Inspecta
akiwa na wasiwasi aliingia chumbani kwake,na alijua atamkuta mkewe akiwa kitandani,
akiwa kalala, na lengo lake ni kumkurupusha kwa hasira na kutoa kipigo cha aina
yake, lakini hasira zile na dhamira ile aliyokuwa nayo ilinywea ghafla, kwani kwanza alihisi mwilini
hali isiyo ya kawaida. Yeye huwa mwili wake unatabia ya kuhisi jambo, hasa
likiwa ni la hatari, mwili humsisimuka au nywele kusimama.
Alipohisi
hiyo hali, akili ikamtuma kuwa kuna tatizo, hapo hapo mwili ukajenga hali ya
tahadhari, na kama angekuwa na silaha angeitoa na kuwa nayo mkononi, lakini
hapo hakuwa na silaha, alichoweka akilini ni kuwa huenda mkewe atakuwa kwenye matatizo.
Hapo
hapo hali ile ya hasira ikabadilika na kujenga hisia za wasiwasi, huruma, na
moyoni akawa anaombea kusiwe na baya lolote kwa mkewe, alianza kukumbuka siku
zake za nyuma, jinsi alivyompenda mkewe hadi wakafikia kuoana, na katika
maongezi yao mara kwa mara kila mmoja alikuwa anaomba atangulie yeye kufa, ili
asije kupata machungu ya kumkosa mwenzake.
Maisha
ni kitu cha ajabu sana, leo imefikia hatua wanasalitiana, wanafanya yale
waliyoapa kuwa hawatafanya, ..
‘Natubu
kwa mola wangu hili kosa sitarudia tena, ni lazima nimpende mke wangu kwa moyo
wangu wote, na nitatubu kwake na kumuelezea yale yote yaliyotokea, kwani hayo
yote yamefanyika sio kwa dhamira yangu…’akawa anajisemesha moyoni huku machoni
akihisi hali ya machozi.
Huruma
ikazidi kuongezeka, akavuta hatua, lakini hali ile mwili kusisimu na nywele
kusimama ikazidi, na na hapo akajua ni lazima kuna jambo baya limetokea, akawa
sasa anaharakisha ili kama kuna lolote
aweze kuchukua hatua za haraka, akashikilia simu yake tayari kwa kuomba msaada
ilibidi, ndio silaha pekee aliyokuwa nayo mkononi.
Akatupa
jicho kitandani,hakuona kitu,..ohoo, kaenda wapi huyu, akajiuliza na akahisi
mwili ukinywea, miguu ikaanza kuishiwa nguvu, lakini kwa ujasiri wa kiaskari
akajikaza, na akatupa jicho na macho yake yakiwa na hisia za kiaskari, yakawa
yamepeleleza eneo lote la chumba, na sakafuni mwa kitanda akaona shuka limedondoka,
kidogo, akahisi nguvu, kuwa huenda mkewe kaenda kuoga au chooni.
Akavua
shati na kubakiwa na vest ya ndani,akijua sasa anahitaji kupambana na lolote
lililopo mbele yake, akatupa jicho chini,akaona kitu,…leso
Kuna
leso yenye alama za damu,….akaisogelea na kuiangalia, sio damu nyingi, ni kama
mtu alipatwa na jereha, akafutia, hiyo sio leso ya mkewe, mkewe ana tabia ya
kununua leso aina fulani,…
‘Hii
itakuwa ni leso ya nani…’akajiuliza akataka kuinama kuichukua, lakini akasita,
akakagua kitandani, akaangalia huku na kule, kunaonyesha dalili zote kuwa mkewe
alilala hapo…hisia nyingine za wivu, kuwa huenda kulikuwa na mtu mwingine,
akakumbuka maneno ya muhudumu wa hoteli, alivyosema;
`…Huyo shemeji yake
….aah, unajua siruhusiwi kuongea zaidi, ila ndio alikuja baadaye, na alipoona
hiyo hali, akamshawishi huyo mwanamke, na baadaye akakubali wakaondoka naye…
‘Ina
maana walikuja pamoja, wakatumia kitanda change…hapana, lakini nitajua tu..’akasema
sasa hali ikibadilika tena, akasogea hadi kitandani.
Kwanza
alisita kukaa kama vile atajichafua, aliona kitanda chake kama ni kichafu,
kimechafuliwa..lakini hali ile ya mwanzo ya kuwa huenda mkewe yupo matatani
ikamrejea, sasa akajipweteka kitandani, akashika kichwa, akiwaza kwa muda,
halafu akainua na kuandalia huku na kule kama anahisi jambo.
Kulikuwa
kimiya kabisa kama hakuna uhai, ni kama vile dunia iliamua kutulia kwa muda,
hakuna hata kitu kinatikisika, ile hali ya matumaini ikaanza kunywea, akaona
kwanini aandikie na mate wakati wino upo, akainuka kitandani na kuanza kutembea
kuelekea chooni…huko ndipo kuna bafu pia, akasogea, kwanza alitaka kupiga hodi,
lakini akasita
Akashika
kitasa cha mlango wa kuingilia huko, na kwa nguvu akafungua na kusukuma, na kwa
haraka akawa keshaingia ndani...
Kulikuwa
kimiya,..na ile hali ya kusisimukwa mwili ikamrejea, akahisi ubaridi mkali,
akaona asipoteze muda, akafungua mlango wa kuingilia chooni, ulipofunguka,
akakuta hakuna kitu…kuna karatasi za chooni, sakafuni, akaona kipande kidogo
kidogo, kina alama nyekundu….damu
Machale
sasa yakamcheza, bila kuchkua tahadhari, akakimbilia mlango wa bafuni, akafungua
kwa haraka, na hapo, akasimama, akaduwaa, …lakini macho kama gololi yakawa
yamesoma eneo lote,na kujua ni nini kipo wapi.
Ndipo
akatupa macho sasa kwa makini, pale kwenye beseni la kuogea, mkewe alikuwa
kalala , kuonyesha alikuwa anaoga, lakini kwa hali aliyokuwa nayo sio ya kuoga,
…
Mkewe
alikuwa kalala kwenye beseni lililokuwa limejazwa maji, mkono mmoja umejikunja
na ulikuwa umefunikwa na maji, ulikuwa umshikilia tumboni, …hapo akaona rangi
ya maji ikiwa imebadilika,…damu, damu….
Kwa
haraka akakimbilia pale, na kuinama kumuangalia mkewe, huku mwili sasa ukiwa
sio wake, ni mwili wa kiaskari, akapeleka mkono shingoni kwa mkewe,…akahisi
mapigo ya damu kwa mbali, akajua bado yupo hai..
Sasa
akatupa macho ndani ya maji, kwanini maji ni mekundu, ….hapo akaishiwa nguvu,
alichosema ni..
‘No,
no….sio kweli, haiwezekani, ….’akashusha mkono hadi ndani ya maji, akagusa
kitu, …kwasababu maji yalishabadilika rangi, na mwanga mle ndani ulikuwa
nihafifu, hakuweza kuona ni kitu, ila alichogusa akajua ni kitu gani, hapo
akili ikaanza kuchanganyikiwa, akaacha kuchukua tahadhari za kiaskari, akawa
amekigusa hicho kitu,na alipogundua hilo kosa ikawa keshachelea
‘Mu-mu-mu-me,
wangu ni-ni-ni-sa-ame-he……’ilikuwa sauti ya mkewe akiongea kwa shida,,
akamsogelea na kumshikilia kichwani, alionekana yupo kwenye hali mbali, akafunua macho kidogo kwa shida, na Inspecta alipoona hivyo, akasema;
‘Mke
wangu, umefanya nini,..kwanini umeamua kujiua…’akasema Inspecta.
‘Si-we-zi,
ku-ku-za-li-li-li-ka,..rafi-ki , y-ya-ko , du-ni-a aaah, -ya-ya-ngu….’akasema na mara shingo ikalegea, akawa kimiya..Inspecta akaanza kuchanganyikiwa, ule ujasiri wa uaskari ukamuishia.
‘No…hapana,
utapona tu mke wangu….usife mke wangu ukaniacha, kumbuka ahadi yetu,....ooh,’akasema sasa akihangaika kutaka kumtoa pale ndani ya maji,
na mara kwa nje akasikia mlango ukigongwa kwa kasi…
‘Fungua
mlango sisi ni askari…’akasikia
Akajua
sasa kuna tatizo, akainama kwanza kuangalia afanye nini, akashusha mikono yote
sasa, ili aweze kumbeba mkewe na kumtoa kwenye maji, mara kwa nyumba mlango
ukafunguliwa kwa kasi, na haikupita muda, hao askari wakawa waeshafika eneo
hilo la chooni,
‘Yupo
huku afande…’sauti ikasema na mara sauti ya uali ikasema nyuma yake;
‘Tulia
hivyo hivyo, upo chini ya ulinzi…’sauti kali ya askari ikasema, na yeye akageuza
kichwa haraka na kusema;
‘Ita
dakitari haraka, mke wangu,yupo mahututi,....’akasema, na alipomshika mkewe na
kwa jinsi alovyolegea, akaishiwa nguvu kabisa, akawa sasa anajaribu kumtoa
kwenye lile beseni lililojaa maji.
‘Tumekuambia
tulia, kabisa, mtieni pingu huyu,…’sauti kali ya askari ikasema.
Akashikwa
kwa nyuma na askari na hapo akawa hawezi kumshikilia tena mkewe, na akageuka
kumuangalia mkewe, na machozi yakaanza kumtoka, akaanza kulia,
‘Haiwezekani,
kwanini,…kwanini…haiwezekani, mke wangu hawezi kufa,….ha…’akasema na askari
wakawa wanahangaika kumtia pingu
‘Kwanini
mnapoteza muda, muiteni dakitari haraka…’akasema
‘Dakitari
keshafika, usitie shaka, ila wewe upo chini ya ulinzi, usivuruge ushahidi…’akasema
huyo askari.
‘Kwa
kosa gani?’ akauliza
‘Kumuua
mke wako…’akasema
‘Mimi
nimuue mke wangu, mna akili kweli nyie…’akasema
‘Umesikika
ukitoa kauli hiyo mbele ya mashahidi wengi, na ndio maana tukawa
tunakufuatilia, na kweli hilo umelifanya, kwahiyo upo chini ya ulinzi…’akasema
huyo askari
Askari
wengine wakaingia wakiwa wamevalia vifaa mikononi, wakaanza kukagua, na mmoja
akasema;
‘Tunaomba
nafasi tufanye kazi yetu, …’akasema askari na docta akasogea pale alipolala mke
wa Inspecta, akaweka vipimo vyake na kuanza kutimiza wajibu wake, na mara akageuka
kumuangalia yule askari aliyekuwa na cheo cha Inspecta, na akatikisa kichwa kama kukubali, kwa muda ule Inspecta hakuelewa ishara ile ina maana gani.
Inspecta
alishanga huyu askari kaja lini, mbona ni sura ngeni kwake, akatulia kwanza
akitaka kusikia kauli ya docta.
‘Mtupe
nafasi kwanza tuweze kufanya kazi yetu…’akasema huyo docta badala ya kusema lolote kuwa mke wake yupo vipi, akili yake haikukubali kuwa amekufa, yeye alijua kapoteza fahamu tu,....
‘Docta
mbona huendeleo kumsaidia mke wangu, …bado yupo hai huyo, mnapoteza muda…’akasema
na docta akageuka kumuangalia, na macho yalipokutana naye, akahisi kitu,
akajiuliza huyu aliwahi kumuona wapi, kuna jicho kama la dharau, au kitu fulani
ambacho Inspecta hakukielewa wakati huo.
‘Usijali,…kazi
itafanyika, ila tunahitaji nafasi…’akasema na Inspecta alipoona kama vile hao watu wanapoteza
muda, akaanza kuleta fujo.
‘Hivi
hamuoni mnapoteza muda, mke wangu hajafa huyo..kwanini docta…’akakatizwa na
askari aliyekuwa akimshikilia, akamkata ngwala, akadondoka chini
‘Mtie
pingu, asiendelee kufanya lolote…’ na Inspecta aliposikia kauli hiyo, akasema;
‘Kwanini
mnafanya hivyo, kwanini mnanifanyia hivyo, nyie hamuoni kuwa mke wangu yupo
kwenye hatari ya kupoteza uhai,…’akasema
‘Wewe
tulia,….ulipofanya hivyo hukujua utaua,…..’akasema askari ambaye hakuweza
kumtambua kwa muda ule ni nani.
‘Unajua
mimi ni nani unayeongea naye, kwanza wewe ni askari gani, sikutambui…?’
akauliza
‘Mimi
ni askari wapya walioletwa, ……nafahamu wewe ni Inspecta, lakini hapa tunatimiza
wajibu wetu, jambo ulilofanya halistahiki, tunawajibika kukutia pingu,na
kuanzia sasa wewe upo chini ya ulinzi…’akasema huyo askari, alikuwa na cheo
sawa na yeye, akakumbuka, kuwa kesho, yaani leo asubuhi, alihitajika kukutana
na askari wapya wawili ambao walitumwa kuja kuungana naye kupambana na hali
iliyokuwa ikiendelea
Alikumbuka
kauli ya mkuu wake, akiongea naye kwa simu, mkuu huyo alimwambia;
‘Nitakutumia
nguvu mpya ambayo utasaidiana nayo kuhakikisha hali ya usalama inarejea mahali
pake….’aliambiwa na ilifanyika hivyo pale alipomwambia mkuu huyo kuwa anahitaji
kikosi maalumu cha kupambana na kundi ambalo analiona ni hatari, kundi
lililojipanga vyema.
‘Kwani
kuna nini kinachoendelea?’ akaulizwa
‘Kwa
uchunguzi wangu, kuna kundi kubwa, ambalo limejijenga ipasavyo, bado
nafuatilia, nikikamilisha uchnguzi wangu nitawaambia…’akasema
‘Basi
kuna kikosi kipya kimerudi kutoka mafunzoni, nitakutumia nikikamilisha uhamisho
wao…’akasema mkubwa wao
‘Sawa
afande…’akasema, na ilipita muda bila askari hao kufika, na usiku wa jana
akaambiwa wameshafika, kwahiyo atakutana nao…
‘Ndio
nyie askari wapya waliofika…?’ akauliza
‘Ndio
sisi…’akasema huyo Inspecta
‘Ok,
ila nawaambia mke wangu akifa mkononi mwenu kwa kupoteza muda, mtawajibika, …’akasema
‘Afe
mara ngapi afande, hebu tuache tufanya kazi yetu…’akasema docta.
‘Eti
nini, hapana, haiwezekani haiwezekani, mke wangu hajafa…..’ Inspecta akawa
analia kwa uchungu, lakini askari hawakumjali, wakamkokota hadi nje, na
walipofika nje, akamuona Inspecta rafiki yake akiwa kakaa kwenye sofa, akiwa
kashikilia shavu,….
NB:
Kwa leo nimeweza kumalizia sehemu hii iliyobakia kutoka sehemu iliyopita
WAZO LA LEO: Tuweni makini sana
na kauli zetu, ulimi unaweza kukuponza, ukakutia hatiani hata kama huna makosa,
mara nyingi hali hii inatokea pale tunapokuwa na hasira. Ukikutwa na jambo la
kukukasirisha, au kutaharuki jaribu kuwa na subira, chunga sana matamshi yako kwani
sio watu wote wana nia njema na wewe, wanaweza kutumia kauli yako kukuangamiza
kwa masilahi yao.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment