Baba wa Maua alikuwa kajipumzisha kwenye kochi lake, siku hiyo alikuwawepo nyumbani pake yake, mkewe alikuwa kasafiri. Akiwa mpweke akajikuta akiangalia taarifa ya habari kwenye runinga, lakini akili yake ilikuwa mbali sana, alishangaa pale alipojikuta akimkumbuka mke wake wa kwanza, ambaye ni marahemi alimuwaza sana mke wake huyo na maisha yake ya mwanzo na mkewe. Na alipokuwa akimuwaza,hapohapo akamkumbuka binti yake ambaye wamekuwa hawawasiliani sana. Akachukua simu yake na kumpigia, simu ikasema unayempigia hapatikani. Alipojaribu mara ya pili akakasirika na kuirusha pembeni ile simu .
‘Toka lini Maua asipatikena kwenye simu, …’ akasema kwa sauti. Kabla hajafanya lolote akaendelea kuwaza, na kujipa matumaini kuwa, amempatia karibu kila kitu muhimu, ingawaje ni kwa masharti, ilibidi afanya hivi ili kulinda maslahi ya familia yake. Hata hivyo hakuwa na wasiwasi na maisha ya binti yake. Akakumbuka kuwa siku ya leo alitakiwa akutane na wakili wake kwa minajili ya kuweka vyema kumbukumbu zake, hasa za mali yake , alikuwa kajadiliana naye kuwa ni vyema akaipitia tena kumbukumbu yake ya mali yake ambayo ilikuwa aianelezea umilikaji, na haki za mali yake akiwa hai na hata akifa, ili baadaye kusije kuwa na matatizo.
Alikuwa kamuamini sana mume wa Maua, na aliona amuweke katika watu ambao wana haki ya kupata chochote katika mali yake. Wazo hili lilimjia pale alipothibitisha kuwa ni mwaminifu na ameyafuta masharti aliyomuwekea karibu yote. Na hili alilifikia umuazi baada ya kuongea na watoto wake wa kiume, lakini hakumueleza chochote Maua, alipanga atamuelezea hilo swala siku ya kikao cha kifamilia ambacho alikipanga akifanye karibuni.
Hakutaka kabisa kubagua watoto wake kila mmoja alikuwa kamuandikisha kile cha muhimu anachotakiwa kuwa nacho, hata hivyo hakusahau kuweka baadhi ya mali yake kama wakifu, na hiyo aliita mali yake baada ya kufa….akacheka na kusema, watu wengi wanajisahau, wanamilikisha mali zao zote kwa wanafamilia na familia yao, lakini hawajikumbuki kabisa wao wenyewe. Hawajui vitu kama wakifu, ni akiba yao baada ya kufa, je wanasahau maisha baada ya kifo, mimi najiwekea `akiba yangu’ kama wakfu, hii ni sadaka ya kuendelea, kwa ajili ya mayatima, shule na hospitali…alipowaza haya alitabasamu.
Akakumbuka watoto wake na maisha yao, hakuwa na shaka nao, kwani kila mtu ana ajira yake, wanaume wote wanakazi nzuri na wamejijenga, kiasi kwamba hawahitaji kabisa msaada wake,…!
‘Mtu ambaye nilikuwa na mashaka naye ni binti yangu kipenzi,akaanza kumuwaza Maua na mume wake, akawaza sana kuhusu maisha yake, …akajiuliza kwanini akaamua kuolewa na mume ambaya hana kazi na wala hazalishi chochote, akaguna na kusema hayo ni maisha yake ambayo hakupenda kuyaingilia, na hata hivyo ameridhika kabisa na mume wake kuwa ni mtu mwema katika familia. Akasema huyu mume wa Maua hataacha kumsaidia kama mtoto wake,…ila kama atafungamana na mashartyi ya familia hii, sijaridhika moja kwa moja na tabia yake lolote linaweza kutoke na nikamtoa kwenye orodha ya watoto wangu, sio yeye tu, hata watoto wangu wengine, wakiharibu nitawaharibu, huo ndio msimamo wake!.
Akaendelea kumuwaza Maua, alikuwa moyoni akimpenda, lakini kila alivyojaribu kuonyesha upendo huo, binti yake alionyesha kinyume chake, hasa baada ya kifoo cha mama yake.
‘Huyu binti sijui kwanini kila ninavyojitahidi awe karibu na mimi , haendani kabisa…ananipa mashaka, hata wakati mwingine namuwaza tofauti na damu yangu….hapana huyu ni damu yangu, hata iweje, hiki ni kipenzi changu, lakini kama atakuwa katika mstari ninao utaka mimi, kama atageuka na kuwa ….hapana sitaki niwaze hayo, najua ni binti mwema kabisa…’ akajikuta kiwaza kwa sauti moyoni.
Mara akasikia simu yake ikiita, akainuka haraja na kuichukua pale alipoitupa pembeni mwa kochi, akaisikiliza na akajikuta akishituka kwa taarifa hiyo aliyoambiwa, hata karibu kuidondosha ile simu,
‘Nini unasema binti yangu yupo hospitalini, kwa ajali au anaumwa, au…’ akauliza akiwa kainuka tayari kuondoka. Alipomaliza kusikiliza yale maelezo akatikisa kichwa na kutoka nje, alimwambia dereva wake ampeleke hospitalini haraka iwezekanavyo, na alipokuwa njiani akawa anawaza yale maelezo kuwa binti yake kalazwa hospitlini baada ya kutokea tatizo ofisini kwao, ingawaje binti yake huyo hajaumia mahala popote, ila kawa kama kachanganyikiwa.
‘Kachanganyikia…! Hii mpya, ni kitu gani kinaweza kumchanganya binti yangu …’ akaichukua simu yake na kuitafuta namba, alipoipata akaipiga, ni moja ya namba zake maalumu. Huyo aliyepigiwa alipoipokea, Mzee akatoa maagizo kwa huyo mtu jamaa kwa lugha wanayoelewana naye, halafu akaikata ile simu. Akaangalia mbele huku akiwaza kwa makini. Na hapo akakumbuka tukio lililotokea karibuni, pale walipokuwa na kikao na wawekezaji wenzake, kikao kile kilitakiwa kifanyike siku ile na kumaliza maswala yote siku ile ile, ikabidi wapange vyumba kwa ajili ya kikao cha usiku kucha,kwani kikao hicho kilitaraji kuisha saa saba au nane za usiku na hapo watachukua vyuma kwa ajili ya kumalizia masaa yaliyobakia,kuwa na hata ya kurejea nyumbani muda kama huo.
Wakati wakiwa katika kikao hicho, ilitokea muda alitoka kidogo kwenye kikao, na mara akamuoan binti yake akiwa kaongozana na jamaa mmoja ambaye baadaye aligundua kuwa ni mmoja wa jamaa anayefanya kazii na Maua,…hakuridhika na hilo, akampigia kijana wake au jamaa yake anayemuamini kwa maswala ya familia yake, na kumwambia ajaribu kuhakikisha usalama wa binti yake, ambaye kaumuona humo hotelini.
Alikumbuka kuwa kesho yake jamaa yake huyo alimletea hiyo taarifa kwa simu, na kumwambia kuwa maelezo mengine kayaweka kwenye bahasha maalumu , lakini alikumbuka kuwa hakuwahi kuyapitia, kwani alichokuwa akikihitaji ambacho ni cha muhimu ni usalama wa binti yake. Hakuweza kuonana na huyo jamaa kwasababau jamaa huyo alikuwa na safari ya nje kimasomo, akaondoka hata bila ya kuonana na yeye,
Akasema kichwani, itabidi nikaipitie ile taarifa nione kulikuwa na kitu gani, na alikumbuka sana jamaa yule alitaka kuongea naye, lakini kwa vile alikuwa kabanwa na shughuli za kazi yake, ikawa vigumu sana, na hakuwa na shaka sana kuwa kuna jambo baya.
Alikumbuka siku ya kesho yake wakati anatoka kwenye ile hoteli alimuon yule jamaa aliyekuwa kaongozana na Maua akiwa katokea pale hotelini, akaingiwa na shaka, mbona yula jamaa alimuona usiku na binti yake na leo asubuhi na mapema kamuona akitoke mle hotelini, ina maana kalala mle hotelini, na kama kalala mle je binti yake aliweza kurudi nyumbani, na kwa muda ule ndipo lipoweza kumpigia simu jamaa yake aliyempa kazi ya kuangalia usalama wa binti yake.
‘Bosi kazi ile nimeifanya, tunaweza kukutana leo mapema asubuhi , kwasababu kama nilivyokuambia nina safiri ya kimasomo, …ila kazi yako niliifanya na maelezo zaidi nimeyaweka kwenye bahasha nitayawakilisha mezani kwako asubuhi hii, na kama tukionana ni muhimu zaidi…’ akasema yule mtu
‘Hayo maelezo umeyaweka katika lugha ya kawaida au kwa lugha yetu…’ akauliza Mzee
‘Lugha yetu mzee, nisisngeweza kumwaga mtama kwenye kuku wengi…’ akasema yule mtu
‘Kwani kuna baya …?’ akauliza mzee
‘Ndio maana nataka tuongea na wewe, …ili tuone kuwa kuna ubaya au ni kawaida tu, kama inawezekana mzee…sio baya sana, lakini nimuhimu kama inawezekana tuongee, kama haiwezekani, nikirudi tutaongea kiundani..’ akasema yule mtu. Na kweli Mzee alipanga kwenye ratiba yake kuwa ataongea na yule mtu, lakini muda ule ulipofika akatingwa na jamabo kubwa la kibishara na alipomalaiza jambo hilo la kazi zake ikawa keshachelewa, jamaa yake alishaondoak kuwahi uwanja wa ndege!
‘Sijui huyu jamaa ataruidi lini na baya zaidi hakuna mawasiliano naye huko alipo. Lakini hakijaharibika kitu nitafuatilia mwenyewe na vijana wangu wengine nione kuna nini…je kulikuwa na jambo siku ile…na jambo gani, inawezekana likawa linahusiana na kuchanganyikiwa kwa binti yangu…itabidi nijue yote hayo kwa haraka sana. Akasema Mzee kimoyomoyo, na kwa muda ule alikuwa keshafika hospitalini akatoka kwenye gari lake na kuingia hospitalini hapo kumuona binti yake.
*********
Maneno akainuka pale alipokuwa kakaa, pale alipoona ana mgeni, na kumwangalia yule jamaa aliyekuja akahisi kuwa alishakutana naye kabla. Jamaa yule alijitambulisha kuwa ni mmoja wa watu wa baba mkwe wake anataka kujua nini kimetokea hadi mkewe kuchanganyikiwa, ..
‘Kuchanganyikiwa, usiniambie kuwa mke wangu kachanganyikiwa, alikuwa na matatizo ya kichwa tu, na …nilimwambia huenda ni malaria, akapime, lakini hakunisikia huenda ndiyo hayo yameoanda kichwani, sina taarifa zaidi maana hawa jamaa wameniweka ndani , kwa uasamaria wema wangu, hebu ongea nao ili nikaonane na mke wangu…’akasema Maneno kwa huruma.
‘Nitajitahidi kufanya hivyo, hilo lisikutie shaka, kama hakuna matatizo makubwa utaachiliwa muda si mrefu, ila Mzee anataka kujua maendeleo ya binti yake, je kuna kitu gani kinaendelea kati yake na wewe, na ujue ukweli ni muhimu sana, kwa manufaa yako, na maisha ya baadaye, klama kuna kitu kisicho cha kawaida ni bora uongee….akijua baadaye kuwa kulikuwa na jambo limetokea ukaficha sidhani kuwa atakuwa na huruma na nyie, unamjua yule mzee alivyo hajali kabisa kuwa ni mwanae au nani kama katoka nje ya mstari wake basi hatamtambua tena, ni bora ujikoshe wewe ili akulinde, kuliko kuanyamaza kimya…’ akasema yule mtu.
Maneno hakuwa na kitu alichokishuku sana kwa mke wake, alikuwa na fikira potofu awalii kuhusiana na mke wake lakini jinsi siku zilivyokwenda aliaanza kuzoea kuwa mke wake ni mfanyakazi na yeye ni baba wa nyumbani, akaridhika na hiyo hali, atafanyaje!
‘Mke wangu kachanganyikiwa kwasababu gani…kuna kitu gani kilichomtokea kule kazini mpaka akapoteza fahamu, je kuna haja ya kumwambia huyu mtu hisia zake, au anayamaze tu…je nikimueleza na ikaonekana Maua kajihusisha na mambo yasiyofaa, akaingia matatani ina maana hata yeye ndio itakuwa basi tena, akatikisa kichwa kukubali kuwa kwa vyovyote iwavyo yeye anatakiwa kuwa uapande wa mke wake, labda kuwe na ushahidi wa moja kwa moja kuwa mke wake anafanya mambo machafu, hayo hayana kuvumilika, nitamwambia baba mkwe bila kuficha.
‘Mimi sina zaidi ya hayo niliyokuambia, aliondoka nyumbani akiwa anaumwa kichwa, akaenda kazini, baadaye niliamua kumfuata ili niua hali yake….’ Akasema Maneno.
‘Kwanini ulimfuata badala ya kumpigia simu …’akauliza yule mtu
‘Simu yake ilipotea na moja ya vitu vilivyompeleka kazini ni pamoja na kufuatilia simu yake..’ akasema Maneno.
‘Hiyo simu ilipotelea kazini au wapi…; akauliza yule mtu.
‘Hakuwa na uhakika, kwani walikuwa na kikao cha wakaguzi wa mahesabu, na kikao hicho kilifanyika hotelini, lakini hana uhakika wapi alipoidondosha ndio maana alitaka kupitia huko hotelini, na kazini kwake…; akasema Maneno.
‘Hoteli gani walipofanyia kikao chao….’
Maneno akakerekwa na haya maswali kwani kuna umuhimu gani kuyajibu maswali haya yote, akakunja uso na kumwangalia yule mtu, akasema `sikumbuki jina la hiyo hoteli, kwani maswali yote haya yanasaidia nini, kwanza nimeshikiliwa kisivyo halali, mke wangu anaumwa,cha muhimu ni kufuatilia haya maswala muhimu, sio kuchimbana-chimbana, naona maswali mengine ukamuulize Maua mwenyewe..’ akasema Maneno na kugeuka kurudi pale alipokuwa kaka.
‘Ushirikiano wako na sisi ndio utakaoturahisishia haya maswala mawili, swala la wewe kuachiwa na kuwa huru na pili kumsaidia mkeo, ili tujua kwanini kachanganyikiwa, ukituambia yale tunayoataka sisi tutajua jinsi gani ya kufanya, u tufanyaje, lakini ukituficha…, tutapata kwa nia nyingine kila tunachokitaka ni swala la muda tu, lakini wewe utaumia kwani tutamwambia Mzee kuwa huna ushirikiano nasi au hutoi msaada kwake na hapo utajijua mwenyewe, je una uhakika ni hayo tu unayoyajua kuhusuiana na mkeo. Hakuna jambo ambalo lilitokea mpaka mkeo akaanza kuumwa kichwa..? akauliza yule mtu.
Swali hilo lilimgutusha Maneno na kugeuka kumwangalia yule mtu, na alipogeuka alimkukuta huyo jamaa kamkazia macho, na ile hali ya kukaziwa macho ikamfanya Maneno ainame chini, akiwaza huyu jamaa ana maana gani, kwanini anamuweka kweny mtego!
‘Mimi ninachokumbuka, ….mmmh, Maua aliporudi toka kazini alikuwa akilalamika kuwa kichwa kinamuuma, hilo ndilo ninalojua, mengine nitayajuaje wakati mimi ni baba wa nyumbani,…au umesahau bwana mkubwa, unakumbuka siku moja ulinishauri kuwa nikubaliane nah ii ya kuwa mimi ni baba wa nyumbani na mke wangu ni mfanyakazi…’ akasema Maneno.
‘Sawa, tutagundua hilo muda sio mrefu, na unakumbuka nilivyokuambia awali, raja ya baba wa nyumbani ni kujua wajibu wake na kinachomsaidia kuishi,kama kuna jambo linaloingiza doa katika hicho kinachomsaidia kuishi ni bora kuwa muwazi kwa Mzee mwenyewe, kwani yeye ndiye anayesaidia kuwa baba wa nyumbani mwenye kila kitu, ukiharibu kwa mzee, huna maana kwake na hata huyo Maua hatakusaidia lolote….sasa una hiari …..kama una lolote nieleze na nakupa muda wa kufikiria, mimi naenda kuangalia uwezekano wa wewe kuwekewa dhamana au kama hakuna tatizo utaachiliwa mara moja!’ Yule jamaa akaondoka na kumuacha Maneno akiwa kaduwaa
Ni mimi: emu-three
4 comments :
Wakati naandika sehemu nilikuwa na mengi zaidi lakini nikajikuta kwenye mitihani na majukum na tatizo sugu la umeme. Nitajitahidi niwezavyo nikiongozwa na maoni yenu!
thanks m3 tupo pamoja mambo mazuri
pole mkuu, umeme sasa imeshageuka kuwa si shida tena bali ni donda ndugu
Pole na kwikwi za umeme ila at least tumepata kipande hiki, tupo pamoja sana
Post a Comment