Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, January 25, 2011

Fasta fasta...!


Utoto una mambo yake, nakumbuka siku moja tukiwa shuleni, shule hizi za kulala bweni, tulimkuta kuku porini, rafiki yangu anayetokea huko kusini mwa Tanzania, akaniambia tumkamate yule kuku tumchinje, tupate kitoweo. Akilini mwangu nikawaza , na kukumbuka hadithi za babu kuwa ukila kuku wa watu mwenyewe akikuloga kuku atakuwa akilia tumboni, siku zote…nikaogopa.


‘Wewe kaa upande ule, tumkamate tupate kitoweo haraka, usizubae(siku hizi inaitwa fasta fasta)! Nilikawa najifanya kumkamata huku nategea akimbie, na kweli alikimbia, na hatukufanikiwa kumkamata. Ikawa heri yetu, inagwaje rafiki yangu alinilaumu sana. Ndio kawaida yetu, ukipata wewe ni mshindi ukikosa …lawama!

Leo wakati nahangaika na usafiri gari la daladala likatukosakosa pale kituoni tuliposimama, limetoka barabarani linapitia eneo wanaposubiri abiria, kukwepa foleni, na ili wafike huko mjini haraka iwezekanavyo…(fasta fasta)! Tuliokuwepo pale tukamzomoa yule dereva, wakati waliopo ndani ya basi wanamshanglilia anavyokatisha barabara, kwasababu wanawahishwa huko wanapokwenda fasta-fasta.  Nikawaza hii haraharaka ina mawili kupata au kukosa, heri ukipata utajipongeza na kuuona huo utaratibu ndio unaofaa, na utaupigia mstari mkubwa, hata kuutafutia mahala pa kujilinda kwenye katiba, lakini ukikosa kuna mawili, kuishia pabaya au kupata ajali. Heri uishie pabaya tutajua kuwa sheria imafuata mkondo wake, lakini ukipata ajali kuna mawili, watu kupoteza maisha yao, au kuharibikiwa na gari na itakuwa mwisho wa ajira…

Wakati nawaza haya nikakumbuka mdahalo wa katiba kule chuo kikuu, wakati tunautizama, mama nanihii akaniuliza mbona yule mtu anaongea kwa kujiamini kiasi kile, haogopi kukamatwa, mpaka anasema …kamuajiri shemeji yake… Sikuweza kumpa jibu la haraharaka kwasababu nilikuwa bado nasikiliza maelezo yaliyokuwa yakitolewa. Lakini akilini kwangu nikawaza kuwa wengi bado wana ile kasumba `yakuogopa kukamatwa’ hata pale tunapotaka kusema `ukweli’. Lakini ukweli halisi unaotokea barabarani, au mitaani, au enzi za shule za kukamata kuku wa watu wanafanya kivitendo, mbona hatuugopi! Ndio hayo maisha ya kutaka vya harakaharaka(fasta fasta)!

Wakati mjadala unaendelea kwenye runinga, mzee mmoja aliyekuwepo nasi akasema, `hivi hawo wanaosikiliza ni wanafunzi au ni vijana wa mitaani’ nikageuka kumwangalia yule mzee kujua ana maana gani. Aklasema, mbona sioni tofauti yao na vijana wengine. Anasimama mtu wanazomea, anasimama mtu wanashangilia, hata kabla hatujasikia hoja ya huyo mtu, haya nayaona kwenye mikutano ya watu wa kawaida, sikutegemea kuyaona mahali kama pale. Je huyu wanayemzomea akizungumza mambo ya maana watasemaje, au akiamua kukaa kimya, na alikuwa na hoja nzuri sana, hawaoni kuwa wamekosa la muhimu…na huyo wanayemshangilia akitoa hoja inayokwenda kinyuma na hicho wanachomshangilia nacho watasemaje?...’ akaniangalia mimi niseme kitu, lakini nikageuka kusikiliza watoa hoja.

Mjadala wa katiba umeanza, na nashukuru sana walioweza kuuanzisha vyema ni hawo waliouandaa hapo chuoni na hata ukaweza kurushwa hewani, na nashukuru kuwa waliwachagua watu wanaokubalika na jamii kuwa wanazungumza ukweli, … ingawaje mijadala kama hii ilishaanza, ila kwa vile walioanzisha mwanzo hiyo huenda walikuwa hawakidhi haja ya `warushaji ‘na kama tujuavyo, mpenda roho hula nyama mbichi, ..sio kila watakaozungumza wataonekana wema, hata kama wakizungumzacho kina wema ndani yake, lazima wapewe kipaumbele wale `wanaotoa hoja zenye kukubalika ama na jamii au na maslahi yetu’ Hilo tuliachie hapa kwanza.

Lakini mimi, kilichonifanya niandika hapa hii leo ni ile hali aliyozungumza mzee wetu hapa, kuwa kama `wasomi’ tuonyeshe mfano, kwakweli mumeonyesha mfano wa mjadala wa wazi na uwazi hiyo haina shaka. Lakinii kuna mambo ambayo tunatakiwa sote tukubali, kuwa kwenye mjadala, tushangilie hoja, au tubeze hoja, tusimzomee mzungumzaji hata kabla hajazungumza, au kumshangilia mzungumzaji kabla hajazungumza hoja yake. Tunajuaje kuwa atakachozungumza kina kidhi haja, tunajuaje kuwa atakachozungumza mtu Fulani tusiyemtaka hakitakuwa na maslahi kwetu. Kumbuka kinachojadiliwa ni katiba, ni katiba ya wote, unaowakubali na usiowakubali, je usiowakubali hutaki wazungumze?

Katiba ni muhimu sana, na kipindi cha mjadala, ni mahala pa kuangalia kila jambo, hata lile unaloliona halina maana kwako, inabidi liachwe lizungumzwe kwanza, kwani kutokana na hilo jambo, huenda tukaweza kupata `umaana wake’ na uwekweje katika ubora , na ili ubora huo auone mzungumzaji na arizike, yeye mtoa hoja na wengine kama yeye’ . Sizani kama unaweza kushangilia kufaulu mtihani kabla hujaufanya, …kwani umeutunga wewe? Basi kama ilivyo darasani au kwenye vyumba vya maabara ni vyema tukasubiri matokeo kwanza kabla ya kupitisha `hitimisho’ Tukifanya fasta fasta kwa kitu kama katiba, ….oh, baada ya miaka mitano, tutahitaji mdahalo kama huu…kama hali itakuwa shwari!

Najua wasomi wanajua hili, lakini kwa tahadhari ni vyema tukakumbushana kuwa sisi ni kiyoo cha jamii. Tabia ya kuzomea, au kushangilia kabla ya hoja, kwangu mimii naona tunatekwa na makundi ya watu. Sisi tunatakiwa tuwe na msimamo wa pamoja wa kisomo bila kujali, mtu, rangi, imani au chama, ili kitakachoandikwa baadaye kisiwe tu kitawasaidia hawo `kikundi’ cha jamii pekee, lakini kiwasaidie wao na wengine pia, si leo tu hata kesho, na hapa tutakuwa tumetimiza wajibu wetu wa kuitwa `wasomi’ Tusitekwe na msemo wa harakaharaka(fasta-fasta) tukapata ya leo tu, au kukosa kabisa, na baadaye jamii zijazo zikaja kutubeza.

Ni mimi: emu-three

9 comments :

Anonymous said...

Harakaharaka haina baraka sio, ni kweli hatutakiwi kuzoema kabla mtu hajazungumza. Lakini hii ni hulka ya binadamu, sio lazima kuwe kwa wasomi au bungeni...lakini ni vyema kweli tukajirekebisha!

Rachel Siwa said...

Nikweli tuwe na subira tusijaji mtu kwa sura tumsikilize kwanza!

lakini kwanini hukwambia yule rafiki babu alinikataza kuiba kuku wa watu?
kwa akili ya utoto ulijua atakuona falaaaaaaaaaaa!!kweli babu alifaa!

emuthree said...

Kwa akili za kitoto asingelinielewa, kwani nilikuwa namjua sana katika mambo hayo ya fastafasta, usizubae, ...achia kuku, kulikuwa na mchungwa ya shule, alikuwa mwepesi kuyachuma, fasta fasta...halafu tunaenda kumuomba...mnapewa kwa nyodo...`nyie malezi, waoga...' siunajua utoto...!

Unknown said...

bado tuna zile kasumba za kumuogopa katibu tarafa anapofoka"nitankutia ndani wewe!" Tujue zama hizo zishapitwa na wakati..

malkiory said...

Unajua tena hapa ni sawa na kuwa na darasa moja lenye mchanganyiko wa wanafunzi wepesi wa kuelewa na wale wazito. Wanafunzi wepesi ni vigumu kusubiri na huwa siyo wavumilivu endapo mwalimu anafundisha jambo ambalo walikwishalijua kitambo. Kwahiyo hapa ni suala la kutafuta balance tu.

Faith S Hilary said...

Mimi naona kama mambo ya uchaguzi uliopita. Mtu anashabikia chama na hata kama akikaa na kusikiliza vyema yule mgombea anachokisema akaona mmmh..hapa si sawa ila kwa ajili ya ushabiki atampigia kura tu anyway....kwahiyo hili swala la "ushabiki" badala ya kutilia maanani kinachozungumziwa, sidhani kama litakwisha! Ni mtazamo wangu tu kaka...ushabiki kitu kingine we acha tu...wengine hapa hata Arsenal afungwe mangapi ila ndio shabiki basi unavumilia hahaha! Mi nipo!

Yasinta Ngonyani said...

Jambo hili ni mara nyingi hutokea watu wengi huwahukumu wengine bila hata kusikia au hata kujua ana tabia gani. Yaani kwa sura tu. Halafu nimecheka kweli hiyo ya kutaka kumkamata kuku ...shule bwana ha ha haaaa Darasa nzuri MMM!

Simon Kitururu said...

Fastafasta nishai!


Nakumbuka enzi za High School Mazengo. Kulikuwa na makundi shuleni,...
... kuna watoto wa DAR, Watoka ARUSHA, Morogoro nk. na kila sehemu unakuwa umebandikwa bila kujua stigma fulani ..

Na kumbuka kulikuwa na vikao vingine kama waliojaa ni watoto wa DAR hapo MTU wa DAR ndio anasikilizwa na ilikuwa kama umetoka KIGOMA hilo tu ndio linaweza kufanya wasikusikilize kisa automatically wanahisi hujui kitu utafikiri KUJUA MAMBO na mikoa mtu atokayo vinauhusiano- na kama umetoka ARUSHA kwa kuwa WATOKAO ARUSHA na DAR ndio wengi walikuwa machekibobu basi starehe tupu ukisikiliza malumbano. :-(

Ushabiki wa mambo ni kitu cha ajabu sana kwa kuwa unaweza kukuta hata WATU wenye akili wanaweza kushabikia kitu ukashangaa kwa kuwa unajua wanapingana nacho ila kiushabiki tu ndio maana wameng'ang'ania kitu. Na ukiingiza udini basi ndio kabisaaa unaweza kukuta mtu anaweza akawa anashabikia tu kisa mtu dini yake!

Ni mtazamo tu!

Anonymous said...

purchase kamagra in u s a [url=http://shopsildenafilus.com]kamagra pills[/url] what is kamagrabuy levitra online canada [url=http://fastshiplevitra.com]cheapest levitra[/url] generic levitra 20mghow long does it take for cialis to work [url=http://achetercialisfr.com]cialis taladafil[/url] cialis online from indiawhat happens when you take viagra [url=http://fastshipviagra.com]Viagra[/url] buying viagra over the internetlevitra every day [url=http://shoplevitra.com]levitra with dapoxetine[/url] levitra without prescription