Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, February 25, 2013

Uchungu wa mwana Aujuaye ni Mzazi-64




Mjomba hali ilizidi kuwa mbaya na dakitari alikuwa hajafika, na kama kweli alipigiwa simu, asingeliwezakana kuchelewa kiasi hicho,…kwa jinsi huyo dakitari anavyowajibika kwa huyo mzee, huwa akipata taarifa, anaweza akaacha gari lake na kuchukua pikipiki, ilimradi awahi kufika, lakini leo haikuwa hivyo; kuna sababu, hebu tuendelee na kisa chetu,

********
‘Au mjomba wangu hakuwahi kumpigia simu…..?’ Mzee akawa anajiuliza , akiwa hajakata tamaa ya kuishi, japokuwa akili ilikuwa inaanza kuingia giza, na alijiona kama vile anajihesabia sekunde za kuishi, kwa jinsi alivyokuwa akijsikia.

Mwili ulianza kuelega na akahisi vitu vikajivuta mwilini, kuanzia kidole gumba, kuna hali ilianza kujitokeza, na ilikuwa kama mishipa ya fahamu inaanza kuacha kufanyakazi, na alihisi kama roho ikiwa inapita kwenye mishipa hiyo na kujitutumua kwa mara ya mwisho. Na hapo akakumbuka maneno ya watu wa dini kuwa roho huanza kutoka kuanzia vidoleni na kupitia kwenye mishipa ya damu na mwishi wake hutokea mdomoni….

‘Ina maana ndio nina kufa, ina maana huyu mwanamke keshanishinda,…haiwezekani, …haiwezekani….nahitaji muda wa kupambana naye..’akawa anajisemea akilini huku akimwangalia huyo mwanamke kwa fahamu za hisia. Na wakati huo huyo mwanamke alionekana kujifanya kuhangaika kuitafuta hiyo dawa, huku na kule, huenda alikuwa hatafuti dawa, alikuwa akitafuta nyaraka anazoziona kwake ni muhimu.

‘Haniwezi, nitapona tu…..’akijipa moyo, na wakati huo huo, aliona kitu cha ajabu ambacho hakikuweza kumuingia akilini mwake….na kilitokea pale mlango ulipofunguliwa, na kuingia wakili wake......

Wakili alatokeza mlangoni, ….kwa akili yam zee, alijua kwa vile ni mtu wake, angalau angelisaidia kuharakisha kuangalia jinsi gani ya kusaidia, lakini yule wakili alipoingia..kwanza alisimama pale mlangoni kwa muda, na wakati huo huo anamwangalia Malikia, na alionekana kutokujali kuangalia kule alipolala mzee, na hakujali kumwangalia Tajiri, alichokuwa akijali ni kumwangalia Malikia….

Mzee macho yake, yalikuwa bado yanaona japokuwa kwa giza giza, alichoona ni mkono wa malikia ukiinuliwa juu, kuashiria ushindi, na alionekana kama kushangilia jambo,….mzee alijua huenda anashangilia kwa vile keshajua kuwa yeye sasa anakata roho, ….lakini alimuona akiwa kashikilia karatasi fulani, ….na akawa anaisoma, na yule wakili, alionekena kama anatingisha kichwa kukubaliana au kushangilia, …na yeye akawa kainua mkoba wake juu, kushiria kuwa kila kitu kipo mle ndani ya mkoba.

Mzee huyu japo kuwa hakuwa na uwezo hata wa kujitikisa, lakini golilo za macho ziliweza kuzunguka, akazungusha zile golili za macha na kumwangalia mjomba wake,….Tajiri, …..

Mjomba wake alikuwa bado kashikilia simu, akionyesha kuwa anaongea, huenda ndio alikuwa akiongea na dakitari…na baadaye akawa kairudisha simu mahali pake, na akawa kasimama kaduwaa, alikuwa akiduwaa kumwangalia wakili, …..alikuwa kaduwaa akishangaa, kama anavyoshangaa mzee wake. Mzee hakuamini, japokuwa alikuwa katika safari ya umauiti, lakini bado alikuwa akijiuliza, inawezekanaje mtu aliyemuamini miaka mingi , ….aje amsaliti ..haiwezekani…wakili wake amfanyie hivyo,…ni wakili yule yule anayemjua au ni mwingine, akageuza golili za macho na kumwangalia wakili, na kumbukumbu za maisha yao nay eye zikamjia

************

Wakili huyu ni rafiki yake toka utotoni, na jirani yake huko kijijini, walisoma shule moja ya msingi, …lakini waliachana pale wakili huyo alipofaulu kwenda sekondari na wakawa wanakutana kipindi cha likizo. Yeye hakupendelea kusoma, akajiingiza kwenye biashara…

Baada ya wakili huyu kumaliza masomo yake huko chuo kikuu, na kufanya kazi serikalini kwa muda, alimua kuacha hizo kazi serikalini, na kuwa wakili wa kujitegemea. Hilo lilikuwa lengo lake toka zamani, kuwa awe wakili ambaye hatazuiwa kufanya yale aliyokuwa nayo moyoni mwake.

Kabla ya kustaafu kufanya kazi serikalini kwanza alishafanya utafiti wake, akagundua kuwa matajiri wengi, anaowafahamu hawana uelewi wa sheria, na kazi zao nyingi, wanaziendesha bila maandishi ya kisheria. Kwahiyo kwanza alichofanya ni kukutana na wale matajiri anaowafahamu na kuwapa shule, na umuhimu wa kuwa na mwanasheria. Ilikuwa kazi nzito, lakini baadaye alifanikiwa.

Kwanza kabisa alianzia kwa marafiki wake wa karibu, ambao kwa kuwatumia, waliweza kuwashawishi matajiri wengine na wafanyabiashara wakubwa, na hata wale wenye uwezo, wakajikuta wakiwa washiriki wa huyo wakili, na hapo akajikuta ana wateja wengi.

‘Mimi nimeamua kuacha kazi za kuajiriwa, na nimemua kujiajiri, na lengo langu kubwa ni kuwasaidia marafiki zangu niliowahi kuishi nao, kwa vile mimi najua sheria, na nyie mna pesa, basi mimi nitawasaidia nyie kisheria, ili mali zenu ziwe katika mikono ya kisheria…’alikumbuka siku walipokutana kwa ajili kuingia mkataba wa kuwa wakili wake

‘Mimi mara nyingi siamini mambo yenu hayo ya kisheria…naishi kivyangu, na kama ikifikia kushitakiana, nitajua huko mbele kwa mbele…;akasema mjomba.

‘Sikiliza nikuambia, sheria ni muhimu sana katika maisha yako, kuna leo na kesho, ..kuna mambo mengi yanapotea au haki nyingi kupotea kwasababu ya kukosa mdhamana, na mdhamana mzuri ni sheria, na sheria husimamiwa na watu walioisomea, wanaojulikana kisheria, kama sisi mawakili…..’alianza kupata shule ya kisheria hadi akakubaliana nayo.

Jamaa huyu akawashikilia matajiri wote na kuwa wakili wao, na kila mwezi akawa akapokea pesa nyingi toka kwa matajiri hawa. Ni kweli alikuwa akiijua sheria vyema…na alikuwa akijua vipi aipindishe ili apate kila anachokitaka….na kila matajiri hawa walipopatwa na misuko suko , akawa anawatetea hadi kufanikiwa na kujikwamua kwenye misukosuko hiyo…na kweli kwa wengine, kama singelikuwa huyu wakili wao , wangelijikuta wakifungwa au kupoteza mali zao zote, lakini wakili huyu aliweza kucheza na sheria na kuwaokoa, …na hapo akajijengea jina.

Wanasema tabia haina dawa, pamoja na ujasiri wa huyu wakili, na pamoja kazi kubwa ya kuwasaidia hawa matajiri, lakini kumbe alikuwa na mipango yake iliyojificha, na tabia hiyo ndiyo iliyokuwa imemfanya jamaa huyu aamue kustaafu huko alipokuwa akifanyia kazi kwa maslahi ya uma, na kudanganya kuwa alistaafu tu kwa vile keshachoka na kazi za kuajiriwa….

Hakuna aliyehangaika kutafuta undani wa huyu jamaa, kwa vile kazi aliyokuwa akifanya ilikuwa ikionekana, na hata umshuhuri wake wa kusimama mahakamani kutetea watu ulikuwa wa hali ya juu, hata kila mmoja akawa na umanifu naye, hata ikafikia kuitwa shujaa wa kizimbani.

Leo Mzee, mjomba aliyaona hayo kwa macho yake, akashuhudia jinsi gani huyo wakili wake alivyokuwa na sura mbili…kumbe sura moja ilikuwa ya kumtimizia matakwa yake, ili aonekane ni mtu mwema, mtu wa sheria, anayelinda maslahi yake, na sura ya pili ilikuwa ya mtu mwingine kabisa…

‘Huyu wakili wako ninamshuku vibaya, huyu ndiye anayemuhadaa mke wako…..na pie ndiye aliyeifanya ile nyumba ndogo iote mbawa, ….kwani yule tajiri aliyevhukua nyumba ndogo yako inasemakana ni ndug wa huyo wakili….;akayakumbuka hayo maneno, aliyoambiwa na rafiki yake.

‘Bwana hayo sio ya kweli, achana na maneno ya uvumishi….huyu wakili ni mtu mwema sana, kila mtu anajua wema wake hawezi katu, akafanya vitu kama hivyo..’akasema Mjomba.

‘Ni kweli hata mimi siamini, hayo nimeyasikia kwa redi mbao zetu….sijalifanyia kazi, ila nilitaka kukutonya tu, kama huamini, kama nilivyo mimi, tuliache kama lilivyo..’akasema rafiki yake huyo na kweli waliliacha kama lilivyo,

********

Mzee, akajaribu kujipa moyo kuwa huenda docta atafika na akaweza kuokoa maisha yake, kitu ambachp aliona ni miujiza, na nia na lengo lake ni kupona ili aje apambane na hawa watu wawili, na aliomba hata kama atakufa, basi mzimu wake urudi upigane na hawo watu wawili, akamtizama mjomba wake, ….alitaka kuhakikisha kuwa je na mjomba wake yupo kundi moja na hawo watu wawili….

Na pale akashikwa na mshangao pale alipomuona mjomba wake wakishikana mashati na yule wakili, na Malikia akawa kama anawatenganisha…na hili likampa faraja kuwa kumbe kweli huenda mjomba wake hayupo na hawo watu…, lakini kitu kilichomshangaza na kujiuliza ni kwanini hakuharakishi kumtafuta huyo dakitari wake.. na mara mlango ukafunguliwa.

Akamuona…

Hali ya mwili ikaanza kubadilika, joto likaanza kujitokeza, mapigo ya moyo yakaanza kufanya kazi, nguvu ikaanza kurejea kidogo kidogo…na mara akamuona akija na kusimama karibu naye, akaweka kidole kwenye shingo yake….ilikuwa kama mtu ameweka waya wa umeme ulioshitua uhai uliokwisha kufifia…

*******


Malikia alipowaona hawo akina mama wawili, akashika kichwa na kuangalia juu, kama vile kichwa kinamuuma, alikaa hivyo kwa muda, halafu akashusha mkono, na kuwanyoshea kidole wale wanawake wawili akisema kwa hasira;



‘Nyie mumefuta nini hapa?’ akauliza Malikia kwa hasira.

‘Nilikuwa nimewaita mimi, kwa maagizo ya …marehe… oh mzee,….hatuwezi kumuita marehemu mpaka docta wake aje athibitishe…mpigieni simu…’akasema Wakili.

‘Marehemu kwani Mzee kafariki, mbona, hakuna dakitari wake?’ akauliza Maua akiwa kashikwa na mshangao, na haraka macho yake yalatizama pale alipolala yule Mzee.

‘Dakitari wa nini, siku za mtu zikifika, hata kama kuna dakitari haisadii kitu, cha muhimu,…na ninashangaa mumefuata nini hapa, mnahuskinajae na huyu mzee…., hamtakiwi kwenye nyumba hii….’akasema Malikia.

‘Nani kasema hawatakiwi…’akasema Tajiri, akiwa bado hajitambui kwa tukio hilo,bado alikuwa na mshituko,..

‘Mimi ndio nasema hawatakiwi, na naona ni bora waondoke haraka iwezekanavyo, kabla hatujawaitia polisi..hili bado ni swala la wanafamilia, na wanaohusika tu…baadaye wanaweza kuambiwa majirani, hawa wanahusika vipi, ….hawa kazi yao ni kudandnia tu, ….wahuni wa mjini’akasema Malikia,.

‘Hivi wewe malikia,una maamuzi gani na hii nyumba, kwani wewe ni nani kwenye hii nyumba, wewe ni mwanafamilia?’ akasema Tajiri.

‘Jamani huu sio muda wa kulumbana,…tunahitajika kuangalia nini cha kufanya, …mukianza kugombana, hata watu watahisi muna jambo baya …kwanza kaeni chini, kama watu waliofiwa,…’akasema wakili.

‘Lakini nani amekufa…?’ akauliza mama mdogo.

‘Mzee unamuona pale kwenye sofa lake, ana uhai yule?’ akasema Malikia huku akimwangalia huyo mama kwa makini, na kabla hajaendelea kuongea Maua akasema kwa sauti ya unyonge, pale alipomuona huyu mzee alivyolala, ikiashiria kuwa kweli anaonekana kama mtu aliyekwisha kukata roho.

‘Lakini dakitari wake yupo wapi?’ akauliza Maua.

‘Hayakuhusu…..wewe kazi yako inajulikana, kukaa mitaani usiku na kuhadaa wanaume za watu’akasema Malikia.

Maua hakujali hayo maneno ya Malikia akasogea pale alaipolala yule mzee, taratibu akaweka mkono wake kwenye shingo, alikumbuka kuwa mtu akiwa kafariki, mapigo ya moyo yanakuwa hakuna , na sehemu muhimu ni kwenye mshipa wa shingoni. Na hapo akaweka kidole chake na kukituliza kwa muda….Akiondoa haraka na kuwamngalia yule mzee, akashangaa kuona wanaangalia..

‘Oh….’Maua akashituka, na akahisi kitu, macho ya yule mzee yakawa kama yanaongea jambo, na yakafumba,…Maua akahisi kitu, akatulia, na kugeka kuwaangalia wenzake.

‘Umegundua nini wewe unayejifanya dakitari?’ akauliza Malikia ambaye alionekana kutotaka kumkaribia huyo mzee, hisia za kuwa huyo mzee ni maiti, zilishajenga kichwa chake, na hisia za kuwa yeye kuwa ni msababishaji wa hicho kifo, zilikuwa zikimsuta….

‘Mimi naombeni mumuite dakitari wake haraka iwezekanavyo, ..kwma nyie hmuwezi naombeni namba ya dakitari wake nimpigie…’akasema Maua

‘Wewe kama nani..huyu mwanamke vipi, …’akasema malikia akimwangalia wakili, wakili alikuwa katulia akiwa kaangalia chini, hakusema neno.

‘Nimempigia mara nyingi hapokei, na kuna muda alipokea mara moja akasema nisubiri kwani yupo kwenye chumba cha upasuaji…’akasema Tajiri.

‘Ukarizika na kukaa kimiya….?’akasema Maua kama anauliza huku akionyesha kushangazwa na kauli hiyo, akageuza kichwa kumwangalia yule mzee, na alimuona akiwa katulia kama alivyomkuta, na kuna wakati alihisi kuwa huenda kweli keshakufa na kule kuona kuwa huyo mzee kamwangalia ni hisia zake tu.

‘Nimekuwa nikijaribu mara nyingi, unafikiri mimi sina uchungu na huyo mzee, ni mjomba wangu, hawa wahuni ndio wamenichanganya…’akasema Tajiri.

‘Nani muhuni hapa, wahuni ni hawa wanawake…..sijui mlikutana nao huko Dar, kwenye mitaa ninayosikia wanajiuza wanawake….waone walivyo….’akasema Malikia akiwaangalia Maua na mama yake mdogo juu chini

Maua aliendelea kupuuza hayo maneno ya Malikia, na akilini mwake akakumbuka siku ile alipokutana  huyo dakitari, alipokuja kumtembelea huyo mzee…Yule dakitari alikuwa na haraka, lakini aliwahi kumpa Maua  kadi yake…..

‘Hii ni kadi yangu, ukiona huyo mzee kazidiwa nipigie haraka, hii hapa ni ya kazini, na hii namba ya chini kabisa ni yangu ya kawaida,..nipigie kwa hii namba ya chini, wengi hawaifahamu, ..na ni namba yangu maalumu kwa ajili ya huyu mzee…nakuomba usimwamshe, ..na usimsumbue….’akakumbuka alivyoambiwa.

Alipokumbuka hivyo, akafungua mkoba wake na kutafuta hiyo kadi , akaiona….na kuipiga hiyo namba,na mara simu ikaanza kuita, ..na mara huyo dakitari akawa hewani. Wakati anaendelea na kupiga simu Malikia alikuwa akiongea na wakili, kwa sauti ndogo, huku akitabasamu, na mara kwa mara alikuwa akimtupia jicho Maua na kumwangalia kwa dharau.

‘Ni nani mwenzangu…..?’ akauliza huyo dakitari.

‘Napiga simu toka nyumbani kwa mzee….eeh,hali yake ni mbaya sana,..eeh, ndio mjomba wake Tajiri’akasema

‘Nakuja sasa hivi, nani wapo humo ndani?’ akauliza huyo dakitari.

‘Yupo, huyo wakili wake, Tajiri na …..Malikia wa nani sijui’akasema Maua akiwa kainama, hakutaka kuwaonyesha watu waliokuwemo humo kuwa anaongea na huyo dakitari.

‘Safi kabisa tunakuja….ndio muda muafaka..’akasema huyo dakitari na kukata simu.

‘Ndio muda muafaka kuna nini kinaendelea hapa?’ akawa anajiuliza na akageuka kumwangalia mama yake mdogo, ambaye kwa muda mwimgi alikuwa akishangaa umaridadi, na ufahari wa hicho chumba, na alikuwa kwenye ndoto ya aina yake, akamsogelea na kumvuta pembeni.

‘Naona hapa hapatufai, tuondeke haraka’akasema Maua.

‘Twende wapi, subiri..hapa pananukia utajiri, hatuwezi kuondoka hivi hivi, kwanza wewe unatakiwa uwe karibu na Tajiri, kama mzee , mjomba wake keshakufa,…unasikia wewe unatakiwa uwe karibu naye kwa ajili ya kumfariji,…usikubali kushindwa na huyo mwanamke,…’akasema akigeuka kumwangalia Malikia.

Malikia aliwaona wakiteta, akawasogelea na kuwaambia, ‘Nyie nilishawaambia muondoke,….’akasema Malikia na kabla hajamaliza, mlango ukagongwa, na wote wakageuza macho kutizama mlangoni, lakini Maua hakutizama mlangoni, alikuwa katizama kwenye kitanda, na akajikuta anatizamana tena na yule mzee, ….

Safari hii, akashikwa na kitu kama mshituko, kwani kweli aliona kama anaangaliana moja kwa moja na huyo mzee, akashituka, akawa kama anaogopa…..akajikuta akisema kwa sauti ndogo

‘Hajafa…’akawa kamshikilia mama yake mkono, …lakini kwa wakati ule hakuna aliyesikia sauti yake, kwani wenzake walikuwa wameshikwa na butwaa , …baada ya mlango kufunguliwa……….

NB: Samahanini sana, nilikuwa nimetingwa na mitihani ya kimaisha,....

WAZO LA LEO: Ukiona kwako kunafuka moshi, ujue kwa mwenzako kunateketea, maisha ndivyo yalivyo.


Ni mimi: emu-three

2 comments :

Shalom said...

Pole sana kwa mitihani maisha ndivo yalivo.

emuthree said...

Shalom nashukuru sana, kwa kuwa nami na kunijali, na wote walionimiss, Tupo pamoja