'Huyu mwenzetu kazidi, anabadili wafanyakazi wa nyumbani kama nguo, na kila anayekuja kwake huondoka bila kwaheri, huu sio uungwana' akasema mama Nanihii.
'Kwani wanaondokaje, ni kwasababu wao hawakubaliani na maisha ya hapo, au masilahi ni duni, au kuna nini?' nikauliza.
'Huyu mwenzetu hana dogo, anawafanya watumishi wa nyumbani kama bidhaa fulani, anawatusi anawatuma kama ile hadithi ya Mhindi na mtumishi wake ya `Jumaa njoo safisha meza, kabla hajaondoka, Jumaa, toto kanya ondoa mavi, kabla hajafanya hiyo kazi, Jumaa, niletee juice ya baridi, kabla hajaondoa mguu, Jumaa....mwisho wa siku huyu Mhindi anakasirika na kusema, 'Veve hujui kazi, kazi zote nimetuma veve hata moja hujafanya, kazi hamna ondoka, veve hufai...
'Je mtu kama huyu ataweza kuishi na mfanyakazi wa ndani? Haiwezekani, kwasababu hana utu, hana ubinadmu, anawafanya wenzake kama roboti, hata roboti ukiliamrisha kazi nyingi kwa pamoja linaweza likabuma...
Wakatii mama Nanihii akinieleza haya mawazo yangu yakaenda mbali zaidi nikakumkumbuka babu yangu mwanahekima wakati anatuelezea jinsi gani ya kuishi na watu. Alisema hivi,
'Huenda miongoni mwenu kuna atakayebahatisha kuwa na kampuni au wadhifa au kubahatisha kuwa na wafanyakazi wake. Kuna watu maalumu unatakiwa kuwajali sana, na hata lugha ya kuongea nawo inabidi iwe ya kinyenyekevu zaidi. Hawa watu ni dhalili ukilinganisha na wenginae lakini kazi zao ni muhimu sana katika maisha yako kuliko ya hawo unaowalipa mishahara mikubwa. Hawa watu wanakujali na kulinda uhaii wako, nawo ni mpishi wako, au mhudumu anayejali tumbo lako, wa pili ni dereva wako anayekuendesha mara kwa mara na watatu ni mlizi wako anayekulinda usiku ukiwa umelala.
Kwa mtizamo wa babu -hekima, mtu kama mpishi wako anaweza akakuwekea sumu, au akakupikia chakula kibaya au akafanya afanyalo na kuhatarisha maisha yako kama hutomjali, na kama unamnyanyasa mara kwa mara anajenga chuki ambayo ikizidi sana anakuona wewe kama mnyama kwakwe, mwisho wa siku anafanya ambalo hakukusudia.
Halikadhalaika dereva wako, huyu anakuendesha, hatakiwi ajae mawimbi ya hasira na chuki kichwani mwake kwa matusi yako au kejeli zako , ambayo yanaweza kumfanya akakugongesha au kuligonga gari ama kwa hasira au mawazo mengi kichwani. Huyu hana tofauti sana na mlinzi wako, ambaye wakati wewe umelala, yeye analinda usalama wako, ukimuizi anaweza akafanya la kufanya au akakukamatishia wezi. Tumeyaona haya katika maisha yetu, na ni vyema tukajifunza nayo.
Cha ajabu hawa watu wanafanywa kama hawana thamani, sio kweli kihivyo, hawa watu wanathamani kubwa kuliko huo mshahara unaowalipa, wajali na uongee nawo kwa busara. Busara hiyo inaweza ikamtoa nyoka pangoni, na wakakuona mtu wa maana sana kwao. Kuna kukosea , kuna wengine usipokuwa mkali wanadumaa na kukudharau, lakini ipo lugha ya busara ambayo inaweza kuwa kali kuliko ukali wenyewe, nayo ni `Nyama ya ulimi, na mdomo wa busara ambao hauna gharama, lakini thamani yake haitabiriki' tuutumie kila wanapokosea kuliko kuwadhalilisha na hatimaye wanajiona kwako hawana thamani.
Huo ndio ujumbe wangu wa leo
emu-three
1 comment :
Hiyo Jumaa, imenichekesha kweli, kwani nakumbuka miaka ile ya 47, ndio maigizo ya shuleni, anyway, enzi hizo bado tulikuwa katika mawimbi ya ubaguzi wa rangi, lakini bado yapo hata maofisini.
Vipi stori yetu utaiendeleza lini, ya uchungu wa mwana?
Post a Comment