`Baba naye bwana kazidi, hata mwezi haujaisha anataka hela ya matumizi, yeye anafikiri nitapata wapi pesa za kumlipa kila mwezi ….’akawa analalamika rafiki yangu, ambaye muda mfupi tu uliopita alikuwa akilalamika kuwa ajira hakuna, ajira zimekaliwa na wazee, hawataki kuachia nafasi.
‘Nakumbuka muda mfupi uliopita ulikuwa ukilalamika kuhusu swala la ajira ukasema ajira zimekaliwa na wazee…’nikamwambia.
‘Ndio wewe huoni, ukifika maofisini, mabosi wakubwa wakubwa wote ni wazee, angalaia hata serikalini, mawaziri, manaibu sijui nani, hakuna vijana,…wakati umefika waondoke na sisi vijana tupate nafasi…tulete mabadiliko, na maendeleo..’akasema.
‘Wewe sasa hivi unalalamika kuhusu baba yako kukudai pesa ya matumizi, baba yako huyo ambaye hutaki akae ofisini tena kwasababu vijana wanataka kushika nafasi…’nikasema.
‘Kwani baba yangu yupo ofisini, baba yangu alistaafu mwaka jana hata kabla ya muda wake….’akasema
‘Kwanini alistaafu..?’
‘Kwasababu ya afya yake, na hataki kusumbuliwa na vijana, ambao hawataki kumsikiliza, wao wamekuja na mambo yao ya chapu chapu,…’akasema huku akicheka.
‘Unaona baba yako ni sawa na hawo unadai waondoke madarakani, kama angelikuwa bado yupo ofisini, usingelisumbuliwa tena, yeye kaachia ngazi ili wewe ushike nafasi yake, na kushika nafasi yake ina maana wewe majukumu yanaongezeka, unatakiwa umuhudumie yeye kama alivyokuhudumia wewe ukiwa mdogo…kufa kufaana, au sio….’nikasema.
‘Tatizo lako hunielewe, na unachanganya mada, …hawo waliopo maofisni sio baba zangu, na pia baba yangu anadai pesa kabla mwezi haujafikia, sasa mimi nitazipata wapi….hebu niambie,…usichanganye mada, tafadhali…’akasema kwa hasira
Tukiwa kwenye mazungumzo hayo nikakumbuka wapi tulipotoka, nikakumbuka enzi za utoto, ambapo tulikuwa tukiwadekea wazazi wetu. Unaona kama jana tu, ulikuwa mtoto, kijana na sasa mtu mzima,….Nikajiuliza je kuna mtu anaweza kuzilipa fadhila za wazazi, jibu ni hapana, labda kulipa kwake, ni hicho kidogo utakachopata umtumie, licha ya kulalamika kuwa hakitoshi,lakini ni haki yao uwatumie. Wao wataishije na wakati hatutaki wake ofisini, na hakuna huduma yoyote ya wazee wetu, au ipo?
Enzi za utoto ambazo tulikuwa tunatembea uchi, hatujali,kwasababu akili za kujua uchi nini hazipo, nashangaa sasa hivi vijana wanavaa nusu uchi, …suruali inashushwa nyuma na chupi zinabakia nje, na wengine hata chupi zenyewe zinakuwa zipo chini, ukiuliza unaambiwa ni fasheni, ni kwenda na wakati,..labda mimi nakosea nikisema ni kurudia wakati, tunarudia utoto.
Tunarudia utoto ambao hata kuku, anaujua akikuona umeshikia mkate anataka akunyang’anye anajua wewe ni mtoto tu utaishia kulia,`mama’ au baba..huku ukuwa uchi,unamuogopa hata kuku, leo umekuwa umeshasahau fadhila.
Je tutakose atukisema kuwa fasheni za siku hizi zinarudia utotoni, au enzi zile, …Hata hivyo tusisahau kuwa kama tupo madarakani, au tunachakarika, tunahitajika kuwalipa wazazi wetu angalau kidogo katika lile fungu tunalolipata, tuache kulalamika kwani ni haki yao, ….hujui kuwa bila wao usingelipata hata hicho kidogo ulicho nacho,usingelweza kupata hata hiyo nafasi ya kulalamika kuwa `wazee hawataki kuachia ngazi’
Ni wazo la leo,nimeliwaza tu,baada ya jamaa kuacha laptop yake akikimbilia kumtumia baba yake pesa kidogo licha ya kuwa analalamika.
Jembe langu halijapata mpini, hata hivyo kisa kitaendelea tuombeane heri tu.
Ni mimi: emu-three
3 comments :
Duuh hii kali!
Kaaazi kwelikweli maisha haya!! Pamoja daima ndungu wangu!!
Hapa ipo hoja
Post a Comment