibitisha hilo, kama ni muhimu,..kuwa wewe ulifanya njama fulani fulani hadi jamaa akaonekana hafai, na mengine zaidi ya hayo…ila kwa hivi sasa  swali langu la muhimu..ni hili…’nikamuangalia moja kwa moja usoni.


‘Wakati upo kitengo hicho cha mikopo, kuna barua nyingi za watu kulalamika kuhusu mikopo yao, na wengine walilalamika kuwa ndugu zao waliofariki wamepewa mikopo ambayo sio sahihi,na zaidi kuna watu walilalamika pesa zinachukuliwa kwenye akaunti zao, wakati wao hawajafanya hivyo…kweli si kweli…?’ nikamuuliza.


‘Mhh….mimi sijui,…ndio eeh, yawezekana, ndio, …na hayo ni mambo ya kawaida tu kwenye sehemu za kazi.., ila mimi nilipokuwa pale, eeh,mmh..…niliwajibu, wathibitishe, kitengo kiliwajibu, na kumbukumbu zilikuwepo, je baada ya kuwajibu wao walifanya nini, je kuna ambao walifika mahakamani..?’ akauliza


‘Ndio hawa hapa, baadhi yao, ndio hawa wamefika mahakamani kudai haki yao…sasa rejea kwenye kumbukumbu za ofisini kwako, wewe uliwahi kuitwa, kutokana na malalamiko hayo,…na pia kutokana na madeni ya watu yliyokaa muda bila kulipwa, wewe kama mkuu wa kitengo ulipendekeza kuwa hayo madeni mengine ya zamani, ya watu waliofariki,  yafutwe kwa vile, hayana namna ya kulipika , kweli si kweli..?’ akaulizwa.


‘Hahaha, kweli umefanya kazi….hilo ni kweli…lakini sio yote yaliyokubalika, mengine utawala ulikataa, na yakaendelea kuwepo, ni mambo ya kawaida au sio…’akasema


‘Je deni hili la …marehemu, mume wa mama mjane, ambaye ni mmoja wa wanaolalamika, ni miongoni mwa hayo yaliyokataliwa,…?’ akaulizwa


‘Mhh…hapana,….’akasema

‘Kwanini….?’ Nikauliza


‘Halikuwa la muda mrefu….’akasema


‘Je wewe kuwepo kwa deni hilo, kuombwa hadi kutolewa, ulilisimamia wewe huo mchakato…?’ akaulizwa, hapo akajifanya kama anafikiria, halafu akasema;


‘Kitengo ndicho kililisimamia…’akasema


‘Wewe si ndio ulikuwa bosi wa hicho kitengo kwa muda huo, au sio…?’ akaulizwa


‘Ndio nilikuwa, lakini niliondoka na mambo yaliendelea au sio…’akasema


‘Kwahiyo unakumbuka hilo deni, kuwa ni wewe ulilipitisha…?’ akaulizwa


‘Naweza nikakumbuka hivyo, sawa, japokuwa nilisimamia madeni mengi tu,.., mhh, unasema lilikuwa la nani, eeh, …sina uhakika, …utanisamehe kwa hilo..’akasema


‘Hahaha,…usijifanye hukumbuki bwana madogo, nafsi inakusuta ,…adui yako mkubwa ambaye ndiye aliyekufanya uhamie hicho kitendo, umusahau,…nakukumbusha, tu…je umelikumbuka hilo deni, ..?’ nikamuuliza.


‘Unajua usiwe unazunguka ungelisema mapema tu, ningekujibu..maana huko unapokwenda, napajua sana, na nilijua lengo lako ni hilo…ni sawa, hilo deni lilitolewa nikiwepo,…na mimi nilipitisha kwa sahihi yangu, nakubalia hilo na ni…baada ya kuhakiki kuwa lina vogezo vyote vinavyohitajika…’akasema.


Pale nikasogea nakuchukua makaratasi,..nikasogea mbele yake…na kumuonyesha.


‘Unazikumbuka hizo nyaraka…’nikamuonyesha, na hapo akatoa macho kama kuigiza kushangaa,..halafu akacheka,..


‘Umezipata sio…hahaha, wewe kweli kiboko, hahaha…’akacheka.


‘Hizi ni stakabadhi halisi zinayoonyesha deni hilo lilivyotolewa,..je stakabadahi hizi, au payment vocha hizi unazikumbuka vyema…?’ nikamuuliza


‘Zipo nyingi sana za namna hiyo….sasa ukiniambia hiyo naikumbuka siwezi kukudanganya, kuwa naikumbuka na ni kweli, au sio, yawezekana isiwe yenyewe, ila zinafanana…’akasema.


‘Hii ni ushahidi uliotoka benki, inasadikiwa hivi vyote niliteketea kwa moto,…’nikasema


‘Sio kweli…’akasema


‘Cha ajabu hizi nyaraka bado zipo hadi leo, ina maana alitokea malaika,akaja kuziokoa, …au niseme nini, mtu akaja kuziokoa, akazihifadhi…’nikasema.



‘Hahaha…utasema upendavyo,…wewe ndio utasema ulizipata wapi, …je nikisema si zitambui utasemaje…?’ akauliza.


‘Najua hutasema hivyo, wewe sio muongo kiasi hicho..na kwanini useme hivyo, wakati kila kitu kipo wazi,…au unataka tuhakiki hilo…?’ nikauliza



‘Haina haja uliza swali lako…’akasema


‘Hizi ni kumbukumbu za benki, zenyewe hazikuwahi kuungua, na mkakati wa ‘moto’ au sio..unaujua sana huo mkakati,  ulitaka baadae hizi zote ziteketee, lakini kwa uweze wa mungu, zikabakia hadi hii leo…’nikasema


‘Sawa…’akasema hivyo tu.

‘Sasa katika kupitia pitia hizi kumbukumbu,....unaiona hii, ni vocha, ya benki kwenda kwa mlengwa,..na hapa kuna sahihi yako, wewe uliyethibitisha kuwa mkopo huo umakamilika, hauna shaka, utolewe…,…’nikasema na akawa anaangalia kama kuhakiki.


‘Najua unajiuliza hivi vitu vimepatikanaje, na yule uliyemtuma akamalizie hiyo kazi , kwanini hakuimalizia, ..mmh, ulichelewa,.kufuatilia hili, au sio….sasa swali langu ni hili, ,…nauliza, je aliyeomba huu mkopo ni nani…?’ nikauliza


‘Kwani jina halionekani hapo eeh,…’akasema


‘Nataka uhakika wako..kauli yako…’nikasema


‘Itakuwa hivyo, ndio yeye, huyi aliyeandikwa jina lake hapo juu, …’akasema


‘Ndio yeye,  aliyekuja kwako , akaomba huo mkopo, ukapitisha, na yeye akaja kuweka sahihi yake hapa, kuwa kaupokea huo mkopo, sawa si sawa…?’ nikamuuliza


‘Sikiliza…’akasema

‘Tumeshakusikiliza sana, sasa tunahitajia ukweli wako…kama kweli nia yako ni kutubu, na kulimaliza hili jambo, jibu kwa ukweli wako..hii hapa ni kumbukumbu halali ya banki ambayo ilikuwa inatumika, kipindi hicho, kweli si kweli…?’ akaulizwa


‘Ni kweli…’akasema


‘Sasa hivi kumbukumbu kama hizo hazitumiki tena, ukiangalia, nembo, ukiangalia maelezo, ya kipindi kile sio sawa na kipindi hiki..kweli si kweli…?’ akaulizwa hapo akasita kidogo

‘Mhh…sijakuelewa hapo…’akasema

‘Wewe una akili sana, hilo sio jambo la kufafanuliwa,…kiri kuwa hapo  mlilofanya  kosa, mlilisahau  hilo…’nikasema na hapo akachukua ile karatasi na kuiangalia kwa makini


‘Mimi siwezi kujua hayo, na naweza kuikana hii kumbukumbu pia, naweza, umeitoa wapi,…sijui kuhusu hilo…’akasema na hakimu akawa anamuangalia kwa uso wa kujiuliza.


‘Wewe si una akili sana, kwanini usilitambue hilo…mmmh, na pia i wewe ulikuwa mtu wa mitandao, ulishindwaje kuibadili hii nembo, si wewe awali ulikuwa unaifanya hiyo kazi, eeh,…ukashindwa kitu kidogo kama hiki, ooh, umeniangusha rafiki yangu..’nikamwambia , halafu kwa sauti ndogo, nikamwambia.


‘Umeliona kosa lako eeh..huchomoki hapo…’nikamwambia na kucheka, na akakunja uso,..lakini baadae akatabasamu, lakini hakusema neno.


‘Wewe ulichukua karatasi mpya, ukajaza tarehe za nyuma, ukasahau kuwa tarehe za nyuma walikuwa wakitumia nembo nyingine si ndio hivyo…, na nembo hizo ni za kificho hata kama ungebadili kwa hapa juu, bado nembo ya kificho ipo, itaonekana, au sio,…kumbuka mchakato w kubadili nembo…na wewe ulikuwepo kwa masilahi ya benki…’nikamwambia na jamaa akatabasamu tu.


‘Ndugu yangu, ..kubali tu kosaaah, hata kama wewe una akili sana lakini ndege mjanja hunaswa kwenye nini…hahaha..’nikacheka jamaa kimia


‘Kabla hujakiri, na ..kama muungwana, ukajisalimisha, kuna jambo jingine, la kukusaidia ili uone kuwa sasa, mchezo wako kwishinie, unatakiwa ukiri kosa, na utubu dhambi zako, na mama yako huko alipo afurahi…’nikamwambia, halafu nikageuka kumuangalia hakimu.


‘Ndugu muheshimiwa hakimu, hili ilikuwa  shida kulitambua hili, ikizingatiwa hapa tunazungumzia benki ambao wana taratibu nyeti, kuna maswala ya sahihi , kuna dole gumba vyote hivyo vinamgusa mlengwa,..utawezaje kufanya jambo kubwa kama hilo kwa mtu mwingine eeh…’nikasema


‘Ni kweli….kila mjanja ana mbinu zake, lakini tunasahau kuwa yupo mwenye uwezo kuliko sisi, ambaye ndiye muumba wetu, yeye, hachoki kuwasaidia waja wake,..kwa uwezo wake tukaja kugundua ujanja huo, lakini  sio sisi, ni kwa uwezi wa mwenyezimungu…’nikasema. Na kumgeukia huo shahidi.


‘Shahidi…umeziona hizi kumbukumbu hapa, mtu akichukua pesa anaweka sahihi yake hapa, si ndio hivyo, na sahihi ni kitu nyeti sana, kweli si kweli ,..awali,..labda mimi sijui,  dole gumba mlilitumia kwa mtu ambaye hawezi kuweka sahihi yake, au sio…?’ nikamuuliza, hapo akacheka kwa dharau kidogo, halafu akasema;


‘Sio kweli…kwa mkopo mkubwa ni lazima aweke sahihi, na mtu yoyote akichukua mkopo, au kufungua akaunti, dole gumba ni muhimu, sasa sijui hiyo hoja wewe umeitoa benki gani…’akasema


‘Sawa sawa kabisa…sasa angalia..hii kumbukumbu hapa, inaonyesha sahihi, si ndio hivyo, na hapa ni sehemu ya dole gumba , sawa…kwanza nikuulize..hii sahihi ni ya nani…?’ nikamuuliza, akaiangalia, halafu akasema ;


‘Ni ya marehemu…’akasema na baadae akashtuka


‘Hebu…’akasema na mimi nikamuangalia wakili ambaye alicheka kwa nguvu.


‘Umeshachelewa mdogo wangu, ujanja mwingi unafanya nini…hahaha…’nikasema


‘Nimechelewa nini hapo…’akasema


‘Umesema hii sahihi ni ya  nani…?’ nikamuuliza


‘Nahisi ni ya marehemu…’akasema


‘Sasa UNAHISI, awali, ulisemaje tena kwa kujiamini,… kwa hivi sasa kwa vile umegundua kosa lako, unasema unahisi… ulishachelewa bwana mdogo, tulichotaka tumekipata kwa hoja hii, au unasemaje…?’ nikamuuliza


‘Kwani hizi kumbukumbu hapa juu zimeandikwa jina la nani,…kwa vile hizo kumbukumbu, ni za mwenye jina hapa juu, kwahiyo moja kwa moja, sahihi itakuwa ni yake,..ndio maana nikajibu kwa haraka hivyo..’akasema


‘Sio kwa vile sahihi hii uliikariri, na uliweza kuirudia bila kukosea angalia hapa pembeni, hii sahihi ni kama mtu alikuwa akiijaribu hapa… tatizo ulijaribia hapa hapa kwenye hii karatasi…ungejaribia kwenye karatasi nyingine bwana…’nikasema na hapo akashtuka na kusema


‘Sio kweli, hata kama naifahamu hiyo sahihi…, naweza kuiweka kama hivyo, na naweza kuangalia sahihi yako, kama haina ugumu, nikaiweka kama ilivyo,…lakini sio mimi niliyeweka sahihi hiyo,..na sina mtindo huo, wa kuweka sahihi za watu… hizo ni shutuma zako na sikubaliani na hiyo shutuma…’akasema


‘Nilikuuliza swali awali..je ni kweli aliyeomba huo mkopo, nikiwa na maana marehemu, ndiye aliyekuja kujaza hii fomu, na akaja kuweka sahihi yake yeye mwenyewe, kuwa anachukua hilo deni, ulisita kujibu hilo swali, je sasa waweza kulijibu hilo swali…’nikaona kama anataka kuongea lakini akaghairi


‘Maana haya yote kujaza fomu ya mikopo, kuja kuweka sahihi kuwa mkopo umekubaliwa na pesa hiyo inawekwa kwenye akaunti ya huyo mteja, yote yalikuwa  yakifanyika ndani ya kitengo chako, mbele ya usimamizi wako, unalikumbuka hilo..na kulikuwa na kamera juu…usisahau hilo kamera huwezi kuzitia moto….’nikamwambia hapo akashtuka

‘Hahaah, kulikuwa hakuna kamera kipindi hicho hpo kitengoni…’akasema

‘Una uhakika gani…kwa vile wewe ndio ulikuwa IT au sio, ulihakikisha hilo halipo au… au….hahaha, ilikuwepo lakini wewe ulikuwa hujui hilo…’nikasema na hapo akaonyesha uso wa kushangaa, halafu akasema

‘Sio kweli….’akasema hivyo


‘Na kipindi kile mlihakikisha anayechukua mkopo anaingia kabisa kwenye ofisi yenu na kuweka sahihi, ili umuone kuwa ni nani……je ni kweli marehemu alifika mbele yako, akaweka sahihi yake…?’ nikamuuliza


Jamaa akabakia kimia


‘Ndugu yangu, kubali tu yaishe…’nikasema

Jamaa akatabasamu,…halafu akaanza kucheka…ghafla akanyamaza, …halafui akaniangalia akiwa kanitolea macho….macho..ya kutisha, huku anahema, .. akasema;


‘Naona unahisi umeshinda, si ndio hivyo....lakini bado hujashinda,…..’akahema kwa nguvu, halafu akawageukia watu, akasema


‘Mimi sijafanya kosa….., nitasema hivyo hadi kesho, hata kama mahakama hii ikiamua vinginevyo….’halafu akanigeukia, na kuanza kuongea…

‘Ukweli…si unataka ukweli….’akasema

NB: Sehemu hii inaendelea


WAZO LA LEO: Ukweli haujifichi, ukweli haupingiki, hata kama wanafiki wataugeuzageuza, lakini ukweli kama ulivyo mwanga, utaonekana hata kama kuna giza nene..
Ni mimi: emu-three

No comments :