‘ Ndugu muheshimiwa hakimu, naomba msichoke maelezo
yangu, maana bila kuyaelezea haya, ukweli halisi hautaweza kueleweka, na tatizo
linaweza lisimalizike, na haki isitendeke, mimi nataka tatizo hili limalizike
kabisa, ili nami niweze kupumzika kwa amani…’akasema.
‘Kama ni jela,..au kuwa huru, au…kaburini…yote
yawezekana au sio kama kweli mtahuku kwa haki …’akaongezea hivyo.
‘Najua yaliyotokea yamewaumiza wengi, ..lakini
tunasahau, kuwa kuna waliokwisha kumia zaidi yao…, mara nyingi tunajali
waliopo, ina maana ambao hawapo hawana haki au sio, asiyekuwepo na lake
halipo…najiuliza tu,..je kama haki haikutendeka, kwa hao ambao hawapo
duniani,…ndio basi tena…ila ni lazima hili liishe maana wengine tunasumbuliwa
na ndoto, tunasumbuliwa na kumbukumbu za nyuma…’akatulia.
‘Kabla sijaingia kwenye kujibu swali lenu la msingi,
japokuwa nimeshaanza kulijibu kwa wenye kufikiri,..kuwa hilo deni ni la nani
hasa.. ….’akageuka kumuangalia wakili wa benki, halafu akageuka kuangalia kule
alipokuwa ameelekea,…
‘Najua nyote mna haraka…mnataka nisema tu, hilo deni
ni la marahemu au sio au ni langu, au ni la mtu fulani, au sio….lakini kwanini
nisema jibu tu, bila kuelezea ukweli wa hilo jibu..sasa naanza hivi…’akainama
kidogo.
‘Lazima niwarejeshe huko …deni lilipoanzia, au
sio…kwangu mimi deni hili lilianzia siku ile nilipopokea ile zawadi, ..maana ndipo mambo
yalianzia…siku nilipojitambua, na kuoenekana
sina thamani mbele ya jamii..lakini thamani yangu ilikuwepo, na kihalali
kabisa..lakini ungelisemaje…eeh, mtoto wa jalalani kama mimi…’akageuka
kumuangalia halimi.
‘Ni lazima nieleze kila kitu, tafadhali mnipe muda wa
kutosha…’akaendelea kusema
Tuendelee na kisa chetu…
*******
Siku.moja aliniita
mama mlezi, kipindi hicho ndio alizidiwa sana, kwani naye alikuwa anaumwa,
magonjwa yale yale yaliyomuondoa mama yangu duniani, japokuwa yeye,
hayakutokana na kupigwa, yeye yalianza tu, japokuwa kihistoria yawezekana ni
kutokana na dhahama za dunia, hilo sitalielezea maana sina ushahidi nalo.
‘Ila nina imani hiyo,
waliosababisha yote hayo…na wao wataishia huko huko…mimi sijui, lakini nahisi
hivyo, …
‘Mimi naweza kusema
tu, yeye alipatwa na maradhi hayo kutokana
na majawaliwa ya mungu…kiukweli alikuwa anaumwa haswa,…alivyoniita ,
nikajua labda, anataka kuniagiza kitu….’akatulia
‘Naomba tuwe na
subira…’akasema pale alipoona wakili wa benki akitaka kumkatiza. Na hakim naye
akamuashiria huyo wakili atulie kwanza…
'Mama unasemaje, vipi
wajisikiaje …’nikamuuliza.
'Mwanangu mimi ninakupenda
sana,..’ akaanza kusema hivyo, sikuona ajabu maana kauli hiyo sio mara ya
kwanza kuisikia kutoka kwake,..ila moyoni nikahisi kuna jambo…akili yangu
huhisi vitu kiajabu sana.
‘Mwanagu, bahati mbaya
mimi sikujaliwa kupata mtoto, na
ikatokea bahati nzuri kukupata wewe…, namshukuru sana marehemu mama yako kwa kuniachia wewe ,
uwe mwanangu....'akasema…na mimi wakati huo nimekaa karibu yake kwenye kitanda
Pale nilipokaa kitandani, nikahisi machozi
kama machozi yanataka kunitoka, maana nilimpenda sana huyo mama, alinilea kama mtoto wake, na kwa
vile sikuwahi kupata malezi yangu mama
mzazi, naweza kusema,…huyo mama alinilea huenda zaidi ya angelifanya hivyo mama
yangu,..sijui kama nakosea, mnisamehe tu…’akatulia
'Ndio mama, utapona
tu, na nimeshapata kazi, japokuwa sio nzuri sana, lakini nitajitahidi utibiwe …’nikasema.
‘Mimi niliambia
usiache shule usome maana kusoma ndio maisha yako ya baadae, unafikiri utapata
pesa gani ya kunitibia mimi…hutaweza, na hakuna dawa tena ya ugonjwa
wangu…’akasema.
Aliposema hivyo,
machozi yakaanza kukubujika, siku alinikatisha tamaa, kiukweli pamoja na
mengine mengi, mama huyo ametaabika sana kutokana na hayo maradhi, ilifikia
mahali hawezi hata kutoka nje, jamaa zake wamemuacha tu,
hawaonekani…walijitahidi awali baadae wakachoka. Nikawa nahangaika naye, ndio
maana yangu nitafanya nini…
'Mwanangu wala
usisumbuke, najua sitapona, na bora nijifie tu, kuliko kuendelea na mateso haya,
na nimemuomba mungu anijalia nife, ili nisiendelee kukutesa wewe zaidi…’akasema.
Hapo mimi nilihisi
mwili ukiniisha nguvu, lakini nilijipa
ujasiri wa kiume. Nikijua ni maneno ya kukata tamaa, ila nikipata pesa ni
lazima nimfikishe hata nchi za nje akatibiwe…angalau niweze kulipa fadhila,
japo kidogo.
'Sikiliza mwanangu,
nilishawahi kukuambia kuwa mimi sio mama
yako wa kukuzaa, na hata kuendelea kukulea wewe, wengi hawakupenda, waliona
kuwa nahangaika na mtoto baki, wakati watoto wa ndugu wapo wengi tu, wakati
mimi mwenyewe nidhofuli hali, sina mbele wala nyuma ila nina utajiri, nyumba,
maeneo niliyowahi kukuonyesha yote ni mali, na yatakuwa mali yako, unakumbuka
mipaka vyema , si ndio hivyo…’akasema.
‘Ndio nakumbuka sana….’nikasema
nikikumbuka maeneo ambayo mama huyo alipenda kunionyesha na mipaka yake, lakini
kipindi hicho sikutilia maanani kivile, niliona tu,…kama mama anamuonyesha
mwanae tu..najua muda wote tutakuwa naye.
‘Na hii ndio sababu
ndugu zangu wengine hawataki hata kuja kunisaidia, eti nabeba mizigo isyo yangu,
eti nataka kumpa urithi mtu asiye damu yangu, ila nasema mali yangu yote hata
nikifa leo, ni ya kwako… na kumbuka jambo moja, nilikuwa hivi mimi…siwezi
kukuacha mwanangu, niliapa mbele ya mama yako kuwa nitakulea hadi pumzi yangu
ya mwisho, na wewe ndiye mwanagu, nimpe nani mali yangu eeh, niliwaelezea hata
ndugu zangu, ndio maana wakaamua kunitelekeza…’akasema
'Mama najua sana hilo,
unanipenda sana, mimi sitak mali, na kama mali ipo kwanini mama tusiiuze ili
utibiwe tu… maana juhudu zangu zote ni ili na mimi niweze kulipa fadhila zako,
japokuwa sitaweza, lakini nitajitahidi kadri ya uwezo wangu kila mshahara
nitakao pata itakuwa kwa ajili yako…’nikasema.
‘Ahsante sana
mwanangu, mola akuzidishie moyo huo..ila wakati umefika,..siwezi kukudanganya
tena…muhimu ni wewe kupambana na maisha, najua nikiondoka hapa duniani, utakuwa
peke yako, ila hutakuwa masikini…’akasema, na mimi muda huo sikuwa na mawazo ya
mali yake kabisa, ..ningelikuwa na wazo hilo ningelifanya jambo la kuja kunisaidia
baadae, niwe na kumbukumbu za kisheria..
