Siku ya kesi ikafika, watu wakajaa mahakamani, utafikiri
kulikuwa na ushindani wa namna fulani, hata ilibidi walinzi wafanye kazi ya
ziada kuweza kuwadhibiti watu waliotoka kusikiliza hiyo kesi,
‘Ni kwanini watu wamekuwa wengi kiasi hiki?’ akauliza
mwandishi mmoja wa habari.
‘Ni kwa vile kesi hii ina utata, na watu wamejikuta kwenye
ushabiki wa pande mbili, wengine wakisema wapo upande wa mwanamke, kwa vile
kuna haki za kutetea haki za mwanamke wanaozulumiwa haki zao, utakuta kundi
wengi wao ni wanawake, na wengine wanadai ni ujanja wa mwanamke, kutaka kupata
mali ya mwanaume kwa vile tu ameishi naye, …’akasema huyo mtu.
‘Kwani wewe unasemaje kuna ukweli wowote kati ya hayo mawili
na upo upande gani?’ akauliza mwandishi wa habari
‘Katika dunia ya leo lolote linawezekana, siku hizi watu
hawajali kuzusha uwongo na kudai mali isiyo halali hili lipo na linawezekana,
sitaona ajabu kwa huyo mwanamke kufanya hivyo, lakini pia kuna hai ya wanandugu
kuja kudai mali ya ndugu yao, wakati hata hawajui hiyo mali ilichumwaje, na
wakishapata wanawasahau hata hao mayatima na mjane…., yaani watoto,
wanatelekezwa kabisa..kwahiyo ukinuliza mimi nipo uapnde gani, siwezi
kukuambia…’akasema mmoja wa watu waliohudhuria kwenye hiyo kesi.
‘Kwahiyo wewe kwa uoni wako, unafikiri hili linawezekana
likapata ufumbuzi mbele ya mahakama?’ akauliza mwandishi.
‘Tatizo kubwa ni mambo ya kisheria, maana mnapoishi ndani ,
kati ya mke na mume, huwa hatujali mambo tunayoona ni madogo mdogo, kama kwenye
hii kesi, kunahitajika stakabadhi za malipo, fikiria malipo ya wakati gani….ukiangalia
makaratasi kama hayo wengine tunafungia maandazi au kuchana chana baada ya
tendo likishapita, je inawezekana kweli huyu mwanamke akapata hizo stakabadhi
zinazohitajika, na kama asipopata hizo stakabadhi ndio basi tena na huenda
ilikuwa haki yake kweli , je atafanyaje….’akasema mama mmoja aliyehojiwa.
********
Sisi tulifika mahakamani mapema, na kukaa sehemu zetu, na
baadaye akafika wakili wetu ambaye lwa muda huo alitokea Dar, siku hiyo hakulala nyumbani kwetu kama
alivyokuwa alitarajia mwanzoni, kwani alisema kuna mambo alihitajika
kuyafuatilia, na pia kazini alikuwa na kesi aliyokuwa akiisimamia.
Alipofika akatusalimia, akatabasamu, lakini lilikuwa lile
tabasamu la kujilazimisha, usoni alionyesha huzuni fulani, moyoni niliwaza kuwa
huenda ni kwasababu ya hii kesi yangu, au vinginevyo inawezekana ni kutokana na
kutokuelewana kati yake na mchumba wake. Nikamwangalia nikitaka kumuuliza kuwa
hana hakuata tatizo lolote, lakini kama vile alifahamu, na huenda hakutaka
kuulizwa maswali binafsi akasema;
‘Msiwe na wasiwasi…hii kesi tutashinda tu, cha muhimu ni
sote tuwe na lengo moja, na kujitahidi kufuata yale yote niliyowaelekeza, na nimejaribu
kuwahusisha watu wa haki za binadamu, wataalamu wa dini, ili tuone watatusaidia
vipi kuhusiana na hili swala, na utakuta wote walikuwa wakisisitiza ushahidi
wamesema hawapendi kuingilia mambo ya kimahakama, na ili kuhalalisha madai yetu
ni vyema tukajitahidi kupata ushahidi wa kuonyesha wazi kuwa ulilipwa hizo
pesa, wao kama watalaamu wa Nyanja zao, hawataweza kusaidia zaidi…’akasema.
‘Kwahiyo kitu kikubwa kwa sasa,….ambacho ndio kinatubana
kisheria,… ni jinsi gani ya kupata huo ushahidi, na kwa vile ni muhimu sana
kwetu, imebidi nilifuatiliea huko kwenye
ofisi ulipolipiwa hizo pesa,japokuwa niliwahi kwenda na mchumba wangu kabla, na
kipindi kile hatukuweza kupata ushahidi wowote, lakini safari hii niliamua kwenda
kivingine, kama mpelelezi, nikijua sasa hilo ni jukumu langu… na huko nimelipua
bomu, maana wao kama kampuni wamegundua mengi yaliyokuwa yakitendeka nyuma ya
pazia,japokuwa mengine hayahusiani na kesi yetu…..’akatulia.
‘Kuna uchafu ulikuwa unachezwa huko na watu wachache bila
kampuni kufahamu, na kwa vile watu hawo wachche wenye tamaa ya utajiri wa
dhuluma waishajiamini, nina uhakika ndivyo walivyofanya kwenye malipo
yako…..hwakujua kuwa za mwizi ni arobaini….’akatulia na kufungua ukurasa wa
akiwa kama anasoma.
‘Wao kama kampuni walipogundua hilo wameamua kufanya
uchunguzi wao wa ndani kwa ndani japokuwa walisema kwa sasa wale wote waliokuwa
wakiharibu kampuni wameshaondolewa, ndivyo walivyoniahidi hivyo, lakini
sikurizika nao, ndio nikaingia hadi ofisi za watu wanaoshughulika na mambo kama
hayo ya ukaguzi wa mahesbabu, watu wa kodi, ili wafike na kuchunguza mambo ya
kimahesabu,..
Wao wakakubli kunipa ushirikiano, kwani hata wao walikuwa na
mpango huo wa kufanya ukaguzi wa mahesabu ya mambo yao ya kodi,moja baada ya
jingine, baadhi ya mambo yakaanza kujitokeza, baadhi ya siri zikaanza kuvuja
japokuwa…’akatulia kidogo huku akifungua makabrasha yake, na akawa anasoma
jambo kwenye moja ya karatasi alizochapisha, …..halafu akasema;
‘Pamoja na juhudi zote hizo, bado kama sisi, hatujaupata ule
ushahidi wenyewe tunaoutaka, lakini kwa hatua tuliyofikia inatoa matumaini…na
tunaweza kumshawishi hakimu kuwa kuna jambo lilifanyika.’akasema.
‘Tunashukuru sana sijui tutakulipa nini…’nikasema.
‘Usijali,….hapa ni kufa na kupona, kwasasa hatutakiwi
kufikiria maswala ya malipo, lakini kwa vile kwa namna moja au nyingine, kuna
gharama tunazipata, kama usafiri, nauli ,uchapishaji na kupoteza muda wetu wa
kazi, na nyie mnakuwa hamuwezi kujumuika kwenye kuzalisha, ….hii yote ni
gharama, na mwisho wa siku gharama hizo zitahitajika kurejeshwa…..kesi kama hii
mwisho wa siku, washitakiwa wakishindwa itawabidi walipe gharama zote….hilo
nitahakikisha kuwa linafanyika…’akasema na kuanza kupekua makabrasha yake, huku
akiangalia saa yake ya mkononi.
***********
Baadaye wakaanza kuingia washitakiwa, wakiwa wameongozana
familia nzima, na walipoingia wakainua juu mkoba wao wakishiria ndio wenye
vielelezo vyote vya kuonyesha kuwa hawakufanya hivyo kwa kubahatisha, na kama
ilivyokuwa kwenye kesi ya kwanza,waliongozana na kundi kubwa la familia, wakiwa
na sare zinazofanana. Katika kundi hilo, kulionekana utofauti kidogo na mwanzo,
kwani kaka mkuu wa familia hiyo hakuweo.
Walipofika sehemu yao na kukaa, wakiwa wanamsubiri hakimu
kuingia, mwanasheria wao, akawa anamtupia jicho la siri mchumba wake ambaye
sasa anaonekana kama amewasaliti. Lakini mwanadada huyo alikuwa kama hajui kuwa
watu hawo wapo, kwani alikuwa kainama akisoma makabrasha yake, na wale wanafamilia wengine wanaotafuta
chokochoko, hawakuweza kuficha chuki zao usoni, kwani kila mara walipokuwa
wakigeuka upande wetu, walionekana wakikunja uso kwa hasira, na wengine
wakionyesha ishara ya kuwa tutafungwa, au tutachinjwa, kwa kupitisha kidole
shingoni, lakini hakuna aliyewajali.
Wakili, mwanadada alikuwa kainama akiendelea kusoma
makabrasha yake hakutaka hata kutizama upande wa wahasimu wake hawo, na mara
chache, alikuwa akiinua uso kuangalia upande ule anapotokea hakimu, na mara
nyingi alikuwa akimtizama mteja wake na kutabasamu kunipa moyo.
‘Msijali tutakachofanya leo ni kuvuta muda, na baadaye
nitaomba muda wa kuweza kuleta ushahidi
muhimu,maana nina imani polisi na hawo wakaguzi wa mahesabau watakuwa wamegundua jambo…haiwezekani pesa
ulipwe wewe na jina liandikwe mtu mwingine,….’akatulia akisoma jambo kwenye
makabrasha yake.
‘Na cha ajabu huyo mtu aliyeandikwa kuwa ndiye aliyelipwa
hajulikani wapi alipo….na kuna kitu kingine ambacho ndicho kilinifanya
niwatafute hawo wakaguzi wa mahesabu, kwanini namba ya stakabadhi ya
malipo,…katika mpangilia namba za risiti za malipo kwenye hilo faili lao,
ambayo inaonyesha kuwa ndiyo iliyolipiwa hiyo pesa ni tofauti na namba
nyingine…..haipo kwenye mtiririko wa namba ….’akasema wakili mwanadada.
Alitulia na kutuangalia kwa muda, kama vile anahitaji
tuongee, na mimi nikaona nifungue mdomo na kusema;
‘Mimi nahisi kuna jambo….maana waliponilipa, nakumbuka
kabisa walinitaka nisaini, halafu wakanipa kopi yangu, wakaniambia niende kwa
karani mtoa pesa…na huko napo nikasainishwa….sasa sijui, na sijui kwanini siku
ile sikuweza kusoma kila kitu….’nikasema nikionyesha huzuni usoni, na baba
akasema;
‘Sisi tunakusikiza wewe wakili wetu, kama kweli umeamua
kutusaidia, mungu akuongoze, na uipate haki kwa ajili ya mwanamke mwenzako….
Kama unavyoona mara nyingi tukishapata jambo, hatuna haja na kutunza stakabadhi
za malipo,…na hata wengi hatusomi kabisa nini kilichoandikwa, .’akasema baba.
‘Haki itapatikana tu,…..ni kweli huo ni udhaifu wa wengi,
maana unapolipwa pesa kuna stakabadhi ya malipo, mara nyingi hizi zinakuwa ni
kitabu, na zenyewe zina namba zinazofuatana, moja , mbili tatu na kuendelea kwa
mpangilia maalumu, sasa haiwezekani namba zifuatane, halafu ikifikia hiyo namba
ya malipo yaliyofanyika …..iwe tofauti,…mia sita na mbili,…. halafu ikitoka
hiyo namba, inaendelea katika ule mtiririko wa mwanzo, na kuendelea kwenye
mfuatano wa kawaida…’akasema huku akijikuna kichwa kwa kidole.
‘Hapa wamebugi,..hapo kama walipanga hupo mpango,
walijisahau….na ndipo unapoona kuwa njia za mhalifu ni fupi….wao walijua
wakiharibu ile stakabadhi halali ya malipo, na kuweka nyingine watakuwa
wameharibu ushahidi….’akasema na kuangalia saa yake. Halafu akageuza kichwa
kuangalia watu waliohudhuria , lakini hakutaka kabisa kugeuza kichwa kuangalia
upande ule wa washitakiwa, akasema;
‘Nashangaa kwanini hakimu kachelewa kuingia..’akasema na
kabla hajamaliza, mara akaja mtu na kusema mawakili wa pande zote mbili
wanahitajika ndani, kuongea na hakimu.
‘Nilijua tu kuna jambo….’akasema huyo mwanadada na kuinuka
na makabrsha yake kuelekea ndani na huku nyuma yake akimfuta yule mwanasheria
wa familia ya washitakiwa ambaye alishatambulishwa kama wakili wa hiyo familia,
japokuwa walisema kuwa kwa vile yeye ni mmoja wa washitakiwa, basi watamtafuta
wakili wao mwingine, lakini hadi muda huo huyo walikili wao mwingine alikuwa
hajafika.
*********
‘Nimewaita hapa kuhusu jambo moja muhimu sana, kuna kesi
imetufikia ambayo inahitajika kusikilizwa leo, kesi hiyo itawagusa wahusika wa
kesi yenu, na kwasababu hiyo tunahitajika kusikiliza kesi yenu kwa haraka,
…..kwahiyo lengo la kuwaita hapa ni kuwekana sawa…japokuwa kesi inayokuja ni ya
kutambulishwa na baadaye itahitajika kwenda kusikilizwa mahakama za juu, kwani inavyoonekana kuna makosa ya jinai na
mauji ndani ya hiyo kesi…’akasema hakimu.
‘Eti nini..na mauji..?’ akashangaa yule mwanasheria wa
familia.
‘Ndio ….lakini kwasasa ninachotaka kuongea ni kuhusu hii
kesi yenu kuna mawili, kwanza kuna wazo lililetwa mwanzoni kuwa hii kesi
ingeliwezekana kusikilizwa kindugu na kumalizika,…hili sijui mnalionaje, kama
mumekubaliana itaweza kusaidia sana, ili tupate kuimaliza kesi yenu , ili
tuendelee na kesi hiyo nyingine….’akasema hakimu.
‘Muheshimiwa hakimu, hayo unayoelezea ni kweli sisi
washitakiwa tulikuwa tayari kwa hilo, kuwa tukutane na wenzetu, ili ikiwezekana
mambo haya tukayamaliza kinyumbani, …..kutokana na wao kukosa ushahidi …..na
kama unavyoona kuna kesi hiyo nyingine ambayo inahusu wahusika wakuu wa kesi
hii….ambayo sijui kama wenzetu wapo nyuma yake au….?’akawa kama anauliza huyo
mwanasheria wa familia.
‘Kama nilivyokuambia hayo yametoka kwa upande wa vyombo vya
usalama, kama unakumbuka kwenye eneo lenu kume kuwa na mauji ya mara kwa mara
yenye utata, ..polisi walikuwa bado wanafuatilia , na uchunguzi wa polisi
umegundua mengi, na kwahiyo kwa vile mahakama yetu ni mahakama ya mwanzo na kesi
hiyo inahusu makosa ya jinai na
mauaji,….kwetu tutaitambulisha tu na kuipeleka mbele...'akasema hakimu huku akiangalia saa yake.
'Kwahiyo ndio maana
ninahitajia kama hamjakuabaliana basi tuanze kesi yenu hiyo kwa haraka,
vinginevyo tuiahirishe, …lakini kama mpo tayari,…tutaendelea, ili haki ipatikane na
kama hampo tayari basi tunaweza kuihairisha hadi tarehe tutakayopanga
baadaye…’akasema hakimu.
‘Sisi kwa upande wetu tupo tayari kulimaliza hilo tatizo
kifamilia, sijui kwa hawa wenzetu ambao ndio walioshitakia, na sioni kwanini
wasikubaliane na hili, wakati hali halisi inajionyesha, na hawana ushahidi
wowote….’akasema mwanasheria wa familia.
‘Tuna mambo ya msingi tunayodai, na sisi tulileta kesi hii
mbele yako muheshimiwa hakimu, kwa kuogopa
kuwa hili tatizo likisimamiwa na wanafamilia halitaleta ufumbuzi wa haki,
..ila kama watakubaliana na madai yetu ya msingi hapa mbele yako muheshimwia
hakimu, sisi hatutakuwa na kipingamizi…’akasema wakili mwanadada.
‘Madai yenu ya msingi kama yapi?’ akauliza mwanasheria wa
familia. Na wakili mwanadada akamwangalia hakimu kama anaweza kuingilia kati
hilo swali. Hakimu akasema;
‘Madai yatu ya msingi ni kama yalivyoanishwa kwenye kesi
yatu, na yalishasomwa mahakamani…..’akasema wakili mwanadada na hakimu
akaingilia kati na kusema;
‘Kutokana na mashitaka yaliyoletwa mbele yangu ni kuwa nyie
mlioshitakiwa mumemiliki nyumba na duka isivyo halali, na kwahiyo wao wanataka
hati ya nyumba na duka kubatilishwa na kumilikishwa kwa mjane kwani vyote hivyo alijenga kwa pesa yake mwenyewe,
….’akasema hakimu na kumwangalia wakili mwanadada, ili kama ana nyongeza, na
kabla wakili mwanadada hajasema kitu, mwanasheria wa familia akasema;.
‘Muheshimiwa hakimu, madai hayo sio sahihi….hilo la kuwa
alijenga kwa pesa yake, sio sahihi, ….kwasababu tulizitaja, hata kama alijenga
yeye, lakini alijenga kutokana na pesa za mumewe, kwani kipindi hicho mumewe
alikuwa jela…..hata hivyo muheshimiwa hakimu,…sisi tupo tayari kukubaliana kuwa
nyumba na duka viwe vya familia yaani mjane na mtoto wawe wakivitumia, lakini
hati miliki, bado iendelee kuwa mikononi
mwa wanandugu hadi hapo mtoto atakapokuwa mkubwa, na tutaibadilisha na
kumwandikisha huyo mtoto, hilo halina kipingamizi….’akasema mwanasheria wa
familia.
‘Muheshimiwa hakimu, kutokana na maelezo ya mwenzetu huyu,
kama alivyoelezea hapo, inaonekana moja kwa moja kuwa hatutaweza kukubaliana
kwa hilo kama litapelekwa kusikilizwa kifamilia, ndio maana tulilileta mbee
yako, …kwahiyo sisi tunaoshitakia, tunaomba kesi yetu iendelee, ama ianze leo,
au kama ulivyosema kuwa kuna kesi nyingine, basi tunaweza kuiarisha kwa leo,
hadi hapo itaposikilizwa tena,…..’akasema wakili mwanadada.
Hakimu akamgeukiwa mwanasheria wa familia , na kumwangalia
kusikiliza atasema nini, na mwanasheria wa familia akasema;
‘Muheshimiwa hakimu, hawa wanataka kupoteza muda bure,
hawana ushahidi wowote wa madai yao, inavyoonekana ni ujanja wa kutaka kumiliki mali isivyo
halali,…na kutumia siasa za hadaa, kwani sasa hivi wamakwenda hadi kwa watu wa haki za
binadamu, ina maana hawaamini mahakama yako…?' akawa kama anauliza halafu akaendelea kuongea;
'Wamekwenda hadi kutafuta makundi ya kutetea haki za akina mama, wakati kesi ipo mahakamani, huku ni kuzarau mahakama yako….kw ujumla muheshimiwa hakimu, sisi hatukumdhulumu mtu,
tumefanya kutokana na utaratibu wa kimila, kisheria…na kutokana na maandishi ya marehemu
mwenyewe aliyotuachia….na kama tutafanya kinyume na hivyo alivyotaka marehemu, haitakuwa haki,....hebu jamani wenzangu fikirieni mara mbili, wewe ulikuwa hai ukataka mali zako zimilikiwe hivi na vile, sasa umefariki, waliobakia nyuma wanafanya kinyume chake, hii tutakuwa tunamtendea marehemu isivyo halali….'akasema huku akionyesha huzuni, halafu akamgeukia mchumba wake na kusema;
'Na huyu
ambaye sasa anasema ni wakili wao, anatafuta mwanya wa kujijengea umaarufu tu,
hakuna kitu kingine hapo muheshimiwa hakimu, ni kujitafutia njia ya kujionyesha kwa watu kuwa anaweza kazi, kwa njia hiyo hutafanikiwa kamwe, kama ni kweli onyesheni huo ushahidi, ushahidi upo wapi…?’akasema mwanasheria wa familia.
‘Hizo ni hoja zako, ….huo ushahidi utapatika mbele ya
mahakama, ninakuhakikishia muheshimwa hakimu, hilo kuwa sisi tuna ushahidi wa
kutosha, na kwanini nitafute umaarufu kwa kudai haki za wanyonge, hiyo ni zarau
muheshimiwa hakimu, sikutegemea kuwa mwenzangu aliyesomea sheria angelizungumza
maneno kama hayo…’akasema wakili mwanadada.
Hakimu alitulia kwa muda, baadaye akasema ,’Inavyoonekana
hakutakuwa na ufumbuzi wa hili tatizo kama litarudishwa huko kwenye familia,
kama ombi lenu la awali lilivyoletwa mbele yangu, na kwahiyo basi kesi yenu
itabidi iahirishwe hadi hapo itakapotajwa tena,….na nawaomba sikuhiyo muwe
mumekamilika na ushahidi na mashahidi ….sitavumilia tena malumbano ya
kibinfasi, yasiyo na ushahidi, nyote mnafahamu vyema sheria …’akasema na mlango
ukafunguliwa ili wanasheria hao watoke.
Mwanasheria wa familia alipotoka nje, akamshika wakili
mwanadada mkono kumsogeza pembeni kaba hawajaingia kwenye ukumbi wa mahakama,
ambapo kulikuwa na tangazo la kuahirishwa kwa hiyo kesi na kutajwa kesi
nyingine itakayosikilizwa.
‘Nyie mumefanya nini….?’ Akauliza kwa hasira huyo
mwanasheria wa familia.
‘Kuhusu nini?’ akauliza wakili mwanadada akiutoa mkono wake
kutoka kwa huyo mwanasheria wa familia.
‘Hii kesi mpya ambayo inamshitakia kaka yangu kuwa eti
anahusika na kundi la mauaji hapo kijijini na nyie mlioipeleka polisi,…nina
uhakika kuwa nyie ndio wahusika na lengo lenu ni kuipaka familia yangu matope,
ionekane kuwa haitendi haki au sio….?’ akauliza.
‘Hiyo sihusiki nayo….kesi yangu ni hii iliyotakiwa kuwepo
leo, hayo mengine, kama alivyosema muheshimiwa hakimu ni mambo ya usalama….kama
kulikuwa na mauji,…kama kulikuwa na makosa, ni lazima wahusika wafikishwe mbele
ya sheria…hilo sio ajabu, ….kuna kosa gani hapo?’ akauliza kwa mshangao.
‘Ninakuonya ….tena unisikie sana, usije ukafikiria kwa vile
tuna mahusiano mimi na wewe ukafikiria nitashindwa kuitetea familia yangu,
….mapenzi hayawezi kamwe, kuweza kunifanya nigeuke nyuma na kuiacha familia
yangu…..kama unahusika na hilo, tutafikishana kubaya…hili nakupa kama onyo,
kama unataka kujionyesha wewe ni bora wa sheria, haya, tutaona mwisho wake
utafika wapi…’akasema kwa hasira.
‘Tusitishane kwa lolote lile, …hiyo ndio kazi yetu, kwani
tulisomea nini….wewe unachotakiwa kuangalia ni haki na sheria sio kutetea ndugu
hata kama ni wahalifu. Na usipoangalia vyema, sizani kama kazi hiyo ya uwakili
utaiweza…kwa mtindo huo, hii kazi hutaweza…ngalia ukweli, usizibe masikio kwa
vile na familia yako,….nakushauri hivyo, kwa vile tumetoka mbali mimi na wewe…..’akasema
wakili mwanadada.
‘Tutaona nini…nasema hivi mimi na wewe sasa hatujuani,
tutajuana kwenye ulingo wa mahakama,…si ndio unataka iwe
hivyo..tutaona….’akasema huku akiondoka kwa hasira.
‘Tutaona nini…hatutakiwi tuone, tunatakiwa sheria isimamiwe
itakiwavyo, sio swala la kutishana na swala la haki na sheria,….unakaribishwa
sana muheshimiwa, tutajuana huko huko mbele ya hakimu…’akasema wakili
mwanadada, akiwafuata watu wake. Lakini machoni, kulishaanza kujenga ukungu wa
machozi.
NB: Ukweli unauma, lakini mapenzi nayo mmmh….
WAZO LA LEO: Tusikubali
kabisa katika maisha yetu tukatawaliwa na jaziba, mara nyingi jaziba,
zinatusukuma kwenye kutenda ubaya zaidi ya ubaya uliotangulia, na kinachofuatia
hapo kulipiza kisasi. Linapotokea tatizo, tuangalie sheria inasemaje, na ni
vyema, ukapata ushauri kwa watu wenye busara kabla hujachukua maamuzi mengine,
kwani huenda ikatoea sisi wenyewe ndio wakosaji, lakini kwa vile imetugusa
wenyewe, na kwa vile hatuwezi kumudu hasira zetu, matokea yake ni jaziba. Na
haki itendwe na kutolewa kwa usawa bila kubagua.
Ni mimi:
emu-three
8 comments :
Da imefika pazuri Sana dada upo juu. Na lazima hali itendeke hapo
Hello. And Bye.
Pole na majukum dada vp mwendelezo lni❓ mn nahic kudata nkiikosa
Pole na majukum dada vp mwendelezo lni❓ mn nahic kudata nkiikosa
Pole na majukum dada vp mwendelezo lni❓ mn nahic kudata nkiikosa
Pole na majukum dada vp mwendelezo lni❓ mn nahic kudata nkiikosa
Pole na majukum dada vp mwendelezo lni❓ mn nahic kudata nkiikosa
Pole na majukum dada vp mwendelezo lni❓ mn nahic kudata nkiikosa
Post a Comment