Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, March 25, 2013

Uchungu wa Mwana Aujuaye ni mzazi-76



‘Mimi kwa kuwasaidia nawaomba muondoke hapa haraka mrudi huko mlipotoka, ……nawaombeni sana, yule mzee anahitajika kutulia, na sisi kama watoto wake ni jukumu letu kumlinda…’akasema binti.

`Na ndio hivyo tupo mbioni kuondoka….’ Akasema Maua

‘Isiwe mbioni, nawashaurini ikiwezekana kesho muwe mumeshaondoka, kwani hali ninayoiona, mkiendelea kuwepo hapa kutazuka mambo mengi mabaya….’akasema huyo binti, kipindi hicho mama yake alikuwa nje, akiongea na simu, baadaye akaja, na kujumuika kwenye hicho kikao.

‘Mama yako yupo wapi?’ akauliza huyo mwanamama.

‘Yupo anakuja, anaweka vitu sawa kwenye duka lake, hawezi kuondoka bila kumuachia mtu, na hatuui haya maongezi yatachukua muda gani…..’akasema Maua.

‘Hayatachukua muda mrefu, ni maswala ya kuwekana sawa tu….’akasema yule binti.

‘Kwani nyie mnatarajia kuondoka lini?’ akauliza yule binti.

‘Mbona tumeshakata tiketi,  kesho tunaondoka, hakuna mwenye haja ya kumsumbua mzee, wenu, na nimekuwa nikienda kwake kwa vile alikuwa akinihitajia, vinginevyo, ….’akasema Maua.

‘Usitudanganye binti, mimi nawafahamu sana, nyie…..’akasema mwanamama. Na mama Maua kawa keshafika, na aliposikia huyo mwanamama akiongea hivyo, akasema;

‘Ni kweli anavyosema binti yangu, yeye alikuja huku kwasababu ya huyo Tajiri, hakuwa na lengo na baba yenu, na kama alivyonielezea awali, safari yao ilikuwa ya kuja kwangu, lakini alipofika hapa, ndio huyo Tajiri ambaye walikfika naye, aka,kuta mjomba wake anaumwa, ikabidi safari ya kuja kwangu isitishwe kwanza….’akasema mama Maua.

‘Hizo ni hadithi za kutunga,…lengo na nia yao hawa watu ni utajiri wa mzee…’akasema huyo mwanamama akimwangalia mama Maua.

‘Sio kweli …..’akasema mama Maua.

‘Wewe sema tu sio kweli, …ila nawaambia ukweli, ule utajiri, isingelikuwa juhudi zangu usingelipatikana, kwahiyo yoyote atakayejifanya kuingiza mguu wake kwa kisingizio chochote kile,…ataishia pabaya….’akasema Mama wa mabinti.

‘Mama, nilishakuambia kama hutaweza kuongea kwa busara, ni bora, usiongee,…’akasema binti yake.

‘Busara gani inahitajika hapa, hawa watu ukujifanya mpole , ukaongea kwa kuwanyenyekea, hutawaweza, hawa wanajulikana, watu wa Dar, ni watata…..mbinu zao, zinajulikana,….ni watu wa kutumia mali za wenzao,…ndio maana wanajiita wabongo. Kutwa kucha kuwazia jinsi ya kupata pesa, kwa kupitia migongo ya wenzao…..’akasema huku akionyeshea mfono mgongoni mwake.

‘Mama…..’binti yake akawa analalamika.

‘Huo ndio ukweli, sisi tunalima, tunaumia,….mazao yetu yanakwenda kwao, wanauza kwa bei mbaya…sukari inalimwa mikoani, inakwenda huko kwao, wanakuja kutupangia bei..unaona mambo yalivyo..watoto wetu wote wanakimbilia huko, hawana kazi, unafikiri watafanya nini, kama sio kujifunza utapeli….. hawataki kujihanganisha, wewe fikiria binti mdogo kama huyu anakwenda kutembea na mzee, kama yule ….’akasema mama wa binti.

‘Mama mimi nakuheshimu sana…hayo unayozungumza, una ushahid nayo…..au unaongea tu kwa vile unataka kuonekana unajua kuongea…’akalalamika Maua.

‘Sikiliza binti, kama hujui maisha yalivyo, muulize mama yako…mimi sio mtu wa kuchezea, utakuja kupata shida, utatamani kujiua…nakuonya tena, rudi kwa amani huko ulipotoka, achana na ndoa za watu, tafuta kijana mwenzako akuoe…nakushauri sana kama binti yangu…’akasema huyu mama akimwangalia Maua.

‘Tumekuelewa,…kama ni hayo yaliyowaleta, tumeshaelewa, maana nona hakuna la maana tutakolojadili hapa,mimi nitailea hiyo mimba ya binti yangu,..sioni shida, …’akasema mama Maua.

‘Kwanini asiende kwa huyo aliyempa uja uzito..kwanini ana kwenda kumsingizia yule mzee , kama sio kutafuta utajiri asiojua wapi ulipopatikana…?’ akauliza mama wa yule binti.

‘Hawa sio wajinga, kwanini wasiende kwa watu wengine , wakaamua kuja kwa huyo mzee, kama nilivyokueleza, wao kuja kwao ilikuwa kwa ajili ya Tajiri, yeye ndiye anawajibika kwa haya yote, na walipofika hapa ,wakatambulishwa kwa mjomba wake, na yeye, ndiye alitakiwa kuhakikisha maswala haya yanatatuliwa kwa amani, lakini ..haikuwezekana kuwa hivyo’akasema mama Maua.

‘Kwanini haikuwezekana?’ akauliza yule binti.

‘Kila wakifika kwenye nyumba ya mzee, walijikuta wakikutana na matatizo, mara mzee, anaumwa, mara hili….na hilo sio swala la kuongea juu kwa juu…..’akasema mama Maua.

*******

Mama Maua alitoka kidogo, kwani alihitajika dukani kwake, na baadaye akarejea, na kuwakuta wajumbe wengine wakiwa kimiya wakimsubiri afike. Mwanamama alikuwa kashika kidevu, akionekana kutingwa na mawazo. Na alipoona mama Maua kaingia,  akageuka kumwangalia Maua na kusema

‘Mimi bado sijawaelewa, ….Mimi hili swala la ujauzito wa huyu binti yako, linanipa mashaka, je huyu mzee anahusika vipi na huo uja uzito wa binti yenu…maana nilivyosikia ni kuwa ni hiyo mimba ni ya Tajiri, au sio?’ Akauliza mama wa binti.

‘Yeye ni ,mjomba wa Tajiri, na kama ujuavyo wajomba ndio watu muhimu wa maswala ay ndoa, na nii mzazi ambaye anaishi na huyo Tajiri, kwanini asihusike….’akasema mama Maua.

‘Na hilo swala la mzee kutaka kumuoa Maua limekujaje…kama ana mimba ya mtu mwingine kwanini mzee atake kumuoa huyu binti yako?’ akauliza mama wa binti.

‘Hayo inabidi umu-ulize mzee, mwenyewe, ….’akasema Maua.

‘Kwanini nimuulize yeye, wakati kuoana ni makubaliano ya watu wawili, ina maana mpaka kufikia hatua ya kutoa hiyo kauli, mlishaongea na kukubaliana, sizani yeye angelifikia uamuzi huo bila ya kuongea na wewe….’akasema huyo mwanamama.

‘Kama ni makubaliano ya watu wawili, basi wewe yanakuhusu nini?’ akasema Maua

‘Nia la lengo letu la kuja hapa ni kujaribu kuyasuluhisha haya mambo, na ikiwezekana mzee, asihusishwe tena…au kusumbuliwa, maana tumeona watu wengi, wanataka kutumia kila mbinu, ili wamuhujumu,….sisi kama familia tumeliona hilo, na ndio maana tunataka kuliweka sawa…’akasema yule binti.

‘Sisi hatuna nia yoyote ya kumhujumu huyo mzee, naombe nileweke hivyo….’akasema Maua.

‘Hatujakushutumu wewe, tumezungumzia kwa ujumla, ..kuwa kuna watu kama hawo,…na pia yule mzee ni mgonjwa,….inabidi tuwe makini na kila jambo litakalomuathiri afya yake, sisi ndio tunayemfahamu, na hatua ya mwanzo ni kumuondolea majukumu mengi aliyokuwa nayo….baba, hahitajiki tena kubeba majukumu mazito, anahitajia kutulia….’akasema huyo binti, na mama yake akadakia na kusema;

‘Na  Mzee kama yule, kumuona binti mdogo kama huyu, ni kujiongezea majukumu…..hakuna cha zaidi atakachokpata….’akasema mama wa binti.

‘Tumewaelewa..na binti yangu hana nia ya kuolewa na mzee, wenu, hilo nawahakikishia, hayo ya kuolewa ni mambo ya mzee wenu mwenyewe, …kama alivyonielezea, na mimi nililipinga mbele yake, kuwa haitawezekana,….yeye akadai anamuhitaji huyu binti yangu kwa vile anaweza kumjali na anajali afya yake….sijui kwanini akafikia hatua hiyo…’akasema mama Maua.

‘Ni uzee tu, sizani kama ana lolote la maana, akili imeshakuwa ya kitoto….’akasema yule mwanamama.

‘Hapana ule umri, bado ana akili sawasawa, nahisi kuna tatizo linalomsumbua yule mzee, na anahitajia msaada na mtu anayeweza kumpa msaada anaohitajia yeye ni mke….sasa sijui kwanini amtake binti yangu wakati wewe mke wake upo, inaonekana kuna kutokuelewana kati yako na mume wako…’akasema Mama Maua

‘Hayo ya mume wangu na mimi hayawahusu…na ninani kawaambia kuwa hatuelewani….migangano ya ndoa ipo, na mwisho wa siku inakuja kusuluhishwa, tatizo ni pale anapokuja kidudu mtu, kutaka kuingilia ndoa za watu, na wanaume walivyo, wao watakimbilia kuoa….kutafuta nyumba ndogo, hawajui kuwa hilo sio suluhisho, itakuwa sawa na kuruka mkoja ukaja kukanyaga mavi…’akasema mama wa binti.

‘Tumewaelewa, sana, basi mimi nawashukuruni kwa kututembelea kama hakuna jingine, tuombeane hei, na tusameheane kwa haya yaliyotokea, ili tukikutana tusalimieane kwa amani….’akasema mama Maua.

‘Hatujamalizana na nyie,…maana kama nilivyowaambia watu wa aina yenu nawafahamu sana…rudisheni pesa mlizomptapeli mzee, na mimi….’akasema Mama wa binti.

‘Pesa gani hizo mlizotapeliwa….!?’ Akauliza mama Maua akimwangalia binti yake, na Maua naye akabakia akiwa ameshangaa.

‘Mbona mimi siwalewi, pesa gani hizo tulizowatapeli?’ akauliza Maua.

‘Msijifanye kushangaa, ..hamkumtuma mama yenu mdogo, kuja kwa mzee, adai kuwa kwenye ile hoteli mnadaiwa pesa, …milioni moja na nusu, na mama huyo akaja kwangu na kuniambia, kuwa anahitajia pesa ya nauli, ili muondoke haraka,….’akasema huyo mama.

‘Mbona haya makubwa…..sisi tumeondoka pale , kwa vile mzee, amekwenda kutushitakia kuwa sisi tumemsingizia mimba, …na hayo alikuja kuniambia mama mdogo, kuwa mzee kaenda kushitaki polisi, …..’akasema Maua.

‘Kwani huyo mama mdogo yupo wapi?’ akauliza binti.

‘Ametoka, amekwenda kujiandaa,…..’akasema mama Maua, akiwa katahayari .

‘Mnaona…mama Maua, unaona wenzako walivyo,…hawa ni watoto wa bongo, ..kwao kuadanganya, na kupata pesa kwa watu,bila hata kuitolea jasho ni jambo la kawaida tu…hawaogopi,…..kwahiyo hata hayo ya ujazito, inawezekana ni mbinu tu, za kuhadaa, ili wapate pesa’akasema mama wa wale mabinti.

‘Wewe mama, mimi siwezi kufanya uchafu wa namna hiyo, na nakuhakikishia kuwa haya yote yasingelitokea kaam isingelikuwa huyo Tajiri, wao ndio walionifanyia haya…wakishirikiana na mama mdogo, mimi ……’Maua akaanza kulia.

‘Usilete ujanja wa kulia lia hapa, hata ulie vipi , mimi ninachohitaji ni pesa, yangu, vinginevyo mnakwenda kulala jela…’akasema yule mama.

‘Pesa hizo msubirini huyo aliyechukua kwenu, ..yeye ndiye anajua hayo, …binti yangu hawezi kufanya hayo, namfahamu sana…’akasema mama Maua.

‘Wewe mama usite-tee uchafu, mji ule unabadilihsa watu, unaweza ukalea, vyema nyumbani, lakini watoto hawa wakikutana na wenzao waanbadilika, sasa jiulieza kama ulimlea vyema, iweje aiswe na aibu ya kwenda kutembea na mzee kama yule….’akasema huyo mama.

‘Wewe mama, nimeshakuambia kuwa sijawahi kwenda kutembea na mzee, wenu,….hayo yanatoka wapi, kwanini unasisitiza hayo kuwa nimetembea na mume wako,….ina maana wema wangu ndio umefikia hapo,…kuja kumuhudumia mzee, wenu akiwa katika hali mbaya, ndio imekuwa hayo..’akasema Maua.

‘Maua mimi nimekuelewa, na nashukuru sana kwa hilo, na hata baba alisema hayo, kuwa usingelikuwa wewe sasa hivi angeliwa keshakufa….;lakini iweje, adaiwe kuwa uja uzito ni wake, hapo ndio sisi tunaingilai kati,..mzee, kwa hali aliyokuwa nayo, angeliweza kumuhitajai yoyote, ..kiujumla, alihitaji mtu wa kuwa karibu naye…’akasema yule binti.

‘Na mimi mwenyewe nimesharudi, nitakuwa naye, kwahiyo nyie hamuhitajiki tena,sawa?’ akasema mama wa yule binti.

‘Sawa sisi hatubishi hayo, ila hilo la pesa, sisi kwetu ni gumu…..’mara simu ya yule binti ikalia.

‘Eti nini…kaja hapo, na polisi wamemchukua....na baba..nini?’ akauliza.

‘Sawa basi tunakuja….’akasema huyo binti na kukata simu, akionyesha uso wa wasiwasi.

‘Polisi …?’ akauliza Maua.

‘Mama yenu mdogo, kashikiliwa na polisi….nahisi ni kutokana na hizo pesa alizochukua, lakini cha ajabu  hajakutwa na hata senti moja, huenda kazificha humu ndani, ….’akasema binti.

‘Inabidi tuzitafute…’akasema mama wa yule binti.

‘Hapana,..hatuna muda huo, mzee, anatuhitaji kwa haraka, na alishasema haina haja, kuwadai, kama watakiri kosa…twende mama..’akasema maam wa yule binti.

‘Subirini tuzitafute hizo pesa, kama zipo humu ndani muondoke nazo, hatuhitaji pesa zenu hata kidogo, hilo sio lengo letu…’akasema Maua, huku akiondoka kuelekea chumba ambacho walikuwa wakichangia na huyo mama mdogo.

‘Utazitafuta nikiwa pamoja na wewe unaweza ukazificha…’akasema mama wa yule binti akimfuta Maua nyuma, wakabakia binti na mama Maua. Baaadaye wakarejea na yule mama akasema;

‘Hakuna hata senti moja, nafikiri kuna sehemu nyingine wamezificha, na hii ya kusema tutafute ni ujanja wao tu,…mimi sijamalizana nao, sikubali kirahisi hivyo, hiyo pesa yangu naombe irejeshwe….’akasema huyo mama.

‘Mama lakini kama uliwapa kwa ajili ya nauli, kwani nini tena unaidai....mama twende haraka, nahisi kuna jambo kwa mzee?’akauliza binti huyo na kusisitiza kuondoka.

‘Sio kwa nauli tu, ….kuna mambo mengine, nilikubaliana na huyo mama mdogo,kumbe ni muongo,…nimegundua kuwa ni utapeli wake….’akasema huyo mama.

‘Mama, achana na hayo, tunahitajika kwa mzee haraka….twende,kama ni huyo mama mdogo mtakutana naye huko huko..kuna tatizo kwa mzee…’akasema yule binti akitangulia kuondoka, na yule mama akasubiri kidogo hadi binti yake alipoondoka.

‘Sikiliza Maua..nasema haya mbele ya mama yako….achana na waume wa watu, tafuta mume wako , kijana mwenzako, hata kama sio kijana, lakini sio sawa na yule mzee, yule ni sawa na babu yako,..achana na tamaa za mali za watu, tafuta mume, muhangaike pamoja mtafuteni mali zenu, ….’akamwanglia Maua kwa macho makali, halafu baadaye akaangalia pembeni na kusema;

‘Musione ile mali ipo vile…., ni watu wamehangaika,…’ akaangalia pembeni na baadaye akageuka kumwangalia Maua, na kusema;

‘Sasa ukitaka kuumia, ingilia hiyo ndoa, ile ndoa, ni mimi na yule mzee tu….’akatulia akimwangalia Maua kwa macho makali. Maua akamwangalia vile vile bila kupepesa macho, hadi yule mama akamgeukia mama yake Maua na kusema;

‘Hata kama Itafikia  hatua yule mzee, aamue kuniacha…kama ilivyokuwa imefikia hivyo…, nawahakikishia kuwa hakuna mwanamke mwingine atakayeweza kuja kukaa na huyo mzee kwa amani…..hilo nawathibitishia…mimi kama binti wa huo ukoo unaoogopewa…’ akageuka tena kumwangalia Maua. Maua alikuwa kainama akiwaza jambo, yule mama akageuka kumwangalia mama Maua akasema;

‘Hebu angalia jinsi mambo yanavyokwenda ndani ya ile familia, hasa baada ya mimi kuondoka,…hakuna amani, kila anayejaribu kuingia pale, hakai kwa amani,….anakimbia mwenyewe,unafikiri kwanini….mimi ndiye mwenye siri ya ile familia,.…mimi ndiye ninayemfahamu fika yule mzee’akageuka kumwangalia Maua,  halafu akageuka kumwangalia mama yake Maua.

‘Tumkuelewa….’akasema mama Maua huku akikwepa kuangaliana na huyo mama usoni moja kwa moja.

‘Mimi kwanza nafurahi kusikia hivyo, ila nakuomba sana, usinipakazie mambo ya uwongo, kuwa eti nimetembea na mume wako,…nakuomba sana hiyo kauli uifute, na ama hilo la kuingilai ndoa za watu, mimi sijawahi kufanya hivyo…kauli hiyo alishawahi kuniambia Malikia, kuwa nimeingilia mapenzi ya watu….’akasema Maua akikunja uso.

‘Achana na huyo mshenzi…huyo atakuwa mfano wa watu wanaoingilia ndoa za watu na mali yao…wewe angalia mambo yako, kesho msionekane hapa, vinginevyo, …..nyumbani kwenu kutakuwa jela, na mwishowe mtaishia kuokokota makopo….sitakubali kamwe, ndoa yangu iingiliwe, hilo ninawahakikishia, na ili hiyo iwezekane, msikanyage pale nyumbani kwa lolote lile…’akasema huyo mama akiondoka.

‘Hakuna mwenye haja ya kuingilia ndoa yako…na sitarajii kufika huko tena….’akasema Maua.

‘Mwacheni huyo mzee ajifie mwenyewe…maana sizani kama ana muda mrefu….’akasema huyo mama na kumfanya Maua amwangalia kwa macho ya wasiwasi.

‘Usishangae kusikia kauli hiyo, mimi nimeishi na yule mzee, miaka mingi, namfahamu fika, na kila hatua inonyesha kuwa analekea kaburini….halafu unakuja kusema una uja uzito  wake. Sasa binti kama unataka kuja kugombea urithi, haya njoo, …lakini sizani kama utaambulia kitu…..’akasema huyo mama.

‘Ina maana umeshamfikiria hivyo….mbona kauli yako …ni sawa sawa na Malikia, ni kama vile mnataka afe?’ akauliza Maua kwa mshangao.

‘Kwani kufa ni ajabu…kila mtu atakufa, lakini ukifikia hatua kama ile, …ni nini kimebakia, kwani usumbue watu….’ Akasema huku akichezea mkoba wake.

‘Lakini hiyo sio kauli nzuri, …kama unajua kufa ni kufa, …lakini sio utamke maneno kama hayo, tena mbele ya binti yake,….ujue kuwa hata wewe unaweza ukatangulia, ukamuacha huyo mzee…’akasema mama Maua.

‘Hilo sikatai..lakini sio kwa hali kama ile, bado uwe unasumbua watu, ….yule mzee, alitakiwa atulie, asubiri kuletewa, lakini kwa umri kama ule bado anataka kila kitu akisimamie yeye..haya sasa unaona bado kwa umri kama ule anataka vibinti vidogo….’akatulia akimwangalia Maua. Maua akataka kusema kitu, lakini akatulia na kwamgalia mama yake.

‘Tunashukuru kusikia hayo,….’akasema mama Maua.

‘Mkanye binti yako, asifike tena pale, hata kama atasikia kumetokea nini, au huyo mzee kama ataweza kukupigia simu, kuwa uende kwa lolote lile, usifike pale kamwe….nipo hapo mwenyewe, mama mwenye nyumba, mama niliyahangaika na ile mali, ole wake akijileta hapo, …yatakayo mpata usije ukanilaumu..’ akasema na hayo maneno ya mwisho aliyaongea kwa sauti ndogo, kama vile hataki binti yake ayasikie

‘Ama kwa huyo malikia mtamsikia siku si chache, akiwa marehemu, na mwenzake, ambao kwa pamoja wameshirikiana kunisaliti, wanafikiria mimi ni mtoto mdogo,ehe ,waulize huko kijijini ninapotoka ukoo wangu unaogopewa….’akasema huku akitembea mwende wa hatua ndogo ndogo kuondoka.

‘Mimi siogopi hivyo vitisho vyako, pale ninapojua kuwa ninachotetea ni haki yangu,….’akasema Maua.

‘Sasa kwa huyo mzee una haki gani..?’ akauliza yule mama akiwa anamwangalia Maua kwa nyuma, kasimama kuelekea mlangoni, na kichwa akakigeuza kwa nyuma akitaka kumwangalia Maua, hakugeuka.

‘Kiukweli mpaka sasa sijajua vyema ni nani hasa aliyenipa huu ujazito, kama ningelimfahamu huyo mtu ni nani, nisingelihangaika kabisa na huyo mzee, ….’

‘Oh kume hata aliyekupa huo uja uzito hujamfahamu , ukaona ujaribu kwa Tajiri, sasa Tajiri kafariki, unaona mtu wa kumbebesha huo ujauzito ni mzee…..kweli nyie ni watu wa ajabu’akasema huyo mwanamama.

‘Mimi nitafanya uchunguzi wangu, na kama nikigundua kuwa huyo mzee anahusika kwa lolote na hili,…sitaogopa kufika hapo….’akasema Maua.

Yule mama akageuka mwili mzima na kumwangalia Maua kwa muda bila kusema neno, halafu akageuka 
upande ule alipokuwa mama yake Maua akawa kama anafikiria jambo, akamgeukia Maua na kumwangalia kwa makini, na Maua akawa kamkazia macho.

Yule mama akauinua ule mkoba wake, aliokuwa kaushikilia mkononi, akafungua zipu yake, na akawa akitoa kitu, ilikuwa ni kadi ya hospitalini, akamsogelea Maua, huku akiwa kashikilia ile kadi mkononi, akasema, kama ananong’oneza, japokuwa hiyo sauti ilikuwa ikisikika kwa mama yake, akasema;

‘Yule mzee hazai, alishazuiwa uzazi….kwahiyo usijidanganye kumsingizia huo ujauzito wako, tafuta mume aliyekupa hiyo mimba, au nenda kamsingizie mtu mwingine, ila kwa yule mzee utaumbuka bure….hii kadi yake, ya huo upasuaji, ….watoto wake wanaitafuta kama ushahidi, sijawapa bado….’ Halafu kama vile kakumbuka jambo, akageuka kwa haraka na kutembea kueleka mlangoni, na alipoukariba ule mlango, akageuka kumwangalia Mama Maua na kusema;

‘Na pia washauri hawa, …..hususani huyu binti yako, kuwa waa-che tabia hiyo ya utapeli, tabia hiyo itawapeleka pabaya, kama anashirikiana na mama yake mdogo, basi ole wenu, hiyo pesa itawatokea puani.…’akasema na baadaye akamgeukia Maua, akawa anamtizama sehemu ya tumboni,, halafu akasema;

‘Nakushangaa ina maana humjui hata aliyekubebesha hiyo mimba, ni ajabu kabisa, ina maana ulikuwa na wanaume zaidi ya mmoja,leo huyu kesho huyu, kweli dunia imekwisha….kweli nyie watoto munatuabisha sana…kwaherini….ila ujumbe ndio huo,….’akasema huyo mama nakuanza kutembea kwa haraka kuelekea mlangoni, hakuangalia nyuma tena.

Maua akataka kusema jambo, lakini akasita, kwani simu yake iilikuwa ikiita, akaipokea bila kuangalia ni nani aliyempigia, na mara akasikia sauti ya…..ilikuwa kama siku inakatika katika kwani sauti ilikuwa ikitoka kwa shida, ….Maua akatamani kuikata ile simu lakini ikawa kama vile hana nguvu ya kufanya hivyo na hapo, ni ile  sauti ilikuwa ikisema.

‘Oh…..Maua….oh…’sauti hii ilikuwa ikitoka kwa shida

‘Nani wewe….?’, akauliza Maua kwa mashaka aikijua kuwa ni watu wanamchezea kwenye simu.

‘Maua… dawa… ya-ngu, wewe- ndi-ye dakitari wa-ngu,..fika-haraka, hali-yangu sio nzuri nakuo-mba sa-sa-na…usiniache nikafa, nina….ujumbe…wa-ko...’simu ikakatika.

‘Ni Mzee, oh, masikini, sasa nitafanyaje...’Maua akajikuta akiongea peke yake, na wakati huo huo, akahisi ile sauti ya mwanamama ikimkanya , ikisema.

`Mkanye binti yako, asifike tena pale, hata kama atasikia kumetokea nini, au huyo mzee kama ataweza kumpigia simu, kuwa uende kwa lolote lile, usifike pale kamwe….nipo hapo mwenyewe, mama mwenye nyumba, mama niliyahangaika na ile mali….ole wake akijileta hapo, …yatakayo mpata usije ukanilaumu..

NB: Jumatatu njema.

WAZO LA LEO: Afya na Uhai wa mwanadamu ni kitu muhimu sana, tupende kuwajali, wagonjwa, kwa hali na mali, kuliko kuchangia sherehe, ambazo ni starehe tu ya kupita. Kila kampuni ni vyema ikawa na bima ya afya kwa wafanyakazi na familia zao, ili kujali afya zao, kuliko kujali marupurupu ya bwana wakubwa. Hii itajenga taifa lenye uhai…huo ndio ubinadamu wa kweli.

R.I.P Mkongwe Chinua Achebe,
 Mpiganaji mkongwe ametangulia mbele ya haki. Kwangu mimi mtu kama huyu kafa kiwiliwili, lakini kiroho, kiakili, tupo naye,....soma vitabu vyake; kama vile Things Fall aparty, au `No longer at Easy'... uongee naye. 
Mungu ailaze roho ya mpiganaji huyu mkongwe mahali pema peponi.








Ni mimi: emu-three

2 comments :

Anonymous said...

Oh kwanini umekatiza bwanaah,...thanks

Anonymous said...

Kweli amekufa kiwiliwili tu, tutakuwa naye kwenye vitabu vyake.