Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, December 21, 2010

Aisifuye mvua imemnyea-14

 ‘Halloh….’ Akasikia sauti ikisema hivyo, hii sio sauti ya…ya…,ha looh, sauti ..ile sauti..looh, akapumua kwa nguvu na kuiweka vizuri sikioni, huku akiwa na kigugumizi cha kujibu, ..!

 ***Nani alyepiga simu, Kabla ya kumsikia aliyepiga simu hebu tumrudie Docta, ambaye sasa atajulikana kama Docta wangu***

                               ****************************
                                  ************************
`Sasa ni muda wa kutafuta mke naona kazi ya nyumba imeshakamilika’ alisema Docta wangu akiangalia dirishani. Alikuwa hajabadili nguo alizokuwa amevaa, na mawazo yake yalikuwa mbali sana leo. Alikumbuka jinsi siku hiyo ilivyokuwa na mihangaiko mingi, kufuatilia umalizaji wa nyumba, kufuatilia hati za kulipia masomo ya Maua, ingawaje hakuwa na uhakika kuwa Maua atakubali kusoma au kabadilii mawazo, lakini aliamini kuwa Maua hawezi kukataa bahati kama hiyo. Alitamani apate kauli ya moja kwa moja toka kwa Maua kuwa yupo tayari kusoma au hana mpango huo, lakini itakua ni ajabu kabisa. Hata jamaa zake anapoishi nao sasa waliliunga mkono wazo hilo la kusoma. Anakumbuka aliongea na baba na mama wa hapo anapoishi nao wakasema kwa upande wao hawana kipingamizi, kwani kusoma ni jambo muhimu sana, na walikuwa wapo tayari kuchangia sehemu ya malipo. Lakini Docta aliwaambia keshalipia kila kitu, wasiwe na wasiwasi.

Akatizama nyota na mbingu, na akajikuta akifikiria neno `mapenzi’ hili lilimjia ghafla, na kutafakari kwanini wanadamu wanapendana, kwanini wengine wanachukiana. Yeye sasa hivi anatafuta mpenzi, lakini kuna ambao wanatafuta uadui, alifikiria haya akiangalia nini kinachoendelea kwenye nyumba, na na kuona kuwa kilichopo mle ni chuki, watu labda hawapendi maendeleo ya wengine, labda…lakini mimisiamini hilo, hiyo ni hisia finyu, maendeleo ya mtu huja kwa mtu mwenyewe, hakuna anayeweza kuzuia maendeleo ya mwingine.

‘Mimi nimekuwa sina mpenzi, ina maana kumtafuta mpenzi ni kazi kama kwenda shule?’ akatikisa kichwa, akafumba macho na kuvuta hisia za sura za wasichana aliowahi kuonana nao, lakini hakuna sura iliyomjia vyema, kila mara sura inayoangaza ni ya msichana aliyemuona, na kuishi naye kidogo, na mazoea yake nay eye yakaleta hisia za kupenda. ‘Naona huyu nimempenda…’ lakini mbona inakuwa kazi kuufikisha huu ujumbe wa mapenzi, …akawaza, kuwa yeye kasoma hadi hapo alipo, inakuwaje kitu kidogo kama hicho kimuumize kichwa…kweli kila kitu kina utaalamu wake…!

Ujumbe huu wa kupenda unastahili umfikie Maua, na naona ili nisiwe na masumbufu moyoni, lazima Maua ajue hili, labda nitakuwa nimeharakisha, labda nita…hapana ni muda muafaka. Lakini lazima nimsomeshe kwanza, ili awe karibu name zaidi, hili ni muhimu sana, akawaza na kukuna kichwa. Akatamani atoke usiku huo hadi Sinza, ili amwambie Maua arejee nyumbani kwani alikuwa anatakiwa kujiandaa kwa masomo na kuna sehemu anatakiwa kuandiak maelezo yake binfasi na kuweka sahihi yake, na hata hivyo kulikuwa na maongezi muhimu kati yake na yeye, lakini akaona sio vizuri kuyaingiza maongezi hayo wakati anatakiwa aweke mawazo yake kwenye masomo kwanza. Aliona kufanyahivyo atamchanganya kichwa, na huenda atamfanya Maua afikirie kuwa kafanya hivyo kama chambo, na sio kwa nia ya kumsaidia.

‘Hivi Maua ananipenda kweli, na nikimwambia maswala ya kuwa nataka yeye awe mke wangu atanikubalia?’ akasema kwa sauti ya chinichini. Najua nikimwambi hawezi kukataa, kwani tulivyoishi naye hapa alikuwa anaelekea kuwa karibu sana na mimi, na ilionyesha dhahiri kuwa ananipenda. Akakumbuka siku ile alivyomuona akiwa kwa akina na Rozi, Rozi alimuulizia kuwa huyu ndiye Docta wako uliyekuwa ukimuongelea, na ilionyesha dhahiri kuwa alikuwa akimuongelea kwa mambo ambayo yalimfanya Maua aone aibu je, yalikuwa maswala ya kimapenzi au yalikuwa na maswala gani.

‘Nimpigie Rozi simu nimuulize au itakuwa sio vyema..’ akatafuta namba ya Rozi kwenye simu yake, akapiga lakini ikanonekana haikuwa hewani akasema hili natakiwa niongee na Mua mwenyewe, afadhali simu ya Rozi imezimwa, kwani naona ningeongea swala ambalo halikuwa na maana kumuuliza Rozi. Akaondoka pale dirishgani hadi kwenye meza, ambayo huweka simu ya mezani, akaiangalia kwa makini , halafu akasimama tena na kurudi pale dirishani. Huu ni usiku kupiga simu kwenye majumba ya watu sio vyema, lakini natakiwa Maua ajue kuwa anahitajika….

Hata hivyo Kuna umuhimu wa kuongea na Maua mwenyewe, hasa kuhusu swala la shule, lazima nisikie kauli yake, isije nikawa nafanya kazi ambayo yeye keshaamua vinginevyo. Ngoja nimpigia simu nimsikie atasemaje nimwambie kuwa kesho nakuja kumchukua, kwani shule imekaribia na pia nilikuwa na maongezi na yeye. Lakini hana simu, lazima nitumie ya mezani ….Lakini nikimpigia nitangulize lipi , shule au maongezi, kama ni shule inabidi apate muda wa shule na kama ni maongezi ya mapenzi basi shule itakuwa haina nguvu sana. Akarudi pale mezani na kuishika simu, akafikiria, nikimpigia akipokea mzee mwenye nyumba inabidi niahirishe hayo maongezi, na akipokea mama mwenye nyumba, nitamuomba kuwa nakuja kumchukua Maua kwani anahitajika kesho kwenye ile shule yao , Je akipokea Rozi, …ngoja nipige tu.

Akajikuta keshazipiga namba , huku akikumbuka jinsi gani Rozi alivyokuwa akimsumbua kwa simu, haipiti siku bila Rozi kumpigia, akidai anataka waonane, ili amsaidie mambo ya masomo. Anakumbuka simu ya mwisho alidai kuwa pamoja na masomo alikuwa na hamu ya kuonana na yeye. Aliogopa sana kusikia hivyo, kwani yule ni mwanafunzi na isitoshe wazee wake ni watu wa heshima, itakuwa sio vyema kama anavyofikiria neno `hamu’ lina maana gani.

Yule ni mtoto wa shule, inabidi aonywe kabisa na mambo hayo…akajaribu kumkumbuka Rozi, kuwa ni mrembo, msomi na anafaa, lakini anatakiwa kupewa muda wa kusoma. Hata hivyo, kwa hisia za mapenzi, hazimpi nafasi sana Rozi moyoni mwake, kwanini…ni Maua tu moyoni. Maua hajapishana sana kiumri na Rozi, labda miezi, lakini Maua, anaonekana mkubwa kwasababu ya maisha aliyopitia. Na kwa vile hasomi, huwezi kuogopa kuongea naye maongezi ya kimapenzi, ingawaje kwa mtizamo wa Docta, alipendelea kumpa muda wa kusoma kwanza na kuimarisha fikira zake! Kwa huyu Rozi inabidi nikipata muda nimuonye, asichanganye masomo na mawazo ya kimapenzi, ingawaje kiumri wake huwezi kumuita mtoto. Nimesoma najua ubaya wa kuchanganya mapenzi na masomo, nitafnya vibaya kama nitamruhusu Rozi ayaingize maswala haya kipindi kama hiki!

‘Halloh, ..’ aliposikia simu imeinuliwa bila kusikia mtu akijitambulisha akaona aanze yeye. akashangaa aliyepokea kaishikilia simu ipo hewani lakini hajibu kitu, ni nani huyu, au ni watoto, wanashindwa kuongea. Akasubiri na baadaye akasikia sauti ikiitikia kwa wasiwasi. Kama hakosei sauti hiyo ni ya..Ma..hapana inawezekana ikawa ya Rozi, maana sauti zao hazitofautiani sana, ile sauti ikajibu kwa wasiwasi ikisema `Halloh’….’ikakaa kimya. Kicwani akasema huyu sio Rozi, Rozi anaongea lafudhi ya Kiingereza kidogo na hujibu kwa kujiamini, huyu atakuwa Maua

`Maua mbona unajibu kwa wasiwasi…’ akasema, huku anajiweka vizuri kwenye kiti. Alishajua huyu ni Maua, na huenda wengine wapo hapo jirani, ndio maana anaogopa kuongea. Kama ni Maua , mambo yatakuwa mazuri, kwani kapokea mlengwa.

‘Maua upo peke yako, kwani kuna kitu muhimu nilitaka kukuambia…’ akasema nakusikiliza, lakini upende wa pili ulikuwa kimya kwa muda tena, na kumfanya Docta awaze kuwa aliyepokea huenda sio Maua.

‘Nipo peke yangu Docta, wakina baba na mama hawapo, na …Rozi yupo chumbani, vipi kuna tatizo nyumbani….’ Akasema Maua.

‘ Hakuna tatizo Maua, ila nataka kukuambia kuwa, kesho asubuhi nitakuja kukuchukua, naomba uwafahamishe wenye nyumba hivyo, ikibidi uage kabisa, kwani shule zinafunguliwa, na…vipi mbona unajibu ukiwa na mashaka, si umesema upo peke yako..’ akasubiri kusikiliza.

‘Ndio nipo peke yangu, lakini…mmmh, alikuja Docta yule rafiki yako akasema ana maongezi na mimi kesho pia, sasa…mnanichanganya kidogo…lakini sawa njoo nichukue, …’ akasema na kukaa kimya.

Docta mwenzangu ana maonezi na Mua? Akajiuliza na kuanza kuingiwa na wasiwasi, akaukumbuka siku ile alipomtajia Maua, na kumuelezea mipango yake ya kumuendeleza, akakumbuka jinsi rafiki yake alivyogutuka na kukaa kimya. Akahisi kuna jambo linaloendelea kati ya Maua na rafiki yake. Je afanyeje kwani kama rafiki yake keshajiingiza kwa Maua anavyomjua kwa utaalamu wa kushawishi basi inabidi afanye juhudi za haraka, na ikiwezekana atoke usiku huu akamchukue Maua nkabla rafiki yake hajamuwahi. Lakini itakuwa sio jambo jema kufanya hivyo, ….

‘Maua tafadhali jiandae asubuhi sana, kwani natakiwa kukuwahisha kule kwenye hicho chuo, kuna maswali ya kumalizia, ili na mimi niwahi kazini, kwahiyo wafahamishe hawo jamaa zako usiku huu, na ujiandae kabisa. Na kuhusu maongezi yako na rafiki yangu, yasikutie mashaka, yule ni rafiki yangu najuana naye, kama una wasiwasi nitawasilina naye, au unajua lolote kuhusina na maongezi hayo. Naomba asikupotezee nafasi hii muhimu, kwani mimi mwenyewe nimeamua kukuendeeleza ili baadaye mmm, uwe na maisha yakujiamini, na mmmh , ukimaliza masomo ninampango wa mimi na wewe…mmh ukiwa tayari, na kama unapenda tue tusihi pamoja…..’

‘Tuishi pamoja…’ Neno hilo lilimtoa Maua kwenye lindi la mawazo, kwani ingawaje alikuwa akisikiliza simu, lakini mawazo yake yalikuwa mbali. `Tuishi pamoja..’ Mimi Maua niwe na bahati hiyo…, Maua alishituka kusikia kauli hii ya mwisho, kwani wakati Docta anaongea, yeye alikuwa anawaza mengi kichwani, je aichie bahati ya kuolewa ili akasome, au akasome, na bahati ya kuolewa ipotee, je..…Docta wangu kasemaje `tuishi pamoja’…haya maneno nimeyasikia kweli au naota, mimi niishi pamoja na Docta wangu….nikweli au sikweli…., tuishi pamoja, kama mfanyakazi wake , kama mke na mume, kama…tuishi pamoja! Oh, naomba ayarudie tena haya maneno niyasikie tena vyema… akawaza, lakini akaona aulize tu!

‘Una maana gani kusema hivyo Docta..’ akauliza kwa makini na kuishikilia simu vyema masikioni, na akili sasa ikawa imetulia kusikiliza kinachoongelewa kwenye simu, kabla hajapata jibu, mlango wa nje ukagongwa, na hiyo sauti ilimshitua hadi akadondosha simu, …akasikia tena mlango ukigongwa, akaikota simu haraka, huku anasikia Docta, akisema `halloh, halloh…’ lakini aliogopa kumjibu, akairudishia sehemu mahali pake haraka na kukimbilia kufungua mlango!

Je itakuwaje, tuzidi kuwepo...!


Ni mimi: emu-three

5 comments :

elisa said...

jamani natamani ingeendelea ....

Pamela said...

M3 hujatutendea haki wafuatiliaji wako jamani ooooh imeishia patamu!sawa wacha tusubiri....

Yasinta Ngonyani said...

Hakika umeacha patamu...twasubiri ila mmm usisahau hiki ni kitabu tosha ..

Anonymous said...

M3 kwakweli sina la kusema wadau hapo juu wamemaliza.

Ni raha tupu, hapo sasa sijui itakuwaje?

Kazi kwake Maua. Bahati iliyoje hiyo, kila mtu anamtaka yeye.

BN

Anonymous said...

Mhhh, raha sana kupendwa, na ukapa unayempenda, na hii siri kubwa ni tabia njema...TABIA NJEMA, kama tungelijua wote hili, natumai ndoa nyingi zingekuwepo na matumaini mema katika familia...Maua ana tabia njema, Rozi ana elimu, lakini wote ni warembo, nani ungemchagua, msomi atakayekupanda kichwani au mmmmh, lakini ana tabia njema!