Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha
Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..
Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.
MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.
TUPO PAMOJA DAIMA
Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;
https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:
https://www.facebook.com/diaryyangu/
`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;
Monday, November 1, 2010
Kikulacho ki nguoni mwako(Somnambulism story) 4
Baada ya miezi mitatu mdogo wangu alipona kabisa, na upelelezi wa polisi ulikuwa umeshindwa kugundua aliyefanya hivyo, kuna muda walimtia hatiani mke na mdogo wake, lakini baadaye ukakosekana ushahidi , na mimi mwenyewe nilipinga sana, hata mdogo wangu hakukubaliana na hilo, yeye alisema likuwa usingizini, na alishitulia na maumivu makali , na alipojaribu kuangalia nini kimetokea akaona giza linatanda usoni na kupoteza fahamu, kwahiyo hana dalili yoyote ya kumgundua aliyefanya hilo.
‘Mimi naona tuyasahau hayo, na mungu amsamehe aliyetenda haya kwani hakujua alitendalo…’ akasema mdogo wangu. Lakni mimi sikukubalina kabisa, nikawaambia polisi kama wameshindwa waniambie nitafute wapelelezi binafsi wanisaidie. Polisi walisema nisiwe na wasiwasi, wao wanajua nini wanachokifanya, mwisho wa siku watagundua na haki itatendeka!
Maisha yakaendela kama kawaida, na siku moja kukatokea mgongano kati yangu na mke wangu. Tulibishana kuhusu harusi a mdogo wake ambaya alitakiwa kuolewa karibuni. Mimi nilipendelea harusi isifanyike kwanza, kwani anaendelea na masomo yake, lakini dada mtu alitaka harusi iwepo kwanza, kwani waoaji hawataki kusubiri.
Majibishano yale yalifikia kuzua mambo yaliyopita . Nakumbuka katika heka heke za uchunguzi askari walimbana sana mke wangu, na hili lilimsoninesha sana moyoni. Sasa katika ubishi huu mke wangu akalikumbushia na kusema, mimi mara nyingi siwi upande wake kwani hata polisi walipomshuku yeye sikuonyesha juhudi za kumtetea, huenda hata mimi nilikuwa na mawazo hayo. Akaongezea kusema, kuwa mapenzi yangu kwakwe yamekuwa yakipungua siku baada ya siku. Nilimkatalia lakini haikusaidia…
‘Naona nyumba hii kila kibaya kinanihusu mimi, ndio maana mlinihisi kumuumiza shemeji yangu…’ akakasirika na kwenda chumbani.
Huwa mke wangu akikasirika ni vyema umpe muda akae pake yake mpaka hasira zishuke vinginevyo mtaishia kutupiana maneno ambayo yanaweza kukutia hasira, kwahiyo mimi nikaondoka kwenda kumtembelea rafiki yangu. Niliporejea nilikuta hasira zimekwisha tukaongea kama kawaida. Lakini nilijua bado moyoni ana kinyongo na mimi.
Ilikuwa usiku wa manane, nikawa naota ndoto mbaya, na kwa mazoea nikiota ndoto mbaya kuna kitu kinaweza kutokea, kwahiyo nikaamuka haraka , na kujikuta nimelala peke yangu. Nikavuta shuke la mke wangu , na kuhakikisha kuwa hayupo. Nikahisi huenda mke wangu katoka kujisaidia, nilipoona muda unakwenda nikaamua kumfuatilia kujua wapi alipokwenda, au kwanini anachukua muda mrefu.
Nilingia chooni nikakauta hayupo, nikatafutafuta maeneo mengine sikumuona, niliporejea chumbani, nikaona kama yeye amelala kitandani, nikafunua shuka, lakini ilikuwa mito imetengeneza ishara ya mtu kulala hapo, sikumbuki kutandika shuka kwa mtindo ule, nikahisi kuna mtu kaingia chumbani nilipotoka, je ni mke wangu, na kaingia saa ngapi na kuelekea wapi tena, na kwanini atandike kwa mtindo ule, au kuna mtu anaichezea! Nikalifunua lile shuka tena kuhakikisha kuwa hakuna mtu aliyelala, nikalirudishaia shuka kama lilivyokuwa. Nikatoka nje taratibu, kuangalia mke wangu kaenda wapi.
Mara nikasikia sauti jikoni, nikajisemea moyoni, labda mke wangu alishikwa na njaa akaamua kwenda kujitengenezea chai, au chochote. Nikatoka chumbani kuelekea jikoni, nilipofika karibu na mlango wa jikoni, nikasikia sauti nyingine chumba cha kupumzikia. Nikashikwa na kigugumizi, nielekee jikoni, au chumba cha mapumziko. Nikasubiri, na mara nikaona kivuli cha mtu, kikitokea jikoni, kivuli kile kilionyesha mtu kashikili kisu mkononi, na ananyemelea kuelekea chumbani kwetu. Nikajiuliza ni nani Yule…nikasubiri nione, kwani mawazo yangu yalishanipeleka kuwa kuna jambazi limekuja na kumuua mke wangu na sasa linataka kunimaliza na mimi. Na kuna wengine wapo chumba cha kupumzikia, leo nitapambana nao kufa na kupona, hata kama ni mashetani.
Kuna mawazo yalinituma kuwa huenda nyumba yangu imeingiliwa na mashetani, lakini sina imani hiyo. Imani hiyo nilijengewa na watu, kuwa niwe makini , kwani madude haya yanaweza kuichezea nyumba, na hata kumtuma mwanafamilia akafanya asichokitaka. Sasa huenda kama imani hiyo ipo, yapo huko chumba cha mapumziko na wamemtuma mwenzao, mimi nitapambana nao mmoja baada ya mwingine. Nikajipa moyo huku woga unatanda mwilini pia!
Kile kivuli kikawa kinkuwa kikubwa, kwa jinsi kinavyosogea karibu na pale niliposimama, woga , hasira vikaniingia, na mwili wa hicho kivuli ukawa unakamilika kutimiza mwili mzima kwa taratibu, na kila dakika ya kukisubiri kitokee chote, ndivyo hasira zilivyozidi kunitanda na kutaka kumvamia huyo mtu kabla hajaingia chumbani kwetu.
Moyo ukanienda mbio, kwani taswira ile ya kivuli, ilikuwa ni ya mwanamke, na jinsi ilivyokuwa ikisogelea mlangoni, ndivyo ilivyojidhihiri kuwa ni kivuli cha mwanamke. Nikajiuliza anaweza akawa mke wangu, lakini mbona anakisu mkononi, au ni shemeji yangu. Nikawa na mashaka na dhana hiyo, kwasababu kama kuna mtu hapendi vitu vya hatari kama kisu , wembe au chochote kinachoweza kumtoa mtu damu ni mke wangu. Mke wangu hapendi damu, na hasa iitwe damu ya mtu. Yeye mwenyewe anajuta kwanini ni mwanamke kwani kwa asiliyao damu haikwepeki!
Huenda ni shemei yangu, ..hapana, ni shemeji kweli, nikajisemea moyoni, shemeji yangu kaingiwa naujasiri gani wa kushika kisu, kwani ni mwogo wa kupindukia, usiku hapendi kutoka nje mwenyewe. Labda ndio chui ndani ya ngozi ya kondoo. Kweli kikulacho kipo nguoni mwako, huyu anaweza akawa shemeji yangu. Nikakumbuka siku mdogo wangu alipoumizwa, asubuhi mtu wa kwanza kukutana naye alikuwa shemeji yangu.
Nikasema huenda ninavyofikria sivyo, huyo anaweza akawa jambazi mwanamke anayetaka kuimaliza familia yangu. Labda keshammaliza mke wangu na anataka kunimaliza na mimi. Hapa kanoa, nimemuwahi.Ngoja nikapambane naye kiume.
Nikavuta hatua ya pole pole nikiwa tayari kwa mapambano, nikasikiwa watu wanaongea tena chumba cha mapumziko na sasa sauti ilikuwa wazi, wakiulizana, kitu. Nikasita kidogo, huku nikitega sikio vizuri. Na mara sura ikajitokeza, nikajiandaa kuvaana naye, lakini moyo ukanilipuka…
****
Oh jamani muda umekwisha mbona muda unaenda haraka hivyo, tuwepo baadaye, tuendelee na kisa hiki. Je huyu mwanamke ni jambazi au ni shemeji mtu? Na hawo waliopo chumba cha mapumziko ni akina nani, ni majambazi mwenza, au ni mashetani yanamchezea jamaa ndani ya nyumba yake mwenyewe!
Ni mimi: emu-three
4 comments :
Mmmmmmmmmh!!!!!!!!!!! M3 wewe ni kiboko mno. yaani nilipokuwa nasoma hii stori mwili wote ulikuwa sio wangu. Nilishikuwa na woga sana. Nilijiona kama ndio mimi natokewa hivyo. Nimeogopa sana. Sasa mbona umeishia patamu hivyo? Tupe huo uhondo M3.
Kwa kweli wewe ni mkali Mungu abariki kipaji chako.
Nakuomba sana M3 usikatishe hii stori tafadhali sana, tupe yote usitubanie pls. Usijali hata kama zikifika page 20 we tupe tu. Yaani ni nzuri na inasisimua na inamafunzo pia. "Lakini inatisha" we acha tu.
Kila la Heri M3, "SALUTI"
BN
Nashukuru BN, nami nitajitahidi kufanya hivyo, na natumai wapenzi wote wa blog hii mtakubaliana naye.
Ninachohitaji kwa wapenzi wa blog ni maoni kwa wingi, mapendekezo na jinsi gani tuiboreshe hii blog!
Nashukuruni sana kwa kunipa moyo, Mwenyezi-mungu awabariki!
Hivi unapata muda gani wa kuziandika hizi storii zako? Hongera sana, na sijui unalipwa? manake vitu kama hivi ni vitabu vizuri tu, nakushauri uchapishe kitabu, tupo wakununua, unawapa watu raha, lakini hakuna hata mmoja atakaye kupa ahsante...zaidi ya pongezi za mdomo!
Na wengine wa copy na kupaste na kuwatumia marafiki zao, kama wameandika wao vile!
Lakini usikate tamaa, nimezipenda na nitaendelea kujiuliza je haya yalitokea kweli?
Ni kweli inasisimua na inafundisha na nasubiri kuona au kusoma mwendelezo, maana ulipofikia ni pazuri kweli ingawa panatisha......
Post a Comment