Kumbe aliyeniokoa alikuwa
mtoto wangu…..’akaendelea kuongea mama kuhusiana na kisa chake.
‘Mtoto wako, ina maana
ni mimi mama, mbona nimesahau?’ nikamuuliza mama na yeye akachekea huku
akiendelea kunisimulia kisa cha maisha yake….
*******
Kipindi mazungumzo yanaendelea kumbe mtoto hakuwa na amani, akaingiwa
na wasiwasi kuwa huenda hawo watu waliopo ndani wanaweza wakamdhuru mama yake,…,
akawa anacheza karibu karibu na mlango,hakuenda mbali, kama nilivyotarajiwa,
alikuwa akichezea kigari chake alichopew na baba yake mkubwa pembeni ya mlango,
huku akiangalia kwa ndani kwenye upenyo wa mlango, kuhakikisha kuwa mama yake
hadhuriki...
Na aliposikia sauti za ukali kutoka kwa baba yake mkubwa,
akahisi hatari akafungua mlango kidogo,na kuchungulia ndani, na hapo ndipo
akaona baba yake mkubwa akiwa anamkaba mama yake. Japokuwa alikuwa mtoto,
hakuweza kuvumilia, akaona ni lazima afanye lolote, kumuokoa mama yake,
akageuka nyuma,… na bahati nzuri akamuona huyo mtu akipita barabarani, wazo la
haraka, likamjia alichofanya ni kumkimbilia na kumweleza ni ni kinachotokea huyo
mpita njia.
Kiukweli huyo mtu alikuwa na safari zake lakini mara kwa
mara alipendelea kupita kwa huyo mama na kumsalimia kumjulia hali,….lakini leo
alikuwa kikazi zaidi, alikuwa katumwa na ofisi, hakutaka kupoteza muda, sasa
kasikia kuna tatizo kwenye hiyo nyumba, ikabidi kwa haraka , kutokana na kauli
ya mtoto aingie ndani ya hiyo nyumba, kuona kuna nini, …..
Akafika kwenye mlango wa hiyo nyumba, na akagonga mlango mara
moja , na mara pili akawa keshaingia ndani, hakusubiri kukaribishwa.Aliogopa
asichelewe na kukuta mtu keshaumizwa au kuuwawa…
‘Kuna tatizo gani humu ndani ….’Akatoa sauti kali ya
kiaskari, na suati ile iliwashitua wote waliokuwmo humo ndani,…sauti hiyo ikamzindua shemeji ambaye kwa hasira zake
hakujua kile kitendo alichokuwa kikifanya kuwa kingeliweza kumtoa mtu roho, alikuwa
kanishikilia shingoni kwa nguvu, na hata sauti ilikuwa haiwezi kunitoka, ulimi
ulishaanza kunitoka, na macho yakwa ynanitoka kwa woga, hata pale nilipojaribu
kuutoa mkono wake sikuweza kufanya hivyo, nahisi ndipo wakati kisu kiliponyoka.
Shemeji mdogo, ambaye alikuwa kashikwa na butwaa, pale kaka
yake alipoanza kuonyesha dalili za hasira, hakuweza hata kuinua mkono kumshika
kaka yake, lakini hatua aliyoiona kwa muda ule , akamsogelea kaka yake na
kumshika mgongoni, na kaka yake alipoguswa tu, na huo mkono bila kugeuka, akageuza
mkono wake, huo ulikuwa huru,na kwa nguvu moja akamsukuma mdogo wake, na kwa vile mdogo wake hakujiandaa na huo
msukumo, akajikuta akiserereka hadi sakafauni na ni muda huo huo, ndipo mlango
ukafunguliwa na aliyeingia kumbe alikuwa ni askari akiwa kavalia kiraia.
‘Hakuna tatizo afande….’alisema shemaji mdogo,akijizoa zoa
skafuni, na kaka yake, aligeuza kichwa kwa haraka kutizama ni nani aliyeingia,
na alipooona ni nani, akamwachia shemeji yake na kujifanya kama vile alikuwa
akimshika shika shameji yake shingoni.
