Ilikuwa kazi kubwa sana kumshawishi kijana wetu kukubali
kuhudhuria kikao cha maridhiano,kama ilivyopendekezwa na hakimu.
Ilibidi, wakili mtetezi kufanya kazi ya ziada, na
hakuchoka, kumuendea jamaa wetu huyu, ambaye kila mara alipofikiwa alidai kuwa
hana nafasi, lakini sasa hakimu akawa katoa agizo kuwa anahitajia hayo
makubaliano ili aweze kumaliza hiyo kesi,
Wakili baada ya kupata maagizo hayo, alikwenda moja kwa
moja kwa jamaa yetu, na kumwambia kuwa sasa asipokubali kuwepo hicho kikao,
kesi itaendelea na itambidi awe anahudhuria mahakamani mara kwa mara…
‘Mimi sina muda huo….’akasema
‘Ndio maana tunahitajika kuwepo hicho kikao cha maridhiano,
ili hakimu aweze kuimaliza hiyo kesi…’akaambiwa
‘Kwani kuna tatizo gani, kwanini hakimu asitoe hukumu tu,
maana kila kitu kipo wazi, mkosaji anajulikana alichokifanya, atoe hukumu….’akasema
‘Wewe unafahamu wazi kwanini hakimu alisitisha kuendelea
na kesi hiyo kwanza…..’akasema
‘Mimi sifahamu ….’akasema
‘Hakimu hakutoa hukumu kutokana na halii halisi, wewe
ulikuwa huwafahamu wazazi wako, na umewafahamu kati kati ya matatizo kama haya,
yeye akachukulia hayo kiubinadamu ili mfahamiane kwanza….’akaambiwa
‘Tunarudi kule kule, hayo hayana maana kabisa, anyway…haya nambieni mnataka mimi
nifanye nini,….?’akasema na kuuliza
‘Tunataka tukutane wewe na wanafamilia, tuone yale mnayohasimiana,
ili tuyamalize haya matatizo, na ikibidi ….kutokana namaridhiani hayo kesi
ifutwe, na nyie make kama familia, unaona hekima ya hakimu…’akaambiwa
‘Nikae meza moja na huyo mzee, sizani kama tutaelewana…yule
mzee ana hasira, na mimi siwezi kuvumilia, kama anajifanya ana hasira mimi ni
zaidi, sitajali kuwa ni mzee…..ndio maana sitaki kabisa kukaa naye meza moja….’akasema
‘Inabidi, ukumbuke yule ni mzazi wako, na inabidi tukae
tuyamalize…ili kesi ifikie mwisho,ikiwezekana kesi hiyo ifutwe,… ili wewe usisumbuliwe
sumbuliwe tena….’akaambiwa na yeye akatulia akiwaza jambo,halafu akasema;
‘Tutakutana wapi na lini, ujue mimi nipo kazini, siwezi
kuacha shughuli zangu kwa mambo haya yasiyo na maana kwangu, nambie…’akasema
akiangalia saa yake
‘Wewe unataka tukutane wapi, nyumbani kwako, au ofisini
kwangu, au twende kabisa huko kijijini, unaonaje hilo, ukienda kijijini wataona
wewe kweli ni muungwana, mtoto mwema unasemaje…?’ akaulizwa
‘Nitakuja ofisini kwako…siwezi kwenda huko kijijini, hao
watu sio wema kwangu. Kijijini….! Hahaha,…..
hapana huko siwezi kwenda kabisa….’akasema
Basi siku ya kukutana ikapangwa,lakini kwa bahati mbaya mzee
huyo, yaani baba yake jamaa, hakuweza kufika kutokana na hali yake kuwa sio
nzuri, lakini wakili mtetezi, akasema kikao kinaweza kuendelea na Profesa
atamuwakilisha kaka yake...yatakayokubaliwa yeye atayawakilisha kwa kaka yake.
‘Kwanini tusiende huko kijijini, alipo huyo mgonjwa ili
yeye mwenyewe, kijana aweze kumuona baba yake na baba yake atasikia faraja,…..?’
Profesa akasema
‘Kijana wako kasema yeye hawezi kwenda huko,….’akasema
wakili alipokutana na Profesa kumpa taarifa hiyo.
‘Mimi nataka kuongea naye kwanza kuhusu hilo, maana ni
muhimu ninawe mikono, nisije kuonekana mimi sikutimiza wajibu wangu…’akasema
Profesa
‘Unataka kuongea nini na yeye, nachelea usije kuharibu,
ukafanya jamaa akatae kabisa kukaa hichi kikao…?’ akaulizwa
‘Yule ni baba yake, ni lazima nimueleze hali
halisi,…’akasema na wakili baadaye akakubali, lakini alitaka na yeye awepo,
kwahiyo wakaongozana hadi ofisini kwa jamaa na bahati nzuri, akakubali kuongea
nao
‘Mnasemaje tena, na kwanini umekuja na huyu mtu…?’
akauliza akimnyoshea mkono Profesa
‘Yeye ana ujumbe muhimu anataka kuongea na wewe
kwanza…’akaambiwa
‘Kwahiyo kikao hakipo tena…?’ akauliza
‘Kikao kipo, ila yeye alitaka kuongea nawe kidogo…msikilize
tu…’akasema wakili,na Profesa akasema;
‘Mimi nilionelea kikao hicho kikafanyike huko kijijini,
kwa kaka,….kwa baba yako ili wewe mwenyewe uone hali ya baba yako, na ukifanya
hivyo , ni kwa faida kwako, utampa faraja yule mzee,hebu jaribu kulifikiria
hilo kama mtu uliyekomaa…’akasema Profesa
‘Unaanza kuleta yale yale…mlitaka niende kuonana na yule
mama, ….nikapoteza muda wangu hakuna kilichosaidia, sasa unataka niende kuonana
na huyo mzee, ili iweje,…kama anaumwa, mpelekeni hospitali, mimi siwezi kufanya
apone, kwani mimi ndiye nimempa huo ugonjwa….’akasema akiwa kasimama ameegemea
mlango.
‘Sikiliza bwana mdogo, kwa mama yako umefanya makosa….wewe
hujui tu….sasa mimi niliona yaliyopita yamepita, sasa jirudi,…hujachelewa bado,…mimi..,
alitaka mkutane naye akupe hata wosia, moyo wake uwe radhi na wewe….umefanya kosa
kwa mama yako, ..hujui mama yako
kaondoka na kinyongo gani, …’akaambiwa
‘Usielete visingizio hapa….yule mama yote alijitakia
mwenyewe, au tusema ni ajali, ni bahati mabaya, mimi sihusiki lolote,…na nilifika,
na siku nilipofika alikuwa hajitambui,….sasa unarudia rudia,..mama, mama….awe
na kinyongo na mimi kwa lipi, ..acha ujanja ujanja wako hapa…’akasema
‘Sikiliza nikuambia….’akasema Profesa na jamaa
akaangalia saa , halafu akasema
‘Hebu nambie wewe ulitaka mimi nikae pale hospitalini
mpaka lini…unafikiri mimi sina kazi kama wewe, kazi kwanza…kazi nimuhimu,
unasikia,mimi sio tapeli kama wewe, kuishi kiujanja ujanja siwezi,…nafanya kazi
ili nipata pato halali….’akasema
‘Sijakataa hilo…lakini mzazi wako naye ni muhimu kwako,
ulitakiwa uonyeshe dalili kuwa unamjali, uonyeshe kuwa ulimkubali, lakini
ilionyesha kwa kila mtu kuwa hukumtaka mama yako, …hiyo ni balaa mbele ya
safari,…’akaambiwa
‘Hebu niambieni, kikao kipo au hakipo….?’ Akauliza akiwa
sasa anataka kuondoka
‘Kikao kipo, ila ilibidi nije na Profesa ambaye alitaka
kuja kukupa huo ujumbe, kama nilivyokuomba mwanzoni na yeye alikuja na wazo
hilo, kuwa ni muhimu kikao hicho kifanyike huko kijijini….’akaambiwa
‘Sikilizeni, kama ni lazima kifanyika huko kijijini….,
basi tuachane na mazungumzo haya, maana kwangu hayana tija yoyote, siwezi
kupoteza muda wangu hadi huko kijijini, siwezi , siwezi, mumenielewa, sasa
muamue wenyewe….’akasema jamaa
‘Hayo mazungumzo mbele ya baba yako yana tija kwako
sana, ujue hao ni wazee wako, huyo ni baba yako, mzazi wako,..na kuridhia naye,
itakusaidia sana katika maisha yako ya mbeleni…’akasema Profesa.
‘Kauli yangu umeisikia sio…Ndio hivyo…., kama kikao
hakiwezi kufanyika hapa mjini,huko kijijini siende, kwanza mimi natafuta nini
huko, haya ni kwa manufaa yao wao wenyewe wanaotaka hii kesi ifutwe, ndio
wahangaike, ….mimi ningelipendelea haki itendeke, sema tu sina muda wa kwenda
mara kwa mara mahakamani, lakini ikibidi, kama watajifanya vichwa ngumu, nitahakikisha
haki inatendeka….’akasema
‘Kwahiyo upo tayari baba yako afungwe?’ akaulizwa na
Profesa na hapo kijana akaangalia saa yake, baadaye akasema…
‘Sasa mniambie moja, hicho kikao kipo au hakipo….?’
Akauliza
‘Kikao kipo tutafanya utakavyo wewe….’akasema wakili na
kumuashiria Profesa waondoke, na Profesa akawa anataka kuongea lakini jamaa
akaondoka kuendelea na kazi zake.
**********
Basi siku
iliyopangwa kufanyika kikao ambayo ilikuwa ni kesho yake, wakili na wakili
msaidizi wakiwa ofisini kwako, na muda mfupi baadaye akafika kijana wetu kama
walivyozoea kumuita, alifika peke yake, mkewe hakuwepo,..
‘Unaona hawa watu walivyo, hawajali muda, sasa huyu
Profesa na ndugu yake wapo wapi….’akaanza kulalamika baada ya kufika na
kusubiri kidogo.
‘Kwa taarifa nilizozipata, baba yako hataweza kufika,
ndio maana walitaka kikao kifanyike kijijini,lakini Profesa atafika,
akimuwakilisha ndugu yake, .’akaambiwa
‘Baba yako, baba yako, mimi sipendi hiyo kauli….’akasema
akikunja uso
‘Lakini tulishakuambia, kama hujarizika, basi tufanye
vipimo vya kitaalamu ili ujirizishe mwenyewe kuwa huyo ni baba yako mzazi…ukagoma,
lakini hata hivyo, kwa ajili ya kumbukumbu hilo litahitajika …kama kesi
itarudishwa mahakamani...’akaambiwa
Profesa akawa kama hajasikia hilo, au kuyazarau hayo maneno
aliyoambiwa yeye aliangalia saa yake halafu akasema;
‘Mimi nitasubiria nusu saa baada ya hapo, nitaondoka, na
msije kunisumbua tena….’akasema
Baadaye Profesa
akafika na wazee wawili
**********
Kikao kikaanza, wakili mtetezi alirejea yake aliyoagizwa
na hakimu na ya kuwa hakimu kasema hayo makubaliano yafikishwe kwake haraka
iwezekanavyo, kwani kesi hiyo imesubirishwa kwa muda mrefu, na huenda hakimu
huyo anaweza kupata uhamisho…
‘Kwahiyo kwanza ni wewe ulitendewa kosa, hadi kesi
ikafikishwa mahakamani kukubali kuwa umesamehe, na huna haja ya kuendelea na
kesi hiyo, lakini kabla ya hilo…’akatulia akifungua makabrasha yake
‘Rejea yale aliyopendekeza hakimu, …hakimu alitaka wewe
na mshitakiwa mfahamiane, kutokana na ombi kuwa wewe ulikuwa humfahamu baba
yako..’akasema wakili
‘Je wewe umeshamfahamu baba yako na kumkubali ….?’
Akaulizwa
‘Hilo linahusiana vipi na kesi,…hebu niwaulize, baba
akimkosea mwanae, mtoto haruhusiwi kumshitaki baba yake…?’ akaulizwa
‘Anaruhusiwa, ….lakini sisi tuliyafanya haya kutokana na
historia yenyewe, kuwa wewe ulikuwa humfahamu baba yako, ndio tukaona kuna
umuhimu wa kuwakutanisha kwanza, huwezi kujua mioyo ya watu hutofautiana,kwa
furaha ya kumtambua baba yako unaweza kusamehe kila kitu,….’akasema
‘Lakini sheria si ipo wazi…ni nani aliyemletea mwenzake
fujo,ni mimi au ni yeye….?’ Akauliza
‘Kwanza tulimalize hili, je umeshamfahamu kuwa huyo mzee
ni baba yako, na ukakubaliana na hilo?’ akaulizwa
‘Mimi nimeshamfahamu huyo mzee …na kama mnadai kuwa ni
baba yangu, mimi siwezi kusema lolote kwa hilo ninachotaka twende moja kwa moja
kwenye swala muhimu, kuhusu hiyo kesi, ….’akasema
‘Hatuwezi kwenda huko mpaka hili swala limalizike, kwani
lipo kwenye mapendekezo ya hakimu na tunahitajika kuepeka marejesho kwa
hakimu….’akaambiwa
‘Ngojeni kwanza, …nyie mna wakili wenu mtetezi, lakini
mimi sina wakili hapa, je mawazo yangu na hoja zangu atazisimamia nani…?’
akauliza
‘Ukumbuke kuwa hiki ni kikao cha kifamilia, ,…hatuhitajii
wewe kuwa na wakili wako, tunaongea haya familia, mimi wakili nimeitwa hapa
niwe shahidi tu, na mtakayokubaliana niweze kuyawakilisha kwa hakimu, lakini
kwa vile mimi ndiye ninayefahamu ni nini hakimu anahitaji, nimeona niwe
msimamizi wa kikao ili mambo yaende vyema…’akasema wakili mtetezi
‘Sikilizeni, …mimi nataka haya mambo tuyamalize, na nipo
tayari kesi hiyo ifutwe,…’akasema na kila mmoja akashusha pumzi ya kuonyesha
kuwa hatimaye mambo yanakwenda vyema
‘Lakini… baada ya hapo, sitaki kujuana tena na hawa watu,
siwataki hata kuwaona kwenye macho yangu….’akasema na wote wakaguna
‘Kwa kusema hivyo una maana gani,…ina maana hujamkubali
huyo mzee kuwa ni mzazi wako, ina maana mlikuwa hamjakubaliana, hukuchukua
taratibu zozote za kuongea naye?’ akaulizwa
‘Sikilizeni, kimaandishi, …kama ni muhimu kuwa hivyo,
…narudia kusema hivi, kimaandishi kama ni muhimu, ile iwe hivyo, ….ili kesi ifutwe, andika na
nitasaini kuwa nimekubaliana na hayo, ..’akasema
‘Unajua hapo hujaeleweka, kwani nia nini, hatuhitaji
kuanya mambo kihivyo, kuwa tuhadae ili kesi iishe,..nia ni kutaka mambo haya
yaishe kwa nia moja, wewe ujumuike na familia yako, ni faraja, eti, wewe
hukuwahi kuwafahamu wazazi wako, na sasa umewapata,, bahati mbaya mama
kafariki,….pole sana….’akasema wakili
‘Muheshimiwa tusifanye mambo yawe marefu,…unajua kwa
kukusaidia tu , kama alivyotaka hakimu, tutafanya,….’akatulia kama vile anachotaka
kuongea ni jambo lenye thamani kubwa, lakini halitakiwi kusikiwa na watu wengi
‘Mimi ni mwema sana, unasikia,…. Kimaandishi tutafanya
hivyo…au sio, kama mnayotaka nyie, si mnataka kesi iishe, isiwe shida,…lakini
tuelewane hapo,….’akatulia kidogo
‘Kuna mambo muhimu nataka tuelewane hapo,….unajua, ndio
maana nilitaka wakili wangu awepo, lakini sio mbaya, …wewe utawakilisha
inatosha…’akasema
‘Wewe ulitaka nini, ili wakili wako ashuhudie, au
akuwakishe, ulitaka nini…?’ akaulizwa
‘Unajua hawa watu ni wajanja sana, na siwaamini
katu….sasa nitakubali kuweka sahihi yangu, lakini ….,’ akatulia kidogo
‘Lakini, nina
masharti, ambayo nataka hawa watu wayakubali, mbele yako wewe kama wakili wao…’akatulia
‘Hatujakuelewa, masharti, masharti ya nini….! Kwasababu
nia yetu ni maelewano, na maelewano manzuri ya kifamilia ni udugu, sioni kwamba
udugu, hasa wa mzazi na mtoto wake kunahitaji masharti , labda , hebu
tueleweshe hapo ni kwanini unaweka masharti …..’akasema wakili mtetezi
‘Ni hivi, kama mnataka mimi nikubali kuwa hiyo kesi ifutwe, si ndivyo mnavyotaka ?’
akawauliza na kabla hajajibiwa akasema….
‘Sasa ili nikubaliane na matakwa yenu, mimi nina
masharti yangu,…mkikubaliana nayo,mimi nitaweka sahihi yangu na mambo yataisha,…kwani
hata mimi nataka yaishe ni malizane na hawa watu,….lakini bila namna, bila
kuwepo na hayo masharti, najua itakuwa mwanzo wa usumbufu….’akasema na kutulia
kidogo
‘Mimi sitaki tena usumbufu na hawa watu, nataka amani ,
unajua wamesababisha naanza kukosana na mke wangu, hivi sasa mimi na mke wangu
hatuelewani, ukiangalia sababu hasa …ni hawa watu…..’akasema akimnyoshea kidole
Profesa.
‘Pole…lakini matatizo ya mke na mume ni kawaida, …muhimu
ni nyie kuelewana, na kama ungekuwa iumeshaelewana na wazazi wako hawa
wangekusaidia ….wazee wana hekima zao…’akaambiwa
‘Hahaha…hawa wanisaidie wakati ndio sababu, na wanataka
iwe hivyo..lakini hawataweza…nikuambie kitu, huyu kaweka fitina mpaka kwa mama
mkwe wangu, naonekana mimi sifai…..sasa nitamuonyesha mkwe wangu kuwa nafaa,
hata bila yeye naweza….’akasema
‘Kumbe….’akasema Profesa akitabasamu
‘Unaona….Hawa watu sio watu wema,….hasa huyu, ….usimuone
hivi, ni mwerevu sana, katika kutafuta jambo atajifanya mwema hujawahi
kuona,ngoja apate…kiburi kinajitokeza,….namfahamu sana, kama ndiye yeye, maana
mpaka sasa sijaamini…’akasema akimnyoshea kidole Profesa
‘Haya hebu tuambie ni masharti gani hayo…..?’ akaulizwa
na wakili akimuangalia jamaa kwa macho yenye shauku
‘Ehee, sasa tunaanza kuelewana, …nataka uyaweke sawa, ni
mashrti muhimu ambayo yatahakikisha kuwa hawa watu hawanisumbui tena….wakiyakubali,
aaah, basi sina shaka, mimi nitakubali kuweka sahihi yangu kwenye hiyo taarifa
inayokwenda kwa hakimu…..’akasema, na wakili akamwangalia Profesa aliyetaka
kuongea jambo….
NB: Naishia hapa muda …mb, hizo zimekwisha,….
WAZO
LA LEO: Katika kumaliza matatizo ni muhimu kila mmoja akapewa
nafasi yake, na kwenye meza ya makubaliano kila mmoja ana nafasi sawa….tusiweke
vikwanza kwa kuangalia masilahi binafsi. Na maongezi yenye nia njema, huleta
tija, kuliko kutumia mabavu,..kwani wakipambana mafahali wawili zinazoumia ni
nyasi.
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
Msione tupo kimia, jembe(laptop) imeharibika, pia mitihan ya hapa na pale, lkn mungu yupo, atatusaidia,zaidi tutembelee facebook
Post a Comment