Docta akasimamishwa kazi
ili uchunguzi ufanyike, na kipindi alichosimamishwa kazi alikuwa hana pesa za
kujikimu, japokuwa alikuwa kitegemea ujuzi wake wa udakitari, na dawa kidogo
alizokuwa nazo lakini hazikuweza kumfikisha popote, kwani matumizi yake yalikuwa
mabaya, akaanza kusota, maisha yakawa magumu....
Tahamaki siku moja
akakutana na rafiki yake waliyewahi kusoma naye, akamchukua na kumpa chakula
cha mchana na hapo wakaanza mazungumzo;
Na jamaa akamwambia kuwa
wanataka waingie kwenye dili ya kipesa, na dili yanyewe inahitajia maandalizi
makubwa, gharama na uvumilivu kidogo,
‘Mimi nataka tuingie
kwenye dili za kipesa, ....’akasema huyo jamaa, na docta kusikia hivyo, `dili
za kipesa’, akagutuka, na kusafisha kichwa kwa kukitikisa, akamkodolea jicho
huyo jamaa yake, moyoni akisema; `anajileta mwenyewe’
‘Sijakusikia vyema, umesema
dili za pesa au za posa, hebu rudia tena nikusikie vyema, maana hapo
umenipandisha uchu wangu, ukitaja dili za pesa mimi napandisha mashetani, hooooho...au
sikusikia vyema, sema tena....’akajitikisa na mwenzake akatabasamu na kusema.
‘Lakini sio rahisi kama
unavyofikiria...inahitaji maandalizi na gharama....’
Ni kweli gharama
zikatumika jamaa akaenda kusoma Marekani, na huko akaonyesha kipaji chake,na
hata wenyewe wakamkubali, na Ulaya na Marekani kama una kipaji mara nyingi
wanataka ubakie huko huko, lakini jamaa akatoa udhuru kuwa alihitajia kurudi
kwanza nchini, ili kuweka mambo yake sawa, na kweli akaruhisiwa akarudi nchini.
Tuendelee na kisa chetu
Siku docta aliporejea hapa nchini kutoka masomoni Marekani, cha
kwanza kukifanya ni kuwachunguza maadui zake, kuona kama kuna usalama, na alikuja
kugundua kuwa mmoja wa maadui zake, yule mdada, siku hizi ni matawi ya juu,
sasa hivi anamiliki kampuni kubwa ya urembo.
‘Nahisi atakuwa ameshasamahe, hata hivyo ni lazima niwe makini...’akajipa
matumaini huku akiendelea na mikakati yake ya kuanzisha hiyo hospitalini akaipa
jina ambalo, alijua haligundulikana kuwa ni yeye, moyoni alikuwa na wasiwasi,
na hakuna kitu alichokigopa kama kwenda jela,...
‘Hata jina nitatumia jina jingine, japokuwa kwenye vyeti, sitaweza kubadilisha kitu...’akasema na kweli
wafanyakazi wake wakawa wanamuita kwa jina hilo alilolibuni yeye mpaka
likazoeleka hivyo.
Baada ya muda akawa ameshafanikiwa kwa kiasi kikubwa, kwani
hospitali aliyoinzisha ilikuwa ikimiminika kwa wingi kila aliyetibiwa hapo
alikuwa wakala wakufikisha ujumbe kwa wengine;
‘Kuna hopitali moja imeanzishwa ni kiboko, kuna docta aliyetoka
Marekani, anajua kazi yake, matatizo ya akina mama, matatizo ya akili, ...yaani
utamwambia tatizo gani ashindwe kulitatua, kweli ana kipaji...’mmoja wa
waliotibiwa hapo akawa anawaambia wenzake.
‘Ni Mmarekani kweli?’ akauliza mwingine
‘Sizani, nahisi ni Mtanzania aliyebobea huko, alisoma huko, na
karudi kuwekeza nyumbani kwake,hata Kiswahili chake ni cha shida....’akasema
mwingine.
‘Nitampeleka mke wangu maana anasumbuliwa na matatizo ya uzazi, ni
miaka mitano sasa akishika mimba inatoka...’akasema
‘Hapo umefika, wahi mapema, maana watu wanavyojaa, ni balaa...’akasema
mwenzake
Sasa ikawa kila aliyetibiwa hapo akawa anapeleka taarifa kwa
wengine, na taarifa zikaenea kwa haraka, na jamaa akajua sasa anatakiwa awe
makini zaidi, akaachia ndevu, na kuwa habanduki na mawani usoni kuficha sura
yake, hata hivyo, hilo halikusaidia, kwani pamoja na kupata elimu na utaalamu
wake, udhaifu wake wa kunywa pombe, haukumtoka, pombe ikawa ni tatizo kwake, na
akilewa hujisahau akavua mawani, akaonekana na watu
Juhudi zake zikamsaidia, ikabidi sasa atafute wasaidizi,
akawachukua watu anaowafahamu, ambao alijua hawatamsaliti, akawapa shule ya
kile alichoona wanaweza kumsaidia, na akawa anawalipa vizuri, na mmoja wa
marafiki zake wa zamani, akamteua kuwa mwekezaji mwenzake, lengo ni kuwa
akiondoka, huyo ataendeleza kazi aliyoianza, na huyu rafii yake alikuwa mmoja
wa madakitari bingwa, kwahiyo kazi iliendelea kama kawaida.
Siku moja wakakaa na rafiki yake huyo na akaona amwambie ukweli,
kuwa yeye hatakaa sana hapa nchini, ana kazi anakwenda kufanya huko Marekani,
na kwahiyo yeye atamwachia kila kitu
‘Mimi nitarudi tena majuu,
kwahiyo wewe utashika usukani wa hii hospitali, nakuaminia rafiki yangu hii iwe
ni kitega uchumi chetu...unaona mambo yanavyokwenda, hapa hatuna shida tena,
sasa tusiangushane....’akamwambia.
‘Usiwe na wasiwasi na mimi, tumetoka mbali, mimi nitahakikisha
kila kitu kinakwenda bara bara...hapa ni mwanzo tu, wewe mwenyewe utaona, wewe
nenda kahangaike huko, na unipigie debe na mimi nikasome zaidi....’akaambiwa
‘Usijali na mimi ndio lengo langu, nataka tuwe na matawi mengi
nchi nzima, na humu kuwe pia kama chuo, mimi nitafanya yote, udakitari na
kufundisha kile ninachokijua, kwa madakitari wetu....’akasema
‘Hilo ni muhimu sana,....’akasema mwenzake
Ni kweli huyo msaidizi wake, alikuwa naye mmoja wa madakitari
wazuri, na hata kaam hayupo, yeye aliweza kufanya mambo mengi, japokuwa hakuwa
na utaalamu kama aliokuwa nao yeye.
Siku aliyoongea na huyu msaidizi wake, ndio siku ambayo alipokea
simu kutoka Marekani kuwa anahitajika, nafasi yake bado ipo, na akawajibu yupo
tayari kwenda huko, na wao wakamwambia kama ni tatizo la usafiri, wao
watagharamia kila kitu, na kweli wakatuma stakabadhi ya usafiri,...
‘Ok, sasa najipanga
kuondoka, wiki ijayo, napanda ndege kurudi kwa wazungu...’akasema kwa
kujiamini, lakini....
*******
Dakitari alisogea dirishani, na kuchungulia kwa nje ili
kuhakikisha kuwa huyo anayemuhisi ndiye huyo kweli,je ndio huyo dada, mmoja wa maadui zake, aliokuwa
akiwakimbia.
Taratibu akafunua pazia la dirishani na kuchungulia nje, huku nesi
akimuangalia kwa mshangao. Jamaa jicho lilipotua kwenye gari, akaachia lile
pazia kwa haraka, akasema kimoyo moyo;
‘Oh ni gari lake,..lakini mbona sijamuona...’akasema na kuinua
pazia tena kuchungulia ni kweli lilikuwa gari la yule adui yake, lakini yeye
mwenyewe hakumuona sehemu ile ya kusubiria wagonjwa, akageuka kumuuliza nesi
wake ili aweze kumuuliza huyo mwanadada mbona hayupo hapo nje...
Alipogeuka kuangalia, alikutwa na mshutuko mkubwa, karibu
akadondoke, maana pale alipokuwa kasimama nesi wake, sasa alikuwa kasimama huyo
mwanadada mrembo, akiwa kashikilia miwani kwenye mkono mmoja na kuigonga gonga
kwenye kiganja cha mkono mwingine, huku akibenua mdomo kwa dharau
Wakaangaliana...na taswira ya tukio lililopita, vile alivyomtendea
huyo mwanadada, lilitanda kichwani mwa
docta, na kumfanya ahisi kujisaidia, hata hivyo akajipa moyo, na kujitutumia,
akataka kusema neno lakini yule mwanadada akamuwahi kwa kusema;,
`Doctor, docta, unarudi bila hodi, ..hahaha, ok, lakini mbona umenisubirisha
sana nje, tofauti na nilivyosikia sifa zako,...ok, lakini kwanza hapa nina RB
yako...’akasema yule mdada akiwa anatoa karatasi kwenye mkoba wake, na kushikilia
karatasi, ilikuwa ni karatasi kutoka kituo cha polisi cha kutaka huyo jamaa
akamatwe kwa kushukuwa kubaka, na kutoa mimba kinyume na sheria za nchi, na pia
kwa kumharibu kizazi huyo binti.
Nesi alikuwa bado kasimama nyuma ya mlango, alikuwa
hajaondoka,akasikia hayo maneno, akashindwa kuvumilia,na akajikuta akiuliza;
‘RB!!?...RB, yanini tena mungu wangu...’akasema
‘Mungu wako wa nini, hebu ondoka hapo bosi wako anafahamu RB, ya
nini,...naomba uondoke hapo mlangoni, haya hayakuhusu...’akasema huyo mdada kwa
sauti kali, na yule nesi akaondoka, akiwa na wasiwasi na bosi wake kuwa leo kaja
kukamatwa kwa kosa ambali hakuweza kulifahamu, yeye anachojua kuwa bosi wake ni
mtaalamu toka Marekani, japokuwa ni Mtanzania.
Yule mdada akahakikisha kuwa yule nesi ameondoka kabisa pale
mlangoni, akafunga ule mlango, na kumgeukia docta, akasema;
‘Docta unafahamu fika kuwa unatafutwa na polisi, unakumbuka kosa ulilolifanya,
sitaki kukumbusha,maana kila nikiliwazia, natamani niwe na bastola nikipasue
kichwa chako,.. lakini kwa hivi sasa hayo tuyaache...’akasema na sasa akawa
anarudisha ile karatasi kwenye mkoba wake, na docta akapumua kidogo.
‘Haya tuyaache, ila mimi
nimekuja na jingine muhimu kwako, hii RB na mambo ya polisi yanaweza kuja
baadaye, kwa leo, chenye umuhimu ni hii kadi...’sasa akatoa kadi kwenye mkoba
wake.
‘Hii kadi ni ya mualiko maalumu.....’akasema na docta akiwa
anapumua kidogo, akahisi kuna kuna mtego mwingine, na aliposikia kadi ya
mualiko, akahisi ni mtego wa huyo mwanadada, nay eye hakutaka kujionyesha zaidi
kwa jamii, akauliza;
‘Kadi ya nini...?’ akasema kwa sauto ya mkwaruzo na yule mwanadada
akamuangalia kwa macho ya udadisi na kubenua mdomo kwa dharau, akasema;
‘Hii kadi imetoka kwa bwana mmoja unayemfahamu sana...’akasema,
huku akiwa kaishikilia ile kadi mkononi, akiipepea huku na huku,
‘Bwana gani...?’ akauliza docta huku akionyesha wasiwasi, hakutaka
kabisa kujihusisha na jambo lolote zaidi ya maandalizi yake ya kwenda Marekani,
na alishaanza kujenga hoja za kumshawishi huyo mwanadada, ikibidi waingie ubia
naye, hayo yaliyotokea nyuma yaishe, kwanza moyoni alishampenda.
‘Bwana Di-amu....’akalitaja hilo, na docta hakuweza kuficha ule
mshituko alioupata ilikuwa kama mtu kaguswa na waya wa umeme
‘Eti nini, Di-amu..., hapana...’akasema kwa wasiwasi na mshangao,
kwa sauti ya kukoroma maana mdomoni mate yalishamkauka na hapo alitamani kupata
kinywaji ili akili iweze kufanya kazi vyema.
Jina hilo lilimfanya akose raha, alijua huyo anaweza kuwa kikwazo
kikubwa sana kwenye safari yake ya kurudi Marekani, sasa akajua keshapatikana na
safari yake ya Marekani inaweza kuingia dosari, akataka kusema neno, lakini mwanadada akazidi
kuongea
‘Natumai unamfahamu vyema huyo mtu, na wajibu wako kwake, cha
muhimu, kabla hujafanya lolote, kabla hujapanda ndege kurudi huko Marekani,
kitu ambacho sizani kama kitakuwepo tena, unahitajika kufika huko
ulikoelekezwa, ukisoma hii kadi itakuelekeza yote...’akasema huyu mwandada akisogea
pale aliposimama huyo docta.
‘Kama sitaki ...na siwezi, nina mambo yangu mengi....’akasema
‘Hahaha, docta, docta,....umesahau eeh, kuwa unatafautwa na
polisi,..umesahau eeh, yale uliyonifanyia, ...docta fikiria kwa makini,
unaifahamu jela wewe...’akasema mdada
Docta akawa sasa anahema kwa haraka, alitamani apate kinywaji,
bila kinywaji haweze kuongea kwa jaziba,...docta alijikuta akiwa imekuwaje huyu
mwanadada awe na mafungamano na mfadhili ambaye sasa alishapanga kumsaliti ....
‘Oh, kumbe huyu mwanadada ni kitu kimoja na Diamu, mbona nimeshapatikana..’akasema
kimoyo moyo, na mwanadada bado akiwa kashikilia ile kadi, na alionekana hataki
kuondoka mpaka ahakikishe huyo docta amekubaliana na huo mualiko, akasema;
‘Unasikia vyema, ukikosa kufika kama ulivyoelekezwa, huyo bwana
Diamu, kasema yeye mwenyewe atahakikisha anakufikisha polisi, nimeshampa nakala
ya hii RB,...’akasema huyo mwanadada, na jamaa akawa kimiya.
‘Natumai unakumbuka kosa
lako, kosa lako lipo kituo cha polisi, wao muda wowote wanaweza kukukamata,
hata huko uwanja wa ndege wameshaweka watu wao, anayekudhamini kwa sasa ni huyu
Diamu, nikuambie ukweli, kama asingelikuwa ni huyo jamaa, ungelishakamatwa
muda mrefu tu, siku unakanyaga uwanja wa ndege kutoka huko Marekani mimi
mwenyewe nilikuwa hapo uwanja wa ndege, nilikuwa nimetoka safari zangu,
nikakuona...’akasema
‘Nilipokuona nilitamani kutapika, nikikumbuka yale uliyonifanyia,
nikataka kupiga simu polisi, lakini nikaingiwa na uungwana, nikaona nikupe
nafasi, uje , uonane na jamaa zako...nikawaarifu polisi, na sasa niliongea na
mkuu wa kituo, akalifufua jarida lako, nay eye mwenyewe akasema atalifuatulia,
huyo mkuu wa kituo, ni mmoja wa jamaa zangu...’akasema
‘Wakatumwa wapelelezi kuhakikisha kuwa hupotei, na mimi mwenyewe,
nikawa nakufuatilia hatua kwa hatua, hadi unafungua hospitali yako mimi
nafahamu, na mimi mwenyewe kwa kuhakiki, niliwahi kuja kutibiwa hapa, japokuwa
niliyeonana na huyo msaidizi wako....’akasema
‘Nafahamu yote, na jinsi unavyowasiliana na watu wako huko
Marekani, jana walikupigia simu kuwa unahitajika kwenda, nafahamu yote, kuwa
sasa unajiandaa kurudi Marekani huko wamekuahidi kazi nzuri, lakini ukumbuke,
mwenye kovu hata siku moja usizani kapoa...kovu uliloniachia ni kubwa
sana,.....’akasema huyo mwanadada, japokuwa alishasahau na ujasiri
ulishajijenga lakini alipofika hapo machozi yalimlenga lenga.
Yule docta akabakia ameduwaa, hakujua afanye nini, alijua kabisa
alishafanya kosa, na hapo alitaka kumwambia huyo mwanadada kuwa atatumua ujuzi
wake wote kuhakikisha anamwezesha huyo mwanadada kurekebishwa kizazi chake
tena, lakini kwa jinsi anavyofahamu itakuwa vigumu, lakini ...
‘Sasa basi,uamuzi upo kwako, uwe na Diamu, ili aendelee kukudhamini,
au uachane naye, ujitutumue kupanda ndege, na nitahakikisha, kuwa siku hiyo
unakamatwa na unakwenda jela...
‘Nina kisasi na wewe, nitahakikisha unakwenda jela, unasikia, hapa
nilipo natamani nikufanye kitu mbaya, mimi sio yule mdada aliyefika kwako
akilia tena...hili chozi linalonilenga lenga, ni kwasababu nakuona bado upo
hai,...’akasema akionyesha uso wa hasira, chuki...
‘Nikuambie ukweli, mimi ni mtu mwingine, nafahamiana na wakubwa,
hapo polisi kuna watu wangu, na wameshalifufua jalada lako la mashitaka,
wameshakusanya ushahidi wote unaohitajika,...mshukuru sana huyo bwana Diamu....’akasema
huyo mdada sasa akamsogelea karibu na wakawa wanaangalia uso kwa uso.
‘Haya niambie docta unasemaje, ...utakwenda kuonana na Diamu, au
nifanye kazi yangu?’ akauliza huku huyo mdada akinyosha mkono kumkabidhi huyo
docta hiyo kadi....
Docta taratibu akainua mkono, huku mkono ukimtetemeka,....
NB: Hebu niambie umeionaje sehemu hii...tuwe pamoja yote haya
yanapatika ndani ya diary yangu , na huyo ni mtu mwingine, akitafutwa kuingia
kwenye mtandao wa Diamu, je alikubali, je safari ilikuwepo..., tuzidi kuwemo
WAZO LA LEO:Maisha ya ujanja ujanja
yana mwisho wake, usione umefanikiwa na mali ya dhuluma ukafikiri umeshinda,
hapana dhuluma uliyomtendea mja wa mwenyezimungu haiishi kirahisi, dhuluma hiyo
itakuandama, ni swala la muda tu, hujui lini hali itabadilika...
Angalia mifano hai, wangapi wangapi wanataabika kitandani,
wakijuta kwa yale waliyowatendea wenzao, dhuluma wizi, ufisadi, ilikuwa kazi
yao, wakatajirika, sasa wapo kitandani, hawajiwezi, utajiri wao hauwezi
kuwasaidia tena, mali ya dhuluma haina msaada tena, waliodhulumiwa wanazidisha
kilio, na kilio cha mwenye kudhulumiwa hakina kinga,...
Oh, ewe mja wa mwenyezimungu, jamaa, tajiri, bosi, muheshimiwa,tubu
makosa yake, muombe msamaha uliyemkosea, rejesha mali ya dhuluma kwa wenyewe
kabla mlango wa toba haujafungwa....
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment