‘Ni wakili mmoja hivi wa kujiegemea,..sio muhimu kumfahamu jina
lake kwa sasa…’akasema
‘Kwangu ni muhimu sana…’nikasema
‘Unajua cha muhimu ni wewe
kukubaliana nami, halafu mengine niachie mimi, maana hili janga bila mimi
kushirikiana nawe, halitaweza kufanikiwa, na ujue lolote baya likitokea
halitaniathiri mimi tu,…’akasema
‘Kwanza nikuambie kitu, siogopi majanga, hayo ni sehemu ya maisha
yangu, sawa naweza kukubaliana na wewe kwa vile kuna huyo mdudu mtu kaingilia
maisha yangu, na mimi hilo ni changamoto, …nataka kumfahamu huyo mtu ni
nani..’nikasema
‘Ndio hapo nikaona tushirikiane, ili tuweze kumnasa huyo mtu…’akasema
‘Achana na huyo mtu, mimi nataka kumfahamu huyo wakili ambaye yupo
tayari kukusaidia ni nani…?’ akauliza
‘Sijakubaliana naye baddo kwahiyo siwezi kukuambia…’akasema
‘Ok, kama hutaki kuniambia tuachane tu, ondoka zako…’nikamwambia
‘Sikiliza nitakuuambia nikirudi huko nilipoitwa, nina uhakika ,
haya mambo yalivyo, yanahitajia mtu kama yeye, yeye huo ni uwanja wake,
hutaweza kumchukua wakili wa aina nyingine akakubaliana na sisi, na kwa hili,
hatutakiwi kwenda polisi, unaona eeh, maana ukifanya hivyo, nyuma yake
utakutana na waandishi wa habari..’akasema
‘Ok, so unataka mimi nifanye nini…?’ nikamuuliza
‘Kwanza unakubaliana na mimi kuwa kuanzia sasa hili la mtoto iwe
siri, hakuna wa kufahamu baba wa mtoto ni nani, na rafiki yako asijue hili
kabisa ..unanielewa hapo, maana akifahamu hilo, sio mimi tu, hata wewe utakuwa
umejiharibia…’akasema
‘Sawa…hilo halina shida, tangia mwanzo hili nilitaka liwe langu
tu, tatizo ni huyo kidudu mtu, na nakuonya, kama wewe upo nyuma ya hilo jambo,
utanitambua mimi ni nani, unanifahamu sio…’akasema
‘Kwanini huniamini…nisingelipoteza muda wangu kuja hapa kwako,…sasa
ngoja mimi niende, nikaonane na huyo mtu, nikitoka kwake nitakuja kukufahamisha
ni nini tulichoongea naye ,sawa ilimradi
wewe umeshakubaliana na mimi ..’akasema akitaka kuondoka
‘Pamoja na hayo, sitaki uwe unakuja hapa kwangu, pili..tusizoeane
kihivyo, mimi sio mpenzi wako na haitatokea kuwa hivyo, maana tangia awali
sijataka mahusiano na wewe, wewe ni mke wa mtu,..na kwa hili imetokea bahati
mbaya, na tatu, msimamo wangu ni ule ule, huyu mtoto ni wangu peke yangu, hana
baba…’akasema
‘Usiseme hivyo kuwa hana baba,..hata hivyo, hayo tutakuja kuongea,
kwasasa sio ya muhimu, tusianze kugombea mtoto, au sio…umenielewa hapo, muhimu
ni kuona jinsi gani ya kulikwepa hili, hivi wewe huoni hatari iliyopo mbele
yetu…naogopa sana mkwe wangu akija kulifuatili,a yule mtu ni hatari, …’akasema
na kuanza kuondoka.
Na alipoondoka tu, simu yangu ikaita, alikuwa ni rafiki yangu
anasema yupo njiani kuja kuniona, hapo nilihisi mwili ukinicheza, maana kuja
kwake nilishamuahidi kuwa nitamuambia kila kitu, lakini kutokana na haya
yanayoendelea sizani kama nitaweza kumuambia.
‘Nduguzanguni, …naongea
haya ili muone kipindi hicho jinsi nilivyokuwa na wakati mgumu , mnaponilaumu
kwanini sikusema mapema, baada ya tukio hili, yaonekana kabda mimi nilifanya
makusudi,..hapana kulikuwa na changamoto zake.
‘Na pia naomba mnivumilie kwa mahojiaono yatakayo kuja kuendelea baadae
nia ni kuja kuwafichulia kile kilichokuwa kimejificha ndani yake, hili tukio
sio rahisi kma lilivyo, kuna mambo yamepangwa,..na huenda hata wahusika wengine
hawalifahamu hilo..’akasema bila kuonyesha hao wahusika wengine ni nani.
*********
Baadae alikuja rafiki yangu tukawa tunaongea na hoja yake ikawa
ile ile ya kutaka kufahamu ni nani baba wa mtoto wangu, sikuweza kumwambia,
nikijua kuwa kuna huyo mdudu mtu, ni lazima nimpate, pili, ni hali halisi
ambayo, nahis nikimuambia rafiki yangu ndio urafiki utakufa kabisa, na kwahiyo sitaweza hata kwenda kusoma kabisa.
Sasa wakati rafiki yangu yupo hapo, simu yangu ikaingia ujumbe wa
maneno, na nilipoangalia, kabla sijaufungua nikahisi ni hao watu, kwa jinsi
ujumbe wenyewe ulivyokuwa kuwa kuna kitu kimebebeshwa kwenye huo ujumbe na ni
picha au video…sikuweza kuisoma ile simu nikapotezea.
‘Mbona huangalii , nahisi kuna ujumbe umetumiwa, akaniambia rafiki
yangu, na kwa haraka nikaufungua huo ujumbe, maelezo, kidogo tu, halafu, fungua
hizo picha kama ushahidi, nikafungua, mamamamah!….nilitamani niirushe hiyo simu
chini, nilibadilika kwa haraka, lakini akili ikanicheza, kwa haraka pale
nikasimama kupotezea, nikasema;
‘Vipi kuna nini…?’ akauliza rafiki yangu
‘Mhh..kuna mtu ana mzigo wangu kasema niende sasa hivi, ni mzigo
muhimu sana, na muda umeshapita,… samahani dada, sio nakufukuza, ila ni muhimu
niende..’nikasema
‘Na mtoto…?’ akaniuliza
‘Usijali, nipo na ndugu yangu hapa, …’nikasema na rafiki yangu akanielewa
akaondoka, na alipondoka nilishukuru mungu, maana nilichotumiwa kwenye simu,
kilitaka nipoteze fahamu, ni picha zile zile, lakini hii ilikaa vibaya
zaidi..kwanza sikuifuta kwa haraka, nikampigia mtu mmoja wa studio, ili
anisaidie, nikamuelezea kuwa kuna mtu ananichezea je unaweza kugundua kuwa
picha hii ni kweli au ya kutengeneza
‘Akasema anaweza…na sikupoteza muda nikaenda kwake, akaichunguza
akasema picha hiyo ni ya kweli na imechukuliwa kwenye kamera za kujificha,
haina shaka,..
‘Unaweza kugundua ni kamera za namna gani ..?’ akasema
‘Hii ni mitambo ya kisasa, inaweza ikawekwa sehemu yoyote,
ikachukua matukio, ni kidude kidogo tu, …’akasema
‘Nawezeje kugunduaje kama bado kipo ndani ya nyumba yangu..?’
nikamuuliza
Akanielekeza jinsi gani ya kukigundua kwa kutumia simu yangu tu ya
mkononi, akaniwekea program fulani kwenye simu yangu, ambayo itanisaidia
kugundua hicho kifaa, basi nikarudi nyumbani, nikajaribu kufanya kama
alivyonielekeza, lakini sikuweza kukigundua hicho kifaa, ina maana kilishaondolewa.
‘Sasa ni nani huyu mtu…’nikajiuliza na kabla sijapata jibu mara
simu yangu ikaita, kuangalia nikagundua kuwa ni mume wa familia,
‘Unasemaje…?’ nikamuuliza nikiwa naona kama ananipotezea muda tu
‘Umetumiwa ujumbe wowote..?’ akaniuliza na hapo nikashtuka, yeye
kajuaje hilo, nikasema hivi tu
‘Na nani…?’ nikauliza
‘Mimi nimetumiwa ujumbe hapa wenye picha, wakasema na wewe
wamekutumia, unaona hizo picha zilivyo, wanataka tuwalipe pesa nyingi, na mimi
sina pesa za kutosha, tufanyeje..?’ akaniuliza
‘Ni nani hao…?’ nikamuuliza
‘Hawajajulikana bado…’akasema
‘Kwahiyo unaniambia mmi nifanye nini, mimi sina pesa, unafahamu
fika mimi namtegemea mke wako, anilipe
mshahara na kazi hiyo ya ajira pesa yake ndio kiduchi hata sisemi ni kiasi gani…’nikasema
‘Sikiliza mwambie rafiki yako umekwama, una tatizo kubwa sana,
kama anaweza akukopeshe milioni kumi hivi…’akasema
‘Milioni kumi!!.Wewe una wazimu kweli mimi sio kama wewe
unayemiliki kampuni pesa kama hiyo kwako ni ndogo au sio…, kwangu mimi ni pesa
nyingi sana.siwezi kufanya kitu kama hicho, hata rafiki yangu atanishitukia..’nikasema
‘Umesoma huo ujumbe kwenye hizo picha, ulivyosema..?’ akaniuliza
‘Mimi sijali, wafanye watakavyo, mimi sina hizo pesa…siwezi
kujiingiza kwenye mtego kama huo…’nikasema ila kiukweli moyoni nilikuwa na
wakati mgumu, yaonekana huyo mtu alishajipanga, na sio rahisi kumnasa kwa njia
rahisi, iliyobakia ni kushirikiana na huyo huyo mume mtu.
‘Kwenye hizo picha kweli kulikuwa na ujumbe wa vitisho, uliandikwa
hivi; je unataka kwenda kusoma, je
unataka urafiki wako na rafiki yako udumu, je rafiki yako akiziona hizi picha
utafanikiwa hayo…tutawasiliana nawe baadae..’’ wakamaliza hivyo
‘Ninakuja kwako nataka kukuelezea nilichokutana nacho huko
nilipokwenda…’akasema, sikuwa na ujanja, nikakubaliana naye tu . ila nikampa
tahadhari kuwa asije na gari lake..
Baadae kweli alifika:
‘Unajua kuna mambo ambayo huwezi kuamini..’akasema
‘Kwanini..?’ nikamuuliza
‘Unafahamu sikuamini hata mimi,…sikutarajia unajua nilikwenda
kuonana na huyo mtu, na nikafuata maagizo yake, ni kwenye mgahawa fulani hivi,
mara akaja mtu, akaniambia naitwa niende sehemu nyingine humo humo, nafika
nakutana na mtu ambaye sikutegeemea kukutana naye hapo…
‘Mtu gani huyo, …?’ nikamuuliza
‘Makabrasha…’akasema
‘Makabrasha anahusikanaje na hili..?’ nikamuuliza
‘Hahusiki, lakini ilikuwa ni bahati kukutana naye hapo…’akasema
‘Kwa vipi..?’ nikamuuliza
‘Kwasabau ndiye wakili niliyepanga nionane naye …’akasema
‘Wewe, ina maana huyo wakili uliyesema anafaa, ndio huyo,..
hahaha, wewe kweli huna akili , kama ndio huyo mimi simo…?’ nikamuuliza
‘Sio kuwa ni yeye anahusika, hapana, yeye anasema kaniona
nikiingia akawa anataka tuongee mambo mengine nikamkatiza kuwa mimi nipo
matatani, ..nilishampigia simu awali, akasema niende ofisini kwake, lakini
nilimuambia hilo jambo sio la kiofisini..’akasema
‘Mjanja huyo ndio huyo huyo kakufanyia hivyo…’akasema
‘Hapana sio yeye, yeye alikuwepo hapo kwa mambo yake tu, ndio
ikaabidi nimuambie, maana bado nilikuwa sijamuambia tatizo lenyewe..’akasema
‘Akasemaje sasa…?’ nikamuuliza
‘Nimpe yeye hiyo kazi ya kukutana na huyo mtu, na yeye atajua
jinsi gani ya kulimaliza hilo tatizo, maana watu wote wenye kazi hizo
anafahamina nao,…nikaona basi nimemaliza tatizo…’akasema
‘Ukakubali…kirahisi hivyo…?’ nikamuuliza
‘Sasa ningelifanya nini,kwa hali kama hiyo, unajua nilichofanya
kweli nlikubali,nikasema sawa kama ana nia kweli ya kunisaidia anisaidie, na
kama ana nia mbaya, nitamgundua tu,… sikuondoka kwa haraka.
Nikajifanya nimeondoka pale,
lakini sikuondoka nilikwenda kwenye duka moja na nikanunua nguo za haraka
nikabadili na kuvaa mawani ya kuficha sura, nikarejea pale na kujificha sehemu ambayo
ningeliweza kuiona ile sehemu niliyotakiwa kukutana na huyo mtu…’akasema
‘Basi kweli,…kwasababu Makabrasha alikaa sehemu ile niliyopanga
nikae mimi, na huyo jamaa akaja kwenye ile meza, unajua,….. ndio maana nasema
sio kweli, jamaa alipogundua kuwa aliyepo hapo ni Makabrasha…kwa haraka akasimama
kuondoka,
Makabrasha akajua jinsi gani ya kumweka sawa, wakaongea na
mwishoni wake nikaona wakikubaliana kwa kushikana mikono, …’akasema
‘Walikubaliana vipi…?’ nikauliza
‘Baadae Makabrasha akanipigia simu ndio akaniambia kuwa kaongea na
hao watu, na wao wamekubali kuachana na hizo picha kama watapata mafaso yao, na
gharama za huo mradi, wamesema mradi huo umewagharimu pesa nyingi, kwahiyo wao,
kwa haraka wahitajia hisa kwenye kampuni yangu, asilimia kumi na ishirini,
akashushana nao hadi kumi na tano, ndio mwisho…na pesa taslimu, milioni
hamisini…’akasema
‘Mungu wangu, mbona ngumu hiyo kwanini hisa za kampuni, huoni hapo
ni mtego, na watu kama hao huwezi kuingiana nao makubaliano ya hisa, watakuja
kuua kampuni…’nikamwambia,
‘Ndio hapo, siwezi kwakweli, lakini sasa nifanyeje…kiukweli hapo
nimechanganyikiwa, hata sijui nifanyeje…’akawa kweli anaonyesha kuchanganyikiwa,
mimi sikuweza kumsaidia kwa hilo, nikasema;
‘Mimi sitaki upuuzi wenu, huyo makabrasha ndiye anakuchezea akili,
wewe hujui tu, mimi hado hapo nimeshaiona hiyo picha, ni swala la kupata
ushahidi tu…’nikasema
‘Sio yeye bwana, yeye hawezi kunifanyia hivyo, yeye pamoja ya kuwa
ni rafiki yangu lakini pia yeye ni kama ndugu yangu tumetokea kijijini kimoja,
kama angelitaka kitu kama hicho angeliniambia, na yeye mbona tunafanyiana kazi
mara kwa mara ...’akasema.
‘Sasa sikiliza umeshanifahamisha hilo, sasa ankuomba, niachie hilo
jambo, mimi nitafanya kivyangu, lakini kwangu hapati hata senti moja, wewe
fanya ufanyavyo, wewe si una pesa, …tumia pesa zako, na hisa zako, shauri
lako,..mimi nitatumia mbinu zangu, huyo mtu kaingia kubaya..’nikasema
‘Ndio maana nimekuja kwako, na nakufahamu wewe ni askari, unaweza
kupambana na mtu kama huyu, kwa mbinu zako za uchunguzi na mimi nitatumia kila
hali, pesa , na kila njia, ili tuweze kupata mwanya wa kumshinda huyu mtu na
mambo mengine yaenda kama kawaida,...’akaniambia
‘Hili sio swala la uaskari, huu hapa ni utapeli, wa kishenzi, na
mbinu kama hizi mwisho wake ni mbaya, sipendi kabisa kujiingiza huko, najua ni
nini kitatokea baadaye, ...tamaa ya namna hiyo inaweza kugharimu maisha ya
watu, na ukiingia huko, ukanaswa kwenye mitegi yao, kuja kujinasua itakuwa
vigumu sana, ..haya baada ya hapo mkakubaliana nini?’ nikamuuliza
‘Mimi sijakubaliana naye bado, maana walichokitaka ni kikubwa sana
kwangu, kwa hivi sasa kwanza sina pesa, pili kampuni ina madeni mengi, na
ukumbuke baba mkwe anafuatilia kila kinachoendelea kwenye kampuni kwa vile
kampuni hiyo imeanzishwa kwa mkopo wake,…..’akasema
‘Hujapanga kitu na yeye unakuja kwangu, mimi sina pesa, mimi kwa
hivi sasa nipo maternity, na zaidi unajua mke wako kaniganda kama ruba, unataka
mimi nifanye nini..?’ nikamuuliza
‘Nafikiri hunielewi na huniamini, nimekuambia kila kitu nimekiacha
mikononi mwa huyo wakili, kaongea naye wakaja na makubaliano hayo, sasa, mimi
nashindwa la kufanya,..na huyo wakili anasubiria jibu langu, nilitaka ushauri
wako hapo, nifanyeje…?’ akaniuliza
‘Ushauri wangu eeeh, waambie, ‘go
to hell’ unasikia, najua unafahamu kiingereza sawa sawa,….unanielewa
waambie wafanye wanalotaka, mimi siwezi kukushauri jambo hapo, huwezi kuwapa
hisa nyingi hivyo, bado wanataka pesa kiasi hicho, kama unazo wape..’nikasema
‘Basi, ngoja nikikutana naye tena nitajua la kufanya, huyo wakili
atanisaidia tu, anafahamu njia ya kupambana na hao watu, atawafanya washuke
shuke, kwa hisa sikubaliani nao kabisa…’akasema
‘Umesema kuwa uliwahi kufanyiwa hivyo, na aliyekusaidia ni huyo
huyo wakili , alikusaidiaje… ?’ nikamuuliza
‘Nikuambie ukweli, yaani sasa nachanagnyikiwa, kwani siku za
nyuma, kama miezi kadhaa nyuma..yawezekana mwaka sasa, sina uhakika..,
nilitakiwa kumlipa binti mmoja pesa nyingi tu, baada ya vitisho vinavyofanana
na hivi, sikuweza kufahamu ni nani, ila huyo binti aliniambia kuwa huyo
anayeshirikiana naye ni mtu wa usalama wa taifa...’akasema
‘Mtu wa usalama wa taifa!, hapana wewe, ulijuaje kuwa huyo mtu ni
mtu wa usalama wa taifa?’ nikamuuliza
‘Ndivyo alivyoniambia hivyo huyo binti...’akasema
‘Usiwe mjinga, ni huyo huyo wakili wako anakuchezea, keshaonja
asali sasa anataka kuchonga mzinga, naona hapo kuna jambo, nahisi wewe
unafahamu zaidi ya hayo...je huyo binti ni nani?’ nikamuuliza
‘Mhh, ni binti mmoja muhuni tu, haina haja kumfahamu, si unajua
zangu, pombe zikinitinga nakuwa sio mimi tena, ilitokea bahati mbaya tu...’akaniambia
‘Au ni yule binti wenu wa ndani mliyesema katoroka..hivi kweli
ilikuwaje, sijamsikia kabisa, sio yeye kweli?’ nikamuuliza na yeye akageuka
pembeni,na kukaa kimiya.
‘Sikiliza, kama unataka kushirikiana na mimi kwa hili, hunabudi
kuniambia ukweli wote je huyo binti ni yule binti wenu wa ndani, na kwanini
alitoroka?’ nikamuuliza.
Hapo alikaa kimia, nikahisi kuna jambo hapo na hapo naweza
kugundua mambo, na huenda huo ndio mchezo wao, na sasa anataka kunitumbukiza na
mimi kwenye huo mtego.
‘Sikiliza unafahamu mimi ni mpelelezi, na kwa hilo naweza
kulifanyia kazi na kuligundua, ..ninaweza kumtafuta huyo binti na kuufahamu
ukweli wote, sasa ili tusipoteze muda niambie ukweli kilichotokea kwa huyo
binti..?’ nikamuuliza
‘Wa nini huyo binti, sitaki kabisa kumuona tena huyo binti, maana
nikimuona nitamweka ndani..hata hivyo yule binti ni wa kijijini tu..,
anahusikanaje na hili…’akasema
‘Una uhakika na hilo…sio yeye uliyempachika mimba ndio akaanza
kudai mapesa mengi…, niambie ukweli au nianze kazi ya kuwapigia simu watu
wangu,wanaomfahamu huyo bint..?’ nikamuambia
‘Unataka nikuambie nini kumuhusu yeye…?’ akauliza sasa akionyesha
wasiwasi fulani. Hapo nikakumbuka kipindi fulani nilizoeana na huyo binti,
ikawa mara fulani akiwa na nafasi ananitembelea, na hapo akilini mwangu ikawa
inaniuliza ni nani angeliweza kufika kwangu kwa uhuru na kuweka vifaa kama
hivyo, ni shuku shuku tu.
‘Kila kitu…ilitokeaje mpaka akatoroka, maana yawezekana ni yeye
kaamua kukuchezea huo mchezo, ili kukukomoa, je ilitokeaje kwa huyo binti, je
ndio yeye aliyesema anashikrikiana na usalama wa taifa, ..na huyo usalama wa
taifa ni nani, nikipata majibu hayo nitaweza kusema neno…’nikasema
Akaa kimia kama anawaza na baadae akaanza kuongea;…
NB: Ngoja niishie hapa kwanza, maana hapa kuna maelezo marefu
msichoke kwanza, lakini hapa hapa mtagundua jambo muhimu kwenye hiki kisa…
WAZO LA LEO: Dunia ya sasa ilivyo, sio vyema
kumuamini kila mtu, watu wengine wanapenda kuwaingiza watu wengine kwenye
biashara haramu, hasa wakishaona mtu mwingine yupo kwenye hali ngumu. Halingumu
zetu, maisha magumu yetu, mitihani mbali mbali ya isiwe ni sababu ya
kujitumbukiza kwenye biashara haramu, tukauza utu wetu na heshima zetu,..tukaja
kuachana na familia zetu, kwa kutumbukizwa jela au kupoteza maisha,…Tuwe na
subira kwani mapito hayo, kwani mitihani hiyo maisha, ni ya muda tu, muhimu ni
kujaribu kutafuta njia halali za sababu ya kupata riziki na pato halali,
tukumbuke baada ya dhiki hiyo, itakuja faraja.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment