Maneno baada ya kuongea na walinzi alilisogelea pikipiki lake, akiwa na nia ya kuliingiza ndani, lakini akawa na shauku ya kuona ni nini kinaendelea, akawa kasimama kwenye pikipiki lake kama vile analirekebisha, huku akiwa anachunguza kwa ndani. Mara akamuona yule mwanamke aliyekuja na gari akiwa kasimama barabarani pengine akiwa na nia ya kutafuta usafiri labda wa taxi, lakini baadaye alimuona akigeukla kule kwenye geti la ofisi , akaangalia kwa muda, halafu taratibu akawa anaingia ndani kwa kupitia sehemu magari yanapoingia kuelekea ndani na wakati huoi walinzi walikuwa hawajalifunga lile geti vyema.
Yule mwanamke alivyoingia pale getini alikuwa kama anajiiba vile, anatembea kiupandeupande na hakupitia pale wanapokaa walinzi, ambapo angepewa ruhusa kama ilivyo kawaida. Maneno akahisi , labda inawezekana akawa mmoja wa wakubwa wa hiyo kampuni. Lakini mbona anatembea kama anajiiba… Akawachunguza wale walinzi kama watamsimamisha lakini aliwaona walinzi kama wanabishana jambo fulani na hawakuwa na mawazo na yule mwanamke, hali hii ilimtia wasiwasi Maneno akadharau utaratibu wa ile ofisi, kwani kiusalama sio vyema.
Alipokumbuka kuwa mke wake yumo humo ndani na yule mpanda pikipiki, ambaye hakumwamini kabisa ,akahisi kuna zaidi ya anavyofikiria, akaona mwili unamsisimuka, na hii kwake ni ishara mbaya. Aliwaza sana mwishowe akawaendea wale walinzi ili kuongea nao, alisimama pale kidogo akiwasikiliza wanachobishana, baadaye akawaambia walinzi kuwa anaingia ndani, walinzi wakamwambia, mbona walishamruhusu, wao hawana kipingamizi, wakijua yeye ni mume wa mmoja wa bosi wao, kumkatalia haiwezekani.
‘Nenda bwana lakini usilete fujo humo ndani, unaweza ukaingiiwa na wivu…hapa ni ofisini bwana…mambo ya kiofisi sio sawa na nyumbani…hahahah’ akasema yule mlinzi huku anacheka, na Maneno naye akatabasamu na kuliendea pikipiki lake akaliingiza ndani kwa kulikokota. Na wakati anafanya hivyo, mara akaona jamaa yule aliyeingia mwanzoni na pikipiki akitoka kwa kasi, hakungoja mlango ufunguliwe vyema, akapenya kwenye ule mpenyo mdogo na huku analisukuma geti kwa mkono na akaingia barabarani kwa kasi ya ajabu.
‘Huyu jamaa vipi anakuwa kama kakurupushwa bwana…’ akasema Mlinzi.
‘Hii ndio kawaida yake au imetokea hivi leo tu..?’ akauliza Maneno huku akiliweka pikipiki lake vyema.
‘Ni kawaida yake, anakuwa na kadharau fulani hivi, …aaah, lakini hatujali tumewazoea watu kama hawa…’ akasema mmoja wa walinzi.
Manneo akazidi kuingiwa na wasiwasi akiwaza kwanini yule jamaa mpanda pikipiki atoke kwa kasi kiasi kile…na mke wake …alipofika hapo kimawazo harakaharaka akauendea mlango wa ofisini, ulikuwa mkubwa na wa viyoo. Huoni ndani, lakini watu waliopo ndani wanakuonawewe uliyepo nje. Anakumbuka siku ya kwanza alipokuja mara ya kwanza akawa anajiangalia kwenye ule mlango kwani upo kama kiyoo cha kujiangalia, akawa anajiangalia na kujiweka vyema, na alipoingia ndani na kugundua kuwa watu waliopo ndani walikuwa wakimuona na kumsanifu akaisikia aibu sana. Basi alipozoea akawa akifika hapo anaingia ndani mara moja.
Alipofika pale mlangoni kabla hajaingia ndani akawa anawaza, je akiingia humo ndani na kukutana na mkewe, akiwa na mabosi zake atajieleza nini…siataonekana ana wivu, au anamchunga mke wake…au atasema kuwa kafuata nini…? Watu wenyewe huenda wanamdharau kwa kuwa hana kazi, yeye ni baba wa nyumbani…Akiwa anawaza hayo baadaye alijisemea moyoni…ngoja niingie ndani kwanza, mengine yatajileta yenyewe,…sidhani kuwa mke wangu hataniamini ni kimwambia nimekuja kumua hali kwani aliondoka akiwa anaumwa …, lakini sehemu nyingine ya ubongo wake ikawa inamuonya kuwa anachofanya sio sahihi…lakini akawa hazijali tena hizo hisia.
‘Aaaah, nitajua hukoo ndani…kwanza mke wangu anaumwa, hilo ndilo la muhimu..’ akasema na kufungua mlango. Alipokanyaga lile busati la mle ndani akajihisi vinginevyo, huwa hapendi kuingia mle ndani, na hasa kukutana na macho ya wafanyakazi wa mle ndani ambao wengi wanakuwa wakimwangalia sana, na hili lilimfanya ajihisi kuwa huenda wanambeza kuwa kamuoa mke mfanyakazi wakati yeye hana kazi!
`Sawa najua wanawaza hivyo, lakini yanawahusu nini..’ akajikuta akisema mwenyewe moyoni.
Akaingia ndani na kutembea haraka haraka kuelekea ofisi ambayo anaitumia mkewe, alishawahi kufika mara nyingi kwahiyo anaifahamu vyema. Wakati mwingine alikuwa akijiona vibaya, kwani anakuja kumuona mkewe kwa shida maalumu, anakawizwa kumuona, wakati mwingine anaambiwa kuwa eti mkewe yupo kwenye mkutano, au ana kazi maalumu asubiri kwanza…mke wangu wananifanyia hivyo! Lakini baadaye aliyazoea hayo akajua ndio utaratibu wa kiofisi.
Siku ya leo alishukuru sana kwa kuwa hakuwakuta wafanyakazi mle ndani kwani ilikuwa siku ya mapumziko. Akatizama huku na kule kuhakikisha, kweli kuwa hakuna watu wengine, akaona kote kimya. Lakini mara macho yake yakamuona mwanamke mmoja mnene hivi akitoka mbio,….ooh, akamkumbuka ni yule mwanamke aliyemuona nje akingia kwenye geti kama anajiiba iba…akasogea pembeni na kujibanza sehemu ili asionekane. Akamwangalia yule mwanamke anachofanya….
Alimuona yule mwanamke akiingia moja ya vyumba vilivyopo mbele ya ofisi, hakuchukua muda mrefu mara akatoka akiwa na chuma mkononi. Maneno alijua huenda ni fundi kachukua chuma kwa ajili ya kazi maalumu,… lakini sura ya yule mwanamke ilionyesha hasira na hata kutembea kwake kulikuwa kwa ujasiri fulani. Akavutiwa na ule mwondoko wa kibabe, akawa anamwangalia kwa makini, aone kile chuma kinaenda kufanya nini, akajisema moyoni, angefurahi amuone akifanya hiyo kazi ya ufundi na kile chuma, akasogea kwa kuificha ficha huku akimwangalia yule mwanamke kwa makini na huku akiogopa asije akageuka na kumuona.
‘Mwanamke kama yule akishika shingo yako sianakumaliza mara moja…angalia lile limkono…duuuh’ akajikuta akijisemea.
Alipofika kwenye chumba kinachoangaliana na chumba cha mkewe, akashangaa, kwani chumba anachofanyia kazi Maua kilikuwa wazi, akaangaza macho kwa haraka kutizama mle ndani, alishangaa kuona baadhi ya vitu vimedondoka chini, na sio kawaida ya ile ofisi, na mara nyingi alipofika mle ndani alikuwa akiikuta ile ofisi ikiwa maridadi, kila kitu kimepangwa vyema kwa ustadi wa hali ya juu…hiyo ndio tabia ya mkewe, hapo machale yakamcheza, akahisi kuna jambo, akamwangalia yule mwanamke akisukuma ule mlango unaoangaliana na ofisi anayofanyia mkewe kwa nguvu.
Maneno akawa kaduwaa, kwani msukumo alioufanya yule mwanamke ulikuwa wa nguvu kama anataka kuung’oa ule mlango, alitumia mkono mmoja na mguu, huku mkononi mwingine akiwa bado kashikilia kile chuma. Maneno akasema ama kweli mwanamke huyu ni jasiri, akamtizama kwa shauku, lakini kwa mshangao akamuona yule mwanamke akisogea kwa ndani na kukiinua kile chuma alichoshika na kumbamiza jamaa mmoja aliyekuwa kainama kwa ndani…Yule jamaa aliyeonekana ndani alikuwa kainama au alikuwa kapiga magoti..kwa vyovyote vile, na ilivyoonekana ni kuwa ,alipoona mlango umefunguliwa akawa kama anainuka, na kutaka kugeuka, kuangalia huyo aliyeingia.
Yule jamaa kabla hajageuka vyema, ndipo akakutana na dhoruba hiyo ya chuma, …kilimgonga wapi, hapo Maneno hakuona vyema kwa ndani, kwani mwili wa yule mwanamke ulikuwa umamziba, lakini kwa uhakikika kile chuma kilitia kwenye kichwa cha jamaa,…hakujua kwanini yule jamaa aliinama au kuchuchumaa, au…vyovyote iwavyo…,yeye alichoona vyema ni kumuona yule jamaa kama anainuka kusimama na alipokuwa usawa wa kusimama, ndipo akakutana na hicho chuma kikigonga kichwani, na damu zikaruka, na pale pale jamaa akadondoka chini.
‘Kaua…jamani kaua, sitaki ushahidi miye…simo kabisa, sijaona kitu..’ Maneno alijikuta akipayuka huku anaangalia pembeni na huku anangalia kule ndani kwa kujiiba, na alishasahau kabisa kuwa alikuwa kajificha na hakutaka yule mwanamke amjue mapema, na hata hivyo yule mwanamke hakujali, au hakusikia yale maneno ya Maneno, kwani kwa haraharaka bila kujali tendo alilolifanya mwanzoni, akakimbilia kwenye kochi zilizopo mle ndani…, wakati huo mlango wa ile ofisi, ulikuwa wazi alipousukuma yule mwanamke, na huwa ukifunguliwa baada ya muda hujifunga wenywe…kwa ule uwazi ulimtosha Maneno kuchungulia mle ndani, na hapo akamuonaa yule mwanamke akielekea kwenye kocho kubwa huku kainua chuma juu, huenda alikuwa akitaka kumalizia kazi yake, au kuna jambo jingine alikuwa akilifuata kwenye kochi. Na macho ya Maneno yakaona kama vile kuna mtu mwingine kalala kwenye kochi, mlango ulishaanza kumziba, akasogea karibu na mlango na kutamani kuusukuma, ilia one vizuri…
‘Yule aliyelala pale ni anaonekana kama ni mwanamke vile,…’akajikuta akisema kama anatangaza mpira, au pambano la ngumi, lakini alishangaa kuona moyo wake ukimwenda mbio, alitamani akimbie aondoke kabisa mle ndani ili asije akashikwa kama shahidi, lakini moyo ulimtaka kuona nini kinaendelea, na hata hivyo akiondoka bila kumuona Maua na ile hali aliyoiona hatakuwa na amani akajikuta akisogea na kuusukuma mlango ufunguke, na kuchungulia…akasahau kabisa ule uwoga wa mwanzo. Na alipomuoa yule mwanamke akiinua chuma…ikionyesha kuwa alitaka kumbamiza yule mwanamke aliyelala pale kwenye kochi, Maneno akaona hiyo haikubaliki, mbona yule mwanamke kalala tu. Maneno akajikuta akiingiwa na moyo wa huruma, na kitu kikamvuta na kujikuta akiusukuma ule mlango kwa nguvu na kuingia ndani ili amuwahi yule mwanamke asiendelee kufanya mauaji.
‘Wewe mwanamke, mbona unajitakia balaa, umeshaua mtu mmoja bado unataka kuua mtu mwingine, halafu ni mwanamke ambaye ukimgusa na hicho chuma ni marehemu…acha…oooh’ akasema huku keshamsogelea.
Alikuwa kachelewa, chuma kilishashuka, lakini kwa ule mshituko wa kusikia mtu akiongea, na kwa vile lile kochi lilikuwa chini kidogo, kile chuma kikagonga sehemu ya kochi ya kuegemea na kukosa shabaha, na hapo hapo Maneno akawa keshafika na kumsukuma yule mwanamke kwa nguvu zote…na yule mwanamke hakutarajia huo msukumo, au kuwa kuna mtu mwingine, kwanza akashikwa na butwaa na pili kushituka aliposikia kuwa kaua na anataka kuua mtu wa pili, na kwa vile alikuwa hakutegemea akajikuta akipepesuka na kudondoka chini, na kichwa chake kikagonga ukutani, na alichokumbuka kuona ni vinyotanyota vikitanda usoni.
Maneno alisikia kichwa cha yule mwanamama kikigonga ukutani na kutoa sauti akajikuta aking’aka na kusema ‘Oh, balaa gani hili tena…’
Alimwangalia yule mwanamke akiwa keshafika sakafuni na kuwa kimya…alipoona vile akashika kichwa na kusema `ooh, mama yangu namimi sasa nimeua…hapana sio kusudio langu…hapana…mungu wangu nisaidie na balaa hili…’ akatoka mle ndani akiwa na nia ya kukimbia, lakini akajikuta akijikwaa, na alipotizama ni kitu gani, akakuta ni mguu wa yule mwanaume aliyepigwa chuma, akakumbuka na kumwangalia vyema, akamuona damu zimetapakaa kichwani na bado zinamvuja, na alipomwangalia vyema akaingiwa na huruma aliona kabisa mtu yule anahitaji msaada wa haraka ili kuokoa maisha yake. Akachukua simu yake ya mkononi na kupiga namba aliyopewa na mkewe kuwa likitokea tatizo ambalo linahitaji usalama ampigie huyo jamaa, kwani yeye ni mkuu wa walinzi na mchapa kazi mashuhuri wa kampuni.
‘Halloh , naomba ufika haraka huku ofisini kuna tatizo kubwa…’ akasema huku anatetemeka. Bahati nzuri huyo mkuu wa ulizi alikuwa kafika hapo kazini kwa kukagua walinzi wake, na aliposikia hivyo hakupoteza muda akakimbilia humo ndani, akifuatana na mmoja wa walinzi wake.
Maneno alipomaliza kuongea akajikuta akitetemeka kwa woga huku akijilaumu kuwa sasa kafanya nini, kwani moja kwa moja yeye ataonekan ndiye muuaji, na…kweli keshamsukuma yule mama ambaye kwa muda ule alikuwa katulia kimya kuonyesha kuwa keshakufa…Akageuka akiwa na nia ya kukimbia, lakini kabla hajainua mguu, mlango ulifunguliwa na askari wakingia wakiwa na silaha zao mkononi.
Maneno alijikuta akiinua mikono juu huku akisema `sio mimi muuaji ni yule mama pale…’ Na kwa muda mwingi mawazo yake yote yalikuwa kwa yule jamaa aliyepigwa chuma cha kichwa hakuwa na mawazo ya kuangalia kwenye kochi, kujua ni nani kalala pale, hakuwa na mawazo ya kumwangalia yule mwanamke aliyedondoka kuwa yupo salama au vipi, hakuwa na mawazo ya kutafuta hivi mke wake yupo wapi kwa muda wote huo…alikuwa ameshika kichwa akimwangalia yule jamaa anavyovuja damu. Na walipotokea wale walinzi akainua mikono juu kama vile anajisalimisha na kusema `sio yeye muuaji…’.
‘Vipi kumetokea nini..’ akauliza yule mlinzi huku akikagua mle ndani. Na yule mlinzi alipona ile hali akasema `Mungu wangu tumeingiliwa…’ harakaharaka akachukua simu yake na kupiga polisi na huku akimwambia mwenzake apige simu kwenye hospitali ya jirani…!
‘Hata mimi nashindwa kujua,…waulize hata hawa walinzi wenzio, niliingia humu kumfuata mke wangu, sijui yupo wapi…na wakati namtafuta mara nilimkuta huyoo mwanamke akifanya haya mauaji,kwa kutumia chuma, nikamwahi na kumsukuma kabla hajammaliza huyo mwanamke aliyelala hapo kwenye kochi…’ akasema Maneno akionyesha kidole kwa nyuma, hakutaka kutizama, kwa woga uliomshika, yeye macho yake kwa huyo mwanaume anayebubujikwa na damu.
‘Huyo mwanamke aliyelala hapo kwenye kochi ndio nani,..?’ akauliza Mkuu wa ulinzi na alipomwangalia vyema akagundua kuwa ni …
‘Si Maua huyu, mhasibu wetu…’ akasema yule mlinzi
‘Eti ni nani, unasema nini wewe,…Maua haiwezekani , ina maana ooh ni mke wangu…oooh…kumetokea nini jamani…Maua wamkuua nini….hapana, haiwezekani…wewe hujafaa…’ Maneno aliigeuka haraka na kuangalia pale kwenye kochi na kumuona mke wake akiwa kalala, …au keshakufa…hakuelewa, alichojua na kukimbilia pale kwenye kochi lakini kabla hajamkaribia….
Ni mimi: emu-three
5 comments :
natamani niendelee kusoma tu isifike mwisho
"nimekua teeeeeeeeeeeeja, teja wa hii blog...nimekua teja oh sijiwezi" Hongera sana ndugu (maana sijui wewe ni he or she vyovyote vile uko juuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuu! Am enjoying the story lete mambo tuendelee kula raha ila inaonekana ndefu eh?
m3 sasa kazi naona bosi kibarua kishaharibika na zaidi family zote mbili hatari sana
nangoja nione itakuwaje
nakupongeza sana m3
umekatisha utamu jamani....... sijui itakuaje. masikini maneno!!!!
BN
Nashukuru wajumbe kuwa tupo pamoja .mambo yanakuja tuombeane heri nitajitahidi kadiri ya uwezo wangu Insh-Allah
Post a Comment