Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, February 22, 2011

Kama hujui kufa, chungulia kaburi


‘Jamani mwanangu , jamani mwanangu yupo wapi…’ kilikuwa kilio cha mama mzazi ambaye alikuwa akimtafuta mwanae wa mwezi mmoja au miwili hivi, na kila mmoja alimwangalia kwa huruma, lakini nani wa kumsaidia kwa muda kama huo, kwani kila mmoja alikuwa akikimbia kivyake, ilikuwa kila mtu anakimbia kuiokoa roho yake kama vile anajua huko aendapo kuna usalama. Na kila mlipuko uliposikika, ulikuwa kama unavuruga akili za watu, na walichojua ni kudondoka chini, kama vile kalikwepa lile bomu na kulala chini, huku akishukuru mungu kuwa kaokoka na hilo bomu limpepita. Wengi walikumbuka kufanya hivyo, kulala chini pale unaposikia mlipuko,…

Nafikiri katika kule kudondoka chini kama unakwepa mlio wa bomu unaposikika na kulala chini na kuinuka tena, kutafuta muelekeo mwingine, ndipo yule mama mzazi kwa kuchanganyikiwa alijikuta akimwacha mtoto wake wa mwezi mmoja au miwili na kukimbia, na aligundua kuwa kamwacha mtoto wake, pale tu alipomuona mwenzake kambeba mtoto wake huku anakimbia mbele kwa mbele! Alijipapasa mwilini huku na huku akimtafuta mtoto wake, utafikiri mtoto huyo alikuwa kamganda mwilini mwake, alijipapasa huku akiuliza `mtoto wangu yupo wapi…’ na kabla hajapata jibu, mara mlipulo mwingine ukasikika tena, mama yule yule akasahau cha mtoto, au kumtafuta mtoto wake na kuanza kukimbia mbele kwa mbele!

Kuna usemi usemao kama hujui kufa chungulia kaburi…na kweli kama hujui vita basi jaribu kuangalia radi inavyopiga na kuchana-chana miti kama unavyochana karatasi vipande vipande! Ndivyo mabomu yale yalivyokuwa yakipasuka na kuchachana miti, na kila kilichopo mbele yake.

Na kwa akili yangu nikajiuliza huyu mtu aliyekaa na kubuni kitu cha hatari kama hiki alikuwa akidhamiria kumuua binadamu huyu-huyu, au kumuua nani, kwani binadamu ni kiumbe dhaifu sana, hahitaji kuundiwa chombo kikubwa kama hicho cha hatari, ili auliwe, kwani nyundo ndogo tu, au …kingeweza kabisa kutosha kumuua huyu mtoto wa adamu kama siku zake zimefika, unaweza ukamgonga na nyundo kichwani akafa, sasa huyo mtaalamu anatengeneza bomu, la kuangamiza….ambalo lina-angamiza hata kile kisicho na hatia…

Hali hii ilidhihiri siku ambayo wengi tuishio maeneo ya huku hatutaisahau! Ni pale mabomu yalivyokuwa yakilipuka na kila baada ya kutanguliwa na mwanga mkali. Na baadaye tuliona mabomu yale yakisambaa hewani kama vimondo, na kuelekea huku na kule na mengine yakija upande tuliopo au kwenda mbali usipopaona.

Mabomu hayo kwa yakini yalikuwa yakienda kutua ama kwenye makazi ya watu, au bahati nzuri yanatua kwenye uwazi. Mabomu mengine yalitupita juu na kwenda kudondokea mbele yetu na huko tulisikia kishindo kilichotetemesha aridhi na aridhi ikatoa upepo kama inapumua vile! Hebu jaribu kujiuilza ilikuwaje kwa wale wenye shinikizo la damu, kwani wengine walizimia, na wakazinduliwa na mlipuko mwingine ulipotokea! Wapo waliopoteza roho zao kwa sababu ya shinikizo la damu, ingawaje hakuguswa na hilo bomu!

‘Jamani tunakufa, yalaah masikini , mungu wangu, mama wee…’ Na mama wee, ilikua ndio nyingi zaidi, na wakati mwingine mama alikuwa karibu ya yule aliyeita mama wee,…lakini kwa muda ule , hata huyo mama naye alikuwa akilia kwa sauti hiyohiyo, ya mama wee, huku akikimbia na hakujua kuwa yeye ni mama, na mwanae anahitaji msaada wake!

Hivi ni vilio vilizidi kila bomu liliposikia likitoa sauti ya hasira, na wakati huo kila mtu kalala chini akiomba mlipuko mwingine usitokee, lakini ilikuwa kinyume chake. Milipuko iliendelea kama radi na kila mwanga ukitokea na moto kutanda hewani, kilichofuatia ni milipuko mkubwa uliotetemesha ardhi, na moto ule ulienea mbingu kwa miali ya moto. Na hali kama hii iliwafanya wengi kukimbia bila kujali kavaa nini, bila kujua wapi anapokwenda, na bila kujali kuwa mtoto wake , mke wake au mume wake kamuacha wapi, yeye anakimbia kuiokoa roho yake.

‘Ilikuwa kuwaje, ..’ ni swali ambalo kila mmoja alipoulizwa baadaye, aliweza kutoa hadithi ndefu ya kusikitisha, kwani ilivyotokea ilikuwa kama mchezo wa kuigiza.

Ilikuwa muda wa saa mbili hivi na kitu, wengine walikuwa ndio wanapakua chakula, wengine walikuwa wakisikiliza taarifa za habari, mipira nk, wengine walishaanza kulala na wengine walikuwa wamekaa mezani wanasubiri mama watoto akiaandaa hiki au kile, ilimradi kila mmoja alikuwa katika shughuli yake ya usiku , na hapo hakuna aliyejua kuwa Mungu yupo, atajuaje kuwa Mungu yupo wakati nafsi imesharidhika kuwa siku imekwisha na muda wa kupumzisha miili yao umekaribia, ….lakini ghafla shughuli hizo zilinyamazishwa na mlipuko mkali na mwanga mkali uliotanda mbinguni. …

Mimi na familia yangu Tulikuwa ndani tunaangalia tamithilia ya `Marchui’ ..`Don’t mess with My angel,…’ na kipindi hicho tulikuwa tukiombea umeme usikatike tena, kwani muda wa siku kadhaa tumekuwa tukiikosa hii tamithilia kwasababu ya kukatika katika kwa umeme,na kukatika huko hakukufuata kabisa ratiba ya mgawo. Na wakati mawazo yetu yamezama kwenye runinga, tukasikia sauti kubwa ikitokea angani, kwa mawazo ya haraka tulihisi mlipuko huo umetokea angani, na huenda ni radi, lakini kwa utani swote tukasema `kuna ndege imelipuka juu nini?’

Kabla hatujapata jibu, milipuko mingine ikasikika na ikisindikizwa na vilio vya watu, hapo tukaona sio kitu kidogo kama tulivyodhania, mara moja tukatoka nje kuangalia hewani, na kweli tuliona moto ukipaa kwenda hewani na mwanga mkali ukiwa unamulika kwa mbele yetu , na kwa umbali ule tulisema kama ni ndege itakuwa imeangukia maeneo ya Gongolamboto, ambapo sio mbali kabisa na tunapoishi. Lakini kabla hatujasema kitu zaidi, milio ya milipuko mingine mikubwa ikasikika , tena na tena, na mbingu ikapambwa na miali ya moto

‘Kama ni ndege imelipuka, inaweza ikarusha mabaki yake hadi huku, na ikadondokea kwenye nyumba italeta madhara, tuwatoe watoto nje….’ Akasema mke wangu, sikumbishia ingawaje mimi nilishahisi sio ndege pekee, kuna zaidi ya ndege na bila kumbishia tukarudi ndani kuwatoa watoto nje!

Kilichofuata ni kuingia ndani na kuwatoa watoto ambao walishaanza kulala, kwani kwa kawaida siku za shule tunawalazimisha watoto walale mapema, na kwa vile umeme ulikuwa hauna nguvu, tunawazuia wasisome ili wasije wakazurika macho yao. Watoto wakawa wanauliza kuna nini, lakini hawakupata jibu la haraka hadi walipotoka nje na kukutana na milipuko mingi iliyokuwa ikitanda hewani na mwanga mkali wa moto.

Wakati tunawatoa watoto, nikakumbuka utani wa jamaa mmoja kwenye daladala, akiwaasa wakazi wengi wa Dar, kuwa wasipende kulala uchi, alidai kuwa wakazi wengi wa Dar wanapenda kulala uchi…alisema `jifunzeni kulala na nguo hata kama ni wanandoa, kwani huwezi jua lini litatokea la kutokea, unaweza ukajikuta unatoka nje uchi!

Sio kama nachekesha watu, kwasababu hili tukio lilitokea kweli, mama mmoja aliyejaliwa umbo kubwa(mnene) yeye alitoka nje akiwa katokea kujipumzisha, na kwasababu ya joto au ndio utaratibu wake, au alitokea bafuni hatujui, yeye aliposikia mlipuko huo na vilio vya watu, alichokumbuka na kuchukua upande wa khanga, na khanga kwake ni ndogo….atajifungaje hiyo khanga wakati mwilini wake ni mnene zaidi ya ile khanga. Hata hivyo hakujali, khanga ile akaiweka begani, mbio… hakukumbuka kuchukua nguo yake maalumu anayovaa kwa dharura, hakukumbuka kuwa yupo uchi, alichokumbuka ni kukimbia kuikoa roho yake.

Alipotoka sebuleni, wenzake walishatimuka, basi na yeye akatoka nje mbio, uchi…hadi barabarani, akakutana na umati wa watu ukiwa unakimbia…hakuna aliyekuwa na mawazo ya kumtizama mwenzake kavaa nini,…yule mama naye akaungana na watu wanaokimbia, hajui kama yupo uchi…na bahati mbaya nyuma yao likawa linakuja gari, ambalo lilikuwa likimulika taa, ukumbuke ni usiku, umeme umeshakatwa, giza totoro, na mwanga unaosaidia na hiyo milipuko ya mabomu…sasa lile gari likawa linammulika kwa nyuma, na watu wapo mbele wanakimbia, ule mwanga ukawa unammulika yeye, kwasababu alikuwa nyuma yaw engine na waliopo ndani ya lile gari, ambalo lilijaza hadi kwenye carrier, walikuwa wakimuona.

Watu waliopo ndani ya lile gari kwa muda ule wakasahau ile dhahama , wakawa wanaangalia picha, isiypofaa kwa watoto wadogo, wakawa wanamtizam yule mwanamama, mnene kweli, na baya zaidi yupo uchi, na jinsi anavyokimbia na ule unene wake ikawa ni kivutio cha muda, na bahati nzuri mama mmoja aliyekuwa karibu naye, akamuona huruma na akajitolea kumfunga khanga yake haraharaka, lakini khanga gani ingemtosha yule mama…na mwingine akatoa kitenge chake, lakini wapi, na hata hivyo kabla zoezi hilo halijakamilika, milipuko ikawasambaratisha na kila mmoja alitafuta njia yake…!

‘Mungu wangu wee, nini hiki jamani…baba kumetokea nini, mbona mbingu inawaka moto…’ watoto wakaanza kulia na kabla hatujawaelezea nini kimetokea, milipuko iliyochana mbingu kwa sauti,ikawanyamazisha kwa muda, na milipuko mingi ikafuata tena na tena na wote wakaaanza kukimbia, ilibidi nifanye juhudi ya ziada kuwazua, kwani nilijua nikiwaachia watakimbia na kupotea, ….

Akili ya tukio la Mbagala ikanijia kichwani, nikajua wazi ni yale, yale, na muelekeo wake unaonyesha kuna kitu kimetokea kama kile kile cha Mbagala. Niliwaza tukio lile kwa haraka kichwani jinsi watoto walivyopoteana na wazazi wao, ilibidi nitumie lugha ya busara kuwatuliza kwanza, kwa kuwaambia kuwa huko wanakokimbilia hakuna usalama, kwani hayo ni mabomu yanalipuka na hatujui yanapodondokea! Cha muhimu tuangalaie kwanza yanavyolipuka kutoka wapi na yanakwenda muelekeo gani ili tujua wapi pakukimbilia..

Siwezi kujisifia kuwa niliingiwa na ujasiri kiasi hicho…, hapana, hakuna angekuwa na ujasiri kwa muda kama ule, ila nilijiuilza kama nitakimbia na kuiacha familia yangu , na kila mmoja akakimbilia upande wake, nini kitafuta baadaye, …nitakuja kuhangaika zaidi , na ningelikuja kujijutia maisha yangu yote kwa kuwaachia watoto na familia yangu ikimbie ovyo. Nikamuomba mungu familia yangu iwe pamoja nami.. Kwa kweli nikikumbuka hiyo hatua ya kuwashawishi familia yangu isikimbie na pale ninapoangalia runinga jinsi wenzangu walivyopata shida kuwatafuta watoto wao baadaye, machozi hunijia machoni!.

Kwa ujumla hakuna aliyependa familia yake isambaratike, ikimbie ovyo kwa muda kama ule, hamna aliyekuwa na ujasiri au ujanja muda kama ule, na yule alaiyebahatika kufanya kama nilivyofanya mimi na familia yangu asije akajidanganya kuwa alikuwa mjanja. Ni uwezo wa yule ambaye hatumtambui kimatendo wakati wa raha, tunamtambua kimaneno tu na mara nyingi tunamtaja na kumuomba kwa muda kama ule ambao unapata janga ambalo huna uwezo nalo tena!

‘Baba unasema ni mabomu yamelipuka, ina maana kuna vita, kwani kuna vita…ina maana hayo mabomu yatatudondokea , na tutakufa…yakidondokea huku nyumba yetu itavunjika, …kwani yakidondoka hapa hatutaumia…’ ikawa maswali mengi huku vilio vikitanda hewani. Na watu wakawa wanatupita bila kututambua tena, nani angemtambua nani, wakati kila mmmoja ameshindwa kuitambua familia yake, anachotambua ni roho yake tu…na walipotuona tumezubaa tukiangalia hewani, wakapiga ukulele.

‘Jamani msikimbie ovyo, hayo mabomu hayawezi kufika huku…’ akasema jirani yangu mmoja akiwa anatusogelea pale tulipo. Nikamuunga mkono, na kabla hajatufikia, milipuko mikali ikasikika na ardhi ikatetemeka,… Nikaangalia angani kuhakikisha kweli hayo ni mabomu, au kuna nini zaidi. Nilipogeuka kumuulizia mwenzangu, nikamkuta keshakimbia, hayupo nasi tena.

`Tukimbieni jamani mabomu hayo yanalipuka kama ya Mbagala….’ Nikasikia sauti nyingine ikisema. Na kweli hali ilionyesha hivyo, kuwa ni mabomu yanayolipuka, nan i zaidi yay ale ya Mbagala. Watu wakawa wanatupita kama mishale. Na familia yangu iliposikia hivyo, ikavutika kukimbia, lakini nikaizuia na kuwambia `huko wanapokimbilia ndipo mabomu yanapodondokea subirini kwanza….’

Watu walikuwa wakikimbia mbele, na wakisikia mlipuko wanarudi nyuma, kwani wengine walikurupuka toka majumbani mwao na kukimbia na hawakujua kama ni mabomu yamelipuka toka wapi, na hawakujua wapi waelekee, na wakisikia mlipuko wanalala chini na wengine wanarudi walipotoka, na wakisikia mlipuko mwingine tena wanakimbia kuelekea kwingine, na jinsi vimondo vya mabomu vinavyopita hewani, ndivyo watu walivyozidi kuchanganyikiwa, kwani haikujulikana wapi yanapotua hayo mabomu. Lakini kila mmoja aliona ni bora kukimbia mbali na huko mabomu yanapotokea…!

Ilishadhihiri kuwa mabomu hayo yanatokea muelekeo wa Gongolamboto, na usalama ulio-onekana ni kukimbia mbali na huko yanapotokea na mbali kwake ni kuelekea mjini.

Haijakaa sawa tukasikia mengine yamedondokea mita chache kutoka tulipo, nikasema sasa hapa hapakaliki, nikawambia familia yangu tusogee mbele kidogo mahali ambapo tunaweza kuona vyema kule yanapoanzia,…na kweli tukawa tunapaona vyema kabisa, mlipuko unavyotokea huanza kama moto mkali kuwaka na kuangaza mbingu, na kinachofuatia ni mlipuko ,na mabomu yanaruka hewani na kusambaa juu, na kueleeka sehemu tofauti tofauti, na ile hali ilikuwa haiangaliki, kwani moto mkali ulikuwa umetanda hewani, huku milipuko ikiendelea kutokea, na mabomu yakiruka hewani .

Tulijitahidi kuangalia , na familia yangu ikawa imeshikwa na fadhaa, na mshituko, hasa ule ukali wa moto ulivyo, na mlipuko unavyokuwa mkubwa, kiasi cha kuathiri ngoma sikio! Tukajitahidi kwa muda kuangalia yale mabomu yanavyotoka kule na kueleeka hewani na kila mlipuko unapotokea tuliangalia yale mabomu ambayo yalikuwa ni moto unaowaka juu kama nyota ndefu, inayopaa juu mbinguni, na kuifuatilia wapi inapotua.

‘Jamani tukimbieni , msisimame tena hapa, yanakuja huku hayo mabomu, hamuoni kusimama hapa ni hatari, kuna moja limedondoka karibu na nyumba yangu, huku hapakaliki tena…’ jirani yangu mmoja akatokea , akiwa katika harakati za kukimbia, na watu wengine wanatupita wakikimbia wao na familia zao, wamebeba watoto, wengine vifua wazi na wanawake wakiwa na khanga moja, bila kujali kuwa huko wanapokimbilia watahitaji nguo.

Hakuna aliyekumbuka kufunga milango, hakuna aliyekumbuka kuwa ndani kaacha nini, na hakuna aliyekumbuka hata kuchukua nauli, ilikuwa mbio na yeye…nyumba yenye thamani kwa kila mmoja ikawa inakimbiwa, kwa muda ule ilikuwa haina thamani tena…

Mimi nikaiambia familia yangu isichanganyikiwe kwanza, tuangalie wapi hayo mabomu yanapoelekea, pili ngojeni nifunge milango, kwasababu hatujui tunakimbilia wapi na huko tutakaa kwa muda gani,… ilikuwa kazi ngumu kuishawishi familia yangu, kwani walishawaona wenzao wanakimbia kuelekea kusikojulikana, ni mbele kwa mbele , …hata mimi nilitamani kukimbia, lakini …., baadaye familia ikatulia wakawa wananifuata mimi jinsi ninavyowaelekeza.

‘Sasa twendeni sehemu ya wazi mbali na majengo, …’ tukasogea hadi sehemu iitwayo Moshi bar, hapa kuna barabara kuu ielekeayo Mombasa, na wazo lilikuwa kama serikali imeligundua hili mapema, inaweza ikatoa magari ya jeshi tukapata misaada, lakini wapi….

Hapo Moshi Bar tukawakuta watu wamelala chini, kila mmoja akihaha kivyake, hapo hakuna cha familia au mtoto, kila mtu la lake na familia yangu ikafuata hivihivyo,ikalala chini, kama vile kuna amri imetolewa, ikawa kila mlipuko ukitokeaa watu wanalala chini na vichwa chini….

Jinsi muda ulivyokwenda na milipuko ndivyo ilivyozidi na tulidhani haitaisha kamwe, na tuliona kama vile ile milipuko inalipuka na huku inasogea mbele kuja huku tulipo, na baya zaidi tulishuhudia mabomu yakitua sio mbali na hapo tulipolala, na kumbe mengine yalikuwa yameshadondokea ndani ya jengo la Moshi bar, lakini halikuleta mlipuko au kubomoa hilo jengo. Kwa muda ule wengi tuliokuwepo hapo hatukujua wapi tuende au tufanye nini, kwani huko wanapokimbilia wenzetu, ndipo mabomu mengi yalipokuwa yanaelekea

‘Kwanini milipuko imekuwa mingi hivyo, na kumetokea nini huko, na inawezekana ni kambi ya Gongolamboto….’ Akasema jamaa mmoja. Hakuna aliyeweza kutoa kauli au jibu, hata uwongo uliogopwa kusemwa kwa muda ule. Kwa jinsi milipuko ilivyokuwa mingi, mbingu ilikuwa inatoa mwanga, na kwa jinsi ilivyoonekana, milipuko hiyo ilikuwa haina ukomo, …

Swali likatujia tufanyeje…maana hatari inazidi kutukaribia…hakuna aliyetoa rai, hapo kila mmoja akainama na kumkumbuka mungu wake kwa imani yake,…angalau hayo mabomu yapite tu hewani yasitudondokee pale tulipolala. Tutakwenda wapi tena, na kama ndio Muumba keshaamua kuwa mwisho wetu uwe hivyo, basi yote ni mapenzi yake!

***

Ilianzia saa mbili au tatu kasoro, hadi saa sita hakuna aliyekuwa na uhakika wa maisha yake, na wale waliobahatika kukimbia walikuwa wameshafika mbali sana, kama hawakukutwa na majanga njiani hatukuwa tunajua wapi na nini kitawasibu huko, huenda ndio salama yao wenzetu wamepona, kuliko sisi tuliobakia hapo…

Na wengi waliotuhadithia kesho yake walisema walikimbia hadi Tazara, Buguruni nk sehemu ambayo kesho yake alipoambiwa arudi , ilibidi atafute daladala, na ukumbuke wengi waliondoka bila nauli bila viatu, na wengine wamevaa nguo ambazo hazikufaa kuvaliwa mbele ya kadamnasi!.

Baadaye ile hali ya milipuko ikawa inapungua, lakini vilio vya watu vinaongezeka, kwani akili zilishaanza kurejea na tafakari za nini kimetokea na je familia yangu ipo wapi, ipo salama au ndio…zikaanza kurejea kwa muda huo kwa wale waliobahatika kuhifadhi simu zao wakijaribu kuwasiliana na ndugu zao, (Wapo waliotupa simu zao, wakiona ni mzigo…) ! Watu wakaanza kupigiana simu, kuuliza jamaa zao wako wapi, wengine wakawa wanapokea simu, wakiuliziwa kuwa wapo salama…. Wengine wakiulizia watoto wao au jamaa zao, …lakini hakuna aliyejua nanii kaenda wapi! Na je kuna usalama au ndio mapumziko mafupi!

‘Zimeni simu..wametangaza kuwa simu ni hatari kwa mabomu..’ Watu wakawa wanasema, na kweli wengi wakazima simu zao.

‘Jamani watoto wangu siwaoni, jamani ….’ Ikawa sasa ya mtafuatane kila mmoja anahangaika kumtafuata jamaa yake lakini haikuwa kazi rahisi. …

                                                                    ******

Ilipofika saa sita usiku, hali ikawa imetulia kidogo, ikabakia watu kutembea huku na kule kuangalia usalama, na ikisikika milio midogo midogo watu wanalala chini. Kuna wale ambao walishuhudia mabomu yakitua nje ya nyumba zao au maeneo ya wazi, na kuna moja lilitoboa ukuta wa nyumba na kuingia ndani halafu likatokea ukuta mwingine na kwenda kuzama aridhini. Ila moja baya sana lilikutana na mtu akiwa katokea mlangoni, na kumchanachana vipande……

‘Sisi tulikuwa tumetokea mbali sana, tukaja kwenye hii nyumba, tukaona tupumzike kidogo, mara tukasikia mlipuko, tahamaki ukuta ukatudondokea na hatujui kuwa waliofukiwa kwenye ukuta huu ni wangapi..’ akasema jamaa mmoja akionyesha ule ukuta . Watu walijaribu kuuinua lakini haikuwa rahisi. Baadhi ya maiti zilitolewa humo, na matukio mengi kama haya yakusikitisha yaliarifiwa kutoka kwa jamaa walioshuhudia.

Hiki ni kizaa zaa cha mwaka, kwani kila mmoja hakuiamini nyumba yake mwenyewe, wengine kwa kuchanganyikiwa waliona nyumba ya mwenzake ni bora kuliko yake. Kwahiyo anakwenda kujificha kwa nyumba ya mtu mwingine, mpaka watu walipoambiwa usalama sio kujificha kwenye nyumba, ni kuhakikisha unakaa sehemu ya wazi ambayo hata jengo likidondoka kwa bomu hatapata madhara na bora ni kulala chini.

Yaliyotokea siku hiyo ni mengi, lakini kwa namna moja, labda niwalaumu sana wana usalama, kwani katika hali kama ile wangejaribu kupita na vipaza sauti na kuwaambia wanachi wafanye nini. Nilipotoa hiyo hoja jamaa mmoja ambaye alionekana ni askari akasema, `hali kama ile hata huyo askari alikuwa akitafuta sehemu ya usalama, atakuwa na muda kweli wa kupita akitangaza, wakati hajui bomu litatua wapi

Ni kweli, lakini kuna watu ambao kwa nia mbaya walikuwa wakisambaza uvumi, ambao uliwazidi kuwachanganya na kuwaogofya watu. Kwa mafano kuna uvumi kuwa, ule mlipuk ulikuwa ndio kianzio unakuja mkubwa zaidi kwani huko maghala yote ya silaha yamagubikwa na moto, kwahiyo watu waondoke haraka.

Nini kilichofuata baada ya uvumi huo, ilikuwa mshikemshike watu walizidi kukimbia ovyo, bila kujua wapi wanapokwenda na wapi kwenye usalama, na matokeo yake ndiyo hayo, watoto kupotoea, wengine kuumia na wengine kufa, wakiwa wamejificha ndani ya majumba yao, au ya watu wengine. Taarifa ya uhakika ungeipata wapi, kama mtunza usalama naye `kala cover’

Tunajua kifo ni kifo, na ukipangiwa kuwa utakufa utakufa tu, hata kama ulifuata msharti hayo, lakini hata hivyo, kinga ni bora, na iliyo bora ni kujua nini ufanye ili kujaribu kukiepuka hicho kifo, kuliko kukimbia ovyo na hujui nini cha kufanya. Walipoteza maisha sio wajinga, na hawakujua kabisa kuwa maisha yao yangeisha kwa namna hiyo. Lakini kila jambo hutokea ili iwe fundisho. Na hii kweli ilinikumbusha kuwa kwa vyovyote iwavyo, mwisho wa maisha ya binadamu ni umauti, lakini je yatakuaje…!

Hii sio mara ya kwanza kwa tuklio kama hili, nilitegemea kuwa wahusika wa usalama wa raia wangelikuwa wamejiandaa vyema kuwasaidia wananchi baada ya tukio la Mbagala, hasa kuwaapa taarifa za haraka, nini kifanyike, na magari au huduma za usafiri kuwepo, lakini hutaamini watu walikimbia umbali mrefu bila kujua wapi wanakwenda wakiwa na watoto, tena watoto wadogo, ….!

Nakumbuka kesho yake watu walikuwa wambeba watoto na mizigo yao kama wakimbizi wakihama majumba yao, wengi wakisema imetangazwa kuwa ikifika saa tano yatalipuka mabomu tena, zaidi yay ale ya usiku, kwahiyo watu waondoke maeneo na kuelekea uwanja wa sabasaba huko mjini. Sasa magari yapo wapi, watu watafikaje huko, hasa watoto, wazee, wagonjwa, akina mama watasafirije..,

Kilichotokea siku hiyo ni kufa kufaana, wenye boda boda wakapandisha dau, sehemu ndogo tu ya safari elifu hadi elifu tatu, kutoka Moshi bar hadi Mombasa na ukibahatika kuipata taxi ni zaudi ya elifu sita hadi kumi, magari ya daladala ndiyo hayakuwepo kabisa, labda malori!

Mji ukaanza kuhamwa, na waliobahatika kurudi nyumbani kukusanya chochote walifanya hivyo, lakini wengine hawakutaka hata kuiona nyumba yake, ikawa yeye na kutafuta usafiri huku hana nauli mfukoni!

Hili linatupa fundisho jingine, kuwa vita sio mchezo, vurugu na uchochezi wa vurugu ambao utaishia kuleta vita sio jambo la kuombea, na hili litafanikiwa tu pale uadilifu wa uongozi, utakapokuwepo, kwani matukio kama haya yanapotokea utakuta wengi wanaoumia ni raia wasio na hatia kabisa, na mwisho wa siku wanafaidi ni wachache…jamani kama kweli hatujui ubaya wa vita basi hilo tuliloliona usiku huo ni utangulizi tu wa kinachoitwa vita…

Usione watu wanakimbia nchi yao waliyoipenda, usione …hakuna wanaopenda iwe hivyo, lakini kama kweli tunahamu na hicho kinachoitwa vita basi waulize wanachi wa mbagala, waulize wananchi wa Gongo lamboto, …maana kama mtu hujui kufa uchungulie kaburi…!

                                                                           ****
NB Kuna usemi usemao, akufaaye kwa ziki ndiye rafiki wa kweli na kwa kiingereza husema ; friend in need is a friend indeed. Tunawashukuru sana wale wote waliokuwa karibu na wahanga wa haya mabomu kwa misaada, kufaraji na kuwa karibu nao, kwani kilikuwa kipindi kizito, kigumu na cha kuogofya. Wengi walishakata tamaa ya maisha, fikiria mtu kufikia hatua ya kumtelekeza mwane bila kujua, sio jambo dogo!



Tunawashukuru sana Tanesco, kwani tangu litokee hili janga, wamekuwa nasi bega kwa bega, kwa kujua umuhimu wa sisi kuwa na umeme, kwani kukiwa na giza, unaweza ukajikuta unalikwaa bomu lililojificha, sijui wamefanya hilo kwa nia yao njema au kwa shinikizo,lakini kwa vyovyote vile iwavyo, kweli mumeonyesha ubinadamu wa hali ya juu. Wananchi wengi katika harakati hizo wamejikuta wakiwa masikini, licha ya kuwa hakupata majeraha au kuvunjiwa chochote, lakini biashara zao zilisimama, pesa nyingi ilitumika, na jeraha la moyo, ambalo huwezi kulizipa kwa thamani yoyote! Na wengi wamewekeza katika shughuli zinazohitaji umeme!


Tulitarajai waajiri wengi wangekuwa mfano wa kuigwa, kwa wafanyakazi wao, kwani wapo wenye wafanyakazi waliotokea maeneo hayo ya Gongolamboto, na hali yenyewe ya kipato inajulikana, sijui kuna ambao wamewapa wafanyakazi wao chochote,angalau hata `mkopo’ sijui...! Kama wapo wamepata bahati hiyo, basi hiyo kampuni, inastahili pongezi,…Misaada hutolewa kibiashara zaidi sio kiutu, kwani kama atamsaidia mfanyakazi wake mmoja au wawili walitaabika na janga hilo watajulikanaje , naye anataka atoe kwa kujitangaza, ili afaidike kibiashara!  Sawa kama nilivyosema, rafiki wa kweli ni yule anayekujali wakati wa shida, wewe mfanyakazi ni `mzalishaji’ tu na ubora wako ni ukiwa mzima…twashukuru sana, kwa wale walioona huruma na kwa utu wema wakawasaidia wahanga wa haya mabomu!.


Ni hayo tu kwa nyongeza

Ni mimi: emu-three
Enhanced by Zemanta

11 comments :

Anonymous said...

Poleni sana jamani ndugu zangu, kwa kweli jinsi ulivyosimulia ni kama vile kiama. Inabidi sasa tuzidi kumcha Mungu maana kwa wale tu wamchao Mungu wanaweza kuwa na ujasiri uliokuwa nao, ulimtanguliza Mungu mbele naye alikuongoza. Nakumbuka siku moja nilikuwa ndani ya daladala ikapinduka hapo Kibasila kwenye mtaro, nilichokifanya ni kuomba tu kwa Allah Subhana wa Taala nikajisemea eeh ya Allah maisha yangu yako mikononi mwako sina uwezo hata kidogo kiumbe mie zaidi ya kukutegemea wewe na kama haya ni mauti yangu basi niko tayari Alhamdullilah! Pale pale nikapata wazo la kujiweka kama mtoto aliye tumboni kwa mama yake yaani nilipostuka watu wanapiga mayowe, damu kila mahali nikatoka salama nilichopoteza ni simu tu basi. Kweli Mungu mkubwa!

malkiory said...

Inasikitisha na kuhuzunisha. Cha ajabu ni kwamba hadi leo waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga taifa pamoja na mkuu wa majeshi wanaendelea kupeta badala ya kujiwajibisha kutokana na uzembe.

Pili, sikufurahishwa na hotuba ya rais kuhusu tukio la Gongolamboto, nadhani haikuwa sahihi kwa rais kutumia maneno ya mtaani kama vile redio mbao na pia kusema jeshi limepata hasara. Badala ya kusema watu wamepoteza maisha na kupata harasa ya mali na nyumba.

Simon Kitururu said...

Poleni sana jamani!

EDNA said...

Duuh!inasikitisha kwa kweli hadi machozi yananitoka...

Rachel Siwa said...

Pole kwa wahanga wote na waTanzania kwa ujumla!siju nini mwisho wa haya mambo,maana wakubwa wanaenda kutalii tuu kwenye tukio!!!!!!Mungu ibariki Afrika,Mungu ibariki Tanzania!.

Yasinta Ngonyani said...

Poleni sana kwa kweli yaani kama vile ndoto nasoma na huku machozi yanadondoka. Nmshukuru Mungu kuwa kuwa upo nasi na pia wengine pia wapo salama. Jamani kwanza Mbagala na sasa hili vipi.Nashindwa kuendelea kusema nimebanwa na hasira..pia uchungu...

emu-three said...

Nashukuruni sana kwa pole zenu majirani zangu, na namshukuru mungu kuwa tupo salama, na huenda wakafanikiwa kuyakusanya mabomu yote yaliyodondoka maeneo tunamoishi, kwani kati ya huenda kuna ambayo bado mazima!

Anonymous said...

Mmmmmmmmmmh! Its too sad.!!!!!! God bless U & your family & all of them. God still you protect u. Protect your country Tz.

Thx God, All the Best.

**********

About your story, u tell us. 2day I know u, your gender.

Thx

Mzee wa Changamoto said...

Na hi ni NAFASI YA PILI
Poleni saana wandugu.
Poleni

Faith S Hilary said...

Hili tukio lilikuwa na kusikitisha kweli na imeonyesha jinsi gani hawa watu wa hukoooo...walivyokuwa wazembe, tunaomba Mungu tu yasitokee tena kwa mara ya tatu ama zaidi kwasababu haya maghala ya mabomu yapo sehemu nyingine jijini.

Story imenigusa kwa kweli, nimepata picha halisi japo sio picha ya kamera lakini kichwani na kufikiria jinsi gani watu walikuwa haelewi cha kufanya. Dada yangu nyumbani kwake nyuma kulianguka bomu pia...yaani hata kama mtu haukuwepo hapo eneo la tukio, sisi wa huku mbali tulikuwa roho juu kujua ndugu zetu vipi. Mungu atunusuru tu kwa kweli.


PS: Anonymous 2:36 umenichekesha ile mbaya! hahaha Naona kwasababu M3 hajaweka picha ama kuzungumzia kuhusu yeye binafsi basi watu wanakuwa hawajui wamuite dada ama kaka...M3 umeona hiyo? Ni wazo tu na sidhani kama anonymous hapo juu yuko peke yake ambaye yuko confused kidogo...no offense :-). nipo!!

Mzee wa Changamoto said...

Candy1 kasema "nimepata picha halisi japo sio picha ya kamera lakini kichwani na kufikiria jinsi gani watu walikuwa haelewi cha kufanya."
HILI SI DOGO
ASANTE