Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, October 21, 2010

Limbwata-2!

 
  Limbwata , limbwata, …kumbe ndilo lilomsaidia shoga yangu, nami nikaingiwa na hamasa ya kulitumia, siunajua tena linapokufika jambo, tafakari zetu hushikwa na ukomo…


Basi ingawaje mwenzangu huyu alinikatalia kabisa kunipa hiyo dawa mimi nilimuomba sana anipe, niliona ndio njia pekee ya kumweka sawa mume wangu, sikua na maana kabisa ya kisasi ila niliona kuwa nitamtengeneza mume wangu awe nitakavyo, lakini rafiki yangu alikataa kata kata, alidai kuwa shangazi yake alimkataza kabisa kumpa mtu mwingine kwa kujua madhara yake, na ufutiliaji wake. Lakini baadaye akanipa!

Yeye alisema kuwa alimwekea mume wake kwenye chakula bila ya yeye kujua na ikaanza kufanya kazi. Alisema kuwa mwanzoni mume wake alikuwa kama mtu aliyekula madawa ya kulevya, au zezeta Fulani ambalo halitaki kuondoka nyumbani, kila mara anataka wawe pamoja, na wakati mwingine alikuwa akitoroka kazini kuja nyumbani. Na yeye alihakikisha anafuata maelekezo ya shangazi yake, kuhakikisha kuwa anamsaidia mume wake kila iwezekanavyo, kiasi kwamba hakuna aliyebaini utofauti!

Basi kwa maelezo yale nikaona nimepata ufumbuzi, licha ya wasiwasi na woga, kuwa nyingine inamuathiri mume kabisa. Basi baada ya maelezo ya jinsi ya kuitumia nikawaambia wazazi wangu kuwa nimeamua kurudiana na mume wangu. Nimekubali kusuluhishwa na turejeane tena.

Nilipofika nyumbani na zile hasira sikupoteza muda, usiku nikakitengeneza chakula kizuri nikamwekea ile dawa katika chakula chake. Kazi ilikuwa jinsi gani yay eye kukila kile chakula, kwani mimi nilitakiwa nisikiguse. Mume wangu akataka tule pamoja, na zaidi akataka kunilisha.

‘Mume wangu mimi sijisikii vyema, nina kichefuchefu, wewe kula tu…mmmmmh, hapana usinilishe…’ nilisema hivyo wakati keshakileta kijiko cheney chakula mdomoni. Nilijifanya nina kichefuchefu na kukimbilia nje. Niliporudi nikakuta mume wangu hajakigusa kile chakula, akasema kama mimi sili basin a yeye kashiba. Na kweli siku hiyo hakukila chakula kabisa. Nikawa sina jinsi ila kukimwaga kwa siri.

Asubuhi nikaona niiweke kwenye chai, lakini hutaamini nilipitiwa na usingizi , nilipoamuka nikakuta mume wangu keshakunywa chai na anajiandaa kuondoka. Nikaona sasa ni mtihani, lakin sikukata tamaa, nikijua leo atarudu mapema, kwahiyo nikakitayarisha chakula chake, na kukiweka tayari, Hutaamini alipokuja alikuaja ba rafiki yake, nikaogopa kabisa kuwaandalia na kujifanya chakula nilichopika hakikubakia, walikuja wageni …

Usiku wake mambo yakawa mazuri, jamaa alikuwa akadai chakula, alikuwa kachelewa name nikawa nimeshakula, kwahiyo alipokuja tu, nikamwambia nipo naoga, kama ana njaa achukue chakula kipo kwenye kabati. Na kweli nilipotoka bafuni nikakuta anakimalizia. Nikaasema saafi mambo sasa yamekamilika.

Siku mbili mambo yakaiva, dawa ikaanza kufanya kazi. Kipindi hicho alikuwa anafanya kazi kwenye kampuni moja ambapo alikuwa anafanya kwa zamu, yaani kuna muda mwingine anatakiwa kuingia usiku au mchana. Basi ikawa hizo zamu hazifuatilii tena, akaanza hata utoro wa kazi ilimradi aje nyumbani.

Ilibadilika na kuwa kero, kwani kila mara akawa yupo nyumbani , na hatimaye akafukuzwa kazi. Ikabidi awe name katika kazi zangu za mama lishe. Mwishowe nikaona imezidi kiasi, nikaona niwasiliane na Yule shoga yangu aliyenipa hiyo dawa akawa hapatikani kwani alikuwa kasafiri kwenda kwao. Nikaanza kuogopa, manake alikuwa hajali kuwa kuna watu , mara anijie kunikumbatia mara hivi nakupenda …yaani kero na karaha.

Kwa sababu ya ile tabia ya kuwa nyumbani wakati wote na hataki kubanduka karibu yangu, ndugu zake wakahisi kuna kitu kimefanyika…siunajua machale ya wazazi kwa watoto wao! Nikaona sasa siri imegundulika nifanyeje? Kila nikimpgia rafiki yangu simu hapatikani!

Siku moja wakaja mama wa mume wangu na mama mwingine toka huko kwao, walisema wanahisi kuwa mtoto wao anahali isiyo ya kawaida kwahiyo wanataka kumpa dawa, nilikataa nikiwaambia mbona haumwi, lakini sijui walimwekea kwenye chakula au walimpaje sijui kwa kweli, kwani siku ya kesho yake alianza kutapika kupita kiasi. Na ile hali ilipokwisha nilimuona mume wangu akiniangalia kwa jicho la hasira.

‘Vipi mbona unaniangalia kwa jicho la ubaya’ nikamuuliza

‘Wewe unafikiri uliyofanya ni mazuri, unafikiri kufanya hivyo ndio utanikomoa au..” akaniambia kwa hasira,

‘Kwani vipi mume wangu…’ nikaongea kwa huzuni, lakini hakunijali na kunisukuma mbali. Nikaona sasa ni tatizo, je nimuongezee ile dawa, lakini shoga yangu aliniambia nisije kumuongezea ile dawa mpaka baada ya miezi mitatu. Nikasema moyoni, nikipata muda nitamuongezea tu hakuna jinsi.

Siku hiyo niliyopanga kumuwekea kwenye chakula, nikawa jikoni nakitayarisha. Nikaelekea pale nilipoificha ile dawa, nikaikua bado ipo. Nilihakikisha kuwa mama anaongea na mwanae huko jikoni. Nikaichukua na kuifungua kwa uangalifu nikachukua kijiko cha chai. Nikaichota, kuhakikisha kuwa haizidi wakati nainua mkono ili niiweke kwenye chakula, nikahisi sipo peke yangu, nikajiuliza ni nani tena huyo wakati nasikia watu bado wanaongea barazani, na mara nikashikwa bega kwa nyuma…

Ni mimi: emu-three

12 comments :

Anonymous said...

Aaaah, umekatisha sehemu muhimu...gosh, lete vitu, nahisi kafumwa, lakini na nani...mmmh, mama yupo ndani anaongea, sasa nani kamfuma...mmmh, kesho tuletee sehemu iliyobakia!

Johprise said...

Mbona inanoga ? ! ! . . .

malkiory said...

Majuto ni mjukuu!

Anonymous said...

hiyo kali mbona unatutisha wenye ndoa zetu? au ndo tuishi kwa kula hotelini nini!!!

emuthree said...

Anonymous wa 11:09 usiogope, kwani hiyo yote ni mitihani, kwani hata ukiwa dereva huwezi kugopa kuendesha gari eti kwasababu umeambiwa barabara ina ajali nyingi!
Cha muhimu ni kujua nini maana ya ndoa, na nini mwenza wako anataka, muelewane na muwe karibu, kama kuna kusisgishana kaeni muelezane!
Mara nyingi haya yote hutokea kwasababu ya kukosa maelewano!

Anonymous said...

Kwa kweli hilo ni fundisho tosha kwa wanandoa wenye tabia kama hiyo, mapenzi sio limbwata ni kuishi kwa kuelewana, kusikilizana na kuheshimiana huku mkiombana msamaha pindi kunapotokea tofauti kati yenu kabla hakujakucha muwe mumemaliza tofauti zenu, sio kuamka na makisirani ya jana yake usiku.

Mzee wa Changamoto said...

Duh!!!
Kumbe kuna PUMZIKO la fikra huku. Hizi tafakari murua zawazisha na hilo ni jambo jema
Wacha niirejee.
LAKINI WAKATI NAIREJEA, NIRUHUSU KUTOKA NJE YA MADA NIKIBAKI NDANI YAKE KUULIZA....LIMBWATA NI NINI WAJAMENI?

Ni kitu, ni hisia ni utashi, ni nini?
Wale wasemao LIMBWATA KIUNONI hutenda na hawatoi. Wale walishao huweka madubwana hawafinyangi mauno. Wale wa Katere** nao nasikia inawabamba wahusika hawasikii. Na wale "wakali wa maombi" wanaomfanya mpenzi agande na asiende kwingine nao waseme ni limbwata?
Hivi limbwata ni nini?
NAWAZA KWA SAUTI TUUUU!!!

Anonymous said...

m3 napenda mafundisho yako nakupa hongera kwa mabadiliko ya blog ila tatizo linakuja unakatisha utamu kama usia wa mama imeishia wp?

emuthree said...

Mzee wa changamoto, labda jibu tunaweza kulisogeza akilini tukisoma sehemu inayofuata, karibu sana!

emuthree said...

Ndugu `Anonymous wa October 24, 2010 12:33 AM:
Umeulizia kuhusu usia wa mama kuwa uliishia wapi: Kile kisa tulikimalizia pale, ili kupeana changamoto cha `itakuwaje' kama ingelikuwa kwako. Tulisubiri mawazo, lakini tulipoona kimya tukajua kuwa watu wametosheka nacho! Mhh, labda tukuulize na wewe je unahisi nini bado kinakosekana, ili tuanzie hapo?
Ni kweli wakati mwingine tunakatisha maelezo ya`tukio' kwani kama tutaandika kama litakiwavyo liwe tunaweza kuandika kitabu kizima, kwahiyo tunafupisha ili tupate mawazo mbadala kwa wengine. Lakini yote ni maoni, kama mpo tayari kusoma `riwaya' kwetu ndio raha, manake kuandika twapenda sana, ila je wenzangu mpo tayari kusoma habari ndefu...
tusaidiane mawazo!

Anonymous said...

Mimi binafsi napenda sana Riwaya za kuccmua ila cjui kwa wenzangu wanapenda ila kwa ombi langu binafsi naomba umalizie kile kisa cha usia wa mama maana kilinigusa sana nakutakia cku njema.

emu-three said...

Tunashukuru kuwa kisa cha usia wa mama kimewagusa wengi, na wazo hilo la `kukimalizia' litafanyiwa kazi...ingawaje tuliweka hitimisho.
Usikonde mdau, na `riwaya' za kusisimua zipo, tutaanza kuziweka hewani karibuni. Kwanza tulitaka visa hivi vya ukweli viingie akilini mwa watu, na kikawaida riwaya hujengwa kutoka kwenye visa vya ukweli ni swala tu la kunyambulisha tukio, kwahiyo, kutokana na visa hivyo vya ukweli tutakuwa na riwaya za kila namna, tuombeane uzima na `ajira' ya uhakika, manake kukuletea haya tunategemea `maofisni'...natumai unanielewa!
Karibu sana na nashukuru sana kuwa mmoja wa wapenzi wa blog hii!