Maua akiwa ameduwaa akiwa mwingi wa mawazo, hasa pale
alipomuwaza mama yake, akijua sasa mama yake keshaondoka, akahisi upweke
fulani, na akiwa hivyo, mara akaingia mtu , mwanzoni alijua ni mama yake
aliyekuwa akifunga mlango vyema, lakini akahisi kuwa mlango upo wazo, hakutaka
kugeuka mara moja, ….baada ya sekunde kadhaa, akageuza kichwa chake na
kuangalia huko mlangoni.
Alipogeuza kichwa chake akiwa anajua kuwa huenda ni mama
yake ambaye huenda aliamua kurudi, lakini kumbe siyo mama yake, aliyekuwa
kasimama pale mlangoni, huku akiwa kaushikilia mlango, na huku akiwa katizama
nje, huko alikotoka, huyu alikuwa sio mwingine, alikuwa ni Tajiri. Maua alibakia
akishangaa, mbona huyo mtu badala ya kuingia ndani, amesimama pale mlangoni,
halafu anaonekana akishughulishwa na jambo jingine……..
‘Labda amefika na maaskari, …..’akasema Maua, huku akijiweka
sawa, akageuza kichwa mara moja na kumwangalia yule mzee ambaye kwa muda huo
alikuwa kajiliza kwenye sofa lake, na alionekana kuchoka,…na ingelikuwa vyema,
kama angepata nafasi ya kupumzika. Maua akataka kwenda kumwambia Tajiri kuwa
mzee hatakiwi kusmbuliwa tena….lakini…
Kabla hajamwambia lolote, yule jamaa akatoka pale mlangoni,
na kurudi huko alipotoka, na mlango ukabakiwa wazi, kwani huo mlango
ukiushikilia kwa muda, na weneywe hukaa hivhi hivyo kwa muda, na baadaye
hujifunga,….Na Maua alipouona upo wazi, alikwenda hadi pale mlangoni, akaufunga ule
mlango, na mara akasikia sauti ya mzee, ikisema.
‘Maua ufunge huo mlango kabisa kwa fungua,….. maana nataka
tuongee, nimeota ndoto, na mimi ndoto hunielekeza jambo,…..nisingelipenda mtu
kuja kutusumbua kabla sijasema hilo ninalotaka kukuambia,….na hata hivyo, naona
muda wa kutumia dawa zangu umefika, kwahiyo kwanza,….sijui tuanze lipi?’ akawa
kama anauliza.
‘Dawa zako ni muhimu Mzee…..kwanza jail afya yako….’akasema
Maua.
‘Ndio maana nakupenda, na nahisi wewe ndiye chagua halisi la
moyo wangu, kwanza nipate hiyo dawa au sio….lakini nikianza na hiyo dawa,
itanilewesha na nitashindwa kukuambia hilo ninalotaka kukuambia,…unaona, sasa
tuanze lipi?’ akawa kama anauliza.
‘Mimi naona unywe dawa zako, na kwa vile mimi bado nipo,
utaniambia tu, hakuna shida mzee wangu…..’akasema Maua. Yule mzee, ambaye alikuwa
kavaa fulana nyepesi, na nguo za kulalia…akachukua shuka, akajifunga kiunoni,
…..na kuvua ile suruali ya kulalia, huku akisema
‘Samahani sana Maua najua wewe ni dawa yangu, lakini siwezi
kupuuza masharti ya dakitari wangu, kweli ni muhimu sana ninywe hiyo dawa yangu, na pia nahitajika
kupumzika…lakini kabla ya hayo yote, nahitajia msaada wako, …..’akasema Huyu
mzee, na Maua akamwangalia kwa mashaka.
‘Msaada gani mzee wangu, ….?’ Akauliza Maua huku anamwangalia
huyo mzee, akiwa kafunga shuka kiuononi….mzee, huyu alionekana kupungua, kwa
muda mfupi, mwili wake, ulikuwa umepungua sana, sio kama alivyoonekana awali.
Yule mzee, alisogea hadi kwenye meza kubwa, akavuta droo
zake na kutoa kichupa kidogo, akakifungua na kukinusa, akakitikisa, halafu,
akamwangalia Maua.
‘Nahitaji unichue na maji ya uvuguvugu….kama hutojali,
ukishamaliza unanipaka haya mafuta…yananisaidia sana…na kwa vile wewe ni dawa
ya moyo wangu, najua leo mwili wangu utakuwa na afya tele…usiniogope, ukiwa na
mimi uwe huru, na nakuhakikishia kuwa siwezi kufanya jambo lolote baya dhidi
yako,….ukiwa hutaki wewe niambie hutaki, au huwezi…siwezi kukushurutisha….’akasema
na huku akijiandaa, akavua kile kifulana chepesi, na kubakiwa kifua wazi,
….alionekana kutokujali.
Maua kwanza alisita kuifanya ile kazi, lakini baadaye akaona
ni kazi rahisi tu, basi akaenda akachukua maji ya uvuguvugu, akayachanganya na
mafuta aliyoelekezwa, akaanza kumchua yule mzee, akiwa amelala kifudufudi,
alifanya hivyo, kwenye mikono, mgongoni na miguuni akitumia kitambaa laini
ambacho alielekezwa na huyo mzee.
‘Oh, ….kweli wewe unafahamu hii kazi, nahisi mwili wote
ukiwa na nguvu,…..nakuhitajia sana Maua katika maisha yangu,…nakuomba sana,
unikubalie ombi langu la mwanzo, kuwa wewe uwe mke wangu, usijali umri….japokuwa
ndoto….kuna njozi, ilinijia ….sijui ina maana gani, lakini usijali….’akasema
huku akijituliza kwenye sofa lake, ilionyesha dhahiri kuwa dawa zimeshaanza
kufanya kazi yake na macho yake yalikuwa yakiishiwa nguvu, kama mtu analiyeweshwa
madawa ya kulevya.
‘Mzee wangu achana na mawazo hayo…mimi ni sawa na mjukuu wako,
hata hivyo kuna mengi ya kuongea, ambayo ni muhimu sana kwangu, lakini kwa sasa
nakuomba wewe upumzike, ukiamuka najua tutaongea kwa marefeu na mapana……’kabla
hajamaliza mlango ukagongwa.
‘Nani huyo tena, …?’ akauliza huyo mzee kwa sauti, na
alipoona kupo kimiya akamgeukia Maua na kusema;
‘Hakikisha kwa yoyote atakayekuja, hanisumbui, ….wengi
wanajua nimeshakufa, waambie hivyo hivyo, kuwa mzee keshakufa,…au
hajazindukana, na huenda hayupo hai’akasema huyo mzee.
‘Eti nini….kwanini niwaambie umeshakufa wakati bado upo hai?’
akauliza Maua.
‘Kama nilivyokuambia…waambie nimeshakua, ni bora kwao…..’Yule
mzee akawa anaongea kama anaweweseka, kuonyesha yupo usingizini…Maua alitulia
kwa muda, ….na alipoona huyo mzee, katulia, kuonyesha kuwa keshalala, …..akatafuta
shuka kubwa jeupe, kwenye kabati, akaja akamfunika vyema, akiacha sehemu ndogo
tu ya usoni ya kutolea hewa,…ili kumfanya yoyote atakeyekuja asimuone vyema,
‘Hapo anaonekana kama kafa kweli….’akasema Maua huku
akitabasamu
*******
Tajiri aliharakisha ili amfikie yule mwanamke , lakini
alishachelewa, kwani yule mwanamke alipotoka nje, aliingia kwenye boda boda, na
ile boda boda ikaondoka, nay eye akabakia na kitendawili kichwani, ambacho
hakuweza kukutegua.
‘Huyu mwanamke ni nani..hii sura kama naifahamu, sio yeye
huyu kweli, lakini sio yeye….hapana, labda awe ni mama yake, ….haiwezekani awe
amechakaaa kiasi
hiki..haiwezekani,….’akawa anaongea peke yake akiwa anasindikiza ile boda boda
kwa macho ambayo ilikuwa inakwenda kwa kasi.
Alipoona hana la kufanya, akarudi ndani, na kuelekea kwenye
mlango wa chumba ambacho mjomba wake yupo, hakujua ni nani mwingine yupo humo
ndani, kwani alipofika mara ile ya kwanza, hakuchungulia ndani, ila alihisi
kama kuna mtu ndani..
‘Huyo anaweza akawa ni dakitari….’akajisemea moyoni, huku
akifungua kitasa cha mlango, na akakuta mlango umefungwa.
‘Ni nani tena kaufunga huu mlango…?’ akauliza na akageuka
huku na kule kuwaangalia wafanyakazi wa humo ndani, lakini wafanyakazi hawakuwepo hapo karibu, walikuwa nje, …akatoka
nje, na huko akakutana na mama mdogo.
‘Heee,..mama kumbe upo hapa,…. nilijua mpo hotelini
kwenu….upo na Maua?’ akauliza.
‘Hujamuona huko ndani,…Heheheee, Maua, anamuenzi mzee, maana
mzee keshazimia kwa dogo dogo, nakuambia ukweli, bosi sasa ukizubaa, mzee
anachukua ngoma ,…na hata mimi naona iwe hivyo, kwa hivi sasa hatutajali kuwa
ana mimba yako’akasema huyo mama.
‘Acha utani wako, mzee yupi anachukua ngoma?’ akauliza.
‘Kuna wazee wangapi humo ndani, …?’ Mama mdogo akauliza
swali huku akimwangalia Tajiri kwa makini, na Tajiri, akawa kama hamsikilizi, ….yeye
akageuka kurudi ndani, akijua kuwa huenda aliyekuwepo huko ndani ni huyo mzee
anayemuongela mama mdogo, na yupo na Maua, kwani asingelikuwa na ujasiri kwa
ukaa na maiti, au huenda mwili wa mjomba wake umeshachukuliwa, ….
‘Kwahiyo una maana Maua yupo huko ndani….na ….huyo mzee?’
Akauliza Tajiri.
‘Ndio maana yake, …..nakuambia mzee haambiwi kitu ….na Maua
naye ..oh, tatizo lake bado mdogo, ningelikuwa mimi…ooho…nisingeliipoteza hiyo
bahati…’akasema huku akitabasamu, na alipomwangalia Tajiri, akainama chini na
kusema;
‘Ndio Maua yupo huko ndani, anamuenzi mzee, siunajua tena
mapenzi ya wazee, wazee wanajua jinsi ya kulea watoto wadogo,….wewe zubaa tu,
..nikuambie kitu bosi wangu, ukitaka niweke mambo sawa, ongeza dau,…nipe mshiko
wa nguvu,..la sivyo,…mzee anamchkua binti kilaini’akasema mama mdogo.
‘Wewe mama wewe, acha tamaa, ina maana pesa zote ninazokupa
hujarizika,….hivi wewe una akili kweli..hayo unayoongea yanatoka akilini mwako,
au ni tamaa ya pesa ndio inakutuma iwe hivyo…..ngoja nikaonane na huyo mzee
wako…’ akasema Tajiri huku akiwa anatembea kuelekea huko ndani.
‘Nikuambia ukweli ….bosiiii, mwenye kisu kikali ndiye
atakayekula nyama….haheee’akasema huyo mama mdogo huku akicheka utafikiri yupo
nyumbani kwake.
Tajiri moyoni alishaanza kuhisi kitu kama wivu, lakini
hakuwa akimuamini sana huyo mama, lakini moyoni mwake, alitaka kumuona huyo
anayeitwa `mzee’ ni nani, au ni yule dakitari,… ni mzee gani huyo anayetaka
kumchukua Maua, hapo akahisi kuna jambo, na ili apate ufumbuzi wake, ni lazima
aingie ndani kwa haraka.
Akafika pale kwenye chumba na alipofungua kitasa , mlango ukawa
haufunguki, ina maana umefungwa kwa ndani, Tajiri, akahisi joto likiogezeka,
wivu ukazidi kumpanda, ….akagonga, kimiya….akatoka hadi sehemu wanapoweka
fungua za akiba. Huwa kuna sehemu wanaweka ufunguo za akiba, ili kama kuna
dharura, huenda mzee kazidiwa ndani, wanazitumia hizo funguo.
Aliporudi, na kufungua mlango, ukafunguka bila hata kutumia
ufungu, akaingia ndani moja kwa moja, na akahisi maji yakimwagika huko
bafuni, akajua kuna mtu anakoga,
akasogea kidogo pale alaipolala mzee wake…..’ na simu yake ya mkononi ikaita.
Ilikuwa ni simu kutoka kituo cha polisi, na aliambiwa kuwa
Malikia anataka kuongea na yeye, na ni muhimu sana, ikabidi asogee pembeni na
kuanza kumsikiliza Malikia;
‘Haya sema…’akaongea akiwa hana shauku ya kumsikiliza.
‘Sikiliza wewe mwanaume, ….usipofanya mpango wa kunitoa humu
ndani, nitahakikisha kuwa na wewe unaingia humu, na ujue ninajua mambo yako mengi….ukumbuke
tulikuwa pamoja katika mpango wa kumuua huyo mzee, na mambo mengine mengi
nilikuwa nikishirikiana na wewe…na mzee…kwahiyo fanya ufanyalo kesho nitoke
humu ndani….kwani nisipotoka , kila mtu kwenye familia ya mzee atajua hilo,
kuwa mimi na wewe tulikuwa na mango mmoja wa kumuua huyo mzee….’akasema
Malikia.
‘Nitajitahidi, lakini polisi wamesema haitawezekana’akasema
Tajiri huku akikunja uso kwa hasira
‘Kwanini haiwezekani,…hakuna kisichowezekana kukiwa na pesa,
tumia pesa, usiwe bahili, nenda na mshiko wa nguvu, kaonane na mkuu wakituo,….kwani
pesa zako, tumia pesa za mzee….kwanza yule mkuu wa kituo ni mtu wangu….mnoko ni huyo jamaa aliyekuja
ambaye nasikia atakuwa ndiye mkuu wa kituo….’akasema Malikia kwa haraka haraka.
‘Hata hivyo…..muda kama huu….’akaanza kulalamika Tajiri
‘Nakuambia ukweli….nenda kaonane na huyo mkuu sasa hivi….unanisikia
lakini….ukumbuke, nina mambo yako mengi, mabaya yako mengi…, ambayo familia ya
huyo mzee, wakiyaona, watahakikisha unakwenda jela, au unakufa, na hutaweza
kurithi chochote kwenye hiyo familia,….nilitaka kumuonyesha mzee wako siku
mbili zilizopita baada ya kusikia kuwa unataka kunisaliti, lakini, nikaona
haina haja,…muda wake utafika tu, na….kama usiponitoa hapa,…hilo litafanyika…..’akasema
Malikia.
‘Malikia sio kwamba sitaki kufanya hilo unalosema, ….nimeshafanya,
nimekwenda kuonana na mkuu wa kituo, nilipotoka hapo tu, nikamfuata….lakini
ndiye huyo huyo aliyesema kuwa dhamana , haiwezekani….lakini nitajaribu kwenda
kumuona tena’akasema huku akiwa na wasiwasi, kwani anavyomjau Malikia, …ni
lazima anaweza kufanya lolote kama akiona hana njia nyingine, …..na anajua kuwa
malikia ana mambo yake mengi ya siri na akiyaweka hadharani …ataumbuka, na
asingelipenda kurudia ule umasikini……
‘Nispofanya jitihada za kumtoa huyu
mwanamke…ataniumbua,…..na nitakosa kila kitu, …haiwezekani,…ni lazima nimtoe
humo ndani kwa njia yoyote ile…..’akawa anawaza akilini.
‘Na sikiliza, najua sasa hivi upo na huyo Malaya…nakuambia
ukweli, kama unataka kuumbuka, endelea kuwa naye…sikiliza wewe mwanaume, achana
na huyo mshamba, malaya wa mitaani, unataak nini kwake, ….kama utaendelea kuwa
naye ujue huyo huyo ndiyee atayakutia hatiani, ….hujiulizi kwanini haya
yataokee hivi sasa alipoonakena huyo kinyamkera wako,….hakikisha wanaondoka
hapa Arusha haraka iwezekanavyo, hawo ni mashushu…wametumwa toka Dar, kuja
kukuchunguza’akasema Malikia.
‘Hawo usiwajali..hawana shida,….na wala sio mashushu kama
unavyofikiria wewe, hawo wamekuja na mambo yao mengine,….ambayo hayakuhusu…’akasema
Tajiri
‘Hawana shida eeh ndivyo unavyojidanganya, ngoja nitoke
humu…na nikitoka tu, nitahakikisha narudi humu, nikiwa najua hakuna kiumbe
ambacho kitafungua mdomo mahakamani, nakuhakikishia nitatoka humu bila hata
msaada wako,…..hilo naapa, kama una mapenzi na huyo Malaya wako, na wengineo,
hakikisha wanauhama huu mji…kabla sijatoka’akasema Malikia na simu ikakatika.
Tajiri,…. alipogeuka, akamkuta Maua keshatoka bafuni, na
alikuwa akifuta maji kichwani huku akionyesha kuwa alikuwa akisikiliza hicho
walichokuwa wakiongea na Malikia…., akamwangalia kwa makini, na Maua akawa
anaendelea kufuta maji kichwani huku anatabasamu, Tajiri akageuza kichwa
kuangalia kule alipolala mzee wake, halafu akageuka kumwangalia Maua.
`Maua ulikuwa na nani humu ndani?’ akauliza Tajiri kwa
hasira
‘Nailikuwa na nani humu ndani….mbona sikuelewi, walikuwepo
wengi kabla hujafika, na…alikuwepo docta, alikuwepo mama….una maana gani
kuuliza hivyo?’ akauliza Maua huku akionyesha uso wa kushangaa.
‘Oh, hamna shida, lakini mmmh, Maua ..una ujasiri gani wa
kukaa humu ndani,…na huyo docta yupo wapi, mbona, hajauchukua huu mwili….na
nimesikia kuna mzee anataka kukuchukua,…ndio huyo docta au ni mzee gani huyo?’
akauliza Tajiri, akihisi wivu ukimtinga akilini.
‘Mwili gani huo, mbona sikuelewi,….na unasema kuna mzee
anataka kunichukua, kunipeleka wapi….mbona uanongea mambo mengi nisiyoyaelewa,
upo sawa kweli?’ akauliza Maua.
‘Mwili gani,…..!’ akasema kwa mshangao, huku akigeuka
kuangalia kule alipolala yule mzee, hakupenda kumwangalia sana, maana akilini
mwake, alikuwa kama anajuta, anahisi kama anahusika katika kumwangamiza mjomba
wake, akasema
‘Si huu mwili wa mzee, ukiendelea kubakia hapa huoni kama
utaharibika, sitaki mzee wangu afanyiwe hivi, ana stahili haki zote, na mimi
ndiye mtoto wake niliyekaribu naye,….’akasema huku akiangalia kule alipolala
mzee wake kwa muda, halafu akageuka kumwangalia Maua.
‘Tajiri, ina maana na wewe ulikuwa katika mpango, wa
kuhakikisha kuwa mzee wako, mjomba wako anayekujali anakufa, na …huna hata haya…ya
kusema hayo unayoyasema…una uhakika gani na hilo unalolisema…!’akawa anataka
kuongea, lakinia akasita.
‘Mimi sikuwa kufikiria hivyo,….hata siku moja, eti nimue
mzee, mjomba wangu, halo halipo kwangu, na sikuwepo katika mpango huo, na
sitaweza kufanya hivyo kamwe, japokuwa yule mwanamke, alikuwa akinishawishi
nifanye hivyo….’akasema huku akionyeshea mkono kwa kupinga hilo, akawa
anatembea huku na kule, kama aliyechanganyikiwa.
‘Usipige kelele….’akasema Maua, alipoona huyo jamaa anaongea
kwa jaziba huku akiwa kazifunga nwele zake kwa juu.
‘Nakuambia ukweli, huyo mwanamke….atakona cha mtemwa kuni….unaona
sasa, sasa hivi anakiona cha mtema kuni….hata hivyo, inabidi nitajihiidi huyo
mwanamke apate dhamana, maana, hata kama mzee angelikuwepo angelifanya hivyo,
kwani alikuwa mtu wake wa karibu….na kashikilia mpini’ Akasema Tajiri.
‘Hivi wewe bado unamwamini huyo mwanamke wako, mtu aliyetaka
kumuua mjomba wako…hebu fikiria hayo aliyomfanyia mzee wako, …huoni
ilivyotokea, kwani kwanini mzee alifikia kuwa katika hiyo hali mbaya…si
ulikuwepo kipindi ambacho mjomba wako, alifikia hatua hiyo mbaya..nakuuliza si
ulikuwepo?’ akauliza na kabla Tajiri hajasema kitu,Maua akasema kwa sauti ndogo, akiogopa kumsumbua
huyo mzee
‘Na…ni nani aliyesababisha yote hayo…..? Na ni nani
aliyeweka sumu…., ili mjomba wako afe..na bado upo nyuma ya huyo mtu, kwa namna
hiyo, kila mtu atakushuku, kuwa na wewe unashirikiana na huko mwanamke…!’akasema
Maua.
‘Usiseme hivyo Maua,..hujui mambo haya yalivyo, adui yako,
…anaweza akawa msaada mkubwa katika kufanikisha mambo haya ya kibishara, na …pia
huyo mwanamke ana siri kubwa sana za mzee,…..na mimi, tusiposhirikiana
naye…ooh, siwezi kukuambia zaidi maana mambo mengine ni ya siri’akasema Tajiri.
‘Mambo gani hayo ya siri, ya kuuana..wewe umeshajua kuwa
huyo ni adui wa mzee wako, na lengo lake ni kuhakikisha huo mzee, anakufa nay
eye, aanrithi mali yake, au sio?’
akauliza Maua.
‘Hayo maswali ya polisi,…..au na wewe ni shushu wao nini,
maana unavyouliza, nakuona kama polisi,…’akasema Tajiri.
‘Kwani hata nikiwa polisi wewe una wasiwasi gani, kama
huhusiki, ….au unahusika ndio maana una kuwa na wasiwasi?’ akauliza Maua.
‘Sikiliza, hata kama wewe ni shushu, mimi sihusiki,
unasikia….na kumbuka safari yetu ya kuja huku, ….na kama unaingiza mambo
mengine, ni bora mrudi huko Dar, nitakuja huko tutayamaliza huko huko…’akasema
Tajiri.
‘Mimi siondoki hapa hadi hapo, nitakapojua ni nini majaliwa
yangu, umeshaniharibia maisha yangu, ….na sijui mama yangu atakuwa katika hali
gani kwa sasa….nahitaji kujua majaliwa yangu haraka iwezekanavyo’akasema Maua,
na alipotaja neno mama ndipo Tajiri akakumbuka…
‘Umenikumbusha kitu, …wakati naingia humu, alitoka mama
mmoja, …..akiwa na haraka, ni nani huyo?’ akauliza huku moyoni akiwa anamwangalia Maua, ambaye kwa muda huo, alikuwa bado kafungwa nguo alilotoka nalo bafuni, ....akawa anaumia kimoyo moyo, .....
‘Mama mmoja, una maana mama yangu?’ akauliza Maua.
‘Hapana sio mama yako, …kuna mwanamke, alitoka humu,….mimi
siongelei mama yako, mama yako namfahamu sana,…..huyo mpenda pesa,…achana naye,
maana kila mara ukikutana naye, anadai pesa, pesa zitamuua…na mara anadai upo
na mzee, kama ningelimkuta humu ndani….ungelianiambia vyema….ole wake’akasema
huku akiangalia huku na kule..
‘Mimi simjui huyo mwanamke mwingine unayemzungumiza…na hata
kama ungelimkuta huyo mzee unayemzungumzia, sijui mzee gani, ungenifanya nini,
kwani tuna makubaliano gani mimi na wewe….makubaliano yetu ni hayahusiani na
lolote ….zaidi ya kuwajibika basi….’akasema Maua huku akijiandaa kuondoka.
‘Sasa unataka kwenda wapi?’ akauliza Tajiri.
‘Kwani hapa ni kwangu hadi nikae humu, nakwenda huko
tulipopanga,….na kesho tunahitajia kujua maswala yetu haya …na nataka tuyaongee
mbele ya mzee wako, maana naona hapa mnataka kunichnaganya kic’ahwa changu,
nyote akili zenu ni sawa…’akasema huku akiangalia kule alipolala huyo mzee.
‘Hayo mengine tuliyotoka nayo Dar, kwa sasa
yasitisheni,…..mpaka haya matatizo yaliyotokea hapa yaishe, ….itakuwa jambo la
ajabu, kama nitakimbilia maswala hayo …..wakati kuna msiba’akasema.
‘Msiba wa nani tena, hivi wewe unaongea nini, mboan
sikuelewi?’ akauliza Maua kwa mshangao.
Tajiri akageuka kuangalia pale alipolala mzee wake, na
akahisi kitu tofauti, kwani alipofika anakumbuka kuwa yule mzee, alikuwa kalala
kaangalia juu, lakini sasa hivi anaona ajabu yule mzee kalala upande upande….
‘Haiwezakani….ni nani kamgeuza mzee?’ akauliza.
‘Wewe mbona hueleweki?’ akauliza Maua akiwa kwenye mshangao.
Tajiri, hakutaka kuongea zaidi, akaenda hadi pale alipolala
mzee wake, akamchungulia na baadaye akainamisha kichwa na
kumsikilizia,…..akainuka haraka, kama vile mtu anaruka, kama vile mtu
aliyeshitulia na kitu cha kuogofya….
‘Ina maana mzee….’akasema kwa mshangao, na akasikia sauti
ikisema.
‘Hebu toka nje, nahitajika kupumzika….na ole wako utoe
dhamana kwa huyo hawara wako…na nakuonya kama wewe una husika kwa lolote lile
na huyo mwanamke wako, ….nitahakikisha huna haki yoyote kwangu….utamfuata huyo
mwanamke wako jela…..’ilikuwa sauti ya mzee, iliyomfanya Tajiri ashikwe na
bumbuwazi, akabakia ameduwaa, aliogopa hata kuangalia wapi sauti ilipotokea,
akasimama kwa muda bila kusema kitu, …..
NB Mvua imeleta mengi…shida za usafiri, mtandao shida….ooh,
lakini hicho kidogo kwa leo kinatosha.
WAZO LA LEO:
Tusipende kuombeana mabaya, tusipende kujenga husuda na chuki, hasa pale
tunapoona mtu fulani kafanikiwa, …cha muhimu ni kujitahidi, kufanya kazi kwa
bidii, huku tukimuomba mungu, kuwa na wewe uwe kama yeye, upate kama yeye,
kihali….tukumbuke kuwa aliyempa yeye, ndio huyo huyo anayeweza kukupa hata
wewe.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment