Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, December 12, 2011

akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli-62 Hitimisho-6



Maua alijikuta akitazama huku na kule akiwa na hamu ya kujua na kuona mengi katika nchi za ugenini, lakini muda huo hawakuwa nao kutokana na kibali chao, ambacho kilikuwa ni cha kumuona mgonjwa kwa siku kadhaa, na hatimaye wanareejea makwao,….

‘Safari nyingine bwana, unakuwa kama mfungwa, yote haya ya nini, eti shangazi,…haturuhusiwi hata kutembea temba kuona mambo ya huku..?’akauliza Maua.

‘Ipo siku utatembea wewe jipange vyema na mumeo, popote unapotaka atakupeleka, huoni kazini anavypandishwa vyeo, sasa hivi ni meneja wa idara yao, mambo mazuri hayataki haraka…’akasema shangazi.

‘Aaah,shangazi unanitibua tena, mimi sijakuuliza mambo ya Maneno, unataka kunitapisha…lakini shangazi umesema baba kakuambia turudi nyumbani harara nanihitaji mimi, na hataki hii safari lakini wewe umeamua kuchukua maamuzi yako, huoni kuwa mtakosana na ndugu yako?’akauliza Maua.

‘Wakati mwingine unapofikia umri kama wakwangu kuna maamuzi unatakiwa uyachukua , na ukiju amaamuzi hayo yanaweza yakawa magumu, lakini ukijua kuwa matokeao yake yatakuwa amzuri na kuondoa kabisa lile pingamizi la mwanzoni,…haya nimeyafanya kwa manufaa ya wengi, wewe mwenyewe usiyehusika kabisa na mambo yao, lakini hata hivyo, sioni kwanini watu waendelee kujenga uadui , wakati wameshakuwa wakubwa na kila mmoja sasa anafamilia yake, sioni sababu, ..wewe utaona tu itakavyo kuwa mwisho wa siku,…’akasema Shangazi mtu.

‘Mimi ninavyomjua baba, mtakosana tu, na sipendi wazazi wangu mgombane kwa kitu ambacho kinaweza kuepukika, kwanini hukumuomba ushauri kabla ya kuamua hii safari…?’ akadadisi Maua.

‘Kama ninefanya hivyo, tusingefika huku, na sizani kama ungelibahatika kujua mambo mengi ambayo kwasasa unastahili uayajue, ungesikia mitaani mambo ya umbeya tu, kama uliwahi kusikia wenzako wakidai kuwa yule sio mama yako unafikiri nini kitafuata baada ya hapo, unaweza hata kutengwa na wenzako wakadai kuwa huna haki na ….mali ya baba yako,’akasema Shangazi huku akimwangalia Maua kwa makini.

‘Mimi wala sihitaji mali hizo za kugombea, kama wataona sistahili, basi, nitatafuta za kwangu, ..’akasema Maua.

‘Achilia mali, ndugu zako wanaweza, ingawaje wewe huna haja ya kuangalia hayo kwasababu unmeolewa na unatarajia kwua na familia yako,…sasa ujue haya nayafanya kwa ajili yako, kwa jaili yenu, na mengine hata baba yako hayajui yalikwaje, kuna mambo mazito….wewe subiri, ila yote tuliyafanya kwa heri tupu…’akasema Shangazi.

‘Hii hoteli inanitia kichefu chefu, kwanini tusiende moja kwa moja kwenye hiyo hospitali, tunasubiri nini..? akauliza Maua.

‘Tunawasubiri wenyeji wetu, hujui kuwa huku tumekuja nchi za watu, pamoja na hilo la kumuona mgonjwa tumakuja kama mualiko wa ndugu yetu mwenye kibali cha kusihi hapa kibiashara..haya ni mambo ya vibali vya kinchi sio kule kwetu unaweza ukawakuta wageni wapo wengi hata vibali hawana, huku wanakufuatilia kuanzia pale tu unapoingia uwanja wa ndege, lakini hayo hayana haja ya kukuumiza kichwa kwa sasa, tutaondoka sasa hivi…kwanza tushuke hapa chini tutatafute nguo za kuvaa’

‘Kwani hizi za kwetu tulizokuja nazo hazifai kuvai , ….kweli nimeona nguo za huku ni maguni marefu na maushungi, unataka tununue kama hizo….hata mimi nazipenda…’akasema Maua, na wakato pale hadi duka moja lililopo hapo chini ya hiyo hoteli.

‘Unapenda nguo gani, kuna haya mavazi wanayopenda kuvaa wenzetu huku India, hili hapa linakufaa unaonaje hili hauni…?’ akasema Shangazi.

‘Shangazi hapana nataka hili, kwanza nililivaa halitaonyesha tumbo langu, na pili rangi yake ya pinki naipenda, ..na tutaoenaka kama watu huku, sio wa kuja, …hili hili shangazi…’akasema Maua huku akilikagua, na wakalichukua hilo, na nguo nyingine baadaye walirudi hotelini kwao na kujiandaa kwa kwenda hospitalini.
Maua alipomaliza kuvaa lile gauni, alijiangalia kwenye kiyoo, na kutabasamu, akasema moyoni, ama kweli nimependeza, nimekuwa kama binti wa Kihindi.

Na mara akaja mtu na kuwaambia taxi ipo nje itakayowapeleka hadi hospitalini, walipokuwa wanatoka wakahisi mtu anawachunguza, hawakumjali wakaingia ndani ta taxi huku Maua akimuuliza shangazi yake huyo mtu anawatakia nini, kwani na huyo mtu alionekana akichukua taxi na kuwafuta kwa nyuma.

‘Hata mimi sijui, …


********

Binti mmoja kiwa kwenye chumba cha hoteli akitoa vitu vyake alivyokuja navyo baaada ya safari ndefu, toka Ulaya, alikikagua chumba alichofikia na kuona kuwa kweli kitamfaa, baadayea aliangalia saa yake na huku akiwaza mengi,…hakutaka kupoteza muda, kwani alichojia hapo ni kumuona huyo mgonjwa na mengine yatafuata kutegemeana na hali ya huyo mgonjwa.

Alifungua mfuko wa nguo yake mpya aliyoinunua, ilikuwa maalumu kwa kwenda kumuona mtu wake aliyemepnda kwa moyo wake, na pia ilikuwa nguo maalumu kwa maeneo ya nchi hii, ikiwa na rangi nzuri anayoipenda ya pink, akaivaa na kujikagua, akasema kimoyomoyo, hii inanifaa sana maana hata tumbo langu litakuwa halionekani…

Aliangalia juu na kushukuru Mungu, kuwa hatimaye amefanikiwa kutimiza lile alilolikusudia , hakutarajia kuwa lingefanikiwa , kwani mtu mwenyewe aliyesumbua moyo wake, akawa tayari kufa kwa ajili yake, mtu ambaye alibadili miono yake ya kuchukia waume,..alitoweka kiajabu na kumuacha hewani, kwani hakujua kabisa wapi atampa.

Siku akiwa katika majonzi kwa kutoweka mtu aliyempenda, ghalfa akaletewa barua, na alipoifungua akaona kuwa yeye ni mmoja wa watu waliochaguliwa kwenda kusoma Ulaya, na safari hiyo ilikuwa imebakia siku chache tu, alishangaa ilikwua wapi, kwani ilionekana ililetwa ni ya siku nyingi.

Hakutaka kupoteza muda, alifanya juhudi zote za vibali na hatimaye akaondoka, huku akiwa hajui hatima ya mtu wake aliyempenda, alichofanya ni kumuachia maagizo jamaa yake mmoja aliyemfaham, kuwa kama itatokea atamuona huyo mtu, amfahamishe haraka, na ikiwezekana akambidhi kwa Inspekta, kwani ndiye mtu aliyemuamini kuwa atamlinda.

Akaingia Ulaya kimasomo, na kujaribu kusahau kabisa mambo ya nyuma, lakini ilikuwa vigumu, kila siku mawazo yake yalikuwa kwa Sweetie wake, na kila mara alijaribu kuwasiliana an jamaa yake huyo kuwa kapata fununu zozote za huyo mtu, lakini hakupata jibu la lolote, ndipo akahisi kuwa huyo jamaa keshatoweka katika maisha yake.

Siku moja ndio akapata taarifa kuwa jamaa yake kaonekana akiwa kalazwa hosptali ya serikali akiwa na hali mbaya, na alihitaji matibabu ya haraka ya upasuaji na upasuaji huo ni mpaka apelekwe India.

Alipopata taarifa hiyo alichanganyikiwa kwani. Hapo alipo hakuwa na hela za kumtosha kumsaidia mgonjwa wake huyo, akaona sasa atafanyaje, akampigia mzazi wake ambaye yupo India kuwa ana mgonwja wake, lakini hana hela za kumtibia, anaomba msaada wao.

‘Kwani huyo mtu ni nani, au ndio huyo mwanaume tuliyesikia kuwa anakusumbua, mtu hajijua, na humjui wapi alipotoka, wewe umeganda kama ruba, ina maana dunia hii hakuna wanaume wengine, kwanini huwi na msimamo kama mimi mama yako, sibabaishwi na wanaume, ungelijua maisha yangu, hadi hatua hii, ungelijifunza mengi, …sasa nikuulize kwanini umemktaa docta Adam, ambaye ni mwanaume mweney sifa, unataka nini tena mwanangu, ’akajibiwa na wazazi wake.

‘Wazazi wangu, sijawaomba ushauri, huyu mtu namfahamu sana mweneywe, nilichotaka kujua kama mtanisaidia au la,…. kama hamtaki kunisadia basi, nitataufa njia nyingine….’akakata simu kwa hasira. Rose na wazazi wake wamekuwa hawasikilizani, na kutokuelewana huku ndiko kulikomfanya Rose aamua kuishi maisha yake mbali na wazazi wake na huwa anakutana nao mara moja moja na kwa jambo muhimu sana,…aliamua kufanya hivyo pale tu alipomalaiza masomo yake na kuanza kufanya kazi, akahama kabisa kwenye nyumba ya familia.

*******

Msuguona wa Rose na wazazi wake ulianza hasa pale aliposalitiwa na wanaume aliofunga nao uchumba, akawa hwasilizi wazazi wake wanapomshauri kuhus mwanaume yoyote aliyetaka kuja kumposa, lakini mama yake hakukata tamaa na ndipo siku moja mama yake akamwambia;

‘Rose kwanini unafanya hivyo, hujui kuwa sisi ni wazazi wako, tunachotaka ni kukusaidia, na mengi tunayokushauri ni kwa ajili ya manufaa yako ya baadaye…’akamwambia mama yake siku moja.

‘Ndio maana sasa nimeamua kujitafutia maisha yangu, ili niweze kutimiza ushauri wenu, siwezi kuwa tegemezi kwenu kwani hili linawakea, …, kazi yenu ya kunilea mumeitimiza, sasa na mimi ni wajibu wangu kuwajibika, …hata hivyo nyie ni watu wa kutembeatembea kwenye mabiashara yenu, sioni haja ya kukaa hapa nyumbani kuwa mlinzi wa nyumba yenu, tafuteni mlinzi awalindie, mimi sitaishi hapa,…’akasema Rose na kweli akatafuta chumba chake cha kupanga, akiwa anafanya akzi serikalini na baadaye alipokutana na Adam, akahama kabisa maeneo ya mjini.

Rose akiwa makitaba, alijaribu kuangalia barua pepe hku akiwa kachanganyikiwa kwa sababu ya simu aliyoipokea kuwa mgonjwa wake kapatikana, na anahitaji matibabu, …na tegemeo lake kwa wazazi halipo, hakutaka kuwanyenyekea , ..lakini hata hivyo hakuwa na njia nyingine, pesa alizokuwa zimemuishia…akawa anasoma baadhi ya barua pepe zake na ndipo akaikuta barua pepe inayomuelekza kuwa kuna pesa zake kaachiwa na Docta Adam, zikiwemo marejesho ya hela alizozitoa mwanzoni kwa ajili ya madeni ya watu aliowadhamini wakaondoka bila kulipa, pesa hizo zilitosha kabisa kuwasaidia watu wasiojiweza.

‘Docta Adam, katoka wapi huyu mtu, na pesa hizi ananitumia mimi kama nani,..’akajiuliza na alipohakikisha kua kweli hizo pesa zipo, sio barua pepe za uwongo, akatoa kibali kuwa pesa hizo zitumike kuwasaidia wagonjwa wasiojiweza na kipaumbele kiwe kwa mgonjwa wake aliyelazwa huko nyumbani kwenye hospitali ya serikali, na kweli hilo likafanyika… na wakati anafuatilia hilo swala la karibu akapokea simu toka kwa wazazi wake kuwa wapo tayari kumsaidia huyo mgonjwa.
‘Nashukuru sana, lakini kwa sasa sihitaji msaada wenu, mgonjwa wangu keshapata njia nyingine, na yupo huko India, tayari kwa upasuaji, kama tukijaliwa tutakutana huko…’akasema Rose, kwa unyenyekevu tofauti na mwanzo mapaka mama yake akamuuliza kuna shida gani nyingine, simu ikakatwa.

Rose alipofika India na kuingia kwenye hoteli yake hakupoteza muda akawapigia madocta wa hospitli anayotibiwa mtu wake, na bahati nzuri, kulikuwa na docta mmoja ambaye alishwahi kutambulishwa na mwanafunzi mmoja aliyekuwa naye huko India, kuwa docta huyo ni bingwa wa upasuaji wamaswala ya kichwa na ubongo. Akampigia simu ambayo ilipokelewa baada ya kuita kwa muda mrefu.

‘Docta nimeshafika nipo moja ya hoteli karibu na hiyo hospitali, nataka kuja kumuona huyo mgonjwa,..naweza kuja sasa hivi…?’akauliza Rose huku akiwa na hamu sana ya kuja kumuona Sweetie mpya,mwenye kumbukumbu zke kamili.

‘Sawa unaweza kuja,lakini utamuona tu, hajazindukana, ila nakupa uhakika kuwa upasuaji umeenda vizuri kabisa lile tatizo tumeshaliondoa, na tunataraji akizindukana hali yake itarudi kama kawaida, iliyobakia ni majaliwa ya mungu, ..unakaribishwa sana docta Rose…nina hamu sana ya kukutana na wewe nimesikia sifa zako toka kwa jamaa yetu aliyekuwa huko masomoni Ulaya..na kama upo tayari naweza kukufanyia mpango ukabakia huku kwetu..tunahitaji sana mtu kama wewe katika hospitali yetu..’akasema huyo Docta bingwa wa upasuaji.

‘Nashukuru sana kama imekuwa hivyo, bado nasoma, nimekuja mara moja kwa ajili ya huyo mgonjwa, …’akasema Rose na kukata simu, hakutaka maneno mengi.

**********

Rose alijitahidi sana kusoma na huku akijaribu kuondokana na mawazo ya nyumbani, hata hivyo akili yake ilishindwa kabisa kumsahau Sweetie wake,alikuwa akiwaza majaliwa yake na hasa baada ya kutoweka kiajabu hata kabla hajamfahamu vyema . Siku hiyo baada ya mitahani, alijikuta akimuwaza Sweetie wake, je ni nani, na alitokea wapi, kwani majibu hayo alikuwa akiyasubiri sana, ..alijuta kutokumdadisi mapema pale alipomuona kaanza kupatwa na fahamu kidogo, akichelea kumharakisha na huenda …sasa ndio huyo kaondoka, na huku kamuachia zawadi ambayo….oh na kushika tumbo, na muda huo akaanza kujiskia vibaya, kizungu zungu kikamuandama, na wakati anajaribu kuingia chumbani mwake, akadondoka mlangoni na kupoteza fahamu.

Alipozindukana alijikuta yupo hospilini, na docta aliyekuja kumtibia alimpa taarifa ambayo haikuwa ngeni kwake, lakini hakutaka kabisa mtu mwingine aijue hiyo hali, ingawae alijua badaye itakuwa haina siri tena, hata hivyo kama itabidi atatafuta kazi mbali na kwao, .
Siku hiyo alipata matibabu na kurejea chumbani kwake akijipa moyo wa kuendeela na msomo yake. Alipofika chumbani kwake na kujilaza kitandani, akajikuta badala ya kulala, akawa anaandamwa na kmbukumbu za nyuma, alikumbuka siku ile alipoamuka ghafla na kujikuta kazungukwa na maaskari,…siku ile aliiona kama siku iliyoanza kumpa upweke akilini.

Siku alipoamuka alijikuta kazungukwa na maaskari, mwanzono hakuelewa kabisa ni hawo maaskari wametokea wapi, kwanza alijua huenda ni wale wapiganaji wa msituni wamekuja kumvamia, lakini akili yake lipokaa sawa, akakumbuka ni nini kilichokuwa kikiendeela, akajiinua na kuwatizama, akisubiri nini kitafuata baadaye.

Akainuka haraka kutaka na kutizama huku na kule huku akilini akijiuliza ni wapi wamempeleka Sweetie wake, kawani alikuwa haonekani pale alipokuwa amelala, alipoona hivyo akatamani kukimbia, lakini mara akamuona Inspekta na mkuu wa ulinzi wa hiyo hoteli, moyo wake ukaingiwa na matumaini, lakini cha kwanza alichotaka kuulizia ni kuhusu mgonjwa wake kaenda wapi, kwani kila alipogeuza kichwa kila upande hakumuona, na hata kabla hajawhi kuuliza hilo swali akawahiwa kuulizwa yeye, ….akabakia kusngaa, kwani hakujua nini kilitokea baada ya kupitiwa na usingizi mzito, kwani alijitahidi kuwa macho muda mwingi, akimuhudumia, lakini ucomvu ukamshika na kutekwa na usingizi...

‘Sasa atakuwa kaenda wapi, au ndio kaingia mikononi mwa hawo jamaa…?’ akauliza mkuu wa usalama wa hiyo hoteli.

‘Sizani kuwa kakamatwa na hawa watu, atakuwa kaamuka na aliposikia milio ya bunduki, akajificha mahali, hebu tuanza kumtafuta mara moja…’Amri ikatolewa, na baada ya msako mwingi bila mafanikio ikabidi waangalia mitambo yao ya usalama ,inayoratibu mizunguko ya humo ndani, lakini hilo lilifanyika baada ya operesheni maalumu ya kupambana na kundi gaidi lililokuwa limejikita humo ndani kumalizika, ilikuwa kazi kubwa mwanzoni, kwani ilibidi kupambana na watu wenye silaha, ambazo hazikujulikana zimepatikana wapi, lakini hata hivyo waliobahatika kuwa na silaha walikuwa ni wachache, kwahiyo zoezi likaisha haraka, licha ya upinzani wa hali juu, ….

‘Maua wewe ndiye unayetafutwa sana, mwenzako haonekani, kwahiyo bado tutakuweka kama chambo ili tuweze kuwakamata wote wanahusika, inasadikiwa kuwa bado hawa jamaa wapo wengi, na kwa kupitia kwa hawo tuliowakamata, tutaweza kuwanasa wote, wapo ambao wameshakubali kushirikiana na sisi, na wanawajua wengi wa kundi hili, na hawa waliokubali ni vijana wetu wenyewe..’akasema Insepkta.

‘ Hata hivyo tunakuhakikishia kuwa tupo pamoja na wewe, tutahakikisha kuwa hawakufanyi lolote, wewe fuata maagizo yetu tu, nia yao sio kukuua, hilo tuna uhakika, ila mwenzako walizamiria kabisa kumuua,…’akaendeela kumuelezea yule Inspekta ambaye tangu mwanzo alishamuelezea hilo jukumu na sasa akamuelekeza jinsi gani ya kufanya.

‘Sawa mimi sijali tena lolote likitokea la kutokea sitojali tena, kama mgonjwa wangu katoweka na huenda wamemuua, basi hata mimi wakiniua sitojali sana, niambieni nifanye nini…’akasema Rose akiwa kakata tama kabisa.

‘Usikate tamaa kiasi hicho na sio nia yetu kuwa wakuue, hapana ila tunataka wajitokeze pale watakapokuona, tunajua lengo lao kubwa ni kukupata wewe, na mwenzako, ..’akasema Insepkta na baadaye wakamalizia masalio ya watu ambao walikuwa humo na wengi walikubali kukamatwa bila kuleta upizani, wale waliokuwa wapinzani ni kikundi cha mwanzo ambacho kilikuwa na silaha, na walipoona mambo yametulia wakaingia chumba cha mitambo ya kuangalia mizunguko ya watu na ndipo wakagundua jinsi gani huyo mgonjwa alivyotoka humo hotelini.

‘Huyu jamaa mimi simwamini, hebu angalia jinsi alivyotoroka humu hotelini, …licha ya kuwa anaonekana ana wasi wasi, lakini mbinu alizotumia hadi kutoka humu hotelini bila kuonekana, anaonyesha anahusiana na hawa watu, mimi naona tumtafute , akipatikana atatusaidia , na sizanikwamba kaenda mbali….’akasema askari mmoja ambaye alikuwa mmoja wa viongozi wa mapambano na wakaanza kumtafuta kila mhali walipozania kuwa huenda yupo bila mafanikio.

‘Mimi siwezi kukubalina na hilo kuwa huyu jamaa ana mahusiano na hawa watu, hebu muangalieni vyema, jinsi alivyoonekana, hata hapa kwenye hii mitambo anaonekana kabisa hana dalili ya uaskari, hapa alibahatisha tu, kafanikiwa kutoka bila kuonekana …kwanza anaonyesha kuchanganyikiwa, ila cha ajabu kwanini alipoamuka tu hakutaka kumwangalia mke wake, mbio mbio kaavaa, na kuondoka hata bila kuangalia nyuma….

Tutamtafute kwanza akipatika atatuambia yote, maana huyu mtu hajulikani kabisa katokea wapi, maana sizani kuwa katokea maeneo ya hapa kwetu, nahisi sio mtu wan nchi hii, ni mamluki huyu, aheri huyu binti ni mtu wa hapa, kwahiyo hana uchungu sana na binti yetu huyu, huoni alipoamuka tu, hakutizama pembeni, yeye na malengo yake, kajiandaa na kuondoka, kazi keshamaliza, tumpate akiwa hai au la, huyu mtu anaonekana ni hatari sana, kama ameweza kuishi nasi hata bila ya kumgundua kuwa ni mtu wa namna gani , ….\akasema askari

‘Tusikimbilie kumhisi vibaya, ngoja kwanza apatikane, sizani kwamba atakuwa kaenda mbali, tukimkamta tutajua yote, lakini mimi bado sijaamini kuwa ni mmoja wa hawo watu, hana dalili hiyo kabisa, wapiganaji wote tunawajua, hata akitembea…’akasema askari mwingine.

‘Hapana hawa wa sasa hivi ni tofauti, na sikuamini kuwa ni maaskari haramia, watu wapo maofisini, wanahudumia jamii, kumbe wana malengo tofauti,…siumewaona mweneywe, maana kama ulivyowaona ni watu wa maofisini, mchana wapo maofisini, usiku wanaingia kwenye kazi nyingine…ni hatari sana hawa watu, maana ni ndumila kuwili. Yaani sasa unashindwa wa kumwamini,…mwishowe tutakwua tukiuana wenyewe kwa wenyewe bila ushahidi…

‘Mimi nina imani haya yatakwisha kwasababu haya yote yametokea kwasababu ya kukosa uadilifu katika uongozi, haki haitolewei sawa, kama kila mtu angelipata haki yake isingefikia hapa, jambo la muhimu ni demokrasia ya kweli, wawepo viongozi wliokubaliwa na watu, waadilifu, wenye dhamana na wanajua kuwa dhamani hiyo ni deni kwao,…sijui kama tutawapata watu kama hawa, maana wengi wao malengo ya ni matumbo yao, wao na familia zao,..’akasema askari mwingine na wenzake wakamwangalia kwa mashaka.

Ndio tatizo hilo, mtu hawi na uhuru wa kusema ukweli, tunaogopa,…hatutafika namna hiyo, usimuogope mtu uliyemuajiri, wewe , mimi , sisi wapiga kura ndio tuliowaajiri viongozi wetu tuliowapigia kura, leo hii tunawaogopa…hatari kabisa` akaendelea kuongea yule askari.

‘Tatizo lako wewe umekuwa mwanasiasa, hiyo sio kazi yako, kazi yako ni kuwajibika jinsi utakavyoamriwa na viongozi wako watawala…’akasema askari mwingine.

‘Hata kama sio mwadilifu, hiyo haipo, lazima uchuje…ndio maana sisi tuna idara zilizokamilika, …jeshi kama jeshi sio bendera fuata upepo, labda tuwe na viongoz mbumbumbu, lakini kama ni wasomi wa kweli, hakuna nchi ingeliharibika…hilo nawahakikishia, maana huwezi kufuata kufua amri tu, bila kuzichuja, bila kuwahoji watoaji na kuwashauri…na ndio maana nchi nyingi kunakuwa na ampigano yasiyo na mingi,..ipo siku mtaelewa maneno yangu…’akasema yula askari na kusogea pembeni.

‘Huyu jamaa mnamuonaje, asije akawa katumwa…’akahoji askari mwingine akimnong’oneza mwenzake.

‘Huyu namfahamu nimesoma naye, zake ndio hizo, na sasa anasomea uongozi, akipata uongozi huyo jamaa, jeshi litabadilika namwaminia sana…’akasema askari mmojawapo.

Mara wakasikia amri kuwa kazi imekwisha na wanatakiwa kurejea kambini kwao, na ni wakati huo Rose naye analetewa barua ya kwenda kusoma nje, …na wakati anaisoma, akaja Inspekta na kumuuliza akiwa na furaha usoni akasema.

‘Rose kwa niaba ya serikali hii tunakushuru sana kwa kujitolea kwako, najua ni wajibu wako kuilinda nchi yako, na hilo ni jukumu la kila raia hasa kipindi cha vita, …taarifa yako imeshapelekwa ngazi za juu, na najua watakufikiria, usijali kuwa umepoteza kazi kwa Docta .

‘Unajua huyuu Docta Adam, nilishamshuku vibaya, hata ile safari ya kwenda kumuona, ilikuwa ni njia ya kumsadia achane na mambo hayo, lakini hakukubali kuwa yupo kundini, na pili inavyonekana hawa watu wamekula yamini ya hali ya juu. Hata hivyo nilivyomuoa, nina imani kuwa kama atawekwa vizuri, akili yake itarejea kweye msimamo anaonekana ni mtu mwema, …kama akipatikana hai, maana hawa watu hawaaminiki, wanaweza hata kuuana wenyewe kwa wenyewe, wakigundua kuwa umewasaliti.

‘Swali moja kwako Rose, wewe unasadikiwa ndiye uliyekuwa rafiki yake mkubwa, ingawaje umesema kuwa urafiki wenu uliishia kwenye maswala ya kazi, nakuamini Rose, lakini hauna chochote kinachoweza kutusaidia kumpata huyu mtu…?’ akauliza Inspekta.

‘Mimi siwafichi, kama ningelijua ningewaambia kila kitu, lakini huyu bwana, alichokuwa kanipendea ni katika kazi na utendaji wangu wa kazi. Ndio mwanzaoni hata mimi ilitokea kumpenda lakini sio kimapenzi, nilimpendea jinsi alivyokuwa akijituma, na nikajitolea kumsadiai katika matatizo yake na mkewe, toka hapo akaniona namfaa, …lakini sivyo ilivyokuwa matarajio yangu…kamwe, sio kihivyo alivyotaka yeye..’akasema Maua akitikisa kichwa.

‘Kwani yeye aliatakaje, na kwanini akutafute sana, au kwanini unahisi hilo kundi linakutafuta wewe na mwenzako..?’akauliza Inspekta.
‘Huyu hanitafuti kwa linguine lolote, zaidi ya wivu wa kimapenzi…tangu aliponitaka kimpanzi nikamkataa, imekuwa ndio hivyo, na hata chuki kwa huyo mgonjwa wangu , …mmh,mume wangu, ilikuwa ni sababu hiyo, anahisi akimuaa hatakuwa na kipingamizi …na alijaribu mara nyingi kufanya hivyo, na hatua ya mwisho alijua kafanikiwa, namshukuru sana dakitari aliyemuokoa …’akasema Rose.

‘Kwanini hasa ukakosana na wazazi wako,…maana wao nimatajiri, sioni kwanini usiwe unaishi katika majumba yao, …unaishi nyumba za kupanga, hili pia linatia wasiwasi, kuwa huenda tabia yako haikubaliki kwa wazazi wako, au unajihusisha na makundi yasiyofaa, maana wazazi wako ni watu wanheshimika serikalini, wamechunguzwa, na hawan doa …hebu niambie kwanini ukosane nao..?’akauliza Inspekta.

‘Licha ya mambo mengine ambayo ni ya kawaida ya kukosana kati ya mazazi na mtoto wake hasa akiwa binti, lakini alyechangia kiasi kikubwa baada ya kusalitiwa na yule mwanaume ..ni huyu Adam..aliongea Rose kwa sauti ya hasira

Inspekta akamwangalia kwa makini na hapo ndipo alipojua kuwa kweli huyu binti hahusiki na kundi la huyo Adam, hasira kama ile angelitoa kila kitu anachokijua kuhusu Adam, akawa anamsikiliza, huku akiwa namwangalia jinsi anavyoongea, kwani Inspekta huyu ana utaalamu wa kumsoma mtu anapoongea na mara moja anaweza kujua kuwa ulichosema ni cha ukweli au uwongo kutokana na kauli ya mtu na hisia anazozionyesha usoni.

`Adam alifanya nikosane na wazazi wangu, kwani alifika hadi huko walipo wazazi wangu, wao hawakai sana hapa nchini, wana miradi yao huko India na sehemu nyingine nisizozijua, alikutana nao akawarubuni kwa maneno matamu, na kwa vile na yeye anazo pesa nyingi, basi wazazi wangu.., wakamuona ananifaa, lakini sikuwa tayari kwa hilo,…wakanipa masharti magumu, nikaona hawa sasa wamevuka mpaka nikaamua kuishi maisha yangu ya peke yangu. Kipindi kile nilikuwa katik wakati mgumu kwani nishafika sehemu siwaamini wanaume tena, baada yakusalitiwa,…’ akasema Rose.

‘Bado sijakuelewa hapo, kama kweli uliwachukia wanaume, je utasemaje kuhusu huyu mwanaume ambaye kila mtu anajua kuwa ni mume wako,kama ulivyoandikisha kila mahali, ilikuwaje akawa tofauti na wanaume wengine…?’akauliza Inspekta.

Rose alitulia kwa muda, akawa anawaza, maana hata yeye bado alikwua akijiuliza hilo swali, kwanini huyu awe tofauti na wanaume wengine,..mwishowe akasema `Ninakiri kuwa huyu mgonjwa aliyetoroka ndiye peke yake aliyenigusa moyo wangu kinamna ambayo siwezi kuelezea,…’ akatulia huku moyoni akiongezea kusema, na ni kweli amekuwa tofauti na wanume wengine..na sijui kama nikimkosa yeye nitajihangaisha na wanaume wengine,..sijui, ya mungu mengi.akamwangalia Inspecta kwa makini, akiwa anatafakari maneno yake, na baadaye akaangalia juu.

Inspekta naye alimwangalia kwa makini huyu binti akahisi licha ya hayo kuna jambo jingine ambalo huenda linamtatiza, huenda ni maswala ya mahusiano, au hayo ya kifamilia, lakini hilo hakulipa uzito sana. Akaweka nadhiri moyoni kuwa hayo mambo yakiisha salama atajitahidi kumsaidia huyu binti, vile awezavyo, huenda anaweza akacheza kama mzazi, na kumsaidia awezavyo, lakini je atakubali kwenda kufanyakazi kwao, Tanzania.

Aliwaza kwa muda bila kusema kitu, na baadaye akaona ayaamini maneno ya Rose, kuwa huenda hahusiki na hilo kundi, licha ya wenzake kung’ang’ania hivyo mwishowe akasema;

‘Sasa Rose wakati napeleka taarifa zako serikalini nikagundua kua kulikuwa na barua yako ya kwenda kusoma nje, barua hii ilikubaliwa siku nyingi sana, na hata hicho chuo kilishakubali kukuchukua, cha jabu barua hiyo iliyoonekana serikalini ni nakala tu, barua halisi ulishatumwa kwako, sijui kulitokea nini, …’akasema Inspekta.

‘Najua sana kuwa kulikuwa na jambo linaendeela hapo kati, maana nilikuwa na vigezo vyote vya kwenda kusoma nje, …wamenileta hiyo nakala leo, na nitajitahidi kwenda kusoma, sijachelewa..’akasema Rose.

‘Hilo nakuunga mkono, kwani zimebakia siku chache za kuondoka, unaweza ukawahi, mengine tuachie wenyewe, …kamani kuhusu jamaa yako tukimpata nitahakikisha kuwa anakuwa katika mikono ya salama, lakini kama sio miongoni mwa hilo kundi la hawa magaidi…’akasema Inspekta.

Rose apofika hapo kimawazo akatabasamu, akajiangalia kwenye kiyoo, moyoni akasema sasa nimekuwa binti mrembo wa Kihindi….akatabasamu na kujiandaa kutoka nje, tayari kwa kuondoka kuelekea hospitalini na alipofungua mlango, akakutana na mtu ambaye alimuashiria kuwa audi ndani, huku akionyesha bastola aliyojificha kwenye koti.

‘Wewe ni nani na unataka nini kwangu..?’akauliza Rose huku akiwa kaingiwa na woga.

‘Hilo utalijua hilo baadaye…twende ndani haraka kama hutaki kuzurika…’akasema yule mtu , ambaye alipofika ndani, aligeukia upande mwingine kama vila anaficha uso wake na akawa anafanya jambo fulani kwenye uso wake, huku akiwa kageukia upende mwingine kiasi ambacho Rose hakuweza kuona kinachofanyika, na hata hakujali kwani aliona huyo mtu anampotezea wakati wake na kwanini amuonyeshee bastola, labda ni majambazi wa nchi hii, akakumbuka visa vinavyotangazwa kwenye runinga kuhusu magaidi..

Rose akaangalia saa yake, na kuguna na kabla hajasema kitu akainua uso wake kumwangalia yule jamaa, kabadilika..ooh,... akashikwa na butwaa, hakuamini macho yake, akabakia kutetemeka miguuni, lakini akajitahidi kujificha,...simuogopi, ni hii hali tu, hali kama hii imekuwa ikimtokea sana, alishajua ni kwasababu gani…akajipa moyo, …alichofanya nikujiegemeza kwenye ukuta asije akadondoka…akahisi kichefuchefu...!


Ni mimi: emu-three

2 comments :

Anonymous said...

Kimia kimia mwendo wa kibongo-shukuran mkuu ubarikiwe kwa kutujali

AMMY K said...

daah sikumbuki kusoma hadithi tamu kama hii em3. daah unatisha kwa utungaji. kila la kheri