Maua alikutana na mabinti wa Mzee uso kwa uso, ilikuwa kama
mfanyakazi anayetafuta kazi, na akawa kwenye chumba cha usaili. Walikuwa kwenye
chumba kingine, baada ya mzee kuomba nafasi aongee na mama yake Maua, ikawabidi
Maua na wale mabinti wawili watoke na kwenda kwenye chumba kingine, kilichokuwa
ni ofisi ya mzee. Mama mdogo akaambiwa asubiri nje, ….
‘Kwanini mimi mnanitenga, hasa kila mkitaka kuongea mambo ya
huyu binti, kwanini mnaniambia niende
nje, wakati mimi nahusika zaidi na huyu binti, kuliko hata mama yake…au hamtaki
niwepo kwenye mgawo….’akalalamika Mama mdogo.
‘Usiwe na shaka, kama ukihitajika, tutakuambia…na kwa
taarifa yako hapa hakuna mgawo wowote…ni maswala ya kuelezana ukweli tu…’akasema
Mzee, na baadaye akawageukia Maua na mabinti zake.
‘Na nyie naombeni nafasi, kwanza nataka kuongea na huyu
mama, ni mama yake Maua, huyu binti hapa, naomba nafasi niongee naye, ili
tuwekane sawa….’akasema huku akisahiria kwa mkono.
‘Sawa baba lakini usije ukahamaki…..maana sisi tulipenda
kila unayeongea naye, tuwepo, ili kuhakikisha huathiriki kwa lolote lile,
lakini tuna imani na huyu mama, maana anaonekana ni muungwana,….’wakasema wale
mabinti.
‘Msiwe na wasiwasi..sitamfanya lolote baba yenu, sina
silaha, …nikagueni kabisa…..sina ganda wala risasi….nitaongea naye kistaarabu
kabisa…’akasema na wote wakacheka, pale alipokuwa akijikung’uta kwenye nguo
zake.
‘Sio hivyo mama…… ni kutokana na afya yake tunahitajika kuwa
makini kwenye maongezi, asije akahamanika,…na vitu kama hivyo, natumai unaelewa
nina maana gani.’akasema mmoja wa wale mabinti, na baadaye wakatoka na Maua
kuelekea kwenye chumba kingine
********
‘Usiogope mpendwa, ….’ Wakasema wale mabinti walipoingia
kwenye chumba kama ofisi.
‘Maua, jina zuri sana, naona linaendana na sura yako, ….kaa
hapo kwenye kiti, leo jisikie kama vile upo ofisini unatafuta kazi, na hapo upo
kwenye chumba cha usaili, unatakiwa ujiamini, …ukijua unatafuta jambo, au sio?’
akasema mmojawapo.
Maua akatabasamu, na akakaa kwenye kiti, huku, akiendelea
kutabasamu, hakusema kitu, ila moyoni alikuwa na mengi, na akitafuta jinsi gani
ataongea na hawo mabinti bila kuleta kutokuelewana kwenye hiyo familia……
‘Kwanini nataka kumtisha binti wa watu…..’akasema mmoja wa
mabinti huku akisogeza kiti na kmshika Maua mkono, akasema;
‘Bintii mwenyewe anaonekana mpole, hana hatia, na naona kama
yupo tofauti na wanavyoongea juu yake, ….lakini binadamu tuna siri nyingi, eti
mpendwa, …wewe ulijuana vipi na baba yetu?’ akauliza.
‘Nilijuana naye hapa hapa……’akasema Maua akimwangali huyo
binti aliyemuuliza swali, na wakawa wanaangaliana uso kwa uso. Binti huyu
alionekana ndiye mkubwa, na hata kuongea kwake, alikuwa akitumia busara zaidi.
‘Mhh, kwahiyo mkajenga urafiki…ukiwa hapa hapa kama
mfanyakazi wake, ….?’ Akauliza.
‘Hapana mimi sio mfanyakazi wake, sijawakuwa kuwa hivyo….’akasema.
‘Ina maana ulikuja kuje hapa, tunaomba utufafanulie kidogo,…samahani kama
kukuuliza hivi tutakukwaza, lakini sisi ni watoto wa huyu mzee, na
tunachohitaji ni ukweli, na kuhakikisha kuwa mzee, habebi majukumu makubwa
ambayo yatamhatarishia afya yake…’akasema huyo binti mmoja.
‘Kama unavyomuona ni mgonjwa,….., na nimesikia wewe umekuwa
karibu naye kipindi alichozidiwa, na ukamsaidia,..’akaongezea kusema huyo
mwingine.
‘Ni kweli….baba yenu anaumwa, na kama mngelichelewa, akaja
kukutana na huyo mwanamke tena, ….ingawaje nasikia wamemfunga, lakini siju kama
atakaa ndani muda mrefu…huyo hana nia njema na
mzee wenu…’akasema Maua
‘Huyo Mwanamke unayemuongela ni nani,…?’ akauliza mmoja
wapo.
‘Si huyo anayeitwa Malikia wa Mererani’akasema Maua.
‘Oh, ….a queen of
Mererani,…..mmh…..na yeye anahusika vipi na baba, msije mkasema na yeye ana
mimba ya baba, ….’akasema mmoja wapo na mwingine akaingilia kati.
‘Huyu mwanamke tunamjua, na sheria itachukua mkondo wake,
….tunachohitaji kutoka kwako ni kutuambia ukweli, …na usjisikie huru, kusema
kila kitu, ili tuweze kusaidiana,….mama yako kazungumza jambo, ambalo kwakweli,
limetushitua kidogo, na kama hatutapata ukweli, basi, kwa kauli ile peke yake,
tunaweza kusema kuna udanganyifu unaendelea, ….kitu ambacho
hatutakivumilia,….sasa hebu tuanze moja baada ya jingine’akasema
‘Mimi sijasema uwongo wowote …’akaanza kujitetea Maua.
‘Usiogope, ….hutujasema kuwa wewe umesema uwongo, ndio maana
tunahitajia kauli yako, na wala usiache kutuambia ukweli,….kwa kauli hiyo, kuwa
hatutavumilia, huenda kuna jambo hatulijui, …. kama kweli ulikuwa na mahusiano
na baba, sio mbaya, hayo ni maisha yake, na ana uhuru huo,… uwepo,….’akasema.
‘Sasa ukweli upi mnahitajia kutoka kwangu?’ akauliza Maua.
‘Kwanza tunataka kujua jinsi gani, ulivyofika hapa….’
‘Mimi nimetokea Dar, tukiwa na mama yangu mdogo,
tuliongozana na Tajiri, mpwa wa baba yako…ndio tulipofika hapa na ndipo nikaonana
na baba yako…na siku nilipokuja hapa nilimkuta akiwa katika hali mbaya, na
nashukuru mungu kuwa niliweza kumsaidia nilivyoweza, na wala sikujua kwa
kufanya hivyo, angefikia kunithamnini kiasi hicho,…ndivyo nilivyojuana naye……’akasema
Maua.
‘Kuja kwenu hapa, ilikuwa na dhamira gani, au kuna udugu
wowote kati ya mzee na nyie, maana anaweza akawa anawafahamu toka huko
kijijini, nimesikia mnatoka eneo moja, japokuwa ni kijiji tofauti au sio?....’akauliza
mmoja wapo na kabla Maua hajajibu mwingine akaongezea kwa kusema;
‘Au mlikuja kwa ajili ya kutafuta kazi, …maana Tajiri, ndiye mkuu wa shughuli za baba, huenda
alikuwa akitafuta wafanyakazi ndio akaona kuwa nyie mnafaa kazi zake..au sio?’
akauliza huyo mwingine, akiinua mikono juu kukolezea maneno yake.
‘Hapana ujio wetu hapa haukuwa wa kutafuta kazi,….kuna mengi
yalitokea huko Dar, na ….nisingependa kuyaongea kama mwenyewe hayupo,….na
tulipofka hapa Dar, na kusikia kuna mjomba wake hapa Arusha ndio tukaona
tuonane naye, ili tupate ufumbuzi’akasema.
‘Mwenyewe yupi?’ akauliza binti mmojawapo.
‘Mpwa wa baba yako, ….Tajiri’akasema Maua
‘Kwanini mpaka awepo, maana yeye kwa hivi sasa yupo kwenye
kesi, na huenda ikachukua muda, na sisi tunataka kuyaweka haya mambo sawa, ili
tuendelee na maisha, ….hili tulilolisikia halimuhusu yeye, ni kati yako na baba
…na sisi linatuhusu sana, kwa vile ni wanafamilia wa mzee, na mwisho wa siku
kama ni hivyo sisi tunahitajika kuwajibika…’akasema.
‘Kwakweli, huyo mpwa wa baba yenu ndiye muhusika mkuu ….kwangu
mimi na ujio wetu hapa, kwani ndiye aliyafanya tukafika hapa , baba yenu, alinihitaji
mimi kwa vile nilifanya yale yanayostahili kwa mtu kama yeye, na huenda
aliyakosa kwa watu wengine, na alipoyapata kutoka kwangu ndio akaniona mtu wa
tofauti…...’akasema Maua.
‘Hapo sijakuelewa, ….una maana gani kusema, huenda aliyakosa
kwa watu wengine, ina maana watu wote aliowahi kuishi naye, hawajawahi
kumfanyia hivyo?’ akauliza
‘Sijui, na wala siwezi kusema hawo alioishi nao hawajawahi
kufamnyia hivyo, nilivyomfanyia mimi, nimewaza tu, na kutoa kauli hiyo, sina
uhakika nayo, …hilo analijua mwenyewe baba yenu na sijui kwanini amenitunuku
kiasi hicho, ….yeye mwenyewe ndiye anayeweza kuelezea na mkitaka kujua zaidi
muulizeni yeye mwenyewe, …’akasema Maua.
‘Sasa hebu tuelezee, siku ulipokuja ukamkuta kazidiwa,
ulimkutaje, na unahisi ni nini kiliweza kumfanya awe hivyo?’ akaulizwa
‘Kwakweli nilimkuta katika hli mbaya sana, …..sijui ni kitu
gani hasa kilimsababishia awe hivyo….hilo swali la kwanini ilikuwa hivyo, ni
bora mkamuuliza dakitari wake na yeye mwenyewe, kwa maana mimi nilimkuta katika
hali hiyo, ni sikuwahi kuwepo kabla,…ila nijuavyo mimi hali kama hiyo kwa mtu
kama huyo, ukiangalia umri wake, huenda na maisha yake kabla,….mara nyingi ni
matatizo ya mashinikizo ya kimaisha, na yakizidi sana, mtu hufikia kuzimia…’akatulia.
‘Hilo tunalijua,….sisi tunachotaka kujua ni nani hasa
aliweza kumweka mzee katika hali hiyo, je ulimkuta mpwa wake, au ni nani
mwingine alikuwepo kipindi hicho,au kama ulisikia kuwa alikuwepo mtu fulani
kabla yaw ewe kufika….maana sisi mwanzoni tulijua ni kwasababu ya maelewano yao
mabaya na mama….’akasema mmojawapo akimwangalia ndugu yake.
‘Kiukweli, na sio kuleta fitina, hali yake imekuwa mbaya kwa
sababu ya kuwepo huyo mwanamke,….’akasema Maua na kukatisha, kwani aliona
kaongea jambo ambalo hakupenda kulisema, aliona kuwa huenda akachonganisha
watu, wakati mwenyewe hayupo.
‘Mwanamke yupi?’ akaulizwa
‘Oh, jamani, naombeni msiniulize mengine, kama mwenyewe
hayupo, naombeni, niulizeni kuhusu mimi, naogopa sana kuwa mbeya…’akasema Mua.
‘Aaah, usiogope, tunajua ….lakini hapo ni kusaidiana
kimawazo, na wala usitie shaka, kuwa kauli yako ni ushahidi, hapana, sisi
tunahitajia njie ya kulitatua hili tatizo, na kujaribu kuwakwepa wale wanaoweza
kumhatarishia maisha mzazi wetu,….kuna watu baba akionana nao kwasasa wanaweza
kumletea hasira, shinikizo, nk, sasa tunahitajia kuwapunguza hawo watu, na hata
simu zao zikipigwa, tutazizuia….sasa tunaomba sana, utuambie ni nani huyo
mwanamke.
‘Na mzungumizia huyo …..anayeitwa malikia wa Mererani’akasema
Maua
‘Oh, Malkia,…the queen
of Mererani nina hamu sana ya kuonana naye uso kwa uso, na sijui itakuwaje,
kama ni mfanyakazi wa baba, itabidi aache kazi, …haiwezekani awe anamsumbua
baba kiasi hicho, hivi ana nini kikubwa mpaka ang’ang’aniwe….hilo tutalifanyia
kazi, …’akasema mmojawapo.
‘Sasa mpendwa hili swali ni la muhimu sana, tunakuomba
utujibu ukiwa huru, kama hutaki hatuwezi kukulazimisha, lakini ni muhimu sana
sisi tujue, kama watoto wa mzee, ambao tunataraji kuchukua hatamu za shughuli
zote za mzee kutokana na hali yake..’akaambiwa.
‘Kama ni swali juu ya mzee wenu, naombeni sana muulizeni
mwenyewe,……’akasema Maua.
‘Swali letu ni kuhusu wewe na mzee, kama alivyodai mama
yako, kuwa una ujazito wake, ni kweli au sio kweli?’ wakauliza huku
wakimwangalia kwa makini.
‘Mama hajui lolote kuhusiana na mimi, na hayo yote
yaliyotokea hayajui kwa undani wake. Mama kaja karibu tu hapa, na leo kama
sikosei ni siku yake ya pili kuja hapa, na wala sikutaka ahusike na lolote
kuhusiana na maisha yangu. Yeye, alikuja mara moja akanikuta nipo namhudumia
mzee, na akachukua mambo juu kwa juu, ….naombeni msimuhusishe mama yangu na
lolote kuhusu juu yangu’akasema Maua.
‘Hujatujibu swali letu, vyovyote iwavyo, jibu la swali hilo
linatakiwa kutoka kwako, na sio kutoka kwa mama yako, mama yako alikusaidia
kujibu….kuelezea ukweli japo kwa ufupi, lakini anayestahili kujibu hilo swalii
ni wewe, je ni kweli una uja uzito wa baba?’ akaulizwa tena.
‘Hilo na mengine yote naombeni, mumuulize baba yenu,
sitaweza kujibu swali lolote kwa hivi sasa,ikizingatiwa kuwa hilo swala la
ujauzito wangu sijaliongelea mimi, aliyeongea ni mama, na mama hajui lolote
kuhusiana na mimi, naombeni, mvute subira, muhusika mkuu wa yote haya, ni
….Tajiri, yeye atakuja kuelezea yote, na kwa vile kuja kwetu hapa ni kutokana
na yeye, na mengine yote yametokea kwa sababu yake….siwezi kusema lolote kwa
sasa, hasa kuhusiana na huu uja uzito wangu…’akasema Maua.
‘Kwani kuna uzito gani wa kutamka, tunachohitaji kwako ni
kukubali au kukataaa,…hatuhitaji maelezo zaidi, .ni kusema tu ni kweli au sio
kweli…mengine yatajileta yenyewe, hatuna nia mbaya na wewe na kama ni kweli,
sisi tunahitajika kuwajibika nao, kama sio kweli, …..’akasema
‘Ukweli ulivyo ni kuwa…..’Maua alipotaka kusema, mara
akaingia Mama mdogo.
‘Hilo swali niachie mimi, nitawasaidia kuwajibu….’akasema
mama mdogo, na ilionyesha wazi, alikuwa sehemu akifuatilia hayo mazungumzo, na
hata wale mabinti wawili wakabakia kushangaa,
Yule mama mdogoma lipoona wale mabinti wameduwaa wakionyesha
uso wa kukerwa, akasimama nay eye akionyesha kushangaa, akasogea na kuwakagua
mmoja mmoja, hadi wale mabinti wakajikuta wakitahayari.
‘Mamamama…kama mngelikuwa Dar, nyie warembo, duuuh, …mbona
mnegetengeneza pesa,aisee, ndio nani nyie?’ akauliza swali kama vile hawafahamu.
‘Kwani wewe ni nani?’ akaulizwa swali na mmoja wa wale
mabinti.
‘Mimi ni mama yake huyu binti mnayeongea naye, na maswala
yake yote niulizeni mimi, kwani mimi ndiye ninayejua yote,kuhusiana na
yeye’akasema huyo mama.
‘Kwani wewe Maua una mama wangapi,?’ akaulizwa na binti
mwingine
‘Huyu ndiye mama yangu mdogo, niliyetoka naye Dar, lakini
naombeni msimuulize lolote kwa sasa, maana anaweza akawachanganya, nawaombeni
sana’akasema Maua.
‘Nitawachanganya nini….Maua hawa kama nilivyosikia ni
mabinti wa huyu mzee, na kwa vile wamekuja ni lazima waambiwe ukweli…japokuwa
muhusika mkuu ni baba yake, lakini kwa vile ……wao ndio wataongoza miradi ya mzee
wao, ni muhimu kuwaambia kila kitu….na huo mzigo ni wa kwao wao, kama familia…..’akatulia
kidogo, halafu akasema.
‘Mna bahati sana, mzee wenu ana roho ya paka, sisi
tulishajiandaa kwa mazishi, sasa nasikia ni mzima, …mmh, mzee wenu kweli ni
kiboko, ndio maana wanaongea mengi kuhusiana na yeye….’akawa anongea na Maua
akaona asipoingilia kati, huyo mama anaweza akaropoka,
‘Mama mdogo, …twende nje kidogo, tuongee pembeni kidogo, huu
sio wakati muafaka wa kuongea mengi, hawa ni watoto wa mzee, na wanahitajia
muda wa kupumzika, na usiwabebeshe mizigo ya mambo ya mitaani,…mengine waachie
wenyewe wataongea,….’akasema Maua na kumvuta mama yake nje.
‘Huyo tutaongea naye baadaye inaonekana ni muongeaji mzuri……’akasema
mmoja wa mabinti hawo,akiwaangalia mama na binti yake, wakivutana kutoka nje,
na hawakuwa na la kufanya ila kusubiria, hadi Maua atakapomalizana na mama
yake. Wakakonyezana, kuashiria wasubiri
************
‘Kuna taarifa kuwa Malikia katoroka , ….’akasema Mzee,
akiwaangalia mabinti zake.
‘Katoroka, ina maana hawo polisi walikuwa wakifanya nini
hadi huyo mtuhumiwa atoroke, …?’ akauliza mmoja wa mabinti zake.
‘Huyo mwanamke, ni hatari, tofauti na watu wanavyo
mchukulia, mwanzoni nilipomfahamu, alikuwa na tabia nzuri sana, lakini kadri
tulivyoendelea kukaa na yeye ndipo nilipoanza kumfahamu vyema, ….ni mwanamke
hatari, …hatari usivyoweza kuamini’akasema mzee.
‘Sasa kwanini ukamuajiri kwenye shughuli zako, huoni kama
unajiwekea hatari, ndani ya nyumba yako, na yote haya nasikia yeye ndiye
muhusika akishirikiana na wakili wa familia,…?’akasema binti.
‘Ni kweli, wote hawo, niliwaamini sana, sikujua kabisa, kuwa
ni nyoka,….nimewagundua baadaye sana, wakati mambo yameshaharibika……na nimewakabidhi
kwa polisi, sio jukumu langu tena….kama wakishindwa, mimi nitajua nini la
kufanya….’akatulia.
‘Baba polisi hawatashindwa, na kwa vile wana ushahidi wa
kutosha, ni swala la muda tu, tatizo ni kama huyo mtu katoroka, je, hawezi kuja
kuleta madhara kwako,….na je hakuna lolote limejificha kati yao na wewe
mwenyewe?’ Akauliza mmoja wa binti zake
‘Polisi wameniambia watazidisha ulinzi, na watamfuatilia,
hatua kwa hatua, lakini hilo hatuwezi kuliamini, kwani kama kaweza kutoroka,
mikononi mwao, ..atashindwa kuja kufanya lolote hapa kwetu…ndio maana
nawatahadharisha mume makini, na polisi wamesema, asitoke mtu yoyote bila
kibali chao,…..’akasema mzee.
‘Sawa mzee, …..lakini tuna mazungumzo muhimu na wewe, maana
tumefika hapa tukakutana na mambo mengi, hilo, …la huyo mwanamke na wakili
wako, ni kubwa sana, lakini pia kuna hili la kifamilia, nalo lina umuhimu wake,
tunahitajia ufafanuzii kutoka kwako, …..’akaambiwa.
‘Naombeni hilo tulisubirishe kwanza,….kwani nahitaji kuongea
na Tajiri, …kuna mambo mengi ambayo yanamuhitajia awepo, ningewaomba hilo swala
la kifamilia, ….hasa kuhusu huyo Maua,…msubiri kwanza, nahitaji muda wa kuongea
na huyo binti mwenyewe,….kwani inaonekana mama yake hajui mengi kuhusiana na
binti yake, na mama yake mdogo, …..mmh, ni mtu wa tamaa ya pesa, anaweza
kuongea lolote, kama kuna pesa,..hana ukweli, mkweli na mtu wa kutegemewa ni
huyo binti, ni mtu muhimu sana kwangu…’akasema Mzee
‘Kwahiyo baba hayo yanayongewa kuhusiana na Maua ni kweli?’
akaulizwa.
‘Ni kweli , ndio ni kweli, lakini yapi, ndio swala muhimu…Ila
kiukweli namuhitajia sana huyo binto katika maisha yangu, kama kweli
mnanipenda, na mnatathamini afya yangu, ….huyo binti ni muhimu sana kwangu,…lakini
naombeni mvute subira, sina nia mbaya kwa yoyote yule, na yote yatategemea yeye
mwenyewe huyo binti,….tulieni,…kwanza….’akatulia kidogo, halafu akasema;
‘Baba,….yupo mama, hujamalizana naye, huoni kwamba, kama
ukileta mke mwingine utajibebesha mzigo juu ya mzigo, na ukizingatiwa kuwa ,
ana ujauzito….sasa hatujui….’akasema binti na mzee akamkatisha na kusema;
‘Hayo ni maneno tu,..hata hivyo, kama ni kweli, nitajua …..Lakini
naombeni muda, maana yeye ni muhimu sana kwangu na kwa afya yangu,
msilichukuliea juu kwa juu, ……kuna mengi yameongelewa hapo, ambayo huenda ni
mbinu tu, …..za kuhadaa, sizani kuwa huyo bintu ana uja uzito,…’akasema na
kuinama.
‘Lakini mzee, wewe si ndiye inajulikana kuwa una mahusiano na
yeye, na ina maana matuanda ya yoye hayo ni pamoja na hayo, ….’akasema binti na
kutulia na mwingina akasema kwa haraka;
‘Hata hivyo baba , nakumbuka kipindi cha nyuma, mlisema kuwa
wewe umezuiwa kutokakupata mtoto, ulifanyiwa upasuaji au kitu kama hicho, sasa
iweje….’akasema huyo binti na mzee wake akamkatisha na kusema;
‘Ndio maana nawaomba mtulie, ….kuzuiwa kutokupata mtoto, sio
kwamba, siwezi kupata mtoto, ….nina nguvu zangu za kutosha, na naweza
kurejeshewa hali yangu nikapata mtoto, ile nilifanyiwa kwa muda, ni kitu
unaweza kuwekewa, na ukitaka mtoto unawezeshwa, kitaalamu….lakini….’akatulia
kwani simu ililia.
Wanafamilia wote wakageuka kuiangalai ile simu, na mzee
alipotoka kuinuka kuipokea, binti yake, akamzuia;
‘Baba simu, yoyote kwa hivi sasa usianze kuipokea wewe, kama
walivyosema polisi, na pili huwezi kujua ni nani anapiga hiyo simu, subiri
kidogo….’yule binti akasogea kwenye ile simu na kubonyeza kitufe walichopewa na
polisi na ndio akaipokea hiyo simu.
‘Ni nyumbani
kwa…….’akaanza kuongea na huyo mpigaji, akakatisha na kusema.
‘Najua mnarekodi haya ninayoongea, …najua polisi
wanafuatilia haya…….’akatulia.
‘Ni nani wewe unayeongea?’ akauliza huyo binti.
‘Nomba niongee na mzee, yeye akisikia sauti yangu atajua
kuwa mimi ni nani, kwani wewe ni nani ?’ akauliza.
Wewe ndiye umpiga simu, unahitaji kujitambusliha kwanza,
…mzee hawezi kuongea na yeyote kwa hivi sasa’akasema huyo binti.
‘Hawezi kuongea wakati nimesikia keshafufuka, ….mzee huyo ni
mwanga, alijifanya amekufa, kumbe yupo hai……’akasema huyo mtu, na yule binti
akakunja uso, hakukata simu, akatulia.
‘Naomba niongee na yeye, ni muhimu sana, na kwa ajili ya
biashara zake , ni kwa ajili ya mambo yake, na
kwa jili ya mpwa wake, ….kuna
mambo muhimu nahitajika kumuelezea, kabla sijatoweka kabisa…..’akasema huyo
muongeaji.
‘Kama hujaniambia wewe ni nani unayeongea siwezi kukuruhusu
ukaongea na mzee’akasema huyo binti.
‘Na mimi siwezi kukuambi mimi ni nani, kwa vile mimi
sikufahamu,..wewe ni nani?’ akauliza.
‘Mimi ni mmoja wa mabinti wa huyu mzee…’akasema
‘Oh, kumbe kweli, mumeshafika..oooh, lakini hata hivyo, haya
yanawahusu sana, nataka kuwalezea kuhusiana na huyo ambaye ni mtendaji mkuu wa
mzee wenu,…na Malaya wake’akasema
‘Nani huyo, na huyo Malaya wake ni nani?’ akauliza
‘Tajiri na huyo Malaya wake Maua’akaambiwa.
‘Ehe….endelea….’akasema huyo binti, lakini kabla hajasikia
zaidi, mzee, akafika na kumnyang’anya ile simu,……
‘Ni huyo mwanamke shetani…hebu nipe hiyo simu niongee naye
mwenyewe….’akasema mzee na kuishikilia ile simu, aliyokuwa kaishika mtoto wake,
na mtoto wake hakutaka baba yake aichukue.
‘Baba, acha kuongea na huyo mtu,…..ata….’akasema huyo binti,
na wakawa kama wananyang’anyana ile simu, na mara wakasikia sauti mlangoni,
ikisema;
‘Sisi ni polisi …..’
‘Polisi?!’ wakajikuta wote mle ndani wakisema hivyo,
Na mmoja wa wale mabinti akafungua mlango, na kweli polisi
wakaingia ndani, wakiwa na silaha mkononi, na mmoja akasema;
‘Kuna simu imepigwa na cha ajabu wote walikuwa wakiongea
humu humu kwenye hili jengo..’akasema polisi.
Mzee akawa anawangalia hawo polisi huku akiwa kashikilia
simu, na bibti ambaye aliamua kuiachia hiyo simu, akasema;
‘Simu tuliyokuwa tukiongea nayo ndio hii, na sijui kama yupo
hewani bado, akajaribu kusikiliza lakini simu ilishakatwa, akasema;
‘Hayupo hewani….
‘Mpigaji wa upande wa pili anapiga kutoka kwenye jengoo hili
hili, …..na askari wameshazunguka jengo hawezi kutoroka,….’akasema na
kuwageukiwa wenzake.
‘Anzeni msako kila kona ya hili jengo, hawezi kutuzidi
ujanja huyu mtu’akasema na wote wakatoka na kuanza kutafuta. Ilichukua nusu
saa, lakini hawakuweza kumpata mtu yoyote.
‘Hakuna mtu yoyote tuliyempata, mna uhakika kweli hakuna
sehemu nyingine ya hili jengo..?’ akauliza yule askari.
‘Hakuna sehemu nyingine kama mumeingia kila chumba, …..basi
ina maana huyo mtu, atakuwa kaweka waya, au …..’akasema mzee.
‘Sio waya…mitambo yetu inaonyesha wazi kuwa wote wawili
mpigaji na mpokeaji waalikuwa kwenye hili jengo,…..’akasema huyo askari.
‘Ni nani huyo mtu mwingine?’ akauliza mmoja wa huyo binti.
‘Ni mmoja wa watuhumiwa ambaye ametoroka rumande, na huyu ni
mtu htari sana, ….ni lazima akamatwe haraka, la sivyo, kunaweza kutokea mauaji,
na ni muhimu sana, msitoke kabisa humu ndani’akasema huyo askari.
‘Kama kaweza kuingia humu na kupiga simu, na hamukuweza
kumpata, ina maana mtu huyo anaweza kufanya lolote bila ya kupatikana..’akasema
huyo binti.
‘Tutampata tu,…..maana keshatuonyesha njia ya kumpata, hilo
ni swala la muda, na kwahiyo tunahitajai ushirikiano wenu wa kila namna,
akiwapigia simu tu, fanyeni kama tulivyowaelekeza,….kutakuwa na watu wetu
watafuatilia kila analofanya,…..tutamkamta tu’akasema huyo askari.
‘Kwani ni nani huyo?’ akauliza tena yule binti aliyeuliza
hilo swali.
‘Ni Malikia wa Mererani….’akasema huyo askari na simu yake
ikaita kabla hajamalizam akaipokea haraka, akawa anasikilia na uso wake
ukabadilika rangi, akageuka kuwaangalia wenzake na baadaye akasema;
‘Hakikisheni dakitari anafika hapo haraka iwezekanavyo,….’akasema
na baadaye akawageukiwa mzee na mabinti zake, na kusema;
‘Tajiri kapigwa risasi na hali yake ni mbaya sana…’akasema
‘Eti nini…..?’ akasema mzee, na mara akashika kifuani, na
kuanza kupepesuka, …..
‘Baba…..’ wakasema mabinti, na mmojawapo akakimbilia
kuchukua kichupa cha dawa.
NB: Ni nini kitaendelea baada ya hapo
WAZO LA LEO: Afya
ya mwanadamu ni muhimu sana, tunapokuwa na wagonjwa wenye matatizo makubwa
ambayo hayahitajii mashinikizo ya kimaisha, kama matatizo ya kupanda au kushuka
kwa mapigo ya moyo, …magonjwa ya moyo, vidonda vya tumbo kisukari, tunahitajika
tuwe makini sana, na watu hawo wanahitajia uangalifu wa karibu. Tuwe karibu
nao, tufuate masharti ya dakitari, na kukwepa kila jambo linaloweza kuwaathiri
afya zao.
Ni mimi:
emu-three
3 comments :
Bonge la wazo hongera sana pamoja daima.
Shalom bonge la wazo, je kisa chenyewe sio bonge...nashukuru sana mpendwa kunipa kampani, ubarikiwe sana.
Yani kila kitu kiko bomba uko juu miram pamoja daima
Post a Comment