Docta akaingia kwenye boda boda, moja kwa moja hadi kwa
Mzee.
Alipofika kwa mzee, akauliza
‘Msaidizi wangu yupo wapi..?’
'Hatujui…’wakasema mke na mume wake
‘Hamjui… kwa vipi,! Kwani
ilikuwaje, akaondoka,.. aliondokaje , ina maana aliondoka bila ya kuaga, au
ilikuwaje,…?’
Tuendelee na kisa chetu...
******************
Docta aliwauliza wana ndoa hao wakionekana kutokuivaana, nahisi ni kutokana na kuchukuliwa kwa binti yao.
Docta hakujali hali ya wanandoa hao, wazee hao, yeye akakimbilia kumuulizia msaidizi wake,.. na aliuliza maswali mengi ya mfululizo, na wakati huo mama mwenye nyumba yeye alishakimbilia chumbani kwake..
Baba mwenye nyumba akawa anaonyesha uso wa
mshango, akiwa haelewi kitu kuhusiana na msaidizi wa docta huyo, na hakuwa na mawazo kabisa ya kuwa huenda kuna tatizo kwa huyo mtu..yeye ndio akasema;
‘Sisi tulikuwa tumetoka
na mke wangu kama ulivyo niagiza kwenye simu, baadae nikarudi ndani, nikamkuta
msaidizi wako kashika mfuko, mifuko hii iliyoandikwa Rambo, na ndani nahisi kulikuwa na
kitu kizito, kwa jinsi alivyokuwa ameushika, maana ni mfuko mkubwa,
lakini kwa muda ule sikuwa na mawazo ya kumdadisi…’akasema
‘Oh….’docta akasema
‘Yeye alisema anatoka
kidogo, atarudi muda si mfupi, …mimi muda huo nimeshazozana na mke wangu
hatulewani, kichwa hakipo sawa, lakini mimi nikajua anataka kutoka nje ili awasiliana
na wewe labda…,na hataki kuongea humu eeh,… kama ulivyosema, ina maana
hamkuwasiliana naye?…’akasema na kuuliza huyo mzee.
‘Mhh..hapana..sijaongea
naye, maana nimekuwa nikimpigia nikawa simpati, nikahisi kuwa kuna tatizo,…hisia
zilikuwa zinaniashiria kuwa kuna tatizo, unajua mzee sijui ..ndio hivyo, wanasema nina hulka au
kipaji cha hivyo,..’akasema.
‘Kwahiyo unahisi
..huenda kuna tatizo..?’ akauliza mzee akiwa sasa na yeye na wasiwasi,
akasimama, huku akiangalia nje.
‘Huyu mtu atakuwa
kaingia kwenye mitego ya hawa watu,…’akasema docta
‘Kwa vipi docta, maana
..alitoka hakuwa na wasiwasi, alionyesha tu yupo safi..sizani, ni hisia zako tu
docta, …’akasema mzee
‘Hao watu wana kila aina
ya mbinu…kwa vile hawajui binti yenu yupo wapi, na huenda binti ….anyway, …muhimu
tumpate huyo mtu…’akasema
‘Ina maana binti yangu
atakuwa ana…jambo na hao watu….?’ Akauliza mzee.
‘Hapana…sizani, ngoja
kwanza tumpate huyu mtu, muhimu ..tujue ni kitu gani wametega,…’akasema docta.
‘Oh, sasa naanza
kuingiwa na wasiwasi…binti yangu ….nataka niongee naye, nijua kama ana jambo na
hao watu…’akasema mzee.
‘Mzee huko
usifike..nilikuambia nini kwenye simu,..kuwa makini,…’akasema docta
‘Sasa tukamtafute wapi
huyo msaidizi wako…?’ akauliza
‘Hilo niachie mimi, wewe
kaaa na mke wako, hakikisha anatulia…’akasema docta
‘Ok…basi unifahamishe
kinachoendelea hata kwa ujumbe..simu yangu inazima zima, si unajua tena..aaah, hali zenyewe ngumu hata simu
nashindwa kununua, tumekuwa kwenye matatizo, matatizo…’akasema mzee.
‘Sasa mzee,nashindwa
hata nianzie wapi, ..hivi ni nani hapo
nje ambaye anaweza kuona watu wakitoka humu ndani kwako wa kuaminika, nijaribu
kumuuliza..?’ akauliza kwa sauti ya chini
Mzee akasogea mlango,
wakawa wanatoka nje na docta, huku akimuambia hivi;
‘Hapo nje kuna fundi mmoja
wa viatu kama hajaondoka, huyo na mwamini sana, muda kama huu, ..nahisi bado
atakuwepo,…unaweza kumuuliza yeye..lakini kwani unahisi kapatwa na jambo baya ..?’
akauliza mzee
‘Muhumu kuonana naye
kwanza….’akasema docta.
‘Haya nenda
nisikucheleweshe,…utanifahamisha kinachoendelea…’akasema huyo mzee, na docta kwa haraka akatembea kutoka nje ya geti, na kukutana na huyo fundi wa viatu, alikuwa
anafunga funga kuondoka.
‘Eti fundi kuna jamaa
yangu tunakuja naye hapa kwa mzee mara kwa mara, kwa leo ulimuona akitoka hapo
mlangoni kwenye geti, na ni muda gani
ulimuona akitoka..?’ akamuuliza huyo fundi maswali kwa mfulululizo.
‘Aaah,.. yule jamaa
mnayeongozana naye..nilimuona akitoka na mfuko wa Rambo, hii mikubwa, ni muda
kidogo,…alitoka kwa haraka akaelekea upande huo… nahisi alikuwa na kitu
labda..anataka kukitupa, maana huko alipoelekea mara nyingi watu wamepafanya kama
ni dampo…’akasema na docta akaangalia upande ule akaona kuna miti miti tu…na
mataka taka
Docta hakuhitaji kuuliza
zaidi, kwa haraka akaelekea upande huo aliolekezwa, hakugeuka nyuma, na sasa
alikuwa akifuatilia hisiza zake, hisia zake humsaidia sana,…kwa kipindi kama
hiki, au kipindi cha hatari…
Akatembea huku akiomba mungu , alijua kwa
vyovyote vile msaidizi wake atakuwa kaingia kwenye mtego fulani, asingeliweza
kuondoka hivyo kimia kimia, halafu ni kwanini aelekee maeneo hayo, na alibeba
nini, akawa anawaza huku anatembea kwa haraka haraka, huku hisia zake zikinusa
kama mbwa...
‘Kama angelikuwa na nia
ya kuondoka asingelikuja upande huu, huku alifuata nini…’docta akawa
anajiongelesha mwenyewe, pamoja na hisia hizo lakini pia laikuwa akitafuta
dhamira, iliyomfanya mtu wake afanye hivyo.
‘Kutakuwa na jambo, hebu
niwaze zaidi,..alipigiwa simu, kuwa achukue mzigo huku, na nani lakini au
aliambiwa apelike huo mzigo, kwa mtu fulani, au ….’akasema akiwa sasa kafika
kwenye gogo la kukalia, hapo akasita, akahisi kuna jambo hapo.
Akasimama na kugeuza
kichwa huku na kule,…upande mwingine kulikuwa na taka taka zimelundikana, kuna harufu
mbaya ya matakataka yaliooza, na alipotizama chini ya lile gogo , akaona
karatasi, akaikumbuka kuiona hiyo
karatasi, lakini yaweza ikawa ni nyingine maana ilikuwa ni kipeperushi cha
matangazo, akaiokota.
‘Kama ni yenyewe,
nitaona ile sehemu alioandika namba ya simu, kwani siku ile alipokichuku ahicho
kipeperushi, alikutana na jamaa yake mmoja, katika kuongea wakapeana namba ya
simu, na akakiangalia hiyo namba kwenye hicho kipeperushi, maana jamaa yake
huyo alikuwa na haraka,..’ ni kweli
kilikuwa ndicho hicho akaiona hiyo namba,…
‘Ok,… kwahiyo atakuwa alifika
eneo hili, ….sasa, ilikuwaje,..kwanini hii karatasi ilidondoka hapa, je
kimakosa au …ni alama,…’akasema.
Akawa anaendelea kukagua
huku na kule, na mara tena akaona waya…akavutika na huo waya, akaufuta, …kwanza
alitaka kuuokota, lakini akasita, baadae alipojirizisha kuwa ni waya tu,
akainama na kuuokota, ulikuwa umezama ndani ya majani.., akauvuta kwa
tahadhari,…
‘Huu waya ni wa laptop,
tena bado mpya, haiwezekani kuwa ulitupwa, mhh…ngoja…’akaingiwa na wazo, kwa haraka akachukua
simu yake na kumpigia mzee.
‘Eti mzee, ulisema kuwa msaidizi
wangu wakati anatoka alikuwa kabeba mfuko wa Rambo, na huwezi kukisia kuwa
alibeba kitu gani, sio kwamba alibeba laptop..?’ akauliza, na mzee akasema hana
uhakika
‘Binti yako ana laptop…?’
akauliza docta mzee akasema ndio
‘Basi hebu ingia
chumbani kwake ukague kama hiyo laptop ipo …’akasema docta, huku
aikisubiria,..hakukata simu, akawa bado anaendelea kuchunguza kwa macho, huku
na kule, baadae mzee akawa hewani akasema hiyo laptop haipo ndani.
‘Ina tumia waya wa namna
gani…?’ akauliza na mzee akasema hiyo laptop, waya wake wa betrii uliharibika
na yeye alikwenda kumnunulia binti yake waya mwingine mpya na una karatasi
imeandikwa,..jina la hiyo laptop, lakini pia
yeye aliandika kwa peni jina la huyo binti kwa herufi tatu za jina la
binti yake...
‘Ndio yenyewe..’akasema
docta, na mzee akamuuliza ndio yenyewe nini kaiona hiyo laptop au kaona nini,
au kamuona msaidizi wake, akiwa …lakini docta hakumpa nafasi ya kuuliza zaidi,
yeye akasema;
‘Ngoja nitakuambia nikihakiki,
sijamuona huyo msaidizi wangu , lakini nahisi alifika maeneo haya, nitakupigia,…’akasema
docta na kukata simu, sasa akiwa kavutika na jambo jingine jipya, hilo likampa
jakamoyo na kuhusi mwili ukimsisimuka zaidi,iliashiria hatari
Docta alihisi sasa mwili
ukimsisimuka, hii ni dalili nyingine hasa anapokaribia hatari..akawa sasa
anakagua hicho alichoona, kwa macho, na huku akiinua mguu kwa tahadhari, huku
anaendelea kuangalia ....
**********
Macho yake yaliona alama
za mburuzo wa kitu kizito, mburuzo huo uliacha alama, na yeye akaufuatilia kwa macho…na huku
anatembea kwa tahadhari, maana inaweza ni chatu kapita,..au kitu kama gunia
nzito lilikuwa linaburuzwa. …au mtu ..’hakutaa wazo hilo liingie akilini.
Sasa akawa anatembea
kufuatilia alama hizo, akazifuatilia hadi akafika kwenye mtaro wa maji machafu,
alama hizo zikaishia hapo, akajaribu kuona kama kuna gunia limetelekezwa au
kitu cha namna hiyo, alichunguza aneo lote hakuona,…
‘Isije ikawa ni chatu…’akasema
sasa akiangalia huu ya miti, kwa uwoga, lakini hisia za uwoga hazikuwepo zaidi
ya hisia kuwa kuna kitu kingine zaidi ya hicho.
‘Lazima kama ni gunia,
au …ningeona hicho kitu, na kwanini huo
mburuto ukaishia hapa, au umezamishwa kwenye huu mtaro…’akasema sasa
akichungulia kwenye huo mtaro…
Ulikuwa ni mtaro mrefu kidogo
wa kupitisha maji,…, na uzuri wake haukuwa na maji, ila una mataka taka..ya
kuoza..
Akagundua kuwa kwenye sehemu ya mbele kuna
majaniyamelazwa, na mengine yamekauka, kuonyesha kuwa kuna kitu kimezamishwa
hapo, hapo akajua huenda ndio hicho kitu kimetupwa hapo, lakini kwa jinsi
majani yalivyowekwa ni kama kimefichwa..
Akasogelea pale na kuinama
na kuanza kupachunguza, kwa tahadhari, kwanza akaanza kuyaondoa yale majani ya
juu,akayasogeza pembeni, inavoonekana huyo mtu aliuweka huo mzigo kama kuuficha
ili jae kuchukua baadae, sasa ni mzigo gani..
Docta akavutika
kuugundua, japokuwa ilikuwa kupoteza muda, ..aliondoa yale majani mpaka
kukatikana uwazi wa kuangalia ndani. Akahakikisha kuwa kuna usalama sio chatu
au kitu cha hatari,…akaona ili agundue vyema hicho kitu ni bora aingie ndani ya
huo mtaro… akatumbukia ndani ya mtaro..kulikuwa kuchafu..lakini ikabidi tu.
Alipofika ndani ya huo
mtaro, akagundua, kitu ni kama furushi, lililofunikwa na shuka jeupe…kwanini
lifunikwe na shuka jeupe, akasogea na kwa tahadhari akawa anavuta ile shuke…oh,…,
ni mtu…
‘Ni mwili wa mtu…’ docta
akahisi mwili ukimuisha nguvu, akavuta ile shuka jeupe kama sanda na
kuhakikisha huo mwili umebakiwa wazi,…shati lilikuwa limelowa damu,….
‘Hizi…huyu..sio…ooh…’aligundua
nguo alizokuwa amevaa msaidizi wake,…lakini kwa jinsi mwili ulivyosokomezwa
hata kichwa kilikunjwa kama mtu anasujudu..hukioni vyema
Sasa akaanza kazi ya
kuusukuma ule mwili mpaka ukafikia sehemu ya kuunyooka kwa kulala, ..haikuwa
kazi rahisi alihitajia msaada, lakini kwa usalama zaidi akaona ahangaike pele
yake.
‘Oh,..mungu
wangu…msaidizi wangu, ..ooh wamekuua..haiwezekani…’akasema sasa hata
mwili ukimuishia nguvu..maana kwa hali aliyoiona sio ya kuona mtu, kwanza damu
nyingi zimevuja kutoka kichwani.
‘Oh, mungu wangu, saidia
mja wako…ni msaidizi wangu, alikuwa katika kuwasaidia waja wako, sio kwa uwezo
wetu, yote haya ni kwa uwezo wako na
rehema zako..,..’akasema
Alijua hataki kupoteza
muda, akaanza kazi ya kumtoa huyo
msaidizi wake kwenye hilo eneo,
ilichukua muda mpaka kumtoa, halafu akaanza kumfanyia huduma ya kwanza, lakini
ilionekana jamaa yake huyo hana uhai..
‘Hapana haiwezekani…mungu wangu saidia mja
wako..’akasema sasa akikata tamaa, na hapo akaona haja jinsi, akachukua simu
yake na kumpigia jamaa mmoja wa bajaji anayemfahamu,..na uzuri wake jamaa huyo
akasema hayupo mbali,a nakuja hapomuda sio mfupi.
Wakati anamsubiria
mwenye bajaji akawa sasa anajaribu kutafuta chochote cha kumsaidia kama
ushahidi, na alipokuwa kifanya hivyo akaona peni, sio peni za bei rahisi, ni
peni maalumu mtu anatengenezewa, inakuwa na nembo ya kampuni au..jina lako…ilikuwa
ndani ya huo mtaro, kashuka tena na akaichunguza ile nembo, lakini hakuweza
kugundua kuwa ni kampuni gani…akaifadhi tu
Na mara mwenye bajaji
akafika, na wakasaidiana kumweka kwenye bajaji.
‘Mzee hii ni maiti,
tunaipeleka wapi…’akasema mwenye bajaji
‘Nani kakuambia ni
maiti..’akasema docta
‘Hapa huwezi kuuliza
huyo keshakufa,..usije kuniingiza kwenye kesi, maisha yenyewe haya nianze
kukimbizana mahakamani, au polisi, hapana mzee..’mwenye bajaji akaanza kuogopa
‘Sikiliza mimi ni docta,
huyu ni mgonjwa wangu wewe tufike hospitali na usihie zako, ni nani atakuuliza…’akasema
docta na baadae jamaa akakubali na wakaelekea hosiptalini.
Walifika kwa docta, na
docta , japokuwa ni rafiki yake lakini akaanza kuweka pingamizi ;
‘Unajua huyu mtu
kapigwa, kaumizwa, na ..na kafariki huyu…’akamkagua na kumpima, docta,…huyu
hayupo hai…’akasema mwenzake kwa mashaka
‘Una uhakika kafariki…? Akauliza
docta sasa na yeye akiwa na mashaka,
maana japokuwa yeye ni docta lakini kwa rafiki yake, ilikuwa hawezi hata
kuhitimisha kuwa msaidizi wake kafa au la…Docta mwenzake sasa akaamua kutumia
vipimo vya ziada kabla hajatoa jibu.
NB: Haya ilikuwaje..
WAZO LA LEO:
Majanga, misiba, mitihani ya maisha inapotokea kwenye jamii, wengi wanaweza
kukimbilia kwenye shiriki na kusema hapa sio bure kuna mkono wa mtu, tunasahau
kuwa kuna mungu..Mola muweza wa yoye ambaye anaweza kutenda atakavyo, na
mitihani ya maisha inatukia ili iwe kama onyo, au kama kumbusho kwetu.., kuwa
sisi hatupo hapa duniani moja kwa moja, naya kuwa pamoja na kuhangaika kwetu katika
kutafuta maisha bora, tunahitajika pi kumkumbuka kutenda mema na kukatazana
mabaya. Na ikitufikia misiba tukumbuke kusema kwake tumetoka na kwake ndio
marejeo yetu
Tuzidini kumuomba mola wetu
atusaidie kutuongoza kwenye njia iliyonyooka, na kwa msiba uliotukuta, kwa
kuwapoteza watoto wetu, na mingine iliyotokea baadae.,. tu poleni sana wazazi, kwani
sisi sote ni wazazi wa watoto hao, na ndugu wa marehemu waliotangulia mbele ya
haki, hii ni misiba yetu sote, na tunamuomba, mola awahifadhi watoto wetu hao,
na ndugu zetu hao walifariki kwenye ajali hizoo na kuwahifadhi mahali pema peponi…Amin
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment