Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, February 28, 2012

Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli-85 hitimisho-29



Mama akiwa katikati ya kundi la wakina mama alijaribu kujiiba kwa kuangali huku na kule, moyo wake ukitafuta wapi ulipowekwa mwili wa mume wake, lakini hakuweza kugundua. Kitu kilichomsaidia ni lile giza, mwanga pale ulikuwa hafifu hasa sehemu walipokuwepo akina mama. Mwanga ulikuwa sehemu ile walipokaa wanaume, hasa sehemu ile ya mbele ambapo walikaa wazee wa jadi.

Wakina mama wote walivaa nguo nyeusi, vilikuwa vitambaa vya kaniki, na kujifunga kichwa ni vitambaa hivyo hivyo vya kaniki vyeusi, na kweney uso zao walijipaka masinzi, na kwa kufanya hivyo, sura halisi za akina mama hawo zilikuwa ahzijulikani. Mama alifanya hivyo hivyo baada ya kuambiwa na rafiki yake, na pale ,walikuwa wameinamisha vichwa vyap chini wakisikiliza mkuu wao jadi, mkuu wa familia.

Mkuu huyu alitumiwa kama muongeaji maarufu, alijua nini cha kuongea kwenye matukio kama haya, na aliogopewa sana, kwani kauli yake ilichukuliwa kama kauli ya `kuhani mkuu’ alikuwa ni kinywa cha wazee wa jadi. Mama alijaribu kujiiba kumwangalia sura yake, na kila mara alipobahatisha kuuona uso wa mtu huyo, alihisi mwili ukimzizima kwa woga, hakujua ni kwanini, labda ni kwasababu ya uwoga, au ni kwa vile alifika hapo bila kuhitajika.

Mama mara kadha alijikuta akijishuku kuwa huenda akina mama waliopo hapo watakuwa wamemgundua na huenda wanaweza wakatoa taarifa kwa watu wao, lakini hakuona mtu aliyemshuku , kwani wengi walionekana kujawa na huzuni, …..Ilionyesha kuwa marehemu mume wake alikuwa akipendwa sana, au alikuwa mtu maarufu sana kwa watu, hao, kwani watu walikuwa wengi na kila mmoj alionyesha huzuni ya hali ya juu.

Akamgaukia rafiki yake aliyekuja naye, ….ilionyesha wazi kuwa hata rafiki yake alikuwa na wasi wasi mkubwa, kwani aliondoka hata bila ya kumuarifiu mume wake , ambaye hakuwepo nyumbani. Rafiki yake huyo ni mmoja wanakijiji wa hapo, alikuwa anajua mambo yote na desturi za hapo, na mara nyingi, mama alimtumia huyo kuundua nini kinachoendelea sehemu anayotoka mume wake, ……….
Siku alipotoka pale nyumbani bila wenzake kujua, alikwenda moja kwa moja kwa rafiki yake huyo akamwambia nini kusudio lake, mwenzake akamwambia kuwa licha ya kuwa alitakiwa kwenda huko kwenye msiba, lakini msiba huo umegubikwa na mambo ambayo yeye hayapendelei, akasema wazi wazi kuwa familia hiyo ni mashuhuri sana na wengi wa wazee wa familia hiyo ndiyo wakuu wa mambo yao ya kijadi, na wanafuatilia sana mambo ya kishirikina, mambo ambayo yeye hayapendi.

‘Mimi siwezi kwenda huko, mambo yao ni kishirikina matupu, unaweza kufika huko ukachaguliwa kutolewa kafara, kama wakikishuku tu ubaya, …..hapana kama unakwenda nenda peke yako, na nakushauri kuwa kama ulishaambiwa usiende usiende, utajitakia matatizo ya bure….’mwenzake akamuonya.

‘Hapana lazima nifike, naombatfadhali nisaidie twende angalau mara moja, halafu tukijua nini kinachoendelea titarudi…’akasema mama.

Baada ya kubembelezwa na kuahidiwa chochote, wakakubaliana na kuondoka pamoja, na ndipo alipoambiwa ni nguo gani wanatakiwa kuvaa kwenye misiba kama hiyo, na pa anatakiwa kunyoa kipara, na kujifubga kitambaa cheusi kichwni, ….

Wakiwa huko walikaa sehemu ambayo wangeliweza kuongea, ili kama kuna maneno hayasikii mwenzake ambaye ni mzaliwa wa huko amtafsirie, na ndivyo ilivyokuwa na aliposikia na ndipo wakasikia kauli ya yule mkuu wa ukoo ikisema;

‘Kwanza kabla ya yote tunamuomba mke wa marehemu na watoto wake waje hapa mbele, …’kauli hiyo ilimshitua sana mama, akahisi ni yeye anaitwa, mbona walishasema kuwa asiwepo hapo kwenye huo msiba, mwenzake akambonyeza atulie.

Mara akatokea mama mmoja akiwa na watoto watatu akamsogelea yule mzee na wakawa wanaongea lugha yao na kwa sauti ndog ambayo hawakuiskia.

‘Najua ndugu yetu alikuwa na wake wawili, lakini mke tunayemtambua sisi kiukoo ni huyu, huyo na watoto ndio warithi halali wa mali yote ya marehemu, na mambo yote ya kimila, tunamshukuru sana huyu mama kwa kuwa mvumilivu na kuwa mstari wa mbele kwa kila jambo linalihusu mila na taratibu zetu, sio huyo mke wa pili ambaye tutakuja kumzungumza mambo yake baadaye….’akasema huyo mzee,

Mama pale alipokaa alishangae kuhusu hiyo kauli kuwa mume wake kumbe alikuwa na mke mwingine, .....hakuamnini masikio yake kwani hata rafiki yake ambaye anakujua sana huko hakuwahi kumwambia hilo, akakumbuka siku moja rafiki yake huyo alimwambia kitu kama hicho, lakini alichukulia kama utani.

Na mara mtu mmoja akawa anamfanyia yule mama mambo yao wanayojua wao wenyewe,na mama hakuwa na hamu hata ya kumtizama huyo anayeitwa ni mke mwenzake, na wale watu walipomaliza kumfanyia yule mambo yao, wakaja akina mama wawili wakamshika mkono na kumpeleka kukaa sehemu sehemu maalumu aliyoandaliwa.

‘Sasa mama huyu yupo tayari kutafutiwa mrithi wake, ambaye kiutaratibu anatakiwa awe mmoja wa ndugu wa marehemu, na tunashukuru sana kuwa yule ndugu yake ambaye alitoweka siku nyingi sana na tukadhania kuwa amekufa lakini kila siku mizumu yetu ilituashiria hivyo kuwa huyo mtu bado yupo hai na anatekeleza majukumu ambayo yanafaa awe hivyo hivyo…..; akasema huyo mkuu na kunyosha kidole mbele ya kundi la wazee waliokuwa wamekaa kimiya.

‘Kijana wetu, sasa tunakukaribisha rasmi kwenye kundi la wazee wa kimila, na ingawaje una mkeo ambaye umekuwa ukimtembelea kisiri, sisi tunalijua hilo, na tunmashukuru sana kuwa hata yeye alikuwa msiri, licha ya kuwa hakukujau kuwa ni miongoni mwa wanafamilia hii, haya yaote yalifanyika kwa maksudi maalumu, amayo hatuwezi kuyasema hapa, hayo ni mambo ya wanafamilia na wazee wa kimila, kazi umemaliza sasa unakaribishwa kundini….’akasema na kwenda kumshika jamaa mmoja mkono

Jamaa yule alisimama na kwenda kukabidhiwa bakora , bakora ile ni maalumu kwa mila hizo, kilikuwa ni kisu kirefu, kilichozamishwa ndani ya bakora hiyo, wewe ukiona utazania ni bakora ya kawaida, lakini akitaka kutumia hichi kisu kirefu kuna jainsi anaivuta na kisu hicho kinatokea na ndivyo alivyofanya huyo jamaa na akamkata kondoo mmoja aliyekuwa kaweka pale mbele shingo kwa mpigo mmoja, na damu yake ikakingwa na wote wakaanza kuinywa…

Mama alihisi kutapika, maana hapendi kabisa damu mbichi, lakini wakina wenzao walizoea hiyo hali walikuwa wametulia kimia, na ile damu ilinywea tu na wanaume, na zoezi hilo lilipokamilika, yule mzee akaogea mbele na kuanza kuongea;

‘Sasa tumeshaipa mizumu haki yao, na sisi tumechangia, enzi zetu, damu hapa ilikuwa ni ya mtu, na mtu ni yule aliyesababisha hiki kifo, bado hatujagundua vyema kuwa huyo mke wa pili na familia yake wanahusika au la, lakini aliyeyatua risasi tumeshamgundua na kazi hiyo imefanywa vyema na kijana wetu ambaye tumemfunza vyema, anajua mbinu zote za upelelezi na uasari hatuna wasiwasi naye, na tuna ushahidi kuwa ni nani kamuua ndugu yetu, kijana wetu aliyekuwa mstari wa mbele kubeba jukumu la familia zetu.

‘Kazi iliyopo mbele yetu ni moja, kulipiza kisasi, hilo ni amri, kama mwanajamii yoyote atauliwa , lazima aliyemuua atafutwe na yeye auwawe, na kichwa chake , kipelekewe mizimu, hata kama hatutapa kichwa chake, lakini lazima sehemu yoyote ya mwili iapatikane na mizimu ipoozwe, ….ingelifaa damu, lakini jinsi ya kumleta huyo mtu hapa mbele imekuwa ni ngumu kidogo, kutokana na mambo yaliyojuu ya uwezo wetu, tungeleiweza kumleta hapa kimazingara, lakini kifo chake, kinatakiwa kiwe sawa na alivyomfanyia ndugu yetu kwanza, halafu mengine baadaye…’akasema huyo mzee.

‘Sasa kuna jambo moja, niliwaambia kuwa ndugu yetu alikuwa na mke wa pili, huyo amekuwa kikwazo kikubwa kwa ndugu yetu na mwanzoni tulitakiwa kuchukua hatua, lakini kwasababu za sheria ya nchi na mambomengine, tukashindwa na hatukuoa kuwa kua haja ya kujiingiza huko kiundani, ilimradi jamaa yetu alikuwa na mke wake wa halali ambaye liawajibika sehemu muhimu, ….lakini….’kabla hajamaliza akatokea mzee mmoja na kumsogelea yule msemaji, akamnon’oneza kitu sikioni.

‘Nashukuru kuwa mambo mengine yamejileta, unajua familia yetu imekamilika, huwezi ukafanya jambo la kisiri hapa, huwa tuna wazee wananua, tuna wazee wanaona zaidi ya mnavyozania, kwahiyo huwezi ukafanya jambo la kisiri lisijulikane, ….na hilo nitamuachia baadaye mzee wetu afanay vitu vyake baadaye, ngoja niwaelezee kuhsu huyo mke wa pili kwanza….’akasema huyo msemaji na pale aliposimama mama akaanza kuhisi wasi wasi.

‘Huyo mke wa pili makosa yake ni kuwa kwanza alidanganya kuwa ana mtoto na marehemu, kitu ambacho sio kweli, ina maana alituletea damu isiyostahili, na baya zaidi akaandikisha urithi sehemu kubwa ya mali ya ndugu yake kwa familia yak hiyo haramu, na zaidi akawa kamteka kiakili, na madawa ya kiwako huko alipotoka, hilo tuliligundua na licha ya kuwa mizimu ilimwendea huyo marehemu na kumkanya na kumpa maagizo yote, lakini hakuweza kuyafuata, na ikawa ndio chanzo cha mikosi yote unayoiona ambayo imekuwa ikiitafuna familia.

‘Sasa basi kimila watu kama hawo wanatakiwa kuondolewa, kama hawataki kuondoka kivyao sisi tutawaondoa kivyetu, na kivyetu ina maana wanakuwa ni damu ya mizmu yetu, …unajau tunatakiwa tusiwe na huruma na watu wasiotuhurumia, kama huyo mwanamke kadiriki kumhadaa mtu wetu hadi kumiliki mali siyo yake, unafikiri ana huruma na sisi, hana…kwahiyo ili aisilete uharibifu zaidi tutafanya lile linalostahili….sasa kabala ya kumalizia mambo mengine, namkaribisha mzee wa kuona mbali afanye vitu vyake…

Yule rafiki wa mama aliyekuwa akamshika mama mkono na kumnong’oneza kuwa waondoke hapo haraka maana huyo mzee ni mwanga, atawagundua na akiwagundua….hamna huruma, lazima damu imwagwe….., mama akawa mkaidi akasema haondoki mpaka aone mwisho wake, na mwenzake akainuka taratibu na kuondoka, akasogea nje ya lile enao akiangalia nini kinataka kufanyika.

Yule mwanamke akaona hapo kunaweza kukatokea baya, akachukua simu yake na kumpigia mume wake ambaye ni mmoja wa maaskari, na mume wake akashangaa kusikia kuwa mtu waliyekuwa wakimlinda ndani keshaondoka hata bila wao kujua, ….akaanza kumlaumu, mkewe kwanini walienda hapo na wanajua nini kitatokea,

‘Huyu rafiki yangu alinisisitiza sana, sasa fanya uwezavyo maana yule mwanga keshaanza mambo yake ‘…akasema huyo rafiki wa mama akipiga piga miguu kwa uwoga.

‘Ngoja niongee na bosi , lakini sijui tutafanyeje maana tulishakubaliana kuwa hatutaingilia mambo yao, sasa nyie mumeharibu mkataba…sijui….’akasema huku naye akihangaika akijua kuwa wamefanya makosa kwa kuwaamini hawo wanawake, kwani wao walijua hawataweza kutok humo ndani, na nguvu yao kubwa waliielekeza kwenye watu wanaoingia. Harakaharaka akampigia bosi wake simu.

‘Bosi kuna jambo limetokea, mke wa marehemu katoroka na kwenda huko msibani, na hapa ninvyokuambia mambo yanaanza kuwa mabaya huko , yule mzee wanayemuita mwanga, keshaanza mambo yake, na nijuavyo huyo mama ni mbaya wa familia lazima atakuwa asusa ya mizimu.Sijui alitokatokaje….’kabla hajamaliza Mpelelezi akampa amri.

‘Chukua gari la king’ora nenda na kikosi chetu maalumu, mkifika hakikisha mnamchukua huyo mama haraka, na mimi namalizia kazi huku, tutakuja na kikosi kingine kusaidia……muwahi haraka kabla hawajafanya mambo yao, hiyo ni amari….’akasema mpelelezi bila kujali makubaliano yao kuwa hawataingilia mambo hawo wazee.

***********
Rose alikuwa keshazindukana na hali yake ilikuwa shwari, na docta akampima na kuhakikisha kuwa hakuna tatizo jingine, baadaye akaaga na kuondoka, huku akiwapa maelekezo kuwa kama kuna lolote litatokea wampigie simu.

‘Tunashukuru sana Docta….’akasema Mgonjwa akiwa na furaha.

‘Nashukuru docta, ….’akasema Rose, huku akijaraibu kujiinua pale alipokuwa kalala, na Mgonjwa akamsaidia kumuinua na alipokaa vizuri wakajikuta wakiangaliana kwa muda, kila mmoja akiwa anawaza lake na wakawanza kuongea alikuwa, akasema kwa sauti ya utani;

‘Leo mgonjwa kawa docta, na docta kawa mgonjwa…nashukuru docta wangu…’akasema Rose huku akisimama na kuelekea dirishani kuangalia nje, nywele zilikuwa zimefumuka, na hakutaka hata kujiangalia jinsi alivyo, alijua kabisa yupo katika hali asiyotka awe lakini hakujali, akakunja uso kwa hasira, huku akikimbuka jinsi alivyokuwa akiteswa kule alipokuwa akshiukiliwa.

Mgonjwa naye kama alivyojulikana kwa jina hilo naye akasimama akimfuata Rose pale aliposimama naye akawa akiangalia dirishani, na kusema;.

‘Usipate shida mimi nipo kwa ajili yako, najua sijui dawa zipi zitakufaa, lakini docta keshasema upo shwari, mimi nitakupa dawa za kukutuliza mawazo, maana naona ulikuwa katika hali numu sana, walikufanya nini hawa watu, kiumbe kama wewe usiye na hatia, hawajui wewe ni mtu muhimu sana katika maisha yetu…au wewe hujui madocta ni watu muhimu sana, hebu fikiria kama isngelikuwa madocta sasa hivi mimi ningelikuwa wapi…?’akasema mgonjwa.

‘Ni kweli usemayo,ila kila nyanja ina umuhimu wake, kwa mfano kamawasingelikuwepo walimu, madoctawangelitokea wapi, kama wasingelikuwepo walinzi wa usalama, nchi ingelikuwaje,kama wasingelikuwepo wafanyabiashara, maisha yangelikuwaje, wakulima halikadhalika, kwahiyo kila nyanja ina umuhimu wake…swali ni je wale wahusika wanawajibika na walio na mamlaka wanawatahamini je, …na vitu kama hivyo.

‘Sawa mpenzi, mmh, maana kila unaloonhea kwangu linakuwa la umuhimu sana,ulitakiwa uwe rasi wa nchi wewe,…na surayako ilivyo, …..siju nikufananishe na nani, kleopatra au nani vile….’akasema kwa utani.

‘Acha utani wako, mimi ni mzuri kulikoa Maua, wewe kila ukilala unamuota Maua , Maua,. Kweli ndugu yangu alikukaa akilini, lakini sio mbaya ndugu yangu kweli mrembo, na kweli alikupenda,…sijui sasa itakwuaje…’akasema Rose.

‘Maua hana tofautoi na Rose, mimi kwangu sasa nawaona kama kitu kiomoja, ni kama ukiwa na mikono miwili kamili, yote ni sawa tu,….’akasema Rose.

‘Sio sawa, kama unatumia kushoto, au mkono wa kulia, uwezo wa kufanyakazi unatofautiana…’akasema Rose.

‘Uwezo kimawazo, lakini kama huo wa kushoto au wa kulia ungeliwekwa sehemu ya mwenzake uwezo ungelikuwa ule,ule , …’akasema Rose, na wote wakatulia kwa muda,baadaye Mgonjwa akauliza swali;

'Hebu nambie ilikuwaje huko ulikotoka, maana umekuja hutamaniki, umechafuka, una midamu, walikuwa wakikutesa, au ilikuwaje….?’ Akauliza mgonjwa.

‘Wewe acha hata kusimulia nashindwa, yaliyotokea huko, sikuweza kabisa kuamini , dunia hii ione tu, kama siri za wanadamu zingeliwekwa wazi mbona watu tungekimbiana, ….hayo mambo niliyokutana nayo, nimeamini kuwa binadamu ni kiumbe wa ajabu sana…..niponea katika tundu la sindani, na kupona huku sio kwa uawezo wangu, nafikiri ni mungu tu alifanya niokoke….’akasema Rose huku akiangali huku na kule kwa wasiwasi, utafikiri anaogopa jambo fulani,

‘Ilikuwaje, hebu niambie…..tafadhali’ akauliza mgonjwa, na Rose akawa akatulia huku katoa macho, na bila kuseam kitu, akakumbuka yale mazungumzo aliyoyasikia pale alipokuwa kashikwa mateka, mazungumzo yale yalimfanya aishiwe nguvu, akiwa anajaribu kukumbuka muda aliokuwa kapoteza fahamu ,……….

‘Huenda sasa hivi wameshamuua mama, sijui nifanyaje sasa hivi, hapana, inawezekana hawajafanya kitu,…’akasema huku akihaha huku na kule.

‘Hebu niambie ni kitu gani, huenda nikaweza kusaidia, ….’akauliza mgonjwa, lakini Rose hakumskiliza, akatoka kwenye kile chumba walichokuwemo na kufika chumba cha maongezi, hakujali tena ile amri waliyopewa kuwa wasitoke nje, na bahati nzuri alikuwa simu ya mezani, akaanza kupiga namba ya mtu anayoikumbuka, huku akilini mwake akikumbuka yale maneno aliyoyasikia kule alipokuwa matekani;

‘Kuna watu wawili wanatakiwa waondolewe kabla mwili wa marehemu kuzikwa, damu yao ni muhimu ili uweze kufanikiwa kurithi kila kitu, wa kwanza ni huyu binti, ambaye yupo mikononi mwako kwa sasa, kazi ni kwako, wa pili ni mama yake, huyu damu yake itatolewa mbele ya jamii, ….’ Rose, licha ya kuwa alikuwa katika hali mbaya, baada ya vipigo, na kupewa madwa yaliyoulegeza mwili wake, madawa hayo yalikuwa yakitoa harufu kali, na ili ifanye kazi vyema, unawekewa kidogo puani, lakini hata hivyo aliweza kusikia hayo mazungumzo

‘Sasa mama yake tutampataje , kwaniyupo kwenye ulinzi mkali sana…..?’ akasiki sauti ikiiuliza.

‘Huyo mama atajileta yeye mwenyewe kwenye msiba, licha ya kuwa yupo kwenye ulinzi, …ndipo hapo utaona miujiza ya mizimu, na licha ya kuwa keshaonywa asifike huko, lakini mwenyewe atajipeleka mikononi mwa wazee wa jadi na mizimu, kwanza hawatamgundua, lakini mizimu inasema humo kwenye msiba atagunduliwa na `mtambuzi wa wanga, na hapo inatakiwa damu yake imwage haraka, na ikishindika hapo,basi hakuna kitakachowezekana tena, mali nyingi ya ukoo itapotea….

‘Kwahiyo mimi sihitajiki katika kumpata huyo mama, na huyu binti nimfanyeje kwa sasa…? ‘ sauti ikauliza.

‘Hulo ni shauri lako,….nakumbuka ulishaambia kabla, ila kumbuka unatakiwa usubiri mpaka usiku, kuna ule mlio ….najua unajua vyema, ukusikia ule mlio ambao ndio muda wa kafara zinapotolewa hapo hapo fanya kama ulivyoagizwa, tumia kile kisu kwenye bakora , hakikisha ncha imetoboa mshipo wa damu shingoni, …., chukua damu yake iwahishe huko msibani,…na sio lazima ufanye wewe, maana wewe una majukumu mengine, …’sauti ikasema.

‘Majukumu gani mengine….?’ Sauti ikauliza.

‘Ukumbuke kuwa utahitajika kuwepo huko kwenye kafara, wewe ni muhusika mkuu, wewe waachie hao vijana wetu hiyo kazi, …kwanza huyo binti hana umhimu sana kama mama yake….’akasikia sauti ikisema.

‘Je akitiroka, maana huyu msichana ni mjanja sana…’sauti ikasema.

‘Hiyo dawa ina nguvu sana, na kama atazindukana mapema, inabidi aongezewe hiyo dawa, ni kiasi cha kutoa maagizo kwa vijana wako, wakikosea, sisi hatuna lawama , itabidi ukubali matokeo, jingine la muhimu na kulipiza kisasi cha ndugu yako, hilo unatakiwa ulifanye kwa mkono wako mwenyewe, na yote hayo yanatakiwa kufanyika kabla ndugu yako hajazikwa. Ikishindikana hayo, ujue kuna mkosi …ujue kuna mengine makubwa yatatokea….na dalili inajionyesha…kwaheri….’sauti ikasema

‘Na dalili gani mbona unanitisha….’sauti ikajijitetea.

‘Sikutishi tangu mwanzo mlishaharibu, mlikuwa mumepewa maagizo haya mapema mkapuuza, sasa mnataka kila kitu kifanyike hatua hizi za mwisho, …..iliyobakia ni juhudi yako mwenyewe, tunakutakia mafanikio mema…..hatuna zaidi la kufanya, yote yatategemea mkutano wa usiku wa leo…..wao wanajua zaidi…’sauti ikasema na Rose hakuweza kusikia zaidi akapoteza fahamu…..

***************

Rose alishituka toka kwenye usingizi mzito, na alipofumbua macho na kuangaza huku na kule, aliona walinzi wakiwa wamelala, ….kwanza alishangaa mikono yake haijafungwa kinyuma na alipokamatwa mwanzoni, walimfunga miguu na mikono. Alijaribu kujisogeza kwa shida, bila kujifungua miguu, kwani alikumbuka, ile dawa aliyokuwa akiwekewa puani, ilikuwa ipo pembeni mwa malinzi mmoja aliyekuwa kalala karibu na meza,

Hakutaka kupoteza muda, akaanza kujisogeza sogeza kwa shida taratibu hadi akaifikia,….ilikuwa ndani ya kichupa kidogo,na pembeni kulikuwa na kitambaa ..ilikuwa kama una unga, akatoa kidogo na kuweka kwenye kile kitambaa, na kumsogelea yule mlinzi, akaweka karibu na pua yake, hakumgusa karibu sana....

Halafu akajisogelea hadi kwa yule mlinzi mwingine na kufanya hivyo hivyo….

Hakupoteza muda kuhakikisha kuwa ile dawa imefanya kazi yake, alichofanya ni kujifungua kamba ile ya miguuni, huku akihisi maumivu makali, kwa kujiburuza kwenye kokoto, kwani chumba kile kilikuwa na kokote, hakikuwa kimeskafiwa, ilikuwa ni kama stoo ya kuhifadhia vitu. Hakujali maumivu, alijali ni kuondoka pale na kuokoa roho yake. Alikimbia hadi karibu na barabarani, hapo bahati nzuri akapata msamaria mwema akampa msaada hadi mjini, kwani huko alikokuwa kapelekwa kumbe ni nje ya mji.

Rose alipokumbuka hayo na ile kauli, ….akawa kama kachanganyikiwa, kwani alijua sasa mama yake atakuwa huko kwa hawo watu, atakuwa kajipeleka mwenyewe kama walivyodai, nia yake kwanza ilikuwa kuhakikisha kuwa kweli mama yake kaondoka nyumbani, kwahiyo kwanza alipiiga simu hukokwao, ikapokelewa na mlinzi, yule mlinzi, aliuliza huyo anayepiga simu ni nani;

‘Wewe usiniuliza kuwa mimi ni nani, ni muhimu sana nikajua kuwa mama yangu yupo hapo au …’ akasema Rose kwa hasira na huyo askari akatululia kumbe alikuwa akimpa kiongozi wao hiyo simu ambaye alimgundua Rose.

‘Mama yako hayupo…wewe upo wapi…?’ alisikia sauti ya mtu mwingine ikiuliza, ilionekana labda ndio mkuu , au kiongozi wa walinzi.

‘Hatujajua kaenda wapi, tafadahli sema ulipo tukufuate, ….’ Rose hakusubiri maelezo zaidi akakata simu na kwa muda huo mgonjwa alishafika pale alipokuwa kasimama, na kumuuliza Rose nini kinachoendelea.

‘Sikiliza wewe bakia hapa kuna jambo kubwa limetokea na mimi nahitajika kufika walipo wazazi wangu, hakikisha hutoki humu….’akasema Rose.

‘Kwanini tusiende wote, unajua Mkiwa wawili ni rahisi kusaidiana…..’akasema mgonjwa

‘Hapa sio swala la kusaidiana,…rudi kule chumbani jifungie, tukiwa wengi ndio hatari itazidi kuwa kubwa, wewe usijali, nisubiri hapa, nitakuja ,…nitakuja kwa ajili yako…’akasema na haraka akambusu mgonjwa shavuni, na kumsukuma arudi huko chumbani, mgonjwa alifanya hivyo kwa shingo upande, yeye akaichukua ile simu pale mezani.

Alijaribu tena kupiga lakini kila namba aliyojarib ilikuwa haipatikani, na hapo akakumbuka kumpigia yule mpelelezi, akajaribu kuikumbuka namba yake , lakini haikumjia akilini mwake, aliitafuta mle ndani hadi akaipata kwenye moja ya knyaraka alizoziona mle ndani, akaipiga ile namba, lakini ilikuwa haipokelewi.

Rose alipoona kuwa akipiga simu huko alipotaka kupiga haipokelewi, akaona kuna umuhimu wa kuchukua hatua, haraka akatoka pale na kuingia kwenye moja ya chumba ambapo aliona kuna nguo zimetundikwa kwenye kamba, bahati nzuri, akaona nguo za kiaskari, akazivaa na kofia yake akahakikisha kuwa kaficha kabisa umbile lake la kike, na haraka akatoka nje,…..

**********
Mpelelezi aliiona ile bastola ikiserereka hadi alipokuwa kajificha , akawa na wasi wasi kuwa huenda hawa jamaa watakimbilia hapo ili waichukue ile bastola, lakini kwa vile walikuwa wakipigana na kila mmoja akijaribu kuichukua, na pale iliposererekea ni kwenye upenyo ambapo kuna kabati kubwa lililoegeshwa , na hapo ndipo alipojificha huku akiwasiliana na wenzake ambao walikuwa wakiona kila kitu kinachoendelea hapo kwenye hiyo ofisi.

Mpelelezi huyu baada ya kugundua kuwa mkuu wao ni mmoja wa kundi hilo haramu aliwasiliana na mkurugenzi wa usalama, na mkurugenzi huyo akamwambia kuwa hata wao walishakuwa na hisia hizo lakini walishindwa kabisa kumpata na ushahidi wowote, na kwahiyo kama kweli anahusika, kazi itakayofanyika ni kuhakikisha ofisi nzima inategeshwa vyombo ya kiusalama ambayo vitakuwa vikionyesha mambo yote yanayofanyika hapo ofisini, …..

‘Hivyo vyombo nani ataviweka, ikizingatiwa kuwa walinzi wote pale ni vijana waaminifu wa mkuu, na inavyoonyesha wengi wao ni watu wake..’akauliza mpelelezi.

‘Hiyo kazi ndogo, tuna vijana wetu wa kufunga umeme, tumeshawaagiza, na kwa vile hilo jengo lina matatizo ya umeme wiki mbili hizi, hawo mafundi wakienda hapo kutengeneza, wataweka hivyo vifaa, hilo lisikutie shaka, cha muhimu ni jinsi kutakavyotokea jambo la kuweka kila kitu wazi, ili tupote ushahidi wa kutosha ….’akasema mkurugenzi. Na mambo yakawa kama yalivyopangwa, kwahiyo Mpelelezi alipewa vifaa vya kuwasilina na watu maalumu ambao walikuwa katika ofisi nyingine.

‘Sogeza hiyo bastola na mguu isionekane, …’akasikia sauti ikamwambia na akafanya hivyo huku akiwaangalia hawo jamaa wawili ambao kwa muda huo walikuwa wakipigana.

Akafanya kama alivyoagizwa, na huku akiwaangalia hawo jamaa wakipigana kwa nguvu zao zote, lakini haikuchukua muda wale jamaa wakasimama kupigana na kuanza kuongea, ….wakakubaliana waingie ndani, na hapo Mpelelezi akaona kuwa itamuwia vigumu kufanya lolote kama hatatoka pale na kusogelea kwenye mlango, na sauti ikamwanbia hivyo hivyo.

Akasogelea mlango na kuskiliza mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea huko ndani, kwani mlango ulikuwa haujafungwa vyema, na mazunguzmo yao hayakuwa mbali na yale aliyoyasikia mwanzoni, akasubiri ajue nini wataongea zaidi , lakini muda ukawa unapita kukiwa na mabishano ya mmoja kudai kadi ambayo ilikuwa na kumbukumbu ya pesa walizoziiba na kuzihifadhi nchi za nje.

‘Wakati umefika, …tumeshapata ushahidi wa kutosha, na kuna mengi ya kufanya, kwahiyo unachotakiwa kufanya ni kufungua mlango kwa nguvu na kuuacha wazi huku umewaelekeza hiyo bastola uliyo nayo…’Mpelelezi akasikiliza maagizo.

‘Kwa hivi sasa watu wetu wapo tayari mlangoni kukusaidia, usitumie silaha kama hakuna ulazima, ila kama huyo mkuu atajaribu kufungua droo ya kwenye meza yake, ambapo keshaweka bastola yake tayari kwa kuitumia, wewe piga risasi kwenye mikono yake, hatutaki auwawe kwani kuna mengi tunahitaji kutoka kwake….’akasikia sauti ikimuelekeza na yeye hakupoteza muda, akasukuma mlango bastola ikiwa mkononi…..

****************

Mama pale alipokuwa kakaa, akahisi mwili kama unamuisha nguvu, alipomtizama rafaiii yake hakumuona kabaisa na hakuju akaenda wapi, na kila alipojaribu kuinuka, akawa hawezi, alikuwa kama kapigiliwa misumari, na mbele yake alimuona yule mzee akifany amanbo yake, alikuwa akiangalia huku na kule huku akairusha kitu kama unga hewani na kuongea maneno fulani ka sauti nyembamba.

Na mara akaanza kuimbisha wimbo wake, kwa maneno ya lugha yao na mama aliyaelewa yana maana gani, alisema;

‘Mwanga mchawi afichuliwe…’ na wengine wanaitikia afichuliwe, nay eye husema tena; `akipatikana tumfanye nini, na watu huitikia, `tumnywe damu yake, mizimu ipate kutulia….’akawa anayarudia hayo maneno mara kwa mara huku anasogela kundi la watu.

Mama pale alipokaa akawa kama kamwangiwa majio,uwoga, na jasho likawa linamtoka, nguvu zikawa zimemuishia na akili ikawa kama sio yake, alijihisi kama sio yeye na akawa akiitikia kama wanavyosema wenzake. Na mara yule mzee akawa mbele uswa wake, akawa anamsogelea huku anaimba na mama na watu wengine wanaimba kumuitikia.

Mzee yule akamsogelea huyo mama na alipofika mbele yake akatikisika sana na kusema `tumempata mwali wetu…oooh, mwanga, …oooh, damu yake ni halali yetu,. …halafu akamshika mama mkono na kumuinua pale alipokuwa kakaa, mama alishangaa kwani mwanzoni hakuweza hata kusimama, lakini aliposhikwa mkono na huyo mzee, aliinuka bila kubisha na aliweza kuinuka, …

Akachukuliwa hadi mbele ya kundi, yule mzee akawa bado anaimbisha huoo wimbo, kuwa mwanga akipatikana damu yake ni halali kwa mizimu, na baadaye akasimama na kumwachia mzungumzaji, mzungumzaji akamsogelea yule mama na kumvua miwani yake, akasimama kwa muda huku akishangaa na kusema;

‘Wewe mama umefuata nini tena huku, jamani mbona mnatutafuta ubaya, kweli wewe mwanga, maana umewezaje kufika hadi hapa……ooh,naomba maji…’akasema na maji akaletewa na kunawa mikono huku akisema;

‘Jamani mimi nanawa mikono, sina lawama, nilijitahidi sana kuwaeelzea hali ilivyo katika mamb yetu haya , hawakuniskia, kwahiyo nawaachia wazee wafanye kazi yako, sina jinsi na sina uwezo wa kuingilia mambo yaliyo juu ya uwezo wangu, …..’akasema na kumguikia yule mama.

‘Kwanini umekuja hapa , Mpelelezi hakukuambia kuwa hustahili kuwepo hapa…?’ akauliza huku akiwangalia yule mama kwa macho ya Huruma.

‘Mimi ni mke halalai wa marehemu, kwanini nisihudhurie mazishi yake, kwanini mninyime hali yangu….’mama akapata nguvu za kuongea.

‘Wewe sio mke halali , mke halali ni yule pale kama ulikuwa hujui, wewe ulikuwa uwe halali kama ungelikubaliana na mila zetu, mila hazikatazi kuwa na wake wengi tu , kama unaweza, lakini wewe hukutii amari zetu, na tulikuomba sana ukakaidi na baya zaidi ukawa anampoteza marehemu, na kumuingiza kwenye mambo ambayo yameiletea familia mikosi, na ulitubambikia mtoto asiye halali na kumrisisha mali ya watu….unalijua hilo, ….’akasema msemaji

‘Mimi sikumfanyia lolote…alinipenda yeye mwenyewe na mali tulikuwa tukichuma sote katina biashara zetu, na kama alimrisisha mali , ni kwa ridhaa yake hakushurutishwa, hayo mumeyazua wenyewe, kwahiyo nina haki kisheri….’akasema mama na watu wakamzomea na huku wakisema kwa sauti;

‘Mwanga, mwizi, mwanga mwizi..’kelelel zilikuwa nyingi sana humo ndani, watu walikuwa wamehamaki na wanataka kuchukua sheria mikononi mwao.

‘Hebu tulieni,…. hatutaki kumuadhibu mtu bila yeye mwenyewekujitetea, na mumesikia akijitetea kuwa yeye kisheria za kiserikali ni mke halali,…hatukatai maana na urembo wako ungeliweza kumhadaa yoyote yule, akakuoa, ….na kama tulivyosema, tulikuwa tayari kukubali kama mke mwingine ndani ya familia yetu….’akasema yule jamaa huku akimwangalia mama chini hadi juu.

‘Kila mmoja alipokuona alijua sasa mwanetu kapata kimwana….unakumbuka tulikuomba sana ushiriki kwenye mambo ya kifamilia, ukakataa, ulikuwa wewe na starehe na kutumia mali isiyo halali yako, na ulisababisha hata mumeo asiweze kushiriki kwenye mambo ya kifamilia, …wewe, sijui umetoka wapi huko unatuletea mambo ya huko kwenu…..ni kosa kubwa sana. Tuliimba mizimu ukusamehe, lakini haikuweza kufanya hivyo….ilisema wewe ukiachiwa utadidimiza familia…’akawaeukiwa wazee na kusema;

‘Mimi kwa kumuonea huruma, kwasababu sio mtu wa nchi hii niliwakanya kuwa kiusalama wake yeye au mtoto wake, au jamaa yao, wasikanyage uwanja huu, …..unaona walivyo wakaidi, ….haya umekaidi, umejileta mwenyewe..labda sio wewe labda ni nguvu ya mizmu imekuleta hapa ili uadhibiwe, mimi sina zaidi ninakukabidhi kwa wazee wao watajua nini la kukufanya…’akasema na kumshika mkono na kumpeleka pale walipokaa wazee..

Yule mzee wanayemuita mwanga, alikuwa kasimama pembeni ya wale wazee, na wakati huo, alikuwa akinguruma kama simba macho yamemtoka, mate yanamtoka kwa uchu, alikuwa akisema `damu , nataka damu yake….damu , nataka damu yake….’

Mama akiwa katoka macho kwa woga, akiwa hana jinsi, kwani alikuwa kama zezeta, kila anachoambiwa anafuata tu, ….mara alipogiswa na kitu kama fimbo, mwili wote ukimlegea na nguvu zikamuishia kabisa, kama vile mwili hauna mifupa, na hapo hapo akadondoka chini,….., kasikia mzee mmoja akisema;

‘Haya mdogo wake mrithi wa familia hii, kazi kwako kuondoa huu mkosi,…maana kaka yako hajarudi, ilitakiwa yeye ndio aianye hii kazi, hata hivyo huku lipokwenda napo kuna umuhimu wake, kwani hatuwezi kumzika merehemu mpaka kisasi chake kifanyike. Sasa wewe unachotakiwa kufanya, ni kuwa uhakikishe ncha ya kisu hiki inalenga kwenye mshipa wa shingo, na damu ikitoka, …..tuachie wenyewe tutajua nini la kufanya…..’sauti ikasema huku watu wakiendelea kuimba, `damu, damu..damu….ya mizimu, daamu iondoe mikosi, …..

Mama alijaribu kuinua mboni za macho aone nini kitafuata, huku akiomba dua zake za mwisho, na kwa mbali akaiona sura ya mume alikuwa kama anamkaribisha, huku kashika mikono yake kifuani. Hapo mama akatamani kumwambia `mume wangu mbona huji kunisaidia, lakini kwa upande mwingine akahisi moyo ukimwambia, `nakuja mume wangu tuishi huko pamoja, mile na milele…

Mara mama akaona ile bakora ikiinuliwa juu, na kitu kama kisu kirefu kikatoka, na ile ncha yake kuelekezwa kwenye mshipa wa damu wa shingo…hata kabla haijagusa mwili wake, akahisi maumivu yakipenya kwenye mishipa ya mwili na hapo akahisi nguvu zikamrejea kiajabu,….akapanua mdomo na kutoa kilio cha yowe, kilio kilichomshitua hata yule aliyeshika ile bakora kama kisu, akatulia, na umati uliojaa pale nao ukatulia, na ghafla, mara sauti ya ving’ora vya magari ya polisi vikatanda hewani….

WAZO LA LEO: Mitihani ya kimaisha ni mingi, nasi kama binadamu kwetu ni mitihani, tusikate tamaa, omba mungu huku unajitahidi, kumbuka kuwa muomba mungu hachoki....

Ni mimi: emu-three

2 comments :

Rachel Siwa said...

Mmmhh ahsante sana Ndugu wa mimi kwa hii shule!Pamoja sana ndugu yangu!

emuthree said...

Nashukuru sana ndugu wa mimi kwa kunipa moyo, maana naandika nikiwa kwenye mazingira magumu(tension), na sijui kama nilichoandika kinakidhi haja, kwanii sina muda wa kukipitia, kutokana na mazingira yenyewe...Lakini tupo pamoja, hapa najipanga kumalizia.
Nawaomba wasomaji watoe mawazo kama kuna mahala tumepasahau,ili kumalizia kukamilishe kila kitu.
Samahanini sana kwa kuwacheleweshea hiki kisa, sio kusidio langu.
Tupo pamoja daima