Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha
Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..
Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.
MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.
TUPO PAMOJA DAIMA
Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;
https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:
https://www.facebook.com/diaryyangu/
`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;
Friday, November 18, 2011
Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli-51
Maandalizi ya harusi yalipamba moto, vikao vya hapa na pale vikafanyika, na siku hiyo Maneno alitembelewa na mmoja wa dada zake, nia kubwa ni kutaka kujua mambo fulani fulani, kabla ya siku yenyewe, maana sherehe hasa ya harusi ni akina mama, huwezi kuwaambia, kitu.
‘Kaka hayo mambo yako ya kutaka sherehe fupi, sijui hutaki hiki, …nimesikia kuwa hutaki rusha roho, wewe, sitaki kusikia hilo, ukumbuke kwenye familia yetu wewe ndiwe kaka pakee, sasa nitapata wapi mwanya wa kujirusha kama sio kwako, nakuomba hayo mambo ya sherehe tuachie sisi dada zako, wewe jiangalie uvaaji wako na wapambe wako, lakini mambo ya shughuli, hayo hayakuhusu….’akasema dada mtu.
‘Tatizo nyie mnaongea tu, mwisho wa siku bajeti ikibana mnanitupia madeni, sipendi nikiwa ndani na mtu wangu kuambiwa hili halijalipwa , hili halikuwepo kwenye bajeti, nataka kila kitu kiende kimpangilio, najua mnataka mengi, kujirusha, sijui na nini, lakini mjue kuna maisha yanaendelea, sherehe ya siku mbili, isiharibu mpangilio wa maisha mengine…’akasema Maneno.
‘Hilo nalijua sana, kwani rusha roho, na mambo fulani, unafikiri yanahitaji mshiko mkubwa hakuna kitu kama hicho, huko tumeshajipanga, wala hatutagusa bajeti yako, kuna mambo ya kigodoro, hayo ni kwa jili yetu, wazazi na walezi wako , unajua tena, hayo ni mambo ya kijamiii huwezi kuyakwepa, …nafikiri tumeelewana…’akasema dada mtu akisimama kuondoka.
‘Sawa, kama ni hivyo sina neno, hapa nawasubiri wapambe wangu kuna kikao kidogo cha kuweka mambo sawa, na vikao vyenu vinaendeleaje?’ akauliza Maneno.
‘Hilo halikuhusu kaka, nimeshakuambia, ondoa shinikizo, usipungue uzito kabisa, hayo ni mambo yetu, wewe kaa pembeni, kazi yako ni kumchora wifi tu, jinsi gani mtakavyolicheza sebene siku ya fungate lenu…’akasema dada mtu , na Maneno akaishia kucheka, kwani wakikutana na dada zake hawa hutaamini kuwa ni kaka na dada, wanataniana kama mtu na binamu yake.
Dada mtu alianza kuondoka na kabla hajafika mlangoni akarudi ghafla na kumkaribia kaka yake na hapo aliongea kwa sauti ndogo;
‘Kaka lakini mumepima, …siunajua tena mambo fulani fulani, halafu unajua siku hizi mambo hayaeleweki,…mara HIV, mara `sikoseli,’ sijui vitu gani,…wewe wajua zaidi, lakini unaweza ukajisahau kwa hilo….?’akauliza huku kamuinamia kaka yake.
‘Dada hayo mambo geni tena, ..tatizo lako unafikiri mimi ni mtu wa kuja, hilo la kupima lilishafanyika siku nyingi, …,tulishapima, na kuonekana sote tupo safi, hata viasilia vya kujua mtoto akizaliwa asije akawa na athari za kurithi, hayo yote tumeyaangalia, hilo lisikutie shaka, tena tumepima mara mbili…’akasema Maneno.
‘Mhh, nakuaminia kaka, wewe ni msomi wa kweli, ….kwahiyo swala la miwaya hatuna wasiwasi nalo, lakini kuna mambo mengine …’akamsogelea kaka yake na kumshika begani , halafu akasita kuongea kile alichotka kukisema, ..baadaye akasema , `Huyo binti namfahamu vyema, mpole na mtaratibu, lakini huwezi jua, isije siku mbili tatu, tumbo hilo…utatuambia vyema, hiyo mimba imetunga saa ngapi kama sio kabla ya ndoa…..au uniambie ukwelia kama mumeshapiamana kinamna nyingine pia, kabla ya ndoa, maana mambo ya siku hizi ni kupimana kwanza, nataka kujua hilo mapema…mimi ni dada yako, aibu ikiibuka mimi ndiye mnyoshewa kidole, una uhakika yupo safi, hana kitu….’akashika tumboni, huku anacheka.
‘Hata kama ana kitu lazima kitakuwa changu, …kwani wewe inakuhusu nini, na kwanini umuhisi hivyo, …ushamuona mhuni sana au vipi…kwanza hebu fikiria, mumewe alitoweka lini, miaka sasa miwili, na hana mtu mwingine zaidi yangu, …sasa , kwanini nitie wasiwasi..’akasema Maneno akitabasamu.
‘Na wewe kaka kweli umo, yaani binti wa watu anaomboleza kwa kufiwa na mume wake, wewe hukujivunga,…hongera kaka, ila nilitaka niwe na uhakika nalo, maana sisi wanawake ni wasiri wa kubwa, unaweza ukawa na kitu, na huyo aliyekubebesha humtaki na umepata chombo chenye nafasi, unafikiri utafanya nini, unambambikia mwenye nafasi…mjini hapa! Kaka nakwambia hapa mjini,….unajua baada ya kujifungua ikionekaan sura sio sawa na mwanaume tunafanyaje tunadai mtoto kafanana na mjomba wa babu wa bibi mzaa baba mdogo..hahaha weya, shaurilo…’akapiga vigelele huku anaondoka.
‘Wanawake bwana, hayo yote ya nini…mimi nimeshafanikiwa kukichukua chombo, sasa wanaanza kuleta majunguyao, wao wanajua nini, wangelijua kuwa hicho chombo, nilikuwa nakiota, nakitamani kwa siku nyingi, ahsante sana Mungu, ahsante sana rafiki yangu kwa kunikabidhi huyu mwanadada, ….oooh, mungu anipe nini tena, hata kama …..lakini mmmh’akaguna na kuwaza, akikumbuak tukio lile la siku ile pale alipokwenda kwenye ile hospitali na shangazi yake , ambapo shsngazi alidai huwa wanakwenda mara kwa mara kuchunguza afya zao. Kwa ujumla waanmjua sana yule dakitari, ni mataalmu wa mambo ya akina mama, lakini kuna shutuma kuwa huyo dakiatari ana mambo mengine ya ziada.
‘Lakini kwa Maua haiwezekani , …’akakumbuka jambo, ambalo aliliona alifanyie kazi baada ya hicho kikao chake na washikaji zake, `Nitamtembeela yule docta, najua nikimpa chochote ataniambia kwanini Maua alifika hapo hospitlini, lazima kuna jambo limejificha hapo, ngoja, kikao kiishe. Ngoja, lazima namimi niwahakikishie kuwa naitwa Maneno, sio wa maneno tu bali na vitendo….’akasimama kwa hamasa.
‘Lakini kama nikigundua kuna jambo baya, …’ akaikuna kichwa, halafu akajiuliza mwenyewe `Jambo baya kama lipi,…’ akajishika kidevu akitafakari, `Kwanza ile hospitali ina sifa mbaya, yule docta ana mambo ya chini kwa chini, nasikia anatoa mimba, sasa kwa mfano, …nagundua kuwa Maua likwenda kutoa mimba..nasema kwa mfano, najua Maua hawezi kufanya jambo kama hilo, ila kwa mfano…’ akasimama na kuchungulia chini kwa muda.
‘Mungu wangu kama ikiwa ni hivyo, mungu wangu, nitaua mtu…..hapo wataniona kuwa sio Maneno yule wanayemjua,sitjali cha shangazi au nani….’akakaa kwenye sofa akitizama juu, akasimama tena huku akiwaza huku anaongea kama vile anaongea na mtu pembeni yake, `Lakini kwa mfano, …tuchukulie Maua ana mimba, …hiyo itakuwa ya kwangu, …ingawaje sizani kama anayo, ni kwa mfano tu …..sasa kama ni ya kwangu, kwanini aitoe,….aaah, hana mimba yule, kwanza aitoe wapi hiyo mimba….hapana, hana kabisa,..yule namuamini sana, …hata haivyo nilishawahi kumuliza siku ile alipojaribu kula chakula na kuanza kujisikia vibaya..akabisha kabisa….maana pale nilishamuhisi kuwa anayo….alibisha’Maneno akawa anaonge peke yake utafikiri kuna mtu mwingine humo ndani , na hapo akikumbuka tukio la siku ile, alipomshuku Maua ……
Aliikumbuka sana ile siku alipotoka kazini muda wa mchana, kwa nia ya kumpitia Maua wakapate chakuala cha mchana pamoja, alitoka kazini mapema, akampitia Maua kumuomba kuwa leo kaamua wakale pamoja hotelini, na Maua akakubali, walipofika kweney hoteli, chakula kikaletwa mezani, ile Maua kikionja tu, akasimama ghafla na kukimbilia chumba cha kunawia. Huko alikaa muda kidogo na aliporudi macho yalikuwa mekundu kama vile mtu aliyekwua akilia.
‘Vipi unajisikia vibaya nini…?’akauliza Maneno.
‘Hapana, sijui nimetafuna kitu gani, maana ile nasikia harufu kinywani, moyo ukatibuka, yaani nimesafisha kila kitu kilichukua ndani, sasa nitakula kwa raha…’akasema Maua.
‘Lakini Maua upo safi kweli ….maana huko kujisikia vibaya nimekusikia mara nyingi, mara moyo kutibuka, tuambiane ukweli…?’ Maneno akazumngumza kwa kufanya utani.
‘Wewe…, una maana gani kusema hivyo, maana mume wangu kaondoka karibu miaka miwili sasa, na simjui mtu mwingine, hiyo shutuma inatoka wapi…au unataka kusema nini…?’ Maua akazungumza kwa hasira.
‘Sina maana mbaya Maua, uwa waridi wa moyo wangu, …lakini kwani mimi siwezi kubadilisha hali yako, unakumbuka siku ile kule Arusha, …inawezekana ikawa ndio sababu, mmh lakini…, samahani sio kwamba nazungumza kukumbushia hilo kwa kulifurahia lile tukio hapana….ila..’Maneno aliogopa alipomuona Maua kabadilika ghafla na sura ilijaa chuki, kuonyesha kukerwa na hayo maneno.
‘Maneno naona umetibua kila kitu, na hata chakula chenyewe kimeniishia hamu, mambo gani unayaongea hayo, unafikiri mimi nilifurahia hilo tukio, kama kuna tukio lililo niumiza katika maisha yangu baada ya kuondoka mume wangu, mojawapo kubwa ni hilo, tukio hilo naliona kama chanzo cha kuharibikiwa na mpangilio wa kaili yangu. Tafadhali kama unapenda tule hiki chakula vyema, basi usiongelee kabisa tukio lile, silipendi kulisikia…’akasema Maua kwa hasira.
‘Maua siku hizi unapendeza kweli, maana hayo siju ndio mafuta au vipodozi unavyovipaka vinazidi kukuremebsha na kuwa mweupe, utafikiri mzungu, mmmh, Maua kama kuna kitu nilichojaliwa nacho na amabacho nitakifurahia, na nimeshakifurahia ni kukupata wewe, naomba siku hiyo ifike haraka tufunge ndoa,…namuomba mungu atupe subira njema, na baraka zake ifike hiyo siku tutangazwe kuwa sasa nyie ni mke na mume…’akasema Maneno kubadili hali ya hewa.
‘Mungu ni mwema, …hilo ndilo jambo la kuomba, ….
Maneno akasimama na kuangalia saa yake baada ya ile kumbukumbu kutoweka kichwani, aliona jamaa zake wakichelewa, kwani hawo ndio washikaji wake wakuu , anawategemea kufanikisha shusguli yake, na kabla hajasogeza mguu , mlango ukagongwa, na akainuka haraka akijua kuwa wageni wake aliowategemea wameshafika, …akafika mlangoni, na kufunguo mlango, moyo ukamlipuka kwa mshituko, akabakia mdomo wazi….
******
Shangazi alipofika kwa Maua alijaribu kukaa na kuongea naye vyema, alimdadisi kwa undani nini wamekigundua huko hospitalini, lakini Maua alisema hakuna, alikataa kata kata kuwa alikwenda kule kwa nia gani, …
‘Maua mimi nakujua sana kuliko unavyojijua wewe, nina uhakika ulikwenda pale kwa nia ya kutoa mimba…kwanini unataka kuniabisha , kwanini mwanangu, ….?’akauliza shsngzai mtu kwa hasira.
‘Wewe shangazi kwanini kama ulijua hukuniambia mpema, mimi nilijua ni hali yangu ile ile niliyokuwa nayo hata alipokuwepo mume wangu, kwahiyo sikuwa na wasiwasi na hilo, …lakini aliponiambia kuwa nina ….oooh sikuamini,…sijui kwanini imetokea hivi, kwanini mimi niingie kweney aibu hii kubwa…sasa shangazi nitafanyaje, nitamwambiaje huyu mwanaume…? Maua akaanza kulia.
‘Maua ndio maana sikutaka uliue hili, nilitaka ulijue hili baada ya kufunga ndoa, maana pupa zako zinaweza zikaharibu kila kitu, sasa sikiliza, hili swala sitaki uliseme kwa yoyote yule, sitaki kabisa kusikia kuwa umemwambia Maneno, swala hilo nitaliongea mwenyewe kwa Maneno, yule nimeshamuweka mkononi, kwanza nilishamtishia kuwa kakuharibu kinyume na maadili yetu ya familia...’akasema Shangazi na kumsogelea binti yake, akamlaza mapajani mwake.
‘Sikiliza Maua hayo niachie mimi, usiseme lolote, unanisikia vyema, na wala usiongeee sana na watu, kuanzia leo utakuwa hutoki ndani, mimi na wewe tu ndio tutakwua tunakutana, hadi siku hiyo ya ndoa, na nitahakikisha inafungwa haraka iwezekanavyo, ili mambo yasije yakajionyesha mapema, nashukuru kuwa mwili wako umeongezeka, na kwahiyo sio rahisi mtu kugundua lolote, kilichabakia ni wewe kujihami….na hilo litawezekana kama utajituliza ndani…unanielewa ?’ akasema Shangazi mtu.
‘Kwanini tufanye hivyo, kwaninitusimwambie Maneno tukaahirisha hii ndoa hadi nijifungue, ndivyo ilivyo kiimani,…huoni tutafanya mambo kinyume na maadili ya kiimani…’akasema Maua.
‘Wengi siku hizi wanaona wakiwa wameshaharibu, harusu nyingi ninazozishuhudia mabinti wengi wana mimba, hata nyingine zinaonekana wazi, sembuse yako, ambayo haijionyeshi kabisa , nakuomabi hilo niachie mimi, …kwanza huyo huyo ndiye aliyekuaribia, atasema nini….akisema nyoko, nitamweka ndani, unanichezea mimi,…kwanza leo nakwenda kwake , huko nitajua nini cha kumwambia, usijali, nakuomba ukae kwa amani, ila kama nilivyokuambia usitoke kabisa humu ndani, ngoja nikapambane na huyo kidume mtu, sikiea anasema nini…’akasema shangazi huku akiondoka.
Njiani alijawa na mawazo mengi, kwani hali ilivyo sasa imekuwa tete, kinyume na mipangilio yake, alikuwa na wasiwasi je kama harusu hiyo ikaahirishwa, na je kama Maneno ataamua kwenda kuonana na huyo dakitari aliyempima Maua na kupewa chochote ili aongee, atashindwa kweli kumwambia ukweli Maneno…akajikuta akibeba mzigo mkubwa wa mawazo, hasa akifikiri wazazi wa Maua ambao wanatarajia kufika karibuni.
‘Ili kuwaweka sawa hawa wazee wanzangu, nitahakikisha ninakaa nao kwangu, na sitawapa muda mwingi wa kukutana na Maua , huyu binti nitamfunda mwenyewe nyumbani kwake, hakuna mtu wa kumuona ona, na nitahakikisha kuwa wazazi wake hawalijui lolote kuhus hilo, …baada ya ndoa kupita, sitajali sana wakijua,….mimi ni shangazi wa kikweli,…’akajipiga kifua kwa kutamba, halafu akaangalia nje gari liliposimama na kusema `Kwanza ngoja nikahakikishe huyu anayejifanya ndiye kidume wa kuharibu watoto wa wenzao, anajau nini kuhusiana na hili na kama ana midadi ya kutaka kujua zaidi, nitacheza naye sahani moja,..huyu hanitii wasiwasi nitahakikisha kuwa namweka sawa….sizani kama atakuwa na moyo wa kwenda kupekenyuea huko hospitalini …’akajipa moyo huku akishuka kwenye gari kuelekea nyumbani kwa Maneno
NB. Nawatakia ijumaa njema
Ni mimi: emu-three
4 comments :
Kuna wapendwa walitoa maoni yao na kwa vile natumia simu ya kiganjani bahati mbaya nikakuta nimefuta hayo maoni, kwanza naomba msamaha,pili kama inawezekana muandike tena hayo maoni
Thanks m-3 kwa kipande hiki. nakutakia weekend njema
week end njema m3 thanks alot sasa afadhali tunateremka na mkasa huu vizuri tu tulikuwa tumesimama sehemu moja
na vp hapo kazini hatujuwi imekuwaje ss wapenzi wa blog hii unisamehe m3 tatizo sipo tanzania ningekuja kukuona tukaongea mawili matatu ila tupo pamoja
Mmmmh,ya leo ni kali sana.Sijaona shangazi mbabe kama wa Maua.
Post a Comment