‘Oh, afande hakuna tatizo, nilikuwa nafanya mzaha na shemeji
yangu hapa….’akasema na mimi ndio nikapata muda wa kupumua, na kikohozi
kikanishika, nikakohoa mfulululizo….mwili mzima ulikuwa hauna nguvu,nikajikuta
nikikaa chini bila kupenda.
‘Unafanya mzaha na shemji yako, huo mzaha gani wa kumkaba
mtu hadi anakosa hewa,…kumbe ni kweli eeh,…sasa upo chini ya ulinzi, kwanza kwa
kuhusika na mauaji yanayoendelea hapa kijijini,…nilikuwa njiani kuelekea kwako,
sikujua kuwa nitakukuta hapa, na pili, kwa kutaka kudhuru….’akasema huyo
askari, akitoa pingu tayari kwa kumfunga shemeji mkubwa, hapo moyo wa huruma
ukanijia.
‘Afa—fa-nde, hakuna shida…’nikasema na nikamgndua yule
askari, ambaye alinitupia jicho mara moja,akasema.
‘Hakuna shida eeh, unafikiri kama nisingelifika mapema hapa
ungelikuwa wapi wewe…, kweli najua hakuna shida,….mimi sio mjinga kihivyo,
natimiza wajibu wangu kisheria…hata kama hamtatoa ushirikiano…’akasema huku akimshika huyo jamaa mikono kwa nyuma.
‘Nyie wanawake mtauliwa majumbani kwenu kwasababu ya ujinga
wenu, hili nimelishuhudia mwenyewe, kwa macho yangu, kama sitafanya jambo, hali
hii inaweza ikaleta madhara kwenye hiki kijiji, ni lazima tatizo hili likome
kabisa hapa kijijini…’akasema huku akimfunga pingu shemeji mkubwa ambaye
alionekana kutahayari, hakuleta ubishi, akatulia hadi pingu zikafungwa
mikononi.
‘Afande, umeingia nyumbani kwa mtu, bila hodi, na kumshika
mtu bila kosa, huoni kuwa unakiuka sheria?’ akasema shemeji mdogo.
‘Na wewe mwanasheria unatetea uhalifu, hivi kweli hapa
nimekiuak sheria, unadiriki kutoa kauli hii wakti umeona fika, kuna mtu alitaka
kudhuriwa…?’ akauliza.
‘Afande hizi hasira tu za kujibishana maneno, hakukuwa na
lengo baya….’akasema huyo mwanasheria.
‘Hivi wewe kweli unfahamu sheria vyema, wewe ndiye kijana
wetu tulitegemea tushirikiane kuondoa huu uchafu unaoendelea hapa kijijini,
wewe unaufumbia macho, ulikuwa kimiya wakati kaka yako…..’akasema .
‘Hapana afande, wakati unaingia ndio nilikuwa najaribu
kusuluhisha,…’akasema.
‘Ahaa..kumbe unafahamu hilo, kuwa kaka yako alikuwa anataka kumdhuru mtu, hebu niambie….na pili
heni niambie kwanini ulikuwa umedondoka sakafuni, kama sio ulikuwa ukijaribu
kumtetea huyo shemeji yako mhalifu…na ilionekana kushindwa kufanya lolote, je
kama nisingelifiak mapema, ingelitokea nini, au kwa vile huna uchungu na huyo
mwanamke…’akasema.
‘Wewe kijana wakati umefika wa kulikomesha hili tatizo hapa
kijijini. Mimi ni askari, na bahati nzuri nimezaliwa hapa kijijini, huwezi
kunidanganya kitu…kama wewe umedanganyika na familia yako, iendelee kuharibu
amani ya hiki kijiji, mimi sijadanganyika….’akasema huku akimwelekeza shemeji
mkubwa kutoka.
‘Twende kituoni, bwana mzee, mimi natimiza wajibu wangu,
sitaweza kuvumilia hii hali…’akasema na wakaanza kutoka nje.
‘Na wewe mdogo mtu, kama unataka kuja kumtetea kaka yako
fika kituoni, na nakutahadharisha ufuate sheria, maana kaka yako huyu kakalia
kuti kavu…ana kesi nyingi za ubabe wake, sijui kama sfari hii ataokoka….’akasema
wakiwa wameshatoka nje, hapo shemeji mdogo, akaniangalia kwa macho yaliyojaa huruma na
kusema;
‘Shemeji pole sana, ngoja niwafuate hawa watu, maana hili
sasa limekuwa ni tatizo, sijui kwanini kaka yangu anashindwa kuhimili hasira
zake…’akasema.
‘Sasa hivi ndio unaongea, wakati kaka yako alikuwa karibu
kunitoa roho,anataka kuniua huku wewe umetulia,hukuweza kabisa kufanya lolote,
na…’nikasema.
‘Shemeji, shemeji…nilijitahidi kukusaidia, lakini namfahamu sana kaka yangu,
akikasirika, hashikiki….nakuomba shemeji ukiulizwa useme hakukuwa na tatizo
lolote…ili umuokoe kaka, huyo ni shemeji yako, baba mkubwa wa mtoto wako…..nakuhakikihishia tutayamaliza haya yote kwa amani kifamilia...’akasema.
‘Unasema nidanganye kuwa kulikuwa hakuna tatizo...kweli kulikuwa hakuna tatizo, tusidanganyane, najua damu ni nzito kuliko maji,....wewe mwenyewe ulijionea ni nini kama yako alitaka kukifanya, je angeniua ungelikuja kusema nini….na wewe mwanzoni ulijadi
kuwa umeachiwa hii familia kuilinda, ndio kuilinda hi familai kwa namna hiyo…..sikuelewi
kabisa, ngoja huyo kaka yako akafundishwe
adabu….’nikasema.
Na yeye akaniangalia kwa macho ya kushangaa, na haraka
akageuka na kutoka nje, na alipotoka tu, mtoto wangu akanikimbilia na
kunikumbatia akisema;
‘Pole mama, ….nilimuona huyu mtu, kumbe ni askari
nikamwambia kuwa baba mkubwa anataka
kumuua mama, …’akasema huku akihema kama vile alikuwa anakimbia.
‘Ahsante sana mwanangu, umefanya jambo la maana….’nikasema.
‘Mama kwanini baba mkubwa
alitaka kukuua…..?’ akauliza huku akiwa kalishikilia gari lake mkononi.
‘Hakuwa anataka kuniua, …..aliku-wa-ameka-ka-sirika
tu,…..’nikasema huku nikishika shika shingo yangu kuhakikisha mfupa wa shingo
haujavunjika maana ilikuwa kama komeo la chuma lilikuwa limeshika shingoni
mwangu, hata kisu kilivyonidondoka mkononi, sikuweza kutambua.
‘Mama kwanini baba mkubwa ni mkali sana….?’ Maswali ya mtoto
yakaendelea.
‘Kwasababu ni baba mkubwa, …hataki kuchezewa…’nikamjibu huku
nikiwaza tukio zima,niliwaza mengi, hasa ya huyu shemeji mkubwa ambaye alishakamatwa
na polisi, nikajiuliza je kama nitaitwa huko mahakamani kwa ajili yake nitasema
nini,……je nikubali kuwa huyo jamaa alitaka kunidhuru, ili akapambane na mkono
wa sheria, au nikatae na kusema ….
