Katika sehemu iliyopita tuliishia pale nesi na dada yake walivyokuwa na furaha kubwa , baada ya kugundua kuwa dada mtu ni mja mzito. Hatimaye yule waliyemuona ni mgumba, kapata ujauzito, ilikuwa furaha iliyoje, mpaka watu wakasahau nini kilichowaleta hapo...hebu tuendelea na kisa chetu.
*********
Rafiki yangu anayenisumulia hiki kisa alikuwa juu kwa juu akitaka kuondoka, nikamuuliza swali,
`Kwahiyo baada ya hapo mtoto akapelekwa kwa mama yake, au ilikuwaje?’ Nikamuuliza rafiki yangu ambaye alikuwa akitaka kuondoka , na mimi na jamaa wengine waliokuwepo wakisikiliza walikuwa na hamu ya kujua nini kilitokea baadaye. Nilijua kama nitamruhusu aondoke itakuwa sio rahisi kumpata tena. Nikamganda kwa maswali!
‘Bwana wee, naona nia yako unataka nikuhadithie kila kitu, nami kuna sehemu sikutaka mtu ajue, kwani kumbukumbu zake zinanitia machungu, lakini ngoja nikuanzie maisha yangu na mama, ingawaje niliishi naye kwa muda mfupi kabla ya kutengana naye katika mzingira ya kutatanisha. Kwani mama alinipenda sana, na hakutaka kabisa niachane naye, nilikuwa kama mboni yake ya jicho, lakini ilivyotokea, tukajikuta tumetenganishwa , ilikuwaje …
Siku moja wakati tupo majalalani tukiokota makombo na masalio ya vyakula waliyotupa matairi, mara ghafla tukazungukwa na mgambo wa jiji. Unajua mgombo wa jiji wapo kila mkoa, mimi kwa vile nilishazoea hizo hangarihangari nikatimua mbio, na tulijua wapi pa kukutana na mama yangu. Mama yeye mara nyingi alikuwa mbishi na aliweza kupambana na watu kama hawo, au vibaka. Ujue hata sisi tulikuwa tukipmbana na vibaka, kutunyan’ganya hata kile kidogo tulichopata.
Mama yangu alikuwa mlezi wa watoto watano kama mimi, kwani hutoamini eneo hilo tuliwakuta watoto wengine wadogo , ingawaje walikuwa na umri mkubwa kidogo ukilinganosha na mimi, lakini walikuwa watoto wadogo , na haikustahili kuwa mbali na wazazi wao hasa mama! Basi mama kwa upendo wa watoto akawa ndio mlezi wao, atakachopata kidogo tunagawana, ingawaje mama alihakikisha kuwa mimi kwasababu ni mdogo kuliko wenzangu Napata klipa-umbele.
Ilikuwa tukiamuka asubuhi, wengine wanakwenda mabarabarani kuomba, wengine wanazunguka kwenye majalala na mama anahakikisha usalama wetu kwa kuwa karibu nasi na kidogo tulichopata tunakaa pamoja tunakula, kama ni pesa, mama anapanga nini tununue. Na watoto wakawa wamemheshimu mama na kumtii kila analosema. Mama alikuwa mkali kwa watoto watukutu, na kwahiyo adabu ilifuatwa.
Ilibidi ikifika jioni lazima maji ya kuoga, na kuhakikisha nguo zetu zipo safi, na usafi wa jalalani unaujua, zitafuliwa na maji machafu angalau sizipate chawa, wakati mwingine ilikuwa ni matambara tu yakusitiri aibu, na mama ikifika jioni anayashona-shona, ili kesho tusiadhirike.
Hapo kweny bonde hilo tulifika baada ya kufukuzwa maeneo ya mjini, Kwani ingawaje sikumbuki vizuri, maisha ya mjini, ila kumbukumbu zinanijia kuwa tulikuwa tukiishi mjini kwa mara ya kwanza, lakini maeneo ya mjini yalikuwa ya mateso, na wahuni , watu wazima walikuwa wengi , kwahiyo mchana mnahangaika, lakini sukiku ulikuwa mbaya sana,kwani usiku hupambani tu na wezi bali wauza unga, wabakaji …balaa mtindo mmoja.
Basi siku hiyo naikumbuka sana, kuliko siku zote ndio siku tulipovamiwa na mgambo, ….nilikimbia hadi juu kidogo ambapo niliweza kuona nini kinatokea kule chini, nikawaona wale mgombo wakitembeza kichapo, hutaamini kuwa binadamu wale hawakuwaonea Huruma binadamu wenzao, badala ya kupmbana na vibaka na wezi mitaani walikuja pale kupambana na masikini wanaotegemea makombo na masalia ya vyakula vilivyotupwa na matajiri, eti nilivyosikia badaye ni kwasababu kulikuwa na mkubwa alitaka kuja hapo, na eneo hilo lilitakiwa kumilikishwa muwekezai mmoja, kwahiyo ilitakiwa akija hapo asione hiyo aibu ya watu kama sisi.
Nilimuona mama kwa mbali akipambana na mgambo mmoja, na baadaye yule mgambo alipomshindwa akawaita wenzake, wakaanza kumpiga, utafikiri wanapiga mwizi, na baadaye nikasikia kwa mbali, wakisema kuwa mama yangu anaonekana ni mwizi kwasababu sura yake ambayo alikuwa akiificha ilikuwa imeharibikwa kwa kupigwa kama kibaka.
Wakaanza kumpiga,niliona kiatu cha mgambo kikitua kichwani kwa mama, nikashindwa kuvumilia, nikakumbuka kipindi tulipowasili hapo mara ya kwanza, nikiwa bado mdogo sana. Ilikuwa usiku tumejibanza kwenye upenyo wa nyumba, na tulikuwa tumaweza kupata chochote na mara mlinzi wa nyumba ile ambayo ilikuwa ndio inajengwa akaja na vijana wanne, wkatavumaia , mama akaanza kupambana nao.
Walikuwa mibaba, yenye nguvu, walipigana na mama, sikujua nini wanataka kutoka kwa mama, kwani kwa walivyoonekana waliweza kutafuta mahitaji yao bila kuja kutuuibia, kwani vijisenti mama alivyopata siku hiyo vilikuwa vya kuuza mchicha na mboga mboga. Mboga mboga hizo zilitoka kwenye bustani mama aliyotengeneza kipindi cha mwanzoni mwa utoto wangu kabla hatujafukuzwa hapo.
Basi tukawa tunauza mitaani tunapata hela ya kula , na kuipikia kidogo, baadaye tunakuja kulala kwenye hilo jumba.Jumba hilo lilikuwa mlinzi, kilichotakiwa kufanywa ni kumlipa huyo mlinzi kiasi fulani kwa siku ili tupate kijisitiri hapo, na kama huna kitu huruhusiwi kulala hapo. Kwasababu nilikuwa mdogo, ikifika usiku nalala fofo, na wala sijui kinachoendelea.
Siku moja, nilikuwa naumwa,mama akahangaika ilia apate hela ya kuitibia, alipata hela sio ya kutosha, akanipeleka hospitalini, nikapata dawa, tukarudi mapema kwenye lile jengo na mlinzi yule haruhusu, kwani hairuhusiwi kuishi hapo, na usiku anafanya kama msaada tu, kwa posho kidogo. Lakini hali yangu ilihitaji kutulizwa mahali, basii mama akaongea na yule mlizi kuwa atalipa hela ya ziadaSasa wale mijamaa walipofika nikajua wanataka hivyo vijisenti, nikatamani kumwambia mama awape tu, wasije wakamuua. Wakamshika mama kwa nguvu, wakampiga, na mmoja akamkaba mama shingo mwingine aka….hapana sitaweza kusahau tukio hilo, maana ingawaje nilikuwa mtoo, lakini nakumbuka kabisa ilivyokuwa. Hawakujali kwa mama kazimia walifanya walichokitaka huku nashuhudia kwa macho yangu, na baadaye wakachukua vile vijisenti, na waliponiona nalia wakanizaba kibao cha nguvu nikapoteza fahamu.
Kumbukumbu hizo zilinijia wakati nipo kilimani pale, nikashuka mbio nikiwa nimeshika kigogo, kwasababu nilikuwa mtoto, mgambo wengine hawakuweza kunijali, wakijua nakimbia tu huku na kule, nilifika pale yule mgambo alipokuwa kasimama akiendelea kumkanyaga mama kichwani na buti lake, huku mama katulia akijaribu kujiokoa, mimi kikakirusha kile kigogo kwa nguvu zote, na kweli kikatua kwenye kichwa cha yule mgambo.
Kwa wakati ule gari la jiji la kuwasomba wote waliokamatwa pale lilishawasili kwahiyo ilie vuruguvurugu na watu kupambana na mgambo hawakuona kile kigogo kimetoka wapi. Kilimgonga yule mgambo aliyekuwa akimkanyaga mama, na alidondoka chini na kupoteza fahamu na hapo mama akapata mwanya wa kuinuka na kukimbia.
Ikabidi tuhame eneo hilo…
‘Lakini rafiki yangu naona kama umeruka sehemu kubwa sana nyuma, mbona hujasimulia jinsi mama alivyompata mtoto wake, na…’ nikamkatisha.
`Ukumbuke kuwa mama ndiye aliyekuwa akinisimulia hiki kisa, na mama alikuwa akinisimulia huku akiwa kalala kwenye kochi, kwani mwanzoni nilikuwa nimekaa naye na kichwa chake kilikuwa kwenye mapaja yangu, lakini baadaye nilipokwenda kumchukulia maji na dawa ya kutuliza maumivu, akawa kalala kwenye kochi, mimi nikiwa nimekaa pembeni nikimsikiliza. Lakini niligundua kitu, kuwa kila muda ulivyokwenda nilimuona mama akibadilika sauti, yaani sauti ilikuwa kama inafifia…nikaingiwa na wasiwasi nikijua kuwa mama hali yake sio nzuri. Na lipofika ile sehemu ambayo nesi alikuwa kifurahia kumuona dada yake ni mja mzito, akanyamaza kimya.
‘Mama vipi mbona unaonekana hupo sawa sawa…?’ nikamuuliza
Na kama vile mama anatoka usingizini akasema hivi ‘Mwanangu…mwanangu..nashindwa kuongea zaidi…nguvu inanishia, ila mwanangu usikate tamaa ya maisha..utafanikiwa tu, nimeridhika kuwa wewe unanipenda sana mama yako na kweli huna kinyongo na mimi kama mkeo anayedai eti mimi nimewaloga….mwanagu…nashindwa kukusimulia mengi yaliyonikuta kukuonyesha kuwa hakuna kama mama, na hakuna mama ……mwanagu…’ akanyamza kimya.
Nilimsogelea nikamuona hatingishiki kabisa, nikajaribu kumwangalia mapigo ya moyo, nikaona kama yamesimama…mungu wangu ina maana mama…hapana haiwezekani, itakuwa kazimia tu…
Nilikurupuka nikatoka nje, nia nimwangalie mke wangu ili tusaidiane tumpeleke hospitalini. Mimi nilikuwa dhaifu sana, nilikuwa napepesuka, kwani nilikuwa nimekonda, mawazo njaa…kwahiyoo hata kumuinua mama peke yangu nisingeweza.
Nilipotoka nje nikashangaa kupo kimya, hakuna cha mke wangu au mtoto. Nikaingia chumbani nikakutana na mshangao, chumba kilikua kama hema, hakuna kitu hata kimoja…hebu jaribu kufikiria chumba kilikuwa kina vitu vingi, kitanda, redio yangu ambayo niliipenda sana, kabati la vyombo, kwani ilibidi tuweke huko chumbani, kupata nafasi ya watu kulala, …vyote vilikuwa vimebebwa.
Sikuamini kuwa tukio hilo limefanyika hapa kwangu, kwani na umasikini wangu wote bado wanachukua hata kile kidogo nilicho nacho, na hata hivyo wamaingiaje na kwa muda gani, na gari lililochukua hivyo vifaa vyangu lilikuja saa ngapi, mbona sikulisikia mngurumo!. Nikatoka haraka hadi nyumba ya jirani kuulizia.
‘Mimi nilijua kuwa mnahama, maana kuna gari lilikuja na kusimama mbali kidogo na hapo kwenu, na watu wakawa wanachukua vifaa hapo kwako wanavihamshia kwenye hilo gari, huku mke wako akiwa anawasimamia …’ akaniambia jirani yangu.
‘Sasa jirani yangu, nina shida kubwa sana, naomba msaada, maana mama hali yake sio nzuri, je mume wako yupo aniazime baiskeli?’ nikamuuliza huku machozi yananitoka.
‘Mume wangu aliondoka kitambo na baiskeli yake, lakini alisema hatakawia, … na huyo anakuja’ akasema yule jirani na hapo nikamuona mume wake akija na baiskeli, nikashukuru sana.
Alipokuja yule rafiki yangu sikupoteza muda nikamwambia hali ya mama ni mbaya sana anisaidie baiskeli ili tumpeleke hospitali…Yeye bila ubishi akaingia ndani kwake halafu akatoka na kunifuata nyumbani kwangu, na mle ndani tulimkuta mama kalala vilevile, ina maana kazimia…sijui, au ndio keshakufa! Kwa hali kama ile, nikawa nimechanganyikwia nahaha huku na kule. Isingekuwa huyo rafiki yangu, sijui ingekuwaje. Yeye alimbeba mama na kumtoa nje, na akachukua simu yake na kumpigia jamaa mmoja mwenye bajaji, na huyu jamaa akaja haraka wakasaidiana kumbeba mama hadi kwenye hiyo bajaji, na sisi tukaingia na kuelekea hospitalini.
Hebu tuishia hapa kwa leo.
Ni mimi: emu-three
3 comments :
nakushukuru m3 kwa kusikiliza maoni yetu hakuna kitu kama mtu kukusikiliza na kukujali umeonesha kutujali sana wafuatiliaji wa visa /mikasa unayotuletea ambayo inanigusa sana
mungu atakupa wepesi wa kila jambo
Ni kisa cha kusikitisa na kutia simanzi kwa kweli, na kina mafunzo mengi sana usiache kukimalizia!
Hakika hapa duniani kuna watu wa kila aina. Kweli Mungu ni muweza. Na nimeamini kweli katika maisha ni vizuri kuwa na majirani, kushirikiana nao vizuri, Rafiki ni bora kuliko mwanasesele...
Post a Comment