‘Nyie watoto hebu muwe na adabu kidogo..’ akasema huku anaufungua mlango, na kabla hajasema zaidi macho yake yakatua pembeni mwa nyumba na akajikuta akishituka na kubakia kukodoa macho ….ajabu kabisa…..!
Kabla hajatizama vyema, yule mwanamama akashituka toka usingizini na kujifunika haraka, halafu akainuka na kupotelea mitaa ya pili. Yule baba akawa anawaza mengi, kuwa huyu mama kapata masahibu gani na ni kichaa au …
‘Vipi mume wangu wamesemaje huko hospitalini..’
‘Mmmm, kuna tatizo, la kikazi, na inavyoonekana ni kuwa mdogo wako alikabidhiwa mgonjwa kumuhudumia, na mgonjwa huyo alikuwa kafanyiwa upasuaji, alikuwa hajazindukana, na katika kumhudumia, akatoka kidogo kufuata dawa, aliporudi huyo mgonjwa akawa….’
Mara simu ikalia na kumkatisha mazungumzo…
*****Je simu ilikuwa ya nini, na kuna maajabu gani kutoka kwa huyu mama wa mitaani....tusishahau kuwa tupo kwenye kisa cha NANI KAMA MAMA...Naomba tuendelee na kisa hiki:*******
***************************************
********************************
*********************
**************
‘Dada nimewaletea mtoto, najua mna hamu sana ya kuwa na mtoto, sasa, nawaambia hivi duwa zenu, mungu kazisikia na mungu kawabariki bila hata ya kupata shida….unajua dada kubeba mimba miezi tisa sio mchezo, tena mtoto wenyewe mzuri , afya tele, hebu mshike umuone…’ akampa dada yake yule mtoto, ambaye alikuwa katulia kimya.
Dada mtu akiwa na mashaka akampokea yule mtoto, huku amemwangalia mdogo wake kwa uso wa kutahayari, akiwaza wapi ndugu yake kampata mtoto mchanga kama yule, akawaza labda matatizo yaliyotokea huku hospitalini yanahusiana na huyo mtoto, …imekuwaje!
`Wewe hebu niambie nini kimetokea, maana mara simu ya matatizo, mara simu kuwa unakuja nyumbani na mgeni, mgeni mwenyewe hatumuoni, sisi tulizani unatuletea shemeji, …sasa na huyu kiumbe wa watu umemleta hapa kufanya nini, mbona bado mdogo anahitaji maziwa ya mama…’ akajikuta akiongea bila kupumzika.
‘Kwanza shemeji yupo wapi, maana hili nataka tuliongee tukiwa wote , maana hili sasa halina hiyari, ama kama hamukubaliani nalo, basi na kazi sina. …mimi kwa dhana yangunimeona kuwa labda hili limetokea ili mpate mtoto..’ akakatisha maneno baada ya kusikia sauti nje.
‘Nataka mtoto wangu…’ na sauti hiyo ikakatishwa na kilio cha mtoto, dada mtu akamshika na kumbembeleza, huku anauliza mama yake yupo wapi, kwani inaonekana mtoto anahitaji nyonyo..’
`Dada toka sasa hivi wewe ndio mama yake, umejifungua katika hospitali yetu, kama unahitaji taratibu za kisheria, tunaziandaa, huyu mtoto hana mzazi, na tatizo lililotokea huko hospitalini, limenifanya nipate mtoto huyu bila kupenda. Mimi bado sijakuwa na uwezo wa kulea mtoto, nikaona niwaletee nyie…ngoja nimtengenezee maziwa yake…halafu sogea huku dada nikuonyeshe, inatakiwa umpe maziwa haya niliyoleta, vipimo vyake vipo kwenye hii chupa, ni maalumu kwa watoto wachanga kama hawa, humpi mengi sana, ila kadri siku zinavyokwenda ndivyo utakavyomuongezea dozi…natumai hili halitakuwa gumu kwako…na..na..’
‘Nataka mtoto wangu…nataka mtoto wangu…’ wakasikia kelele nje
‘Hivi hawo ni akina nani, naona watoto wengi hapo ne, kuna nini…’ akauliza mdogo mtu
‘We acha tu leo siku ya tatu, kila siku `nataka mtoto wangu, nataka mtoto wangu..’ ndio wimbo ulioenea mitaani, na aliyeuleta ni mama mmoja, nafikiri kachanganyikiwa, hatujawahi kumuona maeneo haya kabla…’ akaelezea dada mtu wakati mdogo mtu anajaribu kuchungulia dirishani, lakini hakuweza kumuona huyo mama, kwani alikuwa kasogea nyuma ya nyumba.
‘Hodi hapa…’ Dada mtu na mdogo mtu wakashituka, kwani sauti ilivyopigwa, ilikuwa tofauti na wanavyoijua, mume wake alibadili sauti makusidi kuwachekesha. Na wao wakazania ni huyo mwanamke nje anayecheza na watoto. Kabala mshituka haujawaisha, mlango ukafunguliwa na aliyefungua na mume mtu, …
‘Shemeji naye, umetushitua kweli…’ akasema shemeji mtu, wakasalimiana kwa furaha mtu na shemeji yake, baada ya salamu maongezi yakaanza, kuhusiana na kadhia ya hospitalini.
‘Unasema adhabu yako ni kumlea huyo mtoto, au kumtafuta mtu wa kumlea, na umeona sisi tumchukua awe mwaneti…shemeji kwani umefikia vipi mpaka kutuona hatutazaa, na kama nisipozaa na dada yako nitazaa na wewe…’ mume mtu akaongea kiutani, kumtania shemeji yake lakini moyoni akawa na raha kuwa watakuwa na mtoto, hata kama hawakumzaa wao, lakini ataleta faraja ndani ya nyumba. Na alivyomuoana mkewe akiwa na raha, akajua sasa angalau tabasamu la ndani litapatikana.
Wakakubaliana kumtafuta mfanyakazi wa ndani, na bahati nzuri nyumba ya jirani kulikuwa na binti anatafuta kazi za ndani, wakaamua kumchukua na hapohapo huyo mama hakupoteza muda akatoka kumfuata huyo binti, akimuacha mdogo wake akiongea na shemejie, na alipoletwa huyo binti, akapata maelekezo mengine jinsi ya kumlisha mtoto na kumlea, kwasababu wakati mwingi, dada mtu atakuwa hayupo ana kazi zake za kujiajiri, na hatakuwa akikaa nyumbani wakati wote. Tukio hili likaleta faraja ndani ya familia, na ilikuwa kama vile, dada mtu kajifungua mtoto.
Kesho yake mdogo mtu akarudi kazini kwake, na wakati anaondoka akakutana na umati wa watoto, wakimfuatilia yule mwanamama, akaona ajaribu kumwangalia huyo mama ni nani, lakini haikuwa kazi rahisi, kwani watoto walimzingira, na huyo mama akawa anacheza nao kama mtoto mwenzao. Alichoweza kuona, ni kuwa huyo mama kajifunga usoni kama waitavyo ninja..
‘Sijui ni mama gani huyu…’ akajiuliza yule mdogo mtu, na kuingia ndani ya bajaji kurudi mjini.
Wiki mbili zikapita, familia hii ikawa ni familia yenye mtoto, na kila aliyekuja alitambulishwa kuwa huyo ni mtoto wa familia hiyo, wamempataje, ikawa siri yao. Na mama mtoto wa kufikia kila akirudi nyumbani akawa anashangaa, kuwa yule mfanyakazi wa ndani anakuwa kakaa na yule mama wa mitaani, na mara nyingi yula mama wa mitaani anakuwa kambeba yule mtoto wao, ikabidi aulize kwanini.
‘Mama, huyu mama wa mitaani, anampenda sana huyu mtoto wako, na hutaamini, kila mara huyu mtoto akilia sana, mama huyu hutokea, na akimshika huyu mtoto kichwa, basi mtoto hutulia kabisa. Kama jana, sikukuambia tu, mtoto wako alikuwa akilia sana, kila nikimpa maziwa hataki, basi, wakati huo huo, huyu mama akaja na kumchukua, akamshika kichwani, mtoto akanyamaza kimya…, sasa imekuwa kazi, mtoto akilia namtafuta huyu mama anakaa naye nafanya kazi zangu kwa raha’ akasema yula mfanyakazi wa ndani.
Hili hata yeye mama wa kufikia aliliona, kwani siku moja alikuwa ndani na akasikia mtoto akilia sana, akatoka nje haraka kumchukua kutoka kwa mfanyakazi wa ndani, na alipofika mlangoni kutoka nje, huyo mama wa mitaani akatokea, akiwa kajifunga uso kama ninja, na akamkimbilia yule mtoto na kumchukua , kutoka kwa mfanyakazi wa ndani, alitamani amkemee yule mfanyakazi , lakini mdomo ukawa mzito kusema kitu, na ajabu kabisa, yule mtoto aliposhikwa kichwani na huyu mwanamama akanyamaza kimya. Na yule mama wa mitaani alimbeba kwa muda, halafu akamrudishia yule mfanyakazi wa ndani, na akataka kuondoka. Yule mfanyakazi wa ndani akampa yule mama kipande cha mkate, kwani kwa muda ule alikuwa akinywa chai, yule mama akakataa na kusema kashiba na aliondoka zake alipohakikisha yule mtoto kalala!.
Toka pale mama wa kufikia wa huyu mtoto akawa na mawazo sana na huyu mama wa mitaani, akajiuliza kuna nini kuhusiana na huyu mama, mbona hafanani kabisa kuwa kachanganyikiwa ki hivyo. Na kwanini kajifunika uso wake kininja…ndio maana watoto humtania na kumuita `ninja’ na wakimuita hivyo, huwachapa na fimbo yake. Na akiwachapa huimba wimbi huo wa `namataka mtoto wangu…’
Alipokuja mumewe akasahau kumuuliza kabisa, akasema moyoni, lazima hili swala nimuulizie mume wangu, huenda wameshamfahamu huyu mama ni nani. Sasa leo anapewa habari nyingina kama hiyo kuhusiana na huyu mama. Na wakati wanaongea na mfanyakazi wake wa ndani, akaja mama wa jirani. Mama huyu anaishi nyumba ya pili kutoka nyumba anapotoka huyu mfanyakazi wa ndani, naye alijifungua karibuni, na alikuja kupata maelekezo ya jinsi ya kumpa mtoto wake maziwa ya kopo, kwasababu maziwa yake yana matatizo, na hawezi kumnyonyesha tena mtoto wake.
Alielekezwa kuwa nyumba hiyo, wanamnyonyesha mtoto wao kwa maziwa ya kopo, kwahiyo kama anataka amelekezo awaone, basi akaja hapoo na kuomba hayo maelekezo, na alipokwisha kuelekezwa akaaga kuondoka, lakini kabla hajainuka kabisa, akakumbuka kitu …
‘Jamani mwanangu jana hakulala, kulia usiku kucha, siunajua tena, maziwa yana vidonda, siwezi kabisa kumny0nyesha, huku kwenye chuchu kunauma kweli, na mtoto akwa alilia usiku…mimi na mue wangu tukahangaika, ..nilitamani nimnyonyeshe hivyohivyo, lakini wee…sikuweza, kwani kunakuwa kama kidonda, akigusa tu…mungu wangu! Dakitari alivyoshauri, kiusalama nimuanzishie haya maziwa. Sasa wakati analia, kumbe huko nyuma ya nyumba alilala huyu mama wa mitaani, maana yeye hulala popote tu. Akabisha hodi na kusema, `namataka mtoto wangu..’ tukashangaa, toka lini mtoto huyu akawa wake. Tukadharau kwasababu huu ndio wimbo wake.
Mtoto akawa analia ile ya kutisha, na huyu mama akawa anagonga mlango kwa nguvu, tufungue. Nilitamani nitoke nimfukuzilie mbali, lakini baba watoto kwasababu ya joto akaamua kufungua mlango, kutoka nje. Huyo mama mlango ulipofunguliwa tu akaingia ndani, tukashindwa hata kumzuia, akaja moja kwa moja pale nilipokaa na mtoto, wote tumeduwaa. Kumzuia tunashindwa, tukabakia kimya…Akaja pale nilipokaa, akamwangalia mtoto anavyolia, akasema `mtoto wangu nyamaza..’Akainua mkono wake, sijui alikuwa akisema maneno gani, akamshika mtoto kichwani….mara mtoto kimya, na baada ya muda mfupi mtoto akalala. Halafu yule mama bila kusema kitu huyo akatoka nje na kwenda kulala pale alipokuwa kalala mwanzoni…’Akahadithia huyo mama na kuwaacha wenzake wakiwa wameduwaa, na kabla hawajamuuliza kitu zaidi, huyo mama akaaga kuwa anamuwahi mtoto wake.
Habari hizi za huyu mama na muujiza wake huu, zikaenea haraka, na watu wakaanza kumuita kuwa mama wa mkono wa baraka, na badala ya kuitwa mama wa mitaani, wale waliopata bahati ya kumuona a watoto wanaolia kwa mkono wake, wakawa wanamuita mama mwenye mkono wa baraka.s Sasa ikawa anakaribishwa kila nyumba, ili angalau awashike watoto wao, wapate hizo baraka, lakini yeye mwenyewe huyo mama hakupenda kwenda kuishi mbali zaidi ya nyumba ya huyu mama aliyepata mtoto wa kufikia, akapafanya kama ndio kwake. Na huyu mama wa kufikia akaaamua kumkaribisha kwenye chumba cha uwani, akamwekea godoro la akiba na shuka. Chumba hicho kilikuwa na makorokoro mengi, lakini baada ya siku mbili, kiligeuka kuwa kisafi ajabu, huyo mama alikitenengeneza vizuri na akakipangavuri na baadhi ya makorokoro yasiyofaaiz kila kitu katika hali njema.
‘Huyu mama kweli ni kichaa…mimi siamini, lakini mbona hapendi kuongea, na hata siku moja hajawahi kuacha kichwa na sehemu za uso wake wazi, kwanini…’ wakawa wanajiuliza mama na baba.
‘Kwani inakuhusu nini, ilimradi hana matatizo mwache alale, na kitu cha kuangalai ni huu ugeni wa mara kwa mara wa tu kuja ku…sijui kutibiwa au nini. Wengine hawana heri na sisi, uangalia sana…’
‘Sawa, lakini mbona imekuwa ni Baraka , kwani kile anayekuja na tatizo la mtoto wake lazima aache kitu, hele au unga, au maharage, sasa imekuwa ni neema kwetu…huoni huu sasa ni mradi wa familia..’ akasema mama wa kufikia wa mtoto.
‘Na nimesikia huyu mfanyakazi wa ndani hakai mchana kutwa, na anayemlea mtoto ni huyu mama, ni kweli au si kweli..’ akauliza baba mwenye nyumba.
‘Ni kweli, na nimesema mapaka nimechoka…’ akalalamika mama mwenye nyumba.
‘Mimi naona kama hataki kazi, basi huyo mama tutamlipa badala yake, siumesema anaweza kulea, na huhisi kuwa ana matatizo , basi …’
‘Baba nanihii…unasema nini, huyu mama ndio sioni matatizo yoyote, lakini hatuui huko alikotoka katokaje…hapana, kama huyo mfanyakazi hataki kazi, basi mimi mwenyewe nitakuwa nabaki nyumbani, kazi za kule nitatafuta mtu!
Miezi ikapita , mwaka ukapita, mtoto akawa mkubwa. Na mtu aliyekuwa akimlea huyo mtoto kwa muda wote ni mama wa mitaani, au mama mwenye mkono wa Baraka.
Siku moja alikuja mama mmoja akiwa na mtoto wake, alikuja baada ya kuelekezwa kuwa kuna mama mmoja ambaye, mtoto akiwa na tatizo la kulia, au kushituka usiku, basi mama huyo kwa kutumia mikono yake anamuombea, basi mama huyo akafika kweny hiyo nyumba na mtoto wake mgongoni. Alipofika hiyo siku, hakukuta wenyeji wengine, zaidi ya huyo mama, akamuelezea shida yake, na yule mama akamchukua yuke mtoto na kumshika kichwani, na kweli yule mtoto akatulia kule kushitukashituka.
Sijui ilitokea nini, kwani watu walioshuhudia walisema, walimuona mama huyo akitoa mbio, huku anapiga ukulele..Ikazuka minong’ono mingine kuwa mama wa mkono wa Baraka sio kweli wanavyohisi kuwa mkono wake ni wa Baraka, bali mkono huo ulikuwa eti mkono wa mtoto mchanga, na muonavyo sivyo ilivyo. Kutokana na mkono huo wa mtoto mchanga ambao ndio zindiko lake la uchawi, analoga usiku, anawanga kwa watoto, halafu mkija kwake, anajifanya kuwaponye, kumbe anaondoa mazindiko yake! Mazungumzo haya yalizuka juu kwa juu, na habari hizo zililetwa toka kwa mama huyu, ambaye alisambaza maneno haya kama vumvi katika jangwa…
`Hivi ilikuwaje mpaka ukagundua hilo kuwa mama huyo ni mwanga..’ wambea wakaanza kudadisi
‘Eti nini…hapana haiwezekani, kumbe ndio maana ni mpenzi wa watoto’; watu wakauliza na kuzusha ya kwao…
‘Huyo mama mkimuona alivyo hamtaamini, ni …yupo kama …ni mwanga huyu ndio maana yule mganga aliniambia kuwa kuna mama anatisha kama huyu mama…ndio yeye…hapana, simini, nimemgundua mbaya wangu, ndiye anayewawanga watoto wetu usiku, halafu anakuja kuwashika mkono, kuondoa uchawi wake na kusema anatibu…mumeliwa kweli, …’
‘Basi kama ni mwanga, lazima aondoke, ahamie huko alikotoka, nani anajua wapi alikotoka, huenda huko wamemfukuza, ndio maana akaja hapa kwa mbinu hizo…’ vijana wakaingizwa, na mipango ya kumhamisha ikaanza. Wema wote wa yule mama uliyeyuka kama barafu kwenye maji ya moto.
Siku moja usiku watu wakiwa wamelala, kikasikika kilio, kilio hiki kilitokea kwa nyumba ya wazazi wa kufikia wa mtoto, mtoto ambaye ndiye anayetuhadithia kisa hiki. Kilio hiki kilitokea kwenye chumba cha uwani ambapo mama wa mitaani alikuwa akilala. Chumba hicho sasa kilikuwa kizuri kwani wageni na misaada iliyokuwa ikiletwa, mwenyeji aliona akitengeneze vizuri kwa ajili ya huyu mama. Kilikuwa kilio cha muda mfupi halafu kukawa kimya, na baadaye moto ukazuka kutokea eneo hilo.
Wenye nyumba waliposikia kilio hicho walidharau wakizania kuwa huenda huyo mama alikuwa anaota, au maruerue yake ya kichwani yamempanda, na kwa vile kilitokea kwa muda mfupi, hawakuali, sana…lakini mosho ulipotanda ikabidi wazindikane na kutoke nje. Na walipotoka nje, walikuwa moto umetanda karibu eneo zima la chumba cha uani. Ikabidi heka heka za kuuzima ziannze na majirani wakaja, na bahati nzuri ukazimika.
‘Jamani kimetokea nini, na huyu mama anayelala hapa yupo wapi..’ ikawa watu wanaulizana
‘Au madawa ya kuwangia yamemzidi ikabidi yamlipukiea…’ wabaya wa huyu mama wakaanza visa.
Baba mwenye nyumba akajitosa kwenye chumba, kwani kulikuwa na ahueni kidogo, alitaka kuangalia usalama wa huyu mama. Alivunja ule mlango ambao ulikuwa bado na moto, akaingi ndani. Humo akatizama kitandani, na kumkuta yule mama kalala sakafuni, na kitandani kumjaa damu. Alimsogelea yula mama, na kumkuta akiwa katika hali mbaya sana, akamuinua na kuangalia kuwa bado yupo hai, na akagundua kuwa mapigo ya moyo bado yapo. Na hapo hamu ya kumfunua kile kitambaa anachopenda kujifunga usoni muda wote ikammjia.
Akakitoa taratibu, na kila hatua akawa anashangaa…baadaye akakivua kabisa, alishikwa na butwaa, akajikuta anadondoak chini na kukaa kwa muda, alirudi kumwangalia tena,…mungu wangu, huyu ni mtu au…mbona …hapana, akaaribu kupitisha mkono usoni kwa yule mama, ili kuona kweli ni sura ya mtu…na alipofanay hivyo, yule mama akazindukana, na haraka akakichukua kile kitambaa, akakivaa usoni,lakini kabla hajajifunga vizuri, akamkodolea macho baba mwenye nyumba, na…
‘Wanataka kuniua eti mimi mwanga…mimi sio mwanga jamani…nimewakosea nini walimwengu…’ akaanza kulia na hapo hapo akajifunga usoni na haikuchukua muda akadondoka na kuzirai.
Baba mwenye nyumba alishikwa na butwaa, alikuwa kama kazibwa mdomo kusema, na mwili wote ulikuwa ukitetemeka, na hakujua kwanini…alisema moyoni…ama kwelie dunia ni duara…siamini, ina maana kweli ndio wewe, mtu ambaye nilipa kwa mungu kuwa nikikutana nawe tena, …`ama zako ama zangu..’ leo upo name, nikufanye nini…mtu uliyeitesa roho yangu…hapana sio wewe…lakini mbona sura yako …hapana, sio wewe…lakini ndio wewe, siwezi kukosea abadani…macho yako…macho yako….popote nikiyaona nitakugundua tu…siamini…wewe ni mtu wa mwishi kutegemea kukuona tena!’Alijaribu kusimama akawa nguvu zimemusihia kabisa.
Aligeuza kichwa kumwangalia yule mwanamama, kwa wakati huu alikuwa kashajifunika uso wake, na ilionyesha wazi kuwa kazirai, na baba mwenye nyumba , kumbukumbu zikawa zinamjia na kumpandisha hasira , akatamani amumalize huyo mama, humo ndani ili watu wakiingia wajue alikuwa keshakufa, lakini Huruma ikamuingia, na mapenzi ya asili, mapenzi yale yaliyomfanya akose raha, mapenzi ambayo, yalimtesa miaka mingi , yakamwingia, …ikawa hasira, Huruma, mapenzi, …lakini hasira zikazidi kipimo, akachukua chuma kilichokuwepo humo ndani, akidhamiria kufanya lile alilokuwa nalo siku nyingi, kisasi…akainuka, akainua juu kile chuma, na kukiangalia kichwa cha yule mama….!
Jamani naona huko tuendapo kunatisha, ngoja niishie hapa!
Jamani wanadamu hawana wema, mama wa watu kageuka kuwa mwanga, je ilitokeaje baadaye!
Ni mimi: emu-three
8 comments :
Mmmmh! M3 sijui ni mimi tu au na wengine??? nahisi kama naanza kupotea, ilikuwaje kwenye chumba cha upasuaji????????? maana sijasoma tena sehemu inayoongelea kilichompata mgonjwa. Any way ngoja tusubiri what's next. keep ip up
Oh,naona mbinu niliyoitumia kwenye kisa hiki inawachanganya wengi...kama tutakwenda moja kwa moja na kuelezea nini kilitokea pale, itahistimisha kisa chetu,...naomba tuvute subira ili uone nini kimetokea hapo, lakini nini kimetokea hapo, ni siri ya hiki kisa ambayo itafichuliwa kinamna....!
Hata mimi nina mshawasha wa kujua nini kilitokea, bado nadadisi kichwani..KARIBUNI SANA
mh yule mgonjwa lazima alitoroka na ndo yule mama mwenye mkono wa baraka,tena Mungu alivyo mkuu kamuunganisha na mwanae,kama sikosei au vipi m3?
hii adidhi mwanzoni ilikuwa nzuri lakini kadri inavyoendelea inazidi kupoteza ladha sijuii ni mimi tu naona hivyo au nawengine hata hivyo nisikuvunje moyo unajitahidi ongera
Hiki kisa ni kirafu, na ndio hata mwanzoni nilipokiandika, nilikikatisha, kwasababu matukio yake ni mengi na yanagusa watu wengi, na kama nitakirahisisha hata ule ujumba hautafika...naomba mvute subira, kwani uzuri wake bado upo, na punde mtagundua kwanini ninafanya hivyo. Msijali na TUWE PAMOJA TU
Mkuu mimi ni mtunzi wa hadithi kama wewe, unavyokwepnda upo sahihi kabisa, ...unaandika kama picha, ikiwa inaficha jambo fulani, na likifichuka, basi ushafika mwisho wa picha...ni mtindo mzuri sana, na watu wengi wanapenda `ufupisho' kuwa tukio lijulikane ni nini...sio kwa mambo yote hasa ukiangalia `kisa' ambacho tunadhani ni cha kweli au nicha kweli.
Sasa ukitaka kuandika watu wanavyotaka, ukeli wa kisa unakuwa haupo. Nakuomba uwe katika msimamo wako, andika kama kisa kilivyo, usiyumbishwe, na huo ndio `utunzi' bora
BIG UP...Mimi nimekupata kabisa unalenga nini...
Inafanya mtu uvute fikra so ni kama chemsha bongo fulani, I like it sio unasoma hadithi kama unakunywa maji, lazima ukohoe kidogo haha! Mi nipo sambamba kabisa
nadhani sijachelewa ni kweli inatisha na pia inafikirisha. Mungu kweli ni muongozi.....
Post a Comment