Kama nitasema ukweli, jamii na familia nzima itanisakama na
kuniona sina ubinadamu, hakuna atakayekumbuka kuwa huyo jamaa angeniua kama isingelikuwa
huyo askari kuja kwa wakati, muafaka. Najua hata semeji mdogo alishaanza kunishawisi
nikatae kuwa huyo jamaa hakuwa na lengo baya kwangu. Nikamwangalia mwanangu
akiwa anachezea kigari chake alichopewa na baba yake huyo mkubwa na hapo
nikasikia maneno yake akiongea na mtoto wangu;
‘Haya chukua zawadi
yako hii, kachezee, hizi ndio zawadi za kuchezea, usichezee uchafu, unanisikia
eeh, mtoto mnzuri, mimi ni nani….’
Lakini wakati namuhurumia huyo shemeji yangu, nikakumbuka
maneno ya huyo polisi , siku moja tulipokuwa tukiongea nay eye. Huyo askari
polisi ni mmoja wa wazaliwa wa hapo kijijini siku moja nilikutana naye
akaniambia anasikitishwa na uvunjifu wa amani hapo kijijini, na yeye akaapa
kuwa atafanya kila awezavyo kuhakikisha kuwa amani na utulivu vinakuwepo hapo
kijijini.
‘Tatizo kubwa ni wanakijiji wenyewe…..’akasema.
‘Kwanini unasema hivyo…?’ nikamuuliza.
‘Unauliza kwanini, wakati nyie wenyewe mnafahamu fika kuwa
mnayo nyoka ndani, lakini hamshirikiani kumuua,….na nyoka huyo ana sumu kali. ….’akasema
kwa mafumbo.
‘Ndio hali ilivyo, unajua wengi wanaogopa kuwa wakubwa wanalindwa,
ukiongea tu, unaweza ukajikuta wewe mwenyewe uliyejitolea kuongea ukweli unaingia matatani…’nikasema.
‘Hakuna cha kulindwa wala nini, ni uwoga wenu na uzumbuekuku
wa wanakijiji wenyewe, amukeni mtetee haki zenu, amkeni, muwafichue watu wahalifu
ili hata kama utaonekana mbaya, lakini familia zenu zije kuishi kwa amani…..’akasema.
‘Tatizo na nyie maaskari, mnatusaliti, tunaweza tukajitolea
na kuja kuwaelezea kuwa mtu fulani ni mvunja amani, lakini nyie badala ya kumshughulikia
yeye, mnakwenda kuongea naye, mnaelewana,
na huyo aliyejitolea anageuziwa kibao…’nikasema.
‘Sio kweli….kama mna umoja wa dhati, na mpo pamoja
kuwafichua wahalifu,hilo halitawezekana, maana sisi ni watendaji tu, ….nyie
ndio washika dau, mkitaka kuwe hivi au vile mnaweza, lakini muwe kitu kimoja,
na muhakikishe mnasimamia kwenye haki na kweli, tatizo ni kuwa nyie wenyewe
mumejigawa mapande mapande….’akasema.
‘Hilo ni kweli, kuna ukoo mashuhuri, kuna watu mashuhuri, …..na
wengi wanaangaliwa kutokana na hali za kipato chao, cheo chao….na..na, .
Mwenyewe unajua toka lini maskini akawa na haki ..’nikasema.
‘Huo pia ni unyonge wa kujitakia, haki haina cha umasikini
au utajiri…kukitokea kuonewa kwa masikini kutetewe sawa kama kwa tajiri , halikadhalika,
tatizo likitokea kwa watu mashuhuri, litetewe sawa sawa na wale wasio masuhuri,
mkikubali kujigawa kwa makundi ya namna hiyo, mkawa mapande mapande kwa hali za
kimaisha, itikadi za imani, itikadi za kikabia, ukoo….katika kutetea haki basi
dhuluma inapenyeza makucha yake, na hali kama hiyo inajenga uhasama na chuki,
na baadhi ya watu kuona kuwa wao wanaonewa….’akasema.
‘Ni kweli afande, sasa wewe utatusaidiaje?’ nikamuuliza.
‘Kwanza mjisaidie wenyewe…mimi sitaweza kuwasaidia kama nyie
wenyewe hamtaweza kujisaidia, mimi kama mlinda amani, nikiona kuna tatizo
,nitatimiza wajibu wangu na kuwafikisa wausika kwenye vyombo stahiki, lakini
mwisho wa siku, lazima sheria za kimahakama zihakiki kosa hilo, na ili
ijulikane kuwa ni lazima waite mashahidi walioshuhidia, au wanaofahamu uhalifu
wa huyo mtu kama mashahidi….je kwa mfano kama wewe limetokea tatizo eneo lenu, upo
tayari kusimama kizambani na kutoa ushahidi wa uhalifu, hata kama uhalafu huo
kautenda ndugu yako…ukoo wako, mtu wa imani yako?’ akaniulizwa.
‘Kama ni muhalfu kweli nitasimama na kusema ilivyokuwa…maana
nikificha uhalafu mwisho wa siku ninaweza na mimi nikakutana na janga kama hilo….’nikasema.
‘Wewe unasema tu kwasababu tunaongea, lakini mimi naifahamu
vyema jamii yetu hii ninayoishi nayo, wakinamama kila siku wanapigwa,
wanaumizwa, lakini kesi ikipelekwa mahakamani, utasikia watu wamekwenda kwa hakimu
na kumuomba kuwa kesi hiyo ikaongelewe nyumbani, na ikifikia hapo, ujue,
wameshaitana pembeni, na mwanamke aliyeumiza kahadaiwa, au katishiwa, ….basi
tena, yule askari aliyewajibika kusaidia kumkata huyo mhalifu anaonekana mnoko,
mtu mbaya. Hapo unafikiria nini….?’ Akauliza.
‘Ni huruma, na ujinga…’nikasema.
‘Sio huruma, …ni hivyo unavyoita kuwa ni ujinga, maana huyo
aliyevunja amani, akamuiza, atakuwa haogopi kutenda hilo kosa tena, na wengine hawatajifunza,….
ndio maana unaona uvunjifu wa amani, unaongezeka kila siku, …..sababu kubwa ni
kutokutimiza wajibu wenu kama raia,…..raia mwema anatakiwa kusirikiana na
vyombo vya usalama, …kama nyie hamtoi msaada wa kufichua uhalifu, sisi kama
watendaji tutafanyaje…..nakubali kuwa na sisi pia kuna wenye udhaifu, wakiona
hivyo wanatumia usemi usemao mwenye kisu kikali ndiye mla nyama…..eeh, ..ndio
maisha tumeyachagua wenyewe, …tusilaumiane kwa hilo….’akasema.
‘Nimekuelewa afande, mimi ninakuahidi kuwa likitokea tatizo
kwangu, nitakuwa nawe bega kwa bega, kuhakikisha sheri inafuata mkondo wake,
maana nisipoziba ufa nitakuja kujenga ukuta kwangu kwa gharama kubwa sana….nipo
na wewe afande…’nikasema.
‘Sisi tupo, ahadi kama hizo tumezisikia sana…na watu kama
sisi ambao tumeamua kujiunga na kazi hii kwa moyo mmoja, hatutavunjika moyo,
hata kama nyie raia mtashindwa kushirikiana na sisi….mimi nikiona uhalafu
nitaufanyia kazi, wewe raia ukisindwa kutimiza wajibu, ni shauri lako, ….maana
kuna leo na kesho, usije ukalalamika siku maji yakikufika shingoni…..’akasema .
‘Nashukuru sana afande, tunahitajia watu kama nyie….’nikasema
na kuagana na huyo afande.
Haya, leo hii huyo afande kajitolea kumnasa huyu jamaa,
shemeji mkubwa, kiongozi wa familia ya marehemu mume wangu, ambaye alitaka
kunitoa roho….je nikae kimiya, nimsaliti huyu askari polisi, au niwe pamoja na
wanajamii…?’ nikajiuliza huku nimeshika kwa mawazo.
Mara mlango ukagongwa, na sauti ya shemeji mdogo, ikasikika,
nikajua sasa mambo yameiva ninaitwa kutoa ushahidi, au hunda kaja kunibembeleza
ili nisikubali hayo yaliyotokea, ….nikafungua mlango, na nikajikuta nikiwa
nimesimama mbele ya kundi la wazee, wakiwa wameongozana na huyo shemeji mdogo,
akiwemo na mjumbe
‘Mbona ugeni wa ghafla….?’ Nikauliza.
‘Wazee hawa wamekuja kwa ombi moja, …kaka yangu yupo
matatani, na wewe peke yako ndiye utakayeweza kumsaidia, tafadhali shemeji,
tupo chini ya miguu yako….’wakasema na kwa mbali nikamuona baba wa kufikia
akija kuelekea hapo nyumbani huku akichechemea na bakora, kuashiria madhara
aliyoyapata kutokana na hawa hawa watu.
Je nitafanyaje…
NB: Kwa leo naishia hapa ngoja nikajiandae kumpokea Raisi wa
Marekani, Baraka Obama japo kwa kuteseka kwenye foleni za daladala, maana ….kufa
kufaana, na mgeni aje mwenye afanye nini vile..?.
WAZO LA LEO:
Uvunjifu wa amani, ukiukaji wa sheria, yote haya yanafanyika katika maeneo
yetu, iwe majumbani, mitaani hata maofisini, na wanaotenda hivyo tupo nao, na
tunawafahamu, na tunawalinda, tunasahau kuwa watu kama hao ni kama kufuga nyoka
mwenye sumu, ipo siku anaweza kuja kukuzauru wewe mwenyewe. Teteeni haki kwa
kufichua maovu, bila ubaguzi, kwani kila mtu anawajibika kuwa mlinzi wa taifa
letu ili liwe la amani, upendo , mshikamano na utulivu.
Ni mimi:
emu-three
9 comments :
Muache akaonje joto ya jiwe wala usimuonee huruma nyoka huyu, kuwa na msimamo ktk maisha yako.
Hata wahi kaka sisi engine tutasikia tu, huyo dada aseme ukweli asiogope kutetea haki yake.
Hata wahi kaka sisi engine tutasikia tu, huyo dada aseme ukweli asiogope kutetea haki yake.
Mpe hii Obama, mgeni krbu mwenyeji apone lkn tutapona kweli!!!
Mhhh, ndugu yangu Nancy, jana na juzi, dada, leo kaka M3...mmh, kweli mwandihsi hana jinsia, M3, unakubali kuwa kaka au dada? tehetehe...
Ama kwa uhakika, tuwe wakweli, maana nijuavyo mimi, wanawake, ni wepesi sana kusamehe, huenda akasamahe, ngoja tuone kwenye sehemu ijayo.
`kaka au dada m3, tupo uhondo'
NAWASHUKURUNI SANA WAPENDWA, KUNIUNGA MKONO, INANIPA FARAJA NIKIJUA NIPO NA WATU, HATA JAPO KIMIYAKIMIYA, MIMI NASEMA TUPO PAMOJA, TUKIMSUBIRI OBAMA.
Best @mwajuma, ndugu yangu @ Nancy,na nani vile @ Anony. Tupo pamoja wapendwa.
Jamani @ anonymous, unajua me ckujua huyu mtu anayetupa raha na mafundisho ni jinsia gani mn niliona km Miriam kuja kufwatilia kumbe nakosea ni mira3 nsameheeni jamani km bdo nakosea na pia mnijulishe ni kaka au dada,mana ni ndugu yangu huyu.
Jamani @ anonymous, unajua me ckujua huyu mtu anayetupa raha na mafundisho ni jinsia gani mn niliona km Miriam kuja kufwatilia kumbe nakosea ni mira3 nsameheeni jamani km bdo nakosea na pia mnijulishe ni kaka au dada,mana ni ndugu yangu huyu.
Mnijulishe nsizidi kukosea jamani
Post a Comment