‘Wote mpo chini ya ulinzi…’sauti kali ikasema na mara
wakaingia askari watatu,..na baadaye akaingia docta, ambaye hakusubiri,
alifululiza moja kwa moja hado pale alipolala yule mzee.
Sauti hii iliwashitua wote waliokuwepo humo ndani, na
ilikuwa kama imewaziba mdomo kwa muda, na kuwashikilia viungo vyao na kuwa kama
vile wamegandishwa. Ilionekana kila mmoja kichwani mwake, alikuwa akiwazia kosa
lake,….na hata kutafuta njia ya kujitetea.
‘Kwa kosa gani….?’ Akauliza Malikia huku akijifanya anajiamini
lakini moyoni alishashikwa na mshituka, hakutarajia kabisa kuwa hawo watu
wangelifika hapo, na hata kama wangelifika, alijua ni baadaye sana.
Mara mlangoni akaingia askari mwingine ambaye alionekana ana
cheo kikubwa kuliko wale askari wengine waliokuwepo mle ndani, akaingia kwa
mwendo wa mikogo, hadi akafika mbele ya wale askari wengine, hakuwa na haraka
ya kuongea, akasimama na kumwangalia Malikia moja kwa moja usoni.
‘Malikia,…..mmh, Malikia wa Mererani…natumai
unanikumbuka..’akasema yule askari, na Malikia, akiwa anajifanya hajali
akamwangalia mara moja, na kutembea hatua mbili pembeni, kama vile anakwepa
kuangaliana moja kwa moja na yule askari, akasema;
‘Haina haja ya kukumbuka, kwani una tofauti gani na hawo
askarii wengine, mimi ninachotaka kujua ni kwanini mnaingia kwenye majumba ya
watu,…bila nidhamu na kuanza kuwatishia maisha yao,…..hivi ndivyo polisi
wanavyotakiwa kufanya?’ akageuka na kumwangalia yule askari, ambaye alikuwa bado
anamwangalia.
‘Nidhamu gani unahitajia Malikia,….hatukupiga hodi,…..na kwa
hali ilivyo humu ndani, baada ya kupiga odi mara tatu bila jibu, tuliona ni
wajibu wetu kufungua mlango na kuona ni nini kimetokea, na ukumbuke tulikuwa na
dakitari, ambaye alishapigiwa simu kuwa mzee anaumwa, je ulihitaji tukae hapo
nje hadi muda gani…..?’ akauliza yule askari.
‘Sawa, kaam ni swala la dakitari, ….angelitakiwa aingie yeye
peke yake, lakini mlichofanya nyie, ni kutangulia na silaha zenu na mapingu
mkononi, kama vile hapa kuna mhalafu,…..’akasema.
‘Halafu?’ akauliza huyo askari
‘Halafu nini…..uoni mlovyofanya,…docta alikuwa wa tatu
kuingia, …na hawo askari wao bila kuuliza nini kimetokea , wanatuweka cini ya
ulinzi, kwa kosa gani…hauoni tupo kwenye majonzi, badala ya kuleta ubinadamu,
mnaleta ubabe wenu , haya tuambieni …kosa letu ni nini hadi tunawekwa cini ya
ulinzi katika ali kama hii…?’ akauliza Malikia.
Inspecta wa polisi akageuza kichwa kuangalia kule
kilipokuwepo sofa ambapo yule mzee alikuwa kalala, na kwa haraka akageuka
kuwaangalia askari wake, halafu akamgeukia Malikia akasema;
‘Kwa hali ilivyo hapa , hatuwezi kuongea, maana dakitari
yupo kazini, anahitaji muda, anahitajia utulivu,….nyie wote humu ndani kama
mlivyoamuriwa mpo cini ya ulinzi, ….’akasema huyo askari.
‘Kwa kosa gani?’ aliyeuliza sasa hivi alikuwa ni Tajiri.
‘Kwa makosa mengi, kwanza, kujihusisha na biashara ya madawa
ya kulevya,….kuua, …udanganyifu, blackmail, ubakaji…na mengine mtayajulia huko
mahakamani, lakini kwa hivi sasa mpo chini ya ulinzi mnahitajika kituoni,
…..’akasema na kuwaangalia maaskari wake.
Wakili, aliyekuwa kimiya, akamgeukiwa Tajiri, na pale pale
akafungua mkoba wake na kuanza kuweka baadhi ya nyaraka zake, ambazo alikuwa
kazitoa awali wakati akiongea na Malikia, na yule Inspekta akawa anamwangalia.
‘Kila kitu kilichopo humu ni ushahidi ….rudini nyuma hatua
tatu,…..’akaamrisha, na wakili aliposikia hivyo, akalifunga ule mkoba wake, na
kuushikilia vyema mkononi, hakujali hiyo amri.
‘Muheshimiwa wakili, natuma umenisikia….weka huo mkoba wko
hapo mezani, na rudi nyuma hatua mbili’akasema huyo askari.
Yule wakili akarudi nyuma hatua mbili akiwa kashikilia mkoba
wake. Inspekta akamwangalia mmoja wa askari wake, ambaye alipoona hiyo ishara ,
alikuwa mbele ya yule wakili, na kumuonyesha huyo wakili aweke mkoba wake mbele
yake.
‘Huu ni mkoba wangu una nyaraka za kazi, zangu, kuna nyaraka
za wateja wangu,….siwezi kumpa yoyote, kwa vile ni ukiukwaji wa haki za wateja
wangu…’akasema.
‘Tunakibali kinachoturuhusu kufanya hivyo….’akasema huyo
inspekta na kuonyesha kibali ambacho kilimtaka kuchukua hizo nyaraka, ….kama
ushahidi.
‘Siwezi hata kama mna kibali hicho, kwanza kwa kosa gani,
pili, …..mimi ni wakili, na sheria zinanitambua kwa hilo,..tatu mnanivunjia
heshima yangu kama wakili, kwani mimi ningeliweza kufika huko kituoni bila
kutumia njia kama hii, kama mnaniona nina hatia, au wateja wangu wana
hatia’akasema.
‘Sasa hivi wewe na wenzako wote hapa, ni washukiwa wa
uhalifu, na kwa hiyo unahitajika kituoni, wewe na wenzako, ….kama wewe ni wakili,
sawa, utafanya kai hiyo yako kwa ajili ya wenzako na wewe utafute wakili wa
kukutetea kwa makosa yako, kama itaklubalika kufanya hivyo,….’akasema huyo
askari.
‘Sijakuelewa vyema, ….ina maana na mimi mihalifu?’ akauliza.
‘Wewe ni wakili, na umesikia vyema kauli yangu, kuwa wote
humu ndani mpo chini ya ulinzi, mengine yote mtayajulia huko kituo cha polisi,
kwa makosa niliyowatajia awali…tuna ushahidi na hayo, sio kwamba tumekurupuka
tu….muheshimiwa wakili’akasema yule askari.
‘Hata sisi, mbona sisi ni wageni tu’akalalamika mama mdogo.
‘Hayo yote utajielezea huko mbele, haya vijana wangu fanyeni
kazi yenu….’akatoa amri, na kila mmoja wa wale askari aliyeingia hapo akawa
anafanya kazi, yake,…kuchukua picha, kuandikisha kile kitu walichokihitajia, na
kila mmoja alitakiwa kuandikisha kile kilichokuwa chake na kuweka sahihi yake,
….
‘Haya twendeni kituoni….’akasema huyo askari,
‘Kwa vile kuwepo kwetu humu ndani kunaweza kusababisha docta
ashindwe kufanya kazi yake. Wakili akawa wa kwanza kuongoza njia, na akafuatia
Malikia, na baadaye Tajiri, na wa mwisho kutoka alikuwa malikia, ambaye kabla
hajatoka alipofika mlangoni aligeuza kichwa na kuangalia kule alipokuwepo Docta
akiwa na yule mzee.
Docta alikuwa kainama, akipima mapigo ya moyo ya yule mzee
kwa chombo chake, na yule mzee, alikuwa kageuza shingo akiangalia mlangoni.
‘Oh, kweli, hajafa…’akasema na mlango ukawa umeshajifunga.
********
Docta alibakiwa akiwa kashikwa na butwaa, kwani kwa taarifa
alizopata, yeye alijua kuwa anakuja kuhakikisha kuwa huyo mzee keshakata roho,
lakini cha ajabu….
‘Wameshaondoka…’alishituka na kuachia kile kipimo alichokuwa
akikiweka vyema masikioni ili kujua mapigo ya huyo mzee, akainuka na akajikuta
wakiangaliana na huyo mzee.
‘Oh, maajabu, ina maana….?’ Akauliza.
‘Nimefufuka, …na docta, nimegundua dawa,…hii ni dawa halisi,
haina migogoro wala shaka, haihitajii kunywa au kumeza, ni dawa ya asili,
aliyotupa mungu . Unajua mapaka sasa siamini, unaniona docta nipo mzima kabisa…’akasema
na kuinuka kitandani, japokuwa alikuwa anayumba, lakini aliweza kusimama, na
kuruka ruka.
‘Unaona docta, nipo fiti….chuma cha Mjerumani, unafanya
mchezo nini, …ni dawa isiyo na longo longo’akasema huku akitembea huku na kule.
‘Sasa sikiliza, mimi ni docta, na inabidi ufuate masharti
yangu, kama unajiskia vyema sawa, lakini nahitajika nikuangalie, na
kukuchunguza, ili niwe na uhakika na hilo, rudi hapa kwenye kiti chako cha ezni
nimalize kazi yangu.
‘Ina maana huamini docta, ….haya endelea na vipimo vyako,
utathibitisha mwenyewe kuwa mimi ni mzima, …’akarudi pale kwenye sofa lake na
kulala, na docta akaendelea na vipimo vyake, na alipomaliza akarudisha vifaa
vyake kwenye mkoba wake na kukaa kwenye kiti kilichokuwa pembeni na hilo sofa.
‘Hebu niambie ilikuwaje, ina maana ulikuwa unaigiza kuwa ….upo
taabani ….au uliigiza kuwa umekufa, maana watu wote walifahamu kuwa umeshakata
roho…?’ akauliza huyo docta kwa mzaha. Mara nyingi hawa wazee wanajuana, na
wakikutana katika hali ya kawaida wanaishia kutaniana.
‘Ndio maana nataka uweke hilo kwenye kumbukumbu zako za
udakitari, ….kwanza nikuulize, hivi kweli kuna kitu, ukiwa na shinikizo la
damu,….eeeh, hivi kuna kitu kinaweza kikatokea kikafanya hali yako ikarejea
bila ya kutumia dawa yoyote?’ akauliza.
Yule docta kwanza akamuangalia yule mzee kwa makini, na
akilini mwake, alijua kuwa huenda huyo mzee, anafikiria mambo ya kimizimu au imani,
akawa hana uhakika na hicho mzee anachokisema…..
‘Inawezekana, ukumbuke shinikizo la damu, huja kutokana na
mambo kadhaa, vyakula tunavyokula, mfumo wa maisha,…na ikitokea sababu mfano
mshituko, ..mawazo nk…ndio hapo, unapatwa na hayo matatizo,….sasa kama kuna
kitu ambacho kimetokea, kuweza ..kwa mfano kuzua mawazo, nk…inawezekana
ukajisikia vyema’akasema huyo docta akiwa bado na mashaka kuwa huenda hajajibu
swali la huyo mgonjwa wake.
‘Kwahiyo unanishaurije,…maana wewe mwenyewe umethibitisha
hilo,….kama kuna kitu kama hicho kinaweza kusaidia, hata kuponyesha,….si vyema
kuwa nacho,ikibidi moja kwa moja, …..?’ akawa kama anauliza, na kabla docta
hajamjibu akaendelea kusema;
‘Docta… kiukweli, nilikuwa nipo karibu na kukata roho…sio
kwamba nilikuwa naigiza, au kusingizia…, shinikizo lilikuwa baya kabisa…na
nilikuwa nikihesabu sekunde, …nilishakata tamaa kabisa, nilijua ndio kwaheri….’akatulia
huku akijiweka sawa pale alipokuwa kakaa. Na ili kumuonyesha docta kuwa
keshapona, akainuka na kuanza kutembea tembea huku na huku.
‘Kwani ilikuwaje?’ akauliza docta akiwa anamwangalia mgonjwa
wake, .
‘Ni huyo muhuni, …nimeshawaambia kuwa simtaki aingie hapa
kwangu, maana kila akija, anakuwa kama katumwa kuja kuitikisa roho yangu, ili
iligee na itoke,…akija hapahana subira, mwanzoni alikuwa binti mzuri, kumbe ni
chui aliyevaa ngozi ya kondoo…’akaulia
‘Ni nani huyo unyemzungumzia?’ akauliza docta.
‘Huyo wanayemuita Malikia’akasema huyo mzee, na docta aliona
sio vyema kumkumbusha hayo yaliyopita, akataka kubadili mazungumzo lakini yule
mzee akaendelea kuongea;
‘Huyo binti nia yake nife arithi mali yangu, ..’ akasema
huyo mzee.
‘Kwa vipi arithi mali yako, kwani yeye anastahili vipi kuwa
marithi wako?’ akauliza docta.
‘Docta sikuamini niliyoyaona leo, sikujua kuwa nimezungukwa
na wauaji, ….unajua docta kwa hivi sasa wewe ndiye naweza kukuamini kuwa ni
rafiki mwema kwangu, ….mpaka sasa hainiingii akilini kuwa rafiki yangu wa toka
utotoni kumbe ndiye adui wangu mkubwa’akatulia na kushika kidevu.
‘Mzee, naona tusiongee hayo, unajau unahitajika kupumzika,…..’akasema
docta, na kwa kusema vile akiwa na wasiwasi na afya ta huyo mzee, akawa kama
vile kamwambia huyo mzee aonyeshe kuwa ni mzima au vipi, kwani yule mzee,
alisimama na kuanza kuruka ruka.
‘Docta Nipo fiti…..unaniona, usiwe na wasiwasi kabisa, mimi
sio docta kama wewe, lakini kwa mwili wangu, najijua vyema kabisa, hali niliyo
nayo, sio ya kubahatisha tena, na ili niweze kuendelea hivi hivi nahitajika
kuongea, na kutoa hili ninalotaka kukuelezea;….’
‘Ok, endelea, maana hata mimi nina hamu ya kusikia,…’akasema
docta, aliogopa kuangalia saa yake, akijua huyo ni mmoja wa wateja wake
wakubwa, hatakiwi kuwakirihisha japokuwa alikuwa alihitajika huko hospitalini.
‘Kumbe umzaniye kuwa ndiye rafiki, anaweza kuwa adui wako
mkubwa…nimekosana na mke wangu,..nimkosana na familia yangu, kumbe adui yangu
yupo karibu yangu, anajifanya rafiki mwema, ananishauri, tena kisheria, kumbe
sheria zake ni za kimitego…’akatulia.
‘Ina maana unamzungumzia wakili wako?’ akauliza.
‘Huyo ni nyoka mkubwa…yeye akishirikiana na yule rafiki
yangu mwingine…hutaamini, ni watu niliosoma nao, tunatoka kijiji kimoja, wazazi
wetu walikuwa kama mtu na kaka yake, leo hii…aah, kweli dunia imekwisha’akatulia.
‘Nilipoambiwa mara ya kwanza, sikukubaliana, na nilifanya
uchunguzi wa kina,lakini sikuona huo ubaya wao nikaona kuwa huenda ni mbinu za
watu za kutaka kunigombanisha na marafiki zangu, ..na sikuamini hadi leo
niliposikia kwa masikio yangu mwenyewe…’akatulia.
‘Nitahakikisha wanalipa….na wataozea jela, yeye anajifanya
ni wakili, lakini mimi najua sheria zaidi yake,…sheria nyingine nimezijua kutokana
na yeye mwenyewe na pia uzoefu wa kimaisha umenisaidia sana,…nimejifunza mengi,
na mengi hayo ni pamoja na sheria,kwahiyo hanibabaishi, …..hizo alizokula
zinamtosha, lakini atanirejesha kwa kuozea jela…’akatulia.
‘Yeye kumbe ndiye kiongozi wa kundi lao, yeye akishirikiana
na huyo rafiki yangu mwingine na huyo kimwana wao, wanayemuita malikia….wamakuwa
wakihadaa watu, wakichukua mapicha mabaya, na kuwatishia watu kuwa wasipolipa pesa
wanazohitajia wanawalipua,….pia wamekuwa wakiuza madawa ya kulevya..na hata
mimi walitaka kunishirikisha,…lakini uzee ulinisaidia’akatulia.
‘Ulifanyaje…’akasema docta na muda huo akaangalia saa yake,
na huyo mzee akatambua kuwa docta anahitajiak sehemu nyingine.
‘Yote hayo utayapata mahakamani, …maana mimi niliamua
kushirikiana na vyombo vya dola kuhakikisha kuwa kundi hilo linafikishwa kwenye
vyomboo vya sheria, walifikia hatua ya kumrubuni mjomba wangu, ili aje aniibie,
ili aniingize kwenye biashara hiyo, ..haramu….lakini nilimweka mjomba wangu kiti
moto , nikamuasa hadi tukawa kitu kimoja….akakubali kuwa chambo’akatulia.
‘Kwahiyo yeye hahusiki?’ akaulizwa.
‘Yeye anahusika kama chambo tu….siunawafahamu polisi walivyo,
wao wana mbinu nyingi, ……wanasema ili umkamte mwizi , unaweza ukatumia mwizi
mwenzao….na kweli wamefanikiwa…utasikia mwenyewe siku kesi hiyo ikifikishwa mahakamani,
….’akasema na kurudi kwenye sofa lake akakaa.
‘Sasa mimi nakwenda,…’docta akamosogelea mzee, akainua mkono
wake, na kusikiliza mapigo ya moyo, halafu akatoa kadi yake ya kumbukumbu
akaandika, na baadaye, akachukua mkoba wake, akageuka huku na kule..
‘Kile kichupa cha dawa kipo wapi?’ akauliza.
‘Atakuwa kakificha huyo mwanaharamu..’akasema huku
akiangalia huku na kule.
‘Oooh, mzee, zile dawa ni muhimu sana, usikae mbali nazo,
nilishakuambia ukianza kusikia hali mbaya, meza kidonge kimoja tu….hali yote
inakuwa shwari…sasa ooh, hebu niangalie kama nimekuja na akiba’akafungua mkoba
wake, na kutoa kichupa kingine kikiwa na vidonge ndani yake.
‘Nilikuwa najua bado unzo, kwahiyo sikuhitajika kuja na dawa
nyingine..lakini bahati nzuri kuna kichupa kilikuwepo, sasa hiki weka uchagoni
mwako, pale unapokuwa umejipumzisha hakikisha kinakuwa karibu, ungelikuwa na
mke, ingelikuwa haina shida….’akasema docta.
‘Sasa docta, nilikuuliza swali, je hii dawa iliyonitibu
unaionaje, maana haihitaji hivi vidonge?’ akauliza huyo mzee.
‘Hiyo dawa, ninakushauri, uitumie, …uwe nayo karibu, lakini,
imethibitishwa kitaalamu, maana dawa za kienyeji nyingine ni nzuri, lakini
huenda zikawa na mdhara makubwa ambayo utakuja kugundua baadaye wakati
umeshachelewa, ….nitahitaji kuiona hiyo dawa.
‘Sasa sikiliza,…’akasema na kuinua simu yake, akapiga na
kuongea na mtu.
‘Namuomba huyo binti,…eeeh, Maua, aje hapa haraka’akawa
anaongea na simu.
‘Lakini sasa mzee, mimi ninaondoka….nitakuja baadaye, kuiona
hiyo dawa’akasema huyo dakitari.
‘Sawa wewe ondoka tu, …utakuja kuiona dawa yangu, maana
nitafanya kila njia niwe nayo karibu, …docta hii nina uhakika ndiyo dawa ya
matatizo yangu, ni ponyo la ugonjwa wangu, mwenyewe umethibitisha, kwani
nilikuwa nachungulia kaburi, lakini sasa unanionaje, ….?’ Akawa kama anauliza
na docta akawa keshaanza kuondoka na alipofika mlangoni, akageuka na kusema;
‘Kweli hiyo ni dawa …imekusaidia sana, ila hiyo ya kwangu
hakikisha unakuwa nayo karibu….ni muhimu sana’akasema docta.
‘Docta, …kama nikiipata hiyo dawa…kitulizo cha moyo wangu,
sitahitaji tena hiyo dawa yako….labda….’akasema na docta akatabasamu, hakuelewa
huyo mzee ana maana gani akafungua mlango na kuondoka, na nje akakutana na
akina mama wawili wakiwa wamesimama wakitaka kuingia ndani.
‘Oooh, jamani naombeni msimsumbue huyo mzee tena…..anahitajika
kumpumzika’
‘Lakini kapiga simu akasema anahitaji kumuona binti yangu…’akasema
mama mdogo.
‘Sawa, ila msimsumbue….ooh, nimekumbuka na wewe binti
niliyekutana naye siku ile, basi kadi yangu bado unayo…likitokea lolote
nipigie, ndio wewe uliyenipigia simu eeh, unaitwa nani?’ akauliza.
‘Ndio mimi docta, mimi naitwa Maua, je huyo mzee anaendeleaje?’
akauliza huyo binti huku mama yake mdogo akiwa haamini hayo anayoyasikia,
akashindwa kuvumilia, akasema;
‘Ina maana huyo mzee kafufuka, nilikuambia, huyo mzee ni
mwanga, utajiri wake….’akasema na kukatisha huku akiziba mdomo wake kwa
kiganja cha mkono.
‘Hajambo kabisa…hutaamini, anadai kapata dawa ambayo ndiyo
suluhisho la ugonjwa wake….mzee huyo ana matatizo…mtata kama nini…tatizo lake,
anaamini sana dawa za asili’akasema huku akipanda gari lake na kuanza kuondoka,
alipotoka nje ya geti, akakuta na boda boda ilyosimama ghafla mbele yake, na hapo
hapo akatoka mama mmoja ndani ya boda boda hiyo, kwanza akawa anaingalia hiyo
nyumba kama anahakikisha kuwa ndio yenyewe.
Ile boda boda ikaondoka, na kabla huyo docta hajaondoa gari
lake, yule mama, akalisogelea gari lake na kusimama pembeni, na akawa anagonga
kwenye kiyoo, na yule docta akashusha kiyoo, na kusema;
‘Nikusaidie nini mama ….?’ Akauliza huku akionyesha kuwa ana
haraka, na hakutaka kupoteza muda mwingine kwani huko hospitalini anahitajika.
‘Samahani ndugu, ….wewe ndiye mwenye hii nyumba? ‘ akauliza
huyo mama.
‘Hapana mimi sio mwenye hii nyuma, ila nilifika mara moja, ….ulikuwa
unamuhitajia nani?’ akauliza docta, alisahau kulivua koti lake la udakitari,
kwa ajili ya haraka.
`Wewe ni Docta, ooh,… samhani, lakini nilikuwa, naomba
kuuliza…. nimelekezwa hapa kuwa ninaweza kumpata binti…ni binti yangu,....’akasema
huyo mama
‘Binti yako ….?’ Akauliza huyo docta, akionyesha kushangaa,
halafu akasema;
‘Anaitwa nani huyo binti yako, maana nyumba hii nijuavyo mimi,
kwa sasa hakuna mabinti,…’akatulia kidogo halafu akasema;
‘Ndio wapo wafanyakazi wa kike, lakini ni akina mama sio
mabinti, au labda una maana gani ukisema binti, …?’akauliza docta na muda huo
alikuwa anataka kuondoka maana alishachelewa.
‘Yeye hakai humu, nafikiri amekuja hapa…sina uhakika kwa
vipi, ila nimeelekezwa kuwa ninaweza kumpata humu kwenye nyumba hii,….yupo pamoja
na mama mmoja, ni mama yake mdogo….’akasema huyo mama.
‘Huyo binti anaitwa nani?’ akauliza huyo docta, akiwa
keshaanza kuliondoa gari lake
‘Anaitwa Maua, mimi ni mama yake mzazi…..’akasema huyo mama.
NB: Ukiona hivyo, ndio lala salama, msitie shaka, kisa
kinaishia.
WAZO LA LEO:
Tujitahidi kujenga urafiki, lakini pia tuwe makini na marafiki, kwani sio
marafiki wote ni wema.
Ni mimi:
emu-three
4 comments :
Nimejifunza kitu kutokana na simulizi hii. Hongera sana miram
Nashukuru sana Shalom kama kuna kitu umejifunza, ...leo nimeandika kila kitu, lakini kuweka hewani imegoma,...naendelea kujaribu, ikiwezekana, tupo pamoja, ikishindikana basi kesho tukijaliwa.
Jamani naona hii itakuwa kesho.
It is the best tіme to mаke sоme plans
fοr the future and іt is time to bе hаpрy.
Ӏ've read this post and if I could I want to suggest you some interesting things or suggestions. Perhaps you could write next articles referring to this article. I want to read even more things about it!
Also visit my page ... casino online reviews
Post a Comment