‘Mama, huwezi kuondoka
ukaniacha…’nikasema
'Sawa,..basi tutakufa
wote…’akasema kiutani, huku akijaribu
kucheka.
‘Hapana Mama
hutakufa..nitakupigania, utaenda kutibiwa India…’nikasema kwa kujiamini.
‘Hahaha india,
wanaweza kutibu kifo au….Sikiliza mwanangu, maradhi haya yalianza
zamani…kipindi napambana na ndugu zangu, kuhusu maeneo aliyoniachia mama, mimi
nilizaliwa peke yangu kutoka tumbo la mama yangu, lakini tupo wengi kwenye
familia ya baba, maana baba aliona wake wengi tu..lakini hayo hayakuhusu.
Ila la muhimu ni
ujumbe kutoka kwa marehemu mama yako,… koho, kohooo…’akasema akikohoa kwa
shida.
‘Nakumbuka siku moja, niliwahi kukuambia kuna zawadi aliniachia mama
yako, na nikakuambia ukifanya vizuri kwenye masomo yako, ukapata kazi, ndio
nitakupatia hiyo zawadi,..unakumbuka hilo…’akasema
‘Zawadi, ndio..lakini
hukuwahi kunipatia..japokuwa nilifaulu vizuri masomo yangu, sema tu, nimekatiza
kusoma ili niweze kutafuta kazi, ili nipate pesa ukatibiwe, kwani ilikuwa ni
zawadi gani…?’ nikauliza
‘Ni zawadi maalumu
kwako…ila yenye masharti….’akasema na mimi hapo akilini niliwaza zawadi hiyo ni
ya maelekezo tu, ndivyo akili ilinituma, lakini kwa kauli hiyo ya mama,
nikahisi kuna zaidi ya hivyo ninavyowaza…
‘Mama yako alisema
nije kukupatia hiyo zawadi, wakati muafaka ukifika…lakini naogopa kwa jinsi
alivyoniambia, sizani kama muda huo utafika,…na pia…kohokohoookh….ooh, mungu
nisaidie tu, nitimize haya…’alasema hivyo akionekana kuchoka.…’akatulia.
‘Mama, naona hali yako
sio nzuri, wewe lala utulia, mimi sitamani zawadi yoyote, wewe ndiye zawadi
muhimu kutoka kwa mama yangu, bila yaw ewe maisha yangu yangelikuwaje,…, achana
nayo, muhimu ni wewe mama yangu..’nikasema
‘Sikiliza, ahadi ni
deni, ogopa ahadi uliyoitamka mbele ya marehemu akiwa hai, kuwa kifa ufanye
kadha wa kadhaa..…, zawadi hiyo mama yako alisema nije kukupatia, ukiwa tayari
na maisha yako.., ili isije ikawa sababu ya kushindwa kuendelea na maisha
mengine …maana ya hiyo kauli mimi siijui..ila
alisema hivyo tu…’akasema
'Oh..ni zawadi ya
namna gani mama...?’ nikauliza ili mama asiendelee kuteseka.
'Siku ile mama yako
kazidiwa, akiwa ndio keshajua kuwa hataishi tena, kama ilivyo kwangu mimi,….aliniomba
nikamnunulie karatsi zile za zawadi, akaniambia nimsaidie kuifunga mbele yake,
zawadi hiyo iliweka kwenye bahasha kubwa kwahiyo siku ilikuwa ni kitu gani…
Akasema sasa nifunge
na ile karatasi ya zawadi, akihakikisha
hiyo zawadi imefungwa vyema kama alivyotaka yeye,…nikafanya hivyo, kwahiyo kilichomo
humo…hata sijui ni kitu gani…’akasema
‘Oh, mama, utapokeaje
zawadi hata hujui kuna nini..ndani yake, wewe ungefungua na kuangalia, najua
mama yangu hawezi kunipatia kitu kibaya, lakini wewe ndiye mama yangu mlezi
ulitakiwa ujue kilichomo au sio…’nikasema.
‘Sawa nakuelewa,
lakini hujui kwanini mama yako alifanya hivyo,..huenda aliogopa fitina, huenda
aliogopa, nikifungua, na kuona kilichopo, tamaa itanishika nishindwe kukupatia,
kila mtu ana mawazo yake, na ibilisi ana nguvu sana, sasa mimi sikutaka
kukupatia hiyo zawadi mapema, bado nilikuwa na mashaka kuwa hujatulia, kimaisha…’akasema.
'Mhh, haya mama niambe
ni zawadi gani hiyo, nisikuchoshe, watakiwa kupumzika…’nikasema
Basi, Mama akainua godoro, akatoa mfuko wa
rambo, ndani yake akatoa bobksi lililofungwa kizawadi, akaniambia, …
'Hii ndio zawadi yenyewe…na aliniambia huo ndio urithi
wake ambao alijaliwa kuuweka kwa ajili yako…’akasema.
Nikaipokea ile zawadi,
kwa kusita sita…akili yangu husoma hisia za watu, lakini hizia za nani hapo,
maana hata huyo mtoaji zawadi hajui kilichomo,…nikaipokea na kutaak
kuifungua..yeye akasema…
‘Aaah, kama alifanya
hivyo nisijue kilichomo ndani yake basi chukua muda, ukiwa umepumzika ndani,
peke yako, ndio ufungue hiyo zawadi, hakikisha umejiandaa vyema, usichukulie
mzaha…’akasema.
‘Lakini mama mbona
yaonekana kama ni …aah, hata sijui ni nini...’nikasema nikimtafsiri huyo mama
anavyowaza, kama ni maagizo ya jambo fulani muhimu, ambalo mama alipenda
nilijua, kama ni mali ipo wapi, au…hapo sikuweza kutafsiri zaidi, moyoni kwa muda huo nilitaka nikitoka hapo
nikafanya hata harambee huyu mama yangu akatibiwe, nishapanga mikakati yangu
kichwani.
'Hiyo ndio zawadi na
urithi aliyoniachia mama yako, kwa masharti, usije kufanya kufukuru nayo…alirudia
sana kauli hiyo, kuwa ‘usije kufanya kufuru nayo, usije kukengeuka ukafanya
mabaya, usije ukachukulia vibaya, uwe muadilifu na usimamie kwenye haki …sasa
sijui kwanini alisema maneno hayo…’akatulia.
'Mhh, kufuru...ni …na
ni mabaya gani nitafanya mimi, mama wewe umenifindisha niwe mwema kwa
watu..ndivyo nitakavyo hivyo…mimi nahisi kwa hali ya mama aliyokuwa nayo,
aligundua jambo, ..akashindwa kulifanya, au sio…sasa anataka mimi mwanae
nilifanye,..au ..kitu gani kinaweza kukaa kwenye hilo boksi mapaka nije kufanya
kufuru…’nikasema.
'Wewe utakuja kujionea
mwenyewe, sasa ni zawadi yako na mimi nimetimiza wajibu wangu japokuwa
nilivyoona mimi, wakati wake ulikuwa bado, lakini nitafanyaje..na siwezi
kumpatia mtu mwingine ili aje kukupatia ukishafikia mahali kama alivyotaka mama
yako..zaidi ya hapo mimi sijui……….’akasema akihema kama kweli katua mzigo.
'Ok. Sawa mama mimi
nitafanya kama ulivyoniagiza,…sasa mama nikakununulie nini…?’ nikamuuliza.
‘Kaninunuli chochote
laini kinachoweza kupita kooni…’akasema mama, maana hata kula kipindi hicho,
ilikuwa ni shida, na ninashangaa siku hiyo aliweza kuongea vizuri.
'Sawa mama ngoja
nikaiweke hii zawadi, halafu niende sokoni, nitanunua viazi mbatata, nikupigie
kama uji,..na nyama, si utapenda …?’ nikasema na yeye akatabasamu na kuonekana
kama analala..
Basi nikachukua ile
zawaidi, nikaihifadhi kwenye vitu vyangu muhimu,..bila kuifungua, na cha ajabu
sasa…, nikawa nimesahau kabisa kuhus hiyo zawadi maana wakati huo mawazo yangu
yapo kwa jinsi gani nitamsaidia huyu mama apone…na kiukweli mtu akinipatia
maagizo , hasa watu wakubwa, huwa sina kawaida ya kusahau , lakini hilo
nilipitiwa…’akasema.
Haikupita wiki mama yangu mlezi akafariki,…’hapo akatulia
kwa muda ikawa kama vile hataongea tena…
‘Vipi …’akasema hivyo
hakim.
‘Naombeleza
muheshimiwa hakimu, samahani sana…ni tukio ambalo sitaweza kulisahau..
‘Sawa… siku ya mazishi
sasa…ndio mambo yakanza, kwanza siku ile ile ya kuzika, tumeshamaliza, nipo
kwenye kaburi la mama mlezi, nalia, mtu akaja nyuma yangu akanishika bega.
Nikageuka,..alikuwa
mzee mmoja hivi kashika barua, akasema;
‘Haya ..hii ndio barua
yako…’akasema hivyo tu, na kunikabidhi mkononi, nikaishika sikupenda kuisoma,
huyo mzee alipoona hivyo akasema;
‘Isome kwanza…kabla
sijaondoka…’akasema
Wakati nataka kuisoma,
kumbukumbu za nyuma zikanijia, kumuhusu huyu mzee,..huyu mzee, kipindi fulani
alikuwa akifika kwa mama, na hawaishi kugombana, na nikimuuliza mama kwani huyo
mzee akifika wanasihia kugombana, mama akasema, hayo nisiyaingilie, kwani
hayanihusu…kwahiyo mimi kama mimi sikutaka kufuatilia zaidi.
Leo huyu mzee ndiye
ananipatia hiyo barua..
Hiyo barua nilitakiwa
niisome pale pale…
'Mwanangu, kwaheri,
najua nitakufa...nilitamani nikulee, nilitamani wewe uje kuwa ni jembe langu..nilitamani
unizalie wajukuu, waje kunisumbua, ili nijue usumbufu wa watoto ..
Lakini, sikuumbwa
kuyaona hayo, sikuumbwa kuja kuipata raha ya dunia, maisha yangu kwa ujumla
yamekuwa ni mateso, tokea siku ulipoingia tumboni kwangu …’Nilipofika hapo ndio
nikajua hiyo barua ilitoka wapi..sio ya kutoka kwa mama mlezi.
‘Ni kwanini, maisha
yangu yalikuwa hivyo.....jibu lipo kwenye zawadi atakayokupatia mama niliyempa
jukumu la kukulea, najua atakuja kukupatia, hiyo zawadi muhimu katika maisha
yako,…na baada ya hapo, utaona kila kitu,, utasikia kila kitu, utajua kila kitu…
Na kwa hali hiyo wewe…utajua
ni nini cha kufanya..maana hapo ..sijaficha kitu chochote, …mungu ni shahidi
yangu,..huenda hiyo ikawa ni sababu nyingine ya maisha yako ya baadae..zaidi na
hayo niliomba mungu akupatie.kitu ambacho kitakusaidia, katika maisha yako iwe
karama kwako,..sasa hilo mimi sijui mungu atakupatia karama gani.
Kwaheri mwangu siwezi
tena kuandika zaidi..
Hebu firikia hali kama
hiyo, wewe kama mimi ungelijisikiaje…nilihis ni misiba miwili ipo mbele yangu..
Naona hata herufi za
jina lake hakuweza kuandikwa vyema….mwisho wa hiyo barua, nikamaliza kuisoma na
huyo mzee akasema
‘Sasa huo ndio
ushahidi kuwa wewe ni nani..unasikia, …kabla hatujaanza kuingie kwenye mambo ya
mirathi, ..unanielewa lakini…’akasema huyo mzee , mimi pale sikumuelewa,
nikasema.
‘Sawa mzee ahsante..’nikasema
hivyo, na yeye akageuka kuondoka zake nikabakia mwenye makaburini, nikilia na
kuombeleza…
**********
Kiukweli hapo mimi nilijiona
kama nina msiba juu ya msiba nilijiuliza sana, kwanini mama aliniandikia hayo,
na kwanini …mama mlezi naye kafariki, na kuna nini mbeel ya haya yote.., hapo
ndio nikaingiwa na hamasa ya kwenda kuifungua ile zawadi…aliyoniachia mama
mlezi, lakini sikupata muda huo…
Baada ya mazishi,
ikawa ni kikao cha familia, …
‘Wewe kijana…hatutaki
kukufukuza, wewe utendelea kuishi kwenye hii nyumba lakini utaishi hapo kama
mpangaji, ..’kauli ya huyo mzee aliyenipa hiyo barua, ikasema na kuniacha
kwenye mshangao, maana mimi nilijua yeye ndiye atakuwa msemaji wangu mkuu,
kwani yeye ndiye aliyeambiwa yote na mama mlezi.
‘Lakini babu…nilizoea
kumuita hivyo..’babu’ , japokuwa kumbe ni ndugu mkubwa kwa mama yangu.. na
hakupenda kabisa mimi nimuite hivyo.
‘Unapenda sana kuniita
babu, kwa dharau sio, mimi sio babu yako,..na ukome kuniita babu,… wala hatuna udugu
na wewe, babu , babu, nenda kamuite babu yako hivyo, kama unaye…’akasema kwa
hasira.
‘Samahani
mjomba…nilitaka kusema tu, mama aliniambia hapa ndio kwangu hata akiondoka
duniani..nyumba na mali..yaani maeneo yote ni mali yangu..’nikasema
‘Hahaha, nilijua tu,
unajua wewe umetokea wapi…sisi tulikosana na ndugu yetu huyu kwasababu yako, na
nilijua ipo siku itafika, na ..haya yatafanyika, wewe huna damu na hii familia
kabisa na wala hatujui wewe baba yako ni nani..kwahiyo wewe huwezi kurithi
chochote, kwenye hii familia,.. unasikia, nenda kaulize, au hata kushitaki,
hili eneo, na h ii nyumba ni mali ya familia husika, unasikia..’akasema.
Kiukweli mimi sikutaka
kugombea chochote maana kweli mimi sio mwanafamilia hiyo, nilelewa tu hapo,
moyoni nikasema, msiba ukiisha naenda kutafuta nyumba ya kupanga,..ila watu
sasa, . watu waliojua hayo, hawakuniacha nifanye hivyo…
Watu wakanishawishi
nifungue kesi…ilikwenda nikafanya hivyo, …hahaha, kesi ilinibwaga kama
sijulikani,..sina ushahidi wa maandishi, sina hata ndugu mmoja au jamaa
aliyesimama upande wangu,… na mmoja wa mashahidi aliyekuwa upande wa mzee…pamoja
na ndugu wengine, ni huyo mwenye hiyo nyumba nzuri, inayotaka kupigwa
mnada...
..
‘Huyo jamaa alikuwepo
kipindi hicho cha kesi, sijui wanajuanaje na huyo mzee, na akaongea mengi
ambayo, …ooh, yalinifanya nisiwe na hamu ya kudai tena…’akasema
Sasa baada ya hapo
eneo hilo likauzwa, na aliyeuziwa sasa…ndio huyo aliyenga hilo jumba la
kifahari, nakumbuka siku kabla nilifika na kutaka kuongea naye, huyo aliyeuziwa, ,,kipindi hicho nyumba
niliyokuwa naishi na mama bado ipo, ila mimi mwenyewe sikupenda kuishi hapo
tena, ila vitu vyangu bado vilikuwepo humo ndani,…
Huyo jamaa alinicheka
sana,..kwa dharau..
‘Wewe mtoto kupata
bahati yakulelewa na wanajami wenye huruma ndio umeona mali ni yakko,..kijana
nakushauri jambo moja muhimu kwenye maisha yako…, soma, jitahidi,usome ili upate
kazi, na bidii yako ndio itakusaidia, utafute mali yako ya halali.., usiwe na
tamaa na mali za watu wengine unasikia,…’akaniambia
‘Lakini mimi nilitaka
tu nikueleze ukweli alivyosema mama mlezi, wewe umenunua eneo la dhuluma, sio
vizuri hivyo…’nikasema.
‘Dhuluma unaijua wewe,
na mimi sina makosa, maana eneo hili nimenunua kihalali, kama kuna tatizo
kamuulize mzee mtupe, au nenda mahakamani, kwani mahakama wamekosea, wewe
kiukweli huna haki na mali hiyo kabisa…’akasema hivyo
‘Oh, haya bwana,
..lakini sijamalizana na nyie, ipo siku tu…’nikasema
‘Hahaha, sawa kama unahisi
nimefanyiwa vibaya, kwanini usiende tena mahakamani, haki yako utaipata lakini
sasa utaipata wapi, labda ukaongee na huyo mzee aliyeniuzia eneo hili, akupatie
eneo jingine lakini sio hapa, hapa nilipapenda sana, pamekaa kiulaya ulaya..ndio
maana nimepanunua kwa bei mbaya sana…, na hapa nitakuja kujenga hekalu langu,
hata kama pangelikuwa ni pa kwako ningepanunua kwa bei unayoitaka wewe, …lakini
sasa sio kwako na sio halali yako kabisa, kama nilivyowahi kukushauri nenda
shule, huo mwili usikudanganye, wewe bado mdogo sana…’akasema
‘Ina maana ndio maana
umerubuniwa ili uje kutoa ushahidi wa uwongo..ili uje ujenge hekalu lako hapa…kiukweli
umefanya vibaya sana…’akasema
‘Nimekuambia hivyo,
kama unahisi umedhulumiwa,…nenda mahakamani, mimi sijui, niliongea ninavyojua
mimi…nilivyoambiwa, na kusikia,…sasa mengine siyajui,na kwanini ung’ang’ania,
wewe umezaliwa na huyo mama, .?’ akaniuliza
‘Niende mahakamani ili
iweje, mimi nilijua wewe ni msomo, na unaongea kisomi, lakini usomi wako umeuelekeza
kwenye kufanya mimi nidhulumiwe, ina maana mtu kama mimi sina haki, je kauli ya
marehemu haithaminiwi…na kwa hivi sasa…nitadai nini tena,..mimi mtoto wa
mitaani, majalalani, kama jina langu, yote namuachia mungu..’nikasema
‘Kama marehemu alisema
hayo, ushahidi upo wapi…hakuna , hiyo ni kauli yako tu, ni nani ataamini kauli
yako eeh…hata mimi siwezi kukuamini….’akasema
Kiukweli huyo jama
nilianza kumchukia…moyoni nikaapa kama nitapata nafsi basin a mimi nitakuja
kumuonyesha…
Kipindi hicho alikuwa karudi
mara moja kufuatilia ujenzi wa nyumba yake,…mimi ndio nahangaika nimepata kazi
ya kujishikiza tu, na kazi hiyo nikafukuzwa, maana niliacha kufika bila
taarifa, nikifuatilia hizo mali, na mali nimezikosa..ila ushauri wa huyu jamaa
ukanifanya niingiwe na ari ya kusoma tena, ili nipate elimu nije kupambana
naye,..kiukweli kumri bado nilikuwa mdogo sana.
Nikaanza sasa kusoma
kwa bidiii…ukumbuke mimi nilikuwa na akili ya ziada, kila nilichosoma ikawa
nafanya vizuri, mpaka nikashindwa kujua fani yangu ni nini…
Ukumbuke hadi hapo,
sijaweza kuja kuchukua viti vyangu kwenye ile nyumba na sijakumbuka kuifungua
ile zawadi , ikitokea nikikumbuka, kunatokea tukio fulani la
kunisahaulisha..siku zinakwenda, mwezi, mwaka,…miaka sasa…
Siku moja ndio nikaota
ndoto…moto unawaka, unaunguza kumbukumbu zangu,…unaunguza vitu muhimu sana
kwangu, nikawa nakimbilia kuuzima huo moto, na wakati nakimbia, nikamsikia sauti
ya mama ikisema;
‘Mwanangu, ule moto
umeusababisha wewe mwenyewe…, umeunguza kumbukumbu zote za maisha yako, moto
ukiunguza kitu hakuna kitakachobakia,..moto…ndio unaoweza kuharibu kumbukumbu
zote, unalielewa hilo,..je unakumbuka
nilikuambia nini…’akasema
‘Mama sikumbuki,
lakini nitafanya nini…maana kumbukumbu zangu zote zimepotea..’nikasema
‘Kamuulize mama yao
mlezi atakupatia nyingine, ..na usisahau ujumbe wangu, hapo yaweza kuwa ni
mwanzo tu…moto utawaka sana, usipokuwa makini, …na ukichelewa hutaweza kuuzima,
.utaharibu kumbukumbu zote za maisha yako, na hakuna wa kuja kukusaidia…unasikia,
haya fanya nilivyokuambia...’akasema.
‘Nifanye nini sasa..?’
nikauliza.
‘Wewe ni mjinga sana,
nimekuambia nini,..tumia akili yako vyema,…na kabla ya kuitumia akili yako
vyema ni bora wewe mwenyewe ukajijua , wewe ni nani, hivi kweli unajijua wewe
ni nani, kumbuka jambo moja,…akili yako ndio hazina yako, acha ujinga
wewe..’akasema.
Nakumbuka sana kauli ya mama mlezi, alipenda
kuniambia hivyo, wewe ni mjinga sana tumia akili yako vyema…na kuna siku mama
mlezi akasema, kauli hiyo alizoea kuitumia sana mama yangu mzazi, ukikosea, au
akitaka kukuelekeza jambo fulani,..’wewe acha ujinga, usiwe mjinga, tumia akili
yako…’ lakini hakuweza kuyatamka mane ohayo vyema, kwani hakuweza kuongea vyema…
Asubuhi yake, nikaondoka, kwenda kule kwenye
ile nyumba, nafika nyumba haipo tena, imeshavunjwa, kila kitu kimetupwa tupwa,
moto unawake, kuunguza hayo mabaki ya nyumba, iliyovunjwa na vitu karibu vyote
vimeungua,,kuna nyumba nyingine inaanza kujengwa, kuna mawe yameletwa hapo…haaah…hakuna
kilichobakia, kisa, ili jumba la kifahari liweze kujengwa,
‘Kwanini msingesubiria
nichukue vitu vyangu…’nikauliza
‘Mwenye eneo kasema,
tuvunje, maana humo ndani hakuna cha maana, na tuchome moto kabisa.., maana
kuna kunguni…’nikaambiwa,
Moyoni hasira, chuki,
vikatawala…zawadi ya mama haipo,na wala sijui itakuwa wapi, nikitaka kwenda
kuitafuta siruhusiwi, walinzi wakanizuia na hata kunipiga, hata pale
nilipowaomba wanisaidie kutafuta kama wanaweza kuiona kitu kama hicho,
hawakunisikiliza zaidi ya kunicheka kwa dhihaka.
.
Usiku mmoja nikavizia,
walinzi hawapo ndio nikaenda kuchakura chakura…bahati nikakuta baadhi ya vitu
havijaungua sana, na kuhangaika,..nikaona mfuko wa Rambo, na…nikaufungua, ni
ule ambao uliweka hiyo zawadi, ..lakini sikuweza kuiona kitu kama hicho,
yaonyesha kabisa kuna mtu aliuona, akaitoa hiyo zawadi, ….au ndio imeteketea
kwa moto.
Ni nani huyo…ilinipa
shida sana, na wakati nahangaika mara akatokea mtu kwa nyuma yangu, nikajua ni hao
walinzi, hapo nisubirie kipigo…
‘Unatafuta hiki eeh,…unatafuta
hiki…haya chukua, ….ndio hapo utajijua wewe ni nani na huna haki yoyote na hii
mali, chokoraa mkubwa wewe, mwanaharamu,…mtoto wa jalalani…’akasema huyo mtu na
kunitupia usoni…huku akitamka maneno ya dharau,kwa kadri alivyoweza..
NB: Zawadi ndio hiyo,
je itanisaidia nini, je ilimfanya nini huyo jamaa.., JE inahusiana vipi na hilo
DENI....tutaona kwenye sehemu ijayo…
WAZO LA LEO: Tusipende kutoa ushahidi bila kuufanyia kazi, tukahakiki ,
ukweli wa hicho tunachoombwa kutolea ushahdi, watu wengine huwatumia wenzako
wawe mashahidi ili wanufaike na masilahi yao.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment