Inspecta
aliondoka mapema sana kuelekea ofisini, ni kawaida yake kuwahi ofisini, hasa
akiwa na kazi inayomtinga sana. Lakini kwa vile ilitambulikana kuwa alikuwa
mapumziko ya kuumwa, asingelitakiwa kuwahi hivyo.
Akilini
alikuwa na mengi ya kufanya, na yote yalihitaji tahadhari, kwahiyo akaona ni
vyema afike ofisini kabla watu hawajafika, apitie mambo fulani fulani na
kuyaweka sawa, akajenga nadharia ya kufanya kazi ukiwa na nyuso mbili katika
utendaji wake kuanzia sasa hadi hapo atakapoona mwisho wake, alijua atashinda
tu, hata kama itachukua muda zaidi ya alivyotaka iwe, cha muhimu ni kujifanya yupo
kote kote.
‘Inabidi
nifanye hivyo,..sina jinsi, na nitaona jisni gani nitakabiliana na hili tatizo,
najua nipo peke yangu, na sioni wa kumuamini kwa sasa, lakini huko mbele
nitapata mshirika...’akasema kimoyo moyo.
Akafika
maeneo ya ofisini, na kusalimiana na walinzi wa zamu, hakuongea nao sana, na
hakuhitaji kuangalia nani kafika, alijua muda kama huo ni nadra sana kwa
wafanyakazi kuwepo ofisini, inatokea tu kama kuna kazi ya dharura.
Akaingia
kwenye ofisi yake, ambayo mwanzoni alikuwa akichangia na huyo inspecta mwenzake
lakini baadaye kutoka na majukumu ya kikazi wakapewa kila mtu na ofisi yake.
Alipofungua mlango, akasimama na kuegemea huku ngumi kaweka ukutani, na
kuigemea kwa kichwa huku akiwaza afanya nini..
Akaona
kuwaza haisaidii, akaiendea meza yake na kukaa, kwanza akapitia kwa haraka kazi
zake hakujali kama kuna mtu kazipitia, ni kawaida kama mtu anahitaji kitu
anaweza kuingia kwenye ofisi ya mwenzake akachukua anachohitaji au hata
kufanyia kazi, ilimradi hagusi kazi za mwenzake.
Hakujali sana kuangalia kama kuna mtu alipitia
kazi zake, na kama yupo atakuwa Inspecta mwenzake, yeye alichojali ni jambo
ambalo lilimfanya afike hapo ofisini mapema, na akalitafuta makabrasha
yanayohusiana na kesi iliyokuwa mbele yake, akayapitia hadi pale alipokuwa
ameiahia,...
Akatoa
karatasi za alizokuwa ameweka kuhusu utafiti wake na watu aliowahoji na kuweka
nyingine ambazo zilikuwa za awali kabisa kuwa kesi hiyo haina mshiko, kwani
marahemu alikuafa kifo cha kawaida...
Alipomaliza,
akachukua jalada jingine, akalifungua na kuandika ` kazi maalumu, akaziweka
zile karatasi na kuandika mambo fulan fulani aliyotaka kuyaandika na
alipohakikisha ameandika kila kitu, akatoa ile CD, ni nakala moja aliyoweza
kuichukua kwa siri, kwa yule jamaa wa komputa aliyemkuta kwa yule mdada.
Akaiweka
na ikaanza kufanya kazi,..kitu cha kwanza kuonekana ni nembo ya dunia na
maandidhi makubwa ya ‘Dunia yangu...’ halafu kukaanza maelezo ya mbali mbali ya
miradi, ..ilikuwa kama mradi uliobuniwa, ambao lengo ni kuzalisha na kuwekeza,
na kuwavuta vijana kujiunga,..ulindikwa vizuri sana, na mikakati mizuri..
‘Hii
mikakati ni mizuri sana, lakini hii nembo ina maana gani, je hii ni taasisi au
kampuni ya mtu binafsi...?’ akajiuliza na wakati anajiuliza mara simu yake ya
mkononi ikaita, akaangalia na kuona mpigaji hajulikani, hakuna namba, akahisi
inaweza ni simu kutoka kwa wahasimu wake,...akasita kuipokea, lakini akasema;
‘Kwanini
niogope bwana,..’akaipokea na alipoiweka sikioni akasikia sauti, sauti ambayo
ilimfanya mwili uzizime, na kuanza kukumbuka mambo mengine, ..
‘Baby
naomba tukutane Paradise hoteli, jioni, ukitoka kazini...’akasikia sauti, na
kabla hajasema lolote simu ikakatwa...
‘Baby,....nani
baby wako..na ananitaia nini huyu mwanamke...ooh, hili sasa ni tatizo..anyway
tutaona huko mbele.....’akasema huku akiiangalia ile simu, lakini mwili
ulishanyong’onyea kutokana na ile sauti, na hisia asizozitaka zikamtawala,..akajaribu
kuondoa hayo mawazo kwa kuendelea kuangalia ile CD’s..
Hakupata
maelezo zaidi, zaidi alielekezwa kufungua mtandao wao, na hata alipofungua
mtandao wao aliona maelezo hayo hayo, na walisema ukitaka zaidi ujiunge na
mtandao huo, akajaribu kujiunga lakini haukukubali.
Akaitoa
ile CD, na kuiweka ndani ya lile jarida alilolifungua na akaliweka lile jarida
mahali mahususi , ambapo hakuna mtu anayeweza kuliona, akafunga na ufungua,
halafu akasimama kujinyosha, mara akahisi sauti, akatega sikio na kuangalia saa
yake, kwa muda huo haiwezekani kuwepo mtu.
Akagundua
kuwa sauti hiyo inatokea upande wa ofisi ya pili yake ambapo ndipo alipo Inspecta
mwenzake, na anavyomjua Inspecta mwenzake muda kama huo hawezi kuwepo kazini,
akajiuliza ni nani huyu kaingia ofisini kwa mwenzake.
Kwanza
alitaka kupiga simu, kwani zipo simu za mawasiliano ya ndani kwa ndani, lakini
baadaye akaona kwanini asiende kuangalia yeye mwenyewe, akainuka na baada ya
kuhakikisha kuwa kilie alichokuwa anakifanya kipo salama, akaanza kuelekea
kwenye ofisi ya mwenzake, na alipofika akagonga mlango, lakini kulikuwa kimya,
akashika kitasa na kufungua mlango, hakukuta mtu, akawa kasimama kati kati ya
mlango, hakuingia ndani, akasema;
‘Kuna
hali inayoashiria kuwa kulikuwa na mtu humu ndani...’akasema na kwa vile taa
zilikuwa zimezimwa, akaona huenda ilikuwa ni hisia zake, au kuna panya
wamewaingilia, lakini bado akawa na mashaka, akasema kwa sauti ndogo;
‘Nina
uhakika kulikuwa na mtu humu ndani, ...lakini
ni nani huyo kwa muda kama huo, na alifika saa ngapi....’akajiuliza na baadaye, akageuka na kuurudishia mlango hakutaka
kuingia ndani kuangalia zaidi; akawa anatembea kuelekea nje na kuwakuta walinzi
wa zamu akawauliza
‘Ni
nani aliwahi asubihi ya leo kabla yangu?’ akauliza
‘Ni
Inspecta Maneno...mkuu’akasema mlinzi
‘Oh
alifika saa ngapi, na kaondoka saa ngapi?’ akauliza
‘Alifika
mapema sana, siku hizi anawahi sana, na huondoka kabla watu hawajafika,
kaondoka sasa hivi, na pikipiki, ...’akasema mlinzi.
‘Anafanya
kazi gani ya dharura ?’ akauliza
‘Hatujui
mkuu...’akasema yule mlinzi wa zamu, na Inspecta akaamua kurudi ndani kumalizia
kazi yake.
Ni wakati anapita karibu na ofisi ya Inspcta mwenzake
ndipo akaona karatasi mlangoni, ilikuwa inaonekana kipande kidogo, sehemu kubwa
ilikuwa kwa ndani, akaona ni vyema kuangalia ni karatasi gani, na kama ina
muhimu aihifadhi malai pake...
‘Au
Inspecta aliondosha wakati anatoka...’akasema, akaaona ni vyema aiangalia na
kama ni ya mwenzake akaiweke huko ofisini kwake, na alipojaribu kuivuta ikawa
haitoki, ndipo akaona ni vyema kufungua mlango ili aweze kuitoa vyema, akaufungua
mlango.
Ilikuwa
ni zile karatasi nyeupo zisizo na misitari na mara nyingi zinatumiwa kwenye
komputa, akaigeuza, kwani aliona maandishi makubwa upande wa pili yake, akaikunjua
ile karatasi na maandishi makubwa yaliyoandikwa na kalamu za matangazo
yakaonekana, akayasoma...ooh
Ulikuwa
ujumbe uliolekezwa kwa mke wake, uliandikwa jina la mke wake, halafu maelezo kuwa
yeye hatafika nyumba kwa leo...hapo hapoa, akaukumbuka yale aliyoambiwa na mke
wake kuwa kulikuwa na ujumbe uliosema kuwa yeye hatafika nyumbani, ina maana
gani sasa, umefikaje huo ujumbe hapo, ofisini kwa Inspecta mwenzake, na
akakumbuka mkewe alivyolalamika kuwa ujumbe huo haupo pale alipokuwa ameuweka...
‘Ile
karatasi yenye ujumbe wako kuwa haupo na chini yake kulikuwa na maelezo ukasema
kuna picha zako...mbona siioni, na mimi niliweka hapa, ilikuwa juu juu, na
sizani huyu mfanyakazi wa ndani kaingia na kupekua huku kabatoni, hawezi
kufanya hivyo ni wewe meichukua,?’
Akachukua
simu na kumpigia mkewe, haikupokelewa hapo hapo, iliita kwa muda mrefu halafu
mkewe akawa hewani na kuongea kwa sauti ya mtu anayetoka usingizini
‘Vipi
tena unanisumbua asubuhi hii na mapema kuna nini kimetoka, au ndio unataka
kusema hutarudi leo nyumbani, nimeshakuzoe, haya sema mimi nataka kumalizia
usingizi wangu....’mkewe akalalamika.
‘Uliniambia
uliporudi kutoka nyumbani uliona ujumbe wangu mezani, hebu niambie huo ujumbe ulikuwaje,
....?’ akauliza Inspecta
‘Ulikuwaje
kwa vipi...!’ Akauliza mkewe akipga miayo kuashiria kuwa bado ana usingizi na
anataka kulala, na kabla mume hajafafanua akasema;
‘Ulikuwa,
ni ujumbe umeandikwa kwa maandishi makubwa, sijui ulifanya hivyo kwa vile
unafahamu macho yangu yana shida ya kuona...kwanini unaniuliza hivyo...?’akauliza
mkewe na kupiga tena miayo.
‘Hamna
shida nilitaka kuwa na uhakika tu, maana sikumbuki kuandika ujumbe wowote...’akasema
‘Kama
umeandika shauri lako, huenda aliandika shetani...., kuna jingine au ulitaka
kunisumbua tu, ..’akasema mkewe sasa kwa sauti ya kuonyesha kukerwa.
‘Tutaongea
baadaye nikirudi nyumbani...’akasema na kukata simu, akaichukua ile karatasi na
kuikunja vyema akaiweka mfukoni kwa nia ya kwenda kumuonyesha mkewe akirudi
nyumbani, lakini kabla hajafunga mlango akatupa jicho kwenye komputa kubwa ya
mezani ya Inspecta mwenzake akaona kama
haijazimwa taa za nyekundi zilionekana kuwaka kwenye komputa hiyo.
‘Huyu
jamaa bwana, kwanini kaondoka bila kuzima komputa yake , au kuna kitu alikuwa
akikinakili nini, na kaacha kiendelee kujinakili, lakini hii ni hatari,..ngoja
nihakikishe...’akasema
Akasogea hadi pale kwenye hiyo komputa
kuhakiki, na kama ikiwezekana aizime, akagusa kile kitufe cha kuzimia, baada ya
kuona hakuna kitu chochote kilichopachikwa kwa nia ya kunakili faili, au jambo
lolote.
Alipogusa
kile kitufa mara ile komputa ikiwaka, na mara, nembo kubwa ya dunia ikaonekana
imetanda kwenye kiyoo cha hiyo komputa na maandishi makubwa ya kumeta meta
yakawa yanazunguka, huku kukiwa na jama akiiangalia ile duni aikizunguka na
mikono mbali mbali ikaonekana kama inaishika ile dunia, jamaa anayeiangalia
akawa anatabasamu na akawa anaongea maandishi yakitoka mdomono mwake na kwenda
kuizunguka ile komputa, maneno na maandishi yalisema;
‘DUNIA
YANGU’
‘What,..dunia
yangu..ana maana gani huyu mtu!?’ Inspecta akashituka na kukumbuka maneno hayo
ameyaona wapi, akakumbuka kuwa nembo kama hiyo hiyo aliiona kwa yule mtu wa
komputa aliyekuwa kwa mdada, akakumbuka pia aliyaona kwenye laptop ya mdada
halafu kwenye hiyo CD, aliyokuwa akiiangalia muda mfupi uliopita ile nembo hii
ya sasa ina mtu kakaa kwenye kiti kakunja nne na mikono hiyo ikiwa imeshikilia
hiyo dunia...
‘Hii
ina maana gani?’ akajiuliza kwa sauti, na mara akasikia mlango ukisukumwa akageuka
kuangalia ni nani kaingia na akajikuta akiangalia
na Inspecta mwenzake, akiwa kaweka mikono miwili katikati ya kifua na tumbo,akimuangalia
....
NB:
Nimeona siku isipite bure, angalau tupate sehemu hii ndogo, mitihani ni mingi,
lakini ndio maisha
WAZO LA LEO: Ubaya ni sawa na wizi, kama wasemavyo za mwizi ni arubaini, basi na ubaya
una kikomo chake, usione unawafanyia wenzako ubaya ukawa unashiba, unatajirika,
au unafurahia, ukajiona mjanja, ipo siku utaambuka tu, na kuzalilika, kama
ulivyodhamiria kumzalilisha mwenzako, kwani mwisho wa ubaya ndio huo, kamwe
hauna mwisho mwema, mwisho wake ni kuumbuka tu. Tuache ubaya, tutubu na kuyasafisha
mabaya hayo kwa tuliyotenda kwa kufanya mambo mema.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment