Inspecta akisogea kwenye lile jengo, nia yake kuingia mle ndani kwa njia yoyote ile, hakutaka kufuata utaratibu, akijua kuwa akifanya hivyo huenda taarifa zikavuja, kwahiyo akafuta hisia zake zilivyomtuma. Bila kumuarifu yoyote kusudio lake. Giza lilikuwa kali siku hiyo, lakini kwa uzoefu wake wa kazi kama hii hakuwa na wasiwasi, alikuwa kaiacha pikipiki yake mbali na kutembea kwa mguu hadi kwenye hilo jengo ambalo lilikuwa kama gofu, na alipoona kwenye mlango hakuna mtu akatumia ujuzi wake kuufungua ule mlango wa geti na kuingia ndani baada ya kuhakikisha kuwa hakuna mtu.
Kulikuwa kimya kabisa, akalichunguza lile jengo huku akichukua picha kwa kutumia simu yake yenye kamera na video, kwa nje kabla ya kuingia ndani ya hiyo nyumba, na kuona sehemu kubwa ilivyoharibika, akasogea karibu hadi kwenye mlango wa ile nyumba ambayo kwa upande wake wa nyuma kulikuwa hakujabakia kitu, akajiuliza kichwani, nini atakipata katika hali kama ile, lakini akajipa moyo, na kuingia ndani na kukutana na mabaki ya vigae na makabati, akasogea kwa ndani zaidi akitumia tochi ndogo mithili ya peni, lakini ilikuwa na mwanga mkali sana.
Alikumbuka vyema chumba alichoelekezwa na mmoja wa vijana wake ambaye aliwahi kumtuma kuingia kwenye jengo hilo. . Alimwambia ajaribu kutumia ujuzi wake ili aweze kuingia humo ndani na kupata ramani ,na jinsi kulivyo, kwani kwa taarifa Zilizopo nyumba hiyo imekarabatiwa na kujengwa tofauti na awali na huenda kuna kitu kinaendelea humo ndani. Ilikuwa sio rahisi kuingia ndani ya jengo hilo, lakini kwa utaalamu wa kipelelelezi, yule kijana alifanikiwa kwa shida, ilibidi kijana huyo ajifanye kuwa ni mgeni akimtafuta ndugu yake .Alimtaja jamaa ambaye aliwahi kukaa ndani ya jengo hilo kabla, kuwa ni ndugu yake. Alsema aliwasiliana naye akiwa kijijini na kumwahidi kuwa kuna kazi. Kijana huyo aliweza kumvunga mlinzi wa getini kwa mbinu hizo na akaruhusiwa kuingia ndani, ili akaulizie vyema, kwani mlinzi huyo aliwahi kumsikia jamaa huyo kuwa aliwahi kukaa humo, lakini hana taarifa zaidi.
‘Nenda kamuone jamaa anayelinda kwa ndani yeye ana muda mrefu kwenye jengo hili’.akaambiwa na yule mlnzi wa getini.
Alipoingia humo ndani akakuta mabadiliko makubwa , kwani kabla ukuta huo kurefushwa, jengo hilo halikuwa hivyo, ilikuwa nyumba ya kawaida tu, lakini sasa jengo hilo limeimarishwa zaidi kwa kuongezewa upana na marefu, na kukarabatiwa vyema kuliko ililivyokuwa mwanzo. Limeondolewa bati na kuwekwa vigae, limeongezwa maengo mengine …..
Akakaribia mlango wa hiyo nyumba, na kusikia kitu kama `alarm’ ikilia kwa ndani, na mara mlango mdogo wa kibanda kilichojengwa karibu na huo mlango wa nyumba kuu ukafunguka na jamaa akatokeza na yule kijana akaulizwa yeye ni nani na nani kamruhusu kuingia, akajielezea …na kujifanya ana wasiwasi kuonyesha kuwa yeye ni mgeni wa mji.
‘Wewe vipi, uliambiwa anaishi hapa na nani, kwanza hebu…unasema unatokea wapi…Morogoro, kwanza hapa hakuna kazi, hebu ishia usije ukaniletea matatizo hapa, sijui kwanini yule mlinzi getini alikuruhusu kuingia huku…’ kabla hajamaliza sauti ikatokea kwa ndani ya hiyo nyumba ikiita na baadaye kuulizia kuwa huyo mlinzi anaonge na nani? Inavyoonekana humo ndani kuna mitambo ya kuonyesha mtu anayeingia, ndio maana kulilia kitu kama `alarm’
‘Sasa umenileta matatizo, …nenda ukaonane na huyo bosi huko mtamalizana wenyewe..’ akasema yule mlinzi. Ikawa bahati ya mtende kwani kijana yule alipata nafasii ya kuingia kwa ndani na akakutana na huyo aitwaye bosi, akajielezea na yule jamaa akamwambia kuwa ni kwelii jamaa aliyemtaja aliwahi kuishi hapo , lakini ni zamani sana , sasa hivii hayupo na anasikitika kuwa hajuli wapo anapoishi kwa sasa… !Akaambiwa na yuke kijana akajifanya kulalamika kuwa ataenda wapi na hapa mjini ni mgeni.
‘Hilo halituhusu ndugu, tunakuomba utoke humu ndani, humu hapaingiwi ovyo, na hawa walinzi watawajibika kwa kosa hili…’ akasema yule mtu akimuongoza yule kijana kutoka.
‘Basi naomba uchukua namba yangu hii ya simu, kama itatokea mkamuona naombeni sana mnipigie simu, kwasababu sasa hivi nitaomba omba nauli njiani angalau nirudi kijijini kwetu…’ akasema na kutoa simu yake, kujifanya anatafuta namba yake.
‘Nishakuambia kuwa hatuna muda huo, sawa nipe hiyo namba yako, andika kwenye hiki kikaratasi, maana simu yangu nimeiacha ndani, mimi nitaiweka kama kumbukumbu, lakini sikuahidi chochote…’ akasema yule jamaa huku akimuongoza yule kijana kutoka nje.
Hapo kijana akapata nafasi aliyoitaka na kuitumia vyema, kwani kwanza alipofika ndani macho yake yalicheza kama gololi, jamaa yule alipofungua mlango wa kile chumba alipotokea ule mlango ulikuwa ukijifunga wenyewe kwa taratibu, kwahiyo kwa sekunde hizo chache alichungulia ndani ya kile chumba alichotoka yule jamaa, na masikio yalisikia sauti ya mashine kwa mbali kama zile za watu wa studio!.
‘Wewe mlinzi nini mnafanya, …ok, hilo tutaongea baadaye ile huyu jamaa, kaulizia jamaa yake ambaye kwa sasa hayupo, siku hizi haishi hapa kwahiyo msindikizeni mhakikishe ametoka eneo hili…na hili kosa lisirudiwe tena..’ akasema yule jamaa na kurudi ndani.
‘Sawa bosi, halitarudiwa tena…’ akasema yule askari na kumshika jamaa mkono, ili ahakikishe amemtoa mwenyewe nje.` nyie watu bwana mnajiingilia tu sehemu bila kujua taratibu zao, sasa umeniharaibia mpango wangu wa kuomba mkopo…hebu twende huku nje….’ Akasema yule mlinzi kwa hasira
‘Sasa afande hata wewe nakupa namba yangu kama mtamuona ndugu yangu huyo naomba sana mnifahamisheni, hii hapa ni namba yangu…’, akampa namba yake aliyoiandika kwenye kikaratasi, na kutoka mle, na wakati huo simu yake aliyoitoa akijidai anaangalia namba yake ya simu ikawa imechukua picha sehemu kubwa ya jengo, na alitoka nayo akiwa kaishikilia mkononi na kuweza kuendelea kuchukua picha ambazo zilisaidia kujua ramani ya lile jengo.
Inspekta alimsifia kijana wake kwa kazi nzuri ingawaje ni ya hatari, lakini ndio majukumu yao ya kikazi yalivyo kwani wakati mwingine inabidi ujitoe muhanga kwa ajili ya taifa lako…
Inspekta akawa anazidi kuchunguza lile jango na kusema kwa sauti ya chichini, ‘Kama kweli hili jengo lina mitambo kama hiyo, na imeteketea na moto najua kabisa hawatasumbuka kuihamisha haraka kiasi hicho, lazima mabaki yake yatakuwepo, na lengo langu ni kuwa na uhakika kweli kuna mitambo kama hiyo hapa…?’ akasogea mbele kwa tahadhari huku anafungua mlango wa kile chumba alichoelekezwa na kijana wake, akainua baadhi ya mabaki na kutafuta huku na kule na kweli hakuona dalili ya mashine.
Inspekta akakumbuka taarifa zilizokuwepo kuhusiana na watu hawa, kuwa kwao kuua ni jambao rahisi hasa ukiingilia kazi zao, na wanaua kitaalamu kiasi kwamba hawawezi kupatikana. Wapo vijana wake wamepotea kimiujiza na inasadikiwa kuwa wanaweza kuwa wamauwawa na hawa jamaa. Lakini za mwizi ni arubaini na arubaini yao imeshafika, kasema Inspecta, huku akilini akiendelea kujiuliza, kuna nini wanaficha kiasi kwamba hawataki kugundulika, ina maana nii hiyo mitambo peke yake nan i ni zaidi ya kutengenezea picha, au kuna la jambo jingine kubwa…akaahidi kuwa ataigundua hiyo siri iliyojificha kwa hali yoyote ile…lakini akasema kimoyomoyo, kuwa sio kazi rahisi kugundua katika mazingira kama yale, kila kitu kimeteketea!
Wakati anainua chuma kilichokuwa kimezuia mlangoni, akasikia mlio wa kutikisika, na ghafla akashituka anazama na ukuta kwenda chini…akahaha huku na kule ili kaupata sehemu ya kushika, lakini akajikuta anatua chini huku matakataka , vumbi vikimfunika toka juu…, akajikuta akishangaa, ina maana kulikuwa na shimo,…akajikagua kuhakikisha kua hajaumia na kujikung’uta vumbi na uchafu na kuitafuta tochi yake ambayo ilishamponyoka wakati anazama na ule ukuta, akaiona na kuiwasha mwaga mpana hakuwa na wasiwasi kwani alikuwa kwa chini na akiwasha mwanga kama ule hangaliweza kuonekana na mtu aliyekuwa mbali .
Alijikuta kasimama kwenye mabaki ya mashine yaliyoungua vibaya sana, mashine hiyo iliundwa mfano wa kabati, na waya nyingi zilionekana zikiwa zimening’inia, zikiwa hazifai tena na alipoangalia vyema akaona kabati lililo haribika kabisa na kuona mabaki ya kanda za DVD zikiwa zingine zimegandamana na na kuyeuka kama chapatti, zilikuwa hazifai kabisa, akatoa simu yake ambayo ina kamera ya video na kuchukua picha eneo zima hilo, alijaribu kutafuta kama anaweza kuona kanda zozote ambazo ni nzima lakini hakufanikiwa, zilikuwa hazifai kabisa!
Alipohakikisha kuwa kamaliza kuchukua kile alichokitaka akatoa kidude kwenye simu yake, kidude hicho ni kidogo lakini ndicho kilichohifadhi kumbukumbu zote za picha alizochukua, akakifungwa na kinailoni alichokuwa nacho halafu, akavua kiatu chake na kukizamisha kwenye kwenye upenyo maalumu kwenye kiatu chake, halafu akato kidude kingine kipya na kukiweka sehemu ile ile alipokitoa kile cha mwanzo. Alipomaliza hilo zoezi akaanza kutafuta sehemu ya kuokea kwenda juu , ilikuwa kazi kubwa sana kutafuta njia ya kutoke, kwani ilivyoonekana hicho chumba kilijengwa madhubuti na kwa siri, kiasi kwamba huwezi kugundua, na mlango ulikuwa ukutani kama kabati, ukisimama ndani ya kabati hilo unashushwa kama lifti. Kabati hilo liliungua na kubaki kipande kikionyesha sehemu inaposhuka na kupanda!
Kwa ujasiri wake alifanikiwa kupanda juu akiwa anatokwa na jasho, akatizama huku na kule kuhakikisha kuwa hakuna kiti kingine cha muhimu, alipohakikisha kuwa hakuna kiti cha muhimu akageuka kutoka nje, na alichoshituka ni kusikia kichwa kikigongwa na kitu kigumu kama nyundo na giza likatanda usoni …na alichosikia kwa mara ya mwisho kabla hajapoteza fahamu ni sauti ikisema
‘Mpekueni na hakikisheni kuwa hana chchote cha maana, kama kafa kamtupeni kwenye bonde la maji…kama hajafa hakikisha mnamaliza nimeshajua ni nani, siku nyingi naitafuta nafasi kama hii…ni mtu htaraii sana huyu’ Inspekta akapoteza fahamu.
*********
Kulipopambazuka kikosi maalumu kilifika hapo kupekua na kumtafuta bosi wao, lakini hawakukuta mtu, walitafuta kila kona hakukuwa na dalili yoyote wa bosi wao na watu wote walioulizwa walikataa kata kata kumuona Inspecta katika eneo hilo, hata pikipiki yake ilikutwa imetelekezwa mbali kabisa na neno la nyumba hiyo. ndipo taarifa zikazagaa za kumtafuta Inspecta. Jamaa mmoja ambaye ni mhusika wa hilo jengo akakamatwa kwa kuhojiwa, aliambiwa atakaa kifungoni hadi hapo itakapojulikana wapi Inspecta yupo.
‘Nyie mnajisumbua bure, hakuna lolote ninalolijua, tangu nyumba yangu iungue sijafika eneo hilo, nitahakikisha nawafungulia mashitaka kwa kunishikilia bila kosa..’ akasema yule mtu.
Baada ya siku nzima kuisha bila kujua lolote kuhusu Inspecta, ikaanza kutia shaka, na kikosi maalumu kikaundwa kufuatilia kiundani, lakini hakuna lilogundulika.
***********
Mzee, baba yake Maua alikuwa kwenye ofisi yake akisikiliza taarifa ya mmoja wa kijana wake. Taarifa hiyo ilimchanganya sana, kwani ilionekana kuwa uhasama wake wa yeye na mpinzani wake kibiashara umeibuka tena. Na huenda ni ule mgongano ambao awali ilikwenda mbali hadi serikalini kuwa wanahasimiana kwasabaabu ya wivu wa kibiashara, na hata ukiangia katika mikono ya wanasiasa. Ilifikia hatua mapaka wakaitwa na kusuluhishwa, na ilionekana kama vile mambo yameisha. Na kuonyesha kuwa mambo yameisha mtoto wa Mzee akaajiriwa kwenye kampuni ya mhasimu wake halikadhalika akatokea kijana akajiriwa kwenye kampuni ya Mzee, lakini chini kwa chini uhasama huo uliendelea na kila mmoja alipopata nafasi hakusita kumshambulia mwenzake kilugha za kashifa lakini sio moja kwa moja, ilimradi kuharibiana kibiashara.
‘Hii taarifa inaonyesha dhahiri kuwa mwenzangu kaamua kuniingilia hadi kwenye familia yangu, mbona hili tulikubaliana kuwa lisitokee, biashara iishie kibiashara sio kifamilia. Inaamaana mkwe wake kaamua kumrubuni mtoto wangu na kumuingiza kwenye matatizo, ili kuniharibia, na kupakaza kshifa…inawezekana maana nakumbuka kabisa niliwaona kwenye ile hoteli…’ akawaza na kuichukua ile taarifa, na kuanza kuisoma kwa makini.
Baadaye akamruhusu yule kijana kuondoka, na alikaa na kutafakari kwa makini, kuhusina na taarifa ile, ambayo kama ataiweka wazi kwenye vyombo vya habari italeta mgongano mkubwa sana, lakini kabla ya kufanya hivyo akaona amuite mshauri wake na msaidizi wake wa maswala kama hayo. Akachukua simu yake na kumpigia jamaa yake aje , huku akiwaza kwa makini, na kujiuliza haya mahusiano mabaya yataendelea mapaka lini.
Kampuni ya Mzee ilikuwa miongoni mwa makampuni makubwa hapa nchini, iliweza kujieneza na kusambaza matawi hadi mikoani, na hili lilimjengea sana sifa, na hata akawa anashirikishwa katika maswala makubwa makubwa serikalini, na hili lilimsaidia pia kupata zabuni ambazo zilinufaisha kampuni yake. Kwa hali hii ikaonekana kuwa jamaa anatumia miradi yake kujinufaisha zaidi.
Wakati yeye akiendelea kwa njia hiyo walikuwepo wapinzani wake ambao walikuwa na makapuni yanayoendana nay a kwake, na yalihitaji zabuni kama hizo, na ilipoonekana kuwa Mzee anapata zaidi, makapuni mengina yakaanza kulalama, na hata kujiingiza katika kuhakikisha kuwa kampuni ya Mzee inashuka chini. Mzee hakukubali kwani alikuwa mzoefu na alishajijengea jina, kwani tangu hapo alishawahi kufanya kazi serikalini na kwahiyo anajua nini anachokifanya.
Mmoja wa wapinzani wake wakuu ni baba mkwe wa bosi, huyu alikuwa na makapuni mengi kama alivyo baba yake Maua, na alishawekeza hadi nchi za jirani na kuingia ubia na wawekezaji toka nje. Mzee huyu kama alivyo baba yake Maua, aliwahi kufanya kazi serikalini na baadaye kujiengua kushughulikia kazi zake binafasi na baadaye akawa hashiriki moja kwa moja, ila aliwaajiri watu wengine yeye akiwa pembeni, ila kunapotokea maswala makubwa yanayoingilia miradi yake hasiti kujitokeza na hupenda mara nyingi kutumia vyombo vya habari.
Mzee au baba yake Maua alikaa kwenye kiti chake baada ya msaidizi wake kuingia, na alimwelezea nini amekipata kutoka katika vyanzo vyake vingine, na kumpa huyo msaidizi wake hiyo taarifa. Msaidizi wake ambaye alikuwa makini sana na mtaalamu wa mambo ya kisheria na kibiashara aliisoma ile taarifa kwa muda, halafu akaifunga na kuinuka kwenye kiti.
‘Mzee sio kweli kuwa hili tatizo la binti yako linahusiana na mambo ya kibiashara na uhasama uliojijenga toka awali. Namjua sana mhasimu wako, na wahasimu wengine, lakini kuna usemi usemao, wavumao baharini ni papa, alkini wapo samaki wengine…mhasimu wako huyo anaijua sana sheria, hawezi kufanya kosa kama hili, ambalo lipo waziwazi, hawa ni samaki wengine, ambao kila mara mara wanatumia mwanya wa uhasama wenu kufanya mambo yao, hawa ni wajanja wameamua kutumia mwanya huu ili ionekane hivyo huku wakitimiza malengo yao…acha tufanya uchunguzi tutagundua mengi, kwanza jana niligundua jambo moja kubwa, ambalo kama tutapaya ushitikiano na huyo jamaa tutakuwa tumepiga hatua kubwa sana, na itakuwa mwisho wa hawa samaki ambao ni wabaya kuliko tunavyozania. Naomba mzee tutoke kidogo.
Mzee alishangaa kwanini anaitwa na jamaa yake watoke, lakini kwa vile anamuamini akaondoka naye na kuingia kwenye gari hadi kwenye zahanati moja iliyopo ndani ndani. Walipoingia hapo wakakutana na docta mmoja ambaye alitambulishwa kwa mzee na wakaingizwa kwenye chuma kimoja, ambapo walimkuta mgonjwa kalazwa kitandani, na walipoingia yule mgonjwa aliyekuwa na nadeji kubwa kichwani akainuka na kukaa kitandani.
Mzee alishangaa na kumwangalia yule mgonjwa, akauliza kwa wasiwasi, `vipi inspecta umekumbwa na janga gani ‘
‘We acha tu, nashukuru sana kwa kijana mmoja aliyekuja kunikoa kimiujiza, na kunileta hapa, nikiwa sijitambui, na mapaka sasa hivi sijaonana na huyo, kijana, kaniarifu docta kuwa aliyenileta hapa ni kijana mdogo mdogo tu, na kuacha maagizo kuwa nihudumiwe kwa gharama yoyote. Mzee umejiuaje kuwa nipo hapa, au ni vijana wako?’ akauliza Inspecta akiinuka kujiweka sawa, alionekana bado ana maumivu lakini alikuwa akijilazimisha kiaskari.
‘Sijathibitisha hilo, lakini halina umuhimu sana, cha muhimu ni kujua kuwa upo salama…na kwanini imetokea hivyo ili hatua za muhimu zichukuliwe.
‘Mimi najiona sijambo, ila maumivu machache, zaidi la kuongea kwa sasa sina, kwani hali iliyonitokea ni kushitukizwa, nikiwa katika kuwajibika….huyo jamaa alikusudia kunimaliza kabisa…lakini mungu ni mkubwa, na sasa ama zake ama zangu…’ akasema Inspecta na kukaa vizuri.
‘Nilikuambia toka awali kuwa kundi hili sio mchezo, na kila mara natupa hisia zangu kwa mpinzani wangu wa biashara, lakini sina ushahidi wa moja kwa moja, na hata msaidizi wangu ananishauri hivyo, kuwa sio yeye, sasa ni akina nani na wanatafuta nini?’ akasema Mzee na kuangalia saa yake.
‘Hilo ndio swali la muhimu, awe mpinzani wako au mwingine, ni kujua nini kudio lao, na nina imani kuwa siku zao zimefika..’ akasema Inspecta.
‘Cha muhimu ni kuunganisha nguvu zetu, kile ulichogundua na kile nilichogundua kiweke sahami moja halafu tujua hatua za kuchukua…au unasemaje inspecta?’ akauliza Mzee. Wazo hilo Inspecta hakulipendela kwani hakutaka kuwa anashirikiana na kundi au mtu fulani kabla hajagundua nini kinaendelea, lakini kwa hali aliyokutwa nayo, ikabidi akubali shingo upande, na kusema.
‘Mimi bado sijawa na jambo la kuliweka wazi, bado nafuatilia kwa karibu hisia zangu, lakini hakuna ushahidi wa moja kwa moja, ila labda nilichogundua cha karibuni ambacho kinatakiwa kuwekwa kisheria na hilo ambalo limesababisha hadi kuumizwa….’ Akasema Inspecta bado akiwa na wasiwasi kumwaminii huyu mzee moja kwa moja,
‘Mimi nashaui kuwa tuendelee kucheza hivi hivi, vijana wako ni askari wanajulikana, lakini vijana wangu ni raia hawajulikani hili litawashitukiza hawa magaidi na mafisadi tutawaweka kitanzini,najua kabisa kuna watu walio na nguvu kubwa na wanajifanya wema sana serikalini, lakini sio kweli wanauma na kupulizia, hawa tutawashinda tu,,,’ akasema mzee na kuangalia saa yake tena.
‘Cha muhimu wewe kaaa mafichoni kwa muda kwani wale wote waliotumwa kukuangamiza wamemalizwa, na ijulikanavyo ni kuwa umeshauwawa…saa ikifika utawashitukiza kwa nyuma, watakuwa hawana ujanja….’ Akasema yule msaididzi wa Mzee.
`Sasa hebu tuambie uligundua nini huko kwenye jengo maana tunataka kuhakikisha kazi hii tunaimaliza haraka iwezekanavyo…’akasema Mzee huku akimsogelea Inspecta. Inspecta alifikiri kidogo, halafu akauliza viatu vyake vipi wapi, na alipoletewa akatoa kidudu kwenye kiatu chake na kumkabidhi Mzee.
‘Huu ni ushahidi namba moja wa kumdaka mkuu wa magaidi ni ufisadi….’
Ni mimi: emu-three
4 comments :
aiii m3 kazi sasa kuna nini kinatafutwa ninani hawa magaidi nahisi huyu baba mauwa yumo anatafuta maslahi hajali kitu wala mtu
cant wait
Samira Hata mimi najiuliza hawa watu wanatafuta nini? Ngoja tuzidi kuwemo!
Wakati nahangaika kuwekeza vitu vipya kwenye computa ya ofisini ambayo ndiyo tegemeo langu, mara ghafla computa yangu ikazima, mara ghafla kila kitu kikawa hakifanyi kazi, mtaalamu nasema computa imeingiliwa na virusi, kwahiyo inahitaji matibabu...mpaka lini, mtaalamu anasema hajui, labda leo leo, kesho keshokutwa....Mungu wangu, sasa ina maana!
Nitatumia juhudi nyingine kuhakikisha muendelezo wa kisa hiki unakuwepo, msijali sana Tupo pamoja!
Lakini mnasemaje kuhusu hiki kisa, maana kimtizamo wangu bado kirefu, ila kama kimewachosha, mimi najua jinsi ya kukifupisha!
NO ENDELEA TU M3. TUPO PAMOJA. POLE SANA KWA HILO TATIZO.
C UNAJUA TENA TUPO KWY KAZI ZA WATU. TUNASOMA KIUJANJAUJANJA TU. NDIO MAANA UNAONA KIMYA KWENYE COMMENTS. UNAWEZA UKAKOSA NAFASI LEO, UKASOMA KESHO YAKE STORY YA SIKU 2 AU 3. POA M2 WANGU 2PO PAMOJA, USIKONDE. STORY BABUUUUUUUU KUBWAA.
JAMANI MBONA CKUSOMA PALE BABA MAUA ALIPOPIGIWA CMU KUWA MWANAE KACHANGANYIKIWA ILIKUWAJE?
NA MANENO JE, ALIVYOKUWA AKIMFUATILIA YULE DR. BANDIA ALIKUWAJE? NIN HAMU YA KUJUA.
BN
Post a Comment